STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, September 19, 2013

Chelsea hoi darajani, Barca 'yaua', Arsena yatakata

All smiles: Messi celebrates his opener with defener Dani Alves
Messi akishangilia moja ya mabao yake usiku wa kuamkia leo
Sulley Muntari
Sulley Muntari akishangilia bao la ushindi la Ac Milan alilofunga lala salama
Matchwinner: Marco Streller (second right) steals in at the near post to head Basle's decisive second goal
Basel wakijipatia bao la pili lililoizamisha Chelsea 'darajani' huku Mourhino akipewa ujumbe kupitia mabango kwamba Mata atatakiwa awe uwanjani na siyo kwenye benchi.
 Rumblings of discontent: A Chelsea fan shows his displeasure at Juan Mata's lack of first-team action
WAKATI Jose Mourinho na vijana wake wa Chelsea wakianguka 'darajani' kwa kulala mabao 2-1 mbele ya Basel ya Uswisi, Lionel Messi ameendelea kuboresha rekodi yake ya mabao baada ya kufunga 'hat trick' wakati Barcelona ikiizamisha Ajaz kwa mabao 4-0.
Chelsea ilikumbana na kipigo hicho na kuifanya icheze mechi nne bila kupata ushindi, japo walianza kutangulia katika mechi hiyo iliyochezwa Stanford Bridge kupata bao kupitia Oscar kabla ya Basel kusawazisha mabao yote katika kipindi cha pili.
Mabao ya washindi hao ambao wamekuwa wakizisumbua timu kubwa kila mara katika michuano hiyo, yalifungwa na Salah dakika ya 71 na Streller dakika ya 82.
Katika mechi nyingine Barcelona ikiwa uwanja wake wa nyumbani iliisasambua Ajax ya Uholanzi kwa kuishindilia mabao 4-0, huku 'mchawi mweupe' Messi akitumbukiza mara tatu na kuondoka na mpira wake nyumbani.
Bao jingine la mabingwa hao wa Hispania lilifungwa na Gerard Pique, ilihali Arsenal wakiwa ugenini nchini Ufaransa walitakata baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Olympique Marseille nao Ac Milan ikiwa nyumbani ilifunga Celtic mabao 2-0.
Mecchi nyingine matokeo yake ni Schalke 04 kuilaza Steau Bucharest mabao 3-0, Napoli kuitafuna Borussia Dotmund ya Ujerumani mabao 2-1 nchini Italia, kadhaalika Atletico Madrid wakitakata nyumbani kwa kuilaza Zenit kwa mabao 3-1na Porto ya Ureno kushinda ugenini mbele ya wenyeji wa Austria Wien.

Mabao 58 yafungwa Ligi Kuu, Tambwe nouma Ashanti, Prisons angalau sasa

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhSAUn1hwkMI3BcBcVeWb4YPc0cKNG2217o1rBuA9t_YRDuDqEfojRYqpc29if8_8ljHN5fIIGwDFx3hdNQ8y8cAo4E9tHnw8BP3Wr4L1T4iGcr2gWQ3Ua9aWJGULdoHdk_r9la7cxPVzw/s1600/DSC_0072.jpg
Tambwe Amissi

JUMLA ya mabao 58 yametinga wavuni mpaka sasa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imemaliza raundi nne tangu ilipoanza rasmi Agosti 28 mwka huu, huku Mrundi Tambwe Amisi akiongoza orodha ya wafungaji baada ya jana kutupia mabao manne pekee yake wakati Simba ikiichinja Mgambo JKT kwa mabao 6-0.
Mfungaji Bora huyo wa michuano ya Kombe la Kagame, anafukuziwa na wachezaji wa Yanga na Simba, Jerry Tegete na Haruna Chanongo wenye mabao matatu kila mmoja, huku wachezaji sita wengine wakiwa kwenye nafasi ya tatu na mabao mawili kila mmoja.
Wachezaji hao ni Didier Kavumbagu wa Yanga, Saad Kipanga wa Rhino Rangers, Bakar Kondo wa JKT Ruvu, Elias Maguri (Ruvu Shooting), Jonas Mkude wa Simba na Jerry Santo (Coastal Union).
Safu ya mbele ya Simba ndiyo mpaka sasa inaonekana kuwa kali baada ya kutumbukiza wavuni mabao 11 ikifuatiwa na watani zao Yanga wenye mabao nane, huku timu ya Prisons ndiyo yenye safu butu ya ushambuliaji ikitupia bao moja tu wavuni, ikizidiwa na timu za Oljoro JKT na Ashanti yenye mabao mawili kila moja.
Wakati ukuta wa JKT Ruvu ukiwa mgumu kupitika, ule wa maafande wenzao wa Mgambo JKT ndiyo 'nyanya' baada ya kuruhusu mabao 9 mpaka sasa ikifuatiwa na Ashanti (8) na Prisons iliyofungwa mabao 7.
Mashabiki wa soka watarajie mabadiliko makubwa ya orodha ya ufungaji na hata kwenye msimamo wa Ligi Kuu ambao kwa sasa unaoongozwa na Simba mwishoni mwa wiki wakati ligi hiyo itakapoendelea kwa timu zote 14 kushuka tena dimbani, huku pambano linalosubiriwa kwa hamu likiwa ni Yanga na Azam.
Chini ni msimamo wa sasa wa Ligi hiyo na orodha ya wafungaji mabao;

Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2013-2014                                            P  W  D  L    F  A  GD  PTS
1. Simba                         4   3   1   0   11 2  9   10
2. JKT Ruvu                   4   3   0   1   6  1   5    9
3.  Ruvu Shooting           4   3   0   1   6  2   4    9
4.  Yanga                        4   1   3   0   8  4   4    6
5.  Azam                         4   1   3   0   5  3   2    6
6.  Coastal Union            4   1   3   0   4  2   2    6
7.  Mbeya City                4   1   3   0   3   2   1   6
8.  Kagera Sugar             4   1   2   1   3   3   0   5
9.  Mtibwa Sugar            4   1   2   1   2  3   -1   5
10.Rhino Rangers            4   0   3   1   4  6   -2   3
11. Mgambo JKT           4   1   0   3   1   9  -8   3
12. Prisons                      4   0   2   2   1   7  -6   2
13. Oljoro  JKT              4   0   1   3   2   6  -4   1
14. Ashanti United           4   0   1   3   2   8  -6   1

Wafungaji:

4- Tambwe Amisi (Simba)
3- Jerry Tegete (Yanga), Haruna Chanongo (Simba)
2- Didier Kavumbangu (Yanga), Jonas Mkude (Simba), Bakar Kondo (JKT Ruvu), Elias Maguri (Ruvu Shooting), Saady Kipanga (Rhino Rangers), Jerry Santo (Coastal Union)
1- Abdi Banda, Crispian Odulla, (Coastal Union), Henry Joseph, Betram Mombeki (Simba), Haruna Niyonzima, Nizar Khalfan, Simon Msuva (Yanga), Iman Joel, Salim Majid (Rhino Rangers), Gaudence Mwaikimba, Seif Abdallah, Khamis Mcha, Aggrey Morris, Kipre Tchetche (Azam), Mwagane Yeya, Steven Mazanda, Paul Nonga (Mbeya City), Laurian Mpalilem, Peter Michael (Prisons-OG), Ayoub Kitala, Jerome Lembeli, Cosmas Ader (Ruvu Shooting), Juma Luzio, Masoud Ally (Mtibwa Sugar), Shaaban Juma, Anthony Matangalu (Ashanti Utd), Abdallah Bunu, Emmanuel Switta, Salum Machaku, Amos Mgisa (JKT Ruvu), Fully Maganga (Mgambo JKT), Themi Felix, Godfrey Wambura, Maregesi Marwa (Kagera Sugar), Amir Omary, Shaibu Nayopa (Oljoro JKT)

Matokeo ya mechi za awali


Agosti 24, 2013
Yanga vs Ashanti United (5-1)
Mtibwa Sugar vs Azam (1-1)
Oljoro JKT vs Coastal Union (0-2)
Mgambo JKT vs JKT Ruvu (0-2)
Rhino Rangers vs Simba (2-2)
Mbeya City vs Kagera Sugar (0-0)
Ruvu Shooting vs Prisons (3-0)

Agosti 28, 2013
Mtibwa Sugar vs Kagera Sugar (1-0)
Rhino Rangers vs Azam (0-2)
JKT Ruvu  vs Prisons (3-0)
Mbeya City vs Ruvu Shooting (2-1)
Mgambo  vs Ashanti United (1-0)
Oljoro JKT vs Simba (0-1)
Yanga  vs Coastal Union (1-1)

Sept 14, 2013

Simba  vs Mtibwa (2-0)
Coastal Union  vs Prisons (0-0)
Ruvu Shooting va Mgambo JKT (1-0)
Oljoro JKT vs Rhino Rangers (1-1)
Mbeya City  vs Yanga (1-1)
Kagera Sugar vs Azam (1-1)
Ashanti United  vs JKT Ruvu (0-1)


Sept 18, 2013
Prisons vs Yanga (1-1)
Simba vs Mgambo JKT (6-0)
Kagera Sugar vs JKT Oljoro (2-1)
Azam  vs Ashanti United (1-1)
Coastal Union  vs Rhino Rangers (1-1)
Mtibwa Sugar  vs Mbeya City (0-0)
Ruvu Shooting vs  JKT Ruvu (1-0)

Ratiba ya mechi zijazo mwishoni mwa wiki hii
Jumamosi
Mgambo JKT vs Rhino Rangers
Prisons vs Mtibwa Sugar
Simba vs Mbeya City
Kagera Sugar vs Ashanti United

Jumapili:

 JKT Ruvu vs Oljoro JKT
Azam  vs Yanga
Coastal Union v Ruvu Shooting 

Wednesday, September 18, 2013

Ray, Lulu kunogesha Dar Filamu Festival 2013

http://thumbp4-ne1.thumb.mail.yahoo.com/tn?sid=2126005954&mid=AO9WimIAAAfiUjk68wAAAJhFJXY&midoffset=2_0_0_1_1304473&partid=5&f=1215&fid=Inbox&w=480&h=331
Stanford Kihore (kati) akizungumza huku Lulu kushoto akiwa makini
TASNIA ya filamu Tanzania inakua kwa kasi sana kila kunapokucha lakini pengine ni tasnia pekee ambayo imekuwa na changamoto nyingi, na sintofahamu kwani ndio tasnia ambayo imekosa mtiririko wa matukio ambayo huwa kama motisha kwa wadau na wasanii wa filamu kwa muda mrefu tasnia ya filamu hakuna tuzo zozote takribani miaka sita zilipofanyika tuzo za Vinara 2007/8.

Tuzo na matamasha ya filamu ni vitu ambavyo uchochea sana ubora na ukuaji wa filamu katika tasnia ndio maana sehemu yoyote yenye mafanikio ya filamu lazima utawaliwa na matamasha ya sinema, ukiangalia filamu za kibongo ni nyingi sana na zimekuwa zikizalishwa na kutolewa kwa wingi na kuingia sokoni kwa kasi bila kuwa na mizania yoyote jambo linalotuchelewesha na kushindwa kufikia medani za kimataifa.

Hivi karibuni tamasha kubwa la filamu limezinduliwa na linatarajia kufanyika kuanza tarehe 24 hadi 26 Septemba 2013 katika viwanja wa CoICT- UDSM- Posta Kijitonyama Tamasha litaambatana utoaji wa  Semina kwa wadau wa filamu, kuonesha filamu za kitanzania kwa watu wote bure kwa siku tatu,Kutakua na filamu nne kwa siku kuanzia saa kumi na mbili jioni mpaka saa tano usiku.

Tamasha hilo linaloitwa Dar Filamu Festival (DFF 2013/14) linajenga histori mpya katika tasnia ya filamu kutokana na sera ya tamasaha lenyewe ambalo limekusudia kutoa fursa na kuwajengea uzoefu watayarishaji wa filamu sambamba na wasanii na kubaini umuhimu wa kuwa na matamasha, DFF pia imekusudia kutumia fursa ya kufanya Lugha ya Kiswahili bidhaa yenye mlengo wa kibiashara.

Filamu zitakazoonyeshwa ni zile ambazo zimetumia kuigizwa kwa Lugha ya Kiswahili tu, kwa kuanza ni filamu za Tanzania tu ndiyo zitakazorushwa katika Projecta kubwa kwa siku tatu  kwa jioni kuanzia saa kumi na mbili hadi saa tano usiku, hiyo ni sehemu muhimu sana na kubwa kwani hiyo ni fursa nyingine ya kuongeza mauzo badala ya njia moja tu ya kuuza Dvd pekee.

Ni Tanzania pekee ndiyo ambayo utegemea sana mauzo ya aina moja tofauti na nchi zilizoendelea ambazo kuna aina nyingi za ufanyaji wa biashara ya filamu, ikiwa soko kama uuzaji wa filamu katika majumba ya sinema tukio ambalo huwa la kwanza kabisa, filamu kuonyeshwa awali kabisa kabla ya kuingia  mtaani, filamu ikitoka kila kitu ni biashara.

Katika Dar Filamu Festival 2013/14 inastahili pongezi kwani pia inajenga hadhi kwa waigizaji wetu tayari wasanii ambao wamekuwa na mchango mkubwa wanakuwa mabalozi wa tamasha hilo, msanii Elizabeth Michael ‘Lulu’ anasimama kama mwigizaji wa kike anayewakilisha wasanii wenzake kama balozi anayebeba wengine na alama ya tamasha .

Balozi mwingine Vincent Kigosi ‘Ray’ ambaye akiwa kama mtayarishaji na muongozaji aliyechangia ukuaji wa tasnia ya filamu Tanzania, tamasha limempa nafasi kama official Producer and Director  kwa tamasha kuwaweka mbele wasanii wetu ni njia nyingine ya biashara kwao, mara nyingi kuna changamoto nyingi kwa wasanii wetu pamoja na kuwa na wafuasi wengi bado hawapati nafasi za matangazo.

“Nimefurahia sana kuchaguliwa kama Balozi wa Dar Filamu Festival na ninafuraha sana kwani kwanza kabisa ni kuonyesha uzalendo kwa kuwa na tamasha la filamu linalotuhusu sisi kama watengenezaji filamu za Kiswahili Lugha ambayo wenzetu wakenya na nchi nyingine wanakitumia vizuri na kuwaingizia fedha, huku sisi tukibaki maskini,”anasema Ray.

Mratibu wa tamasha hilo Staford Kihore anasema kuwa katika kufanikisha hilo DFF inakuwa ni chachu ya maendeleo ya tasnia ya filamu Tanzania, huku tukisema kuwa Dar Filamu Festival 2013 kwa kauli mbiu ya ‘Ubora wa Filamu Zetu’ ikiwa ni njia ya kuwakutanisha wadau wote kwa pamoja na kuwa jukwaa linalojenga tasnia ya filamu inayokua kila siku huku pia tamasha likitoa njia nyingine ya soko jipya.

“Kwa tamasha hili la awali tutaonyesha filamu za hapa Tanzania pekee ikiwa ni utambulisho wa Dar Filamu Festival kwa mara ya kwanza kwenu wanahabari, miaka ijayo Tamasha litahakikisha linashirikisha filamu kutoka sehemu mbalimbali zinazotumia Lugha ya Kiswahili  kutoka popote Ulimwenguni,” anasema Staford Kihore.

“Mimi kama Balozi wa Dar Filamu Festival ninaona fahari sana kwa ukuaji wa tasnia ya filamu tunaomba watu waliunge mkono tamasha hili kwani sisi tunapiga hatua katika tasnia ya filamu, wadau waje katika viwanja vya Posta wajionea filamu pia filamu yangu ya Foolish Age itaonyeshwa tena bure kabisa nashukru sana kuchaguliwa waigizaji tupo wengi,”anasema Lulu.

Akiongea na FC mratibu wa Tamasha hilo Staford Kihore pia amesema kuwa katika kuzingatia maendeleo ya tasnia ya filamu siku tatu hizo kila siku imepewa jina kwa filamu zitakazoonyeshwa kuanzia Tarehe 24th September, 2013 siku ya Jumanne ambayo ndio siku ya ufunguzi utakuwa ni usiku wa Bongo Movie Classics, 25th September, 2013 ni usiku wa Quality Nights.

Na ile siku ya mwisho tarehe 26th September, 2013 itakuwa ni Stars Nights siku ambayo kutakuwa na wasanii wetu mbalimbali ambao wanajenga soko hilo la Bongo movie filamu, Tamasha hili linapambwa na wasanii wote wakiwakilishwa na wasanii wenzao wawili ambao ni Vincent Kigosi ‘Ray’ kama Official Producer and Director  for DFF 2013 na Elizabeth Michael ‘Lulu’ kama Official Actress for DFF 2013.

Pia tamasha litaambatana na utoaji wa semina kwa wadau wa filamu kwa asubuhi ambapo madarasa  yataendeshwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Sanaa tarehe 24 September, 2013 masomo ya Uandishi wa Muswada, Uigizaji na  Uongozaji wa filamu yatafundishwa kwa washiriki, 25th September 2013 Siku nzima Makapuni ya Utengenezaji filamu yataonyesha na kutangaza kazi zao kwa wadau mbaliambali.

Tarehe 26th September 2013 ni siku muhimu sana kwani Taasisi kama vile TRA, Bodi ya Ukaguzi wa filamu na michezo ya kuigiza, Wasambazaji wa filamu na taasisi nyingine watakutana katika jukwaa la majadiliano kuhusu mustakabali wa tasnia ya filamu, pia filamu kadhaa zitaonyeshwa na kujadiliwa na wadau watakaokuwepo matukio yote ya asubuhi yatafanyika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam Idara ya Sanaa.

Kampuni ya Haak Neel Production na Filamucentral mtandao wa habari za filamu ndio waandaaji  wa tamasha hilli la Dar Filamu Festival (DFF) 2013,  kwa kushirikia na taasisi kama Bodi ya Filamu na ukaguzi wa michezo ya kuigiza Tanzania, Tanzania Film Federation (TAFF), UDSM- PFA, MFDI, Swahiliwood, Global Publishers.

Na makapuni ya usambazaji wa filamu Steps Entertainment Ltd, Leo Media na kampuni mpya ya usambazaji ya Proin Promotion ambayo imeanza hivi karibuni na kuonyesha dhamira ya kusaidia tasnia ya filamu, pia unaweza kupata habari zaidi kupitia mtandao wa www.dff.or.tz

Baada ya kuja tamasha la filamu ambalo limepokelewa vema na wadau wote ni kama moja ya kuelekea katika Nyanja za kimataifa ni wakati ambao pia Serikali na taasisi nyingine kuunga mkono na kuhamasisha uwepo wa tuzo za ndani, ambazo hazipo kwa muda mrefu tofauti na fani ya muziki ambayo kila aina yake imekuwa na tuzo, pia hivi karibu wadau walikutana kwa kujadili suala la sera ya Filamu.

Kwa shirikisho la wasanii wa filamu Tanzania (TAFF) kuweka mjadala huo ni hatua mojawapo wa kufungua njia ya kuelekea katika medani za kimataifa, pengine sera ya filamu ikiwepo itasaidia tasnia ya filamu kukua zaidi na kuwa rasmi tofauti na ilivyo sasa wadu wadai hivyo.

Tambwe aanza mambo Simba, JKT chali, Azam, Yanga mmmh!

Mrundi Tambwe Amisi akishangilia moja ya mabao yake leo uwanja wa Taifa (Pix:Bin Zubeiry)
MABAO manne ya nyota wa kimataifa wa Simba, Tambwe Amisi kutoka Burundi yameiwezesha Wekundu wa Msimbazi kukalia usukani wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuitafuna Mgambo JKT kwa mabao 6-0.
Simba ilipata ushindi huo mnono kwenye pambano lililochezwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kufikisha jumla ya pointi 10 na mabao 11 ikiwaengua JKT Ruvu iliyokuwa ikiongoza.
Simba imekwea kileleni baada ya waliokuwa vinara JKT Ruvu kulala bao 1-0 mbele ya ndugu zao Ruvu Shooting katika pambano jingine lililochezwa kwenye uwanja wa Mabatini-Mlandizi.
Mabao mengine ya leo ya Simba yaliwekwa kimiani mshambuliaji anayezidi kuja juu nchini wa klabu hiyo ya Simba, Haruna Chanongo. Kwa kufunga mabao hao manne Tamwe ameweka rekodi ya aina yake ya kuwa mchezaji wa kwanza kwa misimu mitatu kufunga zaidi ya mabao mawili katika mechi moja pia kukwea kwenye nafasi ya kwanza ya ufungaji mabao akiwaacha nyuma akina jerry Tegete na Chanongo wenye mabao matatu kila mmoja.
Wakati Simba ikichekelea ushindi huo wa kishindo jijini Dar mabingwa watetezi Yanga waliokuwa mjini Mbeya walijikuta wakipata sare ya tatu mfululizo baada ya Prisons kuwagomea.
Jerry Tegete alitangulia kuipatia bao Yanga kabla ya wenyeji kusawazisha dakika ya 77 kupitia Peter Michael na kufanya mechi hiyo iliyochezw auwanja wa Sokoine kuisha kwa sare ya 1-1.
Waliokuwa vinara wa ligi hiyo, JKT Ruvu walijikuta wakiangukia pua mbele ya Ruvu Shooting kwa kulazwa bao 1-0 katika mechi iliytochezwa uwanja wa Mabatini, Pwani.
Katika pambano jingine lililochezwa kwenye uwanja wa Chamazi, wenyeji Azam ilijikuta wakilazimishwa sare ya bao 1-1 na Ashanti United.
Azam walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia mfungaji bora wa ligi iliyopita, Kipre Tchetche dakika ya 20 ya mchezao kabla ya Anthony Matangalu kuisawazishia Ashanti dakika ya 78.
Katika mechi nyingine zilizochezwa leo Coastal Union ikiwa jijini Tanga imenusurika kipigo baada ya nahodha wake Jerry Santo kusawazisha bao na kufanya wagosi hao wa Kaya kutoka sare ya 1-1 na Rhino Rangers ya Tabora.
Nao Kagera Sugar wakiwa nyumbani kwao uwanja wa Kaitaba walmechomoza na ushindi wa mabao 2-1 dakika za jioni dhidi ya JKT Oljoro, huku Mtibwa Sugar kwenye uwanja wao wa Manungu, walibanwa mbavu na Mbeya City na kwenda nao suluhu ya kutofungana.

Tuesday, September 17, 2013

Hawa ndiyo wanawake vinara wa dawa za kulevya!

KUNA dhana iliyojengeka kuwa wanawake ni watu laini, wapole na wasioweza kufanya mambo ya hatari. Hata hivyo pia kuna wengine wanadai kuwa wanawake ni daraja hatari sana. Machoni huonekana laini lakini wanaweza kutenda mambo ambayo ni vigumu kwa mtu wa jinsia ya kiume kuyafanya. Biashara ya madawa ya kulevya inahitaji watu hatari, katili, wenye roho isiyotishika. Huwezi amini miongoni mwa watu wanaonekana jamali na wapole usoni ndiyo wakali katika biashara hiyo. Wasome vigogo 10 wanawake duniani wanaotisha kwa biashara ya 'bwimbwi' a.k.a ugoro, unga sembe nk
Mireya Moreno Carreon.
Nancy Botwin katika ‘siriz’ yake ya Weeds kwenye TV, anajaribu kuonesha jinsi mwanamke anaweza kuwa hatari katika biashara ya bangi na madawa ya kulevya kwa jumla, hata hivyo katika uhalisia, hajawafikia hata chembe wanawake hawa hatari ambao wameitikisa dunia.
Hawa ni maharamia 10 wauza unga, wametengeneza fedha nyingi na kila mmoja ameshahusika kwa namna moja au nyingine na mauji. Kwa muuza madawa ya kulevya, kitendo cha kutoa roho ya mtu kipo jirani yake sana.
1. GRISELDA BLANCO
Inawezekana huyu ndiye akawa muuza unga mwanamke katili, mwenye uwezo mkubwa kuliko wote kuwahi kutokea katika historia ya dunia. Ameshahusika na mauaji ya watu zaidi ya 200. Ni raia wa Colombia, akiwa na miaka 11, tayari alishahusika na tukio la utekaji wa mtoto. Baadaye alihamia Marekani, kwenye Jimbo la Florida ambako alitengeneza mtandao wa madawa ya kulevya ambao ulimpa utajiri mkubwa.

2.  SANDRA AVILA BELTRAN
Ni raia wa Mexico, alizaliwa mwaka 1960. Aliwahi kupewa jina la Mungu wa Kike wa Madawa ya Kulevya. Vyombo vya habari nchini mwake vikamwita Malkia wa Pacific. Serikali za Marekani na Mexico zinamtaja kuwa kiungo wa magenge ya unga ya Sinaloa Cartel la Mexico na Norte del Valle Cartel la Colombia. Anadaiwa kujipatia mabilioni ya dola kwa usafirishaji wa unga kati ya Colombia, Mexico na Marekani. Kwa sasa yupo gerezani nchini Mexico kwa kosa la utakatishaji wa fedha haramu.

3. ANGIE SANCLEMENTE VALENCIA
Ni raia wa Colombia, aliwahi kushika taji la urembo la taifa katika nchi hiyo lakini alinyang’anywa baada ya kubaini ameshaolewa. Mume wake alikuwa mmoja wa vinara wa unga na walipoachana, alitumia njia zilezile kujipatia utajiri haramu. Alikuwa na genge kubwa la wasafirishaji wa cocaine na kila mtu alimlipa dola 5,000 kwa safari moja. Alisafirisha zaidi Argentina, Uingereza na Mexico. Ana umri wa miaka 35, yupo gerezani Argentina tangu Oktoba 27, 2010.

4. KATH PETTINGILL
Alizaliwa mwaka 1935. Jina lake la utani ni Bibi Kizee Shetani (Granny Evil). Ni mwenyeji wa Jiji la Melbourne, Australia. Alianza kama kahaba kabla ya kugeukia madawa ya kulevya. Alipoteza jicho moja baada ya kupigwa risasi katika moja ya matukio ya uharamia, akimtetea binti yake, Vicky, aliyekuwa anadaiwa dola 300 na maharamia wenzake. Nguvu ya mtandao wa unga aliyoitengeneza, ni hatari na imehusika na mauaji mengi nchini Australia.

5. ENEDINA ARELLANO FELIX
Katika genge ambalo lilikuwa linaongozwa na kaka zake, Ramon na Eduardo, mwanzoni yeye alishika nafasi ya umeneja wa fedha. Baada ya Ramon kuuawa na Eduardo kukamatwa, alishika uongozi. Maofisa usalama wa Mexico waliwahi kukiri kwamba Enedina ndiye alikuwa dira ya kaka zake. Ana umri wa miaka 52, ni msomi mwenye shahada ya uhasibu. Marekani imempiga marufuku kuingia nchini humo. Amebadili mfumo na sasa anaendesha kazi zake kisayansi,
hakuna fujo za magenge ya wahuni kiasi kwamba inakuwa ngumu kumtia hatiani.

6.  BLANCA CAZARES SALAZAR
Ni raia wa Mexico, alianza kujihusisha na utakatishaji wa fedha haramu, aliponogewa akajikita kwenye unga. Ana umri wa miaka 37. Biashara yake ameitanua na yupo makini sana. Anaongoza mtandao mkubwa wenye makundi 42. Ni ngumu kumkamata kwa sababu hahusiki moja kwa moja. Marekani imempiga marufuku kuingia nchini humo.

7. MARIA JIMENEZ
Ana umri wa miaka 27. Alikuwa kiongozi wa genge lililokufa la La Tosca. Baada ya kufanya biashara kwa muda mrefu, alikamatwa mwaka jana nchini kwake Mexico kwa tuhuma za usafirishaji wa unga na mauaji. Baadaye alikiri kuua watu 20 na mpaka sasa yupo jela.

8.  EDITH LOPEZ LOPEZ
Anajulikana kama Malkia wa Kusini. Amekuwa kinara wa madawa ya kulevya tangu alipoolewa na haramia wa unga, Raul Nunez Morales, maarufu kama The Cowboy. Tangu mwaka 2000, Edith amebaki kuwa mmoja kati ya wanawake tisho kwa biashara hiyo haramu duniani.

9. THELMA WRIGHT
Alishirikiana na marehemu mumewe, Jackie Wright katika biashara ya unga kati ya miaka ya 1980 na 1990. Mwaka 1986, mumewe aliuawa, kwa hiyo akashika usukani kwa kulisuka genge lao la Black Mafia ambalo lilifanya matukio mengi. Hata hivyo, kwa kuhofia maisha ya mtoto wake, Jackiem,  kuharibika, aliachana na kazi hiyo na kufanya shughuli nyingine halali. Ni mara chache sana kutokea.

10. MIREYA MORENO CARREON
Ndiye mwanamke pekee kushika nafasi ya juu kwenye Genge la Zetas. Ndani ya kipindi kifupi alifanya matukio mengi ya utakatishaji wa fedha haramu na usafirishaji wa unga. Akiwa nchini kwake, Mexico, mwaka 2010, maofisa usalama wa siri walimkamata akiwa akiwa na gari lenye cocaine na bangi na mpaka leo yupo korokoroni.

Sheikh Ponda akwama kupata dhamana Morogoro



  Sheikh Ponda Akishuka kwenye basi la Magereza tayari kuingia Mahakamani Kusikiliza kesi yake inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoani Morogoro.
Sheikh Ponda anashtikiwa katika Mahakama hiyo akikabiliwa na Mashtaka Matatu ambayo inadaiwa aliyatenda Mkoani Morogoro katika Mkutano hadhara mwezi uliopita.
Kiongozi huyo wa umma wa Kiislam Tanzania amenyimwa dhamana na hivyo kurejeshwa tena rumande mpaka kesi yake itakaposomwa tena Oktoba  Mosi.






 Sheikh Ponda akiwa Chini ya Ulinzi Mkali wakati akiingia Mahakamani kusikiliza kesi yake inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoani Morogoro.




 
Sheikh Issa Ponda akiingia Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoani Morogoro leo kusikiliza kesi yake






 Wafusi wa Sheikh Ponda wakiwa wakiwa mahakamani leo kusikiliza kesi ya Kiongozi wao iliyokuwa imetajwa mahama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro.


Ulinzi mkali ukiwa umeimarishwa mahakamani leo wakati kesi hiyo ikiendelea mjini Morogoro.

Newz Alert: Shule ya Ilboru yafungwa, kisa...!

Waziri Majaliwa alipowahi kwenda kuutuliza mgogoro wa wanafunzi wa Ilboru mwaka jana
TAARIFA zilizotufikia hivi punde zinasema kuwa, serikali imeamua kuifunga kwa muda usiojulikana Shule Maalum ya vipaji ya Ilboru ya jijini Arusha, baada ya kuwepo kwa tishio la kuchomwa moto kutokana na mgogoro uliodumu kwa muda mrefu shuleni hapo.
Imedokezwa wanafunzi wapatao wanne wanahojiwa kutokana na tishio hilo huku wengine karibu 800 wamerudishwa makwao mpaka watakapotangaziwa vinginevyo.
Tangu mwaka jana shule hiyo imekuwa na mgogoro baina ya wanafunzi na uongozi wake kiasi Naibu waziri wa Tamisemi (Elimu), Kassim Majaliwa kulazimika kuingilia kati, lakini hali haijatengemaa hadi hivi karibuni tena kiliponuka tena.

Msiba tena! Prince Ahmed Mgeni hayupo nasi afariki Zenji

Prince Ahmed Mgeni

TASNIA ya sanaa imeendelea kupata misiba baada ya muimbaji nyota wa zamani wa Zanzibar Stars, Prince Ahmed Mgeni kufariki dunia visiwani Zanzibar na jioni hii alitarajiwa kuzikwa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka visiwani humo zinasema kuwa, marehemu Mgeni aliyetamba na kuziba nafasi ya Mzee Yusuf alipojiengua katika kundi hilo na kuunda Jahazi, alifariki usiku wa kuamkia leo katika Hospitali ya Mnazi Mmoja alipokuwa amelazwa.
Taarifa za awali zinasema marehemu alikuwa akisumbuliwa na kifua kikuu (TB) na kulazwa hospitalini hapo kwa muda mrefu.
Mpaka mauti yalipomkuta jana marehemu Mgeni alikuwa mwanamuziki wa kundi la Zanzibar Njema Taarab.
Kifo cha msanii huyo ni muendelezo wa misiba katika tasnia ya sanaa kuanzia mwishoni mwa mwaka jana ambapo imeshuhudiwa waigizaji na waimbaji wakipoteza uhai kwa sababu mbalimbali ikiwamo ajali na maradhi. Mungu aiweze mahali pema peponi roho ya marehemu Ahmed Mgeni na MICHARAZO inawapa pole familia, ndugu, jamaa na rafiki wa msanii huyo pamoja na wadau wote wa sanaa Tanzania. 

Sunday Kayuni kuhudhuria kozi ya wakufunzi CAF

Sunday Kayuni
MKURUGENZI wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Sunday Kayuni atashiriki warsha ya wakufunzi wa makocha wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) itakayofanyika kuanzia Oktoba 22-24 mwaka huu.

Warsha hiyo iliyoandaliwa na CAF kwa ajili ya wakufunzi wake itafanyika nchini Cameroon. Wakufunzi 18 wa CAF kwa upande wa makocha watahudhuria warsha hiyo.

Madhumuni ya warsha hiyo ni kuainisha majukumu yao, kubadilishana uzoefu. Pia kuwapa methodolojia mpya ya ufundishaji na muongozo kuhusu mfumo wa leseni za makocha ambao watautumia katika nchi wanazotoka.

Mbali ya Kayuni Tanzania, wakufunzi wengine ni Ahmed Babiker (Sudan), Amadou Shaibu (Nigeria), Boy Bizzah Mkhonta (Swaziland), Duodu Fred Osam (Ghana), Edussei Anthony (Ghana), Fathi Nossir (Misri), Faouzy Altaisha (Sudan) na Fran Hilton Smith (Afrika Kusini).

Wengine ni Francis Oti-Akenteng (Ghana), Honour Janza (Zambia), Kasimawo Laloko (Nigeria), Mahmoud Saad (Misri), Paul Hamilton (Nigeria), Serame Letsoaka (Afrika Kusini), Shawky Abdel Shafy (Misri), Thondoo Govinder (Mauritius) na Ulric Mathiot (Seychelles),

Tembo Mtoto, nyota iliyozimika ghafla katika ngumi za kulipwa

Bondia Yohana Mathayo 'Tembo Mtoto' (kulia) akichuana na Fadhili Awadh 'Mnyama Chui' katika moja ya mapambano yake enzi za uhai wake.
 Na Magendela Hamisi
SEPTEMBA 12 tasnia ya mchezo wa masumbwi ilimpoteza bondia mahili wa uzito wa kilo kilo 66, Yohana Mathayo 'Tembo Mtoto' (23), akiwa mazoezini kujindaa na pambano lake la ubingwa wa Taifa dhidi ya Abdallah Mohammed 'Prince Nassib'.
Pambano hilo lilipangwa kufanyika Oktoba mwaka huu, jijini Dar es Salaam na kusimamiwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST), lilionekana kuvuta hisia za mashabiki wengi.
Bondia huyo mahili ambaye jina lake lilianza kujulikana baada ya kufanya vema katika mapambano yake mengi, tena kwa kushinda kwa KO, wengi walimtabiri mafanikio makubwa kupitia mchezo huo.
Katika vitongoji vya Jiji la Dar es Salaam, hasa kwenye chimbuko la mchezo masumbwi yakiwemo maeneo ya Keko, Manzese, Tandale, Mburahati, Mabibo, Mwananyamala na maeneo mengine hakuna asiyefahamu jina la Tembo Mtoto.
Kwani kabla ya kuanza kushiriki katika ndondi za kulipwa na kuwatwanga mabondia wengi alitokea katika ujenzi wa mchezo huo kwenye ngumi za ridhaa ambako ndiko wanapotokea mabondia bora Tanzania na ulimwengu kwa ujumla.
Prince Nasseb ambaye ndiye anashikilia mkanda wa taifa wa PST, na ndiye alitakiwa kuzitwangwa na Tembo Mtoto,  anasema kifo cha bondia huyo ni pigo kubwa kwake kwani aliamini ndio alikuwa mpinzani wake aliyebaki katika uzito huo wa kilo 66, kutokana na wengi kuwa dhaifu kwake.
"Sikuweza kuamini baada ya kusikia kifo cha mpinzani wangu,  hali ambayo ambayo hadi leo bado inanipa shida kuamini kama ni kweli Tembo Mtoto amefariki, lakini kikubwa ni kumuombea Mungu ampumzishe kwa amani katika makazi ya milele," alisema.
Mratibu wa pambano hilo ambaye ndiye alikuwa kocha wa Tembo Mtoto, Faraji Ndame anasema kifo cha bondia huyo ni pigo katika klabu yake ya Kwame iliyopo Mburahati kutokana na kuw,a kinara wa kusshinda mapambano mengi.
"Ni bondia ambaye alikuwa na namtegemea katika mapambano mengi na siku ambayo anafariki, kwa kweli sikuamini hadi nilipothibitishiwa na daktari wa Hospitali ya Mwananyamala, kwani kabla hajaanguka wakati alipokuwa akifanya mazoezi ya kupiga begi nilikuwa nikimtazama kwa karibu.
"Hadi anaanguka nilikuwa nikimwona, nilipomfuata kumpa huduma ya kwanza alikuwa akitokwa povu na kizuia meno akawa ameking'ata, mdomo ukawa mgumu kufunguka, tulimtoa kizuia meno na kumvua viatu, kisha tukampeleka Hospitali ya Mwananyala, lakini tukaambiwa  amefariki," anasema.
Rais wa PST, Emmanuel Mlundwa akizungumza na Jambo Leo, kuhusu kifo hicho, alisema wamepokea kwa mshtuko,  lakini kazi ya Mola haina makosa, kinachopaswa kila mmoja kumuombea.
Ninachokifahamu kwa Tembo Mtoto ni kwamba, alikuwa bondia bora mwenye umri mdogo ambaye ndio kwanza alikuwa akiyafuta mafanikio, kwani mapambano mengi aliyocheza alikuwa akishinda kwa KO.
"Katika pambano lake la mwisho ambalo alipigana na Kea Kea alishinda kwa KO, nilikuwa mwamuzi wa mchezo huo, kikubwa ambacho naweza kusema, alikuwa bondia mzuri na atakumbukwa kwa kufanya vema," alisema.
Kocha wa kimataifa wa mchezo huo, Rajabu Mhamila 'Super D', anasema kifo cha Tembo Mtoto ni pigo kubwa katika tasnia ya ngumi kutokana na bondia huyo kuonesha kila dalili za mafanikio katika mapambano yake mengi.
"Kifo cha Tembo Mtoto, hakika kimenishtua kwani ni bondia niliyekuwa nikimfahamu tangu akiwa katika ridhaa, alikuwa akifuata ushauri kwangu," alisema.
"Alikuwa akiupenda mchezo husika, aliuheshimu, aliuthamini kama sehemu ya kazi yake, huku akifanya  mazoezi ya kutosha na kuuthamini mchango wake," anasema Super D.
Dk. Kulwa Killaga ambaye mara nyingi huwapima mabondia kabla ya mapambano, anasema kifo cha Tembo Mtoto kimemshtua, hasa baada ya kukubaliana mambo mbalimbali.
"Nilipozungumza naye mara ya mwisho, aliniomba niwe meneja wake, nikamshauri awe mbali na vitu vilivyo kinyume na maadili ya mchezo wa ngumi kwa lengo la kuepuka athari zinazoweza kujitokeza," anasema.
Anasema kuwa, mara nyingi alikuwa akilalamika kuhusu waratibu kuwapiganisha mabondia bila kufuata utaratibu wa muda wa pambano hadi pambano, madhara yake ni vifo.
"Mfano bondia kapigana wiki moja au mbili, kabla hajafikisha miezi mitatu anapigana tena, hali hiyo ni mbaya sana," anasema.
Anasema kuwa, waratibu wanatakiwa kudhibitiwa katika hilo ili kulinda maisha ya mabondia ambao wengi wao hawana elimu ya kutosha katika hilo na ndicho kinachowagharimu wengi. Pia, anawataka waachane na utumiaji wa bangi.
"Bangi ni kitu kingine kibaya kinachosababisha vifo kwa mabondia, hivyo wadau wa mchezo huo wanatakiwa kuwashauri mabondia wanaotumia madawa ya kulevya," anasema.
Bondia Fadhili Awadhi wa klabu ya Jitegemee, aliyewahi kutwangana na Tembo Mtoto, mwanzoni mwa mwaka huu, alisema kifo cha mwanamasumbwi huyo kimemhuzunisha.
"Niliwahi kupanda ulingoni na marehemu Tembo Mtoto enzi za uhai wake, nikamshinda kwa KO katika raundi ya nne, kifo chake kinanipa majonzi na wakati mwingine nashindwa kuamini," alisema.
Rekodi ya bondia huyo alipigana mapambano saba ya ngumi za kulipwa, alishinda mara nne na kupigwa mara moja na  kutoka sare mara mbili.
Tembo Mtoto alijiunga na ngumi za kulipwa mwaka 2011, akianza safari yake ya masumbwi kutwangana na Seba Temba wa Morogoro, pambano lingine lilikuwa Agosti na kufanikiwa kumtwanga Shujaa Keakea kwa TKO.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi, Amin

Kitimtim cha Ligi kuendelea kesho, Yanga kuvuna nini Mbeya, Simba kupigishana kwata na Mgambo, Azam,Ashanti Dar


Simba
Yanga

Azam
Ashanti United
 
Mgambo JKT

Na Boniface Wambura 
KIVUMBI cha Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara kitaingia raundi ya nne kesho (Septemba 18 mwaka huu) kwa mechi saba katika viwanja saba tofauti.

Vinara wa ligi hiyo, JKT Ruvu wanaonolewa na Kocha Mbwana Makata watakuwa ugenini Uwanja wa Mabatini, Mlandizi Pwani kuumana na 'ndugu' zao Ruvu Shooting ya Charles Boniface Mkwasa. 

Mechi hiyo inatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwa washabiki mkoani Pwani kutokana na aina ya soka inayochezwa na timu hizo.

Baada ya sare dhidi ya Mbeya City wikiendi iliyopita, Yanga inaendelea kubaki Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya ambapo itacheza na Tanzania Prisons katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Simon Mbelwa kutoka Pwani.

Nayo Simba itaumana na Mgambo Shooting Stars ya Tanga katika mechi itakayopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Mechi hiyo itakuwa chini ya Kamishna David Lugenge kutoka Iringa.

Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Oljoro JKT kutoka Arusha na wenyeji Kagera Sugar wakati Azam na Ashanti United zitakwaruzana kwenye uga wa Azam Complex ulioko Chamazi jijini Dar es Salaam.

Mwamuzi Jacob Adongo kutoka Mara ndiye atakayechezesha mechi kati ya Coastal Union na Rhino Rangers itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. 

Mtibwa Sugar inarejea uwanja wake wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro ambapo inaikaribisha Mbeya City ya Kocha Juma Mwambusi.

Wakati huo huo, Ligi Daraja la Kwanza (FDL) nayo inaendelea kesho (Septemba 18 mwaka huu) kwa mechi moja ambapo Lipuli ya Iringa ambayo wikiendi iliyopita ilicheza Mkamba mkoani Morogoro inapita mjini Morogoro kuikabili Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Kamati yafafanua uwakilishi wa wajumbe Mkutano Mkuu TFF



Na Boniface Wambura
KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesema uwakilishi wa ujumbe kwenye Mkutano Mkuu unaanzia kwenye chama cha mpira wa miguu cha mkoa, kufuatiwa na chama shiriki na baadaye klabu ya Ligi Kuu.

Mwongozo huo juu ya uwakilishi wa wajumbe kwenye Mkutano Mkuu umetolewa kutokana na maombi ya Sekretarieti ya TFF kwa kamati hiyo iliyokutana jana (Septemba 16 mwaka huu) baada ya kubaini baadhi ya wajumbe wanashikilia nafasi mbili kwenye vyama tofauti.

Kwa mujibu wa Ibara ya 5 ya Katiba, kuna makundi ya aina tatu ya wanachama wanaounda TFF. Makundi hayo ni vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu.

Sekretarieti ya TFF imebaini kuwa kuna baadhi ya viongozi wa kuchaguliwa wa mikoa ambao pia ni viongozi wa vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu, hivyo wana nafasi zaidi ya moja ya kuingia kwenye Mkutano Mkuu.

Hivyo, kutokana na mwongozo huo ushiriki wa wajumbe kwenye Mkutano Mkuu wa TFF utaanzia chama cha mkoa, kufuatiwa na chama shiriki na baadaye klabu za Ligi Kuu.

Pia nafasi ambazo zinaweza kuwakilishwa kwenye Mkutano Mkuu kama mhusika hayupo ni za Mwenyekiti atakayewakilishwa na Makamu Mwenyekiti, na Katibu atakayewakilishwa na Katibu Msaidizi.  Nafasi za ujumbe wa Mkutano Mkuu na ile ya mwakilishi wa klabu hazina uwakilishi kama mhusika hayupo.

Monday, September 16, 2013

Kivumbi cha Ligi ya Mabingwa Ulaya kuanza kesho, Moyes kuanza vipi?

Eti babu we ulikuwa unafanyaje mpaka ukatisha? Kama Moyes akimuuliza Sir Alex Ferguson

KIVUMBI cha Ligi ya Mabingwa wa Ulaya hatua ya makundi kinatarajiwa kuanza kesho, ambapo 'Mashetani Wekundu', Manchester United itaanza nyumbani dhidi ya Bayer Liverkusen ambapo mashabiki watataka kuona kocha David Moyes atavuna nini katika mechi yake ya kwanza katika michauno hiyo akiwa na Man Utd
Moyes aliyemrithi kocha mwenye mafanikio wa klabu hiyo aliyestaafu Mei mwaka huu, Sir Alex Ferguson atakuwa uwanja wa nyumbani wa Old Trafford, akiwa na kumbukumbu ya kukwama na Everton aliyokuwa akiinoakutinga hatua ya makundi msimu wa 2005-2006 baada ya kutolewa hatua ya mwisho wa mchujo kwa kung'olewa na Villarreal ya Hispania kwa jumla ya mabao 4-2.
Je, mbinu alizorithi toka kwa SAF zitamsaidia kuweza kufanya kweli kwenye kundi lake la A ambalo linaoonekana kuwa jepesi kulinganisha na mengine? Bila shaka ni suala la kusubiri kuona baada ya mechi hiyo ya kesho na nyingine za kundi lake lenye timu nyingine za Real Sociedad ya Hispania ambayo kesho pia itakuwa nyumbani kuialika Shakhtar Donetsk ya Ukraine.
Katika kivumbi hicho kesho pia itashuhudiwa mechi za makundi mengine matatu ya BC na Dna ratiba yake inaonyesha kuwa Galatasaray ya Uturuki itaumana na Real Madrid ambayo juzi ilimuongezea mkataba mpya nyota wake Cristiano Ronaldo na kumfanya awe mchezaji anayelipwa zaidi duniani, huku ikiwa na mchezaji ghali zaidi duniani kwa usajili Gareth Bale.
Pambano jingine la kundi B kwa kesho ni København  itakayoumana na Juventus, wakati mechi za kundi C itazikutanisha timu za Benfica ya Ureno dhidi ya Anderlecht ya Ubelgiji, huku Olympiakos Piraeus ya Ugiriki ikitarajiwa kuvaana na PSG ya Ufaransa.
Mabingwa watetezi, Bayern Munich ya Ujerumani yenyewe itaanza kibarua cha kutetea taji hilo iliyotwaa Mei mwaka huu kwa kuilaza Borussia Dotmund, nyumbani kuvaana na CSKA Moskva na Viktoria Plzeň itaialika Manchester City.
Keshokutwa Jumatano, kutakuwa na mechi nyingine za makundi manne yaliyosalia ambapo ratiba kamili ni kama ifuatavyo:
Schalke 04 vs Steaua BucharestChelsea   vs Basel
Olympique Marseille vs Arsenal
Napoli   vs Borussia Dortmund 
Austria Wien vs Porto
Atlético Madrid  vs Zenit
AC Milan vs Celtic
Barcelona  vs Ajax

Jeshi la Polisi Mbeya laonya mashabiki wa soka wenye vurugu


  RPC Mbeya, Diwani Athuman
 
JESHI la Polisi Mkoani Mbeya limewaonya mashabiki wa soka mkoani humo ambao Jumamosi walifanya vurugu kubwa na kusababisha kuutia doa mkoa huo katika medani ya soka.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi hilo mkoani humo limewaonya mashabiki hao kuwa kama watgaendelea kufanya 'upuuzi' wao kama walivyofanya katika pambano kati ya Mbeya City na Yanga basi watakiona cha moto.
 Jeshi hilo limelaani vurugu hizo ikidai linauchafua mkoa wao na pia ni tishio kwa Mbeya kuweza kufungiwa na hivyo kuwanyima mashabiki wa kweli wa soka kushuhudia mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Taarifa rasmi ya jeshi hilo la Polisi iliyotiwa saini na ASP P Mhako kwa niaba ya RPC Diwani Athuman isome mwenyewe hapo chini;
--
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA  KAMISHINA MSAIDIZI WA POLISI DIWANI ATHUMANI ANAWATAKA MASHABIKI NA WAPENZI WA MPIRA WA MIGUU WAACHE VITENDO VYA KUFANYA VURUGU KATIKA MICHEZO ITAKAYOKUWA IKIFANYIKA KATIKA UWANJA WA KUMBUKUMBU YA SOKOINE NA MKOA KWA UJUMLA, KWANI VURUGU HIZO ZITASABABISHA MICHEZO HIYO KUHAMISHIWA SEHEMU NYINGINE NA WAPENZI KUKOSA BURUDANI  PIA WANANCHI KUKOSA KIPATO, HIVYO KUUTANGAZA MKOA WETU VIBAYA. 
 
VURUGU ZILIZOTOKEA JUMAMOSI TAREHE 14/09/2013 KWA MASHABIKI KULISHAMBULIA GARI LA VIONGOZI WA TIMU YA YANGA LILILOKUWA LIMEPAKI NJE YA UWANJA PIA KULISHAMBULIA KWA MAWE GARI LILILOKUWA LIMEBEBA WACHEZAJI WA TIMU YA YANGA NA KUHARIBU KIOO CHA MLANGO WA DEREVA NA KUFANYA MAANDAMANO AMBAYO YAMESABABISHA USUMBUFU KWA WATUMIAJI WENGINE WA BARABARA SI CHA KIUNGWANA NA KISIJIRUDIE TENA KATIKA MICHEZO MINGINE.

KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA HAKURIDHISHWA NA VITENDO HIVYO NA KUWATAKA MASHABIKI NA WAPENZI WA MPIRA WA MIGUU KUWABAINI NA KUWATAMBUA  WALE WOTE WATAKAOFANYA VURUGU NA KULIJULISHA JESHI LA POLISI.

AIDHA JESHI LA POLISI HALITAVUMILIA VITENDO HIVYO NA KWA YEYOTE ATAKAYE/WATAKAO BAINIKA HATUA KALI ZA KISHERIA ZITACHUKULIWA ZIDI YAKE/YAO.

Signed by:
[P.A MHAKO – ASP]
Kny: KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

Vijana wa Airtel Rising Stars wakabidhiwa bendera

 Katibu Mkuu wa Shirikisho la mpira wa Miguu Tanzania,Angetile Osia (kushoto) akimkabizi bendera ya Taifa,kapteni wa timu ya vijana ya wasichana wa Artel Rising Stars,Stumai Abdallah timu hiyo inaondoka leo kuelekea Nigeria kushiriki mashindano ya Afrika ya Airtel Rising Stars.
 Katibu Mkuu wa Shirikisho la mpira wa Miguu Tanzania,Angetile Osia (kushoto) akimkabizi bendera ya Taifa,kapteni wa timu ya vijana ya wanaume wa Artel Rising Stars,Athanas Shindeka timu hiyo inaondoka leo kuelekea Nigeria kushiriki mashindano ya Afrika ya Airtel Rising Stars.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la mpira wa Miguu Tanzania,Angetile Osia (kushoto) akikabizi bendera ya Taifa,kwa timu za vijana za wasichana na wanaume wa Artel Rising Stars ,timu hiyo inaondoka leo kuelekea Nigeria kushiriki mashindano ya Afrika ya Airtel Rising Stars.

Wamalawi wamiminika uhamiaji kujiandikisha zoezi la utambuzi wa wahamiaji haramu

Raia wa Malawi wakijiandikisha katika Idara ya Uhamiaji, Mkoa wa Dar es Salaam leo kuhusu zoezi linaloendelea la kuwatambua wahamiaji haramu jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Felix Mwagara, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).


Baadhi ya raia wa Malawi wakiwa katika foleni ya kujiandisha leo kwenye ofisi za uhamiaji jijini Dar es salaam 
Zoezi la utambuaji ya wahamiaji  haramu likiendelea wahamiaji wakiwa katika ofisi ya uhamiaji leo jijini Dar es salaam

Ivory Coast vs Senegal, Ghana dhidi ya Misri Top 10 WC Afrika


SHIRIKISHO la Soka Afrika, CAF limetangaza ratiba ya mchujo wa mwisho kwa timu za nchi za Afrika kuwania kucheza Fainali za Kombe la Dunia za mwakani ambapo vinara wa kandanda Afrika na wababe wa Tanzania, Ivory Coast imepangwa kuanzia nyumbani dhidi ya majirani zao Senegal.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo ya CAF ni kwamba mechi za kwanza zitachezwa Oktoba 10 na zile za mwisho zitakazoa wawakilishi watano wa Afrika watakaoenda Brazil zitachezwa Novemba 14 mwaka huu.
Wakati Ivory Coast walionyakua nafasi ya kwanza katika kundi C lililokuwa na timu za Morocco, Tanzania na Gambia ikipangwa na Senegal iliyoiengua Uganda wiki iliyopita, wawakilishi wa ukanda wa CECAFA, Ethiopia yenyewe imepangwa na Nigeria na itaanza kibarua chake nyumbani mjini Addis Ababa.
Mechi nyingine itakzikutanisha Tunisia dhidi ya Cameroon, huku Burkina Faso kuumana na Algeria na Ghana watavaana na Misri.

Hawa ndiyo warembo walioingia Top 5 ya Redd's Miss Tanzania 2013

Warembo watano waliofanikiwa kuingia hatua ya nusu fainali ya Redd’s Miss Tanzania 2013 wakiwa katika picha ya pamoja jana. Kutoka kushoto  ni Miss Tanzania Photogenic 2013, Happiness Watimanywa, Miss Tanzania Talent 2013, Prisca Clement, Miss Tanzania Personality, Severina Lwinga, Miss Tanzania Top Model 2013, Narietha Boniface na Miss Tanzania Sports Woman, Clara Bayo. (Na Mpigapicha Wetu). 

Hafsa Kizinja amuenzi Mzee Gurumo kiaina

 Malkia wa Zouk nchini Hafsa Kazinja akiwa na Omari Mkali (kushoto) na Abdul Salvador baada ya kukamilisha kurekodi wimbo wa 'NIMUOKEOE NANI' katika Studio za OM Productions jijini Dar es salaam wikiendi hii.
Omary Mkali akiwa katika pozi la picha na Hafsa.
Hafsa Kazinje akiwa Studio.

DAR ES SALAAM, Tanzania
Baada ya ukimya wa muda mrefu,   Malkia wa Zouk Tanzania,  Hafsa Kazinja,  anaibuka upya katika fani akiwa na ingizo lake la kwanza kati  ya kumi aliyoandaa kwa kuimba wimbo maarufu wa NUTA Jazz Band uitwao “NIMUOKOE NANI”  anauouleta hewani katika mahadhi ya Zouk.

Hafsa Kazinja anasema ameamua kurudi ulingoni kwa kutoa wimbo huo ili kumuenzi Mzee Muhidin Maalim Gurumo ambaye amestaafu rasmi fani ya muziki baada ya kufanya kazi hiyo akiwa na bendi mbalimbali tokea mwaka wa 1960.

“Nimeamua kuimba wimbo huu wa “NIMUOKOE NANI” ili  kumuenzi gwiji huyu wa muziki kwani wakati yeye anastaafu na mimi ndiyo naibuka upya baada ya kukaa kimya kwa muda”, anasema Hafsa ambaye alitoka kwa wimbo wake wa “PRESHA” aliomshirikisha Banana Zorro.

Hafsa ameandaa wimbo huo wa “NIMUOKOE NANI” katika studio za OM Productions ya jijini Dar es salaam chini ya wanamuziki nguli, Abdul Salvador na Omari Mkali.
“Nafurahi kwamba wimbo wa NIMUOKOE NANI nimeuimba baada ya kupata Baraka zote toka kwa mtunzi na mwimbaji wake Mzee Gurumo mwenyewe.

“Haikuwa rahisi kama inavyoweza kudhaniwa kwani baada ya kwenda kumuona nyumbani kwake alinifanyisha mtihani wa kuuimba wote kabla ya kuridhika maana alisema asingefurahi kuona wimbo wake unaimbwa hovyo hovyo na kuharibiwa radha yake”, anasema Hafsa, ambaye hivi sana anamalizia ngoma zake zingine tisa alizotunga mwenyewe, kabla ya kuvamia anga kwa mara ingine.

Hafsa anasema katika ukimya wake amekuwa akifanya utafiti na kujifunza kwa undani zaidi fani ya muziki, akipata mawaidha maridhawa toka kwa wanamuziki nguli ndani nan je ya nchi wakiwemo Muhidin Maalim Gurumo, Omar Mkali, Abdul Salvador na Lokassa ya Mbongo wa Congo aliyekutana na kufanya naye kazi alipokuwa ziarani Marekani hivi karibuni.

Msanii huyu wa kizazi kipya anasema ataitambulisha rasmi ngoma ya “NIMUOKOE NANI” katika tamasha la kumuenzi Mzee Gurumo lililopangwa kufanyika OKtoba 1, 2013 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam.

“Natumaini wapenzi wa muziki watafurika kwa wingi kwenye tamasha hilo name naahidi kuitendea haki ngoma ya “NIMUOKOE NANI” hivyo wasikose kuja kujionea wenyewe jinsi sie wa kizazi kipya tunavyoweza kufanya kazi na wakubwa wetu wa kazi, anaongezea Hafsa ambaye pia anaandaa video yake pamoja na ya ngoma zake zingine mpya.

Mkongwe Abdul Salvador, ambaye alikuwa mmoja wa waanzilishi wa  bendi ya TANCUT ALMASI YA Iringa iliyotamba na mtindo wake wa “FIMBO LUGODA”, anamtaja Hafsa kazinja mmoja wa wanamuziki wa kike waliojaaliwa sauti nzuri na kipaji cha hali ya juu hapa nchini.

“Kwa kuweza kuimba wimbo wa Mzee Gurumo na kupatia kisawasawa inadhihirisha kwamba Hafsa ni mwanamuziki aliyekomaa maana si mchezo kuimba nyimbo ya wakongwe kwa ufasaha kama alivyofanya Hafsa.
“Na hii inadhihirisha kwamba uwezekano wa kizazi kipya na cha zamani kufanya kazi pamoja ni mkubwa sana na sioni kwa nini isiwe hivyo”, anasema Salvador.

Omari Mkali, aliyetamba na bendi ya CHUCHU SOUNDS, chini ya marehemu Yusuf Chuchu, naye anamwelezea Hafsa Kazinja kama moja ya majembe ya muziki hapa nchini kwa upande wa kinamama, na kwamba anaweza kufika mbali endapo kama moto aliokuja nao upya atauendeleza.

IMETOLEWA NA
OM PRODUCTIONS NA HISIA SOUNDS