STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, January 18, 2013

RAIS ZUMA AWAPA UBINGWA BAFANA BAFANA

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma akionyesha ufundi wa kuchezea mpira wakati alipoitembelea timu ya taifa ya nchi hiyo, Bafana Bafana, kwenye Uwanja wa Orlando mjini Soweto, Afrika Kusini Januari 15, 2013.
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma akipozi na wachezaji wakati alipoitembelea timu ya taifa ya nchi hiyo, Bafana Bafana, kwenye Uwanja wa Orlando mjini Soweto, Afrika Kusini Januari 15, 2013.

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma akizungumzana wachezaji wakati alipoitembelea timu ya taifa ya nchi hiyo, Bafana Bafana, kwenye Uwanja wa Orlando mjini Soweto, Afrika Kusini Januari 15, 2013.

Kama Dinho vile... Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma akionyesha ufundi wa kuchezea mpira wakati alipoitembelea timu ya taifa ya nchi hio, Bafana Bafana, kwenye Uwanja wa Orlando mjini Soweto, Afrika Kusini Januari 15, 2013.

RAIS wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amesema anajiamini kwamba wenyeji watazima shutuma wanazoelekezewa na kubakisha nchini humo kombe la Mataifa ya Afrika 2013 kama walipolitwaa mara pekee mwaka 1996 wakati michuano ilipofanyika nchini humo.
nchini humu," alisema Rais Zuma. 
"Nilikuwa nawaeleza wachezaji kwamba (wale) wanaoshutumu hawajawahi hata kuugusa mpira. Hawaujui 'ladha' yake. 

"Tumeridhika kwamba timu imeandaliwa vyema kwa ajili ya michuano hii. 

"Ni lazima watulie, wasiwe katika presha, hawapaswi kusikiliza shutuma hizi. Ni lazima waweke akili katika kile walichojiandaa kukikafanya na watakifanya. 

"Najiamini sana wakati huu kuliko wakati mwingine wowote kwamba tutawaonyesha watu kuwa sisi ndiyo Wasauzi. 

"Nimewaambia wachezaji 'nataka kulishika kombe', na kuligusa inamaanisha kwamba tubaki nalo hapo. Na watalitwaa. Hatupaswi kuhofia chochote."

AZAM WATUA SALAMA KENYA KUCHEZA KUCHEZA MECHI KESHO

Kikosi cha Azam kilipokuwa kikishangilia taji lao la Mapinduzi iliyotwaa wiki iliyopita visiwani Zanzibar kwa kuilaza Tusker ya Kenya katika mechi ya fainali.
KIKOSI cha timu ya Azam kimetua salama jijini Nairobi jana na kesho wanatarajiwa kushuka dimbani kuumana na AFC Leopard kabla ya Jumapili kuivaa Sofapaka kisha kumalizia mechi yao ya tatu dhidi ya KCB.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtandao wa klabu hiyo ukimnukuu kocha wao mkuu, Stewart John Hall, mechi zote hizo zitachezwa kwenye uwanja wa Nyayo ambapo leo walitarajiwa kuanza mazoezi katika uwanja huo kwa ajili ya mechi hizo za kujiandaa na mechi za duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara itakayoanza Januari 26.
“Tutacheza michezo mitatu, michezo yetu itahusisha timu zenye viwango vizuri katika ligi ya Kenya ambazo ni A.F.C Leopard, Sofapaka na K.C.B, mechi hizo zitasaidia kuimarisha timu yangu” alisema Stewart.
Kocha Stewart alisema watafanya mazoezi na kucheza mechi katika viwanja aina mbili vyenye nyasi za kawaida na zenye nyasi bandia kwa kuwa katika michezo ya ligi viwanja hivyo vinaendana na mazingira ya Tanzania.
Azam FC itamaliza safari yake ya maandalizi na mechi za kirafiki siku ya Jumanne kwa kuvaana naK.C.B kwenye Uwanja wa City mchezo ambao utakamilisha safari hiyo ya siku saba.
Wachezaji walioko jijini ni Mwadini Ally, Aishi Manula, Jackson Wandwi, Himid Mao, Samih Haji Nuhu, David Mwantika, Luckson Kakolaki, Jockins Atudo, Michael Bolou, Humphrey Mieno, Khamis Mcha, Gaudence Mwaikimba, Uhuru Selemani, Brain Umony, Malika Ndeule, Omary Mtaki, Abdi Kassim ‘Babi’, Abdalah Seif, Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
Father alisema kuwa mechi yao ya awali itakuwa dhidi ya Sofapaka itakayochezwa kesho kwenye dimba la Nyayo, kabla ya kucheza mechi nyingine baadae japokuwa watawakosa Gor Mahia waliokuwa wamepania kucheza nao.

Zahoro Pazi aanza kujaribiwa Bondeni, akiri kazi nzito

Zahoro Pazi (kulia) hapa akiwa mazoezi ya Azam


MSHAMBULIAJI wa Azam aliyekuwa amesajiliwa kwa mkopo na JKT Ruvu, Zahoro Pazi aliyepo nchini Afrika Kusini kuwania kucheza soka la kulipwa ameanza majaribio yake katika klabu ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini, Bloemfotein Celtic.
Akizungumza na MICHARAZO jana usiku kutoka Afrika Kusini, Pazi alisema majaribio yake yalianza juzi katika uwanja wa klabu hiyo wa Seisa Ramabodu, uliopo mji wa Bloemfotein.
Pazi alisema mazoezi yake kwa siku ya kwanza yalikuwa ni ya mwili tu kwa ajili ya kuangaliwa stamina na pumzi na anashukuru aliyafanya mwanzo mwisho licha ya kwamba yalikuwa magumu kwake.
"Kaka nimeanza leo matizi hapa Bloemfotein but nimekutana na physic si mchezo ila nimekomaa hadi mwisho maana nilishatiwa upepo na Kilinda (kocha wa JKT Ruvu- Charles Kilinda)  hatujasuga mpira kabisa kwa leo," alisema Pazi.
Pazi aliongeza kuwa alitarajiwa kuendelea na majaribio yake leo na kuendelea kwa siku 10 kabla ya kurejea nchini kusubiri majibu yake iwapo amefuzu au la.
Mchezaji huyo aliyewahi kujaribiwa na klabu za Kaiserlauten ya Ujerumani na Nadi ya Oman, alisema anamuomba Mungu amsaidie kufuzu majaribio yake ili aweze kutimiza ndoto zake za kucheza soka la kulipwa aliloliota kwa muda mrefu.
Pazi, mtoto wa kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Idd Pazi 'Father' aliivutia klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini iliyopo nafasi ya saba katika ligi hiyo iliyosimama kupisha Michuano ya Afrika, alipokuwa DR Congo na timu yake ya Azam.
Kabla ya hapo klabu hiyo ilimuona kinda huyo katika michuano ya Kombe la Kagame iliyokuwa ikichezwa nchini na kurushwa na kituo cha Supersport cha Afrika Kusini.

WAGOMBEA ZAIDI WAJITOKEZA TFF, PAZIA KUFUNGWA LEO



WAKATI leo ndiyo mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu za kuwania uongozi kwenye uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) waombaji 36 walikuwa wameshachukua na 18 kurejesha fomu hizo hadi jana.
Idadi hiyo ni kufikia jana mchana (Januari 17 mwaka huu). Pia Kamati ya Uchaguzi ya TFF inasisitiza kuwa wanaorejesha fomu hizo kwa email wanatakiwa kuzituma kwa Katibu Mkuu wa TFF kwa email ya tfftz@yahoo.comna si kwa email binafsi za wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi au maofisa wa TFF.
Waombaji wanne walioongezeka katika orodha ni Blassy Kiondo kwa Kanda ya Katavi na Rukwa, Eliud Mvella (Mbeya na Iringa), Geofrey Nyange (Morogoro na Pwani), na Omari Abdulkadir kwa Kanda ya Dar es Salaam.
Orodha kamili ya waombaji ni Athuman Nyamlani, Jamal Malinzi na Omari Mussa Nkwarulo (urais) wakati waombaji wa umakamu wa rais mpaka sasa ni Michael Wambura, Ramadhan Nassib na Wallace Karia.
Kwa upande wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji na kanda zao kwenye mabano ni Salum Chama (Kagera na Geita), Mugisha Galibona, Samuel Nyalla, Titus Osoro na Vedastus Lufano (Mara na Mwanza).
Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Charles Mugondo na Elly Mbise (Arusha na Manyara), Yusuph Kitumbo (Kigoma na Tabora), Ayubu Nyaulingo, Blassy Kiondo, Nazarius Kilungeja na Selemani Kameya (Katavi na Rukwa) na James Mhagama (Njombe na Ruvuma).
Athuman Kambi na Zafarani Damoder (Lindi na Mtwara), Hussein Mwamba na Stewart Masima (Dodoma na Singida), Farid Nahdi, Geofrey Nyange na Twahili Njoki (Morogoro na Pwani), Elias Mwanjala na Eliud Mvella (Iringa na Mbeya), Khalid Mohamed (Kilimanjaro na Tanga) na Muhsin Balhabou, Omari Abdulkadir na Shaffih Dauda (Dar es Salaam).
Kwa upande wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board) waliochukua fomu mpaka sasa ni wawili tu. Yusuf Manji amechukua fomu ya uenyekiti wakati Said Mohamed amechukua fomu ya kuwania umakamu mwenyekiti.
SUPER WEEK TENA NDANI YA LIGI KUU YA VODACOM
Mzunguko wa pili ya Ligi Kuu ya Vodacom utaanza Januari 26 mwaka huu huku kukiwa na maombi ya televisheni ya SuperSport kuonesha mechi za Super Week kama ilivyokuwa katika mzunguko wa kwanza.
Raundi tano za awali katika ratiba ya mzunguko wa pili zinabaki kama zilivyo wakati nyingine zilizobaki zitatolewa baada ya kuingiza mechi za Super Week.
Wakati huo huo, mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza unatarajia kuanza Januari 26 mwaka huu. Ratiba ya ligi hiyo na tarehe rasmi ya kuanza itatangazwa baada ya kupitiwa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inayotarajiwa kukutana mwishoni mwa wiki.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

EXTRA BONGO KUANZA KUGAWA ZAWADI KWA MASHABIKI LEO

BENDI ya Extra Bongo 'Wana Next Level' chini ya Ally Choki leo inatarajiwa kuanza kugawa zawadi kwa mashabiki wao katika onyesho litakalofanyika kwenye ukumbi wa Meeda Club, Sinza Mori.
Extra Bongo imeanza wiki nne za kugawa zawadi kwa mashabiki wao, kama njia ya kurudisha shukrani zao kwa mashabiki hao ambapo washindi wa tatu watakaocheza vema miondoko ya bendi hiyo watazoa vitita vya fedha zipatazo 300,000.
Mgawanyo wa fedha hizo ni kwamba mshindi wa kwanza atazoa Sh 150,000 na wa pili kukamata kitita cha 100,000 na atakayekuwa wa tatu atambulia 50,000.
Choki alisema baada ya makamuzi hayo ya Meeda leo bendi yake itaelekea ukumbi wa Garden Breeze, Magomeni Mapipa kwa ajili ya bonanza lao kabla ya Ijumaa kugawa tena zawadi kwa mashabiki wa TMK.
Akizungumzia shoo ya Jumapili hii, Choki alisema, bendi yake imepania kuhakikisha inakonga nyoyo za mashabiki wao wa Magomeni na maeneo ya jirani na kwamba, kila atakayehudhuria atakubaliana na hilo.
“Kazi zetu zinatambulika, watakaokuja watashuhudia shoo kali kutoka kwa wanamuziki na wanenguaji mahiri wa dansi. Waje kwa wingi na kila atakayeingia Garden Breeze, hatojutia uamuzi wake wa kuja kujinafasi nasi wana wa ‘Next Level’ wikiendi hii,” alitamba Choki.
Aidha, mkongwe wa dansi Afrika Mashariki na Kati, Tshimanga Kalala Asosa, naye atafanya vitu adimu akiwa na bendi yake ya Bana Marquiz, watakapotumbuiza kwenye ‘kijiji hicho cha maraha’ cha Garden Breeze leo usiku.
Assosa maarufu kama ‘Mtoto Mzuri’, alisema, amejiandaa kukonga nyoyo za mashabiki kwa vibao vyake vipya na vya zamani, vikiwamo vile vilivyompa umaarufu mkubwa, kiasi cha kuitwa hapa nchini kuanzisha bendi kongwe ya Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde Ngoma ya Ukae’ mwaka 1978.
“Nitawapa mashabiki vitu vipya na vile vyote nilivyopata kuimba katika bendi zangu tangu nikiwa Zaire (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo), hadi hapa Bongo,” alisisitiza Assosa bila kutaja nyimbo hizo na kuwataka mashabiki wa muziki wa dansi kufurika Garden Breeze.

SERIKALI YABARIKI FAINALI ZA TAIFA MISS UTALII TANZANIA 2012/13


Serikali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania, kupitia Baraza la Sanaa la Taifa, limebariki kufanyika kwa Fainali za Taifa za Miss Utalii Tanzania 2012/13 baada ya kuridhishwa na maandalizi yaliyo fanywa na Miss Tourism Tanzania Organisation waandaaji wenye dhima ya kikomo ya kuandaa na kuendesha mashindano hayo kitaifa na kimataifa, pia kwa kuzingatia sheria za nchi, kanuni na Taratibu za mashindano.

Serikali pia imeridhishwa na jinsi Fainali za ngazi za mikoa na kanda zilivyofanyika kwa mafanikio,ambapo kila mkoa umepata washindi wenye sifa za kuwakilisha mkoa husika katika Fainali za Taifa mwaka huu,ambapo jumla ya warembo 60 waingia rasmi kambini kesho katika hoteli ya Ikondelelo Lodge Dar es Salaam, kuanza mbio za kuwania Taji
hilo la Taifa.

Washindi wa 1-5 wa Fainali za Taifa ,watawakilisha Tanzania katika mashindano mbalimbali ya Dunia yakiwemo ya International Miss Tourism World, Miss Tourism United Nation, Miss Heritage World, Miss Tourism University World, Miss Globe International n.k

Miss Utalii Tanzania ,hadi sasa tunashikilia Jumla ya mataji 5 ya Dunia na kimataifa, yakiwemo ya Miss Tourism World 2005-Africa,Miss Tourism World 2006-SADC,Miss Tourism World 2007-Africa, Miss Tourism Model Of The World 2008-Personality n.k

Fainali za Taifa mwaka huu zimepangwa kufanyika wiki ya kwanza ya Februari ,wilaya ya Temeke na mkoa wa Dar es Salaam ukiwa umepewa heshima ya kuwa wenyeji wa Fainali hizo.

Asante,
Erasto Gideon Chipungahelo
Rais

Wednesday, January 16, 2013

Azam kwenda Kenya kujifua zaidi

 
BAADA ya kutwaa Kombe la Mapinduzi mwishoni mwa wiki visiwani Zanzibar, Azam FC inatarajiwa kuondoka nchini Alhamisi kwenda Nairobi, Kenya kwa ziara ya wiki moja ya michezo ya kirafiki, kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho.
Katibu Mkuu wa Azam FC, Nassor Idrisa ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba katika ziara hiyo watacheza mechi tatu za kujipima nguvu dhidi ya timu za Sofapaka, AFC Leopards na Gor Mahia kabla ya kurejea nchini Januari 23.
Nassor alisema ziara hiyo ni maalum kwa ajili ya kuiweka sawa timu yao kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.
Nassor amesema anaamini timu za Kenya ni nzuri na zitawapa changamoto nzuri kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na kuingia kwenye Kombe la Shirikisho.
“Tumekuwa katika programu ndefu ya maandalizi tangu Desemba, tukianzia Kongo (DRC) ambako tulicheza mashindano na kuchukua Kombe, tumetoka tumeingia kwenye Kombe la Mapinduzi tumeshiriki na kuchukua Kombe, na sasa tunakwenda Kenya,”alisema Nassor.
Katibu huyo alisema kikosi kizima cha Azam kitakwenda Kenya kwenye ziara hiyo na baada ya hapo timu itarejea tayari kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.
 

IMEHAMISHWA: BIN ZUBEIRY

Emmanuel Okwi aiacha Simba solemba atua Etoile du Sahel


Emmanuel Okwi

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi wa Simba anadaiwa kujiunga na klabu ya Etoile du Sahel ya Ligi Kuu ya Tunisia kwa dola za Kimarekani 300,000 (Sh. milioni 472).
Taarifa zilizopatikana jana jijini zinadai kwamba Okwi amekamilisha vipimo vya afya na kila kitu na tayari amesaini mkataba na klabu hiyo na atakuwa analipwa mshahara wa dola za Marekani 15,000 (Sh. milioni 24) kwa mwezi. Hata hivyo, haikuelezwa ni mkataba wa muda gani.
Taarifa hizo zinasema kuwa tayari Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage ameshatua nchini humo kwa ajili ya kuweka mambo sawa na kwamba sehemu za fungu hilo la usajili wa mchezaji huo zitagawanywa pia kwa klabu ya SC Villa kulingana na mkataba.
Okwi aliyekuwa akipiga chenga kuripoti kambini Simba na ameachwa katika safari ya Oman ambako mabingwa hao wa Tanzania Bara wameweka kambi kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Baada ya kumaliza mkataba wake wa awali na Simba Desemba mwaka jana, Okwi aliongeza mkataba wa miaka miwili na ‘Wekundu wa Msimbazi’ ambao kabla hajaanza kuutumikia, ameamua kuhamia Sahel.
Okwi akiitumikia timu ya taifa lake la Uganda


Mbio za uchaguzi wa TFF zapambamoto

Michael Wambura



ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Tanzania (FAT sasa TFF), Michael Wambura na kiongozi wa zamani wa klabu iliyokuwa Ligi Kuu ya Moro United ‘Chelsea ya Bongo’, Muhsin Balhabou ni miongoni mwa wadau wa soka walichukua fomu jana kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Wambura amechukua fomu kuwania umakamu wa rais huku Balhabou akiwania nafasi ya ujumbe katika kamati ya uchaguzi ya TFF. Uchaguzi huo utafanyika Februari 24 jijini Dar es Salaam
Tayari wagombea wengine wawili, Makamu wa Pili wa Rais anayemaliza muda wake, Ramadhan Nassib na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji inayomaliza muda, Wallace Karia wameshachukua fomu za kuwania nafasi anayoiwania Wambura.
Wanamichezo wengine waliochukua fomu jana ni pamoja na Mbasha Matutu, Salum Chama, Titus Osoro na Zafarani Damoder ambao wote wanawania pia nafasi za ujumbe wa kamati ya utendaji ya TFF.
Wagombea wengine waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania ujumbe ni Salum Chama anayewania kupitia Kanda ya Kagera na Geita, Mugisha Galibona, Samuel Nyalla, Titus Osoro na Vedastus Lufano (Mara na Mwanza), Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Charles Mugondo, Elly Mbise na Twahili Njoki (Arusha na Manyara) huku Yusuph Kitumbo (Kigoma na Tabora).
Ayubu Nyaulingo, Nazarius Kilungeja na Selemani Kameya (Katavi na Rukwa) na James Mhagama (Njombe na Ruvuma), Athuman Kambi (Lindi na Mtwara), Hussein Mwamba na Stewart Masima (Dodoma na Singida), Farid Nahdi (Morogoro na Pwani), Khalid Mohamed (Kilimanjaro na Tanga) na Muhsin Balhabou, Shaffih Dauda na Zafarani Damoder (Dar es Salaam).
Taarifa iliyotolewa jana na Afisa Habarin wa TFF, Boniface Wambura, imeeleza kuwa jumla ya waliochukua fomu hadi sasa ni watu 26, lakini idadi hiyo ni ya wale wanaochukua fomu hizo katika ofisi za TFF. Fomu hizo huchukuliwa pia kupitia tovuti ya TFF (www.tff.or.tz) na mwisho wa kuchukua na kuzirejesha ni keshokutwa Ijumaa, saa 10:00 jioni.
Mwaka 2004, Wambura pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa FAT, Muhiddin Ndolanga, waliangushwa na Tenga lakini mwaka 2008, Wambura alijitosa tena katika nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais lakini jina lake lilienguliwa kwa maelezo kwamba hakuwa na sifa ya uadilifu.
Hata hivyo, mwaka jana Wambura akiwa anawania nafasi ya uenyekiti wa Chama cha Soka cha Mkoa wa Mara (FAM), jina lake lilienguliwa na baada ya kukata rufaa lilirejeshwa lakini muda wa uchaguzi ulikuwa umeshamalizika na hivyo alishindwa kuwania cheo hicho kama alivyodhamiria.
Juzi, Tenga alitangaza wazi kwamba hatawania tena cheo hicho na hivyo kuwapunguzia 'presha' wale waliokuwa wakihofia kutwaa fomu za kuwania uenyekiti wa shirikisho hilo kwa sababu yake.
Katika hatua nyingine, Said Mohamed amechukua fomu ya kuwania umakamu mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board).

Mkina, Ochieng waiponza Simba

Mkenya Pascal Ochieng

WACHEZAJI Pascal Ochieng na Shija Mkina wameiponza klabu ya Simba baada ya uongozi wa mabingwa hao wa soka Tanzania Bara kutakiwa kufika mbele ya Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoa maelezo kuhusiana na madai mbalimbali ya wachezaji hayo.
Mkenya Ochieng aliwasilisha barua katika ofisi za (TFF) Desemba 19 mwaka jana akiliomba shirikisho hilo kumsaidia kupata haki zake zikiwamo fedha zake za usajili, Sh. milioni sita na mashahara wake wa mwezi mmoja (Novemba 2012), ambao hata hivyo hakuwa tayari kutaja ni kiasi gani kwa madai kuwa ni siri yake na Simba.
Ochieng, ambaye alilazimika kuununua mkataba wake wa miezi sita na klabu ya AFC Leopards ya Kenya ili ajiunge na Simba, alinukuliwa akisema kuwa anaidai Simba dola za Marekani 8,000 (Sh. milioni 12.6) na kwamba hajapatiwa barua ya kuvunjwa kwa mkataba wake na klabu hiyo, hivyo anaamini kuwa bado yeye ni mwajiriwa wa ‘Wekundu wa Msimbazi’.
Kwa upande wake, Mkina ambaye hivi sasa anaichezea kwa mkopo klabu ya ligi kuu Bara ya Kagera Sugar (akitokea Simba), anadai Simba haijamlipa Sh. milioni sita zilizokuwa zimebaki baada ya kusaini mkataba nao kwa makubaliano ya Sh. milioni 10 na kwamba walimlipa fedha ya utangulizi Sh. milioni nne mwaka 2010.
Mkina pia anadai kuwa uongozi wa Simba umekuwa ukimzungusha katika malipo ya fedha zilizobaki na kwamba anawadai pia fedha za mshahara wake wa miezi mitatu (Septemba – Novemba, 2012).
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam jana, Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kuwa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ili ilikutana jijini Dar es Salaam Jumamosi kupitia masuala mbalimbali yakiwamo madai ya wachezaji hao.
Wambura alisema kuwa baada ya kamati hiyo kupitia madai ya Ochieng na Mkina, iliamua kuzikutanisha pande zote (Simba na wachezaji wanaolalamika) ili iwahoji kwa pamoja Jumamosi ya Januari 19.
“Ni kweli tulipata barua za wachezaji hao. Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ilikaa Jumamosi iliyopita ikaamua kuwaita viongozi wa Simba na wachezaji wanaolalamika ili wahojiwe kwa pamoja Jumamosi,” alisema Wambura.
Baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Novemba mwaka jana huku timu yao ikifanya vibaya na kuangukia katika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, viongozi wa Simba waliamua kusitisha mikataba ya baadhi ya wachezaji wao wakiwamo beki Ochieng na mshambuliaji Daniel Akuffor wa Ghana.

Zahoro Pazi aenda kujaribiwa Afrika Kusini

Zahoro Pazi akiwa kando ya 'mkoko' wake hivi karibuni mitaa ya Temeke Maduka Mawili

MSHAMBULIAJI wa zamani wa timu za Mtibwa na Azam aliyekuwa ametua JKT Ruvu kwa mkopo, Zahoro Pazi, ameondoka nchini juzi usiku kuelekea Afrika Kusini kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Ligi Kuu ya Bloemfotein Celtic.
Akizungumza na MICHARAZO muda mchache kabla ya kupaa kuelekea nchini humo, Pazi alisema kuwa safari yake imefanywa na wakala wake ambaye hakupenda kumtaja jina na kwamba mipango hiyo ilikuwepo tangu mwishoni mwa mwaka jana.
Pazi, alisema kwamba klabu hiyo ya Bloemfotein Celtic inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini, ilivutiwa naye kupitia michuano ya Kombe la Kagame pamoja na kutuma maskauti wao walipoenda DR Congo kushiriki michuano ya Kombe la Hisani.
"Ndoto zangu za kucheza soka la kulipwa baada ya kukwama mara mbili Ujerumani na Umangani naona zinaelekea kuwa kweli kwani nimeitwa na klabu ya Bloemfotein Celtic kwa ajili ya kufanyiwa majaribio," alisema Pazi.
Pazi, mtoto wa kipa nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kutamba na timu za Pilsner, Simba, Taifa Stars na El Merreikh ya Sudan, Idd Pazi 'Father' alisema ana imani kubwa ya kufanya vema majaribio yake.
"Sina hofu yoyote na safari yangu hii, kama niliweza kuivutia Kaiserslautern ya Ujerumani sidhani kama nitashindwa Afrika Kusini muhimu niombeeni dua Mungu anifanyie wepesi," alisema Pazi.
Kinda hilo lililozaliwa Julai 4, 1989 akiwa mtoto wa mwisho kati  ya watoto wawili wa Idd Pazi, alisema majaribiuo yake amedokezwa yatakuwa ya wiki moja na kama kutakuwa na lolote la ziada atalifahamisha NIPASHE akiwa nchini humo.
***

Tuesday, January 15, 2013

UNAAMINI MAMBO YA UTABIRI? MSOME MAALIM HASSAN YAHYA 





MAALIM  Hassan Yahya Hussein, ameibuka na kupinga vikali utabiri uliotyolewa na Sheikh mmoja kwamba Rais wa mwaka 2015 lazima awe mwanamke akidai ana lengo la kuwakatisha wanaume wanaoota kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao.
Pia ameweka bayana kwamba ndani ya mwaka huu kutakuwa na vifo vya kushtukiza na vibaya kwa waandishi wa habari, wasanii na watunzi wa vitabu kuliko ilivyokuwa mwaka uliopita.
Maalim Hassani Yahya Husseni mrithi wa aliyekuwa mtabiri maarufu nchini Sheikh Yahya Husseni, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam majuzi na kudai kwamba  kwa kawaida utabiri uhusisha mwaka husika kwa kila mwaka hata kama mengine hutokea mbele zaidi.
 Alisema kwa mwaka 2013 utabiri utaanza rasmi Machi 21 na kudai kiutabiri huwezi kutoa utabiri katika matukio ya mwaka mmoja mbele, kama ilivyuofanywa na Sheikha Khalifa Khamisi na kudai kitendo chake ni sawa na kutaka kuwakatisha tamaa baadhi ya watu wenye nia ya kutaka kugombea nafasi hiyo  2015.
“Huwezi kutoa utabiri wa miaka miwili mbele hata Sheikh Yahya Hussein mtabiri aliyekuwa akikubalika hakuwahi kufanya hivyo, pia sikubaliani naye kuwa rais ajaye atakuwa mwanamke hata ukiangalia katika njia zetu za utabiri ambazo ni namba zinapingana na hilo”alisema.
Alisema matokeo ya utabiri kama huo ni sawa na uwamuzi wa kuwafungia milango kidemokrasia baadhi ya wanasiasa wenye nia ya kugombea urais mwaka 2015.
“Kuna baadhi ya viongozi wakiwemo Lowassa na Membe wanadaiwa kuwa huenda wakagombea nafasi hiyo, kwa kufanya hivyo itakuwa ni kuwakatisha tamaa”alisema.
Akizungumzia utabiri wa mwaka huu, alisema kuwa kuna viongozi wengi, wabunge, wakuu wa mikoa na wengine watatoa matamshi ya  utatanishi na kusababisha hofu na mitafaruku itakayowafanya watu kupigana.
 Vile vile alisema wapo wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wataungana katika masuala ya msingi yatakayohusu utaifa bila kujali itikadi zao za kivyama au kimajimbo.
Maalim Hussein alibainisha kuwa Rais Jakaya Kikwete ataunganisha nchi na kuwa moja yenye uimara wa utaifa kuliko watangulizi wake, akishirikiana zaidi na wanasiasa na viongozi wa dini kuondoa mtikisiko wa uvunjifu wa amani uliyojitokea mwaka jana.
Aidha, Chama kimoja cha siasa kitajitokeza na kitachochea kujitenga na kuunda Taifa lake hata hivyo, kusudio hilo halitafanikiwa kwani litapingwa na Watanzania wote kwa kauli moja na vitendo.
Maalim Hussein pia alisema kutatokea vifo vya ghafla kwa watunzi wa hadithi na vitabu, wandishi wa habari, wanasiasa na wasanii ambapo matukio hayo yatakuwa mabaya zaidi kuliko mwaka jana. 
Akigusia Uchaguzi Mkuu utakaofanyika hivi karibuni   nchini Kenya ambao ni majirani, alisema kuwa Muungano wa CORD, ukiongozwa na Raila Odinga utashinda uchaguzi huo, ambao ana amini utakuwa wa amani na tulivu.
“Ushindi huo utakuja baada ya kuushinda Muungano wa Jubilee ukiongozwa na akina Uhuru Kenyata na Ruto pamoja na ule wa Musalia Mudavadi unaoitwa AMANI”alisema.

ZAWADI ZA EXTRA BONGO KUANZA KUTOLEWA MEEDA CLUB

Ally Choki na Athanas Montanabe wakiwajibika jukwaani

MASHABIKI wa bendi ya Extra Bongo wanatarajiwa kuanza kuzoa zawadi katika shindano lao maalum lililopewa jina la 'Wiki 4 za Zawadi Extra Bongo' siku ya Jumamosi katika onyesho litakalofanyika kwenye ukumbi wa Meeda Club, Sinza Mori, Dar es Salaam.
Shabiki atakaayecheza vema katika onyesho hilo atazoa kitita cha Sh Laki Unusu (150,000) huku wa pili akizoa Laki Moja (100,000) na wa tatu yeye ataambulia Nusu Laki (50,000).
Mkurugenzi wa Extra Bongo, Ally Choki alisema utaratibu huo wa kutioa zawadi hizo kwa mashabiki wao utafanyika katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya jijini Dar es Salaam kwa muda wa mwezi mmoja kuanzia Januari 19.
Choki alisema mara watakapotoka Meeda Extra Bongo watapeleka zawadi kwa mashabiki wao wa Temeke kabla ya kuelekea Kibaha Pwani na mahali pengine watakapoona panafaa kwenda kumwaga zawadi hizo kama njia ya kurudisha shukrani kwa mashabiki wao waliowaunga mkono tangu bendi hiyo irejee upya 2010.
"Tunataka mashabiki wafurahie burudani na pia kuondoka ukumbini wakiwa na zawadi kama ambavyo walivyokuwa wanatuunga mkono tangu tuliporejea kwa awamu ya pili na sasa tukielekea miaka mitatu," alisema.
Choki alisema kila watakapokuwa wakikaribia kumaliza onyesho watawapigia sebene mashabiki wao na kuchuana wenyewe na watawapa fursa mashabiki watazamaji kuteua washindi ambao watapewa chao hapo hapo kabla ya kuelekea mahali pengine hadi watakaporidhika na kusitisha mchuano huo.
Naye kiongozi wa safu ya uenguaji ya Extra Bongo, Hassani Mussa 'Syper Nyamwela' alisema anadhani mchuano huo ni fursa nzuri ya mashabiki wao kuifurahia Extra Bongo sambamba na kutunisha mifuko yao kwa kuonyesha umahiri wao wa kucheza miondoko ya bendi hiyo.
"Badala ya kutozoea kwa muda mrefu kutuona wanenguaji na wana Extra Bongo kwa ujumla kuonyesha umahiri wa kunengua safari hii ni zamu yao kushindana wenyewe kwa wenyewe na kuzoa fedha taslim bila zengwe wala nini, na huu ni mwanzo tu tutarejesha fadhila kwa mashabiki kadri tutakavyojipanga," alisema.

Bendi hiyo ya Extra Bongo inayotamba na vibao matata kama 'Ufisadi wa Mapenzi', 'Mjini Mipango', 'Mgeni' na nyingine, itakuwa bendi ya kwanza kwa mwaka huu na siku za karibuni kufanya kitu kama hicho ili kuwafurahisha mashabiki ambao wamekuwa wakiwaunga mkono kwa kuhudhuria maonyesho wao kila mahali.

Extra Bongo waja na Wiki 4 za Kutoa Zawadi kwa Mashabiki

Mkurugenzi wa Extra Bongo Ally Choki akiwapagawisha mashabiki wa bendi hiyo katika moja ya maonyesho yao
BENDI ya dansi inayotisha nchini kwa sasa, Extra Bongo 'Wana Next Level' a.k.a Wazee wa Kizigo imeandaa wiki nne za kuwazawadiwa mashabiki wake katika shindano maalum litakalofahamika kwa jina la 'Wiki 4 za Zawadi za Extra Bongo'.
Shindano hilo litakaloshindanisha mashabiki wa bendi hiyo kwa kunengua miondoko ya bendi hiyo ya 'Kizigo' ndani ya wiki nne mfululizo ambapo kwa kuanzia watatoa zawadi hizo kwenye ukumbi wa Meeda Club, Sinza jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa bendi hiyo, Ally Choki alisema katika shindano hilo mashabiki watatu watakacheza vema muziki wa bendi hiyo watawazadiwa vitita vya fedha taslim ukumbini.
Choki alisema mshindi wa kwanza katika shindano hilo lililoandaliwa kwa nia ya kuongeza hamasa kwa mashabiki wao kupima kama nao ni wakali wa muziki atapewa Sh 150,000 wakati wa pili atazawadiwa Sh 100,000 na wa tatu ataambulia Sh 50,000.
"Extra Bongoi tunatarajia kuja na Wiki Nne ya Zawadi kwa Mashabiki ambayo rasmi itaanza Jumamosi kwenye ukumbi wa Meeda Club, Sinza kabla ya kuelekea TMK Ijumaa ya Januari 25 ksiha kuangalia kama tuhamie Bagamoyo au Kibaha," alisema Choki.
Choki alisema uzinduzi rasmi wa shindano hilo utasindikizwa na wakali wa muziki wa kizazi kipya, Amin, Linah na Ditto kutoka THT na Saynag wa Respect.
"Yaani ni burudani kwa kwenda mbele pamoja na kuwashuhudia mashabiki wakichuana kucheza Kizigo, pia watawashuhudia wakali wa muziki wa kizazi kipya ambao watatusindikiza katika wiki hizo nne za kutoa zawadi kwa mashabiki wetu," alisema.
Choki alisema japo mpambano huo wa mashabiki sio shindano haswa kwa sababu halitakuwa na majaji wala waamuzi, zaidi ya mashabiki lakini wamefanya hivyo ili kuonyesha namna gani wanavyowathamini mashabiki wao waliowaunga mkono karibu miaka mitatu ya kurejea kwao upya katika 'game'.

Zola D, P Funk wote wana Knockout

Msanii Zola D akiwa katika pozi


MSANII nyota wa muziki wa hip hop nchini, David Michael 'Zola D' ameuanza mwaka 2013 kwa  kishindo kwa kuachia wimbo wake mpya uitwao 'Knockout' aliomshirikisha mtayarishaji mahiri wa muziki, P. Funk 'Majani'.
Tayari wimbo huo uliotolewa katika 'audio' na video tayari umeshaanza kurushwa hewani katika vituo vya redio na runinga nchini, huku Zola D akidai hizo ni salamu zake kwa mashabiki kwamba mwaka 2013 amejipanga kuwapa raha mwanzo mwisho.
Zola D alisema kuwa, wimbo huo ameurekodia studio za Bongo Rocords kwa Majani na video ameifanya chini ya kampuni yake ya Uncle Films akishirikiana na kampuni ya Benjamini wa Mambo Jambo.
"Katika kuwapa raha mashabiki wangu, nimeachia hewani wimbo wangu mpya uitwao 'Knockout' ambao nimeimba na P Funk 'Majani' ambayo pia nimeitolea video yake na tayari imeshaanza kuchezwa na vituo vya redio na runinga," alisema Zola D.
Mkali huyo ambaye pia ni mwanamasumbwi wa uzito wa juu nchini, alisema wakati wimbo huo ukiendelea kutamba hewani, ameshaanza maandalizi ya kufyatua kazi nyingine mpya, japo hakupenda kuweka hadharani kwa madai ni mapema mno.
"Ndugu yangu unajua siku hizi wasanii wamekuwa wepesi kuiba 'idea' za wenzao, hivyo kutaja jina la 'project' yangu mpya ijayo inaweza kuwa mtaji kwa wachakachuaji, ila mashabiki wakae wakijua kuna burudani mpya nawaandalia," alisema Zola D.
Msanii huyo alisema kazi hiyo mpya huenda ikakamilika ndani ya wiki ijayo kabla ya kufanyiwa utaratibu ya kuachiwa hewani baada ya kukamilika kila kitu ikiwemo kurekodiwa kwa video yake.

Sunday, January 13, 2013

GOLDEN BUSH VETERANI WALIVYOISASAMBUA WAHENGA FC JANA

Mlezi wa timu ya Goldoen Bush Veterani, Onesmo Waziri 'Ticotico' akihojiwa na waandishi wa habari katika mchezo wao na Wahenga Fc ambapo timu yao ilishinda mabao 4-3.

Mshambuliaji Herry Morris akitafakari wakati wa mapumziki, ambapo alishatupia mabao mawili na kuisaidia Golden Bush kushinda mabao 4-3.

Wachezaji wa Golden Bush Veterani wakiwa mapumziko


Herry Morris akihojiwa na waandishi

Beki wa timu ya Golden Bush, Majaliwa 'Afande' akijohiwa pia kwenye mchezo huo

Yona Babadimo wa Wahenga Fc naye akihojiwa wakati timu yake ikichezea kipigo toka kwa Golden Bush jana jijini Dar es Salaam waliposherehekea Mapinduzi na kuukaribisha mwaka 2013


Mengi Matunda mchezaji wa Wahenga akijohiwa baada ya kupumzishwa na benchi lake la ufundi

Said Swedi 'Panucci' akikokota mpira katika pambano lao la jana

Njoo sasa! Ndivyo anayoelekea kusema beki wa Wahenga 'Mohammed huku Godfrey Katepa wa Golden Bush akimfuata

Achia wewe! Said Swedi (3) akichunana na mchezaji wa Wahenga katika pambano lao la jana

Kama Ronaldo! Mchezaji wa Wahenga akijiandaa kupiga mpira huku Shaaban Kisiga (19) wa Golden Bush akimfuatilia sambamba na wachezaji wenzake

Mimi ndio Macocha! Macocha Mayay wa Wahenga akimtoka Godfrey Katepa (kulia) huku akichungwa na Salum Swedi 'Kussi' wa Golden Bush Veterani.

Wachezaji wa Wahenga na Golden Bush wakiwajibika uwanjani timu zao zilipokutana jana na Golden Bush kushinda mabao 4-3

Macocha wa Wahenga Fc akijaribu kutafuta mbinu za kumtoka Saidi Swedi wa Golden Bush

Mzee Hamis wa Wahenga akikokota mpira pembeni ya uwanja wa TP wakati timu yake ilipoumana na Golden Bush na kuchezea kichapo cha mabao 4-3

Wazir Mahadhi (10) akichuana na wachezaji wa Wahenga wakati akiiongoza timu yake kulipa kisasi cha mabao 4-3 kwa wapinzani wao.

Pilikapilika uwanjani wakati Wahenga Fc na Golden Bush zilipomenyana jana jijini Dar es Salaam

Onesmo Waziri 'Ticotico' (4) akipongezwa na Athuman Machupa wakati wakimpisha uwanjani jana katika pambano lao dhidi ya Wahenga Fc.

Jamani Mpo Wapi! Beki wa Wahenga Fc akijiandaa kupiga mpira mbele

Mahadhi akichuana na mchezaji wa Wahenga katika mechi ya jana

Said Swedi 'Panucci' (3) akitafakari namna ya kuupiga mpira wakati wa pambano lao la Golden Bush dhidi ya Wahenga ambapo walifanikiwa kushinda mabao 4-3

Macocha Mayay wa Wahenga (kulia) akiwatoka wachezaji wa Golden Bush, Shaaban Kisiga (kushoto) na Shija Katina (8)

Berki wa Wahenga Fc akihamisha mpira mbele ya Herry Morris (kulia)

Hapa Kazi Tu!

MTANIKOMA! Macocha akiwaacha wachezaji wa Golden Bush katika pambano la jana, mchezaji huyu ndiye aliyekuwa nyota kwa upande wa Wahenga, japo timu yake ililala kwa mabao 4-3


Jamani eeh inakuwaje magoli yamerudi? Ndivyo anavyoelekea kuhoji kocha Madaraka Seleman wa Golden Bush wakati wa mapumziko ambapo timu yake ilikuwa imefungana mabao 2-2 na Wahenga Fc licha ya wao kuongoza kwa mabao 2-0. Waliporejea uwanjani kwa ngwe ya pili walirekebisha makosa na kuisambaratisha Wahenga kwa magoli 4-3

MTANIJUA LEO! Nyota wa Wahenga Macocha Mayay akiwakimbiza wachezaji wa Golden Bush, Godfrey Katepa (9) na Majaliwa (14) wakati timu zao zilipomenyana jana kwenye mechi maalum ya kuukaribisha mwaka 2013 na kusherehekea sikukuu ya Mapinduzi. Golden Bush ilifanikisha kushinda mabao 4-3