STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, July 23, 2013

Majanga: Msafara wa mazishi ya wanajeshi waliouwawa Darfur wapata ajali

 Picha mbali mbali za ajali ya gari iliyokua katika msafara wa maziko ya wanajeshi waliouawa Darfur iliyotokea Mwanakwerekwe sokoni umbali wa mita 300 kutoka Makaburi ya Mwanakwerekwe ambapo ndiko walipozikwa Wanajeshi hao.(Picha na Haroub Hussein).






                                            Gari lililopata ajali

Lililoua mdogo wake kwa mibangi lanaswa na Polisi

JESHI la polisi mkoa wa Singida limefanikiwa kumkamata Elibariki Alphoce (21) mkazi wa kijiji cha Kizega wilaya ya Iramba, anayetuhumiwa kumuua mdogo wake Mariam (9) mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya msingi Kizega.

Elibariki anatuhumiwa kumuua mdogo wake Mariam Julai 16 mwaka huu katika kijiji cha Kizega kwa kumkatakata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili na kisha kuteganisha kichwa na kiwiliwili.

Ilielezwa kuwa Elibariki ni mtumiaji sugu wa madawa ya kulevya aina ya bangi.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida ACP Geofrey Kamwela, amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa Julai 18 mwaka huu akiwa amejificha kando kando ya mto Ruruma wa kijiji cha Ruruma tarafa ya Kiomboi.

Polisi Dar wayanasa majambazi 8 na silaha 7 lakana Mnyika kukoswa na bomu

IMG_9423
Baadhi ya askari polisi wakionyesha kwa waandishi wa habari silaha zilizokamatwa kutoka kwa watuhumiwa wa matukio ya ujambazi.

IMG_9432
DCP Mlege akitoa taarifa ya mafanikio ya Jeshi hilo kwa waandishi wa habari ambapo akizungumzia suala la Mh. Mnyika amesema askari No. E. 5340 D/CPL Julius aliyekuwa ndani ya gari la polisi PT. 1902 alikuwa anasogeza boksi lenye mabomu ya kutoa machozi ya kurusha kwa mkono, kwa bahati mbaya bomu hilo lililipuka ndani ya gari hilo na halikuleta madhara yeyote kwa askari polisi wala raia waliokuwa eneo la uwanja wa Sahara uliopo Mabibo ambako chama cha CHADEMA kilikuwa kifanye mkutano wa hadhara tarehe 21 Jula 2013 kinyume na utaratibu.

Jeshi la Polisi Kanda maalum Dar es Salaam limefanikiwa kukamata sila 5 ikiwemo SMG moja, Shortgun mbili, Riffle Mark 3 tatu, Pisto moja, Risasi 56, Maganda ya Risasi 17 na Majambazi 8.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Kamishna wa polisi kanda hiyo, DCP A.M. Mlege amesema zoezi hilo lilifanyika Julai 18 mwaka huu katika maeneo ya Magomeni wilaya ya Kinondoni.

Amesema pia Jeshi hilo limeweza kukamata magari ya wizi matano, Injini tatu za magari, Vipande vya magari yaliyokatwa spea na wezi watano wa magari.

Katika hatua nyingine Jeshilo limekanusha habari zilizotolewa katika vyombo vya habari kuwa mbunge wa Jimbo la Ubungo Mh. John Mnyika kukoswa na bomu na kumjeruhi mmoja wa wafuasi wake.

Aidha limeomba siku zingine kabla ya kutoa habari ni vizuri likaulizwa ili kuthibitisha au kukanusha.

DCO Mlege amesema pia Jeshi la polisi Kanda maalum Dar es Salaam limemkamata tapeli hatari anayetumia namba tofauti za mitandao ya simu na majina ya watu maarufu anajulikana kwa jina la Mfaume Omari maarufu kama ‘Mau’.

Chanzo - MOBLOG 

Rais wa Zanzibar aongoza mazishi wa wanajeshi waliouwawa Darfur

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, (wa tatu kulia) akijumuika na Vingozi na Waislamu wengine katika kuwaswalia  Merehemu Sgt. Shaibu Shehe Othman, na Cpl Mohammed Juma Ally katika Msikiti wa Nuru Muhammad, Mombasa mjini Unguja leo. (Picha zote na Ramadhan Othman, Ikulu)
 Wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania wakibeba Jeneza la mwili wa Marehemu Sgt Shaibu Shehe Othman, baada ya kuwasili mjini Zanzibar akiwa ni miongoni mwa wanajeshi 7 waliouwawa kwa kupigwa risasi Jimbo la Darfur nchini Sudan hivi karibuni.

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, akitia udongo katika kaburi la Marehemu Sgt. Shaibu Shehe Othman, aliyezikwa leo katika makaburi ya Mwanakwerekwe mjini Unguja. 
 Baadhi ya Wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Tanzania na Ndugu na Jamaa wa marehemu Sgt Shaibu Shehe Othman, na  Cpl Mohammed Juma Ally wakishiriki mazishi hayo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, (katikati) na Viongozi na Waislamu, wakiangalia  Wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Tanzania, walipokuwa wakitoa heshima za mwisho kwa marehemu Sgt. Shaibu Shehe Othman, wakati wa mazishi yake katika makaburi ya Mwanakwerekwe leo.

SHIWATA watakiwa kuchangia ujenzi wa nyumba Mkuranga

Mwenyekiti wa SHIWATA, Cassim Twalib 'Teacher' (kushoto)
Na Mwandishi Wetu
MTANDAO wa Wasanii Tanzania (SHIWATA) umewataka wanachama wake kuchangia ujenzi wa nyumba zao katika kijiji cha Mwanzega, Mkuranga ili kukamilisha mradi huo.
Mwenyekiti wa Mtandao wa Wasanii Tanzania (SHIWATA), Caasim Taalib alisema jana Dar es Salaam katika mkutano wa wanachama wanaochangia ujenzi ambapo mpaka sasa nyumba 29 zimekamilika na wanachama 220 wamechangia ujenzi na jumla zilizokusanywa ni mil. 82.5.
Alisema SHIWATA haina fedha za kujenga nyumba za wanachama wake wala haina chanzo cha mapato kama si kwa njia ya kuchangishana na baada ya hapo kuwakabidhi wale waliokamilisha uchangiaji wa ujenzi wa nyumba hizo.
‘Ujenzi wa nyumba za wasanii utafanikiwa kwa kila mwanachama kuchangia nyumba yake kwa kujiaminisha kuwa hakuna utapeli wala biashara katika gharama za ujenzi wa nyumba hizo’alisema Taalib.
SHIWATA ambayo inaundwa na wasanii, wanamichezo, wanahabari na vijana wapatao 7,000 ilikuwa ikabidhi nyumba Agosti mwaka huu kwa mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Jellah Mtagwa na wasanii wengine 14 ambao wamekamilisha michango ya ujenzi  wa nyumba zao katika kijiji chao cha Mwanzega Kimbili, Mkuranga.
Wengine watakaokabidhiwa nyumba zao ni msanii maarufu nchini, Lumole Matovola ‘Big’ wa Bongo movie ambaye ni mwanachama wa SHIWATA wangine ni Mwandishi wa Habari, Josephine Moshi, Farida Ndimbo wa Jeshi la Magereza, Flora Kafwembe wa JKT Mgulani na Nyanza Kisadugwa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).  
Mpaka sasa SHIWATA imejenga nyumba 29 kwa ajili ya wasanii katika eneo la hekari 300 na wanajiandaa kulima shamba la hekari 500 walizonazo ili kujikwamua kimaisha.
              

Master Kinyogoli awafua mabondia Idd Mnyeke, Ibrahim Class

 Bondia Ibrahimu Class 'King Class Mawe' kushoto akipambana na Iddy Mnyeke wakati wa mazoezi yanayoendelea katika Kambi ya Ilala Amana CCM mabondia hao wanafanya mazoezi kwa ajili ya mashindano yao yatakayo fanyika baada ya kumarizika mwezi mtukufu wa Ramadhani 


Bondia Iddy Mnyeke  akipambana na Ibrahimu Class 'King Class Mawe' wakati wa mazoezi yaliyofanyika katika kamba ya Amana CCM Dar es salaam mabondia hao watapanda ulingoni kuwakabili wapinzani wao baada ya kwisha kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani 

Bondia Iddy Mnyeke  akipambana na Ibrahimu Class 'King Class Mawe' wakati wa mazoezi yaliyofanyika katika kamba ya Amana CCM Dar es salaam mabondia hawo watapanda ulingoni kuwakabili wapinzani wao baada ya kwisha kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani kulia ni kocha Mkongwe Habibu Kinyogoli 'Master' 
Bondia Omari Bai kushoto akisimamiwa kupiga begi na Kocha Kondo Nassoro wakati wa mazoezi yaliyofanyika katika kambi ya Ilala 
Bondia Iddy Mnyeke  akipambana na Ibrahimu Class 'King Class Mawe' wakati wa mazoezi yaliyofanyika katika kamba ya Amana CCM Dar es salaam mabondia hawo watapanda ulingoni kuwakabili wapinzani wao baada ya kwisha kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani kulia ni kocha Mkongwe Habibu Kinyogoli 'Master' 
BONDIA IDDY MNYEKE AKIWA KATIKA POZI
Bondia Iddy Mnyeke  akipambana na Ibrahimu Class 'King Class Mawe' wakati wa mazoezi yaliyofanyika katika kamba ya Amana CCM Dar es salaam mabondia hawo watapanda ulingoni kuwakabili wapinzani wao baada ya kwisha kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani Picha na BLOG YA SUPER D
Bondia Iddy Mnyeke  akipambana na Ibrahimu Class 'King Class Mawe' wakati wa mazoezi yaliyofanyika katika kamba ya Amana CCM Dar es salaam mabondia hawo watapanda ulingoni kuwakabili wapinzani wao baada ya kwisha kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani 
IDDY MNYEKE
BONDIA OMARI BAI AKIPIGA BEGI
Bondia Omari Bai kushoto akisimamiwa kupiga begi na Kocha Kondo Nassoro wakati wa mazoezi yaliyofanyika katika kambi ya Ilala

Kim atamba Stars imjeiva kuwang'oa Uganda The Cranes

Kim Poulsen
 Na Boniface Wambura
KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amesema kikosi chake kimejiandaa kuikabili Uganda kwenye mechi ya marudiano ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) itakayochezwa Jumamosi jijini Kampala.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza leo, Kim amesema tangu kikosi chake kimeingia kambini Julai 14 mwaka huu, wachezaji wamekuwa wakifanya vizuri kwenye mazoezi na wako tayari kwa ajili ya mechi hiyo.

“Uganda ni timu bora kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati. Mechi itakuwa ngumu, tunaamini tunakwenda kufanya vizuri. Tayari tunayo mikakati kwa ajili ya mechi hiyo, tunakwenda kuikamilisha Kampala,” amesema Kim.

Hata hivyo, Kim amesema licha ya mwitikio mzuri wa wachezaji kwenye mazoezi lakini wanakabiliwa na changamoto ya wengi wa wachezaji kuwawamefunga wakati wachezaji wanapokuwa kambini wanatakiwa kula, kunywa na kupumzika.

“Hiki ni kipindi kigumu kwa mpira wa miguu, na suala la kufunga ni la kiimani ambapo hatuwezi kuwazuia wachezaji kufunga. Karibu nusu ya wachezaji wanafunga, hii ni changamoto ambayo tunaiheshimu,” amesema Kim na kuongeza kuwa ni wazi kikosi chake cha kwanza kitakuwa na mabadiliko baada ya beki Shomari Kapombe kwenda kwenye majaribio nchini Uholanzi.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inaondoka Mwanza kesho (Julai 24 mwaka huu) saa 7.25 mchana kwa ndege ya PrecisionAir na kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe saa 8.15 mchana.

Wachezaji waliomo kwenye msafara huo ni makipa Juma Kaseja, Mwadini Ali na Ali Mustafa. Mabeki ni Aggrey Morris, David Luhende, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Nadir Haroub na Vincent Barnabas.

Viungo ni Amri Kiemba, Athuman Idd, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Khamis Mcha, Mudhathir Yahya, Salum Abubakar na Simon Msuva. Washambuliaji ni John Boko, Juma Luizio na Mrisho Ngasa.

Kampuni ya Isere Sports yagawa vifaa


Mkurugenzi wa masoko wa Kampuni ya Isere Sports inayoshuhulika na uagizaji na uuzaji wa vifaa vya michezo,Abbas Isere (kulia) akimkabidhi jezi Katibu Mipango wa timu ya Fresh Niga ya Kilwa Masoko ,Maulid Mtika maarufu Milulu zenye thamani ya Sh. 350,000.

Isere sports yatoa jezi kwa timu ya Kilwa Masoko
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Vifaa vya michezo, Isere Sports imetoa jezi seti moja yenye thamani ya sh. 350,000 kwa timu ya Fresh Niga ya Kilwa Masoko inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu wilaya ya Kilwa.
Katibu Mipango wa timu ya Fresh Niga, Maulid Mtika akipokea jezi hizo jana alisema msaada huo ni mfano wa kuigwa na wafanyabiashara wengine wenye uwezo wa kusaidia kuibua vipaji vya vijana kwenye soka.

Mtika ambaye ni maarufu kwa jina la Milulu alisema imefika wakati Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litafute njia ili lishuke mpaka ngazi ya wilaya kujua matatizo yanawakabili timu ili kutafuta vipaji vya wachezaji watakaochukua nafasi ya waliopo Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars).

'Tunao vijana wenye vipaji vya kucheza soka kufikia ngazi ya timu ya taifa, kinachowanyima nafasi ya kuonekana ni vifaa vya michezo tunaomba TFF ishuke mpaka ngazi ya wilaya kuwasaidia vijana kukuza vipaji.
Alitoa wito kwa wadau wa michezo kujitokeza kusaidia timu ambazo hazina wafadhili lakini kuna vijana ambao wako tayari kuonesha vipaji vyao
Mkurugenzi wa Masoko wa Isere Sports, Abbas Isere alisema jana kuwa msaada huo ameutoa ili kukuza vipaji vya soka katika wilaya hiyo ambao wanahitaji misaada kama hiyo ili kuendeleza vipaji.

Monday, July 22, 2013

Hatimaye ratiba Ligi Kuu yatoka, Simba, Yanga kuanza na wageni zenyewe kuumana Okt. 20

http://blog.pesatimes.com/wp-content/uploads/2013/06/kochaaa.jpg
Yanga itaendelea kubebana kama hivi katika ligi ya msimu huu itakayoanza Agosti 24?
Na Boniface Wambura
LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara msimu wa 2013/2014 inatarajiwa kuanza  kutimua vumbi rasmi Agosti 24 mwaka huu kwa timu zote 14 kuwa viwanjani katika miji saba tofauti, ambapo mabingwa watetezi Yanga wataanza kibarua dhidi ya Ashanti United, jijini Dar..

Hata hivyo, kabla ya ligi hiyo kuanza kutakuwa na mechi ya kufungua msimu (Ngao ya Jamii- Community Shield) kati ya bingwa mtetezi Yanga na Makamu bingwa Azam itakayochezwa Agosti 17 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mbali na pambano la Yanga na Ashanti litakalopigwa kwenye uwanja wa Taifa, siku hiyo ya ufunguzi wa ligi hiyo, Mtibwa Sugar na Azam zitaonyeshana kazi kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro huku JKT Oljoro na Coastal Union zitapepetana mjini Arusha kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Simba wenyewe wataanzia ugenini mjini Tabora kuumana na 'wageni' Rhino Rangers, kwenye uwanja wa Ally Hassani Mwinyi, wakati  Mgambo Shooting itaialika JKT Ruvu katika Uwanja wa Mkwakwani, mjini Tanga huku wageni wengine wa ligi hiyo Mbeya City watakuwa nyumbani mjini Mbeya kuikaribisha Kagera Sugar katika uwanja wa Soikoine na Ruvu Shooting na Tanzania Prisons zitaumana Mabatini, Mlandizi.

Pambano la watani wa jadi nchini lenyewe kwa raundi ya kwanza litachezwa Oktoba 20 ambapo Simba watakuwa wenyeji kabla ya kurudiana mwakani April 27, katika moja ya mechi za kufungia msimu Yanga wakiwa ndiyo wenyeji wa pambano hilo.

Mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo utamalizika Novemba 3 mwaka huu wakati wa pili utamalizika Aprili 27 mwakani. (Ratiba kamili ya ligi hiyo itatupiwa hapa MICHARAZO muda si mrefu)

Taifa Stars kuifuata Uganda The Cranes keshokutwa

Stars na The Craned walipoumana katika mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam
Na Boniface Wambura
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inaondoka Mwanza keshokutwa (Julai 24 mwaka huu) kwenda Kampala, Uganda kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Kombe la CHAN itakayochezwa Jumamosi (Julai 27 mwaka huu) Uwanja wa Mandela kuanzia saa 10 kamili jioni.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iko kambini jijini Mwanza chini ya Kocha Kim Poulsen tangu Julai 14 mwaka huu kujiandaa kwa mechi hiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya hizo mbili itacheza Fainali za CHAN zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.

Timu hiyo itaondoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza saa 7.25 mchana kwa ndege ya PrecisionAir, na inatarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe saa 10.15 jioni.

Wakati huo huo, Kocha Kim Poulsen kesho (Julai 23 mwaka huu) atakuwa na mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia maandalizi ya kikosi chake. Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi kwenye hoteli ya La Kairo jijini Mwanza.

Pepe Reina kutimkia Napoli kumfuata kocha Rafa Benitez

http://i.telegraph.co.uk/multimedia/archive/02622/pepe_reina_2622933b.jpg
  GOLIKIPA wa klabu ya Liverpool, Pepe Reina anatarajiwa kujiunga na timu ya Napoli ya Italia kwa mkopo wa muda mrefu.
Kocha wa Napoli Rafael Benitez amekuwa akimkufukuzia Mhispania mwenzake huyo ambaye alikuwa nambari moja kipindi chake Anfield, baada ya kushindwa kumnasa mlinda mlango wa QPR Julio Cesar.
Reina mwenye umri wa miaka 30, alitarajiwa kurejea mazoezini katika klabu yake jana Jumapili kwa kujiunga na wachezaji wenzake huko katika ziara ya maandalizi ya msimu.
Liverpool ilimsainisha mlinda mlango Simon Mignolet raia wa Ubelgiji kutoka katika klabu ya Sunderland kwa ada ya uhamisho ya pauni milioni £9 mwezi uliopita.
Reina alijunga na Liverpool akitokea Villarreal mwaka 2005.

JK kuongoza watanzania kuwaaga wanajeshi waliouwawa Darfur


 

RAIS wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwaongoza Watanzania kuiaga miili ya askari saba wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waliouawa katika jimbo la Darfur nchini Sudan.
 
Shughuli ya kuiaga miili hiyo iliyowasili nchini juzi, itafanyika leo kwenye viwanja vya makao makuu ya jeshi hilo, Upanga jijini Dar es Salaam.

Miili ya wanajeshi hao iliwasili nchini juzi kwa ndege maalumu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu J. K Nyerere, Terminal One na kwenda kuhifadhiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Lugalo jijini Dar es Salaam.

Wanajeshi waliouawa ni Sajenti Shaibu Othuman, Koplo Oswald Chaula, Koplo Mohamed Juma, Koplo Mohamed Chikilizo, Rodney Ndunguru, Peter Werema na Fortunatus Msofe.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano, Makao Makuu ya JWTZ, ilieleza kuwa askari hao wataagwa leo na shughuli hiyo itahudhuriwa na familia, makamanda wa jeshi na viongozi wa Serikali.
 

“Shughuli ya kuaga kwa heshima za kijeshi itaanza saa tatu kamili asubuhi katika viwanja vya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Upanga na itaendelea mpaka mchana kabla ya kusafirishwa,” ilisema taarifa hiyo.
 

Wanajeshi hao ambao ni miongoni mwa askari wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kulinda Amani katika Jimbo la Darfur nchini Sudan, waliuawa kutokana na mashambulizi ya kushtukiza yaliyofanywa na waasi wanaopigana na Serikali, hivyo kuwa ni mara ya kwanza kwa idadi kubwa ya wanajeshi wa Tanzania wanaolinda amani katika nchi mbalimbali kuuawa kwa wakati mmoja.
 

Mwili wa Mr Bomba kuagwa muda huu Muhimbili rariba kamili hiko hivi

REV. John Makanyagana
Msanii John Makanyaga enzi za uhai wake
MWILI wa muigizaji mkongwe nchini, Mchungaji John Makanyaga unatarajiwa kuagwa asubuhi hii katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kabla ya saa 8 kufanyiwa misa kwenye Kanisa la Anglicana tayari kwa ajili ya kusafirishwa kwenye kuzikwa kwao Mpwapwa.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa hivi punde na Adam Malele' Swebe', mmoja wa waigizaji wenzake wa zamani wa Kaole Sanaa Group, mwili wa msanii hiyo aliyefahamika zaidi kama Mr Bomba utafanyiwa misa ya maombezi kanisa la Ilala Sharifu Shamba
Swebe alisema baada ya ibada hiyo ya mazishi kanisani hapo, mwili huo utasafirishwa kwenda Mpwapwa Dodoma kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika kesho Jumanne.
Marehemu Mr Bomba alifariki juzi hospitali ya Muhimbi kwa tatizo la uvimbe wa kansa katika ini na enzi za uhai wake alitamba na tamthilia mbalimbali kupitia kituo cha ITV kabla ya kuhamia kwenye filamu.
Pia alikuwa ni mwalimu na Mcghungaji wa kanisa la Anglakana mpaka mauti yalipomkumba, ambapo yamekuja huku watanzania wakiendelea kuuguza machungu ya vifo vya wasanii wengine wa uigizaji na muziki vilivyotokea mfululizo tangu mwaka jana.

Mwakyembe, Maugo kupaa kesho kwenda Russia

Mada Maugo

Benson Mwakyembe (kushoto)
MABONDIA watanzania wanaocheza ngumi za kulipwa, Mada Maugo 'King Maugo Jr' na Benson Mwakyembe wanatarajia kuondoka nchini kesho (Jumanne) kuelekea Russia kwa ajili michezo yao ya kimataifa dhidi ya wenyeji wao.
Wanamasumbwi hao wataondoka majira ya saa 10 jioni na watapanda ulingoni Jumamosi ya wiki hii katika mipambano yao ya uzito wa kati wa Kilo 75 (Super Middle).
Rais wa TPBO-Limited, Yasin Abdallah 'Ustaadh', aliiambia MICHARAZO kuwa, Maugo yeye ataenda kupigana na Movsur Yusupov  wakati Mwakyembe ataonyeshana kazi na Apti Ustarkhanov kwenye michezo itakayochezwa kwenye ukumbi wa Trade &Intertainment uliopo mjini Kasiysk, nchini Russia.
Ustaadh alisema mapambano yote hayo yatakuwa na raundi 8 kila mmoja na kwamba Watanzania hao wataungana na wakala wao kutoka Kenya, Thomas Mutua katika mji wa Dubai.
Rais huyo wa TPBO alisema mpinzani wa Maugo rekodi yake inaonyesha amecheza mapambano matatu na yote ameshindwa moja likiwa kwa KO wakati mpinzani wa Mwakyemba amecheza mechi mbili na kushinda moja na kuchapwa moja.
Hata hivyo, alisema pamoja na rekodi hizo zisizovutia kwa wapinzani wao, bado Maugo na Mwakyembe wanapaswa kwenda nchini humo na tahadhari kubwa kwani Warusi huwa hawaruhusu mabondia wa ngumi za kulipwa kucheza mpaka wawe wamepitia ngumi za ridhaa na kushiriki michezo ya Olimpiki.
Akizungumza safari hiyo, Mwakyembe aliiambia MICHARAZO asubuhi hii kwamba licha ya kutomfahamu vyema mpinzani wake, lakini anawaahidi Watanzania kwenda kuwawakilisha vyema katika mchezo huo wa kimataifa ambao ni wa pili kwake nje ya nchi.
"Naahidi sintowaangusha watanzania katika mechi hiyo ya Jumamosi, naenda nikiwa na imani ya kutaka kuweka rekodi kwa kumtwanga mwenyeji wangu na kurejea nchini kwa heshima zote, najiamini kwa mazoezi niliyofanya," alisema.
Kuhusu safari hiyo, Mwakyembe alisema kila kitu kimekaa vyema na kwamba panapo majaliwa ataondoka na mwenzake (Mada Maugo) kesho saa 10 jioni.

Suarez aitamani Arsenal, apanga kuiambia Liverpool

 http://images.dailystar-uk.co.uk/dynamic/58/photos/888000/620x/4888.jpg
MSHAMBULIAJI Luis Suarez anajiandaa kuiambia Liverpool kwamba anataka kuhamia Arsenal.
Gazeti la Sunday Mirror limesema kuwa Liverpool wanamsubiri Suarez aombe rasmi kuondoka ndiyo wamruhusu wakati mshambuliaji huyo wa Uruguay atakapowasili kutoka mapumzikoni mjini Montevideo na kujiunga na kambi ya mazoezi mjini Melbourne.
Arsenal wameongeza matumaini ya kumpata mchezaji huyo na wanatarajiwa kurejea Anfield na ofa nono zaidi baada ya ofa yao ya awali kukataliwa.
Suarez aliweka moyo wake kujiunga na Real Madrid lakini miamba hao wa Hispania hawajajitokeza tena kutaka kumsajili baada ya kuweka wazi kwamba ofa yao ya mwisho wanayoweza kutoa ni paundi milioni 25.
Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers, alisema kuwa thamani ya Suarez ni sawa na ya Muuruguay mwenzake, Edinson Cavani aliyeuzwa kwa paundi milioni 55 kutoka Napoli kwenda PSG. 
Arsenal wameripotiwa kuwa tayari kutoa paundi milioni 40.
Kocha Arsene Wenger anaona Suarez hana shida licha ya kuadhibiwa kwa kumfanyia vitendo vya kibaguzi Patrice Evra na kumng'ata Branislav Ivanovic kwa vile nyota huyo wa Uruguay ni mchapakazi.

Shasta ahairisha kugawa utamu wa penzi

http://thumbp4-ne1.thumb.mail.yahoo.com/tn?sid=2126005954&mid=ACbkimIAAAlPUdQbXwAAAJWB87w&midoffset=2_0_0_1_35347&partid=2&f=1215&fid=Inbox&w=480&h=297
Shasta akiwa katika pozi nyumbani kwake

MSANII wa filamu aliyejitosa pia katika muziki, Leah Mussa 'Shasta' amesitisha kwa muda harakati za kusambaza wimbo wake uitwao 'Utamu wa Penzi' ili kupisha mwezi mtukufu wa Ramadhani, imeelezwa.
Akizungumza mwishoni mwa wiki, Shasta alisema kuwa wimbo huo alioimba na H-Mbizo umeshakamilika na kilichobaki ni mambo madogo tu na kwamba, baada ya kumalizika kwa mfungo na sikukuu ya Idd ataendelea na kazi ya kuusambaza.
"Sasa wimbo huu utatoka baada ya Sikukuu ya Idd El Fitri," alisema Shasta ambaye amejitosa katika muziki baada ya kuvutiwa na wimbo 'Majanga' wa shoga yake na msanii mwenzake katika  filamu, Snura Mushi.
Baadhi ya filamu alizoshiriki Shasta ni 'Ong'wana', 'Julia', 'Kisasi za Mzimu', 'Siri za Majini' na 'Deception'.

Golden Bush Fc yazinduka Ligi ya Kinondoni

Vijana wa Golden Bush wakiwa mazoezini na kocha wao Shija Katina (kushoto) wakipeana mikakati ya kusaka ushindi katika Ligi daraja la Nne wanayoicheza kwa mara ya kwanza
BAADA ya wiki iliyopita kutibuiliwa rekodi yake ya ushindi mfululizo kwa kulazwa na Kijitonyama, timu ya Golden Bush Fc jana ilizinduka katika Ligi Daraja la Nne wilayani Kinondoni kwa kufanya 'mauaji' ya kutisha dhidi ya Shein Rangers kwa kuinyuka mabao 4-1.
Pambano hilo lililochezwa kwenye uwanja wa Mwananyamala, jijini Dar es Salaam lilishuhudia vijana wa Golden Bush inayonolewa na kocha Shija Katina na Madaraka Seleman 'Mzee wa Kiminyio' wakicharuka tangu mwanzo wa mchezo ili kurejesha heshima yake katiika lig hiyo.
Vijana hao walipata mabao yao yaliyotosha kuwafanya wafikishe pointi 15 katika kundi lake baada ya kucheza mechi 6 yalitumbukizwa kimiani na aliyekuwa nyota wa mchezo, Adilu aliyefunga mawili, Said na Kenan.
Timu hiyo inatarajiwa kushuka tena dimbani siku ya alhamis, ambapo uongozi wa timu hiyo umesema vijana wao watashuka wakiwa na lengo moja tu la kuendeleza vipigo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya pili na hatimaye kuipanda Ligi Daraja la Tatu.

Washindi shindano la kusoma Qur'an wapatikana

Msomaji wa Quran tukufu katika mashindano ya kitaifa, Abdallah Abdulkadri akisoma wakati wa fainali zake jana.

Msomaji wa Quran tukufu katika mashindano ya kitaifa, Seif Salim Said ambaye ni mremavu wa macho akisoma wakati wa fainali zake jana

Baadhi ya viongoza wa Dini wakifatilia mashindano hayo katika ukumbi wa Diamond Jubilee
Baadhi ya wanafunzi walioshiliki katika kusoma

Qur'an tukufu

Msomaji wa Quran tukufu katika mashindano ya kitaifa, Ummy Swaleh Said ambaye ni mlemavu wa macho akisoma wakati wa fainali hizo.

Baadhi ya waumini wa Dini Ya Kislam wakiongozwa na mratibu wa mashindano ya usomaji wa Qur'an Bi. Aisha Sururu wakifuatilia fainali hizo.
Bi Aisha Sururu akifuatilia mashindano hayo yaliyomalizika jana
Zawadi walizopewa washindi

Mgeni Rasmi wa Mashindano ya kuifadhi Quran tukufu kitaifa Dk, Suleiman Ally Yussuf katikati na Mkurugenzi wa Kituo cha Utamaduni cha Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ,Morteza Sabouri wakimkabidhi zawadi wa cherehani mshindi wa kusoma juzuu 20

Mgeni Rasmi wa Mashindano ya kuifadhi Quran tukufu kitaifa Dk Suleiman Ally Yussuf kulia na Mkurugenzi wa Kituo cha Utamaduni cha Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ,Morteza Sabouri wakimkabidhi zawadi ya bajaj  pamoja na pesa taslmu laki tano mshindi wa kuhifadhi Quran tukufu, Suria Ally Bakari.

Mgeni Rasmi wa Mashindano ya kuifadhi Quran tukufu kitaifa Dk Suleiman Ally Yussuf (kulia) akimkabidhi mshindi Abdul Hamid zawadi yake ya bajaj na pesa taslimu.


Baadhi ya washindi wa kuhifadhi Quran Tukufu wakiomba Dua baada ya kumalizika mashindano hayo

Afande Sele kuweka Dini videoni


Afande Sele akiwajibika jukwaani
MKONGWE wa muziki wa hip hop nchini, Seleman Msindi 'Afande Sele' yupo katika harakati za kufyatua video ya wimbo wake mpya unaoendelea kutamba kwenye vituo vya redio uitwao 'Dini Tumeletewa'.
Afande Sele aliiambia MICHARAZO kuwa ijapokuwa hivi sasa yupo mapumzikoni kuupisha mfungo wa mwezi wa Ramadhani, lakini bado anaendelea na mipango ya kukamilisha video ya wimbo huo ili kukata kiu ya mashabiki wake ambao wengi wamekuwa wakiiulizia mara kwa mara.
"Niko mbioni kutoa video ya wimbo Dini Tumeletewa nilioimba na Belle 9. Ikikamilika itasambazwa ili mashabiki wa muziki washuhudie kile nilichoimba,"alisema Afande.
Katika hatua nyingine, Afande Sele alisema kuwa tangu atoe wimbo huo amekuwa akipokea pongezi nyingi na kuombwa atoe video yake.
Msanii huyo amekuwa akijizolea sifa kemkem kutokana na nyimbo zake nyingi kuwa na mashairi yenye kugusa hali halisi ya maisha ya Mtanzania.

TMK Wanaume Family Sasa Tufurahie


KUNDI la muziki wa kizazi kipya la TMK Wanaume Family 'Mapanga Shaa', linatarajiwa kuuachia hewani wimbo wao mpya uitwao 'Tufurahie'.
Wimbo huo uliokamilika wiki iliyopita ni kati ya kazi mpya za kundi hilo baada ya kutamba na 'Kichwa Kinauma' na 'Tutaonekanaje'.
Akizungumza na MICHARAZO, Meneja wa TMK, Said Fella alisema wimbo huo ulirekodiwa katika studio za Tuddy Thomas wa Ngoma Records na utaachiwa leo Jumatatu.
Fella alisema katika wimbo huo, kazi kubwa imefanywa na YP, Mheshimiwa Temba na Said Chegge, na kwamba wanatumai utafanya vizuri kama ilivyokuwa kwa nyimbo zao nyingine.
"Umeandaliwa vizuri na hivyo tunaamini kwamba nao utatamba," alisema Fella.
Katika hatua nyingine, Fella alisema video ya wimbo wa msanii Is'haka Aslay 'Dogo Aslay' uitwao 'Bado Mdogo' alioimba kwa kushirikiana na Linnah wa THT imekalimika.
Wimbo huo umeelezewa na Dogo Aslay kuwa ni kisa cha kweli, akidai kwamba yupo mama mwenye umri mkubwa aliyekuwa akimghasi kwa kumtaka kimapenzi licha ya yeye kumkatalia kwa kumwambia kuwa yeye (Aslay) bado mdogo na hivyo asingependa kujihusisha na masuala hayo ya mapenzi.

Mbwana Samatta azidi kung'ara Afrika

Mbwana Samatta alipokuwa akiitumikia Stars dhidi ya Morocco

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ameendelea kung’ara katika michuano ya Afrika, baada ya mwishoni mwa wiki kuifungia timu yake ya TP Mazembe ya DR Congo bao lililoipa sare ya 1-1 ugenini dhidi ya ESS ya Algeria.
Katika pambano hilo lililochezwa Ijumaa kwenye uwanja wa Mei 8, 1945 la ufunguzi wa hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Afrika kwa kundi B, wenyeji walilazimika kulichomoa bao hilo la Samatta.
Samatta alifunga bao hilo katika dakika ya 81 , lakini hata hivyo dakika mbili baadaye wenyeji walichomoa kupitia kwa beki wao Mourad Delhoum.
TP ya Samatta sasa itarejea nyumbani kuisubiri FUS Rabat ya Morocco katika pambano lao litakalochezwa mjini Lubumbashi Agosti 4.

Sunday, July 21, 2013

Maskini! Papii Kocha alilia tena Rais Kikwete

MUIMBAJI Nyota wa zamani wa bendi ya FM Academia, Papii Kocha amemuandikia ombi jingine maalum Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kumuomba MSAMAHA wa kufutiwa adhabu yake ya kifungo cha maisha jela alichopewa yeye na wanafamilia yake kwa kesi ya kubaka.
Ujumbe huo unaelezwa ni wa mara nyingine tena kwa msanii huyo aliyepo gerezani na baba yake, japo hakujawa na hakika kama barua hizo zinamfikia Mheshimiwa na kuzisoma au la. Ebu isome mwenyewe barua hiyo ya 'Mwana Mfalme' Papii Kocha kwenda kwa Rais Jakaya Kikwete...inaumiza!
MF/NA: 836'04 Johnson Nguza
(Papii Kocha) Gereza Kuu Ukonga
S.L.P 9091
Dar es Salaam
Mh. Rais Jamuhuri ya Muungano Tanzania

YAH: MAOMBI YA KUPEWA MSAADA (MSAMAHA) WA KUFUTIWA ADHABU YA KIFUNGO NILIYOPEWA NA MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI KISUTU.

Husika na somo hilo hapo juu. Mimi ni mfungwa katika gereza kuu Ukonga. Kwa heshma na taadhima na kwa kutambua utu na huruma yako ya kiMUNGU ulionayo dhidi ya binadamu wenzako pamoja na mamlaka uliokabidhiwa na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Naanguka na kushika miguu yako mitukufu muheshimiwa rais....Nakuomba msaada (msamaha) kwako muheshimiwa rais, kwa njia hii ya maandishi kusudi niweze kuondolewa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani, niliyohukumiwa na mahakama tajwa hapo juu. Mh.Rais mimi nimefungwa nikiwa bado kijana mwenye umri mdogo, na ukweli kutoka moyoni sikufanya kosa hilo.

Si mimi, baba yangu Nguza wala ndugu yangu yeyote aliyefanya kitendo kile. Lakini wenye mamlaka wakatuona tuna hatia na kuamua kuteketeza kizazi chetu gerezani.

Natamani kiama ifike ili mwenyezi Mungu aweke wazi ukweli wote uliojificha nyuma ya pazia. Mpaka sasa natambua wazi hatima pamoja na dhamana ya maisha yangu ipo katika mikono yako mitukufu Mh. Rais Naomba huruma yako muheshimiwa Rais maana mimi ni mtoto wako ninaehitaji huruma yako wewe mzazi. Lakini pia sisi ni binadamu wenye nafsi na miili kama wengine. Waliotumia mamlaka yao kutuweka gerezani nao ni binadamu pia, wenye miili na nafsi.

Ipo siku nafsi zetu zitapaswa kutoa hesabu ya tuliyoyafanya hapa duniani. wakati huo miili yetu tunayoitumia kunyanyasa wanyonge itakuwa imeoza mavumbini.

Natumaini kauli yako ya mwisho ndio itakayoleta pumzi ya uhai nafsini mwangu. Nakutakia kazi njema, afya njema na maisha marefu. Mungu akubariki. Wako mtiifu

Mfungwa NO:836'04 JOHNSON NGUZA (PAPII KOCHA)
 
Udaku Specially