STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, April 1, 2013

Bandari yaonja kipigo, Gor Mahia, Sofapaka ziking'ara KPL

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Kenya, Tusker




BAADA ya ushindi mfululizo, vijana wa Bandari Kenya mwishoni mwa wiki waliisherehekea vibaya sikukuu ya Pasaka baada ya kunyukwa na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL)  Tusker kwa mabao 2-1, huku Gor Mahia na Sofapaka zikipata ushindi katika mechi zao zilizochezwa jana.
Kipigo ilichopewa Bandari inayochezwa na watanzania wanne waliowahi kutamba na klabu za Simba na Yanga imeipomosha timu hiyo kwa nafasi moja nyuma toka ya tano hadi sita ikizimwa na kasi yake ya kutoa vipigo kwa wapinzani wake baada ya kushinda mara mbili mfululizo na hivyo kusaliwa na pointi zake nane.
Bandari waliokuwa ugenini ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao kwea kuwashtua vijana wa Tom Olaba kocha aliyewahi kuinoa Mtibwa Sugar kwa bao lililofungwa na Eric Okoth kabla ya Jesse Were na Mganda, Andrew Ssekyayomba kuzima matumaini ya Bandari kupata ushindi wa tatu mfululizo.
AFC Leopard wakiwa ugenini walikiona cha mtema kuni siku ya Jumamosi baada ya kunyukwa mabao 2-1 na Muhoroni Youth, huku vijana wa KCB jana walirejea kileleni mwa msimamo baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya mabingwa wa 2010 Ulinzi Stars na kuwaengua Thika United waliokuwa wamekalia kiti hicho kwa saaa 24 baada ya Jumamosi kuicharaza Chemelil 2-1.
Mabao ya vijana hao watunza fedha wa benki ya biashara ya nchini, yaliwekwa kimiani na Jacob Keli na Edward Mwaura na kuifanya timu yao irejee kileleni kwa kujikusanyia pointi 14, mbili zaidi ya Thika.
Nao mabingwa wa zamani wa Kombe la Shirikisho Afrika, Gor Mahia jana ilizinduka katika ligi hiyo kwa kuidonyoa Mathare United kwa bao 1-0 baada ya wiki iliyopita kuzimwa na Ulinzi kwa kulazwa mabao 2-0.
Ushindi huo umeifanya Gor Mahia inayochezwa na kipa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ivo Mapunda kukwea hadi nafasi ya 10 ikiwa mbele ya mabingwa watetezi Tusker waliopata ushindi wake wa kwanza katika mechi tatu ilizocheza msimu huu.
Mabingwa wa zamani wa Kenya, Sofapaka nao jana walitoa kipigo kitakatifu kwa Karuturi Sports kwa kuikong'ota mabao 4-2 katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo ya Kenya.
Matokeo kamili ya mechi za ligi hiyo ya jirani zilizochezwa mwishoni mwa wiki ni kama ifuatavyo;

Nairobi City Stars v Sony Sugar (2-1)
Thika United v Chemelil (2-1)
Western Stima v Home Boys (1-0)
Muhoroni Youth v Leopards (2-1)
 Tusker  v Bandari (2-1)
KCB v Ulinzi Stars (2-0)





Sofapaka v Kurituri Sports (4-2)






Gor Mahia v Mathare United (1-0)







































Sikinde yachekelea ujio wa Mbinga

Adolph Mbinga (kulia) akicharaza gitaa kando ya Hassan Rehani BItchuka
UONGOZI wa bendi ya muziki wa dansi ya Mlimani Park 'Sikinde' umesema kutua kwa  Adolph Mbinga kumeiongezea nguvu bendi yao ambayo leo inamalizia shamrashamra  za Sikukuu ya Pasaka eneo la Mivinjeni, Dar es Salaam.
Mbinga, nyota wa zamani wa bendi kadhaa ikiwamo African Stars, Mchinga Sound na  Levent Musica, ametua Sikinde wakati bendi hiyo ikimpoteza muimbaji wao nyota,  Athuman Kambi aliyekimbilia Msondo Ngoma.
Katibu Mkuu wa Mlimani, Hamis Mirambo alisema wanaamini kwa uzoefu alionao  Mbinga utaisaidia Sikinde kuzidi kusimama imara na kuwakimbiza wapinzani wao katika  muziki wa dansi.
Mirambo alisema uzuri wa Mbinga mbali na kucharaza magita, pia ni mtunzi na  muimbaji kitu ambacho kitaisaidia Sikinde baada ya kuondokewa na wanamuziki wake  kadhaa wakiwamo waliofariki au kutimkia kwa mahasimu wao Msondo Ngoma.
Mirambo alisema bendi hiyo baada ya kumtambulisha Mbinga mwishoni mwa wiki, leo  watamalizia zoezi hilo katika siku ya Jumatatu ya Pasaka eneo la Mivinjeni, Kurasini.
"Tutamalizia kumtambulisha Mbinga na nyimbo zetu mpya," alisema  Mirambo.

---------

Bessa alia wasanii kunyonywa jasho lao


Salim Mbwana 'Bessa' a.k.a Madhira
MCHEKESHAJI Salim Mbwana 'Bessa' amedai kuwa sanaa ya maigizo nchini bado haijanufaisha wadau wake kulingana na ukubwa wa kazi wanayofanya kutokana na kuwapo kwa unyonyaji na wizi unaofanywa na watu wachache waliohodhi soko la fani hiyo.
Bessa ambaye ni mlemavu wa miguu, alisema kwa namna wadau wa sanaa hiyo wanavyochapa kazi, ni wazi kwamba wangekuwa mbali sana kiuchumi akitolea mifano wasanii wa Nigeria.
"Bado sanaa haijaleta mafanikio kama jasho linalovuja kwa wasanii, kuna haja ya  kuongezwa juhudi za kunusuru fani hii ili wadau wanufaike kama wasanii wenzao wa  kimataifa," alisema Bessa anayejiita 'Madhira'.
Alisema hata yeye mwenyewe pamoja na kujivunia umaarufu mkubwa alionao, tangu aanze kuuza sura kwenye filamu na vichekesho mbalimbali, bado hawezi  kutembea kifua mbele kujisifia mafanikio kwani yupo 'choka mbaya'.
"Sanaa haijaninufaisha ipasavyo, sina cha kujivunia kwa vile kuna hali ya ubabaishaji mkubwa kwa wasanii nchini kunyonywa na kuibiwa jasho lao," alisema Bessa.
Mkali huyo aliyewahi kutamba na utunzi wa riwaya katika gazeti hili, kwa sasa ndiye  mtunzi mkuu katika kampuni iliyompa ajira ya kudumu ya ASl Riyamy.

Irene Paul Hofu filamu ya Kanumba

Irene Paul aliyecheza kama mhusika mkuu katika filamu ya Love & Power

MUIGIZAJI kinara wa filamu ya mwisho ya nyota wa zamani wa fani hiyo nchini, Steven Kanumba iitwayo "Love and Power', Irene Paul amedai anahofia kufufua upya majonzi ya kifo cha Kanumba kilichotokea Aprili mwaka jana.
Irene alinukuliwa wiki hii akisema kutoka kwa filamu hiyo kutaamsha majonzi yake na ya mashabiki wakubwa wa marehemu Kanumba anayetimiza mwaka mmoja  tangu afikwe na mauti ghafla nyumbani kwake Sinza Vatican.
"Kwa kweli sitamani hata kuiona filamu hiyo, naamini itafufua upya majonzi ya  kumpoteza Kanumba ambaye kwangu ni mmoja wa wasanii wakubwa zaidi kuwahi kutokea nchini," alisema  Irene.
Filamu hiyo inatarajiwa kuachiwa rasmi Aprili 12 ikiwahusisha washiriki watatu ambao wametangulia mbele ya haki bila wenyewe kuishuhudia kazi hiyo.
Wasanii hao waliofariki ni Husseni Mkiety 'Sharo Milionea' na John Stephano Maganga waliofariki kwa nyakati tofauti mwishoni mwa mwaka jana.
Kwa mujibu wa taarifa za wasambazaji wa filamu hiyo, inatarajiwa kuzinduliwa rasmi  siku ya kumbukumbu ya kifo cha Kanumba Aprili 6 kabla ya kuingizwa sokoni wiki  inayofuata.
Inaelezwa kuwa simulizi la filamu hiyo linashabihiana na tukio halisi lililosababisha kifo cha Kanumba.

Kava la filamu ya mwisho ya Marehemu Kanumba

IBF Afrika sasa yahamia Botswana


 
Rais wa IBF Africa, Onesmo Ngowi (kushoto)
RAIS wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati, Mtanzania Onesmo Ngowi amewasili katika jiji la Gaborone, Botswana kupromoti ubingwa wa IBF wa Kimataifa katika uzito wa Bantam.  
Bondia wa Botswana Lesley Sekotswe na bondia mwenzake kutoka nchini Namibia Immanuel “Prince” Naidjala walitoka sare wakati wakishindania ubingwa huo katika pambano lililofanyika katika jiji la Windhoek, Namibia tarehe 20 Mei  mwaka huu.  
Ujio wa Rais Ngowi ulikuwa unangojewa na wadau wengi wa ngumi katika nchi hii tangu aitembelee Botswana mwaka 2002 wakati wa mpambano kati ya bondia wa Botswana Thuso Kubamang na Peter Malinga kutoka nchini Afrika ya Kusini.  
Rais Ngowi atakutana na viongozi wa serikali ya Botswana pamoja na wadau mbalimbali wa ngumi na safari yake itaanzia jiji kuu la Gaborone mpaka jiji la pili kwa ukubwa la Francistown ambako wadau wengi wa ngumi wanamsubiri kwa hamu.  
Nchi ya Botswana ni nchi yenye msingi mzuri sana wa ngumi za ridhaa lakini tatizo kubwa limekuwa ni namna ya kuwaendelza wanapofikia kikomo kwenye ridhaa. Kikao cha Ngowi na viongozi wa serikali wa Botswana kitaweka msingi mzuri wa namna ya kuwaendeleza mabondia wa Botswana. 
Botswana ni nchi inayopakana na Namibia kwa hiyo mpambano wa Sekotswe na Naidjala unategemewa kuwa na wapenzi wengi wa ngumi kutoka katika nchi hizi mbili.

Picha, Promota Kinda Nangolo wa Namibia akimwaga Rais wa IBF/Africa Onesmo Ngowi wakati akiondoka nchini humo kuelekea Botswana!

Sunday, March 31, 2013

Liverpool yazinduka EPL, yaifumua Aston Villa kwao

http://cache.images.globalsportsmedia.com/news/soccer/2013/3/31/315082header.jpg
Nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard akishangilia bao la jioni ya leo

MABINGWA wa zamani waUlaya, Liverpool jioni ya leo imezinduka tena kwenye Ligi Kuu ya England baada ya kupata ushindi wa mabo 2-1 ugenini mbele ya wenyeji wao Aston Villa.
Mkwaju wa penati iliyopigwa na nahodha Steven Gerrard katika dakika ya 60 ndiyo iliyoihakikisha Liverpool ushindi wa pointi tatu muhimu baada ya kwenda mapumziko wakiwa nyuma kwa bao 1-0 lililotupiwa kambani na Mbelgium mwenye asili ya DR Congo, Christian Benteke.
Benteke alifunga bao hilo katika dakika ya 31, akimaliza kazi nzuri ya Gabriel Agbonlahor.
Wageni waliingia kipindi cha pili kwa kasi na iliwachukua dakika mbili tu kusawazisha bao kupitia Jordan Henderson na dnipo kwenye dakika ya 60 Gerrard akatupia mpira wavuni kwa penati  baada ya Luis Suarez kuangushwa langoni mwa Aston Villa alipokuwa akienda kumsalia kipa wa Brad Guzan.
Hata hivyo ushindi huo wa leo umeiacha Liverpool katika nafasi ya saba, ikiwa imecheza mechi 31, ikiwa nyuma ya wapinzani wao, Everton walioishinda jana bao 1-0 dhidi ya  Stoke City.

Maiti sasa zafikia 29 ajali ya jengo lililoporomoka Dar

Zoezi la kusaka miili zaidi ya watu likiendelea kufanywa kwa umakini mkubwa
Mojawapo ya magari kibao yaliangukiwa pia na jengo hilo
Wengine walikuwa ndani ya magari yao wakati mjengo ukiporomoka na kuwafunika
Jengo pacha... ujenzi wa jengo hili lililopakana na jingine lililoanguka umesitishwa kwa muda na serikali ili kupisha uchunguzi kwani mwenye jengo hili ndiye mmiliki wa lile lililoanguka na pia kampuni ya ujenzi ni ileile, mkandarasi ni yuleyule na mahala penyewe ni hapa hapa, kwenye makutani ya barabara ya Morogoro na Indira Gandhi.   

Jengo pacha la ghorofa 16... ujenzi wa ghorofa hili umesimamishwa kupisha uchunguzi. Mmiliki wa jengo hili ndiye mmiliki wa lile lililoanguka, kampuni ya ujenzi ni ileile, mkandarasi ni yuleyule na mahala penyewe ni hapa hapa kwenye makutani ya barabara ya Morogoro na Indira Gandhi.  
Idadi ya miili ya watu walionasuliwa kutoka katika kifusi cha jengo la ghorofa 16 lililoporomoka juzi wakati likiendelea kujengwa kwenye makutano ya Morogoro Road na Indira Gandhi sasa imefikia 29, imefahamika.  

"Hadi sasa tumeshapata miili ya watu 29 kutoka kwenye kifusi cha mabaki ya jengo lililoanguka," Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick amesema leo Machi 31, 2013.

Ameongeza kuwa waokoaji sasa wanaendelea kusaka miili zaidi katika lililokuwa jengo la chini ambako kulikuwa na ghala la vifaa na inadhaniwa kuwa huko ndiko kulikokuwa na watu wengi zaidi; na kwamba zoezi la kusaka miili litaendelea mpaka wahanga wote wapatikane.

Rais Jakaya Kikwete, ambaye alitembelea eneo la tukio juzi katika siku ya Ijumaa Kuu, ameagiza kwamba wahusika wote waliosababisha maafa hayo wafikishwe mbele ya mkono wa sheria na hadi sasa, polisi wamesema kuwa tayari wameshawatia mbaroni watuhumiwa wanne.

GOLDEN BUSH VETERANI YAIZAMISHA WAHENGA

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEigEXcYZjHBYFe7oOEgW5OFabOhx7fWDF32Rsh1DNIyJgIuc8Evl-_yJ_6-t3SWerT20D7radHa4TQSZKy32dCj_g7jev9QWI1KeveOocs9OaXA0c4U8BREl7bBYDCuQ4pz95KuTxPJFBI/s1600/Golden+Bush+Veterani.JPG
Kikosi cha Golden Bush Veterani
 
WAKALI wa soka la maveterani jijini Golden Bush Veterani jioni ya leo imeisherehekea vyema sikukuu ya Pasaka baada ya kuwafumua wapinzani wao wakuu, Wahenga Fc kwa kuwalaza mabao 2-1 katika pambano maalum lililochezwa kwenye uwanja wa Kinesi, Ubungo Dar es Salaam.
Mchezo huo uliochezwa huku mvua kubwa ikinyesha na kuhudhuriwa na Kamanda wa Polisi, Thobias Andengenye ulishuhudiwa Wahenga wakitangulia kupata baop la kuongoza lililotumbukizwa wavuni na Albert Shao.
Hata hivyo Golden Bush iliyokuwa ikiongozwa na nahodha wake, Onesmo Wazir 'Ticotico' ilisawazisha bao hilo kupitia kwa nyota wa pambano hilo, Sadick Muhimbo na kufanya hadi mapumziko timu hizo ziwe nguvu sawa.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko ya wachezaji ambapo iliongeza uhai wa pambano hilo ambalo pande zote zilionyesha kulikamia na kuhiotaji ushindi ili kulinda heshima mbele ya mwenzake, japo utelezi na maji yaliyosababishwa na mvua iliyokuwa ikinyesha ilipunguza utamu wa soka la timu hizo.
Golden Bush ilifanikiwa kuandika bao la pili la la ushindi kupitia kwa 'Super Sub' wao De Natale alifumua shuti kali baada ya mabeki wa Wahenga kuzembea kuokoa mpira langoni mwake.
Mpaka filimbi ya mwisho ya mwamuzi wa pambano hilo, Ally Mayay ilipolia kuashiria pambano hilo limemalizika Wahenga walijikuta hoi kwa wapinzani wao kwa kula kichapo cha mabao 2-1.

Saturday, March 30, 2013

Maiti 21 zapatikana ajali ya ghorofa, nane washikiliwa na Polisi

Ibrahim Kissoki (kushoto) anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Dar kuhusiana na ajali ya jengo lililoporomoka jana asubuhi. Hapa alikuwa akimfafanulia jambo Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge.


WAKATI maiti nyingine ikiwa imepatikana jioni hii na kufanya idadi ya waliokufa kwenye ajali ya jengo la ghorofa 16 lililoporomoka kufikia 21, watu nane akiwamo Diwani wa Goba, Ibrahim Kissoki wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kutokana na mkasa wa ajali hiyo.
Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, RPC Suleiman Kova, amenukuliwa hivi punde kuwa Kissoki ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni yua Ujenzi ya Lucky Construction Ltd na watu wengine saba akiwamo wamiliki wa jengo hilo na wakandarasi na maafisa wa Manispaa ya Ilala wanashikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano zaidi ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Kova, alisema mpaka sasa wakati zoezi la uokozi likiendelea eneo la tukio mitaa ya Indra Ghandi na Zanaki watu waliofariki katika ajali hiyo ni 21, nane kati yao wakiwa wameshatambuliwa na ndugu zao.
Kamanda huyo alisema wanaendelea kusaka wahanga wa ajali hiyo kuona kama watapata miili minmgine ya waliozikwa na kifusi cha jengo hilo linalomilikiwa na mfanyabiashara maarufu nchini, Ally Raza.
Tunaendelea kufuatilia taarifa na tutawaletea hapa hapa.

Vita vya Ligi Kuu Bara ndiyo kwanza vimeanza


 
http://3.bp.blogspot.com/-4Yv7aB6pBF4/UQJ6EXASNmI/AAAAAAAAiMo/jfdsnoiqHiQ/s1600/VPL.png
MATOKEO ya mechi zilizochezwa jioni ya leo za Ligi Kuu Tanzania Bara yamebadili msimamo na kutoa dalilia kwamba vita vya kuwania ubingwa na vya kuepa kushuka daraja vimeanza upya.
Yanga na Azam zinaendelea kubanana kwenye uwaniaji wa ubingwa, huku Toto African, Polisi Moro, African Lyon zikiwa bado katika vita kali ya kuepuka kushuka daraja mkiani.
Sare ilizopata Toto African na Polisi Morogoro katika viwanja vyao vya nyumbani dhidi ya wapinzani wa jadi nchini, Simba na Yanga zimezifanya timu hizo kurejea mkiani wakiipokea Lyon.
Toto imerudi mkiani ikilingana pointi 18 na Polisi ila uwiano wa mabao ndiyo unaowatofautisha nyuma ya Lyon walioifumua Coastal bao 1-0 na kufikisha pointi 19.
Kileleni, licha ya Yanga kuendeleza rekodi ya kutopoteza mchezo wowote wa ligi hiyo ndani ya mwaka 2013, lakini imeshindwa kutimiza ndoto ilizokuwa nazo leo za kuivua Simba ubingwa iwapo ingeshinda mbele ya Polisi na sare iliyopata Simba jijini Mwanza.
Suluhu ya kutofungana imeifanya Yanga kufikisha pointi 49 na kuendelea kuipa nafasi Azam kuwakaribia baada ya wauza Lambalamba haop kushinda bao 1-0 uwanja wa Mabatini.
Kagera iliyosaliwa na mechi nne imenufaika na kucheza nyumbani kwa kushinda mechi ya pili mfululizo na kukwea nafasi ya tatu, ikiiengua rasmi Simba, huku Coastal Union yenye ndoto za kumaliza katika Tatu Bora imekwama mbele ya Lyon, huku JKT Ruvu iliyozinduka katika mechi yao ya mwisho dhidi ya Polisi Moro imeendelea kuchechemea msimu huu.
Misimu mitatu iliyopita JKT Ruvu ilitisha na ukali wake kwa sasa umehamia kwa Ruvu Shooting ambayo hata hivyo leo ilishindwa kukwepa kipigo cha nyumbani mbele ya Azam waliosalia nafasi ya pili katika msimamo huo wa ligi kuu.
Msimamo kamili wa Ligi hiyo ilioyosaliwa raundi chache kabla ya kufunga msimu ni kama ifuatavyo:

                                  P     W    D     L     F      A       D      Pts
1. Young Africans     21   15     4     2     37     12     +25   49
2. Azam                    21   13     4     4     36     16     +20   43     

3. Kagera Sugar        22   10     7     5     25     18     +7     37    
4. Simba                   21     9     8     4     30     19     +11    35 

5. Coastal Union      22     8     8     6     23     20     +3      32   
6. Mtibwa Sugar      22     8     8     6     24     22     +2      32   
7. Ruvu Shooting     21     8     5     8     21     19     +2      29    
8. JKT Oljoro FC     22     7     7     8     22     24     -2      28    
9. JKT Mgambo      21     7     3     11     14     21     -7     24
10.Ruvu Stars          21     6     4     11     19     34     -15   22
11.Tanzania Prisons 21     4     8     9       11     20     -9     20   
12.African Lyon      22     5     4     13     15     32     -17   19
13.Polisi Morogoro  22     3     9     10     11     21     -10   18   
14.Toto Africans      22     3     9     10     19     30     -11   18
            

Yanga yabanwa, Simba yaporomoka, Azam, Kagera zatakata

Yanga waliobanwa Morogoro
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba imezidi kuporomoka kwenye msimamo wa Ligi kuu baada ya Kagera Sugar kuiengua nafasi ya tatu kutokana na kupata ushindi wa mabao 3-1 mbele ya Mtibwa Sugar wakati 'Mnyama' akiambulia sare ya mabao 2-2 jijini Mwanza mbele ya Toto African.
Simba iliyobanwa Mwanza na Toto African

Kagera imeilaza Mtibwa Sugar mabao 3-1 na kufikisha pointi 37 wakati Simba kwa sare hiyo ya Toto imefikisha pointi 35 na kutoa nafasi kwa Yanga na Azam kuzivua taji lake inalolishikilia kwa sasa.
Simba ilishtuliwa kwa bao la kuongoza la Toto lililofungwa dakika ya 25 kabla ya Simba kuchomoa dakika tatu baadaye kupitia ramadhani Mkopi na kufanya hadi mapumziko matokeo yawe 1-1.
Kipindi cha pili Simba ilifunga bao la pili kupitia Mrisho Ngassa kabla ya Toto kusawazisha kupitia kwa Ramadhani na kufanya timu hizo zigawane pointi moja moja.
Yanga iliyokuwa mjini Morogoro ilishindwa kuivua Simba ubingwa na badala yake kutoa mwanya kwa Azam kuendelea kuwafukuzia katika mbio zao za kuwania taji la ubingwa msimu huu baada ya kulazimishwa suluhu ya kutofungana.
Kikosi cha Kagera Sugar kilichoiengua Simba nafasi ya tatu
Azam ilipata ushindi wa bao 1-0 kwenye uwanja wa Mabatini, Mlandizi Pwani na kufikisha pointi 43 na kupunguza pengo lililokuwa awali la pointi nane na kufikia sita.
Bao la Azam liliwekwa kimiani na kinara wa mabao wa Ligi Kuu kwa sasa Kipre Tchetche na kuifanya Azam kuiacha Simba kwa pointi 8.
Azam waliitungua Ruvu Shooting

Jijini Dar es Salaam African Lyon imeiduwaza Coastal Union kwa kuilaza bao 1-0 wakati Arusha wenyeji, JKT Oljoro waliilaza maafande wenzao wa JKT Ruvu kwa mabao 2-0 na kuzidi kuimarisha mbio zake za kuelekea kwenye nafasi ya kuepuka kushuka daraja.
Matokeo kamili ya mechi za leo ni kama ifuatavyo hapo chini:
 Polisi Moro v Yanga (0-0)
JKT Oljoro v Ruvu JKT (2-0)
Kagera Sugar v Mtibwa (3-1)
Toto African v Simba  (2-2)
African Lyon v Coastal (1-0   )
Ruvu v Azam   (0-1)

Idadi ya waliokufa ajali ya Ghorofa yaongezeka


IDADI ya watu waliofariki katika tukio la kuporomoka kwa ghorofa lilililokuwa likijengwa imeongeza na kwa sasa imefikia watu 20.
Tayari watu waliopoteza ndugu zao katika ajali hiyo iliyotokea jana kweye mtaa wa Indra Ghandi wamemiminika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kutambua miili ya ndugu zao.
Mpaka sasa miili ya watu nane imetambuliwa wakiwemo watu watatu wenye asilia ya Asia na wengine waliosalia wakiwa ni wafanyakazi waliokuwa wakijenga ghorofa hilo.
Pia hospitalini hapo imeonwa viungo vya watoto na watu wazima vilivyokatika na kutia hali ya simanzi, huku juhudi zikifanywa kupata majina ya watu waliopoteza uhai huo na wale ambao wamenusurika kwenye ajali hiyo.

  

Golden Bush Veterani, Wahenga kesho hapatoshi Kinesi

Onesmo Waziri 'Tictico'
PAMBANO la kirafiki la kusherehekea sikukuu ya Pasaka kati ya Golden Bush Veterani na wapinzani wao wakuu, Wahenga Fc limehamishiwa uwanja wa Kinesi, Ubungo jijini Dar es Salaam.
Awali pambano hilo lilipangwa kufanyika kwenye uwanja wa TP Afrika, Sinza, lakini kutokana na mvua zinazoendelea jijini Dar zimeufanya uwanja huo kujaa maji na hivyo kutofaa kutuchezeka.
Mlezi na Msemaji wa Golden Bush, Onesmo Waziri 'Ticotico' alisema muda wa kuanza pambano hilo ni ule ule wa saa 10 jioni japo wamebadili uwanja.
"Napenda kutoa taarifa kwamba ile game yetu ya kesho imehamishiwa uwanja wa Kinesi, hii imetokana na hali ya mvua iliyoharibu kabisa uwanja wetu wa TP maarufu kama Nangwanda Sijaona. Game itaanza muda uleule wa saa kumi na nusu jioni.
Ticotico alisema kikosi chao kimejiandaa vya kutosha kuweza kula Pasaka vyema kwa kuilaza Wahenga Fc.





Twanga kusindikiza uzinduzi wa Miss Tabata 2013

Wanamuziki wa bendi ya Twanga Pepeta wakiwajibika jukwaani, kesho watazindua shindano la Miss Tabata 2013

UZINDUZI  wa shindano la kumtafuta Miss Tabata 2013 unafanyika kesho Da West Park, Tabata jijini Dar es Salaam.
Katika uzinduzi huo, jumla ya walimbwende 26 watambulishwa kwa mashabiki kwenye onyesho hilo ambalo litaenda sambamba na kusherekea sikukuu ya Pasaka.

Mratibu wa shindano hilo, Joseph Kapinga alisema jana kuwa warembo hao watatambulishwa pamoja na washiriki wa Miss Mzizima.

Kapinga aliwataja warembo wa Tabata watakaotambulishwa kuwa ni Martha Gewe (19), Zilpha Christopher (19), Hidaya David (22), Aneth Ndumbalo (19), Amina Ally (18), Dorice Mollel (22), Eunice Nkoha (19), Kazunde Kitereja (19),  Angela Fradius (19), Domina Soka (21), Rehema Kihinja (20), Glory Jigge (18) na Sophia Claud (21).

Aliwataja wengine ni Lilian Mpakani (19), Lilian Msanchu (19), Rita Frank (20), Pasilida Mandali (21), Rachel Mussa (19), Jasmin Damian (18), Angelina Mkinga (19), Mercy Mwakasungu (20), Tunu Hamis (19), Blath Chambia (23), Ray Issa (22), Shamim Abass (22) na Shan Abass (22).

Utambulisho wa warembo hao, utasindikizwa na burudani kabambe kutoka bendi ya Twanga Pepeta “Wazee wa Kisigino”.

Kapinga alisema wapenzi wa tasnia ya urembo Jijini Dar es Salaam, watapata fursa ya kuwaona warembo hao kabla ya shindano lenyewe litakalofanyika Mei mwaka huu.

Onyesho hilo limedhaminiwa na Konyagi, CXC Africa, Fredito Entertainment na Saluti5 na kuandaliwa na Bob Entertainment na Keen Arts.

Washindi watano kutoka Tabata watafuzu kushiriki Miss Ilala baadaye mwaka huu.

Anayeshikilia taji la Miss Tabata ni Noela Michael ambaye pia ni Miss Ilala.

Simba kutema ubingwa leo? Azam, Ruvu patachimbika Pwani


Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba

Azam watakaovaana na Ruvu Shooting mkoani Pwani
USHINDI wowote itakayopata  vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga  kwenye pambano lake dhidi ya Polisi Moro jioni ya leo na watani zao Simba kueteleza jijini Mwanza mbele ya Toto African itaipa Yanga nafasi ya kulishika taji la ubingwa kwa mkono mmoja ikisubiri kukabidhiwa rasmi mechi mbili zijazo.

Yanga itashuka dimba la Jamhuri kumenyana na wenyeji wao, ikiwa ina pointi 48 kibindoni, huku watani zao wanaoshikilia taji hilo kwa sasa wakiwa nafasi ya pili na pointi zao 34, sita nyuma ya wanaoshika nafasi ya pili Azam itakayokuwa dimba la Mabatini-Mlandizi, Pwani kuumana na wenyeji wao Ruvu Shooting.

Simba inahitajika kupata ushindi katika mechi yake ya leo itakayopigwa CCM Kirumba iwapo inahitaji kuendelea kutambulika kama bingwa mtetezi, kwani matokeo yoyote kinyume na ushindi itakuwa imelipema rasmi taji hilo na kuliachwa likigombewa na timu za Yanga na Azam.

Tayari kocha msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelu na baadhi ya wachezaji wa kikosi cha mabingwa hao wameapa kufa kiume leo Kirumba ili kufuta machungu ya kugaragazwa bao 1-0 na Kagera Sugar katika mechi yao iliyopita iliyochezwa siku ya Jumatano.

Julio alisema licha ya kuwakosa wachezaji wake kadhaa wakiwemo 'mapro', Mussa Mudde na Abel Dhaira na kuumia kwa Kiggy Makassy na Haruna Chanongo kuwa na hatihati ya kucheza leo, bado anaamini kikosi chake kitafanya vyema mbele ya Toto.

Hata hivyo kocha wa Toto, Athuman Bilal 'Bilo' alinukuliwa jana akisema kuwa wanaichukulia mechi yao ya leo kama fainali kwa kuhitaji pointi tatu muhimu ili wajinasue eneo la mkiani linalotishia kuirudisha timu yake kwenye Ligi Daraja la Kwanza.

Mechi nyingine za leo Azam watakuwa wakiendeleza harakati zao za kuifukizia Yanga kileleni kwa kuumana na Ruvu Shooting inayonolewa na kocha Charles Boniface Mkwasa.
Azam inahitaji ushindi ili kuweka hai matumaini ya kuweka rekodi ya kuwa bingwa wa Tanzania iwapo Yanga itateleza kileleni, licha ya kwamba imeachwa nyuma pointi 8 mpaka sasa.
Azam inaivaa Ruvu ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-0 iliyopata kwa Prisons Mbeya, na ikiwa inajiandaa kurudiana na Barracks YCII ya Liberia katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mtibwa Sugar imesafiri mpaka Kagera kwa ndugu zao Kagera Sugar wanaoendelea kuchekelea ushindi dhidi ya Simba juzi Jumatano, kila moja ikisaka ushindi na pointi tatu kuimarisha nafasi yake katika msimamo wa Ligi hiyo inayoelekea ukingoni kwa sasa.
JKT Ruvu waliozinduka katrika mechi yao ya mwisho kwa kuilaza Polisi Moro mabao 3-2 itakuwa ugenini uwanja wa Sheikh Amri Abeid Kaluta, jijini Arusha kuumana na wenyeji wao JKT Oljoro iliyo chini ya kocha Mbwana Makatta.
Pambano la mwisho kwa mujibu wa ratiba inayoonyesha kuwa Coastal Union wamesafiri kutoka Tanga kuja Dar kuumana na African Lyon katika pambano linalotarajiwa kuchezwa kwenye uwanja wa Chamazi, huku Mgambo Shooting watakuwa wakila shushushu kama ilivyo kwa Prisons ya Mbeya.
Je ni timu ipi italia au kucheza jioni ya leo? Bila shaka ni jambo la kusubiri kuona baada ya dakika za 90 za mapambano hayo.

Waliokufa tukio la kuporomoka jengo Dar wafikia 18

Mashuhuda wakiangalia jengo lililoporomoka jana asubuhi katika makutano ya Morogoro Road na Indira Gandhi jijini Dar es Salaam.

Watu wa Msalaba Mwekundi wakibeba moja ya majeruhi wa tukio hilo la jana
 
Rais Kikwete alipotembea eneo la tukio la jengo lililoporomoka wakati likiendelea kujengwa
WAKATI zoezi la uokozi kwenye tukio la ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa lililokuwa likijengwa mtaa wa Indra Ghandi, likiendelea taarifa ambazo zilizothibitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mecky Sadick zinasema kuwa miili ya watu 17 wakiwamo watoto wawili mpaka sasa imeshapatikana.Hata hivyo muda mfupi uliopita imeelezwa imeopolewa maiti nyingine na kufanya idadi sasa kufikia 18, huku taarifa ya awali ikisema miili ya watoto waliokolewa kwenye ajali hili iliyoacha majonzi kwa Watanzania wakijiandaa kuisherehekea sikukuu ya Pasaka ilikuwa wawili.
Mapema asubuhi Mkuu huyo wa mkoa alinukuliwa kwamba miili iliyopatikana mpaka usiku wa jana ni 15 ya watu wazima na miwili ya watoto na kwamba mmiliki wa jengo hilo na baadhi ya wakandarasi walikuwa wametiwa mbaroni kwa ajili ya kusaidia uchunguzi wa tukio hilo.
Mkuu wa Mkoa alisema kuwa bado juhudi zinafanywa kutafuta miili ya watu wengine ambapo idadi ya majeruhi waliokuwa wamenasuliwa kwenye mkasa huo walikuwa zaidi ya 20 mpaka mapema leo asubuhi.
Taarifa zaidi zitawajia japo inaelezwa ni vigumu kwa sasa kupatikana kwa mtu aliyehai katika kifusi kinachoendelea kufukuliwa kwa kushirikisha vikosi vya majeshi na wasamaria wema waliojitokeza tangu jengo hilo linalodaiwa la orofa 16 kuporomoka asubuhi ya jana wakati watu wakiendelea na ujenzi.

Albinus wa Namibia bingwa mpya wa Dunia






BONDIA  Albinus Felesianu wa Namibia leo ameudhihirishia ulimwengu kuwa yeye kweli ndiye Mfalme wa uzito wa unyoya duniani kwa vijana baada ya kumgalagaza bondia Herbert Quartey wa Ghana katika mpambano wao uliofanyika katika ukumbi wa Windhoek Country Club Resort  and Casino leo tarehe 29, March 2013.
Umati wa watu wasiopungua elfu 20 walijazana katika ukumbi huo wa burudani wakimshangilia kwa nderemo na vifijo bondia wao Albinus wakati alipokuwa anafanya vitu vyake kwenye ulingo.

Baada ya mtangazaji wa ulingo kutamka kuwa “Na sasa bingwa mpya wa uzito wa unyoya duniani kwa vijana ni Albinus Felesianu” mayowe ya wapenzi wa ngumi waliojazana katika ukumbi huo yaliweza kusikika kilometa tatu mpaka katikati ya jiji la Windhoek.

Hata hivyo, haikuwa kazi rahisi kwa Albinus kuunyakua mkanda wa ubingwa wa dunia kwa vijana kwani Mghana Herbert Quartey naye alikuwa mbogo kwani alirusha kila aina ya masumbwi yaliyomo kwenye kitabu.

Wawili hao walichapana makonde mazito kama watu wenye uzito mkubwa na kama sio uwezo na ujuzi wa referii Deon Dwarte wa Afrika ya Kusini kazi ingekuwa ngumu sana kwani kila bondia alijaribu kumpata mwenzake katika sehemu zinazoumiza ili kuumaliza mpambano mapema lakini ujuzi na ubishi wa kila mmoja ulifanya kusiweko na knockout yoyote!

Hii ni mara ya kwanza kwa nchi ya Namibia kuweza kuandaa mpambano wa ubingwa wa dunia wa IBF na wakali hao waliweza kuufanya umati wote uliohudhuria kulipuka kwa makelele ya kushangilia kila wakati.

Alikuweko Harry Simon, ambaye ndiye Mnamibia aliyeweza kuufanya mchezo wa ngumi kupendwa na kuwa maarufu sana nchini humu. Uwezo na utukutu wa Harry Simon ulingoni umeufanya mchezo wa ngumi kupendwa karibu na kila Mnamibia.

Walikuweko pia wageni wengine wengi lakini kampuni ya simu ya Telecom ambayo ndio waliokuwa wadhamini wa mpambano huo imejikusanya kila aina ya sifa na upendo kutoka kwa wananchi wa Namibia jinsi inavyo dhamini mchezo wa ngumi!

Mpambano huu uliandaliwa na Kinda Nangolo wa kampuni ya Kinda Boxing Promotions ambayo ndio waandaaji wa mpambano ujao wa mwezi wa Mei wa bingwa wa IBF Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati katika uzito wa unyoya bondia Gottlieb Ndokosho. Mpambano wa IBF wa Kimataifa wa bondia Harry Simon nao utafanyika mwezi wa Juni.

Aidha, Immanuel “Prince’ Naidjala”wa Namibia na Lesley Sekotswe wa Botswana watarudiana tena mwezi wa July kumpata bingwa wa kimataifa wa uzito wa bantam baada ya kutoka sare walipokitana wiki iliyopota nchini Namibia.