STRIKA
USILIKOSE
Thursday, September 27, 2012
Cheka, Nyilawila kupimwa afya uzito kesho, kuvaana PTA J'mosi
BINGWA wa ngumi za kulipwa anayetambuliwa na ICB na IBF-Afrika, Francis Cheka na aliyekuwa bingwa wa Dunia wa WBF, Karama Nyilawila wanatarajia kupima uzito na afya zao kesho tayari kwa pambano lao la Jumamosi kuwania ubingwa wa UBO-Mabara.
Mabondia hao wanatarajiwa kupambana katika pambano la uzani wa Super Middle la raundi 12 kwenye ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam siku ya Jumamosi.
Mratibu wa pambano hilo, Robert Ekerege wa Afrika Kabisa Entertainment, alisema Cheka na Nyilawila watapimwa uzito na afya zao sambamba na mabondia wengine watakaowasindikiza kwenye pambano lao kwenye ukumbi wa Mawela jijini Dar.
Ekerege, alisema kupimwa kwa afya na uzito wa mabondia hao ni kuashiria kuiva kwa pambano hilo la kimataifa litakalochezewa na mwamuzi toka Malawi.
"Tunatarajia kuwapima afya na uzito wao mabondia wote watakaopigana Jumamosi, karibu mabondia wote wameshatua Dar tayari kwa zoezi hilo litakaloanza kufanyika saa 5 asubuhi ili kujiweka tayari kwa mchezo huo utakaofanyika PTA," alisema.
Aliongeza kuwa, maandalizi ya ujumla wa pambano hilo la Cheka na Nyilawila ambalo ni la tatu kwao kukutana na yale ya utangulizi yamekamilika ikiwemo kubadilisha mgeni rasmi wa siku hiyo kutoka Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo , Amos Makalla hadi kuwa Kamanda wa Kanda Maalum Dar, Afande Suleiman Kova.
Ekerege alisema wamemkosa Waziri Makalla waliokuwa wamempanga awali kwa vile atakuwa safarini na hivyo kumpa jukumu la kumvika mshindi wa pambano hilo la kesho Mlezi wa mchezo wa ngumi nchini, Kamanda Kova aliyethibitisha kushiriki.
Aliongeza kuwa katika mapambano hayo bendi maarufu ya Mashukaa Band 'Wana Kibega' ndio watakaotoa burudani ukumbini.
Mwisho
Arsenal, Man Utd, Liverpool zang'ara Kombe la Ligi
| Mchezaji Ignasi Miquel akishangilia bao lake dhidi ya Coventry City |
Arsenal iliisasambua Coventry City kwa mabao 6-1 kwenye pambano lililochezwa uwanja wa Emirates mjini London, wakati mahasimu wao Tottenham walipata ushindi wa magoli 3-0 dhidi ya Carlisle United ikiwa ugenini.
Manchester United wenyewe walipata ushindi wa mabao 2-1 wakiwa uwanja wa Old Trafford dhidi ya Newcastle United, wakati Liverpool ilitoka kupokea kichapo katika Ligi Kuu toka kwa wapinzani wao wa jadi Man United iliitafuna West Bromwich Albion kwa idadi kama hiyo ya mabao 2-1.
Mechi nyingine zilizochezwa jana WPR ilijikuta ikinyukwa nyumbani na Readind kwa mabao 3-2 na Norwich City iliilaza kwa bao 1-0 timu ya Doncaster Rovers.
Matokeo kamili ya mechi za michuano hiyo kwa siku ya jana ni kama ifuatavyo:
| Norwich City | 1-0 | Doncaster Rovers | |
| QPR | 2-3 | Reading | |
| Arsenal | 6-1 | Coventry City | |
| Celtic | 2-1 | Benfica | |
| Manchester United | 2-2 | Newcastle | |
| Carlisle United | 0-3 | Tottenham | |
| West Brom | 1-2 | Liverpool | |
| More: Scores | Fixtures | League Cup | |||
Coastal yatakata Mkwakwani, Toto ikiendeleza mdudu wa sare
MABAO mawili toka kwa mshambuliaji nyota na mzoefu, Nsa Job na jingine la Daniel Lyanga jana yaliipaisha timu ya Coastal Union hadi nafasi ya pili mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuilaza Kagera Sugar goli 3-2.
Huo ni ushindi wa pili kw atimu hiyo baada ya awali kufanya hivyo katika mechi ya fungua dimba la Ligi Kuu dhidi ya 'majirani' Mgambo Shooting kabla ya kutoka sare mbechi nyingine mbili.
Katika mfululizo wa ligi hiyo timu ya Toto Africans ya Mwanza imeendelea na mdudu wake wa sare baada ya jana kutoka suluhu ya bila kufungana na wenyeji wao Polisi Morogoro.
Hiyo ni sare ya nne kwa Toto Africans baada ya awali kufanya hivyo dhidi ya JKT Oljoro ilitoka sare ya 1-1, Azam 2-2 na kisha Mgambo Shooting mechi yao iliyopita.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea mwishoni mwa wiki kwa michezo kadhaa itakazozihusisha timu za Azam, Yanga na Simba ambazo kwa sasa zinawindana kwa ajili ya pambano lao litakalofanyika Jumatano ijayo jijini Dar.
Wednesday, September 26, 2012
SHINDALO LA UCHORAJI KWA TAASISI ZA KIELIMU
Shindalo la Uchoraji Kwa Taasisi za Kielimu
Image
Profession ikishirikiana na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kwa mara nyingine
inatangaza kuanza kwa muhula mpya wa pili wa Shindano ya Uchoraji maalumu kwa
Taasisi za elimu.
Shindano ambalo pia linajulikana
Kama: Educational Drawing Competition au Image Profession Educational Drawing Competition,
lina malengo ya kuibua vipaji katika fani ya uchoraji kwa kuzingatia uwekezaji
kwa watoto na vijana.
Theme/Wazo kuu la mwaka
huu: ART IMITATES LIFE au SANAA HUFUATISHA MAISHA
Makundi ya ushiriki
´ Chekechea,
´ Elimu ya Msingi,
´ Elimu ya Sekondari na
´ Elimu ya Juu
Kwa maelezo na taratibu
za Shindano tembelea Facebook Page/Group “Tanzania Drawing Competition” au wasiliana na BASATA au
DRAWING COMPETITION – IMAGE PROFESSION,
P O BOX 92 DAR ES SALAAM.
SIMU: +255 222 664 740 / +255 713 484 040
/ +255 714 676 217 / +255 716 430 084
EMAIL:
info@imageprofession.comKamanda Kova ambadili Waziri Makalla pambano la Cheka, Nyilawila
![]() |
| Kamanda Kova |
Mratibu wa pambano hilo litakalofanyika siku ya Jumamosi kwenye ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam, Robert Ekerege aliiambia MICHARAZO kuwa, kumekuwa na mabadiliko ya mgeni rasmi badala ya Waziri Makalla sasa atakuwa Kova ambaye ni mlezi wa ngumi Tanzania.
Ekerege alisema Kova amechukua nafasi ya Makalla kutokana na waziri huyo kupangiwa safari nje ya nchi ambayo itafanyika wakati pambano la Cheka na Nyilawila likifanyika PTA.
Mratibu huyo alisema kutokana na udhuru huo wameona ni vema nafasi hiyo achukue mlezi wao wa ngumi, Kamanda KOva ambaye ameshaitikia wito huo wa kuwa mgeni rasmi ambapo ndiye atakayemvisha mkanda mshindi wa pambano hilo la uzani wa Supermiddle la raundi 12 litakalochezwa na mwamuzi toka Malawi.
"Kwa sababu zilizo nje ya uwezo wetu, tumeamua kubadili mgeni rasmi wa pambano la jumamosi badala ya kuwa Waziri Makalla sasa ni Kamanda wa Kanda Maalum ya Mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova, Waziri atakuwa safarini na hivyo hataweza kuhudhuria kama tulivyotangaza awali," alisema Ekerege.
Aliongeza, ugeni wa Kova katika pambano lao limewaongezea uhakika wa ulinzi wa kutosha siku ya mchezo huo ambao unawakutanisha Cheka na Nyilawila kwa mara ya tatu katika safari yao ya ngumi baina yao.
Ekerege alisema maandalizi mengine yanaendelea kama kawaida ambapo mabondia wote watakaopanda ulingoni wanatarajiwa kupima afya na uzito wao kesho kwenye ukumbi huo tayari kwa pambano la Jumamosi ambalo linadhaminiwa na kinywaji cha Coca Cola na kondomu za Dume na litapambwa na burudani toka kwa Mashujaa Band waliopania kuwachezesha wapenzi wa ngumi mtindo wao wa 'Kibega'.
Manchester City hoi Kombe la Ligi, Chelsea yaua
![]() |
| Wachezaji wa Man City wakiwa hoi baada ya kujifunga moja ya mabao yaliyoizamisha jana mbele ya Aston Villa |
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya England, Manchester City, imeanza vibaya msimu kwa kung'olewa mapema kwenye michuano ya Kombe la Ligi baada ya kulazwa mabao 4-2 na Aston Villa, huku vinara wa ligi hiyo ya England, Chelsea ikitoa kichapo cha mabao 6-0 kwa 'Mbweha'.
Kipigo hicho toka kwa Aston Villa, kimempa wakati mgumu kocha wa Man City, Roberto Mancini, kwani ni dalili za kushindwa kurejea mafanikio iliyopata msimu uliopita ilipotwaa taji la Ligi Kuu baada ya miaka 50.
Matokeo mengine ya mechi za jana za michuano hiyo ya Kombe la Ligi ni kama ifuatavyo;
Bradford iliinyuka Burton Abilion mabao 3-2 katika muda wa nyongeza, Chelsea ilivuna ushindi wa mabao 6-0 kw Wolves, Crawley ilinyukwa mabao 3-2 na Swansea, Leeds United ikainyoa Everton magoli 2-1.
![]() |
| Wachezaji wa Chelsea wakishangilia moja ya mabao yao katika mechi ya Kombe la Ligi jana usiku |
Mgunda afuata nyayo za Saintfiet atimuliwa Coastal Union
| Hemed Suleiman 'Morocco' (kushoto) aliyetua Coastal Union |
Morocco, aliyekuwa akiinoa timu ya taifa ya Zanzibar, anatarajiwa kuiangalia Coastal ikicheza pambano lao dhidi ya Kagera Sugar litakalofanyika kwenye uwanja wa Mkwakwani, chini ya kocha wa makipa, Juma Pondamali aliyekuwa ameachiwa timu baada ya Mgunda na msaidizi wake, Habib Kondo kutimuliwa.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jijini, uongozi wa Coastal ulifikia maamuzi hayo katika kikao kilichofanyika jana asubuhi na kwamba wamewatimua kufuatia kutoridhishwa na kiwango cha wachezaji wa timu hiyo licha ya kutofungwa mechi.
"Tayari wameshajulishwa maamuzi haya na Morocco atakuwa jukwaani kesho na ndiye atakayeongoza jahazi," alisema kiongozi mmoja wa juu wa timu hiyo.
Chanzo hicho kilisema kuwa katika mchezo wa leo, kocha wa makipa, Juma Pondamali ndiye atakayeiongoza timu hiyo na wanaamini mabadiliko yatazaa matunda.
Mgunda mwenyewe alinukuliwa jana akidai kuwa ameamua kujiondoa Coastal kwa nia njema na mapenzi mkubwa aliyonayo kwa timu hiyo aliyowahi kuichezea kwa mafanikio enzi zake za uchezaji.
Mgunda alisema aliona ni bora ajiondoe kutokana na shinikizo kubwa lililopo ndani ya Coastal ambayo imejiwekea malengo makubwa katika msimu huu wa ligi na kuwataka mashabiki na viongozi wa timu hiyo kumheshimu na kuyaheshimu maamuzi yake yaliyokuja wakati Coastal ikiwa nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi kutokana na kushinda mechi moja na kupata sare mechi mbili.
Simba yaenda Zenji kuiwinda Yanga, Jangwani wakimbilia Bagamoyo

MABINGWA watetezi wa soka nchini Simba imeondoka jijini jana kuelekea Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi ya kujiwinda na pambano lao na watani zao Yanga litakalochezwa Jumatano ijayo.
Timu hizo mbili zinatarajiwa kukutana katika pambano la kwanza kwa msimu huu litakalochezwa kwenye uwanja wa Taifa na kurushwa 'live' na kituo cha Super Sport, huku Yanga ikiwa na deni kubwa la kipigo cha mabao 5-0 iliyopata katika pambano baiona yao lililofungia msimu uliopita.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu', alinukuliwa jana kuwa wachezaji wote 29 wa timu hiyo wameondoka na wanatarajia kurejea keshokutwa kwa ajili ya kuvaana na Prisons ya Mbeya kabla ya kurejea tena visiwani humo kuweka kambi hadi siku ya mchezo wao na Yanga.
Alisema kuwa wakiwa Zanzibar wataendelea kufanya mazoezi ya ufukweni na ya uwanjani na wanaamini kambi yao itazaa mafanikio kwa kushinda mechi hizo zinazowakabili.
Wakati Simba ikienda kujichimbia Zenji, watani zao walikuwa katika mchakato wa kuelekea mjii Bagamoyo kwa ajili ya kujiandaa na pambano hilo la watani zao na lile la Jumamosi ijayo itakapoumana na African Lyon.
Yanga imepania kulipa kisasi cha mabao hayo 5-0 iliyofungwa na Simba Mei 6, lakini pia wakiwa na deni la miaka zaidi ya 30 ya kipigo cha mabao 6-0 ilichopewa na Simba mwaka 1977.
YANGA HATARINI KUSHUSHWA DARAJA - MADENI YA PAPIC NA NJOROGE YAWAPONZA FIFA
![]() |
| Kikosi cha Yanga kilichopo hatarini kiushushwa daraja |
![]() |
| Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Oseah |
Tumepokea
barua kutoka Kitengo cha Sheria cha Shirikisho la Kimataifa la Vyama
vya Mpirawa Miguu (FIFA) likitutaka tuitaarifu Yanga kuhusu mashtaka
yaliyowasilishwa na kocha wazamani wa klabu ya Yanga, Kostadin Papic.
Katika malalamiko yake, Papic anadai kuwa hajalipwa malimbikizo ya
mshahara wake yanayofikia kiasi cha Dola 12,300 za Kimarekani. Katika
barua yake, kocha huyo anadai kuwa alikuwa akiwasiliana na maofisa na
viongozi wa Yanga, lakini hakupata ushirikiano na hivyo kuamua kwenda
FIFA. TFF ilifanya juhudi za kuwasiliana na Yanga kuhusu malalamiko hayo
ili kujaribu kumzuia kocha huyo asishtaki FIFA, lakini juhudi hizo
hazikuzaa matunda.
Kama
chombo kinachosimamia uendeshaji wa mpira wa miguu nchini, TFF
imesikitishwa na habari hizo na inaiomba klabu ya Yanga kufanya kila
jitihada kuhakikisha kuwa inawasilisha taarifa zote muhimu na nyaraka
zinazohusiana na stahiki za kocha huyo ili kama ilishamalizana naye,
sifa ya klabu ya Yanga isafishwe. Tayari barua imeshaandikwa kwa klabu
ya Yanga kuitaka itekeleze utashi huo mapema iwezekanavyo.
Tukio
hilo, si tu linachafua sifa ya klabu ya Yanga, bali soka ya Tanzania
kwa ujumla kutokana na ukweli kwamba ikishadhihirika kuwa kuna tatizo la
malipo ya makocha nchini, ni dhahiri kuwa itakuwa ni vigumu kwa klabu
zetu na hata timu za taifa kupata makocha wazuri kutoka nje kwa kuwa
watakuwa wamejengeka hofu ya kufanya kazi nchini.
Hili
ni tukio la pili kwa Yanga baada ya mchezaji wake mwingine, John
Njoroge kuishtaki klabu hiyo FIFA na kushinda kesi yake iliyoamuliwa
mwezi Januari na Kitengo cha Usuluhishi wa Migogoro cha FIFA (DRC).
Ushindi wa Njoroge unamaanisha kuwa iwapo Yanga itashindwa kutekeleza
kumlipa mchezaji huyo kasi cha Sh milioni 17, inaweza kujikuta katika
adhabu ambayo itatulazimisha tuishushe daraja; kuinyang’anya pointi kwa
kiwango kitakachotajwa na FIFA; kuipiga faini au adhabu zote kwenda kwa
pamoja. Tunaiomba Yanga itekeleze hukumu hiyo kwa wakati uliotajwa
kwenye barua ya FIFA ili kuepuka hatua hizo.
Suala
la Njoroge ni moja kati ya matukio mengi yanayohusu ukiukwaji wa
taratibu za kuvunja mikataba yanayofanywa na klabu zetu. Kuna malalamiko
ya wachezaji wengi dhidi ya klabu zao za zamani kuhusu kutolipwa
stahiki zao. Hivyo TFF inatoa wito kwa klabu kujiepusha na vitendo hivyo
kwa kuwa vinawanyima haki wachezaji, lakini pia vinachafua sifa ya nchi
iwapo wachezaji wanachukua hatua za kwenda kwenye vyombo vya juu.
Tumekuwa
tukisoma kwenye vyombo vya habari kuhusu kutimuliwa kwa sekretarieti
nzima ya Yanga kutokana na kuonekana kuwa ina udhaifu. Taarifa hizo
hazijaifikia rasmi TFF. Kiutaratibu, Yanga inatakiwa iwsasilishe majina
ya maofisa watakaofanya kazi na TFF kwa sasa na itakapoajiri
sekretarieti ya kudumu, basi itume barua nyingine ya kuwatambulisha
watendaji wake.
Kama
itakuwa imeitimua sekretarieti nzima, basi TFF inapokea taarifa hizo
kwa masikitiko makubwa. Si nia ya TFF kutetea watendaji wazembe, lakini
klabu hazina budi kufuatilia kwa karibu utendaji wa sekretarieti zao ili
isije ikafikia wakati sekretarieti nzima inaondolewa kwa makosa ambayo
yangeweza kusahihishwa kama kungekuwa na ufuatiliaji wa karibu. TFF
imekuwa ikitoa mafunzo kwa watendaji wa klabu ili waweze kufanya kazi
zao vizuri na kwa mintaarafu ya mpira wa miguu na hivyo kuondolewa kwa
timu nzima kama hiyo kunamaanisha kuwa ni upotevu wa rasilimali ambayo
imetumika kuwapa elimu ya kutenda kazi zao vizuri. TFF ilishafanya kozi
ya Event Management kwa ajili ya watendaji wa klabu; semina ya kuangalia
upya maazimio ya Bagamoyo kwa watendaji na viongozi na pia kozi ya
utawala hivyo haipendi juhudi hizi zipotee
kirahisi.
Angetile Osiah
KATIBU MKUU
Monday, September 24, 2012
Vincent Barnabas akiri ligi ngumu msimu huu
![]() |
| Vincent Barnabas (kushoto) akiwa dimbani na timu ya taifa , Taifa Stars |
WINGA machachari wa timu ya soka ya Mtibwa Sugar, Vincent Barnabas amesema matokeo ya mechi za awali za Ligi Kuu Tanzania Bara zimeonyesha jinsi gani msimu huu utakuwa na ligi ngumu isiyotabirika kirahisi.
Aidha nyota huyo aliyewahi kutamba na timu za Kagera Sugar, Yanga na African Lyon, ameitabiria klabu yake ya Mtibwa Sugar kufanya vema tofauti na msimu uliopita ilipomaliza ikiwa nafasi ya nne.
Akizungumza na MICHARAZO, Barnabas, alisema kwa mechi za raundi tatu zilizokwisha kucheza mpaka sasa inaonyesha wazi ligi ya msimu huu sio nyepesi kama watu walivyokuwa wakiifikiria.
Nyota huyo alisema kutokana na mwenendo wa ligi hiyo, ni vigumu kutabiri mapema nani anayeweza kuwa bingwa kwa vile ligi bado haijatulia.
"Sio siri msimu huu ligi imeanza kuonyesha ni ngumu kwa aina ya matokeo yaliyopatikana, naamini ugumu huu umetokana na klabu zote kujipanga vema na kusaidia kuongeza ushindani," alisema.
Juu ya Mtibwa ambayo ilianza kwa sare dhidi ya Polisi Moro kabla ya kuilaza Yanga mabao 3-0 na kuzimwa na Azam mwishoni mwa wiki kwa bao 1-0, winga huyo alisema anaamini itafanya vema msimu huu tofauti na ligi iliyopita.
"Kwa namna tulivyo, naamini tutafanya vema, licha ya ugumu unaoonekana kwenye ligi ya msimu huu, wachezaji tumejipanga kuipigania timu ili imalize msimu tukiwa katika nafasi bora zaidi ya msimu uliopita," alisema Barnabas.
Kwa matokeo ya mwishoni mwa wiki, Mtibwa imejikuta ikiachwa nafasi ya sita ya msimamo ikiwa na pointi nne sawa na ndugu zao za Kagera Sugar na Yanga iliyozinduka kwa kuilaza JKT Ruvu mabao 4-1, ikizizidi uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Mwisho
Mashali, Sebyala kumkumuka Mwl Nyerere kwa masumbwi Dar
| Med Sebyala wa Uganda akiwa na taji lake la ubingwa wa Uganda |
| Thomas Mashali wa Tanzania akiwa na ubingwa wake wa TPBO |
BONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchini, Thomas Mashali anatarajia kuzidunda na Mganda Med Sebyala katika pambano la kuwania taji la Afrika Mashariki siku ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.
Pambano hilo la uzati wa kati la raundi 10 limepangwa kufanyika Oktoba 14 kwenye ukumbi wa Friends Corner, Manzese Dar es Salaam.
Mratibu wa pambano hilo litakalosimamiwa na Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania, TPBO, Regina Gwae alisema tayari wameshamalizana na mabondia hao kwa ajili ya pambano hilo la kimataifa.
Regina, alisema pambano hilo ni fursa nzuri kwa Mashali anayeshikilia ubingwa wa Taifa wa TPBO kujitangaza kimataifa iwapo atafanikiwa kumnyuka Sebyala.
“Huwezi kwenda nje kama ndani hufanyi vizuri na huwezi kwenda Ulaya, iwapo unashindwa kutamba Afrika Mashariki, hivyo tumeona tumpe Mashali mchezo huu ili akifanya vyema aweze kuvuka mipaka ya sasa, "alisema Regina.
Regina alisema ana matumaini mpambano huo utakuwa mzuri na utakaovutia kutokana na ukweli mabondia wote wawili wana sifa zinazofanana waking'ara ndani ya nchi zao.
Alisema Sebyala ni mmoja wa bondia wazuri waliowasumbua baadhi ya nyota wa ngumi nchini kama Rashid Matumla na Francis Cheka aliowahi kuja kucheza nao hapa nchi katika mechi za zisizo za ubingwa.
Mratibu huto aliwaomba wafadhili wajitokeze kwa ajili ya kudhamini mchezo huo unatarajiwa kuwa na mapambano ya utangulizi.
Mwisho
Maugo kuwania ubingwa wa WBF Arusha
| Bondia Mada Maugo |
BONDIA nyota wa ngumi za kulipwa nchini, Mada Maugo anatarajiwa kupanda ulingoni mjini Arusha kuzichapa na Mustapha Katende kutoka Uganda katika pambano la kuwania ubingwa wa Mabara wa WBF.
Pambano hilo la uzani wa Super Middle la raundi 12 litafanyika Oktoba 28 kwenye ukumbi wa Triple A, jijini humo na kusindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi pamoja na burudani ya muziki wa kizazi kipya.
Akizungumza na MICHARAZO leo asubuhi, Maugo alisema awali pambano hilo litakalosimamiwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania, PST, lilikuwa limkutanishe na bondia toka Iran, Gavad Zohrenvard.
Maugo alisema hata hivyo bondia huyo wa Iran amepatwa na dharura na hivyo kupangiwa Mganda ili kuonyeshana nae kazi siku ya pambano hilo.
"Natarajia kupanda ulingoni Oktoba 28 kwenye ukumbi wa Triple A mjini Arusha kuzichapa na Mganda, Mustapha Katende, ambapo pia tutasindikizwa na michezo mbalimbali ya utangulizi," alisema.
Alitaja baadhi ya mabondia watakaowasindikiza siku hiyo ni Robert Mrosso wa Arusha atakayepigana na Selemani Said 'Tall' wa Dar na Abbas Ally wa Arusha dhidi ya Joseph Marwa wa Zanzibar.
Bondia huyo aliyepanda mara ya mwisho ulingoni April mwaka huu kuwania ubingwa wa IBF-Mabara dhidi ya Francis Cheka na kupigwa, alisema amejiandaa vya kutosha kuweza kunyakua taji hilo la WBF dhidi ya Mganda.
"Naendelea kujifua kwa ajili ya kuhakikisha natwaa taji hilo, sambamba na kusaidia kutoa hamasa kwa vijana wenye vipaji vya ngumi mkoani Arusha," alisema Maugo.
Mwisho
WAZIRI MAKALLA MGENI RASMI PAMBANO LA CHEKA< NYILAWILA
![]() |
| Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Amos Makalla atakayekuwa mgeni rasmi katika pambano la ngumi la kuwania ubingwa wa UBO Mabara kati ya Francis Cheka na Karama Nyilawila |
NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni Vijana na Michezo, Amos Makalla anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wa pambano la kimataifa la kuwania ubingwa wa Mabara wa UBO kati ya mabondia Francis Cheka na Karama Nyilawila.
Pambano hilo litafanyika kwenye ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam Septemba 29, na waratibu wa mchezo huo, kampuni ya Afrika Kabisa Entertainment wamesema Waziri Makalla ndiye atakayemvisha taji mshindi.
Promota Robert Ekerege, aliiambia MICHARAZO kwamba tayari amehakikishiwa na Waziri Makalla kuwa mgeni rasmi katika pambano hilo la Super Middle la raundi 12 amblo litasindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi.
"Mgeni rasmi katika pambano letu kati ya Cheka na Nyilawila atakuwa Naibu Waziri wa Michezo, Amos Makalla, na kila kitu kimekamilika katika maandalizi ya pambano hilo," alisema Ekerege.
Ekerege alisema mbali na Waziri Makalla, pia siku ya pambano hilo litahudhuriwa na Mlezi wa mchezo wa ngumi nchini, Suleiman Kova ambaye ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa, katika kunogesha pambano hilo mabondia kadhaa karibu 10 watapanda ulingoni kuwasindikiza akina Cheka kwa kucheza michezo ya raundi sita kila moja na wa watasindikiza na burudani toka Mashujaa Band.
"Mashujaa Band ndio watakaosindikiza michezo hiyo yote ambayo itakuwa na ulinzi wa kutosha ili kudhibiti vitendo vyote vya kihuni ambavyo vinaweza kutuharibia," alisema Ekerege.
Mwisho
VAN PERSIE AIZAMISHA LIVERPOOL, ARSENAL WAISHIKA MANCHESTER CITY, DEMBA BA HASHIKIKI...MILAN, INTER HOI!
LONDON, England
PENATI ya Robin van
Persie kuelekea mwishoni mwa mechi iliipa Manchester United iliyocheza chini ya
kiwango ushindi wa ugenini wa 2-1 dhidi ya wachezaji 10 wa Liverpool katika
mechi yao iliyojaa hisia ya Ligi Kuu ya England kwenye Uwanja wa Anfield huku mabingwa
watetezi, Manchester City wakishikiliwa kwa sare ya nyumbani ya 1-1 dhidi ya
Arsenal leo.
Mholanzi Van Persie
aliwahakikishia ushindi Man U wakati alipopiga penati ya shuti kali
iliyomshinda kipa Pepe Reina kufuatia Glen Johnson kumuangusha Antonio
Valencia.
Licha ya kucheza
chini ya kiwango, Man U walipanda hadi katika nafasi ya pili katika msimamowa
ligi wakiwa na pointi 12, wakizidiwa kwa pointi moja tu na vinara Chelsea.
Man City walipata
sare ya tatu katika mechi zao tano za mwanzo wa msimu baada ya Laurent Koscielny kuisawazishia Arsenal kwa
bao la 'usiku' kufuatia goli la utangulizi la Joleon Lescott kuwapa wenyeji
uongozi hadi mapumziko. Timu zote mbili hazijafungwa na kufikisha pointi tisa.
Tottenham Hotspur
wamefikisha pointi nane baada ya Jermain Defoe kuwafungia bao la ushindi wa 2-1
dhidi ya Queens Park Rangers, ukiwa ni ushindi wa kwanza wa nyumbani wa
Tottenham chini ya kocha Andre Villas-Boas.
Demba Ba alifunga bao
pekee lililowapa Newcastle United ushindi wa 1-0 dhidi ya Norwich City
inayonolewa na kocha wao wa zamani, Chris Hughton.
Hiyo ilikuwa ni mechi
ya kwanza kwenye Uwanja wa Anfield tangu kutolewa kwa taarifa ya Hillsborough iliyowasafisha mashabiki wa
Liverpool ambao awali walikuwa wakilaumiwa kwa kusababisha vifo vya mashabiki
96 kwenye mechi yao ya nusu fainali ya Kombe la FA mwaka 1989.
Balaa kwa Liverpool
lilianza katika dakika ya 39 wakati mchezaji wao Jonjo Shelvey alipotolewa nje
kwa kadi nyekundu.
Hata hivyo, Liverpool
walipata bao walilostahili baada ya kuanza kipindi cha pili kupitia shuti la
Steven Gerrard, lakini Man U wakasawazisha dakika sita baadaye kupitia shuti la
"upinde" la beki Rafael.
Bao la 'usiku' la Van
Persie, ambalo ni la tano kwake msimu huu, limemuacha kocha Brendan Rodgers
akikosa ushindi baada ya mechi tano za mwanzo wa msimu, ikiwa ni rekodi
"mbovu" kabisa katika historia ya klabu hiyo kwenye Ligi Kuu ya
England.
Yanga kupokwa ushindi dhidi ya JKT Ruvu?
![]() |
| Kikosi cha timu ya Yanga |
LICHA ya kuchekelea ushindi wa mabao 4-1 iliyopata dhidi ya JKT Ruvu, mabingwa wa Kombe la Kagame, Yanga huenda wakapokwa ushindi wao huo iliyopata juzi kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar iwapo itabainika wakikiuka kanuni za ligi juu ya idadi ya wachezaji wa kigeni kucheza mechi moja.
Yanga katika mechi yao na JKT iliwachezesha wachezaji wake wote watano wa kigeni, kitu kinachoelezwa ni kinyume na kanuni inayoruhusu klabu kuwatumia wachezaji wasiozidi watatu kucheza mechi moja ya ligi.
Katika pambano hilo la juzi Yanga iliwachezesha mapro wake wote akiwamo kipa Yew Berko, beki Mbuyu Twite, kiungo Haruna Niyonzima, mshambuliaji Didier Kavumbagu na winga Hamis Kiiza.
Micharazo, imedokezwa kwamba uongozi wa Simba tayari unajiandaa kuwasilisha barua ya kupinga kitendo kilichofanywa na watani zao za kuwatumia wachezaji wake hao wa kigeni katika mechi moja, ingawa tunaendelea kufuatilia kuona kama Yanga ilikiuka kanuni ya ligi kuhusu wachezaji au la...
Kama itakuwa imekiuka kuna uwezekano Yanga wakajikuta wakipokwa ushindi huo na kuzidi kuwasononesha baada ya kutoka kwenye machungu ya kushindwa kufurukuta katika mechi zao za awali ambapo ililazimishwa suluhu na Prisons Mbeya kabla ya kulala mabao 3-0 kwa Mtibwa Sugar.
Simba yazidi kupaa Ligi Kuu Tanzania Bara
| Amri Kiemba wa Simba ajijaribu kumtoka beki wa Ruvu katika pambano lao la jana |
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,
Simba, wameendeleza wimbi la ushindi wa asilimia 100, baada ya kuibuika na
ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting, pambano lililochezwa leo kwenye Uwanja
wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Simba ilipata bao la kuongoza dakika ya 30, likiwekwa
nyavuni na nyota wa kimataifa wa Zambia, Sunzu kwa kichwa maridadi akimalizia
krosi iliyopigwa baada ya kazi nzuri ya kuwachambua mabeki iliyofanya na Said
Nassor ‘Cholo’ aliyepanda kusaidia mashambulizi.
Dakika 38, Kiemba akawachachafya wachezaji wa Ruvu, kabla ya
krosi yake kukosa mmaliziaji na kuishia mikononi mwa Benjamin Haule.
Simba iliendelea kushambulia ambapo katika dakika ya 44, beki Mau
Bofu wa Ruvu alimwangusha Sunzu ndani ya 18 na mwamuzi Swai kuamuru ipigwe penati. Akuffor
akabeba jukumu la kupiga tuta hilo, ambalo mlinda mlango Haule alipangua na
kuwa kona tasa.
Hadi mapumziko, Simba ilitoka ikiongoza kwa bao hilo, huku
mashabiki waliohudhuria mechi hiyo wakishuhudia maamuzi tata ya mwamuzi Swai,
aliyeonekana dhahiri kutowajali vibendera wake Samwel Mpenzu na Godfrey Kihwili
wote wa Arusha pindi wanapoashiria madhambi.
Kipindi cha pili kilianza kwa Ruvu kushambulia lango la
Wekundu na kama si umakini mdogo miongoni mwa washambuliaji wake Paul Ndauka,
Hussein Said na Hassan Dilunga aliyekuwa akipenya kirahisi safu ya ulinzi,
wangeweza kupata mabao.
Sunzu akafanya shambuliazi kali dakika ya 55 lililotokana na
jitihada binafsi akiwalima chenga mabeki, kabla ya Ruvu nao kurudi langoni mwa
Simba na Dilunga (Hassani) nusura aipatie bao timu yake, kabla ya mawasiliano
madogo na Abdulrahman Mussa kumgharimu.
Ruvu ikapata bao la kusawazisha mnamo dakika ya 78,
lililowekwa nyavuni na mtokea benchi Seif Rashid, akitumia makosa ya beki Juma
Nyoso wa Simba, aliyeshindwa kuondoa hatari langoni akiwa peke yake na
kuukanyaga mpira huo na kuteleza, ambapo Seif aliunasa na kumchambua Juma
Kaseja.
| Daniel Akuffor akimtoka beki wa Ruvu Shooting |
Wakati wengi wakimiani matokeo ya pambano hilo yangebaki
kuwa ni sare ya bao 1-1, mtokea benchi wa Simba, Christopher Edward aliyeingia
kuchukua nafasi ya Akuffor, akaipatia timu yake bao la pili dakika ya 87 kwa
shuti na kuamsha mamia ya mashabiki wake jukwaani.
Saturday, September 22, 2012
Minziro amrithi Saintfeit, Mwalusako arejeshwa Jangwani
![]() |
| Lawrance Mwalusako |
Taarifa zilizopatikana mapema leo leo asubuhi inasema kuwa, Mwalusako atakaimu nafasi ya ukatibu Mkuu iliyokuwa ikishikiliwa na Celestine Mwesigwe,huku Sekilojo Chambua akiteuliwa kuwa meneja wa timu na mtangazaji wa Cloud's, Abdul Mohammed akimrithi Louis Sendeu aliyekuwa amemaliza mkataba wa kuwa Afisa Habari wa Yanga.
Kutokana na mabadiliko hayo leo Yanga itashuka dimba la Taifa kuvaana na JKT Ruvu ikiwa chini ya safu mpya ya benchi lake la ufundi, Minziro akiongoza kama kaimu kocha Mkuu.
| Fred Felix Minziro |
MECHI ZA ‘LIVE’ SUPER SPORTS LIGI KUU TANZANIA BARA
Septemba 21, 2012
MUDA WA MECHI ZA ‘LIVE’ SUPER WEEKEND
Mechi tano za Ligi Kuu ya Vodacom za Super Weekend katika mzunguko wa kwanza zitakazooneshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Super Sport zitaanza kati ya saa 1-.30 jioni na saa 1 kamili usiku.
Septemba 28 mwaka huu kutakuwa na mechi kati ya Azam na JKT Ruvu itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 1 kamili usiku. Mechi ya Simba na Tanzania Prisons itakayochezwa Septemba 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itaanza saa 11 kamili jioni.
Yanga na African Lyon zenyewe zitapambana Septemba 30 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11 kamili jioni wakati Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar zitaoneshana kazi Oktoba 1 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni.
Mechi ya mwisho katika Super Weekend itakuwa Oktoba 3 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwakutanisha watani wa jadi Yanga na Simba, na itaanza kutimua vumbi saa 1 kamili usiku.
TWFA YATANGAZA KAMATI YA UCHAGUZI
Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) kimetangaza Kamati ya Uchaguzi yenye wajumbe watano kwa ajili ya uchaguzi wake unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.
Kaimu Mwenyekiti wa TWFA, Margreth Mtaki amewaambia Waandishi wa Habari, Dar es Salaam leo kuwa kamati hiyo itaongozwa na Ombeni Zavala, na itarajia kutangaza mchakato wa uchaguzi huo Jumatatu (Septemba 24 mwaka huu).
Aliwataja wajumbe wengine wa kamati hiyo yenye jukumu la kuendesha uchaguzi wa chama hicho kuwa ni Rachel Masamu, Lloyd Nchunga, Nancy Mabula na Maneno Tamba.
Pia aliwataka wadau wa mpira wa miguu wa wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika TWFA mara Kamati ya Uchaguzi itakapoanza mchakato.
Wakati huo huo, uchaguzi wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Kilimanjaro (KRFA) na Manyara (MARFA) unafanyika kesho (Septemba 22 mwaka huu).
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Mpasuko wa kisiasa waibuka tena Zanzibar
Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar
CHAMA cha Wananchi CUF kimesema kimegundua kuna viongozi wa SMZ hawataki maridhiano yaliyozaa serikali ya Umoja wa Kitaifa, Novemba mwaka 2010.
Tamko hilo limetolewa na Mkurugenzi wa habari, Uenezi na mawasiliano ya umma wa CUF jana Salim Bimani Abdalla, kufuatia vurugu zilizotokea katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu Septemba 16 mwaka huu.
Alisema kwamba chama hicho tayari kimewafahamu baadhi ya Viongozi kutoka CCM wanaopinga serikali ya Umoja wa kitaifa na tayari wanajitayarisha kuwashitakia kwa wananchi kupitia vyombo vya kutunga sheria Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) na Bungeni.
Alisema kwamba hatua hiyo itasadia wananchi kuwatambua viongozi wenye kinyongo na mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ambayo yaliruhusu mfumo wa mpya wa serikali ya pamoja.
“Kuna Viongozi wa Serikali hawataki maridhiano yalioleta serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar tumewafahamu kupitia uchaguzi wa Bububu,”alisema Bimani.
Alieleza kwamba vurugu za askari wa Vikosi kutumia nguvu kubwa ikiwemo kutisha watu kwa risasi za moto ni ushaidi wa kuwepo kuwepo viongozi ambao hawataki kubadilika na kumaliza siasa za uhasama visiwani humo.
Alisema kwamba hakutegemea vikosi vya SMZ kutumia nguvu kubwa ikiwemo kutumia risasi za moto kupiga hewani wakati Vikosi hivyo vipo chini ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais (IKULU).
Aidha alisema kwamba katika kampeni za uchaguzi huo kuna viongozi wa CCM walitumia majukwaa vibaya ikiwemo kutoa lugha za matusi dhidi ya viongozi wa CUF wanaoshiriki kuunda serikali ya Umoja wa kitaifa.
Akizungumzia tuhuma hizo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema tuhuma za CUF hazina msingi wowote na zimelenga kuficha ukweli na kuwadaganya wananchi.
Alisema kwamba chimbuko la vurugu katika uchaguzi huo limetokana na Viongozi wa CUF kupeleka Vijana 3000 usiku wa kuamkia uchaguzi na kuwapa kazi ya kutisha watu ikiwemo kuhakiki wapiga kura waliokuwa wanajitokeza wakiwa katika magari kinyume na sheria ya uchaguzi.
Vuai alisema kwamba vijana wa CUF walikuwa wakizuia watu kwenda kupiga kura hasa wafuasi wa CCM na kutoa vitisho kabla ya askari kuamua kuwatawanya katika maeneo ya vituo vya wapiga kura.
Vuai alisema kwamba wangalizi wa uchaguzi kutoka CUF wakiwemo mawaziri baadhi yao walifanya kazi kukagua kadi za wapiga kura wakati sio majukumu yao.
Alisema kwamba sheria za uchaguzi zilianza kuvunjwa mapema na baadhi ya Mawaziri wa CUF kutokana na kutumia magari ya umma wakati wa kampeni na uchaguzi kinyume na sheria na misingi ya Utawala bora.
Alisema kwamba CCM ilitarajia kuwa CUF watafanya kampeni za kistarabu baada ya kumaliza tofauti za kisiasa tangu kuuda serikali ya pamoja, lakini wameshindwa kubadilika na kuendeleza siasa za chuki na uhasama kinyume na mataraji ya wananchi.
Vuai alisema kwamba katika uchaguzi huo watu wenye asili ya Pemba awakuhojiwa uhalali wa kupiga kura tofauti na watu wenye asili ya Bambi, Makunduchi au Donge katika uchaguzi huo.
Vuai alisema akiwa kama muasisi wa muafaka kutoka CCM anajuta kwa kupoteza muda kutafuta amani ya Zanzibar baada ya kuibuka wanasiasa wanaorudisha siasa za chuki na ubaguzi na kuvuruga amani na Umoja wa kitaifa.
Alisema kwamba CUF imeshindwa kufanya siasa za kistarabu ikiwemo kukemea vitendo vya kuhatarisha amani na umoja wa kitaifa vinavyoofanywa na Jumuiya ya Uamsho na mihadhara Zanzibar. (JUMIKI).
Alisema Uamsho wamekuwa wakitoa lugha chafu dhidi ya Viongozi wa Kitaifa na waasisi wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Najuta kupoteza muda wangu kutafuta muafaka wa amani ya Zanzibar wakati wezetu awataki kuacha siasa za chuki na uhasama,’alisema Vuai ambaye alikuwa Mjumbe wa kamati ya Muafaka.
Alisema kwamba akukuwa na sababu za msingi kwa viongozi wa CUF kuhakiki kadi za wapiga kura katika vituo wakati ndani ya chumba cha wapiga kura kuna mawakala wa vyama na orodha ya majina ya wapiga kura yakiwa na majina na picha za wahusika.
Katika uchaguzi huo mgombea wa CCM Hussen Ibrahim Makungu aliebuka mshindi kwa kumtagulia mgombea wa CUF Issa Khamis issa ambaye amegoma kusaini matokeo na kutangaza kupiga matokeo mahakama Kuu ya Zanzibar.
Mwisho
WAISLAM WAWAZIDI KETE POLISI WAANDAAMANA NA KUFANYA KONGAMANO DAR LICHA YA KUPIGWA MKWARA
| JUMUIA NA TAASISI ZA KIISLAM TANZANIA WAKIWA KATIKA MAANDAMANO YA KUTOA TAMKO LA WAISLAM NCHINI DHIDI YA MAREKANI KURUHUSU KUTOLEWA FILAMU INAYOUKASHIFU MTUME MUHAMAD |
| JUMUIA NA TAASISI ZA KIISLAM TANZANIA WAKIWA KATIKA MAANDAMANO YA KUTOA TAMKO LA WAISLAM NCHINI DHIDI YA MAREKANI KURUHUSU KUTOLEWA FILAM INAYOUKASHIFU MTUME MUHAMMADI SAW |
| JUMUIA NA TAASISI ZA KIISLAM TANZANIA WAKIWA KATIKA MAANDAMANO YA KUTOA TAMKO LA WAISLAM NCHINI DHIDI YA MAREKANI KURUHUSU KUTOLEWA FILAM INAYOUKASHIFU MTUME MUHAMAD |
| waumini wa kiislam wakiwa katika kongamnao lao la kulaani Marekani kwa kuruhusu kutengenzwa kwa Filamu inayomkashfu Mtume Muhammad 'SAW' jana kwenye viwanja vya Kidongo Chekundu, jijini Dar es Salaam |
| Umma wa Kiislam ukiwa kwenye kongamano lao lililofanyika jana jijini Dar |
| Umma wa Mtume Muhammad SAW, ukiwa kwenye kongamano lao la kulaani utengenezwaji wa filamu ya kumkshfu Mtume Muhammad SAW. |
CHANZO:MZUKA WA FUNGO
IBF YAWATEUA MAKAMU WANNE WA RAIS KATIKA BARA LA AFRIKA, GHUBA ZA UARABU NA UAJEMI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARITAREHE 20/09/2012
Shirikisho la Ngumi la
Kimataifa IBF limepanua wigo wake wa kusimamia na kuratibu ngumi katiuka bara
lka Afrika, Mashariki ya kati, Ghuba ya Urarabu na Ghuba ya Uajemi. Katika
miaka ya karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa sana la vijana wengi kujiunga na
ngumi na hivyo wengi kuhitaji huduma za shirikisho la IBF.
Ili kujiweka vizuri
katika nafasi ya kutoa huduma nzuri inayotakikana, IBF imewateua Makamu wanne
wa rais watakaomsaidia Raia wa Shirikisho hili Bwana Onesmo Ngowi.
Uteuzi huu umefuata
mambo yafuatayo: Upendo wa wahusika wenyewe kwa mchezo wa ngumi, nafasi
aliyonayo kwenye jamii, ukaribu wake na vijana, uwezo wake kielimu na michango
yake kwa michezo.
Wafuatao wameteuliwa
kuwa makamu wa Rais kuanzia mwisho wa mwezi huu:
Ayman Saad Bait-Saleem (Oman);
Makamu wa Rais, Fedha
Ayman ni mhandisi mwenye
shahada ya uzamili kutoka katika chuo kikuu cha Karolina ya Kusini (University
of South Carolina, Colombia South Carolina, USA.) mwa nchi ya Marekani. Amefanya kazi kama Meneja Mkuu wa
bandari ya Sultan Qaboos kwa miaka mingi, Meneja wa kampuni ya
APL Moller Group ya Denmark nchini Oman, Kampuni ya Marekani ya ushauri wa
Kihandisi na nyingine nyingi. Kwa sasa Ayman ni mfanyabishara mwenye kampuni nyingi nchini Oman mojawapo
ikiwa ni AL SWAYNI SPORT SERVICES
katika jiji la Muscat, Oman
William Steven Kallaghe
Makamu wa Rais, Utawala na Masoko
William ni msomi
aliyebobea katika masuala ya Uchumi na Utawala na alisoma katika chuo kikuu cha
Budapest,
Hungary. Ana uzoefu
mkubwa kwenye masuala ya uchumi na masoko na amefanya kazi na makampuni kadhaa
kama Mkurugenzi Mkuu wa benki ya kiislamu ya NBC, Meneja Miradi wa benki ya
CRDB, Meneja wa Masoko wa Kanda wa kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kabla ya
kuhamishia ujuzi wake kama Mkurugenzi wa Masoko wa Benki ya NBC.
Henry Mann-Spain (Ghana)
Makamu wa Rais, Operations
Henry ni mfanyabishara
aliyeboboea kwenye biashara mbalimbali na analimiki makampuni makubwa ya
kutengeneza bidhaa za kilimo kama nguo na vyakula vya kugandishwa (Frozen Food).
Ana Shahada ya Uzamili
wa Biashara (MBA) kutoka katika Chuo Kikuu cha Harvard kilichopo katika jimbo la
Massachusetts nchini Marekani. Henry amefanya kazi kwa miaka mingi na mashirika
ya kimataifa yakiwamo UNHCR, ILO na UNDP.
Kwa sasa ni Mkurugenzi
Mkuu wa Makampuni ya Golden Crescent Ltd yanayojishughulisha na kutengeneza
bidhaa kutoka kwenye mazao ya mifugo na kilimo nchini Ghana na kuyauza nchi za
Ulaya, Marekani na Asia.
Louaa Debes (Misri)
Makamu wa Rais,
Ubingwa na Viwango
Louaa ni mfanya biashara anayeishi katika jiji la cairo nchini Misri na
ana uzoefu nkubwa kweney masuala ya biashara za kutengeneza nguo.
Louaa Debes amesoma biashara kwenye Chuo Kikuu cha Cairo na amefanya kazi
na taasisi za serikali kabla ya kuanzisha shughuli za biashara. Debes anamiliki
makampouni ya ulinzi, maduka makubwa (Super markets) pamoja na kamouni ya
ukodishaji wa magari.
Imetolewa na:
Onesmo A.M. Ngowi
Rais
IBF katuka bara la Afrika, Mashariki ya Kati, Ghuba ya Uarabu
na Uajemi.
(IBF President for Africa, Middle East, Arabian and Persian
Gulfs)
Subscribe to:
Posts (Atom)


.jpg)








