STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, January 2, 2014

'Mjeda' awatungua risasi wawili na kuwaua mwaka mpya


MWANAJESHI wa Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ), ambaye jina lake limehifadhiwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya  kuwaua kwa kuwapiga risasi vijana wawili na kisha kuwajeruhi vibaya wengine wawili walipokuwa katika shamrashamra za kuukaribisha mwaka mpya.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa sita na robo usiku wa kuamkia jana, katika eneo la Pugu Kinyamwezi, Ilala jijini Dar es Salaam.

Akizungumza  jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Marietha Minangi alisema tukio hilo lilitokea baada kundi la vijana waliokuwa wakisherehekea mwaka mpya kuzingira gari la mwanajeshi huyo aliyekuwa akielekea nyumbani kwake Pugu Kinyamwezi, akitokea katikati ya Jiji kwa shughuli zake.

Alisema mwanajeshi huyo alikuwa na gari aina ya Toyota Rava 4 na  baada ya kufika katika eneo hilo alizingirwa  na  kundi la vijana hao waliokuwa wakisherehekea mwaka mpya na ndipo aliamua kutoa  bastola yake na  kufyatua risasi ambapo iliwapata vijana hao na kufa papo hapo na kujeruhi wengine.

Aliwataja waliokufa katika tukio hilo kuwa ni Ibrahim Mohamed(16) mkazi wa Pugu Kinyamwezi, Abubakari Hassan(14) naye mkazi wa Pugu Kinyamwezi.

Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Rupano Wanga(17)  mkazi wa Pugu Makange na Kassim Abdul  (16), mwanafunzi wa shule ya sekondari Tandika.
Minangi alisema polisi walifanikiwa kumkamata mwanajeshi huyo na kumweka rumande  katika kituo cha polisi cha stakishari usiku huohuo.

Alisema vijana hao waliojeruhiwa walipelekwa Hospitali ya Amana kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.

Wakati huohuo, wakazi wa Kiwalani, Wilayani Temeke walipata wakati mgumu baada ya kutokea kwa kundi la vibaka waliokuwa wakipora simu, fedha na kutembeza mapanga kwa wakazi hao.

Kwa mujibu wa baadhi ya wakazi wa maeeno hayo, kundi hilo lilikuwa likizungukia kila nyumba na katika nyumba za starehe na kila aliyekutwa nje walichukua simu yake, fedha  na wengie kupigwa mapanga.

Yaya Toure 'anusa' tuzo nyingine Afrika


CAPE TOWN, Afrika Kusini
YAYA Toure anatarajiwa kutangazwa kuwa Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Afrika na kuifikia rekodi ya kuibeba tuzo hiyo mara tatu mfululizo baada ya kutajwa katika orodha ya wachezaji watatu walioingia fainali kwa ajili ya tuzo hiyo itakayotolewa mwezi huu.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilipunguza majina ya wanaoiwania tuzo hiyo 2013 kutoka 10, huku Toure akibaki na wachezaji 'wachovu' Didier Drogba (Ivory Coast) na John Obi Mikel (Nigeria/ Chelsea).
Jopo la makocha wa timu za taifa kutoka nchi 54 za Afrika litaamua mshindi, ambaye atatajwa katika hafla itakayofanyika mjini Lagos Januari 9.
Miongoni mwa waliokatwa katika orodha hiyo ni Mohamed Aboutrika, kiungo veterani wa Misri, ambaye Novemba aliiongoza klabu yake ya Al Ahli kutwaa taji la tano la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ndani ya miaka kumi iliyopita.
Mwingine aliyekatwa ni Jonathan Pitroipa, nyota wa timu ya taifa ya Burkina Faso ambayo iliukosa ubingwa wa Mataifa ya Afrika nchini Afrika Kusini mwanzoni mwa mwaka na kwenye kampeni za kufuzu kwa Kombe la Dunia.
Wote hao walitarajiwa kuwa washindani wa karibu zaidi wa Yaya Toure, ambaye anapewa nafasi kubwa kushinda kutokana na mafanikio binafsi katika mwaka ambao hapakuwa na wachezaji waliokuwa na mafanikio binafsi.
Toure aliisaidia Ivory Coast kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia na amerejea kuwa nguzo muhimu katika kikosi cha klabu yake ya Manchester City ya Ligi Kuu ya England.
Kama atafanikiwa kuitwaa tuzo hiyo, kiungo huyo atakuwa mchezaji wa tatu kuitwaa tuzo hiyo mara tatu mfululizo, akiwafikia Abedi Pele wa Ghana aliyeitwaa kuanzia 1991-93 na Samuel Eto'o kuanzia 2003 hadi 2005.
Mikel, ambaye anasota benchi katika klabu yake ya Chelsea, ametajwa kutokana na mchango wake katika kuisaidia Nigeria kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia na kutwaa ubingwa wa Mataifa ya Afrika mwanzoni mwa 2013.
Drogba ni mshindi mara mbili wa tuzo hiyo lakini straika huyo wa Galatasaray ameshangaza wengi kutajwa katika orodha ya walioingia fainali mwaka huu baada ya mwaka ambao alitemwa katika timu yake ya taifa ya Ivory Coast.

Manchester Man 'nyanya' kwa Tottenham

Adebayor akifuka juu kuupiga mpira uliozaa bao la kwanza la Spurs
Adebayor akiifungia Spurs bao la kuongoza
Oyoooooo! vijana wa Spurs wakishangilia bao lao la pili
MASHETANI Wekundu wamezidi kumweka pabaya kocha wake, David Moyes baada ya jana kupokea kipigo cha mabao 2-1 wakiwa nyumbani  mbele ya vijana wa Tottenham Hotspur.
Manchester Utd ambayo msimu huu imekuwa 'urojo' ilipokea kipigo hicho ikiwa ni mara ya kwanza baada ya kipindi kirefu kufungwa na Spurs nyumbani kwake.
Mabao ya Emmanuel Adebayor aliyefunga kipindi cha kwanza kwenye dakika ya 34 na jingine la Eriksen la dakika ya 66 yalitosha kuizamisha Mashetani hao.
Bao la kufuitia machozi la vijana wa Moyes lilifungwa dakika moja baada ya Spurs kupata bao lao la pili kupitia kwa Danny Welbeck.
Kipigo hicho kimeifanya Man Utd iporomoke kutoka nafasi ya sita hadi ya saba na kuipisha Spurs kuwa juu yao kwa tofauti ya pointi tatu.
Spurs ambayo imekuwa na matokeo mazuri tangu ilipomtimua AVB na kupewa Tim Sherwood imekusanya pointi 37 huku Man Utd ikiwa na 34. dakika ya 67. Timu zote zikicheza mechi 20 kila moja.

Wednesday, January 1, 2014

Ajali! Wa3 wafa, basi la Taqwa lapata ajali Moro

Taarifa zilizofika hivi punde zinasema kuwa basi la Taqwa limegongana na lori na kusababishja ajali ya watu watatu na wengine kujeruhiwa.
Ajali hiyo inadaiwa kutokea eneo la Mikumi, mkoani Morogoro wakati basi hilo likidaiwa kutaka ku-overtake lori na kukutana uso kwa uso na lori jingine na kusababisha vifo vya abiria hao wanawake wakiwa wawili na mwanaume mmoja.
Taarifa zaidi zinaendelea kufuatiwa na mtajulishwa
1388581742264 1388581761327


PIGO! Waziri Mgimwa afariki, Rais Kikwete amlilia

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Waziri wa Fedha, Mheshimiwa William Mgimwa, aliyekuwa pia Mbunge wa Jimbo la Kalenga (Mkoa wa Iringa) kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Rais Kikwete amesema kuwa taifa limempoteza Waziri Mgimwa katika kipindi lilipokuwa linamhitaji zaidi kutokana na mchango wake mkubwa ambao amekuwa akiutoa kupitia nafasi zake za Waziri wa Serikali na mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Kalenga.

Kifo cha Mheshimiwa Mgimwa kimetangazwa mchana wa leo, Jumatano, Januari Mosi, 2014, na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK) Balozi Ombeni Sefue kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika tangazo lake, Balozi Sefue amesema kuwa Waziri Mgimwa ameaga dunia asubuhi ya leo saa 5:20 (Saa za Afrika ya Kati) katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic , Pretoria, Afrika Kusini ambako amekuwa amelazwa kwa muda sasa.

Balozi Sefue amesema kuwa maandalizi ya kuurudisha nyumbani mwili wa Waziri Mgimwa yanafanywa na Serikali kwa kushirikiana na familia yake na kuwa taarifa zaidi za suala hilo zitatolewa baadaye kwa kadri zinavyopatikana na maandalizi yanavyoendelea.

Katika salamu zake kwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda na kwa familia ya Marehemu Mgimwa, Rais Kikwete amesema:  “Sina maneno ya kutosha kuelezea mshtuko na huzuni yangu kubwa kufuatia taarifa za kifo cha Mheshimiwa Mgimwa.

Binafsi nimemtembelea mara mbili kwenye Hospitali alikokuwa amelazwa na mara ya mwisho hali yake ilikuwa imeimarika. Tulizungumza kwa kiasi cha dakika 10 hivi akanielezea nia yake na tamaa yake ya kurejea nyumbani kwa sababu hali yake ilikuwa nzuri.”

Ameongeza Mheshimiwa Rais Kikwete: “Sote tunajua mchango wake katika Serikali. Sote tulitamani kuendelea kuwa naye, lakini haya ni mapenzi ya Mungu.”

“Napenda kutoa pole nyingi na rambirambi zangu za dhati kwa wana-familia wote kwa kuondokewa na mhimili wao. Naungana nanyi katika kuomboleza msiba huo mkubwa. Napenda mjue kuwa msiba huu ni msiba wangu pia. Machungu yenu ni majonzi yangu,” amesema Rais Kikwete.

Rais pia amewatumia rambirambi wananchi wa Jimbo la Kalenga akisema kuwa wamempoteza mwakilishi na mtetezi mahiri wa maslahi yao.

Mgimwa aliyezaliwa January 20, 1950 na kuwa mbunge wa jimbo la Kalenga mkoani Iringa kupitia chama cha Mapinduzi (CCM)

Dk. Mgimwa alikuwa mkufunzi katika Chuo cha Benki mkoani Mwanza, kabla ya kufanikiwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mkoa wa Iringa, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Arsenal yarejea kileleni, Chelsea, Liver zaua Suarez hakamatiki

Nicklas Bendtner
Nicklas Bendtner akifunga bao la kwanza la Arsenal
Fernando Torres
Torres alipoondoa 'gundu' kwa kuifungia Chelsea bao la kwanza
Daniel Agger scores for Liverpool
Liverpool ilipoisulubu Hully City uwanja wa Anfield

Nicolas Anelka of West Bromwich Albion takes on Michael Williamson (right) and Yohan Cabaye of Newcastle
West Bromwich walipoilaza Newcastle United kwa bao la mkwaju wa penati

MABAO ya dakika za lala salama wameiwezesha Arsenal kurejea tena kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England, huku Chelsea ikiendelea kuonyesha makali yake kwa kupata ushindi ugenini dhidi ya Southampton.
Aidha Liverpool nayo imerejesha makali yake baada ya kusimamishwa hivi karibu kwa kupokea vipigo viwili mfululizo baada ya kushinda nyumba mabao 2-0, Luis Suarez akifunga bao lake la 20 katika ligi ya msimu huu.
Nicklas Bendtner aliifungia Arsenal bao dakika ya  88'  na Tim Walcott kuongeza bao la pili dakika za nyongeza za mchezo huo kumalizia kazi ya Jack Walshere iliifanya Arsenal ipumue kwa kuilaza Cardiff City na kurejea tena kileleni ilipokuwa imeshushwa na Manchester City iliyoshinda ugenini jioni hii.
Arsenal imefikisha pointi 45 moja zaidi ya City na kurejesha msimamo wa awali uliokuwapo baada ya timu zote za Top 4 kushinda jioni hii, Chelsea ikiinyoa Southampton mabao 3-0 huku Liverpool ikiwa nyumbani ikiitambia Hull City mabao 2-0.
Katika mechi ya Chelsea mabao yao yalifungwa na  Fernando Torres dakika ya 60 kabla ya William kuongea la pili dakika ya 71 akimalizia kazi ya Oscar.
Oscar aliihakikisha Chelsea inayonolewa na Jose Mourinho ushindi kwa kufunga bao la tatu dakika nane kabla ya kumalizika kwa mchezo huo akimalizia kazi ya Eden Hazard.
Liverpool ilipata ushindi wake nyumbani kupitia kwa Daniel Agger dakika ya 36 na Luis Suarez akafunga bao lake la 20 katika dakika ya 50 na kuipa 'vijogoo' hao wa Anfield ushindi muhimu katika mbio zake za kuwania ubingwa unaoshikiliwa na Manchester United.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizomalizika hivi punde, Crystal Palace ikiwa nyumbani ililazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Norwich City, Fulham iliinyoa West Ham United kwa mabao 2-1 ikiwa nyumbani na     Stoke City iliing'ang'ania Everton na kutoka sare ya  1-1.
Nayo West Bromwich baada ya kufanywa asusa kwa muda mrefu imejitutumua nyumbani kwa kuilaza Newcastle United kwa bao 1-0.
Msimamo wa ligi hiyo unaonyesha Arsenal wapo kileleni ikiwa na pointi 45 ikifuatiwa na Man City yenye pointi 44, kisha Chelsea ikifuatia ikiwa na pointi zake 43 na Livewrpool kurejea kwenye Top 4 kwa kufikisha pointi 39 na Everton ikikamilisha Tano Bora na pointi zake 38.
Pambano la mwisho la ligi hiyo itazikutanisha Manchester United itakayokuwa nyumbani dhidi ya Tottenham ambapo hata zikifungana haziwezi kubadili msimamo wa juu kwani zote zina pointi 34.

City yauanza mwaka kileleni, ila...!

Fernandinho low strike puts Manchester City ahead against Swansea City.
USHINDI wa mabao 3-2 iliyopata klabu ya Manchester City dhidi ya wenyeji wao Swansea City imeiwezesha timu hiyo kukwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England jioni hii ikiengua Arsenal iliyopo uwanjani kwa sasa ikiumana na Cardiff City.
City itakuwa kileleni kusubiri kuona kama itaendelea kusalia au itarejea nafasi ya pili kutegemea matokeo ya Arsenal waliopo nyumbani kwao uwanja wa Emirates.
Fernandinho ndiye aliyeanza kuiandikia City bao la kuongoza dakika ya 14 kabla ya Wilfried Bony kurejesha sekunde chache kabla ya mapumziko akimaliza kazi ya Guzman.
Kipindi cha pili kilianza kwa City kuongeza bao la pili kupitia kiungo wa kimataifa wa Ivory Coast, Yaya Toure katika dakika ya 58  kabla ya Kolarov kuongeza bao jingine la tatu katika dakika ya 66 na kuipa nafuu City ugenini.
Hata hivyo  wenyeji walichomoa bao moja baada ya Bony kufunga bao jingine dakika ya 90 ambalo hata hivyo halikuisaidia Swansea kupona na kipigo kwa wageni wao ambao kwa ushindi huo wamefikisha pointi 44.

Monday, December 30, 2013

Rais Kikwete akabidhiwa Rasimu ya Katibu Mpya

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete leo amepokea rasmi Rasimu ya Katiba Mpya ambayo itajadiliwa hapo baade na Bunge maalum la Katiba. 
Rais Kiwete aliipokea Rasimu hiyo kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba katika makabidhiano yaliyofanyika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam. Kuisoma zaidi rasimu hiyo Bofya hapa RASIMU YA KATIBA

Miyeyusho abadilishiwa mpinzani toka Kenya

Bondia Joshua Amukulu (kushoto) kutoka Kenya akitunishiana misuli na Francis Miyeyusho wakati wa upimaji uzito kwa ajili ya mpambano wao utakaofanyika kesho Desemba 31. Awali ilitangazwa Miyeyusho angepigana na David Chalanga.

Bondia Kalama Nyilawila kushoto akitunishiana misuli na Ibrahimu Maokola  baada ya kupima uzito kwa ajili ya mpambano wao utakaofanyika Desemba 31 siku ya jumanne katika ukumbi wa New Msasani Club.
Bondia Francis Miyeyusho akipima uzito kwa ajili ya mpambano wake  Joshua Amukulu kutoka Kenya utakaofanyika kesho jumanne katika ukumbi wa Msasani Club.
BONDIA FRANSIC MIYEYUSHO AKIHOJIWA NA WAANDISHI WA HABARI BAADA YA KUPIMA UZITO KWA AJILI YA MPAMBANO WAKE NA MKENYA JOSHUA AMUKULU UTAKAOFANYIKA DESEMBA 31 KATIKA UKUMBI WA MSASANI CLBU (PICHA ZOTE NA SUPER D)
Bondia Ibrahimu Class 'king Class Mawe'  kushoto akitunishiana misuli na Mustafa Dotto  baada ya kupima uzito kwa ajili ya mpambano wao utakaofanyika kesho jumanne katika ukumbi wa Msasani Club.
IBRAHIMU CLASS 'KING CLASS MAWE AKIPIMWA AFYA
 IDDY MNYEKE AKIPIMWA AFYA

TBF yapata viongozi wapya, Maluwe, Phares chali Dodoma

Michael Maluwe (kushoto) na Magessa waliangushwa jana Dodoma
SHIRIKISHO la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) limefanikiwa kupata safu mpya ya uongozi baada ya John Bandie kuchaguliwa kuwa Rais Mpya wa shirikisho hilo.
Uchaguzi huo ulifanyika jana mjini Dodoma na kutangazwa na Mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Jamal Rwambow.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Dodoma na kuthibitishwa na mmoja wa makocha maarufu wa mchezo huo aliyechaguliwa kuwa Kamishna wa Ufundi na Mashindano Manase Zablon kupitia akaunti yake ya facebook, Rais huyo mpya alipata ushindi huo akimgaragara Phares Magessa.
Magessa alikuwa Makamu wa Rais katika uongozi uliomaliza muda wake ambaye alijikuta akipata kura 19 dhidi ya kura 24 za mpinzani wake aliyeibuka mshindi.
Katika nafasi ya Makamu wa Rais ilienda kwa Hamis Jafar aliyepata kura 39 za Ndiyo huku nne zikimkataa kwani alikuwa mwenyewe katika nafasi hiyo.
Kiongozi maarufu wa zamani wa mchezo huo, Saleh Zonga aliibuka kidedea kwenye nafasi ya Katibu Mkuu, akimshinda aliyekuwa Katibu Mkuu Msaidizi, Michael Maluwe kwa kupata kura 24 dhidi ya 13 za mpinzani wake.
Amina Ahmed alifanikiwa kuchaguliwa kuwa Mhazini wa shirikisho hilo kwa kupigiwa kura za ndito 43, huku Manase Zablon akichaguliwa kuwa Kamishna wa Ufundi na Mashindano kwa kupata kura 37 za ndiyo na mbili kumkataa.
Wengine walishinda katika uchaguzi huo ambao awali ulipangwa kufanyika Desemba 10 mjini Mbeya na kukwama kabla ya kuhamishiwa Dodoma ni Michael Mwita aliyechaguliwa Kamishna wa Mipango kwa kura 39, huku Kamishna wa Watoto na Shule ikienda kwa Patrick Matete, Angela Bondo akichaguliwa Kamishna ya Wanawake na upande wa Walemavu nafasi ilienda kwa Aziz Mtogole.

Swagger sasa aja na Bongo Series Extra

Swagger katika pozi
MTAYARISHAJI wa filamu aliyewahi kutamba kwenye muziki wa kizazi kipya akiwa na kundi la Crime Busters, Hussein Ramadhani 'Swagger' anatarajiwa kuibuka na kipindi kipya cha burudani cha kwenye runinga kiitwacho 'Bongo Series Extra'.
Akizungumza na MICHARAZO, Swagger alisema kipindi hicho kitakachokuwa kikionyesha tukio kali la wiki, onyesho 'live' la burudani jukwaani, mahojiano ya msanii mkali wa wiki pamoja na kuangalia watoto wa mitaani waishivyo na pamojana mapitio ya filamu, kimeshakamilika ingawa bado hajajua kitarushwa kwenye kituo gani.
"Kila kitu kimekamilika na tayari nipo kwenye mazungumzo na baadhi ya vituo vya televisheni kwa ajili ya kuruhusu kurushwa hewani, hivyo wapenzi wa burudani wakae mkao wa kula kupata burudani ya aina yake kwani Bongo Series Extra imeshiba vya kutosha," alisema.
Swagger aliyeanza kuigiza michezo ya kwenye runinga kupitia kundi la Niger Theare akiwa na mmoja wa waasisi wa michezo ya kwenye televisheni kupitia kituo cha DTV, Qudrat Olomoda 'Chombeza', alisema aliamua kuja na kipindi hicho chenye mambo mseto ili kuwakamata mashabiki ambao walikuwa wanakosa kipindi cha namna hiyo.
Alisema ukiondoa masuala ya muziki na filamu pia kipindi hicho kitakuwa kinamulika maisha halisi ya watoto wa mitaani ili kusaidia kuizundua jamii na serikali kwa ujumla kujua tatizo hilo namna lilivyo na kuangalia jinsi ya kuwasaidia.
"Hakuna asiyejua tatizo la watoto wa mitaani au wanaoishi katika mazingira magumu, lakini nani anayejua ugumu wanaokutana nao mitaani, watasaidiwaje ili kuwafanya wafurahie maisha kama watoto wengine. Hivyo tumeona tuje namna hiyo," alisema Swagger.
Swagger ambaye kwa sasa yupo mbioni kukamilisha filamu yake mpya iitwayo 'Nyaraka' iliyowashirikisha wasanii mbalimbali wakiwemo Mzee Magari na wengine alisema anatarajia maombi yake ya kurusha kipindi hicho yakikamilika na kukubaliwa mashabiki wa burudani na jamii nzima itaburudika vya kutosha.

Kocha Logarusic 'afagiliwa' Simba

Ibrahim Twaha, katika mazoezi ya siku za nyuma
Kocha Logarusic aliyefagiliwa
KIUNGO Mshambiliaji wa klabu ya Simba, Ibrahim Twaha 'Neymar', amemwagia sifa kocha mpya wa klabu hiyo, Zdravko Logarusic 'Loga' kwamba ni bonge na kocha na kuwa na imani ya kuipa Simba ubingwa katika Ligi Kuu msimu huu.
Aidha mchezaji huyo amesema anashukuru ameanza mazoezi mepesi baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu, japo anajisikia vibaya kuikosa michuano ya Kombe la Mapinduzi inayotarajiwa kuanza rasmi kesho visiwani Zanzibar.
Akizungumza na MICHARAZO, Twaha aliyesajiliwa na Simba kutoka Coastal Union akifahamika kwa jina la utani kama 'Messi' na kubadilishiwa jina kuwa 'Neymar', alisema japo hajaanza kufundishwa na kocha huyo lakini amekuwa akihudhuria mazoezi ya timu hiyo na kuvutiwa na ufundishaji wa Logarusic.
Twaha alisema Mcroatia huyo ni bonge la kocha na hataki mchezo na anayependa timu kucheza kwa kasi kitu ambacho kwa wachezaji waliopo Simba akiwemo yeye wataimudu na kuiletea klabu yao mafanikio.
"Siyo siri kocha wetu mpya ni kocha mzuri, anataka timu icheze kwa kasi na wachezaji kujituma na kujitambua bila kusubiri kusukwa kitu ambacho ni kizuri na nina imani ataisaidia Simba kutwaa ubingwa msimu huu," alisema Twaha.
Twaha, alisema kitu cha muhimu kwa wachezaji wenzake kuzingatia maelekezo ya mwalimu huyo aliyedai ni mmoja wa makocha wasiotaka masihara kazini kitu ambacho anaamini kitajenga nidhamu nzuri kwa timu yao.
Mchezaji huyo aliyekuwa majeruhi wakati duru la kwanza la Ligi Kuu Tanzania Bara likielekea ukingoni, alisema anashukuru hali yake imeanza kutengemaa kwa kufanya mazoezi mepesi akisubiri ripoti kamili ya daktari wa timu yao ili kama aanze kujumuika na wenzake.
"Nashukuru nimeanza kufanya mazoezi mepesi, na leo jioni natarajia kuonana na daktari kunikagua, ila najisikia vibaya kuyakosa mashindano ya Kombe la Mapinduzi, lakini kama hali itaimarika zaidi naamini nitaanza mechi za duru la pili la ligi kuu mwakani," alisema Twaha.
Simba ilimnyakua Logarusic aliyewahi kuinoa Gor Mahia-Kenya baada ya kumtimua Abdallah Kibadeni mara baada ya kumalizika kwa duru la kwanza.

Oscar Joshua 'aigwaya' Al Ahly Ligi ya Mabingwa Afrika

Oscar Joshua
BEKI kisiki wa timu ya Yanga, Oscar Joshua ameibuka na kuitahadharisha klabu yake kwa kuitaka kuwa makini na kujiandaa vyema kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ili ising'olewe mapema kwenye michuano hiyo.
Joshua, beki wa pembeni alisema mechi ambayo Yanga inapaswa kuwa makini nayo ni ile dhidi ya mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Al Ahly ya Misri watakaocheza nao iwapo watafanikiwa kuing'oa Komorozine ya Comoro.
Joshua alisema Al Ahly ndiyo timu pekee inayoonekana kuwa kikwazo kwa Yanga na kama itajipanga na kuitoa itajifungulia njia ya kufanya vyema kwenye michuano hiyo itakayoishiriki mwakani.
Akizungumza na MICHARAZO, Joshua alisema Al Ahly ni hatari sana kwa Yanga, lazima klabu yao ijiandae na kujipanga vyema.
"Al Ahly ni hatari sana wale, ni muhimu kwetu kujipanga vyema ili kuweza kuwatoa. Hii ndiyo timu tishio kwa Yanga michuano ya mwakani," alisema.
Beki huyo anayemudu nafasi nyingi uwanjani mbali na kucheza kama beki wa kushoto alisema, kwa kikosi kilichopo Yanga ikijipanga inaweza kufanya maajabu.
Yanga inatarajiwa kuvaana na Al Ahly katika mechi ya raundi ya kwanza mapema mwezi Machi, na hii ni iwapo tu watafanikiwa kuindosha mashindanoni Komorozine ya Comoro wanaotarajiwa kuanza nao kwenye hatua ya awali kati ya Februari 7-9 na kuridiana nao wiki mbili baadaye.
Rekodi pekee ya Yanga ya kujivunia kwenye michuano hiyo ya Afrika ni kucheza hatua ya makundi mwaka 1998 na kucheza Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mara mbili mfululizo 1969 na 1970.

Miyeyusho, Mkenya kumaliza ubishi kesho Msasani


BINGWA wa Ngumi za Kulipwa wa Kimataifa anayetambuliwa na UBO, Francis Miyeyusho na Mkenya David Chalanga wanatarajiwa kupima uzito na afya zao asubuhi hii kabla ya kesho kupanda ulingoni kupigana jijini Dar es Salaam.
Mabondia hao watapigana kesho kwenye ukumbi wa New Msasani Club katika pambano lisilo la ubingwa la kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka 2014 ambalo litasindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi.
Kwa mujibu wa Rais wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO-Limited), Yasin Abdallah 'Ustaadh' mabondi wote watakaopanda kesho ulingoni watapimwa uzito wao leo kuanzia saa 3 asubuhi.
Ustaadh alisema zoezi hilo la upimaji wa afya na uzito litafanyika kwenye ukumbi huo wa New Msasani na kuwasisitizia mabondia hao kuwahi mapema.
Mkenya David Chalanga aliwasili nchini juzi usiku akitokea kwao Kenya tayari kwa ajili ya pambano hilo la uzani wa Bantam.
"Bondia David Chalanga ameshatua nchini kwa ajili ya kupigana na Miyeyusho na Jumatatu (leo) watapima uzito na afya zao kabla ya kupanda ulingoni Desemba 31," alisema Ustaadh.
Ustaadh alisema wengine watakaopima uzito na afya zao leo kabla ya kusindikiza pambano la Miyeyusho ni Kalama Nyilawila atakayecheza na  Ibrahimu Maokola,  Ibrahimu Class 'King Class Mawe' atakayevaana na Mohamed Kashinde.
Mabondia wengine watakaopigana hiyo kesho ni Cosmas Cheka dhidi ya Idd Mnyeke, Anthony Mathias atakayepimana ubavu na Fadhili Majiha na Nyota wa muziki wa Hiphop, Karama Masoud 'Kalapina' ataonyeshana kazi na Kimbunga Noma .
Kocha wa Ibrahim Class, Rajab Mhamila 'Super D' aliiambia NIPASHE bondia wake yupo tayari kumtoa nishai mpinzani wake kwa jinsi alivyomuandaa.
Super D, alisema anaamini bondia wake atamshinda Kashinde mapema ili kuendeleza rekodi yake na kuuaga vyema mwaka 2013.

Sunday, December 29, 2013

Zilizoboronga dirisha dogo zapewa muda hadi Jan.10 kurekebisha

 
Awadh Juma (kulia0 mmoja wachezaji sita wapya wa Simba.

KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imekutana Jumamosi (Desemba 28, 2013) kujadili mambo mbalimbali yaliyofikishwa mbele yake ikiwemo usajili wa dirisha dogo ambapo klabu zenye matatizo zimepewa hadi Januari 10 mwakani kurekebisha.
Taarifa ya TFF, imesema baadhi ya klabu ikiwemo Simba zimezidisha idadi ya wachezaji, hivyo zimepewa hadi muda huo kupunguza ambapo zikishindwa kazi hiyo itafanywa na Kamati yenyewe.
Simba ina nafasi tano za kujaza kwenye dirisha dogo lakini imewasilisha majina ya wachezaji sita.
Pia klabu nyingine zimetakiwa ama kuvunja mikataba ya wachezaji au kuendelea kuwa nao, na si kuendelea kuwalipa mishahara wakati imeshawaondoa katika orodha yao.
Kuhusu mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi aliyesajiliwa Yanga, TFF imesema inafahamu kuwa klabu ya Simba bado haijalipwa fedha za kumuuza klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia na itasaidia kufuatilia FIFA fedha za mauzo ya mchezaji huyo.

Rage funika bovu...awagaragaraza akina Kinesi hivi hivi

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
MWENYEKITI wa Simba, Ismail Aden Rage amewagaragaza wapinzani wake baada ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kumtambua na kumtaka aitishe Mkutano Mkuu kwa klabu hiyo kwa mujibu wa taratibu za klabu ya Simba.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyokutana Jumamosi (Desemba 28, 2013) kujadili imebaini upungufu kadhaa wa kisheria kwenye uamuzi wa Kamati ya Utendaji ya Simba uliofanywa Novemba 18, 2013 kwa kumsimamisha Mwenyekiti wao.
Upungufu huo ni pamoja na ukiukwaji wa Ibara ya 33 ya Katiba ya Simba juu uitishaji wa mkutano, ajenda ya kumsimamisha Mwenyekiti kuwasilishwa kwenye kikao kwa utaratibu wa mengineyo.
Changamoto nyingi zilizoelekezwa kwa Mwenyekiti huyo zingeweza kupatiwa ufumbuzi kwa kutumia Ibara ya 16(2) ya Katiba ya Simba.
Hivyo, agizo za Rais wa TFF, Jamal Malinzi kumtaka Mwenyekiti wa Simba aitishe mkutano lipo palepale. Pia Mwenyekiti ametakiwa kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti kwa kuzingatia Katiba ya klabu hiyo.
Katika mkutano huo wa kujaza nafasi, ndiyo utakaojadili mgogoro kati ya Mwenyekiti na Kamati yake ya Utendaji. Nafasi hiyo kwa sasa inakaimiwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Joseph Itang’are baada ya Geofrey Nyange aliyekuwa akiishikilia kujiuzulu.
TFF inakumbusha wanachama wake wote (vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu) kuzingatia Katiba zao. Kamati pia imegundua ukikwaji wa maadili katika suala hili, hivyo, litapelekwa katika kamati husika.
Kwa vile maslahi ya TFF ni kuona mpira wa miguu unachezwa kwa utulivu, itazikutanisha pande husika wakati wowote kuanzia sasa.
Katika hatua nyingine, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imekitaka Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) kuwasilisha ajenda na muhtasari wa vikao vilivyofanya uamuzi wa kumvua madaraka Katibu wake Riziki Majalla.
Ajenda na muhtasari unaotakiwa ni wa vikao vya Kamati ya Utendaji iliyomsimamisha Katibu huyo kutokana na tuhuma mbalimbali dhidi yake, na Mkutano Mkuu ambao ulimvua madaraka.
Aidha, TFF imewataka wanachama wake kuheshimu uamuzi halali unaofanywa na vyombo vyake kwa kuzingatia katiba na kanuni zake.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imetoa maelekezo hayo baada ya klabu ya Stand United kukata rufani kupinga uamuzi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuagiza mechi yao ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya Kanembwa JKT iliyovunjika kurudiwa Februari Mosi mwakani mjini Tabora.
Sekretarieti ya TFF iliwasilisha suala hilo kwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ili itoe mwongozo kwa vile uamuzi huo uliofanywa na TPLB hauwezi kukatiwa rufani kwa mujibu wa Kanuni za ligi husika.
Kamati imesisitiza kuwa hiyo ni falsafa ya mpira wa miguu ambapo uamuzi unaofanywa uwanjani haukatiwi rufani, hivyo uheshimiwe kama ilivyo kwa masuala ya mpira wa miguu kutopelekwa katika mahakama za kawaida za kisheria.
Wakati huo huo: Wanachama wa klabu ya Pan African wametakiwa kufuata ngazi husika pale wanapoona viongozi wa klabu yao wanakwenda kinyume na Katiba yao.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imetoa mwongozo huo kwa wanachama wa Pan African baada ya kumwandikia barua Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kulalamikia uongozi wao wakati wao si wanachama wa TFF.
Wanachama hao wanalalamikia uongozi wa klabu yao kwa kuitisha mkutano wa uchaguzi kabla ya ule wa kawaida ambao unatakiwa kufanyika mara moja kwa mwaka.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imelazimika kutoa mwongozo huo kwa vile wanachama hao katika malalamiko yao wamekigusa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) ambacho ni mwanachama wa TFF.
Pan African ni mwanachama wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ilala (IDFA) ambao ndiyo wanachama wa DRFA. Hivyo, TFF imemtaka mwanachama wake DRFA kupitia IDFA kufuatilia tatizo hilo na kulipatia ufumbuzi.

Mohammed Matumla akabidhiwa Bodaboda lake

BONDIA Mohamed Matumla akiwa amepanda pikipiki yake baada ya kukabidhiwa.
Promota wa mpambano wa masumbwi Kaike Siraju katikati akimwinua mkono juu bondia Mohamed Matumla baada ya kumkabidhi pikipiki yake kwa kumshinda Nasibu Ramadhani wakati wa sikukuu ya krismas na kuibuka na bodaboda hiyo.
Promota wa mpambano wa masumbwi Kaike Siraju katikati akimpongeza bondia Mohamed Matumla baada ya kumkabidhi pikipiki yake kwa kumshinda Nasibu Ramadhani wakati wa sikukuu ya krismas na kuibuka na bodaboda hiyo. Kushoto ni Baba wa bondia huyo Rashidi Matumla na wa pili kulia ni Meneja Mkuu wa G S Group Limited wasambazaji wa pikipiki ya Haojue ambao wametoa pikipiki hiyo,Bruce Shi
Meneja Mkuu wa G S Group Limited wasambazaji wa pikipiki ya Haojue ambao wametoa pikipiki hiyo, Bruce Shi akimpongeza bondia Mohamed Matumla baada ya kumkabidhi bodaboda hiyo.

Friday, December 27, 2013

Jackie Cliff AKAMATWA NA MADAWA YA KULEVYA CHINA...


.
Mwanamke wa Kitanzania mwenye umri wa miaka 28 ambae ni video Queen wa nyimbo ya Linex -KIMUGINA amekamatwa na kilo 1.1 za dawa za kulevya aina ya heroin huko Macao. Dawa hizo zilikutwa tumboni mwake baada ya kushtukiwa na kufanyiwa X-ray ambapo alikutwa na jumla ya vidonge 66 vyenye thamani ya dola za Kimarekani 137,720.
Mwanamke huyo alikuwa akisafiri kutoka Thailand akielekea Macao Jumanne iliyopita. Aliwaambia polisi kuwa

alikuwa anaelekea Guangzhou ambao ni mji wa jimbo la Guangdong huko China.



Pichani ni mwanamke huyo wa Kitanzania (akiwa amefunikwa uso) aliyekamatwa na kilo 1.1 za heroin huko Macau. Hapo amepigwa picha na vidonge vyake kwenye press conference huko Macau, Disemba 19, 2013.

Mwanamke wa Kitanzania mwenye umri wa miaka 28 amekamatwa na kilo 1.1 za dawa za kulevya aina ya heroin huko Macao. Dawa hizo zilikutwa tumboni mwake baada ya kushtukiwa na kufanyiwa X-ray ambapo alikutwa na jumla ya vidonge 66 vyenye thamani ya dola za Kimarekani 137,720.

Mwanamke huyo alikuwa akisafiri kutoka Thailand akielekea Macao Jumanne iliyopita. Aliwaambia polisi kuwa alikuwa anaelekea Guangzhou ambao ni mji wa jimbo la Guangdong huko China.


Polisi wakichunguza vidonge ambavyo huyu mrembo alikuwa amevimeza.


Ok kwa wale walokuwa wakilalamika 'habari nusu nusu' huyo binti anaitwa Jackie Cliff. ..appeared in Diamondz Nataka Kulewa. Was a runners up or something kwenye Miss Tz huko nyuma.






Waandishi wa habari wakipiga picha vidonge vya heroin alivyokamatwa navyo mremboi huyu wa Kitanzania

Chanzo cha habari: jamiiforum.
You might also like
- See more at: http://onelovetz.blogspot.com/2013/12/jackie-cliff-akamatwa-na-madawa-ya.html?utm_source=feedburner&utm_medium=feed&utm_campaign=Feed%3A+blogspot%2FhgdRs+%28Onelove+Tz%29#sthash.zSUH9Hcq.dpuf