STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, May 3, 2013

Mfanyabiashara Kariakoo ajirusha toka ghorofa ya 9, kisa...

Mfanyabiashara huyo akiwa hoi kando ya gari alilolidondokea ambalo liliharibika vibaya kama inavyoonekana pichani
MCHANA wa leo mitaa ya Kariakoo, mtu mmoja aliyetambulika kwa jina moja tu la Shirima,  ambaye anadaiwa ni mfanyabiashara katika moja ya maduka yaliyopo eneo hilo la  Kariakoo, Dar es Salaam, amejirusha toka ghorofa ya 9 ya Hoteli ya Concord.
habari ambazo zimepatikana na kusimuliwa na mashuhuda wa tukio hilo lililosikitisha wengi, linasema kuwa mfanyabiashara huyo alijirusha toka kwenye jengo hilo na kuangukia gari kabla ya kukimbizwa hospitali kwa uangalizi zaidi maana haijafahamika kama kapoteza Maisha au bado yu hai.

Mfanyabiashara huyo alijirusha toka ghorofani na kuangukia Gari aina ya Toyota Corolla ambayo ni taxi iliyokuwa imepaki nje ya hoteli hiyo....chanzo cha kujirusha kwa mfanyabiashara huyo bado hakijafahamika mpaka sasa.

Mashuhuda wa tukio hilo lililotokea muda si mrefu wanaeleza kuwa walipatwa na mshuko baada ya kusikika kishindo cha kitu kilichokuwa kimeangukia gari hilo na waliposogea kushuhudia ndipo walipobaini kuwa alikuwa ni mtu huyo alietambulika kwa jina moja la Shirima.

Azam yaendelea kuanika sababu za kuing'oa AS FAR Rabat kesho nchini Morocco

Mshambuliaji John Bocco 'Adebayor' akichuana na wachezaji wenzake mazoezini mjini Rabat, Morocco kujiandaa na pambano lao la kesho dhidi ya AS  FAR Rabat

Na Patrick Kahamela, Rabat
SIKU chache zilizopita tulijadili juu ya sababu mbili kati ya sita, kwa nini Azam FC ina nafasi kubwa ya kuibwaga AS FAR, katika, katika makala ya jana tuliangalia jinsi Azam FC ilivyofanya maandalizi kabambe kwa kuijengea timu kujiamini kwa kuipa mechi za majaribio na maandalizi mengine. Baada ya hapo tulijadili jinsi Azam FC ilivyo na wachezaji kabambe wenye uwezo wa kupambana na timu yoyote kwenye mashindano ya Afrika. Tulifanikiwa kuwaangalia wachezaji wa eneo la ulinzi pekee, leo tutawaangaliwa wachezaji wa kiungo na ushambuliaji na sababu nyingine nne zilizosalia zinazoifanya Azam FC iwe katika nafasi kubwa ya kuitoa AS FAR.

Azam FC wakati wa dirisha dogo ilimsajili mchezaji wa kiungo toka SOFAPAKA Ochieng Humphrey Mieno, tangia kuwasili mieno amekuwa habanduki kwenye kikosi cha kwanza na kazi yake nzuri imeiwezesha Azam FC kufikia mafanikio iliyonayo hadi sasa. Mieno ni mrefu kwa kimo, ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, mzuri kwenye kusoma mbinu za adui na kupanga mipango ya kuizima na ana uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo wa ushambuliaji na ulinzi. Hakika usajili wa Mieno umekuwa wa maana kubwa kwa Azam FC.

Tanzania kwa sasa inajivunia kuwa na wachezaji wenye kiwango cha juu cha uchezaji na ndiyo maana timu ya taifa imekuwa ikifanya vizuri. lakini ukiwaomba mashabiki wakutajie wachezaji watatu bora zaidi nchini basi bila shaka watakuambia ni Mbwana Samata wa TP Mazembe, Shomary Kapombe wa Simba na Salum Abubakar Sure Boy wa Azam FC. Sure boy amekuwa mchezaji wa kipekee kabisa kwa sasa… uwezo wake wa kupokonya mipira, kumiliki mipira na kuipa timu umiliki wa mpira ni wa hali ya juu sana. Sure Boy anazurura sana uwanjani na hachoki kirahisi. Azam FC inajivunia kumtengeneza mchezaji huyu ambaye alitua Azam FC akiwa na miaka 16 tuu na kwa sasa amekuwa lulu inayong’aa.

Utawaambia nini mashabiki juu ya Sure? Utawaambia nini wachezaji wenzake? Muulize kocha wake juu ya Sure, wote watakuambia ni mchezaji wa dunia yake na wa kipekee. Hakika silaha kubwa ya Azam FC kesho ni Salum Abubakar.

Azam FC imejaaliwa kuwa na wachezaji wengi wa kiungo lakini Jabir Aziz Stima ana sifa ya kipekee inayomfanya kuwa mchezaji muhimu kikosini. Stima ambaye alikuwa hakosekani kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Marcio Maximo ni mchezaji pili wa Afrika baada ya Dedier Drogba kuweza kuifunga Brazil goli, je ulikuwa unalijua hilo? Stima alifuga wakati Stars ilipocheza na Brazil na kufungwa 4-1 kwenye mchezo wa kirafiki mwaka 2010. Stima ni bingwa wa kukaba. Kocha wake Stewart Hall anamuita mbwa wa polisi, muingize Stima uwanjani kisha mwambie akakabe kisha uone kama wapinzani wataweza kupiga zaidi ya pasi tano. Katika mchezo wa kesho ambao ni wa ugenini… Stima anatarajia kuwa na sehemu muhimu.

Sifa za kukaba za Stima pia anazo muaiverikosti Kipre Michael Bolou na hii inaifanya Azam FC iwe na uwigo mpana wa kupanga kikosi. Kocha akitaka wakabaji basi atawapanga Jabir Aziz na Kipre Bolou, lakini akitaka kucheza mpira basi atawatumia Abdi Kassim, Humphrey Mieno, Sure Boy na Mwaipopo. Wachezaji wote hawa wamesafiri na wapo katika hali nzuri. Ni suala la kusubiri tuu kuona nini kitatokea hiyo kesho.


Kipre Bolou alisajiliwa wakati wa dirisha dogo la msimu uliopita baada ya pacha wake kipre tchetche kuonesha mafanikio makubwa. Tangia awasili kipre Bolou amekuwa mhimili mkuu wa eneo la ulinzi. Amecheza karibu mechi zote na ilipobidi alifunga magoli mazuri sana. Azam FC inajivunia kuwa na mchezaji wa kimataifa wa aina ya Kipre Bolou.


Baadhi ya wachezaji wa Azam wakipasha nchini Morocco
Baadhi ya msafara wa Azam ukiwasilia Rabat, mbele ni Patrick Kahemela na kocha Stewart Hall
Ibrahim Joel Mwaipopo ni mmoja kati ya wachezaji waliosajiliwa na Azam FC mara baada ya kupanda ligi kuu misimu minne iliyopita. Mwaipopo mchezaji anayetumia zaidi mguu wa kushoto amekuwa akicheza kwenye eneo la kiungo cha ulizi na kazi yake imekuwa ya uhakika kiasi cha kumfanya kuwa na mkataba wa muda mrefu na Azam FC. Mwaipopo ana jicho la kuona nafasi, ana pasi za uhakika fupi na ndefu lakini pia anajua kupiga mashuti yenye macho. Ukiomuona mazoezini utaamini kuwa anakwenda kuanza kesho lakini ukimkuta anaanzia bechi huta shangaa kutokana na aina ya wachezaji ambao Azam FC inao kwa sasa.

Abdi Kassim Babi ni mchezaji mzoefu zaidi kwenye kikosi cha Azam FC na siku hizi amekuwa na uwezo wa kucheza kama mshambuliaji wa kati au kurudi kwenye eneo lake la kiungo na kucheza kama namba kumi. Babi ana uzoefu wa mashindano ya ngazi hii na uzoefu wake unatarajia kuisaidia sana Azam FC hapo kesho. Ukitafuta wachezaji wa kiungo wa Tanzania watano wenye uwezo mkubwa wa kufunga na kupiga mipira ya adhabu basi hutaacha kumtaja Abdi kassim.

UONGOZI BORA WENYE BENCHI BORA LA UFUNDI NA MIPANGO NA DHAMIRA YA USHINDI


Azam FC ina uongozi bora na makini chini ya bodi ya wakurugenzi inayoongozwa na management ya Bakhresa Group, uongozi wa Azam FC chini ya mwenyekiti Said Muhammad ulichukua kila tahadhari kwa ajili ya mchezo huu ikiwemo kutanguliza timu ya watu saba kufanya ushushushu wa mazingira yalivyo na maandaliza kabla timu haijawasili. Mashushushu hao waliuarifu uongozi umuhimu wa kuwahi na Azam FC iliandika barua TFF kuomba mechi yale na Coastal Union irudishwe nyuma ili kuweza kuwahi Rabat. Azam FC iliwasili Rabat siku sita kabla ya mchezo kuweza kufanya mazoezi kwa zaidi ya mara nane ili kuzoea hali ya hewa ya baridi kali iliyopo hapa.
 
Pia klabu ilinunua nguo za michezo za kuvaa kwenye baridi kwa ajili ya wachezaji, soksi nzito za miguuni na mikononi, fulana za kukaba za kuvaa ndani pamoja pamoja na raba za kushindia ili kuondoa sababu za hali ya hewa kuweza kuathiri maandalizi ya timu na uwezo wa timu uwanjani.


Azam FC inakaa kwenye hotel ya nyota tano ya Golden Tulip Farah hapa Rabat hii inawafanya wachezaji wasiwe na manung’uniko na wasiathirike kiasaikolojia kutokana na matatizo ya huduma. Viongozi wamekuwa wakihakikisha timu inapata kila inachohitaji na hadi sasa hakuna tatizo lolote lililojitokeza.


BENCHI LA UFUNDI
Azam FC ipo chini ya kocha Stewat Hall, huyu ni mwalimu wa kiwango cha juu sana akiwa anamiliki cheti cha ukocha cha UEFA PRO LICENCE inayomfanya kuwa mkufunzi wa makocha kule uingereza.



Makocha wa Azam, Waingereza John Stewart Hall na Kally Ongalla
  
Stewart Hall kwa kushirikiana na wasaidizi wake wamepata nafasi si tuu ya kuangalia mikanda ya video ya AS FAR waliyotafutiwa, lakini pia wamepata nafasi ya kuwaangalia AS FAR ‘live’ wakiwa uwanjani na hii inawapa uelewa zaidi na kubuni mbinu za kuwakabili.


Azam FC imekamilika na imekuja na timu kamili akiwemo kocha mkuu Stewart Hall, wasaidizi wake Kalimangonga Ongala na Iddi Abubakar, Mtunza vifaa Joseph Nzawila, Meneja Jemedary Said na Daktari Juma Mwanandi Mwankemwa. Hakika timu imejipanga na ina hamu ya kushinda na kuiweka Tanzania kwenye ramani ya soka.

Golden Bush Veterani wapeleka 'maafa' Staki Shari Ukonga


 
Wazee wa Kazi, Golden Bush Veterani
 
Wazee wa Staki Shari Veterani walioumizwa na Golden Bush juzi
WAKALI wa Soka la wazee jijini Dar es Salaam, Golden Bush majuzi waliendeleza libeneke lao baada ya kuwanyuka Staki Shari Veterani kwa mabao 4-0 katika pambano maalum la kusherehekea sikukuu ya Wafanyakazi 'May Day'.
Kwa mujibu wa msemaji na mlezi wa klabu ya Golden walipata ushindi huo katika pambano hilo lililochezwa Ukonga na kuwashtukiza wenyeji wao kwa mabao mawili ya haraka kabla ya Staki Shari kukomaa.
Hata hivyo pamoja na kutuliza akili na kushambulia lango la wageni wao, haikuwasaidia kuwazuia wazee wa Golden Bush waliokuwa wakiongozwa na nyota wa zamani wa timu za Simba na Yanga pamoja na msemaji huyo, Onesmo Waziri 'Ticotico' kwa kuruhusu mabao mengine mawili.
Ticotico alisema kwa namna walivyokuzishughulikia timu zao pinzani ndani ya wiki mbili wameamua safari hii kupumzika kabla ya kuangalia waelekeze mashambulizi yao mitaa ipi ya jijini au nje ya Dar es Salaam.

Kiporo cha Simba, Ruvu Shooting kupigwa J'pili Taifa


Na Boniface Wambura
LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea Jumapili (Mei 5 mwaka huu) kwa mechi moja tu ya kiporo kati ya  Ruvu Shooting dhidi ya Simba itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.15 jioni.

Hiyo itakuwa mechi ya raundi ya 24 kwa timu hizo ambapo Simba iko nafasi ya nne ikiwa na pointi 39 nyuma ya mabingwa Yanga wenye pointi 57, Azam yenye pointi 48 na Kagera Sugar ambayo ina pointi 40. Ruvu Shooting iko katika nafasi ya saba ikiwa na pointi 31.

Pambano hilo awali lilikuwa lichezwe Aprili 25, lakini likaahirishwa dakika za lala salama kutokana na uwanja huo wa Taifa kutumiwa na serikali kwa maandalizi ya sherehe za Muungano zilizofanyika siku iliyofuata kwenye uwanja wa Uhuru unaoendelea kutengenezwa.

Hadi sasa mabao 348 yameshafungwa katika ligi hiyo huku Yanga ikiongoza kwa kufunga 45. Polisi Morogoro yenye pointi 22 katika nafasi ya 12 ndiyo iliyofunga mabao machache ikiwa nayo 13 tu.

African Lyon yenye pointi 19 katika nafasi ya mwisho ndiyo inayoongoza kwa kuwa na kadi nyingi. Timu hiyo inayofundishwa na Charles Otieno ina kadi 44 ambapo kati ya hizo nne ni nyekundu. Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro yenyewe inaongoza kwa kuwa na kadi nyingi nyekundu ambapo hadi sasa inazo saba.

TFF kukutana kujadili utekelezaji wa maagizo ya FIFA

Rais wa TFF, Leodger Tenga



Na Boniface Wambura
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inakutana Mei 9 mwaka huu jijini Dar es Salaam kupokea na kupanga utekelezaji wa maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kuhusu uchaguzi wa shirikisho.

Kikao hicho cha dharura chini ya Uenyekiti wa Rais wa TFF, Leodegar Tenga kitakuwa na ajenda hiyo moja tu katika kuhakikisha utekelezaji wa maelekezo ya FIFA unafanyika haraka ili uchaguzi ufanyike ndani ya muda uliopangwa.

FIFA katika maelekezo yake imetaka kwanza ziundwe Kamati ya Maadili na Kamati ya Rufani ya Maadili kabla ya kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi wa Kamati mpya ya Utendaji ya TFF. FIFA imeagiza uchaguzi uwe umefanyika kabla ya Oktoba 30 mwaka huu.

TFF yaitakia kila la heri Azam Morocco

Watanzania wanatarajia furaha kama hii kwa Azam iwepo pia katika pambano lao la kesho nchini Morocco

Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaitakia kila la kheri timu ya Azam katika mechi yake ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika itakayochezwa Morocco kesho (Mei 4 mwaka huu).

Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya pili ya michuano hiyo itachezwa jijini Rabat kuanzia saa 11 jioni kwa saa za Morocco. Timu hizo zilitoka suluhu katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.

Azam iko nchini Morocco kwa karibu wiki nzima sasa ikijiandaa kwa mechi hiyo chini ya Kocha wake Stewart John Hall. Msafara wa Azam nchini humo unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Eliud Mvella.

25 waripoti kambi ya Young Taifa Stars

Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen
Na Boniface Wambura
Wachezaji 25 kati ya 30 walioitwa na Kocha Kim Poulsen kwenye kikosi cha pili cha Taifa Stars (Young Taifa Stars) wameripoti kambini ambapo mazoezi yalianza tangu jana jioni (Mei 2 mwaka huu).

Kocha Kim amewaitaka wachezaji katika kambi hiyo ya siku tano ili kuangalia uwezo wao katika maeneo kadhaa kwa lengo la kupata baadhi ambao anaweza kuwajumuisha kwenye kikosi cha Taifa Stars siku za usoni.

Wachezaji watano walioshindwa kujiunga katika kambi ya timu hiyo iliyoko hoteli ya Sapphire jijini Dar es Salaam ni Aishi Manula, David Mwantika, Himid Mao, Samih Nuhu na Seif Abdallah ambao wako Morocco na timu yao ya Azam.

Kamati ya Mashindano TFF kupitia mchakato wa Ligi ya Mabingwa wa Mikoa


Na Boniface Wambura
Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inakutana Jumapili (Mei 5 mwaka huu) kupitia maandalizi ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) iliyopangwa kuanza Mei 12 mwaka huu.

Tayari mikoa 18 kati ya 27 kimpira imeshapata mabingwa wao kwa ajili ya RCL itakayotoa timu tatu zitakazopanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao (2013/2014).

Kamati hiyo chini ya Uenyekiti wa Blassy Kiondo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF itapokea taarifa ya maandalizi ya ligi hiyo kutoka Idara ya Mashindano ya TFF na kufanya uamuzi juu ya mikoa ambayo haijawasilisha mabingwa wao.

Ligi hiyo itachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini, na ratiba (draw) itapangwa wakati wowote. Ada ya kushiriki ligi hiyo kwa kila klabu ni sh. 100,000 na usajili utakaotumika na ule ule wa ligi ngazi ya mkoa. Hakutakuwa na usajili mpya wa wachezaji.

Yanga, Coastal wavuna Mil.66


Na Boniface Wambura
Mechi namba 172 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Coastal Union iliyochezwa juzi (Mei 1 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 imeingiza sh. 66,022,000.

Watazamaji 11,478 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 15,378,927.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 10,071,152.54.

Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 10,230 na kuingiza sh. 51,150,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 69 na kuingiza sh. 1,380,000.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,819,793.62, tiketi sh. 3,818,890, gharama za mechi sh. 4,691,876.17, Kamati ya Ligi sh. 4,691,876.17, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,345,938.09 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,824,618.51.

EXCLUSIVE: HATIMAYE NSA JOB APELEKA JINA LA KIGOGO TFF

MSHAMBULIAJI wa Coast Union, Nsa Job amewasilisha barua kwenye Shirikisho la soka (TFF) ambayo inamtaja kigogo ambaye alimpa rushwa.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilimtaka mchezaji huyo kujieleza kutokana na kukaririwa akiongeza katika kituo kimoja cha radio akikiri kupokea rushwa ya sh2mil kwa mmoja wa kiongozi wa timu kubwa ili acheze chini ya kiwango pindi walipokuwa wanacheza na timu hiyo.

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kuwa tayari mchezaji huyo amekwisha tuma barua ya kujieleza nao wameamua kulipeleka suala hilo katika kamati ya nidhamu ambayo inatarajiwa kukutana wiki ijayo.

Alisema mbali na suala hilo pia kamati hiyo itapitia mambo mbali mbali ya ligi kuu ambayo yametokea ikiwemo suala la viongozi ambao walikuwa wanatoa maneno ya uchochozi.

Alisema viongozi wanatakiwa kufuata taratibu na kanuni za soka sio kuongea ongea vitu visivyo na maana ambavyo vitaleta matatizo katika soka.

Moja ya Viongozi ambao watajadiliwa ni Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga baada ya kudaiwa kutoa maneno ya uchochezi pindi TFF, walipohairisha mechi yao dhidi ya Mgambo JKT ya Tanga.  


CHANZO:SHAFII DAUDA

LADY JAYDEE KUZINDUA ALBAMU MIAKA 13 ya KISANII


Binti Machozi a.k.a Comandoo, Lady JayDee
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Katika mwaka huu 2013, Inatimia miaka 13 tangu nianze kazi ya muziki.
Nashukuru MUNGU tuko pamoja na pia, nashukuru umma wa Tanzania kwa kuendelea ku support muziki wa Tanzania na kunipa nguvu mimi kama msanii.
Nashukuru vyombo vyote vya habari vinavyoshiriki kikamilifu kukuza na kulinda sanaa ya Tanzania bila kujali maslahi binafsi.
Tumeandaa sherehe kubwa na nzuri ya miaka 13 ya LADY JAYDEE, katika muziki.
Na mdhamini mkuu kwa upande wa media ni East Africa TV.
Sherehe ya miaka 13 ya Lady JayDee katika muziki itaambatana na uzinduzi wa album yangu ya sita inayokwenda kwa jina la NOTHING BUT THE TRUTH ambayo ina jumla ya nyimbo 10.
Katika sherehe hizo pia kutakuwa na show ya nyimbo zote bora za JayDee nikishirikiana na baadhi ya wasanii wenzangu hapa nchini.
Sherehe zitafanyika Ijumaa tarehe 31 May 2013.
Nawakaribisha wote tufurahi pamoja
Na Mungu awabariki

Chelsea, Benfica kucheza fainali ya UEFA League


Chelsea wakishangilia moja ya mabao yao jana dhidi ya Basel
Oscar Cordozo akishangilia moja ya mabao yake mawili aliyoifungua Benfica jana na kuipeleka fainali ya Europas League


CHELSEA ya England usiku wa kuamkia leo imefanikiwa kutinga fainali ya Europa League baada ya kuifunga Basle ya Uswisi mabao 3-1 katika pambano la marudiano la Nusu Fainali ya ligi hiyo lililochezwa uwanja wa Stamford Bridge.
Ushindi huo mnono umeifanya Chelsea kutinga hatua hiyo kwa jumla ya mabao 5-2 baada ya wiki iliyopita kuinyuka Basle nyumbani kwao mabao 2-1 na sasa itavaana na Benfica ya Ureno ambayo jana ikiwa nyumbani ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Waturuki, Fenerbache.
Chelsea walitanguliwa kufungwa bao na wageni wao dakika chache kabla ya mapumziko kupitia Salah kabla ya kurejesha mabao hayo mara baada ya kuanza kwa kipindi cha pili.
Fernando Torres aliisawazishia Chelsea bao dakika ya 50 kabla ya Victor Moses kuongeza la pili dakika mbili baadaye na David Luiz kupigilia msumari wa mwisho dakika saba baadaye kwa kufunga bao la tatu.
Nayo Benfica ikiwa nyumbani iliwatungua Fenerbache kwa mabao 3-1 na kushinda kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya wiki iliyopita kufungwa bao 1-0 ugenini.
Mabao ya wenyeji yaliwekwa kimiani na Gaitan dakika ya 9 kabla ya Dick Kuyt kusawazisha kwa njia ya penati dakika ya 23 na Cordozo kuongeza bao la pili kwa Benfica dakika ya 35 na kufanya hadi mapumziko matokeo kuwa 2-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Cordozo aliiandikia tena Benfica bao la tatu na kuihakikishia nafasi ya kucheza fainali za michuano hiyo itakayopigwa Mei 15 kwenye mji wa Amsterdam, Uholanzi.

Thursday, May 2, 2013

Mazoezi ya Miss Kibaha 2013 yapamba moto


Mkufunzi wa Warembo wa Redd's Miss Kibaha Rehema Uzuwiya akizungumza na warembo hawo wakati wa mazoezi yao yanayo endelea katika ukumbi wa Vijana Kinondoni picha na www.burudan.blogspot.com

Warembo wa Redd's miss kibaha wakiwa katika pozi wakati wa mazoezi yao

Warembo watakao wania taji la Redd's Miss Kibaha wakiwa katika pozi wakati wa mazoezi yao yanayoendelea katika ukumbi wa vijana Kinondoni Dar es salaam picha na www.burudan.blogspot.com

Kivumbi ya UEFA Ndogo ni leo, Chelsea kupenya kwa Basel

http://www.thenewstribe.com/wp-content/uploads/2013/04/Chelsea-vs-FC-Basel-1.jpg
Vita hii ya Basel na Chelsea inatarajiwa kujirtudia tena usiku wa leo kwenye UEFA League

IKIWA na faida ya ushindi wa mabao 2-1 iliyopata ugenini dhidi ya Basel ya Uswiss, Chalsea itawakaribisha wageni wao hao kwenye nusu fainali ya pili ya Ligi Ndogo ya Ulaya katika pambano litakalochezwa uwanja wa Stanford Bridge, jijini London.
Chelsea am,bayo inashuka dimbani ikiwa na furaha ya ushindi wa mabao 2-0 iliyopata dhidi ya Swansea City katika Ligi Kuu ya England itahitaji ushindi au sare yeyote kuweza kufuzu fainali za michuano hiyo zitakazofanyika Mei 15.
Kocha wa Chelsea, Rafa Benitez ameweka bayana wameweka akili zao kwa ajili ya pambano hilo wakiwa na tahadhari kubwa kutokana na wapinzani wao kutotabirika akikumbukia walivyowaondoa michuanoni Tottenham katika mechi ya robo fainali.
Benitez amenukuliwa akisema watashuka dimbani wakiwa na dhamira kuu ya kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi ya leo, lakini hawaipuuzii Waswisi hao ambao wametoka kupokea kichapo cha mabao 3-0 katika mechi ya ligi ya nyumbani kwao dhidi ya Luzern Jumapili iliyopita.
Naye kocha wa Basel Murat Yakin, amedai inahitgaji miujiza kidogo kuweza kuwaondosha Chelsea katika hatua hiyo ya nusu fainali na wao kutinga fainali.
Yakin alisema hata hivyo wachezaji wake wana ari kubwa na kujiamini kupita kiasi katika pambano hilo la leo dhidi ya kigogo kingine cha jiji la London baada ya awali kuiondosha Tottenham kwa mikwaju ya penati kufuatia kutoka sare ya mabao 4-4 katika mechi zote mbili.
Bila shaka ni suala la kusubiri kuona kama vijana wa darajani watatinga fainali ya pili mfululizo ya michuano ya Ulaya baada ya mwaka jana kucheza Ligi ya Mabingwa na kuiondosha patupu Bayern Munich waliotinga tena fainali hizo msimu huu baada ya jana kuing'oa kwa aibu Barcelona kwa mabao 7-0.
Pambano jingine la pili la nusu fainali ya marudiano usiku wa leo ni kati ya timu za Benfica na Fenerbache nchini Ureno.
Wenyeji hao walichezeas kichapo cha bao 1-0 ugenini nchini Uturuki wiki iliyopita, hivyo kuhitaji ushindi ili kuweka hai matumaini ya kucheza fainali hizo za UEFA Ndogo wiki mbili zijazo mjini Amsterdam, Uholanzi.

Redd's Miss Kigamboni 2013 kumekucha!

Somoe Ng'itu (wa pili toka kulia akiwa na wanahabari wenzake

FIFA yatengua uchaguzi wa TFF, kisa...!



Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limelitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuanza upya mchakato wa uchaguzi baada ya kubaini kasoro iliyotokana na ukosefu wa kutokuwepo vyombo vya kushughulikia ukiukwaji wa maadili.

FIFA ambayo ilituma ujumbe wake katikati ya mwezi uliopita kufanya utafiti kuhusu mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa TFF ambao ulisimamishwa baada ya baadhi ya wagombea kulalamika, imetaka uchaguzi ufanyike kabla ya tarehe 30 Oktoba 2013, lakini ukitanguliwa na mabadiliko ya katiba ambayo yatahusisha uundwaji wa vyombo vya kushughulikia ukiukwaji wa maadili.

Raiswa TFF, Leodegar Tenga aliwaambia waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa shirikisho hilo kuwa suala la Tanzania lilijadiliwa kwenye kikao cha Kamati ya Dharura ya FIFA kilichofanyika tarehe 28 Aprili 2013 na maamuzi yake kutumwa juzi kwa barua iliyosainiwa na KatibuMkuuwa FIFA, Jerome Valcke.

Baada ya kupokea barua hiyo, Rais wa TFF alifunga safari kwenda Dodoma jana kukutana na Mheshimiwa Waziri na Naibu wake pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT). 

“Matarajio yetu sote yalikuwa kupokea majina ya waliopitishwa ili tufanye uchaguzi. Kinyume chake tumepokea maagizo hayo. Hata hivyo tumeona kuwa hili ni jambo la kheri kwa vile siyo tu haki itatendeka bali pia itaonekana imetendeka.” alisema Tenga, ambaye alishatangaza kuwa hatagombea tena urais baada ya kuliongoza Shirikisho kwa vipindi viwili vya miaka minne kila kimoja.

“Lengo letu ni kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa na uchaguzi kufanyika mapema iwezekanvyo kabla ya tarehe iliyotolewa. Yale mambo nayoweza kufanyika kwa pamoja yatafanyika ili tuharakishe utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na FIFA.”
Uchaguzi wa TFF ulipangwa kufanyik tarehe 23 na 24 Februari 2013 na ulikuwa ukielekea ukingoni, lakini baadhi ya wagombea walienguliwa katika hatua ya mwisho na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF na ndipo walipo andika barua FIFA kuomba iingilie kati.

Rais Tenga alisema kuwa ujumbe wa FIFA ulikutana na pande zote zilizoathiriwa na mchakato wa uchaguzi na kwamba baada ya kukusanya taarifa hizo, maagizohayo ya FIFA sasa yatakuwa ni suluhisho la matatizo ya muda mrefu katika uendeshaji wa mpira wa miguu nchini.

Katika barua hiyo, FIFA imeiagizaTFF:
1.   Kuunda vyombo sahihi (Kamati ya Maadili itakayokuwa na vyombo viwili ambavyo ni cha kutoa maamuzi ya awali na cha rufaa) ambavyo mamlaka yake yatakuwa ni kushughulikia masuala ya ukiukwaji wa maadili;
2.   Kufanya mabadiliko ya katiba kwa kuzingatia uundwaji wa vyombo hivyo;
3.   Kuanza upya kwa mchakato wa uchaguzi wa Kamati ya Utendaji kwa kufungua milango kwa wagombea ambao walishachukua fomu na wagombea wapya:
4.   Shughuli hiyo ikamilike ifikapo tarehe 30 Oktoba 2013.
Katika kutekeleza hayo, TFF inatakiwa iitishe Mkutano Mkuu wa Dharura kwa ajili ya kufanya mabadiliko ya Katiba kwa ajili ya kuunda kamati hizo za maadili na Kanuni za Uchaguzi kabla ya kuendelea na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Kamati Mpya ya Utendaji.

Katika maoni yake FIFA imeeleza kuwa katika mchakato, Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliwaengua au kupitisha baadhi ya wagombea kwa kubaini kuwa walikiuka Ibara ya 9 (7) ya Kanuni za Uchaguzi na pia Ibaray a 29 (7) ya Katiba ya TFF ambavyo vinahusisha suala la kufungua kesi mahakamani, kufuja fedha za shirikisho na ukosefu wa uwajibikaji wa pamoja.

Hata hivyo, FIFA ilisema kuwa watu hao walitakiwa waadhibiwe kwanza na kamati husika (kamati za maadili) kabla ya kuenguliwa na kamati za uchaguzi za TFF.

“Kutokana na ukosefu wa kamati za maadili matokeo yake, mmoja wa wagombea amekuwa akienguliwa kwenye uchaguzi kila anapombea bila ya kujua adhabu yake ni ya muda gani,” inasema barua hiyo ya FIFA.

Rais Tenga ameagiza kuitishwa kwa kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji ya TFF kupokea maagizo ya FIFA na kupanga ratiba ya utekelezaji wake kwa lengo la kuhakikisha kuwa mchakato huu unatekelezwa mapema iwezekanavyo.


Shule 20 za Sekondari kuonyeshana ubabe Copa Coca Cola Ilala


JUMLA ya Shule 20 za Sekondari na Academia 10 za soka zinatarajiwa kuchuana katika mashindano ya Copa Coca Cola Wilaya ya Ilala yatakayoanza rasmi Mei 12 wilayani humo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Soka cha Ilala (IDFA) Daud Kanuti alisema timu hizo zitachuana kwenye viwanja vitatu tofauti vya Airwing-Ukonga, Shule ya Benjamini Mkapa, Ilala na Kinyerezi.
Alisema maandalizi ya michuano hiyo yanaendelea vyema ikiwamo kutolewa ratiba ya makundi ya timu hizo shiriki.
"Michuano yetu ya Coca Coca Cola Ilala inaanza rasmi Mei 12 mwaka huu kwa kushirikisha timu 20 za Shule za Sekondari na 10 za vituo vya kukuzia na kuendeleza soka, ambapo zitachuana katika viwanja vitatu tofauti,' alisema Kanuti.
Kanuti aliongeza wakati michuano hiyo ya Coca Coca ikianza Mei 12, Ligi Daraja la Tatu wilayani humo, itaanzaa kutimu vumbi lake Jumamosi Mei 4.
Alisema Ligi hiyo kuwaniwa bingwa wa Ilala na timu za kushiriki Ligi ya Kanda itashirikisha jumla ya timu 20 kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Katibu huyo alisema tayari timu zote zimeshapewa ratiba ya michuano hiyo itakayochezwa pia kwenye viwanja vitatu tofauti vilivyopo wilayani humo.

Kaseba kuzipiga na Mkenya mwezi ujao

Japhet Kaseba

BINGWA wa Taifa wa Ngumi za Kulipwa wa uzani wa Kati anayetambuliwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST), Japhet Kaseba anatarajiwa kupanda ulingoni mwezi ujao kupigana na bondia kutoka Kenya, Joseph Odhiambo Magudha katika pambano la kimataifa.
Pambano hilo litakalosindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi litaratibiwa na kampuni ya Bigright Promotion chini ya Ibrahim Kamwe.
Akizungumza na MICHARAZO Kamwe alisema pambano hilo litakalokuwa la raundi 10 litafanyika mwezi ujao jijini Dar es Salaam katika ukumbi na tarehe itakayotangazwa baadaye.
"Kampuni yetu imeandaa pambano la kimataifa litakalomkutanisha Japhet Kaseba dhidi ya Mkenya Joseph Magudha litakalofanyika mwezi Juni na kusindikizwa na michezo nkadhaa ya utangulizi," alisema Kamwe.
Kamwe alisema pambano hilo ni fursa nzuri ya Kaseba kurejea kwenye ngumi za kimataifa baada ya kutamba nyumbani aklitokea kwenye mchezo wa Kick Boxing alipokuwa bingwa wa Afrika na Dunia.
Mratibu huyo alisema maandalizi ya pambano hilo na mengine ya utangulizi yameanza ikiwamo kuwasainisha mikataba mabondia hao kwa ajili ya michezo hiyo ya mwezi Juni.
Alisema mabondia watakaosindikiza pambano hilo la Kaseba na Mkenya ni pamoja na Kamanda wa makamanda atakayezipiga na Ibrahim Maokola, Juma Seleman dhidi ya Issa Omar, Juma Fundi dhidi ya Moro Best na Yohana Matyhayo atakaychpana na Mkenya Joseph Onyango.
Mara ya mwisho kwa Kaseba kupanda ulingoni ni Machi mwaka huu alipopigana na Maneno Osward katika pambano la marudiano la ubingwa wa taifa, ambapo kama ilivyokuwa pigano lao la mwaka jana, Kaseba aliibuka mshindi kwa pointi.

Ni fainali ya Wajerumani, Barca wapigwa tena nyumbani na Bayern

Arjen Robben akionyesha manjonjo ya ushindi

Aah hii aibu bana! Kipa wa Barcelona na beki wake wakiwa hoi

Wachezaji wa Bayern Munich wakipongeza baada ya kuisasambua Barcelona nyumbani kwao jana


Kocha wa zamani wa Barcelona, Pep Gardiolla aliyetua Bayern Munich akishangilia ushindi wa timu yake mpya na Franky Ribbery


BARCELONA, Hispania
BAYERN Munich walitinga katika fainali ya kwanza ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya itakayokutanisha Wajerumani watupu wakati walipoisambaratisha Barcelona 3-0 kwenye Uwanja wa Nou Camp jana na kusonga mbele kwa jumla ya magoli 7-0.
Mabingwa hao wapya wa Ligi Kuu ya Ujerumani waliimaliza mechi mapema wiki iliyopita kwa ushindi wa 4-0 nchini Ujerumani na hapakuwa na namna ya kufufuka kwa Wahispania hao wakati Arjen Robben alipofunga goli la kuongoza dhidi ya kipa Victor Valdes katika dakika ya 49.
Kudhalilika kwa Barca kulikamilishwa mwishoni mwa mechi wakati Gerard Pique alipojifunga mwenyewe na Thomas Mueller, ambaye alifunga magoli mawili katika mechi yao ya kwanza, akapachika la tatu kwa kichwa.
Barca, kama Bayern ambao wanafukuzia taji la tano la Ulaya, wanategemea kipaji cha Lionel Messi, ambaye anarejea kutoka katika majeraha ya misuli ya nyuma ya paja na ambaye aliachwa benchi, lakini bila ya Mwanasoka Bora wa Dunia huyo hawakuwa na makali yoyote.
Bayern watacheza dhidi ya Borussia Dortmund katika mechi ya fainali kwenye Uwanja wa Wembley mjini London Mei 25 baada ya Dortmund kuitoa Real Madrid kwa jumla ya mabao 4-3 juzi Jumanne.

Cheka ni nouma amzima Mashali na kutibua rekodi yake ya kutopigika


Bondia Fransic Cheka Kushoto akipambani na Thomas Mshali wakati wa mpambano wao uliofanyika katika sikukuu ya mei mosi katika ukumbi wa PTA Sabasaba Dar es salaam Cheka alishinda kwa KNOCKOUT raundi ya kumi Picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com
Bondia Fransic Cheka Kushoto akimshambilia kwa makonde ya nguvu Thomas Mshali wakati wa mpambano wao uliofanyika katika sikukuu ya mei mosi katika ukumbi wa PTA Sabasaba Dar es salaam Cheka alishinda kwa KNOCKOUT raundi ya kumi Picha nawww.superdboxingcoach.blogspot.com
Bondia Shabani Mhamila 'Star Boy' kushoto akioneshana umwamba wa kutupiana masumbwi na Yusuph Jibaba wakati wa mpambano wao uliofanyika mei mosi katika ukumbi wa PTA Saba saba Dar es salaam Star Boy alishinda kwa KNOCKOUT raundi ya nne Picha nawww.superdboxingcoach.blogspot.com
Bondia Shabani Mhamila 'Star Boy' kushoto akioneshana umwamba wa kutupiana masumbwi na Yusuph Jibaba wakati wa mpambano wao uliofanyika mei mosi katika ukumbi wa PTA Saba saba Dar es salaam Star Boy alishinda kwa KNOCKOUT raundi ya nne Picha nawww.superdboxingcoach.blogspot.com
Bondia Shabani Mhamila 'Star Boy' kushoto akioneshana umwamba wa kutupiana masumbwi na Yusuph Jibaba wakati wa mpambano wao uliofanyika mei mosi katika ukumbi wa PTA Saba saba Dar es salaam Star Boy alishinda kwa KNOCKOUTraundi ya nne Picha nawww.superdboxingcoach.blogspot.com
Bondia Shabani Mhamila 'Star Boy' akishangilia ushindi uku akiwa amebebwa juu juu kama mkungu wa ndizi Picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com
Bondia Cosmas Cheka kushoto akipambana na Charles Mashali wakati wa mpambano wao uliofanyika katika ukumbi wa PTA Sabasaba siku ya mei mosi Cheka alishinda kwa ponti mpambano huo Picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com
Kocha wa Kimataifa wa Mchezo wa Masumbwi Rajabu Mhamila 'Super D' akimsindikiza wakati wa kupigana bondia Ibrahimu Class 'King class Mawe wakati wa mpambano wake na amos mwamakula
Bondia Amos Mwamakula kushoto na Ibrahimu Class 'King Class mawe' wakisubili matokeo ambapo class alishinda kwa point Picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com
Bondia Thomas Mashali kushoto akioneshana umwamba wa kutupiana makonde na Fransic Cheka katika ukumbi wa PTA Sabasaba Dar es salaam Cheka alishinda kwa KNOCKOUT



Shomari kimbau akiwa na Cheka baada ya kumvisha ubingwa wa IBF Africa aliokuwa akiutetea
Kotoka kushoto ni Kocha wa mchezo wa ngumi Kimataifa Rajabu Mhamila 'Super D' mdau ambaye ajajulikana jina Mtaalishaji wa mpambano kati ya Fransic Cheka Vs Thomasi Mashali Adamu Tanaka 'Tunaluza' na MC wa mpambano huo COOL p
Rashidi Mhamila 'Ngade akiwa amepozi na Bad Boy wakati wa onesho hilo



BONDIA machachari wa ngumi za kulipwa, Francis Cheka usiku wa kuamkia leo ameendeleza rekodi yake ya kuwapiga mabondia wenzake nchini baada ya kumtwanga kwa KO ya raundi ya 10 Thomas Mashali na kunyakua zawadi ya gari na kutetea taji lake la IBF-Afrika.
Cheka kwa kumpiga Mashali amefanikiwa kumvunjia rekodi mpinzani wake ya kutopigika nchini tangu ajitose kwenye ngumi hizo za kulipwa, ambapo kipigo cha jana kilikuwa cha kwanza kwake.
Mashali alikuwa na rekoidi ya kucheza mapambano 9 na kushinda nane na kutoka droo moja, lakini ukali wa ngumi za Cheka zilimfanya asalimu amri katika raundi hiyo ya 10 akiwa amebakisha mbili tu kumaliza mchezo huo uliokuwa wa raundi 12 la uzani wa Super Middle.
Ushindi huo wa Cheka umemfanya kuendeleza rekodi yake ya kuwapiga mabondia karibu wote nchini na kutowahi kupigwa katika ardhi ya Tanzania tangu mwaka 2008 akiwa amewachakaza karibu nyota wote nchini na Afrika Mashariki na Kati.
Cheka kwa kutetea taji lake sasa atapaswa kujiandaa kupambana tena na Mmalawi Chiotcha Chimwemwe aliyemtwanga kwa pointi walipoikutana katika pambano lililofanyika mjini Arusha ambapo alikuwa pia akitetea taji hilo alililotwaa kwa kumtwanga Mada Maugo, Aprili mwaka jana.

Wednesday, May 1, 2013

AZAM INA KILA SABABU ZA KUSHINDA MOROCCO

Khamis Mcha 'Vialli' nyota wa Azam katika pambano lao dhidi ya As Far Rabat jijini Dar na kuisha kwa 0-0

Kikosi Tegemeo cha Azam

Azam wakijifua mjini Rabat

Wachezaji wa Azam, walipokuwa wakijiandaa na pambano lao dhidi ya BYCII

Na Patrick Kahemela, Rabat
KIKOSI cha timu ya Azam Fc ipo mjini Rabat ikijiandaa kukabiliana na AS FAR kwenye mechi ya raundi ya mwisho ya 16 bora za kombe la shirikisho. Azam FC imetua hapa na wachezaji 23, benchi lote la ufundi isipokuwa Ibrahim shikanda pekee aliye masomoni Nairobi na uongozi karibu wote na kwa pamoja kama timu Azam FC ina dhamira ya kuifunga na kuisukuma nje ya mashindano timu ya AS FAR.
Kuna sababu sita zinazoifanya Azam FC iamini na ijiamini kuwa inaweza kushinda kwenye mtanange wa jumamosi hii. Sababu hizo ni maandalizi bora, wachezaji wazuri, Uongozi Mzuri, benchi bora la ufundi chini ya Stewart Hall, Mipango mizuri na dhamira ya kupata mafanikio. Makala hii itakayowajia katika sehemu tatu itachambua vipengele vilivyoaninishwa hapa chini.
MAANDALIZI MAZURI
Timu za Tanzania kwa miaka mingi zimekuwa zikishiriki mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na CAF, kwa Azam FC hii ni mara yake ya kwanza kupata nafasi hii. Lakini unaweza kuona utofauti mkubwa wa maandalizi kati ya Azam FC na timu nyingi za Tanzania na utofauti huo ndiyo unaoifanya Azam FC hadi sasa kuweza kucheza mechi tano pasi na kupoteza mchezo hata mmoja.
Azam FC baada ya kujua kuwa itawakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa iliamua kufanya juhudi za makusudi za kujiandaa kwa kiwango cha mashindano hayo yanayoandaliwa na CAF.
Azam FC ilifanya ziara na kucheza mechi nane za kimataifa za kirafiki nje ya ardhi ya Tanzania, ilikwenda Kinshasa Congo DRC na kushiriki Congo Charity Cup ambako ilitwaa kikombe kabla ya kusafiri tena hadi Nairobi ambako ilipata nafasi ya kucheza mechi nyingine tatu.
Lengo la ziara hizi ilikuwa ni kuwapa ukomavu na uzoefu vijana wake ili wanapokuwa kwenye mashindano ya CAF hasa wanapocheza mechi za ugenini wasiwe na hofu. Hakika matunda ya ziara hizi tunayaona kwani Azam FC imeshinda ugenini mechi zake zote mbili za awali hadi sasa.
Maadalizi ya Azam FC kwenye mashindano haya pia yalihusisha utafutwaji na usajili wa wachezaji wenye viwango vya kuweza kucheza na kuisaidia timu, uboreshwaji wa kambi ya mazoezi ya Chamazi mapema kwa ajili ya kambi ya nyumbani, ununuzi wa vifaa bora vya mazoezi na kadhalika.
UWEZO WA WACHEZAJI
Timu ni wachezaji, bila ya wachezaji bora wenye nidhamu, viwango bora na malengo ni sawa na bure. Azam FC ililitambua hilo mapema… Azam FC haikukurupuka kusaka wachezaji kwa mkupuo, usajili wa wachezaji kwa ajili ya mashindano ya CAF ulifanyika kwa umakini kwa muda mrefu huku klabu ikijiwekea malengo ya kuwa na kikosi bora kitakochoweza kupambana na kuvifunga vigogo vya soka la Afrika.
Leo ukiwaangalia wachezaji 25 wa Azam FC waliosajiliwa kwenye mashindano ya CAF utaungana nami kuwa ni wachezaji sahihi kwa mashindano haya.
Wachezaji wa Azam FC wana nidhamu na vipaji vya hali ya juu. Wote wana viwango vya kuweza kuwemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania na kuanza kwenye kikosi cha kwanza. Hapa nitazungumzia sifa za wachezaji wa eneo la ulinzi tuu kwa ufupi… halafu muendelezo wa makala hii utawaletea wachezaji wa kiungo na baadaye washambuliaji.
MWADINI ALLY; Golikipa chaguo la kwanza la kikosi cha timu ya Taifa ya Zanzibar na sehemu ya kudumu ya kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania. Ana uzoefu mkubwa wa michezo ya kimataifa akiiongoza Zanzibar kushika nafasi ya tatu mara mbili kwenye mashindano ya CECAFA. Ni golikipa hodari ambaye Azam FC tunajivunia kuwa naye
AISHI MANULA, utasemaje juu ya kipaji cha kijana huyu toka Morogoro? Wengi wanamfananisha na golikipa wa zamani wa Tanzania na Simba Mohammed Mwameja. Aishi anajiamini, ana umbo zuri na kipaji kikubwa sana. Ndiyo maana haishangazi kwa nini yeye ni golikipa namba moja wa timu za vijana za taifa na chaguo namba tatu la Taifa Stars ya kocha Kim Poulsen
HIMID MAO; Ana miaka 20 tuu lakini ni mkongwe ndani ya kikosi cha Azam FC, Himid ni kiungo mwenye sifa za kukaba ambaye sasa anacheza kama beki wa kulia wa Azam FC. Hakuna aliyeshangaa jina lake lilipoitwa na Kim Poulsen kuwa sehemu ya wachezaji 30 bora nchini wanaonyemelea nafasi za walio timu ya Taifa. Himid Mao aliibukia kwenye mashindano ya Copa Cocacola na baadaye kuwa nahonda wa timu za taifa za Tanzania chini ya miaka 20. Kabla ya mwalimu wa wakati huo wa Azam FC Itamar Amorim kumpa nafasi kwenye kikosi cha kwanza akitokea Azam Academy. Himid anafanya vizuri sana kwenye kikosi cha Azam FC hadi sasa.
WAZIRI SALUM; huenda ndiye mchezaji mwenye kipaji kikubwa cha kumiliki mpira kuliko wachezaji wote nchini Tanzania kwa sasa. Waziri Salum, naye yumo kwenye daftari la kocha Kim Poulsen na ni mwanachama wa kudumu wa kikosi cha Zanzibar heroes. Mguu wake wa kushoto ni kama mkono wa paka kwani anaweza kufanya lolote na mpita kwa kutumia mguu huu. Ana mbinu za kukaba, ana krosi za hatari na chenga za maudhi. Ni hadhina kubwa kwa Azam FC na taifa la Tanzania
JOCKINS ATUDO; beki bora wa ligi kuu ya Kenya KPL msimu uliopita Jockins Atudo alitua Azam FC wakati wa dirisha dogo la Disemba mwaka jana ili kuimarisha ukuta wa Azam FC kwa ajili ya mashindano haya. Tangia atue Azam FC Atudo amethibitisha kuwa waliomchagua kuwa beki bora hawakukosea. Kocha wa zamani wa Harambee Stars James Nandwa alisema wakati tunataka maoni yake juu ya atudo kabla ya kumsajili kuwa ukiwa na beki kama Atudo unapata vitu viwili, kwanza uongozi ndani ya uwanja pili beki mwenye kipaji, nguvu, kimo na kujitolea… hakika kila kocha angependa kuwa na Atudo kwenye kikosi chake
LUCKSON KAKOLAKI; labda ndiye mchezaji mwenye busara zaidi kwenye kikosi cha Azam FC kiasi kwamba wachezaji wenzake wanamuheshimu na kumkubali kama kaka. Busara hizi za nje ya uwanja pia unaweza kuziona ndani ya uwanja mbapo Luckson amekuwa mhimili mkuu kwa Azam FC hasa pale eneo la ulinzi linapokabiliwa na majeruhi. Kiwango chake cha uchezaji kimekuwa cha uhakika wakati wote na hili alilithibitisha kwenye mechi ya awali dhidi ya AS FAR ambapo aliingia katika dakika ya sita baada ya Atudo kuumia na kucheza kwa ustadi mkubwa sana Luckson ni mchezaji mmoja wapo ambaye tunaweza kusema ana damu ya bluu (yaani ana damu yenye rangi ya Azam FC)
DAVID MWANTIKA; Tanzania tumejaaliwa kuwa na mabeki wazuri lakini hatujawahi kuwana beki wa kiwango cha David Mwantika tangia kuondoka kwenye ramani ya soka kwa Boniface Pawasa. Mwantika hapitiki kwa namna yoyote ile… Mwantika ana nguvu za asili na mwili uliojengeka. Wenyewe wanyakyusa wanamuita Bedui… Mwantika ana spidi ya upepo na amekuwa maarufu ndani ya wachezaji wa Tanzania lakini alikuwa na umaarufu mdogo nje kutokana na timu yake ya Prisons kutopewa nafasi sana na vyombo vya habari. Lakini ukikutana na washambuliaji wa ligi kuu watakuambia kuwa beki wanayemuogopa zaidi nchini ni David. Juzi kim Poulsen amemjumuisha kwenye kikosi chake na bila shaka wala wasiwasi Mwantika atavuka kwenye kikosi cha Young taifa Stars na kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Taifa Stars muda si mrefu
Katika makala zijazo, tutawaletea maelezo ya wachezaji waliosalia wa kiungo na ushambuliaji pamoja na sababu nyingine nne zilizosalia za kwa nini Azam FC itaifunga AS FAR ambazo ni UONGOZI BORA, BENCHI BORA LA UFUNDI, MIPANGO MIZURI, na DHAMIRA