STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, April 19, 2013

RT yajihakikishia wakimbiaji wawili wa kwenda Russia

Katibu wa RT, Seleman Nyambui

WANARIADHA Faustine Mussa na Joseph Daudi wa mbio ndefu za marathon wamefuzu kushiriki mashindano ya riadha ya dunia yatakayofanyika Agosti 10 hadi 18 jijini Moscow, Urusi.
Katika mashindano hayo yanayoshirikisha wanariadha wanawake na wanaume kutoka nchi mbalimbali duniani, Tanzania inatarajiwa kupeleka wanariadha zaidi ya watatu endapo watafikia viwango vinavyotakiwa katika mashindano hayo.
Akizungumza juzi Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha (RT), Suleiman Nyambui, alisema wanariadha hao wamefuzu kutokana na viwango walivyoonyesha wakati wakiwania kushiriki michezo ya Olimpiki.
"Tayari tuna uhakika wa kuwa na wanariadha wawili wenye sifa ya kushiriki katika mashindano ya dunia kwa mbio za marathon... sasa bado tunasubiri kupata washiriki watakaofuzu kwa  mbio za mita 5,000 na 10,000," alisema Nyambui.
Aliwataja wanariadha wanawake ambao RT inatarajia kuwa watafikia viwango vya kufuzu kwa michuano ya dunia kuwa ni pamoja na Zakia Mrisho (mita 5,000), Sara Ramadhan, Jacqueline Sakilu na Mary Naal wanaokimbia mita 10,000

Thursday, April 18, 2013

Fabregas ataka fainali ya El Clasico Ulaya

Cesc Fabregas

KIUNGO nyota wa Barcelona, Cesc Fabregas amesema anatamani Fainali za Ligi ya Mabingwa ya Ulaya mwaka 2013 izikutanishe timu hasimu za Hispania.

Vigogo hao wa La Liga wanatarajiwa kuvaana na Bayern Munich na Borussia Dortmund katika mecni za Nusu Fainali zitakazochezwa wiki ijayo.
 Fabregas pamoja na kutambua ugumu wa pambano lao dhidi ya Bayern, lakini anaamini huenda mahasimu hao wa Hispania watacheza fainali zitakazofanyika Wembley, Uingereza.

"Nataka fainali kati ya Real Madrid na Barcelona. Itakuwa ni mechi muhimu na ya kihistoria katika soka," nahodha huyo wa zamani wa Arsenal alisema.
Kiungo huo aliyekuwa akihojiwa na kituo cha Radio cha RAC1, alisema; "Hata hivyo kitu cha muhimu kwa sasa ni pambano letu na nusu fainali dhidi ya Bayern. Itakuwa mechi ngumu na isiyotabirika," alisema Fabregas.
Pia kiungo huyo alizungumza kurejea kwa kocha wao, Tito Vilanova na Eric Abidal ambao wanapigana dhidi ya ugonjwa wa Saratani, na kudai itawahamasisha zaidi wachezaji dhidi ya pambano hilo dhidi ya Bayern.
"Tito na Abidal wametuongezea chachu ya kukupigana na kutinga fainali," alisema.

HUKUMU KESI YA PONDA YAAHIRISHWA MPAKA MEI 9

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania Sheikh Ponda Issa Ponda (kulia) akiwa na mshtakiwa mwenzake Saleh Mkadamu wakielekea  kupanda basi la magereza baada ya hukumu ya kesi yao kuahirishwa hadi Mei 9. Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake 49 wanakabiriwa na makosa matano ya kula njama na kuingia kwa jinai katika uwanja namba 311/3/4 kitalu T uliopo Markaz Chang'ombe na wizi wa vifaa mbalimbali vya ujenzi vyenye thamani ya Shs milioni 59 mali ya kampuni ya Agritanza. (Picha na Habari Mseto Blog) 
 Saleh Mkadamu akipanda basi kuelekea mahabusu
 Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania Sheikh Ponda Issa Ponda akipanda basi la magereza.
 Ulinzi mkali kila kona ya mahakama
 Askari wakiimarisha ulinzi nje ya Mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo.
 Msafara wa magari ya Polisi wakisindikiza gari la magereza lililomchukua Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania Sheikh Ponda Issa Ponda wakati wakielekea mahabusu baada ya hukumu ya kesi yao kuahirishwa leo hadi Mei 9.
Wafuasi wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania Sheikh Ponda Issa Ponda wakiwa wamekusanyika nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo wakati hukumu ya kesi yake ilipoahirishwa leo.

HATIMAYE BI KIDUDE APUMZISHWA KABURINI VISIWANI ZENJI

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,alipohudhuria nyumbani kwa Marehemu Bi Fatma Baraka (KIDUDE) kuhani kwa Familia ya marehemu leo asubuhi Rahaleo Mjini Unguja. (Picha na Ramadhan Othman, Ikulu)
 Akina Mama mbali mbali waliofurika katika maziko ya Msanii Maarufu Marehemu Bi Fatma Baraka (KIDUDE)huko nyumbani kwake Rahaleo mjini Unguja leo.
Maelfu ya wanannchi na waislamu waliofurika katika msikiti wa Mwembr shauri katika maziko ya Marehemu bikidude leo,na kuzikwa kijini kwao Kitumba Wilaya ya Kati Unguja.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,(wa nne  kushoto) akijumuika na viongozi na waislamu katika kumswalia Marehemu Msanii maarufu Fatma Binti Baraka (kidude) katika msikiti wa Mwembeshauri Mjini Unguja leo.

 Vijana waliobeba Jeneza la mwili wa Marehemu Msanii maarufu Fatma Binti Baraka (kidude) wakati wa maziko yake yaliyofanyika leo huko kijijini kwao Kitumba,Wilaya ya Katri Unguja,ambapo maziko yake yamehudhuriwa na wasanii mbali mbali ndani na nje ya nchi. 
 Baadhi ya Wananchi waliohudhuria katika maziko ya marehemu Bi Fatma Baraka (Kidude)  kijijini kwao Kitumba,Wilaya ya Katri Unguja.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,(kutoka kulia) Rais wa  jamhuri ya Muungano Dk. Jakaya Mrisho Kikwete,Makamo wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif,na Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi,wakiitikia dua baada ya maziko ya Msanii maarufu Fatma Binti Baraka (kidude) aliyefariki jana na kuzikwa leo Kijijini kwao Kitumba,Wilaya ya Kati Unguja.

Soko la wanandinga wa Kiafrika lapanuka Ulaya, Tanzania mmmh!


Wachezaji wa Kiafrika wazidi kupata soko Barani Ulaya hivyo Watanzania wasichezee fursa ya soka la kimataifa.
*  Zaidi ya Mawakala 15 wawasiliana na Tanzania Mwandi kuwahitaji wachezaji

Zaidi ya mawakala 15 tayari wamewasiliana na Kampuni ya Tanzania Mwandi kuwahitaji wachezaji mbalimbali kwaajili ya kuwapeleka kwenye klabu za barani Ulaya, Asia na Afrika ili kucheza soka la kulipwa.

Mwitikio huo umeongezeka kutokana na vijana wa kiafrika kuwa na soko kubwa katika ulimwengu wa sasa wa mpira wa miguu kwa nchi mbalimbali kama Sweden, Uholanzi, Denmark, Ureno na nchi nyinginezo.

Arne Anderson kutoka AA Football Service ya Sweden amesema kuwa binafsi yuko tayari kuchukua wachezaji wawili kwaajili ya kuwatafutia clubs nchini humo kwani tayari mafanikio ya wachezaji watano wa kiafrika aliowapeleka yamempa maombi ya timu nyingi za Sweden.

“Niko tayari kuchukua wachezaji wawili endapo tutakubaliana kuhusu maslahi yangu pindi wachezaji hao wakianza kucheza hapa”, Arne amesema.

Kutokana na mafanikio hayo na maombi ya mawakala lukuki Kampuni ya Tanzania Mwandi inazidi kuwasisitizia wachezaji wa Kitanzania kujaza fomu zinazopatikana kupitia blog.tanzaniamwandi.co.tz ili kufanya majaribio ya kucheza soka nchini Sweden, Norway, Denmark, Uholanzi, Ureno, Uswiss, Ufaransa na Ubelgiji, barani Asia (Kuwait, China, Qatar nk) na klabu nyingine barani Afrika.

Mpaka sasa jumla ya wachezaji wa kitanzania 15 wamekwishajaza fomu za haraka kwenye tovuti ya Tanzania Mwandi huku kampuni ikiwa imepokea pia maombi ya wachezaji 25 kutoka nje ya nchi.

“Maombi yanazidi kuja ingawa tunawahimiza Watanzania wasikimbie kiingilio cha shilingi 300, 000 wakumbuke kuwa wanafanya majaribio wakiwa nyumbani na watakapopata timu Kampuni ya Tanzania Mwandi haitachukua chochote kwenye mikataba yao, ni wao na mawakala ndio watakokubaliana juu ya watakachokipata kutoka kwa klabu husika”, alisema Teonas Aswile, Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzania Mwandi, waandaaji wa African Youth Football Tournament.

Aswile amezialika klabu mbalimbali za ligi kuu ya soka Tanzania Bara na Visiwani kutazama wachezaji watakaofika katika michuano hiyo kwani wapo baadhi ya wachezaji kutoka nje ya nchi ambao watafika na wangependa kucheza soka la Tanzania.

“Kati ya wachezaji 25 wa nje ya nchi wengine wameomba tuwatafutie timu hapa nchini hivyo klabu zikija zinaweza kuwapata wachezaji hao wakiwa huru kwasababu watakuja kwa gharama zao kufanya majaribio nchini. Pia klabu hizo zitumie fursa hii kuuza wachezaji wake.”

Michuano ya African Youth Football Tournament inatarajia kufanyika Juni 10 hadi 14 mwaka huu katika uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam na kushirikisha vijana kati ya miaka 18 hadi 21 kutoka Tanzania na bara zima la Afrika. Taarifa zaidi kuhusu michuano hiyo zinapatikana kupitia;  blog.tanzaniamwandi.co.tz

Imetolewa na Idara ya Habari
Kampuni ya Tanzania Mwandi,
TANCOT House, Ground Floor,
S. L. P 79944,
Dar es Salaam.

Yanga, maafande wa JKT Ruvu kuonyesha ubabe J'2


JKT Ruvu Stars
Yanga
Na Boniface Wambura
VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga inayofukuzia kwa karibu taji la msimu huu inatarajiwa kushuka dimbanio Jumapili kwa ajili ya kuumana na maafande wa JKT Ruvu katika mechi pekee ya ligi hiyo wikiendi hii itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mbali ya mechi hiyo, nyingine zitakazochezwa mwezi huu ni kati ya African Lyon na JKT Ruvu itakayofanyika Aprili 24 kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam wakati Aprili 25 ni kati ya Ruvu Shooting na Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Nayo Coastal Union itaikaribisha Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga katika mechi itakayochezwa Aprili 27. Uwanja wa Taifa utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Simba na Polisi Morogoro itakayofanyika Aprili 28.

Yanga wanaoongoza msimamo wa Ligi hiyo ikiwa na pointi 53 ikifuatiwa na Azam yenye pointi 47 wakati Kagera Sugar wanashika nafasi ya tatu wakijikusanyia jumla ya pointi 40 na kufuatiwa na Simba na Mtibwa Sugar ambazo kila moja ina pointi 36 kisha wagosi wa kaya, Coastal Union wakifuatia nafasi ya sita.,
Mpaka sasa timu tano za Polisi Moro, African Lyon, Toto Africans, JKT Ruvu na Mgambo ndizo zilizopo kwenye vita ya kuepukana kushuka daraja zikipisha kwa tofauti ndogo ya pointi kati ya 19 na 25.

Yanga, Mgambo JKT wavuna Mil 24 Mkwakwani

Hamis Kiiza alipokuwa akiwania mpira na beki wa Mgambo JKT juzi kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga


Na Boniface Wambura
PAMBANO la  Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Mgambo Shooting na Yanga lililochezwa jana (Aprili 17 mwaka huu) Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga limeingiza kiasi cha sh. 24,865,000 kutokana na watazamaji 4,386.

Viingilio katika mechi hiyo namba 162 iliyomalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 vilikuwa sh. 10,000 kwa jukwaa kuu na sh. 5,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 5,547,337.50 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 3,792,966.10.

Asilimia 15 ya uwanja sh. 2,820,680.08, msimamizi wa kituo sh. 120,000, kamishna wa mechi sh. 90,000, waamuzi sh. 270,000, maandalizi ya uwanja sh. 100,000 na tiketi sh. 1,587,500.

Mgawo mwingine ni gharama za mechi sh. 1,692,408.05, Kamati ya Ligi sh. 1,692,408.05, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 846,204.05 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga (TRFA) sh. 658,158.69.

Makocha Azam Far Rabat kuteta kesho

Kocha wa Azam, John Stewart Hall

Na Boniface Wambura
Makocha wa timu za Azam, Stewart John Hall na AS FAR Rabat ya Morocco, Abderazzak Khairi watakutana na waandishi wa habari kesho (Aprili 19 mwaka huu) kuzungumzia mechi yao itakayofanyika Jumamosi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mkutano huo ambao pia utawahusisha manahodha wa timu hizo mbili utafanyika saa 5 kamili asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Barabara ya Uhuru na Shaurimoyo.

Timu hizo zitakutana katika mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho itakayoanza saa 10 kamili jioni. Mechi ya marudiano itachezwa nchini Morocco wiki mbili baadaye.

Wednesday, April 17, 2013


Bondia Fadili Majia akiwa na kombe la ubingwa wa kimataifa wa ngumi alililonyakua nchini Indonesia wiki iliyopita alipo mpiga bondia Heri Amol  hapa alipolakiwa baada ya kutua jijini Dar es Salaam jana. Kutoka kushoto ni Kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini, Rajabu Mhamila 'Super D', mabondia Japhet Kaseba, Kanda Kabongo na Pendo Njau.
Kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini Rajabu Mhamila 'Super D' kushoto akifurahia jambo na bondia Pendo Njau baada ya kumpokea Fadhili Majiha katikati aliyerudi na kombe la ubingwa aliouchukua Indonesia wiki iliyopita  baada ya kumtwanga bondia Heri Amol wa pili ni Japhet Kaseba mwingine ni Kanda Kabongo.

JKT Ruvu yaapa kupambana mpaka mwisho Ligi Kuu

Kikosi cha JKT Ruvu Stars

WACHEZAJI wa klabu ya JKT Ruvu wameapa kupigana kufa na kupona ili kuhakikisha timu yao haishuki daraja kutoka Ligi Kuu Tanzania Bara, wakizitangazia vita na kuzitaka zikae chonjo timu nne watakazokutana  nazo kabla ya kumaliza mechi zao za msimu.
JKT Ruvu ambayo kwa msimu huu imeonekana kutetereka tofauti na msimu kadhaa ya nyuma ambayo ilipokuwa ikimaliza ligi katika Nne Bora, ni miongoni mwa timu zilizopo katika eneo la hatari la kushuka daraja ikiwa na pointi chache huku ligi ikielekea ukingoni.
Baadhi ya wachezaji wa timu hiyo wamesema pointi moja waliovuna Mkwakwani-Tanga mbele ya Coastal Union waliotoka nayo sare ya 0-0, wamepata nguvu ya kuhakikisha wanafanya vyema katika mechi zao zilizosalia ikiwamo dhidi ya Yanga Jumapili jijini Dar es Salaam.
Kessy Mapande mmoja wa wachezaji waandamizi wa timu hiyo, alisema mechi nne zilizosalia kwao
ni kama fainali kwa kuamini kuteleza kidogo tu kutairudisha JKT Ruvu Ligi Daraja la Kwanza kitu ambacho hawakati kukisikia hata kidogo.
Mapande walisema mechi zao nne zilizosalia ikiwamo ya Jumapili dhidi ya Yanga, African Lyon, Prisons ya Mbeya na ile ya mwisho dhidi ya Mtibwa Sugar zote wanazichukulia kwa uzito mkubwa wakipania kushinda au kupata pointi za kutosha za kuwaepusha kushuka daraja.
"Tutapambana mpaka dakika ya mwisho kuhakikisha tunapata ushindi na kuvuna pointi za
kutunusuru kushuka daraja, yaani mechi zilizosalia kwetu ni kama fainali tutashuka dimbani
kupigana kiume kuinusuru JKT isirudi daraja la kwanza," alisema Mapande.
JKT ambayo imepoteza aliyekuwa kocha wao, Charles Kilinda aliyetangaza kujiuzulu kutokana na
timu kufanya vibaya msimu huu, mpaka sasa ipo katika nafasi ya 11 baada ya juzi kupata suluhu
Tanga iliyoifanya ifikishe pointi 23 na kuishusha Toto katika nafasi hiyo.
Kikosi hjicho cha maafande kitashuka dimbani Jumapili kuwakabili Yanga kabla ya Jumatano ijayo
kuvaana na African Lyon uwanja wa Chamazi kisha kuumana na Prisons wiki ijayo kwenye uwanja
huo huo wiki ijayo na kwenda kumalizia Manungu dhidi ya Mtibwa Sugar Mei 18

Benny Ngassa ataka wadau wa soka Ilala kuisaidia Ashanti United

Kikosi cha Ashanti kilichorejea Ligi Kuu

Benny Ngassa katika pozi
BAADA ya kuthibitishwa rasmi kuwa miongoni mwa timu tatu zilizopanda Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao, baadhi ya wachezaji wa Ashanti United wamewaomba mapema wadau wa soka wa Ilala kuiunga mkono kwa hali na mali ili ifanye vyema katika ligi hiyo.
Wachezaji hao walisema juhudi walizofanya kuirejesha tena Ashanti katika ligi hiyo baada ya misimu kadhaa ya kusota Ligi Daraja la Kwanza ni lazima ziungwe mkono kwa wadau kuiwezesha timu hiyo kufanya usajili mzuri na kumudu gharama za ushiriki wa ligi kuu msimu ujao.
Mmoja wa wachezaji hao, Bennedict Ngassa, alisema bila wadau wa soka wa Ilala kuiunga mkono klabu yao katika ushiriki wa ligi kuu msimu ujao, timu inaweza kuyumba na kufanya vibaya kitu ambacho alisema wachezaji wa Ashanti wasingependa kuona baada ya kuipandisha timu daraja.
"Tunashukuru kwa kufanikiwa kuipandisha timu daraja na kuirejesha Ashanti Ligi Kuu, lakini kazi bado haijaisha kwa wale wote waliokuwa wakituunga mkono, tunahitaji sapoti zaidi katika maandalizi na ushiriki wa ligi hiyo ili tusirudi tena FDL (ligi daraja la kwanza)," alisema Ngassa.
Ngassa aliyetua Ashanti baada ya kushuka daraja na timu ya Moro United msimu uliopita na kuifungia mabao matatu, alisema nguvu ya pamoja na sapoti toka kwa mashabiki na wadau wote wa soka wa Ilala, ili kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri na kutisha kwenye ligi hiyo.
Ashanti United iliyowahi kucheza na kutamba kwenye ligi kuu kabla ya kushuka msimu wa 2007-2008,
imerejea tena katika ligi hiyo ikiwa sambamba na timu za Mbeya City na Rhino Rangers ya Tabora baada ya kufanya vyema katika mechi zao za Ligi Daraja la Kwanza iliyomalizika hivi nkaribuni

Bi Kidude kuzikwa kesho, wengi wamlilia

Bi Kidude enzi za uhai wake

MKONGWE wa muziki wa taarab nchini aloyejipatia umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi, Fatuma Bint Baraka Bint Khamis 'Bi Kidude' aliyefariki asubuhi ya leo anatarajiwa kuzikwa kesho visiwani Zanzibar.
Bi Kidude anayekadiriwa kuwa na umri zaidi ya 100, alifariki Bububu Zanzibar kutokana na kuugua kwa muda mrefu maradhi ya Kisukari.
Taarifa kutoka kwa ndugu za marehemu zinasema kuwa Bi Kidude alizidiwa kwa siku nne mfululizo kabla ya kufariki leo na kwamba mwili wake utapelekwa kwake Rahaleo kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika kesho. 
Bi Kidude aliyezaliwa katika kijiji cha Mfereji Maringo, akiwa mmoja wa watoto saba wa mchuuzi maarufu wa nazi wa eneo hilo na alianza kuimba akiwa mwaka 1920 kabla ya kutoka kwao baada ya kulazimishwa kuolewa.
Enzi za uhai wake alifanya kazi ya sanaa akiimba na makundi mbalimbali za muziki wa mwambao uliomtangaza vyema ndani na nje ya nchi.
Baadhi ya makundi aliyoyafanyia kazi mwanamuziki huyo aliyewahi kwenda kuimba Misri ni pamoja na Egyptian Musical Club ya Dar es Salaam, Cultural na vingine.
Nyimbo zilizompa umaarufu ni pamoja na Muhogo wa Jang'ombe na alikuwa akishiriki maonyesho mbalimbali ya jukwaani ambapo hivi karibuni alitunukiwa tuzo ya maisha katika Tamasha la Filamu za Nchi za Majahazi, ZIFF.
Pia alitapa tuzo za Womax na mwaka jana katika kusherehekea miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania alkitunukiwa nishati ya heshima na rais Jakaya Kikwete.
Pia alikuwa akishirikishwa nyimbo za wasanii mbalimbali wa kizazi kipya baadhi wakitumia pia nyimbo zake, huku akiwa mwingi wa utani.
Marehemu Bi Kidude hakubahatika kuzaa mtoto kwa mujibu wa maelezo yake mwenyewe alipohojiwa enzi za uhai wake.
Baadhi ya wasanii mbalimbali nchini kama akina Jacob Stephen 'JB', Lady Jay Dee, Fid Q na wakali wengine wameonyesha kusikitishwa na kifo cha mkongwe huyo kwa kudai Tanzania imepoteza lulu katika tasnia ya sanaa.
Huku wakimtaja kama 'kungwi' katika muziki na masuala ya 'Unyago' akiwafunda wanawake jinsi ya kuheshimu ndoa zao pamoja na kuwa na maadili mema ndani na nje ya ndoa zao sambamba na kwenye  jukwaa la sanaa ili wadumu kama ilivyokuwa kwake.
Pamoja na sauti tamu aliyokuwa nayo Bi Kidude mwenyewe aliwahi kukiri kuwa ni 'mlevi' wa kutupwa wa kuvuta sigara.
Mungu Amlaze Mahali Pema Peponi Bi Kidude Ameen!

Yanga yabanwa, Mtibwa yainyuka Oljoro, Toto ikizama Kaitaba


WAKATI vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga ikicheleweshewa sherehe zake za ubingwa Mkwakwani, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar zimetaka nyumbani kwa kuzizamisha JKT Oljoro na Toto African.
Yanga ilisimamishwa kwa kusubiri dakika za jioni kupata bao la kusawazisha la kusawazisha mbele ya Mgambo JKT iliyoongoza kwa bao 1-0 wakati wa mapumziko.
Bao lililoinusuru Yanga na kipigo cha kwanza tangu duru la pili kuanza lilifungwa na Simon Msuva na kuifanya Yanga kuongeza pointi moja kileleni ikifikisha 53 na sasa kusubiri mechi ijayo dhidi ya Ruvu Shooting kujiweka tayari kushangilia ubingwa.
Mgambo kwa sare hiyo imefikisha pointi 25 na kupata matumaini ya kusalia Ligi Kuu, kutokana na ukweli bado ina mechi tatu mkononi na inahitaji pointi moja tu kujihakikishia usalama wa kusalia katika ligi hiyo.
Mtibwa ikiwa nyumbani uwanja wa Manungu imeilaza Oljoro JKT kwa bao 1-0 lililofungwa katika dakika ya 37 na Twaha Ally, na kuwafanya mabingwa hao wa zamani kufikisha pointi 36 sawa na Simba na kurejea kwenye nafasi yake ya tano iliyoshikiliwa kwa muda na Coastal ambayo jana iliiengua baada ya kupata sare kwa JKT Ruvu.
Nako mjini Bukoba, Kagera Sugar ilipigilia msumari wa mwisho katika jeneza la Toto Africans baada ya kuilaza kwa bao moja lililofungwa dakika za mapema na Themi Felix na kuzidi kuiweka pabaya wageni wao kusalia kwenye ligi hiyo msimu ujao.
Toto kwa kipigo hicho imendeelea kusalia na pointi 22 ikisaliwa na mechi moja tu, na kusalimika kwake kubaki ligi kwa msimu ujao itategemea na matokeo ya mechi yake ya mwisho na kuziombea Mgambo JKT na JKT Ruvu ziteleze katika mechi zao kitu ambacho ni miujiza mitupu.
Kabla ya kwenda Kagera, Toto ilitishia isingeenda kwa madai wanakaribia kumaliza mechi zao wakati timu nyingine zikiwa na mechi chache kitu ambacho kinaweza kuwaathiri kimatokeo na kiushuka daraja kionevu.
Hata hivyto kwa mkwara waliochimbwa na TFF walilazimika kwenda na kukumbana na maafa hayo ambayo yanaifanya timu hiyo kuelekea kurudi ligi ya FDL baada ya kuwa na misimu mibaya katika ligi hiyo.

MTANZANIA KUONGOZA UJUMBE MKUTANO WA NGUMI MAREKANI


MTANZANIA  Onesmo Ngowi ambaye ndiye ni Rais wa Shirikisho la Ngumi la Kimataifa katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati, ataongoza ujumbe mzito kutoka bara la Afrika na Ghuba ya Uajemi kwenye mkutano wa 30 wa Shirikisho la Ngumi la Kimataifa na Chama Cha Ngumi Cha Marekani (IBF/USBA).
Mkutano huo utafanyika katika hotel ya nyota tano ya Concorde Berlin iliyo karibu na Kanisa la kumbukumbu la Kaiser Wilhelm pamoja na taasisi ya Helmut Newton na Jumba la ukumbusho wa Picha jinini Berlin, Ujerumani.
 
Ujumbe atakaoongoza Ngowi utajumuisha wajumbe kutoka katika nchi za Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati na mpaka sasa ni nchi 31 zitakazo jumuika katika ujumbe huo ambao utajumuisha viongozi wa mashirika mbalimbali ya kusimamia utalii, biashara na michezo.
 
Mbali na kuhudhuria mkutano huo utakaofanyika kwa siku sita kuanzia Mei 21 mpaka Mei 26, ujumbe wa Ngowi utafanya pia mazungumzo na viongozi pamoja na taasisi mbalimbali zinazosimamia Utalii, Uwekezaji pamoja na Utalii wa Michezo katika nchi ya Ujerumani na nchi nyingine za Ulaya ambazo zitatembelewa na ujumbe huo.
 
Katika msafara huo ambao utajumuisha pia viongozi wa bodi za Utalii na Michezo kutoka katika nchi za Botswana, Afrika ya Kusini, Ghana, Misri na Falme za nchi za Kiarabu (UAE),ujumbe huo utatembelea pia nchi za Ufaransa, Ubeljiji, Uhispania pamoja na Uholanzi!
 
Ngowi amewahimiza watanzania juu kuchangamkia fursa za kujitangaza kibiashara nje ya nchi na kuwataka kujituma. “Ni muhimu Watanzania wakafungua macho na wajue kuwa dunia sasa ni kijiji na wasipoangalia watajikuta wanabaki nyuma kila mara” aliema Ngowi ambaye kwa ujumla alionyeha kusikitishwa na muitikio mdogo wa watanzania kwenye masuala ya kujitangaza kibishara nje ya nchi.
 
Ujumbe wa Ngowi utaondoka barani Afrika tarehe 17 Mwezi Mei na kuelekea Dubai ambako ndipo wajumbe wote watakapokutana tayari kwa msafara wa kuelekea jijini Berlin, Ujerumani!

Yanga kuvuna nini kwa Mgambo, Toto kujishusha daraja?





VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga leo watakuwa Mkwakwani Tanga kukabiliana na wenyeji wao Mgambo JKT, akili zao zikiwa kwenye taji la ubingwa ambalo kwa sasa halina mwenyewe baada ya Simba kulitema wiki iliyopita.
Yanga inahitaji pointi tano tu katika mechi zake nne zilizosalia kabla ya kumalizika kwa msimu wa 2012-2013 kutangazwa kuwa bingwa, na tayari wameapa kwamba leo ni lazima Mgambo walegee kwao kabla ya kuwakabili JKT Ruvu Jumapili kwenye uwanja wa Taifa.
Ingawa leo kuna mechi nyingine mbili, ikiwamo iliyo katika hatia hati ya kuchezwa kati ya Kagera Sugar dhidi ya Toto African, macho na masikio ya mashabiki wa soka yapo Mkwakwani kutaka kusikia na kuona kama Yanga itaendeleza rekodi yake ya kutopoteza mechi yoyote ndani ya mwaka 2013.
Yanga imeapa kuvuna pointi tatu katika pambano hilo litakalochezeshwa na mwamuzi Athuman Lazi kutoka Morogoro atakayesaidiwa na Michael Mkongwa wa Iringa na Godfrey Kihwili kutoka Arusha na kamishna wa mchezo huo anatarajiwa kuwa Godbless Kimaro kutoka Moshi, ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwa bingwa mpya wa Tanzania na kutwaa taji la 23 katika ligi hiyo tangu mwaka 1965.
Kocha wa  Ernie Brandts, alinukuliwa jana kuwa mchezo huo wa leo, utamwongezea asilimia 10 kati ya 90 alizokuwa nazo za kutwaa ubingwa na kudai kuwa awali alitishwa na kasi ya wapinzani wao Azam ambao Jumapili iliyopita walisimamishwa na Simba kwa kutoka sare ya mabao 2-2.
Licha ya kujipa asilimia hizo endapo watashinda mchezo huu, amewataka vijana wake kutokuwa na papara ili kuhakikisha wanashinda na kutimiza malengo yao kabla ya ligi kuisha.
Hata hivyo Yanga itawakabili Mgambo bila baadhi ya nyota wake ambao ni majeruhi na wengine wagonjwa akiwamo kiungo mahiri, Haruna Niyonzima, beki Juma Abdul na mshambuliaji Didier Kavumbagu.
Afisa Habari wa Yanga, Baraka Kizunguto alitamba kuwa licha ya kuwakosa nyota hao bado Yanga wapo imara kuweza kuvuna pointi tatu ili kuwaweka karibu na ubingwa na kuikimbia Azam waliopo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo ambao watakuwa 'likizo' kujiandaa na pambano la kimataifa dhidi ya FAR Rabat ya Morocco katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ukiondoa pambano la Mkwakwani, jioni ya leo pia kutakuwa na mechi nyingine zinazohusisha timu ndugu za Mtibwa Sugar na Kagera Sugar ambazo zitakuwa viwanja vyao vya nyumbani kuzikaribisha JKT Oljoro na Toto African, japo Toto imesisitiza kuwa haitakwenda Kagera kuumana na Kagera Sugar leo.
Katika pambano la Manungu, Mtibwa na Oljoro zitahukumiwa na mwamuzi Israel Mkongo, ambapo wenyeji watakuwa wakisaka ushindi utakaowawezesha kuchupa hadi nafasi ya tano baada ya jana kuenguliwa na Coastal baada ya kuambulia sare ya 0-0 mbele ya maafande wa JKT Ruvu.
Yanga ina pointi 52, ikifuatiwa na Azam pointi 47, Kagera Sugar pointi 37, kisha kufuatiwa Simba yenye pointi 35 na kufuatiwa na Coastal na Mtibwa zenye pointi 33 kila mmoja na kutofautiana kwenye uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Washelisheli kuzihukumu Azam na FAR Rabat J'Mosi


Na Boniface Wambura
TIMU ya AS FAR Rabat ya Morocco itakayoikabili Azam kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho inatua nchini leo (Aprili 17 mwaka huu) saa 7.30 mchana kwa ndege ya Qatar Airways.

Msafara wa timu hiyo wenye watu 28 kwa ajili ya mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili itakayochezwa Jumamosi (Aprili 20 mwaka huu) saa 10 kamili jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utafikia hoteli ya Sapphire iliyoko maeneo ya Kariakoo.

Wakati Azam imetinga hatua hiyo baada ya kuitoa timu ya Barrack Young Controllers II ya Liberia kwa jumla ya mabao 2-1, AS FAR Rabat imeingia raundi hiyo moja kwa moja kutokana na nchi hiyo kufanya vizuri kwenye michuano ya klabu Afrika.

Timu nyingine ambazo zimeingia raundi hiyo moja kwa moja katika Kombe la Shirikisho kama ilivyo AS FAR Rabat ni Asec Mimosas ya Ivory Coast, Atletico Petroleos (Angola), C.S.S. (Tunisia), DC Motema Pembe (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), El Ahly Shandy (Sudan), Enppi (Misri), Heartland (Nigeria), Ismaily (Misri), Lobi Stars (Nigeria), U.S.M. Alger ya Algeria na Wydad Casablanca (Morocco).

Mwamuzi Emile Fred atakayesaidiwa na Steve Maire, Jean Ernesta na Jean Claude Labrossa wote kutoka Shelisheli ndiye atakayechezesha mechi hiyo. Kamishna ni Abbas Sendyowa kutoka Uganda. Waamuzi watawasili nchini kesho (Aprili 18 mwaka huu) jioni.

Tuesday, April 16, 2013

MO kuiongoa Kamati ya Saidia Stars Ishinde

Mhe Mohammed Dewji
MBUNGE wa Singida Mjini, Mhe Mohammed Dewji ataiongoza Kamati ya Saidia Taifa Stars iliyotangazwa leo na serikali ikiwa na wajumbe 11.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo kamati hiyo itakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha Stars inajiandaa na kushiriki vyema kwenye michuano ya kimataifa.
Taarifa hiyo ya serikali imewataja wajumbe 11 wa kamati hiyo kuwa ni; Mohammed Dewji (Mbunge) Bi Teddy Mapunda, Dk Ramadhani Dau, Dioniz Malinzi, Asji Shabir, George Kavishe, Mohammed Raza (Mbunge), Leodger Tenga, Joseph Kusaga, Kapt John Komba na Zitto Kabwe (Mbunge).
Taarifa rasmi ya serikali ni kama ifuatavyo:
 
Kama mnavyofahamu, hivi sasa Timu ya Taifa ya mpira wa Miguu kwa Wanaume (Taifa Stars) ipo kwenye michuano ya kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Brazil mwaka 2014.
Katika Afrika, Tanzania (Taifa Stars) imepangwa kundi C kati ya makundi 10. Kundi C linajumuisha timu za Ivory Coast, Morocco, Gambia na Tanzania.
Kwa sasa katika kundi C, Taifa Stars inashika nafasi ya pili ikiwa na alama sita (6), nyuma ya Ivory Coast yenye alama saba (7), Morocco ina alama mbili (2) na Gambia ina alama moja(1).
Kwa mara nyingine Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inapenda kuwapongeza Taifa Stars, kwa kazi nzuri ambayo wameishaifanya ikiwemo ushindi wa Bao Tatu kwa Moja dhidi yaMorocco. Watanzania wote na Wadau wa Soka nchini wamefurahishwasanana mafanikio yaliyofikiwa na Taifa Stars na yenye kutupa matumaini  katika kuitayarisha Taifa Stars kufuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia  kwa mwaka 2014 nchiniBrazil.
Kwa hali ilivyo hivi sasa, Taifa Stars ipo katika nafasi nzuri ya kufuzu. Ili Tanzania tuweze kufuzu, Taifa Stars inatakiwa ishinde mechi zote tatu (3) na kuongoza kundi C na baadae iingie katika Timu kumi (10) bora na kisha zipatikane Timu tano (5) kutoka Afrika ambazo zitakuwa zimefuzu kwenda Brazil katika Fainali za Kombe la Dunia kwa mwaka 2014.  Tunaamini hili linawezekana.
Sasa kwa kuzingatia uzito wa jukumu lililo mbele yetu na kwa Taifa Stars kwa ujumla; Serikali imeunda Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars.
Jukumu la msingi la Kamati tunayoiunda ni kuhakikisha Taifa Stars inawezeshwa na kuandaliwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuunda kikundi cha kuishangilia timu ya Taifa ndani na nje ya nchi. Wajumbe wa Kamati ya Taifa Stars Stars itakayoongozwa na Mhe. Mohamed Dewji ni hawa wafuatao:-
 1. Mhe Mohamed Dewji           -       Mbunge
2. Bi. Teddy Mapunda             -       Montage
3. Dkt. Ramadhani Dau           -       Mkurugenzi Mtendaji NSSF
4. Bw. Dioniz Malinzi               -       Mwenyekiti BMT
5. Bw. Abji Shabir                  -       New Africa Hotel
6. Bw. George Kavishe            -       TBL
7. Mhe. Mohamed Raza           -       Zanzibar
8. Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
9. Bw. Joseph Kusaga             -       Clouds
10. Mhe. Kapt. John Komba    -       Mbunge
11. Mhe. Zitto Kabwe             -       Mbunge
Kamati hii iliyoteuliwa leo, naomba ianze kazi mara moja.  Hadidu za rejea zitakazowaongoza kutekeleza majukumu yao chini ya Kamati hii watazipata kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Kamati itashirikisha wadau mbalimbali kadri itakavyoona inafaa.
Serikali inaahidi kutoa ushirikiano utakaohitajika katika kuhakikisha Kamati hii inafanya kazi vizuri ili kuiwezesha Taifa Stars kushinda Mechi zote zilizombele yetu.
Aidha nichukue fursa hii kutoa wito kwa Watanzania wote, kuiunga mkono Taifa Stars na Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars kwa hali namalikatika kuhakikisha timu yetu inafuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia.
Kwa niaba ya Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri Mkuu naomba niwasilishe salaam zao za kuwapongeza Vijana wetu wa Taifa Stars, pamoja na benchi la ufundi likiongozwa na Kocha Mkuu Kim Poulsen. Kwa pamoja wanaomba Taifa Stars iendelee kujipanga kwa mechi zijazo.  Nawahakikishia kuwa Serikali, Watanzania na wadau wa Soka nchini wapo nyuma yao.
Mungu Ibariki Taifa Stars.
Mungu Ibariki Tanzania.
Dkt. Fenella Mukangara (Mb)
WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
16 Aprili, 2013


Coastal Union yangang'aniwa mkwakwani


MABINGWA wa zamani wa Tanzania, Coastal Union ya Tanga jioni ya leo imeng'ang'aniwa nyumbani na JKT Ruvu ya Pwani katika pambano lililochezwa kwenye uwanja wa Mkwakwani-Tanga.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo MICHARAZO ilipenyezewa hivi punde kutoka Tanga zinasema kuwa timu hizo zimetoshana nguvu kwa kushindwa kufungana katika pambano lililokuwa kali na lenye ushindani.
Kwa matokeo hayo timu hizo zimegawana pointi moja moja na kuifanya Coastal ifikishe pointi 33 na kulingana pointi na Mtibwa Sugar, lakini uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa yanaifanya ikwee nafasi ya tano huku maafande wa JKT wakifikisha pointi 23 na kuchupa kutoka nafasi ya 12 hadi ya 11.
Kipute cha ligi hiyo kinatarajiwa kuendelea tena kesho kwa mechi tatu katika viwanja vya Mkwakwani Tanga kati ya vinara Yanga na wenyeji wao Mgambo JKT, Mtibwa Sugar itakuwa nyumbani kuumana na JKT Oljoro na Toto African itasafiri hadi Kagera kuwakabili wenyeji wao Kagera Sugar kwenye uwanja wa Kaitaba.

Tetemeko la Ardhi laleta maafa makubwa Iran

 
TETEMEKO la Ardhi lenye ukubwa wa 7.8 limeupiga mji wa Khash nchini Iran na mpaka sasa inaripotiwa zaidi ya watu 80 wamepoteza uhai wao.
Tetemeko hilo ambalo limezipiga pia nchi za Pakstani, India na Qatar na kusababisha uharibifu na watu kadhaa kujeruhiwa, ambapo kwa habari za sasa zinasema kwa Iran waliofariki ni 81 na zoezi la uokozi linaendelea hali inayobashiriwa huenda idadi ya vifo vikaongezeka.

Wamorocco watakaoikabili Azam kutua kesho

Kikosi cha As FAR Rabat kinachotarajiwa kuja nchini kesho kuvaana na Azam
Azam wakataowakaribisha Wamorocco kwenye uwanja wa Taifa Jumamosi.
Na Boniface Wambura
WAPINZANI wa Azam katika michuano ya Kombe la Shirikisho, AS FAR Rabat ya Morocco wanatarajiwa kutua nchini kesho (Aprili 17 mwaka huu) saa 7 mchana kwa ndege ya Emirates.
Msafara wa timu hiyo wenye watu 28 utafikia hoteli ya Sapphire iliyoko maeneo ya Kariakoo, Dar es Salaam tayari kwa mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili itakayochezwa Jumamosi (Aprili 20 mwaka huu) saa 10 kamili jioni Uwanja wa Taifa.
Azam na FAR wataumana katikia pambano la raundi ya pili maarufu kama 16 Bora kuwania nafasi ya kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi za klabu barani Afrika.
Azam iliing'oa BYCII kwa jumla ya mabao 2-1 katika mechi ya raundi ya kwanza awali ikitoa pia Al Nasir Juba ya Sudan Kusini.
Wawakilishi hao pekee wa Tanzania ndiye jicho na roho ya mashabiki wa soka nchini kufuatia wawakilishi wengine wakiwemo Simba na Jamhuri -Pemba kung'olewa mapema kwenye michuano hiyo.
Tayari kikosi cha timu ya Azam ambayo mwishoni mwa wiki waliisimamisha Simba katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kutoka nao sare ya mabao 2-2 imeshaingia kambini kujiandaa na pambano hilo ambalo Azam watahitajika kushinda nyumbani ili kujiweka katika nafasi nzuri kwa mechi ya marudiano ugenini wiki mbili zijazo.
Kwa muda mrefu klabu za kutoka Kaskazini mwa Afrika zimekuwa zikizisumbua timu za Tanzania na Azam wanaoshiriki michuano hiyo ya kimataifa kwa mara ya kwanza wanahitajika kuufuta uteja huo mbele ya Wamorocco hao ambao ni timu ya maafande.

TFF yamlilia Meja Jenerali Makame Rashid


Makamu wa Rais, Dk Gharib Mohammed Bilal akitoa heshima ya mwisho kwa mwili wa Meja Jenerali Makame Rashid ukiwa kwenye jeneza lake.

Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko za kifo cha Mkuu wa zamani wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Makame Rashid kilichotokea juzi (Aprili 14 mwaka huu) kutokana na maradhi jijini Dar es Salaam.

Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kutokana na mchango aliotoa Meja Jenerali Makame Rashid ikiwemo kuwa mlezi wa timu ya Ruvu Stars wakati huo akiwa Kamanda (CO) wa Kikosi cha Ruvu JKT.

Pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mdhamini (Trustee) wa TFF wakati huo ikiitwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) na wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya katika miaka ya themanini alikuwa sehemu ya mafanikio kwa timu ya Tukuyu Stars ya Mbeya iliyotwaa ubingwa wa Tanzania Bara mwaka 1987 ikiwa ndiyo kwanza imepanda kucheza Ligi Kuu wakati huo ikiitwa Ligi Daraja la Kwanza.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Meja Jenerali Makame Rashid, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Maziko yanatarajiwa kufanyika leo (Aprili 16 mwaka huu) nyumbani kwao mkoani Mtwara. Mungu aiweke roho ya marehemu Sembwana mahali pema peponi. Amina

VPL KUTIMUA VUMBI VIWANJA VITATU KESHO



Na Boniface Wambura
LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Aprili 17 mwaka huu) kwenye viwanja vitatu huku vinara wa ligi hiyo Yanga wakifukuzia ubingwa huo jijini Tanga.

Yanga inayoongoza ligi ikiwa na pointi 52 itakuwa mgeni wa Mgambo Shooting katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Athuman Lazi kutoka Morogoro kwenye Uwanja wa Mkwakwani. Waamuzi wasaidizi wa mechi hiyo ni Michael Mkongwa wa Iringa na Godfrey Kihwili wa Arusha wakati Kamishna wa mechi hiyo ni Godbless Kimaro kutoka Moshi.

Kagera Sugar na Toto Africans zitaumana kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba katika mechi namba 164 itakayokuwa chini ya mwamuzi Martin Saanya wa Morogoro.

Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro, na wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 4,000 utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mtibwa Sugar yenye pointi 33 na Oljoro JKT yenye pointi 28.

Israel Nkongo kutoka Dar es Salaam ndiye atakayechezesha mechi hiyo akisaidiwa na Hamis Chang’walu (Dar es Salaam) na John Kanyenye (Mbeya). Kamishna wa mechi hiyo ni Ramadhan Mahano kutoka Iringa.

Mamuu ana Tatakoa akiwabeba walemavu

Mamuu (kulia) akiwa na Baby Madaha walioicheza filamu hiyo ya Tatakoa

MWANAHABARI aliyejitosa kwenye fani ya uigizaji na utayarishaji wa filamu nchini, Mariam Mndeme 'Mamuu' amefyatua filamu mpya iitwayo Tatakoa iliyowashirikisha nyota kadhaa nchini.
Mamuu, aliyewahi kuwa mtangazaji wa TBC na kufanya kazi katika magazeti ya Global Publisher, alisema filamu hiyo ni ya pili kwake baada ya awali kuitoa 'Pooja'.
Mwanahabari huyo aliiambia MICHARAZO kuwa, filamu hiyo ya 'Tatakoa' iliyowashirikisha wakali kadhaa ipo hatua ya mwisho kabla ya kuachiwa hadharani.
Mamuu alisema mbali na yeye wakali wengine waliyoicheza filamu hiyo ni pamoja na Baby Madaha, Frola Mvungi, Salma Jabu 'Nisha', Husna Idd 'Sajenti'.  Alice Bagenzi 'Rayuu', Jumanne Kihangale 'Mr Chuz'. Kupa, Zerisha na wengine.
"Baada ya kimya kirefu tangu nilipotoa Pooja, nimekuja na filamu nyingine mpya iitwayo 'Tatakoa' ambapo mimi na Mr Chuz ndiyo wahusika wakuu, huku Baby Madaha akicheza jana 'Jini-Joka'," alisema Mamuu.
Msanii huyo alisema filamu hiyo kazi hiyo mpya ni mwanzo wa kuwapa mashabiki wake burudani ndani ya mwaka huu, akiwa pia mbioni kuratibu kipindi maalum kwa ajili ya walemavu waliokata tamaa waliopo maeneo ya vijijini.
"Nimeona kama mwanajamii napaswa kutoa mchango wangu kwa walemavu kwa kuandaa kipindi hicho kutakachokuwa kikionyesha matatizo ya watu hao na kusaidia kupata misaada itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi," alisema Mamuu.
Mamuu alisema kipidni hicho anachokirekodi kuwasaidia walemavu anapigwa tafu na kigogo mmoja wa serikalini ambaye ji waziri, lakini aliyekataa kumtaja jina kwa sasa na mwingine ni Wema Sepetu