STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, March 19, 2014

Breaking News: Goli la Kavumbagu laua shabiki Taifa

KAVUMBAGU (KULIA) AKISHANGILIA NA WENZAKE BAADA YA KUIFUNGIA YANGA BAO DHIDI YA AZAM FC KWENYE UWANJA WA TAIFA, DAR, LEO.
Shabiki anayeaminika ni wa Azam FC, ameanguka na baadaye kupoteza maisha, dakika chache baada ya mshambuliaji wa Yanga,  Didier Kavumbagu kuifungia timu yake bao.


Baada ya Kavumbagu kufunga bao hilo, shabiki huyo aliyekuwa amevaa jezi nyeupe na kutambulishwa kwa jina la Deodatus Isaya Mwakiangula.
Imeelezwa Mwakiangula ni meneja wa baa ya Rose iliyo katika eneo la Kimara jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa madaktari viongozi waliokuwa kwenye Uwanja wa Taifa, leo na kumhudumia Mwakiangula kabla ya kupoteza maisha, Nassor Matuzya alithibitisha kuhusu kifo hicho.
Madaktari hao walifanya juhudi kuokoa maisha ya MWakiangula lakini hata hivyo ilishindikana.

Kavumbagu alifunga bao lake katika dakika ya 14, hata hivyo baadaye Azam FC walisawazisha zikiwa zimebaki dakika 8 mpira kwisha kupitia Kelvin Friday.

SALEHJEMBE

Yanga yabanwa Taifa, Azam yaendeleza rekodi

* Hamis Kiiza 'Diego' akosa penati
Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao lililofungwa na Didier Kavumbagu (wa pili kulia), wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara ilipopambana na Azam  FC kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo. Timu hizo zilitoka sare ya 1-1. (Picha na Francis Dande)
Heka heka: Golikipa wa timu ya Azam FC, Aishi Salum akiokoa moja ya hatari langoni mwake.
Mfungaji wa bao la Yanga, Didier Kavumbagu akitafuta mbinu za kuwatoka mabeki wa Azam FC.
Beki wa Azam FC, Gadiel Michael akimiliki mpira (kushoto) akiwania mpira huo ni mshambuliaji wa yanga, Hamis Kiiza. 
Mashabiki wa Yanga, wakiwa hawaamini timu yao ikibanwa na Azam
Mshambuliaji wa Yanga, simon Msuva akimtoka beki wa Azam FC, Kipre Bolou

BAO la dakika ya 83 lililofungwa na kinda Kelvin Friday lilizima ndoto za Yanga za kutaka kuvunja rekodi ya Azam ya kutopoteza mchezo wowote katika Ligi Kuu Tanzania Bara na kuisaidia vinara hao kupata sare ya bao 1-1 dhidi na watetezi hao.
Yanga waliokuwa wakitaka kulipa kisasi cha kulazwa mabao 3-2 katika mechi ya kwanza bao la uishindi likifungwa pia na kinda mwingine wa Azam, Joseph Kimwaga, watajilaumu baada ya kupata penati iliyopotezwa na mshambuliaji Hamis Kiiza 'Diego'.
Kipa Aishi Manula aliyekuwa nyota wa mchezo huo kwa leo alipangua mkwaju wa Diego na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda kabla ya beki wake wa pembeni, Erasto Nyoni kulimwa kadi baada ya kuzozana na mwamuzi Hashim Abdallah.
Bao la Yanga lililowapa matumaini ya kupunguza pengo la pointi baina yao na vinara hao wa ligi hiyo, liliwekwa kimiani dakika ya 14 kupitia kwa Didier Kavumbagu bao lililodumu hadi mapumziko.
Washambuliaji wa Yanga watajuta kwa kuikosesha mabao timu yao baada ya kukosa mabao mengi ya wazi wakiongozwa na Kiiza, Emmanuel Okwi na Kavumbagu kabla ya Husseni Javu kuingia.
Kwa matokeo hayo ya leo, Azam wameendelea kujiimarisha kileleni kwa kufikisha pointi 44, nne zaidi ya Yanga inayokamata nafasi ya pili ikiwa na pointi 40 na kufuatiwa na Mbeya City yenye pointi 39.
Hata hivyo Yanga bado ina mchezo mmoja mkononi baada ya klucheza mechi 19 wakati Azam imecheza 20.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea wikiendi kwa michezo kadhaa ambapo Yanga itasafiri hadi Tabora kuvaana na Rhino Rangers na Simba itaumana na Coastal Union Mkwakwani Tanga.

Yanga, Azam ni vita tupu taifa

Azam Fc

Yanga SC
VITA tupu na pambano la kisasi baina ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga na vinara wa sas wa ligi hiyo, Azam wakati wababe hao wawili watakaposhuka dimbani leo kupepetana katika pambano pekee litakalochezwa uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Yanga itashuka dimbani leo ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 3-2 iliyopewa na wapinzani wao ambap hawajapoteza mchezo wowote mpaka sasa katika ligi ya msimu huu ikiweka rekodi tangu walipopanda Ligi Kuu msimu wa 2008.
Azam inayoongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 43 itaikabili Yanga ikiwa na kumbukumbu ya ushindo mnono iliyopata kwa mabingwa wa zamani wa kandanda Coastal Union waliowacharaza mabao 4-0, huku Yanga ikishuka Taifa ikitoka kulazimishwa suluhu na mabingwa wa 1990-2000 na 2000-2001,  Mtibwa.
Watetezi wanahitaji ushindi katika mechi hiyo ili kulipa kisasi na pia kupunguza pengo la pointi na wapinzani wao waliowazidi pointi nn4, kwani wenyewe wana pointi 39 licha ya kuwa na mchezo mmoja mkononi.
Hata hivyo mechi hiyo ni ngumu kutabirika kutokana na ubora wa klabu zote mbili ambazo zitawakosa baadhgi ya nyota wao walio majeruhi.
Yanga wenyewe wataikabili Azam ikiwa imekamilika baada ya kurejea dimbani kwa nyota wake kama Haruna Niyonzima, Mrissoh Ngassa na Mbuyi Twitte, licha ya kukosa huduma za kipa Deo Munishi 'Dida;.
Makocha wa timu zote mbili wamenukuliwa kuwa vijana wao wapo tayari kwaajili ya pambano hilo, huku viongozi wa Azam wakiwa na imani kubwa ya kuibuka wababe kwa Yanga ili kutimiza lengo lao la kuwa mabingwa wapya wa Tanzania Bara baada ya kukwama misimu miwili mfululizo wakishika nafasi ya pili.
Je ni Yanga watakaoibuka kidedea na kulipa kisasi katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Hashim Abdallah au ni Azam itakayoendelezaubabe na kuking'ang'ania kiti cha uongozi wa ligi hiyo leo? Tusubiri

Abdallah Juma alia na Yondani, refa red card aliyolimwa Jamhuri

Abdallah Juma enzi akiichezea Simba
MSHAMBULIAJI wa Mtibwa Sugar, Abdalla Juma amelia na mwamuzi Zakaria Jacob na beki wa kati ya Yanga, Kelvin Yondani kutokana na kadi nyekundu aliyopewa kwenye mchezo wao na Yanga wikiendi iliyopita ulioisha kwa suluhu.
Juma, alisema alilazimika 'kuchapa' Yondani baada ya kushindwa kuvumilia vitendo alivyokuwa akifanyiwa na beki huyo uwanjani alivyovilalamikia kwa refa, lakini alipuuzwa mpaka alipandwa na hasira na kulimwa kadi hiyo.
Mshambuliaji huyo, mmoja wa wachezaji watatu waliofunga hat trick kwenye Ligi Kuu ya msimu huu, alisema Yondani alikuwa akimchezea kibabe wakati mwingine kumfinya, kumpiga makusudi na hata alipolalamika alipuuzwa.
"Laiti mwamuzi angekuwa 'fair' na kusikiliza malalamiko yangu juu ya uhuni nilikuwa nafanyiwa na Yondani naamini nisingefia pale, sijawahi kupewa kadi ya njano wala nyekundu kabla ya tukio hilo la Jamhuri, nimeumia sana," alisema.
Hata hivyo aliwaomba radhi wachezaji wenzake wa Mtibwa kwa kadi hiyo na kuelezwa ni vigumu mtu kuvumilia katika mazingira aliyokutana nayo siku ya mchezo huo kutokana na kuichachafya ngome ya Yanga na kumdhibi kihuni.
"Baada ya kuonekana tishio kwao waliamua kutumia 'uhuni' kunidhibiti na kwa kuwa refa alikuwa upande wao, walifanikiwa kunitoa mchezoni na kulimwa kadi hiyo ambayo ni ya kwanza kwangu tangu nianze kucheza soka," alisema Juma.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa AFC Arusha, Kagera Sugar na Simba alilimwa kadi hiyo nyekundu na mwamuzi Jacob dakika ya 53 baada ya kumchezea rafu mbaya, Yondani, kabla ya hapo ndiye mchezaji aliyekuwa tishio kwa Yanga.

Mwisho

Askari kanzu, Camera maalum kulinda pambano la Kaseba, Mashali PTA

Kaseba

Mashali
ASKARI kanzu na Kamera Maalum ndizo zitakazotumika kudhibiti hali ya ulinzi katika pambano la kimataifa la ngumi za kulipwa kuwania mkanda wa UBO Afrika kati ya Japeph Kaseba 'Champion' na Thomas Mashali 'Simba Asiyefugika' litakalofanyika Machi 29.
Pambano hilo la uzani wa kati litafanyika kwenye ukumbi wa PTA-Sabasaba jijini Dar es Salaam ambapo kutokana na mabondia hao wawili kuwa na mashabiki wengi, waratibu wake wamepanga kuimarisha ulinzi ili kuwafanya mashabiki watakaofika ukumbini kutokuwa na hofu juu ya usalama wao.
Akizungumza na MICHARAZO, promota wa pambano hilo litakalosindikizwa na michezo mingine kadha ya utangulizi, Ally Mwazoa alisema ili kulinda usalama siku ya mchezo huo watatumia kamera maalum kunasa matukio ndani na nje ya ukumbi ili ikitokea tatizo iwe rahisi kuwabaini wahusika.
Pia alisema mbali na kamera hizo, pia watatumika askari kanzu ambao watakuwa wakifuatilia matukio ndani na nje ya ukumbi ili kuweza kudhibiti uvunjifu wowote wa amani kwenye pambano hilo linalowakutanisha kwa mara ya kwanza Kaseba na Mashali.
Mwazoa alisema utaratibu huo pia utatumika katika pambano litakalofanyika April 26 ambaloo pia ameiandaa yeye kati ya Francis Miyeyusho dhidi ya mtoto wa bingwa wa zamani wa dunia wa WBU, Rashid Matumla, Mohammed Matumla 'Snake Boy Jr'.
Kuhusu maandali ya pambano la Kaseba na Mashali, Mwazoa alisema kila kitu kimekaa vyema na kwamba michezoi ya utangulizi siku hiyo itakuwa ni katika ya Haji Juma dhidi ya Juma Fundi, wakati Fred Sayuni atapambana na Rajabu Mahoja na Zuber Kitandula atamenyana na Issa Omar wakati Bakari Dunda ataoneshana ubabe na Baina Mazola
Pambano jingine lililokuwa liwakutanishe Allen Kamote wa Tanga dhidi ya Fadhil Awadh la kuwania ubingwa wa UBO-Mabara limefutwa kutokana na kifo cha Awadh aliyefariki jijini Dar es Salam baada ya kuugua ghafla na kuzikwa juzi mjini Morogoro.

Mashetani Wekundu leo ni kusuka au kunyoa Ulaya

Manchester United
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Englan ambao wapo kwenye msimu mbaya, watakuwa na kazi nzito leo mbele ya Olympiakos ya Ugiriki, ili kuamua hatma yao ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwakani.
Kipigo cha 2-0 ilichopewa ugenini wiki mbili zilizopita zimeifanuya Mashetani Wekundu hao kulazimika kushinda nyumbani kwenye uwanja wa Old Trafford ikiwa ndiyo nafasi pekee kwao kuweza kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kutokana na kupoteza nafasi ya kushiriki michuano hiyo msimu ujao kupitia nafasi nne za juu katika msimamo wa Ligi Kuu England.
Man United kwa sasa inashika nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu  ikiwa ponti 12 nyuma ya timu inayoshika nafasi ya nne, Man City ambayo hata hivyo ipo nyuma mechi mbili dhidi ya Man U.
Timu inayoongoza msimamo huo ni Chelsea ikiwa na pointi 66, ikifuatiwa na Liverpool na Arsenal ambazo zina pointi 62 huku Tottenham ikishika nafasi ya nne kwa pointi 53 ikifuatiwa na Everton yenye pointi 51 tatu mbele ya Man U.
Kwa mantiki hiyo kama United itashindwa kuibuka na ushindi dhidi ya Olympiakos leo na kisha kucheza kwa 'jihadi' hadi kutwaa ubingwa, itakuwa imepoteza nafasi ya kushiriki michuano hiyo msimu ujao kutokana na matumaini yao ya kumaliza nafasi ya nne kutoweka.
Tangu klabu hiyo ianzishwe imeshiriki michuano hiyo ya Uefa mara 26 huku ikiutwaa ubingwa huo  mara tatu, hivyo kuikosa michuano ya msimu ujao itakuwa mwanzo mbaya zaidi kwa David Moyes tangu alipomrithi Sir Alex Ferguson aliyeiongoza timu hiyo kwa mafanikio makubwa kuanzia 1986-2013. United imeutwaa ubingwa Uefa msimu wa 1967–68, 1998–99 na 2007–08
 Kadhalika hii itakuwa mara ya pili mfululizo kwa Man United kutolewa katika hatua ya 16 bora baada ya msimu uliopita kutolewa na Real Madrid kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya mechi ya awali Santiago Bernabéu kumalizika kwa sare ya 1-1 na mechi ya marudiano Old Trafford Madrid kushinda 1-2.
Hata hivyo, Man United itashuka katika Uwanja wao wa Old Trafford ikichukua tahadhari kubwa dhidi ya mshambuliaji wa Arsenal anayeichezea Olympiakos kwa mkopo, Joel Campbell ambaye alitupia moja kati ya mabao hayo mawili.
Campbell ambaye tayari amepania kuonyesha makali yake kwenye dimba hilo, amesema ni vema kwenda Old Trafford na kuonyesha kiwango kwa kuwa wanaamini kuna mafanikio makubwa wanakaribia kuyapata.
"Tunajua tunakaribia kupata mafanikio fulani makubwa," mshambuliaji huyo wa Olympiakos raia wa Costa Rica alisema.
"Kuonyesha uwezo Old Trafford ni kitu muhimu sana. Ninaamini ni ndoto kubwa za wachezaji."
Jana usiku miamba minginine ya England, Chelsea ilikuwa na kibarua kigumu nyumbani dhidi ya Galatasaray baada ya mechi ya awali kutoka sare ya bao moja, huku Real Madrid ikikamilisha ratiba nyumbani dhidi ya Schalke 04 kutokana na kushinda 6-1 ugenini katika mchezo wa kwanza.
Borussia Dortmund ni timu nyingine ambayo itakuwa nyumbani leo kuikaribisha Zenit St Petersburg bada ya awali kushinda ugenini 4-2.
Galatasaray ambayo ilikuwa ikihofiwa kuhitimisha safari ya Chelsea katika michuano hiyo, kutokana na kuwa na mshambuliaji wa zamani wa miamba hiyo ya England, Didier Drogba, kama itakuwa imefanikiwa kuitoa 'The Blues', itajiwekea rekodi nzuri dhidi ya timu za England kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya 16 bora baada ya misimu iliyopita kuzitoa Arsenal na Manchester City.
United ambayo Jumapili ilikubali kipigo cha mabao 3-0 nyumbani dhidi ya Liverpool, matumaini yake yapo zaidi katika michuano hiyo ya Ulaya baada ya kuonekana kuwa katika wakati mgumu kutinga nne bora kwenye Ligi Kuu England ili kupata nafasi ya kushiriki ligi hiyo yenye utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu msimu ujao.
Licha ya kuwa katika wakati mgumu, Kocha David Moyes amesema kikosi chake kitapigana kutoka kwenye kucha hadi katika meno ili kuuweka msimu hai.
"Wachezaji wapo makini zaidi wakiwa wanamaanisha Jumatano (leo) na nini tunachotakiwa kukifanya," Moyes alisema.
"Tumepata jambo la kwenda kulifanya, kwa hiyo tunatumai tutalifanya hilo."
United ina rekodi ya ushindi nyumbani ya alisimia 100 dhidi ya wapinzani wao wa Ugiriki, kwani  Olympiakos imepoteza mechi 11 ilizocheza katika ardhi ya England.
Man United inaogopwa kutokana na rekodi yake ya kupindua matokeo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya 2007 'kuichenjia kibao'  AS Roma kwa kuichapa 7-1 baada ya mechi ya awali kufungwa 2-1.
Olympiakos pia itashuka uwanjani ikiwa na hamasa ya ushindi wa mabao 2-0 iliyoupata Jumamosi dhidi ya Panathinaikos na kuzidi kujihakikishia kutwaa ubingwa wa Ugiriki.
Pambano jingine la leo litazikutanisha timu za Borussia Dotmund itakayoikaribisha Zenith iliyowafungwa nyumbani kwao kwa mabao 4-2

Dar Modern kuuza sura videoni


KUNDI la Dar Modern 'Wana wa Jiji' lipo wilayani Lushoto-Tanga likirekodia video za nyimbo za albam zao mbili walizozizindua hivi karibuni wakati wakiwatambulisha wasanii wao wapya.
Akizungumza na MICHARAZO kutoka Lushoto, mmoja wa waimbaji nyota wa kundi hilo, Hassan Kumbi 'Hassani Vocha', alisema tayari asilimia kubwa ya video hizo zimesharekodiwa.
Albamu hizo ni; 'Oh My Honey' na 'Kitwitwi' zenye nyimbo kama 'Oh My Honey', 'Naenda kwa Mume Wangu', 'Sikuamini Macho Yangu' na 'Malipo Duniani', 'Kitwitwi', 'Ngoma Imepasuka' na 'Siwanyimi Uzuri'.
Dar Modern ilianzishwa mwaka 2006 na imeshatoa albamu zaidi ya tano zikiwamo za 'Ni Vijimambo Tu', 'Sote Twasaka Riziki', 'Gharika la Moyo (Pembe la Ng'ombe)', 'Ndugu wa Mume Mna Hila', 'Toto la Kiafrika' na 'Nauvua Ushoga'.

Baby Madaha aachia mbili akiwa Kenya

 



MICHARAZO MITUPU
Baby Madaha katika pozi tofauti
NYOTA wa filamu na muziki nchini anayefanya shughuli zake kwa sasa nchini Kenya, Baby Madaha, ameachia kazi mpya mbili akiwa nchini humo.
Kazi hizo mbili moja ni ya filamu na nyingine ya muziki, fani iliyomtambulisha baada ya kushiriki shindano la kusaka vipaji vya kuimba la BSS.
Akizungumza na MICHARAZO, nyota huyo wa 'single' ya 'Summer Holiday', alisema filamu aliyoiachia inafahamika kwa jina la 'Gell Bladder' aliyoigiza na wasanii kadhaa nyota wa hapa Tanzania akiwamo Mariam Mndeme 'Mamushka' na wengine kutoka Kenya.
Baby alisema kwa upande wa muziki, ameachia 'single' iitwayo 'Mr DJ' ambayo ameirekodia katika studio za Candy Records zinazomilikiwa na 'mabosi' wake anaofanya nao kazi kwa sasa.
"Nimeachia kazi mbili moja ya muziki na nyingine ya filamu. Wimbo unaitwa 'Mr DJ' nimerekodi katika studio za Candy na filamu nimecheza na wasanii kadhaa maarufu wa Kenya na nyumbani yupo Mamushka na mimi mwenyewe," alisema.
Baby Madaha aliyewahi kufunika na wimbo wake wa 'Amore' uliokuja kuzaa albamu yenye jina kama hilo, alisema pamoja na kuachia kazi hizo yupo mbioni kuendelea kuwapa burudani mashabiki wake

Chelsea hiyoo robo fainali, Real yaua tena Wajerumani


Etoo akifunga bao la kwanza la Chelsea
Bale akimpongeza Ronaldo baada ya kutupia mpira kambani kutokana na pasi yake
VINARA wa Ligi Kuu ya England, Chelsea imedhihirisha kiu yao ya kutwaa taji la Liugi ya Mabingwa Ualaya kwa mara nyingine baada ya usiku wa jana kuikwangua Galatasaray ya Uturuki kwa mabao 2-0 na kutinga Robo Fainali.
Mabao ya Samuel Eto'o katika dakika ya nne na jingine la Gary Cahil kwenye dakika ya 43 yalitosha kuivusha vijana na Jose Mourinho na kuwafuta machozi mashabiki wa England ambao wiki iliyopita walishuhudia timu zao mbili za Arsenal na Manchester City ziking'olewa mashindanoni.
Kwa ushindi huo wa jana, Chelsea imeweza kuitupa nje timu ya nyota wa zamani Didier Drogba kwa jumla ya mabao 3-1 kwani katika mchezo wa kwanza walifungana bao 1-1 nchini Uturuki.
Katika mechi nyingine ya michuano hiyo, Real Madrid waliendeleza moto wao kwa kuizabua Schalke 04 ya Ujerumani kwa mabao 3-1 na kusonga robo fainali kwa jumla ya mabao 9-2.
Madrid ikiwa uwanja wa nyumbani wa Santiago Bernabeu ilipata mabao yake kupitia kwa nyota wake ambaye amezidi kuweka rekodi ya mabao kati ligi hiyo Cristiano Ronaldo katika dakika ya 21 na 74 na jingine likifungwa na Alvaro Morata.
Bao la kujifutia machozi la wageni lilitupiwa kambani na Tim Hoogland dakika ya 31 na kuwafanya Schalke kuaga kwa aibu michuano hiyo kwa msimu huu.
Katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo kumaliza timu za mwisho za kutinga robo fainali, Manchester United itakuwa nyumbani kuikaribisha Olympiacos ya Ugiriki waliowatambia kwao kwa mabao 2-0  nayo timu ya Borussia Dotmund itaikaribisha Zenit.  Katika mechi yao ya kwanza Wajerumani walishinda ugenini kwa 4-2
Timu sita za kwanza kufuzu robo fainali ya michuano hiyo kwa mwaka huu ni watetezi Bayern Munich, Barcelona, Atletico Madrid, PSG, Chelsea na Real Madrid

Tuesday, March 18, 2014

Hawa ndiyo wanasoka, makocha waliovuna fedha nyingi 2013

ronmessi622302_346025aJarida linaloheshimika kwa kiasi katika ulimwengu wa soka duniani ‘France Football’ leo hii limechapishwa listi ya wachezaji na makocha 20 wanaolipwa fedha nyingi ndani ya msimu mmoja.
Mapato ya wanasoka hao yamejumuishwa kutoka kwenye mishahara yao, na mikataba mbalimbali waliyonayo ya kibishara pamoja na bonasi wanazopata. Listi ipo kama ifuatavyo.

WACHEZAJI WALIONGIZA FEDHA NYINGI MIEZI 12 ILIYOPITA
  1. Lionel Messi – €41m
  2. Cristiano Ronaldo – €39.5m
  3. Neymar – €29m
  4. Wayne Rooney – €24m
  5. Zlatan Ibrahimovic – €23.5m
  6. Radamel Falcao – €21.2m
  7. Sergio Aguero – €19.7m
  8. Thiago Silva – €17m
  9. Eden Hazard – €16.8m
  10. Franck Ribery – €16.5m
  11. Fernando Torres – €16.2m
  12. Yaya Touré – €16m
  13. David Silva – €15.5m
  14. Gareth Bale – €14.5m
  15. Bastian Schweinsteiger – €14.5m
  16. Luis Suarez – €14.2m
  17. Mario Gotze – €13.9m
  18. Philip Lahm – €13m
  19. Gianluigi Buffon €12.9m
  20. Blaise Matuidi €12.9m
WACHEZAJI WALIONGIZA FEDHA NYINGI MIEZI 12 ILIYOPITA
  1. Jose Mourinho – €17m
  2. Pep Guardiola – €15m
  3. Roberto Mancini – €14m
  4. Carlo Ancelotti – €13.5m
  5. Fabio Capello – €12m
  6. Marcelo Lippi – €11.5m
  7. Arsene Wenger – €9.6m
  8. Roberto Di Matteo – €8.2m
  9. Andre Villas-Boas – €6.9m
  10. Rafael Benitez – €6.8m
  11. Luciano Spalletti – €6.5m
  12. Jurgen Klopp – €6.5m
  13. David Moyes – €6.4m
  14. Manuel Pellegrini – €6.4m
  15. Walter Mazzarri €6.1m
  16. Gerardo Martino – €5.4m
  17. Antonio Conte – €5.4m
  18. Claudio Ranieri – €5.2m
  19. Laurent Blanc – €4.2m
  20. Jorge Jesus – €4m
*Villa-Boas na Di Matteo wanaonekana kushika nafasi nzuri kwenye listi kwa sababu bado wanalipwa mishahara yao na Chelsea pamoja na Tottenham bbada ya vilabu hivyo kuwavunjia mikataba yao

Zantel yaipiga tafu CHANETA Klabu Bingwa ya Netiboli EA

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgvIIqu2KQRtz5d2FzsbLsP2QOSKbCUpep8SuRKj5U-M_VlpLawEw_r0qz8yMGoiJ-4NlGwjXN8IdS09n2z21ZgHjJ6nf9zPrSzYaQU22pKMbcG6BcgOdmQb-mhVUEkb-DEB0ly4MvBXD0/s640/DSC00021.JPG
Katibu Mkuu wa CHANETA, Anna Kibira

 KAMPUNI ya mtandao wa simu za mkononi ya Zantel, imesikia kilio cha Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) baada ya kutoa kiasi cha Sh. Mil 10 kufanikisha Fainali za Klabu Bingwa ya mchezo huo kwa Afrika Mashariki itakayoanza Jumamosi jijini Dar es Salaam.

CHANETA kwa kipindi kirefu imekuwa ikipiga la mgambo kuomba wadhamini na wafadhili kujitokeza kufanikisha michuano hiyo ambayo mpaka sasa timu 22 zimethibitisha kushiriki, zikiwemo klabu za Tanzania Bara na Visiwani.

Taarifa juu ya udhamini huo wa Zantel usome mwenyewe hapo chini: 

Zantel supports Tanzania Netball Association

Zantel Tanzania has handed over a support of 10 million Tanzania shillings to the Tanzania Netball Association (CHANETA) for the development of netball in the country.
Handing the cheque to the Permanent Secretary of the Ministry of Information, Youth, Culture and Sports, Honorable Sihaba Nkinga, Zantel Chief Commercial Officer, Sajid Khan said Zantel aims to support the development and prosperity of netball in the country.
‘As great supporters of sports fraternity in the country, we are happy to announce our support to the Netball association of Tanzania because netball is a very important game in Tanzania sporting landscape and it has good following in the country’ said Khan.
Khan further reiterated Zantel’s commitment towards supporting sports in the country, both at grassroots and professional level, through the sports associations and the ministry.
Speaking after receiving the cheque Nkinga expressed her appreciation towards Zantel for their generous support.
‘The involvement of Zantel will greatly contribute to the performance enhancement and development of Netball in Tanzania and will make the vision of CHANETA a reality’ said Nkinga.
Speaking at the event, CHANETA Chairman, Ana Kibira said Zantel’s support has come at the right time as they are in final preparation of the East Africa Netball Competition.
Kibira also noted that the sponsorship is a milestone for CHANETA and they are certain that the sponsorship will make it possible for netball to go far.
‘We thank Zantel for this great support, and we want to assure them their support will go direct in supporting our programs and general development of netball in Tanzania’ said Kibira.

Zantel has been in support of various sports in the country, and this is the second time they are sponsoring netball as last year they also did the same.

Newz Alert! Ajali mnbaya yatokea Morogoro


Chumba cha habari cha Globu ya Jamii hivi punde kimearifiwa na kutumiwa picha za tukio la ajali eneo la Mikese na Mdau Martin Mnyenyelwa,lakini hakutufahamisha kuhusiana na athari ya ajali hiyo akiwa kama shuhuda wa tukio hilo. Kulingana na tukio ya taarifa hii kuwa nyembamba,basi tuvute subira tutajuzana kadiri ya zitakavyokuwa zikiiingia kwenye chumba chetu cha habari 
CHANZO : MICHUZI BLOG








Mastaa Bongo Mpo! Ronaldo aokoa maisha ya mtoto

 
MADRID, Hispania
MWANASOKA bora wa dunia, Cristiano Ronaldo amedhihirisha kuwa ni mtu mwenye huruma baada ya kujitolea kulipa gharama za upasuaji wa mtoto mwenye umri wa miaka 10.

Mtoto huyo, Erik Ortiz Cruz, anasumbuliwa na matatizo mbalimbali ya kiafya na upasuaji ndio pekee utakaoweza kunusuru maisha yake.

Familia ya mtoto huyo imeshindwa kumudu gharama za matibabu ya mtoto huyo hospitali, ambapo gharama za kila kipimo ni pauni 5,020 za Uingereza na upasuaji ni pauni 50,240.

Kutokana na hali hiyo, Ronaldo ameguswa na jitihada zinazofanywa na familia hiyo kwa ajili ya kukusanya fedha za kulipia matibabu ya mtoto huyo na kuamua kubeba mzigo huo.

Awali, Ronaldo aliombwa kuchangia viatu na fulana ili vipigwe mnada kwa ajili ya kuchangia fedha za matibabu hayo, lakini aliamua kwenda mbali zaidi kwa kulipa gharama hizo.

Mapema mwaka huu, Ronaldo alisherehekea tuzo ya kuwa mwanasoka bora duniani na watoto wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kansa, akitekeleza ahadi aliyoitoa mwaka jana alipohojiwa na kituo cha redio cha Hispania.

Ronaldo alikutana na watoto hao wakati wa kipindi cha redio hiyo cha Partido de la 12 Novemba mwaka jana na kusema, iwapo atashinda tuzo hiyo, atasherehekea nao.

Afande kuzichezea Yanga, Azam kesho viingilio vyatajwa

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhNgRNeFylmsnnymnSCcIYonoCmcTVtwhsWiev1tkabvVA5Ap2gi4if2mY_-IqwoMi_WH02dJU5jQ9-6aM-B9yEX4V6UTWv1H6dujSz5nCGauRXz3Y3NDLejSHWxDEWpJxQZul65V3hJQzg/s1600/Yanga+Vs+Azam.JPG
Kesho shughuli itakuwa kama hii Taifa
REFA ambaye ni askari wa jeshi la Polisi Tanzania, Hashim Abdallah wa Dar es Salaam ndiye atakayechezesha mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Yanga na Azam itakayochezwa kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni.
Hashim atasaidiwa na Anold Bugado wa Singida, Florentina Zablon wa Dodoma na Lulu Mushi wa Dar es Salaam, wakati Kamisaa atakuwa Emmanuel Kavenga kutoka Mbeya na mtathimini wa waamuzi ni Alfred Rwiza wa Mwanza.
Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo zitaanza kuuzwa saa 2 asubuhi katika magari maalumu kwenye vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Ubungo Terminal, mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Samora/Ohio, OilCom Ubungo, Buguruni Shell, Dar Live- Mbagala, kituo cha daladala Mwenge na Uwanja wa Taifa.
Baada ya Saa 6:00 mchana mauzo yote yatahamia Uwanja wa Taifa ambapo milango kwa ajili ya mechi itakuwa wazi kuanzia saa 7.30 mchana.
Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 30,000 kwa VIP A, sh. 20,000 kwa VIP B na C wakati viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani kiingilio ni sh. 7,000.

31 waitwa Ngorongoro Heroes


http://api.ning.com/files/B1324qSIT2YHP3VnpeUs2tV6urKULGbGsXIW0ivs62epVguIVD-y1Y2QLatDIYJg4xIYEO7CJ8*76ZSUaM*o62wepyIvErnO/NGORONGOROHEROESGLOBAL.jpgWACHEZAJI 31 wameteuliwa kujiunga na timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 (Ngorongoro Heroes) kwa ajili ya michuano ya Afrika ambayo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Senegal.
Ngorongoro Heroes itakayokuwa chini ya Kaimu Kocha John Simkoko akisaidiwa na Mohammed Ayoub inaingia kambini kesho (Machi 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi ya kwanza dhidi ya Kenya itakayochezwa kati ya Aprili 4-6 jijini Nairobi.
Kikosi kinachounda timu hiyo ambayo itarudiana na Kenya kati ya Aprili 25-27 mwaka huu jijini Dar es Salaam kinajumuisha pia baadhi ya wachezaji walioonekana katika mpango wa ung’amuzi wa vipaji kwa ajili ya maboresho ya Taifa Stars.
Wachezaji walioitwa ni makipa Aishi Manula (Azam), Hamad Juma Hamad (Scouting- Temeke), Manyika Peter Manyika (Scouting- Ilala) na Mwinyi Hassan Hamisi (Mtende, Zanzibar).
Mabeki wa pembeni ni Ayoub Semtawa (Coastal Union), Edward Charles (JKT Ruvu), Frank Linus Makungu (Scouting- Rukwa), Gabriel Gadiel Michael (Azam), Hussein Mkongo (Ashanti United) na Ibrahim Said Mohamed (Chuoni, Zanzibar). Mabeki wa kati ni Bashiru Ismail (Tanzania Prisons), Faki Rashid Hakika (Ashanti United) na Pato Ngonyani (Majimaji).
Viungo ni Ally Nassoro (Coastal Union), Bryson Raphael (Azam), Farid Musa (Azam), Hamid Mohamed (Mbeya City), Hassan Mbande (Mtibwa Sugar), Ibrahim Mohamed Ibrahim (Scouting- Ilala), Idd Seleman (Ashanti United), Mohamed Issa Juma (Acudu, Afrika Kusini), Muhsin Ally Muhsin (Scouting- Kinondoni), Seleman Magoma (Scouting- Ruvuma) na Tumaini John (Scouting- Mwanza).
Washambuliaji ni Ally Salum Kabunda (Ashanti United), Ibrahim Hamad Hilika (Zimamoto, Zanzibar), Jafari Mwambusi (Mbeya City), Kelvin Friday (Azam), Ramadhan Bilal (Mlale JKT), Salum Abdilah Mineli (Ndanda) na Sibiank Lambard (Tanzania Prisons).

Airtel yakabidhi Mil 5 Tuzo za Mwanamakuka, Leila Mwambungu aibuka kidedea


Afisa Uhusiano wa Airtel, Jane Matinde (kushoto) akimkabidhi mfano wa hundi Mwenyekiti UWF na Mratibu wa Mradi wa Tuzo za Mwanamakuka Maryam Shamo wakati wa hafla ya Tuzo za Mwanamakuka 2014 ambapo Airtel Tanzania ni moja kati ya Wadhamini wa tuzo hizo ambazo Leila Mwambungu  aliibuka mshindi wa mwaka 2014. Wengine pichani kulia ni Mkurugenzi  Mkuu wa TWB Bi Margreth Chacha.
Afisa Uhusiano wa Airtel, Jane Matinde (kulia) akimpongeza mshindi wa tuzo ya Mwanamakuka 2014 Leila Mwambungu mara baada ya kutangazwa katika hafla iliyofanyika Escape One, Mikocheni Dar es Saalam.
Mshindi wa Tuzo za Mwanamakuka 2014, Leila Mwambungu akitoa shukrani zake mara baada ya kutangazwa katika hafla iliyofanyika Escape One siku ya Jumamosi. Kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) Margreth Chacha.
KAMPUNI ya simu za mkononi ya Airtel, imekabidhi waandaaji wa Tuzo za Mwanamakuka, Umoja wa Wanawake Marafiki (UWF) kiasi cha Sh. Mil. 5 wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo za Mwanamakuka-2014 zilizofanyika jijini Dar es Saalam, ambapo Leila Mwambungu aliibuka mshindi wa mwaka huu akiwabwaga washiriki wenzake tisa aliochuana nao.
Tuzo ya mwaka huu ilishirikisha washindi 10, watano wa mwaka 2012 na wengine wa mwaka 2013 kupima mafanikio yao kibiashara baada ya kunyakua tuzo na zawadi ya fedha katika shindano hilo lililoasisiwa mwaka juzi.
Mshindi huyo aliyekuwa mshindi wa pili wa tuzo za mwaka jana, aliibuka kidedea baada ya barua iliyoeleza alipotokea, alipo na malengo yake baada ya kushinda tuzo hiyo kutia fora na kumpa ushindi mbele ya wenzake.
Kampuni ya Airtel, imekuwa ikidhamini tuzo hizo tangu zilipoanzishwa safari hii ilikabidhi kiasi hicho cha fedha kupitia kwa Afisa Uhusiano wake, Jane Matinde aliyeeleza furaha waliyonayo kudhamini tuzo hizo kwa miaka mitatu mfululizo.
Matinde alisema Airtel wanajisikia faraja kuona wamekuwa sehemu ya kuleta mabadiliko kwa wanawake kupitia tuzo hiyo na kuahidi kuendelea kushirikliana na UWF kuhakikisha mabadiliko hayo yanawafikia wanawake wengi zaidi nchini.
“Tutaendelea kushirikiana na UWF, ili kuhakikisha tunawafikia wanawake wengi zaidi nchini,” alisema Matinde.
Kwa upande wa mshindi wa Mwanamakuka 2014, Leila Mwambungu alisema amejisikia furaha sana kushinda tuzo hiyo akidai hakuwa ametegemea na kuwashukuru waandaaji na wadhamini wake na kuomba waendelee kuwasaidia kuwakwamua wanawake nchini ambao wamejitosa kwenye shughuli za ujasiriamali.
"Naona fahari na furaha kuwa mshindi wa tuzo hizi za mwanamakuka kwa mwaka huu, napenda kuwashukuru sana waandaaji wa tuzo hizi kwa kuniona kupitia juhudi ninazoziweka katika kazi zangu na biashara zangu. Mpaka sasa nimeweza kuajiri watanzania kupitia biashara zangu. Kiasi nilichozawadiwa kitanisaidia kukuza zaidi mtaji wangu. Nashukuru sana," alisema mshindi huyo.
Naye Mwenyekiti UWF na Mratibu wa Mradi wa Tuzo ya Mwanamakuka, Mariam Shamo alisema tuzo hiyo inaendelea kukua na kuzidi kuiboresha na kudai lengo la shindano la mwaka huu lilikuwa kupima maendeleo ya washindi wao 10 kuona jinsi gani biashara zao zinavyosonga mbele baada ya kumzawadia aliyefanya vizuri zaidi.
"Tunashukuru sana Airtel kwa kushirikiana nasi miaka mitatu kwa sasa na tunaamini kuwa bado wataendelea kutoa mchango wao na kushirikiana nasi na kutuunga mkono kwa miaka mengine ijayo na kuhakikisha lengo letu la kumwinua mwanamke wa kitanzania linafikiwa," alisema Mariam.
Washiriki wa tuzo za mwaka huu walikuwa ni Tatu Ngao, Mwananne Msekalile, Sikudhani Daudi na Nasra Aziz walioshinda mwaka 2012 na Aziza Mbogolume, Leila Mwambungu, Theonistina Renatus, Maajab Yusufu na Agnes Daudi walioshinda mwaka 2013.

Chelsea kuifuta machozi England leo Ligi ya Mabingwa Ulaya?

CHELSEA leo inatarajiwa kuvaana na Galatasaray, ambapo mashabiki wa England wanataka kuona kama watawafuta machozi baada ya timu zao mbili za Arsenal na Manchester City ziking'olewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Timu nyingine ya England itakayoshuka dimbani kesho ni Manchester Unitd ambayo imewakatisha tamaa mashabiki wao kwa mwenendo wao mbaya na hivyo kutokuwa na tumaini nao kama watavuka 16 Bora na kuingia Robo fainali dhidi ya Olympiacos ya Ugiriki waliowanyoa 2-0 ugenini wiki mbili zilizopita.
Chelsea iliyoambulia sare ya 1-1 inavana na Gala, huku mshambuliaji wake wa zamani Didier Drogba hajui ni kwa namna gani ataweza kucheza kwa hamasa kubwa katika Uwanja wa Stamford Bridge  katika mechi hiyo ya leo.
Drogba alitwaa ubingwa wa England mara tatu, Kombe la FA mara nne, Kombe la Ligi mara mbili na ubingwa ulioweka kumbukumbu Ligi ya Mabingwa Ulaya 2012 akifunga penalti ya mwisho akiwa na Chelsea kwenye mechi ya fainali dhidi ya Bayern Munich katika Uwanja wa Allianz Arena.
Alifunga mabao 157 katika mechi 341 alizoichezea Chelsea kati ya 2004-12 huku akichaguliwa kama mchezaji wa kiwango cha juu zaidi katika historia ya klabu hiyo.
"Ni klabu ambayo nimepata uzoefu wa kila kitu," Drogba aliiambia tovuti ya UEFA (www.uefa.com). "Nimepata uzoefu wa kiwango cha juu, mechi kubwa na imenipa fursa ya kuwa karibu na wachezaji bora duniani.
"Ni kipindi maalumu kwangu kwa sababu sijui ni kwa vipi morali wangu utakuwa. Ninakubaliana kabisa kuhusu hili," alisema jijini Istanbul baada ya kutoka sare ya 1-1 na Chelsea.
Jose Mourinho alionekana akikaribia kumwaga chozi baada ya kupewa mapokezi mazuri katika awamu yake ya pili Stamford Bridge mwanzoni mwa msimu lakini anaamini Drogba anastahili heshima zaidi kutoka kwa mashabiki.
"Nadhani ninaruhusiwa kusema kwamba nitapata mapokezi mazuri kwa sababu ninajua mashabiki wa Chelsea na uhusiano wetu ulivyo wa kipekee," alisema Drogba.
"Itakuwa ni vizuri kuwaona kwa mara nyingine. Ninamtazamo wa mbeleni katika hilo."
Mourinho alimnunua Drogba na kumpeleka Stamford Bridge akitokea Olympique Marseille ambapo waliweza kushirikiana vema katika kufanya makubwa.
"Wakati Chelsea ikifikiria kunisajili, alikuwa ni Mourinho ambaye alikuja kuniona," alisema mchezaji huyo (36)- "Alisema, 'kama unataka kuwa mshmbuliaji mkubwa kama Thierry Henry ama Ruud van Nistelrooy, unapaswa kuja na kucheza chini yangu.
"Ni kweli nilikuwa mchezaji mzuri nikiwa Ligi ya Ufaransa lakini alinifanya kuwa mmoja kati ya wachezaji bora Ulaya. Ndiyo maana mimi, kwa Jose tunaweza kwenda sambamba hadi mwisho wa dunia.
Miamba hiyo ya Uturuki ni timu inayokuja kwa kasi, hivyo Chelsea itahitaji kufuta makosa yake baada ya Jumamosi kuangukia kichapo dhidi ya Aston Villa.
Ronaldo kuendelea kuweka rekodi Ulaya leo?
Katika mechi nyingine ya leo vinara wa Hispania, Real Madrid,  itakuwa inakamilisha ratiba yake ya kusonga mbele dhidi ya Schalke 04 baada ya mechi ya awali kuibuka na ushindi wa mabao 6-1 ugenini.
Katika mechi ya leo Real inatarajia kumpa nafasi Isco kuonyesha thamani yake baada ya kushindwa kupata namba ya kudumu chini ya Carlo Ancelotti tangu alipojiunga na timu hiyo kwa fungu kubwa akitokea Malaga.
Isco alikuwa ni biashara kubwa sokoni msimu uliopita baada ya kuiwezesha Malaga kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo, Ancelotti anaamini bado Isco anaweza kuzoea nafasi mpya anayochezeshwa, kama ilivyokuwa kwa Mholanzi Clarence Seedorf.
"Anahamasisha kupata namba ya kuanza kikosi cha kwanza. Kwa sasa ninamuamini. Mwanzoni alikuwa kama ilivyokuwa kwa Seedorf ambaye baadaye alipata uzoefu na kuwa mchezaji muhimu kwa Milan," Ancelotti alisema mapema mwezi huu.
Kivumbi kingine cha ligi hiyio kuhitimisha timu mbili za mwisho za kutiunga robo fainali zitachezwa kesho kwa mechi kati ya Manchester United itakuwa nyumbani kuikaribisha Olympiakos Piraeus kwenye Uwanja wa Old Trafford, ikiwa inaugulia kipigo cha mabao 3-0 ilichopewa wikiendi na Liverpool.
Pambano jingine litakuwa kati ya wanafainali wa mwaka jana, Borussia Dortmund itakuwa nyumbani nchini Ujerumani kuivaa Zenit St Petersburg waliowanyonyoa kwao mabao 2-0.
Timu za Bayern Munich ya Ujerumani, Barcelona ya Hispania, PSG ya Ufaransa na Atletico Madridi zenyewe tayari zimetangulia hatua hiyo baada ya kiushinda mechi zao wiki iliyopita.

Ngassa, Niyonzima warejea Yanga, Dida akiwakosa Azam

WAKATI winga machachari Mrisho Ngassa akianza kujifua na wenzake mjini Bagamoyo kwa ajili ya mechi yao ya kesho dhidi ya Azam, kipa tegemeo wa Yanga kwa sasa, Deo Munishi 'Dida' ataikosa mechi hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana  na jeraha la mkono.
Kwa mujibu wa  Daktari wa timu hiyo, Juma Sufiani, Dida hatakuwamo katika kikosi chao cha kesho ingawa wachezaji waliokuwa wagonjwa,  Mrisho Ngassa na Haruna Niyonzima wenyewe wameanza kujifua.
"Niyonzima (Haruna) na Ngasa (Mrisho) wamerejea kikosini na wameshaanza kujifua lakini tutamkosa kipa Dida katika mechi yetu inayofuata kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya mkono," alisema Sufiani.
Niyonzima alikuwa anakabiliwa na malaria, huku Ngasa akisumbuliwa na majeraha ya nyama za paja na Twite (ruhusa).
Wakati Yanga hali ikiwa hivyo kuelekea kwenye mchezo wao wa kesho ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki kuona nani atakayemtambia mwenzake, wapinzani wao waliowafungwa mabao 3-2 katika mechi ya kwanza pia watawakosa wachezaji kadhaa ambao ni majeruhi.
Meneja wa Azam , Jemedari Said aliwataja wachezaji hao ni Haji Nuhu, Joseph Kimwaga ambao wanauguza magoti.
Jemedari alisema wachezaji wengine wote wapo fiti kwa ajili ya mechi hiyo ambayo wanahitaji kushinda ili kutimiza ndoito zao za kutwaa ubingwa baada ya misimu miwili wakiishia kukamata nafasi ya pili nyuma ya Simba na Yanga.
Azam, inaoongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 43 baada ya majuzi kuifumua Coastal Union kwa mabao 4-0, huku Yanga ikikamata nafasi ya pili baada ya kuambulia sare na Mtibwa japo wanalinga pointi na Mbeya City waliopo nafasi ya tatu wakiwazidi mabao ya kufunga na kufungwa.

Ruvu Stars waachia tatu, wajipanga kurekodi video

Roggert Hegga enzi akiwa Twnaga Pepeta
BENDI mpya wa muziki wa dansi ya Ruvu Stars, imekamilisha kurekodi nyimbo zao tatu mpya na tayari wameanza kuzisambaza kwenye vituo vya redio kwa ajili ya kuchezwa hewani.
Mmoja wa viongozi na muimbaji wa bendi hiyo yenye maskani yake Mlandizi, Pwani Rogert Hegga 'Catapillar', alisema wamemaliza kurekodi nyimbo hizo katikati ya wiki iliyopita na tayari baadhi ya vituoi zimeanza kuzirushwa hewani wakijiandaa kurekodi video zake.
Hegga alizitaja nyimbo zilizorekodiwa ambazo ndizo zinazoitambulisha bendi hiyo kwa mashabiki wa muziki wakiwa wanataka kurejesha enzi za bendi za majeshi kutamba nchini ni pamoja na 'Network Love' utunzi wa  Mhina Panduka 'Baba Danny' a.k.a Toto Tundu, 'Jua Kali' wa Kuziwa Kalala na 'Spirit' ambao ni utunzi wake (Hegga).
"Tumeshakamilisha kurekodi nyimbo zetu za utambulisho na tumeshasambaza na baadhi ya vituo zimeanza kuzicheza," alisema Hegga.
Mtunzi na muimbaji huyo wa zamani wa bendi kadhaa maarufu nchini ikiwamo ya African Stars, Mchinga Sound, G8 Wana Timbatimba na Extra Bongo, alisema vibao hivyo ni mwanzo wa maandalizi ya kupakua albamu yao na kuwataka mashabiki wasubiri kupata uhondo zaidi.
"Mashabiki wajiandae tu kupata burudani, nyimbo hizi zitaleta mapinduzi makubwa katika muziki wa dansi kwani zimeenda shule na studio tuliyorekodia ni bab'kubwa," alisema.
Baadhi ya wanamuziki wanaounda bendi hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ni Khadija Mnoga 'Kimobitel', Hamis Amigolas, Hegga, Victor Mkambi, Mhina Panduka na wengine waliotoka bendi kadhaa za jijini Dar es Salaam.