 |
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe Mizengo Pinda |
WATU 10,799 wamenaswa wakijihusisha na dawa za kulevya katika kipindi cha miaka mitano pekee na kuonyesha namna gani biashara ya dawa hizo lilivyo tatizo nchini.
Kwa mujibu wa hutuba ya Waziri
Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda, iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Urasimu na Bunge) William Lukuvi katika Siku ya Kupiga vita Dawa za Kulevya Duniani ni kwamba biashara ya dawa za kulevya ni tatizo nchini.
Pinda alisema kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania
wanaojiingiza katika biashara haramu ya dawa za kulevya ndani na nje ya
nchi na kwamba, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita watuhumiwa
10,799 walikamatwa kwa kujihusisha na dawa hizo.
Aidha, amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la biashara haramu ya dawa za kulevya nchini.
“Vile vile katika kipindi hicho jumla ya Watanzania 240 walikamatwa
katika nchi mbalimbali, zikiwamo Brazil, Pakstani na Afrika Kusini,”
alisema Pinda.
Alisema hali hiyo imekuwa ikiharibu taswira ya nchi na kusababisha
Watanzania wasio na hatia kupata usumbufu, masharti magumu wanapotaka
kusafiri kwenda nchi mbalimbali duniani.
Pinda alisema hali hiyo inatokana na sifa mbaya inayojengeka kwa Watanzania wanaosafiri katika nchi hizo.
Alisema zipo dalili kwamba, endapo biashara hiyo itaachwa iendeleee,
athari zaidi, zikiwamo kuingiliwa kwa misingi ya kiutawala na
wafanyabiashara wa dawa kwa manufaa binafsi, kuongezeka kwa waathirika
wa rushwa.
Aidha, alisema uwapo wa biashara hiyo huongeza mzunguko wa fedha haramu
na kusababisha mfumko wa bei na hivyo kuongeza hali ya umaskini.
Pinda alisema kwa mujibu wa vyombo vya dola, takwimu zinaonyesha viwango
vya Heroin na Cocaine zinazoendelea kukamatwa nchini, kuanzia mwaka
2000 ni vikubwa kuliko vile vilivyokamatwa miaka 10 iliyopita.
Alisema mwaka huu pekee kumekuwa na ukamataji mkubwa wa dawa za kulevya
katika eneo la kimataifa la Bahari ya Hindi karibu na nchini .
Kwa mujibu wa Pinda, jumla ya kilo 914 za Heroin zilikamatwa na kikosi kazi cha kuzuia uharamia cha Jeshi la Kimataifa.
Alisema askrimu, mikate na maandazi vilivyofanyiwa uchunguzi katika moja
ya shule jijini Dar es Salaam vilibainika kuwa na kiasi kidogo cha dawa
hizo za kulevya.
Aliwataka walimu na walezi kuwa makini na watu wanaouza vyakula katika
maeneo karibu na shule ili kuepuka wauzaji hao kuwafundisha wanafunzi
kutumia dawa za kulevya.