STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, February 10, 2014

Abdallah Juma aililia TFF, alia na Nkongo

Abdallah Juma enzi akiwa Simba
MSHAMBULIAJI nyota wa Mtibwa Sugar, Abdallah Juma ameliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwafuatilia kwa ukaribu marefa wanaochezesha Ligi Kuu ili kuepusha 'maafa' yanayoweza kutoka uwanjani kutokana na maamuzi yao mabovu na yenye upendeleo.
Pia ameliomba shirikisho hilo kuweka chini ya uangalizi uwanja wa Sokoine-Mbeya ambao kwa msimu huu umekuwa ukilalamikiwa na baadhi ya klabu kukithiri kwa vitendo vya hujuma kwa timu wageni.
Mshambuliaji huyo pekee mzawa aliyefunga hat-trick kati ya tatu zilizofungwa msimu huu, alisema waamuzi wamekuwa wakifanya maamuzi mabovu yanayowatia hasira wachezaji na mashabiki.
Mchezaji huyo alisema ni vyema TFF wakawa wanafuatilia waamuzi hasa kwenye mechi hizi za duru la pili ambalo klabu huwa zikitafuta nafasi za kuwania ubingwa na kuepuka kushuka daraja.
"Mimi huwa siyo mlalamishi kwa waamuzi, lakini tulichofanywa jana kwenye uwanja wa Sokoine kwa kunyimwa mabao mawili ya wazi moja nikilifunga mimi kwa shuti kali la mbali inaumiza," alisema.
Alisema mbaya alienda kumuuliza mwamuzi, Israel Nkongo sababu ya kulikataa bao lake lililokuwa la kusawazisha na kuishi kutupiwa maneno machafu na kejeli.
"Sidhani kama huyu mwamuzi anastahili kuendelea kuchezesha ligi kwa alichokifanya kwetu na hasa kwangu kwa kunitusi baada ya kwenda kumuuliza," alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba.
Strika huyo alisema mbali na TFF kuwafuatilia kwa makini waamuzi walioteuliwa kuchgeza mechi za lala salama za ligi hiyo, pia waumulike uwanja wa Sokoine kwa kukithiri vitendo vya uzalendo.
"Majuzi wenzetu wa Ruvu Shooting walifanyiwa vitendo kama hivyo, jana tumefanyiwa sisi na hata Yanga, Ashanti walishakuja hapa na kulalamika, ni vyema TFF wakaufuiatilia uwanja huu," alisema.
Juma alisema kunyamazia vitendo vya kizalendo siyo tu vinatrudisha nyuma soka, lakini pia vinahatarisha usalama na amani uwanjani kwa sababu zipi timu ambazo mashabiki wao siyo wavumilivu.
"Fikiria jana tu imetokea rasbha kubwa uwanjani baada ya mechi kwa kuharibiwa kwa viti sababu ya maamuzi ya upendeleo yaliyofanywa je kwa mashabiki wahuni hali inakuwaje," alihoji mchezaji huyo wa zamani wa AFC Arusha.
Mtibwa Sugar ilikuwa uwanja wa Sokoine kuumana na Mbeya City na kulazwa mabao 2-1, huku viongozi wake wakilalamika kunyimwa mabao mawili ya wazi na mwamuzi Nkongo ambaye MICHARAZO halikufanikiwa kumpata kujibu tuhuma alizotupiwa na Juma.

Full Maganga alitoa bao lake la Simba kwa mwanae

Full Maganga
MFUNGAJI wa bao pekee lililoiua Simba kwenye uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Full Maganga wa Mgambo JKT amesema bao hilo ni zawadi maalum kwa mwanae kipenzi, Jamilat (5).
Aidha amesema amejisikia faraja kubwa kuwatungua Simba kutokana na ukweli kwa muda mrefu alikuwa na ndoto za kuzifunga timu kubwa nchini na kuahidi bado zamu ya Yanga watakapoumana nao.
Akizungumza na MICHARAZO kwa njia ya simu mapema leo kutoka jijini Tanga, Maganga alisema bao alilofunga juzi wakati wakiizamisha Simba kwa bao 1-0 analitoa kwa mwanae huyo anayempenda kupita maelezo.
"Bao langu la jana ni zawadi maalum kwa mwanangu kipenzi, Jamilat mwenye miaka mitano, nilijiwekea ahadi kuwa ni lazima niwatungue Simba na Mungu amenisaidia nimefurahi sana," alisema.
Aliongeza kuwa, amekuwa na ndoto za muda mrefu kuwazifunga timu kubwa na bahati imekuwa kwake na kuahidi atafanya hivyo siku timu yao itakakapoumana na Yanga.
"Bado zamu ya Yanga, naamini Mungu atanijalia kutimiza hilo kama nilivyotimiza kwa Simba na furaha zaidi ni kwamba timu yangu imepata pointi tatu muhimu tulizokuwa tunazihitaji," alisema Maganga.
Mgambo ambayo pamoja na ushindi huo bado imesalia mkiani, iliiduwaza Simba kwa kuwalaza bao hilo lililofungwa na Maganga katika dakika 28 za kipindi cha kwanza.
Pamoja na Maganga kufunga bao hilo lililomnyima raha kocha wa Simba, Zdrakov Lugarusic, lakini kazi kubwa iliyofanywa na kipa wao Salehe Tendega aliyeokoa michomo hatari ya nyota wa Simba.
Mgambo JKT itasafiri hadi mjini Tabora kuvaana na Rhino Rangers mechi itakayochezwa Jumamosi ijayo.

Kocha Marsh asubiri vipimo vya mwisho kuanza matibabu

Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Sylvester Marsh (Pichani kushoto) ambaye amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) anasubiri vipimo vya mwisho ili aweze kuanza matibabu.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemtoa kocha huyo nyumbani kwake jijini Mwanza na kumleta Dar es Salaam kwa lengo la kuhakikisha anapata matibabu zaidi na kwa uangalizi wa karibu.
Tayari majibu ya kipimo cha kwanza yameshapatikana, hivyo yanasubiriwa majibu ya kipimo kingine ili aweze kuanza rasmi matibabu, lengo likiwa ni kubaini kitaalamu ugonjwa unaomsumbua.

Twiga Stars kuagwa Jumatano

TIMU ya Twiga Stars itaagwa rasmi Jumatano (Februari 12 mwaka huu) tayari kwa safari ya Lusaka, Zambia kwa ajili ya mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) ambayo fainali zake zitafanyika Oktoba mwaka huu nchini Namibia. Msafara wa timu hiyo itakayoondoka kwa ndege ya Fastjet utaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Ahmed Idd Mgoyi.

Hafla ya kuwaaga wachezaji wa timu hiyo itafanyika saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF. Timu hiyo itaondoka Februari 13 mwaka huu alfajiri tayari kwa mechi hiyo itakayochezeshwa na waamuzi kutoka Rwanda.

CCM yashukuru wananchi kuikataa CHADEMA chaguzi ndogo za udiwani

NAPE NNAUYE
DAR ES SALAAM, Tanzania
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimewashukuru Watanzania kwa kukiamini na kukipatia ushindi wa kishindo katika uchaguzi mdogo wa udiwani uliofanyika jana katika kata 27 na CCM kushinda kata 23. 
Akitoa shukrani hizo, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amesema leo kwamba siri ya CCM kuimwaga CHADEMA ni uadilifu katika kuwatumikia wananchi na kwamba, kushindwa kwa chama hicho ni ushahidi kwamba hakikubaliki na Watanzania wamewathibitishia kwamba hawajazoea vurugu.
Nape alisema CCM inaahidi kuendelea kuwatumikia Watanzania kwa amani na utulivu kwa kuwa ina uzoefu wa kufanya siasa kistaarabu na ndio siri ya kukubalika kwa wananchi.
Akizungumzia kushindwa kwa CHADEMA alisema wamehukumiwa kutokana na vurugu na kupiga watu kwenye kampeni za uchaguzi na ndio maana wametumia gharama kubwa na helkopta tatu na kuambulia kata tatu.
"CHADEMA wamevuna walichopanda Watanzania hawapenda vurugu, wamezoea amani na utulivu sasa wamewaadhibu kwa kuwanyima kura na huo ni ushahidi kwamba Watanzania hawakiamini," alisema.
Katika uchaguzi huo CCM ilishinda katika kata CCM ilishinda katika kata 23 za Kibindu na Magomeni (Pwani), Kiwalala na Namikage (Lindi), Ubwage (Shinyanga), Ibumu na  Nduli (Iringa), Kiomoni na Mtae (Tanga), Nyasura(Mara), Malindo, Santillya (Mbeya), Partimbo(Arusha, Mkwiti (Mtwara), Tungi na Ludewa (Morogoro) na Mrijo (Dodoma).

Rais Kikwete aifariji familia ya Marehemu Patrick Qorro

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiweka saini katika kitabu cha maombelezo ya msiba wa aliyekuwa Mbunge wa Karatu Waziri wa Kilimo na Ushirika Serikali ya awamu ya kwanza, Mhe. Patrick Qorro (72) aliyefariki  dunia usiku wa kuamkia Jumamosi baada ya kuugua kwa muda mfupi na kulazwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha Mifupa ( MOI)  jijini Dar es Salaam. 

Marehemu Qorro ambaye wakati wa Serikali ya awamu ya kwanza aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali, ikiwamo Waziri mdogo wa Kilimo na Ushirika na baadaye kuwa waziri kamili wakati wa awamu ya pili, alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kuvuja damu kwenye mzunguko wa kichwa kulikosababishwa na hitilafu ya figo.Kwa mujibu wa msemaji wa familia, Bw. James Bwana, Marehemu anatarajiwa kuagwa rasmi kesho kabla ya kusafirishwa Jumatano hadi Kijiji cha Mbulumbulu, wilayani Karatu, mkoani Arusha kwa ajili ya mazishi.Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimfariji mjane wa marehemu Dkt Martha Qorro na wanafamilia wengine nyumbani kwa  aliyekuwa Mbunge wa Karatu Waziri wa Kilimo na Ushirika Serikali ya awamu ya kwanza, Mhe. Patrick Qorro (72)  aliyefariki  dunia usiku wa kuamkia Jumamosi baada ya kuugua kwa muda mfupi na kulazwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha Mifupa ( MOI)  jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU

TFF yawafungia wachezaji watano JKT Kanembwa


KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imewafungia mechi tatu wachezaji watano kati ya tisa wa timu ya Kanembwa JKT waliolalamikiwa na Sekretarieti kwa kumpiga mwamuzi kwenye mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) iliyochezwa Novemba 2 mwaka jana.
Wachezaji hao ni Bariki Abdul, Mrisho Musa, Nkuba Clement, Nteze Raymond na Philo Ndonde. Wachezaji ambao hawakutiwa hatiani kutokana na ushahidi dhidi yao kutojitosheleza ni Abdallah Mgonja, Mbeke Mbeke, Ntilakigwa Hussein na Uhuru Mwambungu.
Mechi hiyo dhidi ya Stand United iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga ilivunjwa na refa Peter Mujaya dakika ya 87 kutokana na kupigwa na wachezaji hao baada ya kuamuru ipigwe penalti dhidi ya timu yao.
Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Ibara ya 49 (1)(b) ya Kanuni za Nidhamu za TFF baada ya kupitia vielelezo vilivyowasilishwa na Sekretarieti ya TFF ambavyo ni ripoti ya refa, ripoti ya kamishna wa mechi hiyo na video iliyoonesha tukio hilo.
Pia kabla ya kutoa adhabu baada ya kusikiliza utetezi kutoka kwa walalamikiwa ambao ni wachezaji hao na timu yenyewe ya Kanembwa JKT. Nayo Kanembwa JKT imetiwa hatiani na kupigwa faini ya sh. milioni ambayo inatakiwa kuilipa kabla ya kucheza mechi inayofuata.
Kamati hiyo iliyokutana jana (Februari 9 mwaka huu) chini ya Mwenyekiti wake Tarimba Abbas, kwanza imelaani kitendo cha wachezaji wa timu hiyo kumzonga refa, kwani vitendo vya aina hiyo ndiyo vichocheo vya vurugu viwanjani.
Lakini pia imempongeza nahodha wa Kanembwa JKT, Mbeke Mbeke kwa kuwa mstari wa mbele kuwazuia wachezaji wenzake waliokuwa wakimpiga refa wa mchezo huo.
Vilevile Kamati hiyo imesema aliyesababisha matatizo hayo ni refa Mujaya, na ingawa ilikuwa na uwezo wa kumchukulia hatua lakini haikufanya hivyo kwa vile hakukuwa na mlalamikaji na tayari Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilishamwadhibu.
Wakati huo huo: Vyama vya Mpira wa Miguu vya mikoa vimetakiwa kuwasilisha majina ya mabingwa wao kufikia Machi 30 mwaka huu kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL).
Timu zote zitakazofuzu kucheza RCL zinaruhusiwa kusajili wachezaji wapya wasiozidi watano kutoka ndani ya mkoa kwa kufanya taratibu za uhamisho. Kamati imesisitiza kuwa usajili wa RCL ni uleule uliotumika kwenye Ligi ya Mkoa.
Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana Februari 6 mwaka huu imekataa ombi la Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) kuongeza timu za Ligi ya Mkoa kutoka 20 hadi 24.
Ikiwa chini ya Mwenyekiti wake Geofrey Nyange, Kamati hiyo imesema kwa mujibu wa Kanuni ya Ligi ya Mkoa, ligi hiyo inatakiwa kuwa na timu kati ya 16 na 20, hivyo vyama vya mpira wa miguu vya mikoa vinatakiwa kuendesha ligi kwa kufuata kanuni.
Kamati hiyo imeongeza kuwa hata kama ingekubalia ombi la MZFA kiutaratibu lisingewezekana kwa vile kanuni hufanyiwa marekebisho baada ya msimu kumalizika, wakati ombi hilo limewasilishwa katikati ya msimu.

KWA HUDUMA ZA MAFOTO EBU CHEKI HAPA

MAFOTO PRODUCTION & ENTERTINMENT KWA MAHITAJI YAKO YA STILL PICTURE, VIDEO SHOOTING, MUSIC & Mc's KATIKA SHEREHE YA AINA YEYOTE. 

KAZI NYINGINEZO:- VIDEO EDDITING, COVER DISGNING, PPS ZA DK 3, POSTERS ZA AINA MBALIMBALI COVER CD PRINTING, BURNING CD N.K. WASILIANA NASI KWA NO, 0787 200005/0754, 0655-306109/0714 656660 

BARUA PEPE:- muhidinuk@yahoo.co.uk,sufianimafotoblog@gmail.com AMA TEMBELEA www.sufianimafoto.com

OFISI ZETU ZIPO KIJITONYAMA NYUMA YA KITUO CHA POLISI MABATINI, BARABARA YA SPIKA WA BUNGE

Barcelona yarejea kileleni, Messi moto mkali

At the double: Messi (left) scored twice to help Barcelona to a 3-1 win against Sevilla
Messi akishangilia moja ya mabao yake na Pedro
NYOTA wa Argentina, Lionel Messi anayichezea Barcelona jana alidhihirisha bado ni moto wa kuotea mbali baada ya kuisaidia klabu yake kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 ugenini dhidi ya Sevilla.
Messi aliifungia Barca magoli mawili moja la kila kipindi huku bao la mapema la Alex Sanchez na lingine la jioni la Cesc Fabregas yalitosha kuirejesha mabingwa hao watetezi kileleni mwa msimamo waking'oa Real Madrid na Atletico Madrid waliokuwa juu yao.
Barcelona wamerejea kileleni wakiwazidi wapinzani wao uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa, licha ya zote kulingana pointi 57.
Wenyeji ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Moreno katika dakika ya 15 kabla ya Sanchez kusawazisha dakika ya 34 na baadaye Messi kufunga bao la pili dakika ya 44.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Messi kuongeza bao la tatu katioka dakika ya 55 kabla ya Fabregas kuhitimisha ushindi huo mnono kwa bao la dakika ya 87.

Sunday, February 9, 2014

Manchester Utd yazidi kuchechemea yabanwa nyumbani na Fulham

Darren Bent scores Fulham's equaliser
Darren Bent akiisawazishia Fulham bao dakika za lala salama
BAO la dakika ya 94 lililofungwa na Darren Bent liliiokoa Fulham dhidi ya kipigo toka kwa Mashetani Wekundu, Manchester United waliokuwa nyumbani kwao na kutoka sare ya 2-2.
Manchester United walioonekana kama wamevuna pointo zote tatu baada ya Robin van Persie na Michael Carrick kufunga mabao mawili na kuinyamazisha Fulham waliotangulia kupata bao la mapema la dakika 19 lililofngwa na Steve Sidwell.
Juan Mata alimtengenezea nafasi nzuri van Persie aliyefunga bao la kusawazisha dakika ya  78 kabla ya Carrick kuongeza la pili dakika mbili baadaye.
Hata hivyo mashabiki wa Old Trafford wakiamini wapata ushindi nyumbani, Bent alifunga bao la kusawazisha dakika nne za nyongeza za mchezo huo na kuipa pointi moja Fulham ugenini.
Matokeo hayo yameendelea kuiacha Manchester ambayo Jumatano itaifuata Arsenal iliyonyukwa jana na Liverpool kwa mabao 5-1, ikibaki nafasi ya saba ikiwa na pointi 41.

KMKM yawa Urojo Ethiopia kama Chuoni Zimbabwe

KMKM ya Zanzibar
KLABU za Zanzibar zimeendelea kuwa urojo baada ya jioni hii KMKM kutandikwa mabao 3-0 na Dedebit ya Ethiopia katika Ligi ya Mabingwa Afrika kama ilivyokuwa 'ndugu' Chuoni nchini Zimbabwe jana kwenye Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji wao How Mine.
Kwa mujibu wa matokeo kutoka Addis Ababa, wenyeji walipata mabao yao katika vipindi vyote viwili, hadi mapumziko waliongoza kwa bao 1-0 lililoifungwa na Dawit Fekadu dakika ya 16.
Kipindi cha pili kilikuwa kigumu kwa KMKM baada ya kuongezwa mabao mengine mawili yaliyofungwa na Shimekit Gugsa dakika ya 52 kabla ya Micahel George kumalizia kazi dakika sita kabla ya pambano hilo kuisha.
Kwa matokeo hayo klabu za Zenji zimeendelea kuwa wasindikizaji katika michuano ya kimataifa kwani KMKM italazimika kupata ushindi wa mabao 4-0 ili kusonga mbele, kazi ambayo pia inayo Chuoni iliyopigwa 4-0 na How Mine ya Zimbabwe jana na kuonekana ni ndoto kushinda nyumbani 5-0.

Adebayor aipaisha Spurs, waishusha Everton

Emmanuel Adebayor
Adebayor akipongezwa na Paulinho baada ya kufunga bao pekee dhidi ya Everton

Tottenham 1-0 EvertonMSHAMBULIAJI kutoka Togo Emmanuel Adebayor jioni hii ameiwezesha Tottenham Hotspur baada ya kufunga bao pekee lililoiwezesha kuizima Everton na kurejea kwenye nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu ya England.
Adebayor alifunga bao hilo lililokuwa la tano kwake msimu huu kwenye ligi hiyo katika dakika ya 65 akimalizia kazi nzuri ya Kyle Walker na kumtungua Tim Howard na kuifanya Spurs kufikisha pointi 47 na kuwa nyuma ya Liverpool yenye pointi 50.
Everton waliokuwa wakishika nafasi ya tano kabla ya mchezo huo, imeshuka hadi nafasi ya sita ikisaliwa na pointi zake 44.
Muda mchache ujao, Manchester United wanaokamata nafasi ya saba watakuwa uwanja wake wa nyumbani wa Old Trafford kupepetana na Fulham katika pambano jingine la ligi hiyo.

Azam yatamba Afrika, yawapiga Wamakonde kidude

AZAM FC imepata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Ferroviario de Beira ya Msumbiji katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali Kombe la Shirikisho Afrika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam jioni hii.
Shukrani kwake mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 41 baada ya kutengewa pasi nzuri ya kichwa na Mganda Brian Umony na kufumua shuti kali.
Mchezo ulikuwa mkali dakika zote 90 na mashambulizi yalikuwa ya pande zote mbili.
Wachezaji wa Azam wakimpongeza Kipre Tchetche leo Chamazi

Mshambuliaji wa Ivory Coast, Kipre Tchetche na Mganda Umony kwa pamoja na Mzanzibari Khamis Mcha ‘Vialli’ walikuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Ferroviario.  
Kipindi cha pili, Ferroviario walicharuka zaidi na Azam nao walipoteza nafasi kama tatu za kufunga mabao mwanzoni. 
Refa Mutaz Abdelbasit Khairalla na wasaidizi wake Waleed Ahmed Ali na Aarif Hassan Eltom wote kutoka Sudan walionekana kabisa kuwapendelea wageni katika maamuzi yao. 
Dakika ya 70 beki mmoja wa Ferroviario aliunawa mpira wazi wazi kwenye eneo la hatari kufuatia shuti la Kipre Tchetche mbele ya refa, lakini akapeta. 
Kiungo mkabaji wa Ferroviario, de Beira akipiga tik tak dhidi ya mshambuliaji wa Azam FC, Brian Umony leo Chamazi
Kipre Tchetche akimtoka beki wa kushoto wa Ferroviario, Emidio Matsinhe leo

Matokeo hayo yanamaanisha Azam itakuwa na kazi ngumu katika mchezo wa marudiano wiki mbili zijazo nchini Msumbiji, wakitakiwa kulazimisha sare ili kusonga mbele.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ali, Erasto Nyoni, Malika Ndeule, Aggrey Morris, Said Mourad, Kipre Balou, Salum Abubakar, Himid Mao, Khamis Mcha/John Bocco dk61, Kipre Tchetche na Brian Umony/Jabir Aziz dk81.
Ferroviarrio; William Manyatera, Zefanis Matsinhe, Emidio Matsinhe, Abrao Cura/Kiki Simao, Edson Morais, Reinildo Mandava, Valter Mandava/Hery Antony, Antonio Machava, Manuel Fernandes, Mario Sinamunda na Manuel Correia/Dje Buzana.

BIN ZUBEIRY

Simba ya Logarusic yafa Tanga, Mbeya yainyuka Mtibwa, Coastal yatamba Tabora, Oljoro yanabwa na Kagera

Mgambo JKT
Mbeya City
Coastal Union iliyoshinda ugenini mjini Tabora dhidi ya Rhino Rangers
Mtibwa Sugar iliyokufa jijini Mbeya kwa mabao 2-1
BAO pekee la dakika ya 28 lililofungwa na Full Maganga limetosha kuiua 'Mnyama' Simba inayonolewa na kocha mwenye mbwembwe, Zdravko Logarusic mbele ya Mgambo JKT katika pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara lililochezwa Mkwakwani Tanga.
Simba ambayo iliitafuna Mgambo iliyokuwa ikifundishwa na King Abdallah Kibadeni kwa mabao 6-0 licha ya juhudi za kutaka kurejesha bao hilo ilishindwa kabisa kuwapa raha mashabiki wake kwa kukubali kipigo cha pili kwa msimu huu na cha kwanza chini ya Logarusic tena kwa timu kibonde ya Mgambo.
Huo ni ushindi wa pili mfululizo kwa Mgambo JKT ambayo ilikuwa ikiburuza mkia kwa kipindi kirefu baada ya wiki iliyopita kuicharaza Ashanti United uwanja wa cha Chamazi.
Ushindi huo umeifanya timu hiyo inayonolewa na kocha mpya Bakar Shime imefikisha pointi 12 huku Simba ikisaliwa na 31 na kushuka nafasi ya nne iliyokuwa awali baada ya Mbeya City kushinda mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar mjini Mbeya.
Bao la Mtibwa lilifungwa na Jamal Mnyate kabla ya Mbeya kurudisha bao kupitia na Peter Mapunda kwa kichwa na bao la ushindi  lilifungwa na Amani Kibokile. Dakika mbili kabla ya kumalizika mchezo Mtibwa ilipata bao la kusawazisha ambalo hata hivyo lilikataliwa na mwamuzi Israel Mkongo.
Mechi nyingine zimeshuhudia Coastal Union ikipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji wao Rhino Rangers ya Tabora kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, huku Oljoro JKT ilibanwa nyumbani na Kagera Sugar na kutoka nao sare ya 1-1.

DAVID NAFTALI: Kiungo anayetaka viongozi wa soka kuacha mambo ya mwaka '47




David Naftali katia picha tofauti akiwa nchini Kenya
WAKATI wachezaji wenzake wanaocheza nje ya nchi wakirejea nyumbani, kiungo mkabaji David Naftal anasema hana mpango huo kwa sababu havutiwi na mfumo wa soka uliopo nchini.
Nyota huyo wa zamani wa timu za AFC ya Arusha na Simba anayeichezea Bandari ya Mombasa inayoshiriki ligi kuu ya Kenya anasema mfumo wa soka nchini hauthamini na kuwajali wachezaji kama ilivyo Kenya.
Anasema tangu atue nchini humo miaka mitatu iliyopita, hajawahi kusikia viongozi wa klabu wakiwatuhumu wachezaji kuzihujumu timu zao au kuuza mechi kama ilivyozoeleka hapa, hasa kwa Simba na Yanga.
"Huku matokeo ya aina yoyote yanachukuliwa sehemu ya mchezo," anasema. "Tanzania timu ikifungwa tu anatafutwa mchawi na watu wa kwanza huwa wachezaji bila kujali wanavyovuja jasho uwanjani kupigania timu."
Anasema vitendo vya kuwatuhumu wachezaji ni mambo ya kizamani yanayowavunjia heshima na kuwakatisha tamaa.
Naftal anayemudu nafasi nyingi uwanjani, anasema lazima viongozi wa soka wa Tanzania wabadilike na kutambua mchezo huo una matokeo matatu: kushinda, kufungwa na sare. Aidha, anasema, wasiamini timu zao ni bora kiasi cha kutofungika.
Mkali huyo anayefurahia kucheza Kenya na kuaminiwa na klabu yake ya Bandari, anasema kuwapo kwake nchini humo kumemfundisha mambo mengi ikiwamo tofauti iliyopo baina ya soka la Tanzania na nchi hiyo jirani.
Anasema Tanzania ina wachezaji wengi wenye vipaji lakini wasimamizi wa soka wamejisahau na kuelekeza  macho mijini. Pia anadai mfumo wa soka wa Kenya na Tanzania kwa ngazi za klabu umetofautiana sana, Kenya klabu zikiendeshwa 'kisomi' kulinganisha na Tanzania licha ya kwamba mchezo huo unaingiza fedha nyingi zaidi nchini.
"Kenya klabu zake zipo kiprofesheno zaidi kulinganisha na Tanzania, ila kifedha Tanzania ipo juu ndiyo maana wachezaji wa kigeni wanamininika huko."
Naftal anasema ndoto zake ni kuzidi kusonga mbele na ndiyo maana hana mpango wa kurudi nyumbani.
Anasema kwa sasa anafanyiwa mipango na wakala wake kwa ajili ya kwenda kucheza nchini Afrika Kusini wakati mkataba wake ukielekea kugota ukingoni Septemba.
Naftal ambaye ni shabiki mkubwa wa klabu ya Manchester United lakini anayemzimia kiungo Yaya Toure wa Manchester City, na ambaye wakati akiwa Simba alianza kucheza kama mshambuliaji, anasema anafurahishwa na changamoto zinazotolewa na klabu za Mbeya City na Azam katika ligi kuu ya Bara kwa sababu "itasaidia kuvunja ligi ya timu mbili za Simba na Yanga."
Anasema kuibuka kwa Mbeya City ni dalili za wazi kwamba mikoani kuna wachezaji wenye vipaji na kama kutakuwa na wawekezaji wanaweza kuleta mapinduzi katika soka la Tanzania.
"Ni lazima TFF na serikali kutupia macho soka la mikoani, kule ndiko kunakoweza kupatikana akina Samuel Et'oo na Didier Drogba wa Tanzania,Mbeya City ni mfano halisi."
" anasema.
NIPASHE JUMAPILI

Simba, Mbeya City kuombeana mabaya leo VPL?

Mbeya City
Simba
LICHA ya kwamba zitakuwa kwenye viwanja tofauti, lakini timu za Simba na Mbeya City zitakuwa zikiombeana mabaya watakapokuwa wakiumana kuwania pointi tatu ili kujiweka pazuri kwenye msimamo.
Simba watakuwa ugenini kuuamana na Mgambo JKT, wakati Mbeya itakuwa nyumbani uwanja wa Sokoine kuumana na Mtibwa Sugar.
Mechi hizo mbili kati ya nne zinazochezwa leo zinafuatiliwa kwa karibu kutokana na timu hizo kulingana pointi na zikifukuzana kwenye msimamo unaoongozwa na Azam ambayo leo itakuwa na majukumu ya kimataifa katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Ferroviario de Beira ya Msumbiji.
Timu hizo zina pointi 31 kila mmoja na zinatofautiana uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa na kila mmoja watakuwa wakiwaombea wenzao wateleze ili kukalia nafasi ya tatu na kuwasogelea Yanga waliopo nafasi ya pili na pointi zao 35.
Kocha msaidizi wa Simba Seleman Matola amesema timu yake imepania kupata ushindi katika mchezo wa leo wa ligi kuu ya soka ya Bara dhidi ya Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani, hasa baada ya kupata sare kwenye mechi iliyopita dhidi ya Mtibwa Sugar.
"Ile sare ilimuuma kila mtu kuanzia wachezaji mpaka benchi la ufundi," alisema Matola.
Aidha, alisema kuwa hakuna majeruhi kwenye kikosi chake na kila mchezaji amepewa majukumu kuhakikisha wanapata pointi tatu. Mgambo inashika mkia katika msimamo wa ligi kuu ikiwa imeshinda mara mbili katika michezo 16 mpaka sasa.
Matola alisema kupoteza mchezo au kutoka sare wakati wapinzani wao wakipata ushindi kutawaweka katika mazingira magumu.
"Mbio za ubingwa ni ngumu hivyo hatutakiwi kupoteza mchezo sasa hivi... tunajua Mgambo wanacheza mpira wa nguvu lakini tumejiandaa kuwakabili."
Mbeya wenyewe watrakuwa na kibarua kigumu kwa Mtibwa Sugar na kocha wake, JUma Mwambusi amenukuliwa akisema wamejiandaa kushinda nyumbani baada ya kuteleza ugenini mvele ta Yanga.
Mbeya City, 'ilitenguliwa udhu' na Yanga kwa kufungwa kwa mara ya kwanza kwenye ligi hiyo iliyoipanda msimu huu baada ya kunyukwa bao 1-0 kwenye uwanja wa Taifa wiki iliyopita na kutibua rekodi yao waliyokuwa wanachuana na Azam ambayo ndiyo pekee sasa haijapoteza mchezo wowote katika ligi hiyo.
Mbali na mechi hizo mbili zinzofuatiliwa, leo pia kutakuwa ni michezo mingine miwili Oljoro JKT kuikaribisha Kagera Sugar uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha na Rhino Rangers kuikaribisha Coastal Union mjini Tabora katika pambano litakalochezwa uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

MASHINDANO YA NGUMI YA NELSONI MANDELA OPEN CHAMPIONSHIP YAMALIZIKA KAWE

Bondia Rudia Mashala kushoto akioneshana umwamba wa kutupiana makonde na Ratifa Khalidi wakati wa mashindano ya Nelson Mandela Open Champion Ship yaliyo malizika katika viwanja vya Kawe Dar es salaam Ratifa alishinda kwa point Picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com

Bondia Ezira Paur wa Kigoma akipambana na Hafidhi Kassimu wa Ngome wakati wa mashindano ya Nelson Mandela Open CHampion Ship yaliyomalizika kawe Dar es salaam Paur alishinda kwa point Picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com

Baadhi ya watu waliofulika kuangalia michuano hiyo

Meya wa Kinondoni akizungumza wakati wa kufunga mashindano hayo

Mjumbe wa maendeleo ya wanawake katika mchezo wa masumbwi nchini Aisha Vonialis katikati akiwa na mabondia wa kike waliopigana na kunyakuwa zawadi mbalimbali

Meya wa Manspaa ya Kinondoni Yussuph Mwenda akimkabizi  Mwenyekiti wa timu ya Mkoa wa Kigoma  Eddie Kikwesha  baada ya kuibuka timu yenye Nidhamu katika mchezo wa masumbwi katikati ni Mjumbe wa maendeleo ya wanawake katika mchezo wa masumbwi nchini Aisha Vonialis

Katika picha ya pamoja
Rais wa Shilikisho la ngumi za Ridhaa Nchini BFT Mutta Rwakatare akimzawadia kocha wa timu ya kawe baada ya kuibuka washindi wa tatu katika mashindano hayo

Real Madrid bila Ronaldo yaua nyumbani, Gale atupia moja na kusaidia jingine

Gareth Bale akifunga bao la kwanza la Madrid ikiwa nyumbani jana
BILA ya nyota wake Cristiano Ronaldo anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu, Real Madrid usiku wa kuamkia leo wamezidi kujiimarisha kileleni kwa La Liga baada ya kuishindilia Villareal kwa mabao 4-2.
Pambano hilo lililochezwa kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu, wenyeji Madrid walianza mapema kuonyesha dhamira yao ya kupata ushindi kwa kuandika bao la kwanza lililofungwa na Gareth Bale katika dakikia ya 7 tu ya mchezo.
Mfaransa Karim Benzema aliiongezea Madrid bao la pili dakika ya 25 akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Bale na dakika mbili kabla ya mapumziko, Mario aliifungia wageni bao la kufutia machozi.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kushambuliana na kufanya mabadiliko kadhaa yaliyozisaidia timu hizo, japo wenyeji walinufaika zaidi kwa kuongeza mabao mengine mawili yaliyofungwa na Jesé Rodríguez dakika ya 64 baada ya kazi nzuri ya Angel di Maria na Benzema kuongeza jingine dakika ya 76 japo wageni alitangulia kupata bao lao la pili la kufutia machozi lililowekwa kimiani na Giovan dos Santos dakika ya 69.
Ushindi huo umeifanya Madrid kufikisha pointi 57 sawa na Atletico Madrid ambayo yenyewe iulinyukwa ugenini mabapo 2-0 na Almeria na kumpoteza kipa wake aliyeoonyeshwa kadi nyekundu.
Katika mechi nyingine za ligi juzi Espanyol ilishinda bao 1-0 nyubani dhidi ya Granada huku Valencia jana iliishindilia bila huruma Real Betis kwa mabao 5-0 na Rayo Vallecano kuichapa Malaga mabao 4-1.
Leo kutakuwa na mechi nyingine kadhaa ya ligi hiyo ambapo Osasuna itaumana na Getafe, Real Valladolid kuvaana na Elche, huku Real Sociedad itaonyeshana kazi na Levante, Sevilla itaikaribisha mabingwa watetezi Barcelona na keshokutwa Celta Vigo itaialika Athletic Club nyumbani kwake.

AC Milan Mwaka wa Majanga, Napoli yainyoa 3-1

Adel Taarabt akiifungia Milan bao la mapema
MWAKA wa tabu umeendelea kuiandama timu ya AC Milan baada ya usiku wa kuamkia leo kupokea kipigo cha mabao 3-1 ikiwa ugenini dhidi ya Napoli na kuzidi kuiweka pabaya mabingwa hao wa zamani wa Ulaya.
Milan ambayo kwa sasa inanolewa na kocha Clerence Seedorf, imekuwa na mwenendo wa kusuasua katika Ligi Kuu ya Italia (Seria A) ndani ya msimu huu ambapo kwa kipigo cha jana kiliwaacha kwenye nafasi yao ya 10 ikiwa na pointi 29 ambapo ni 30 nyuma ya vinara wa ligi hiyo, Juventus wenye pointi 59 na mchezo mmoja mkononi.
Wageni ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 8 lililofungwa na mchezaji mpya aliyesajiliwa toka Fulham ya  Uingereza, Adel Taarabt kabla ya  Gökhan  İnler kuisawazishia Napoli dakika tatu baadaye akimalizia kazi nzuri ya Jorginho.
Matokeo hayo yalisalia hadi timu hizo zilipoenda mapumziko kabla ya wenyeji kuanza kwa kasi kipindi cha pili na kujipatia bao la pili lililowekwa kimiani na Muargentina, Gonzalo Higuain dakika ya 56 akimaliza kazi ya Inler.
Higuain aliihakikishia Napoli ushindi mnono nyumbani kwa kuifungia bao la tatu dakika ya  82 akimalizia pasi ya José Callejón.
Matokeo hayo ameifanya Napoli kujikita katika nafasi ya tatu mbele ya Fiorentina kwa kufikisha pointi 47.
Fiorentina imefikisha pointi 44 baada ya mapema jana kupata ushindi wa mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Atalant, huku Udinese ikishinda pia nyumbani kwa kuilaza Chievo mabao 3-0.
Ligi hiyo itaendelea tena leo kwa michezpo kadhaa Torino  itaumana na Bologna,    Sampdoria itapepena na Cagliari, Parma itaialika Catania, Livorno itaumana na Genoa,
Hellas Verona itakwaruzana na vinara wa ligi hiyo Juventus, Lazio itaikaribisha Roma na Inter Milan itaumana na Sassuolo.