STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, February 16, 2014

Messi aendelea kufanya maajabu Barcelona ikiua 6-0 nyumbani

Yebaaa! Watatukoma mwaka huu, Messi na Neymar wakipongezana jana
LIONEL Messi ameendelea kudhihirisha hana mpinzani katika medani ya ufumaniaji nyavu wakati usiku wa kuamkia leo alipotupia mabao mawili na kuisaidia Barcelona kuishindilia Rayo Vallecano kwa mabao mabao 6-0 katika mechi ya La Liga, Hispania.
Adriano Correia  alianza kuiandikia Barca bao dakika ya pili tu ya mchezo huo akimalizia kazi ya Pedro kabla ya Messi kuanza vitu vyake kwa kufunga bao la pili dakika ya 36  kwa pasi ya Fàbregas, mabao yalidumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa wenyeji kuandika bao la tatu kupitia Alexis Sanchez aliyemalizia pasi ya Messi katika dakika ya 53.
Pedro aliiongezea Barca bao dakika tatu baadaye kwa kasi nzuri ya Fabregas ndipo Messi aliporejea tena kambani kwa kufunga bao lake la pili lililokuwa la tano kwa Barca akisaidiwa na Sánchez na msumari wa mwisho ukapigiliwa na Neymar dakika moja kabla ya kumalizika kwa mchezo huo na kuirejesha Barcelona kileleni ikiitoa Atletico Madrid waliokuwa wamekaa baada ya jana kushinda mabao 3-0 dhidi ya Real Valladorid.
Timu zote zimelingana pointi zikiwa na 60 kila mmoja ila zinatofautisha uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa, huku wakifutiwa kwa karibu na Real Madrid ambayo itashuka dimbani leo ugenini dhidi ya Getafe.
Katika mechi nyingine iliyochezwa jana Levante ilishinda nyumbani bao 1-0 dhidi ya Almeria na Celta Vigo imepata ushindi wa mabao 2-0 ugenini leo Jumapili dhidi ya wenyeji wao Villarreal.

Saturday, February 15, 2014

Manchester City waikalisha Chelsea FA Cup

Manchester City celebrate
Samis Nasir akipongezwa na wachezaji wenzake baada ya kufunga bao la pili lililoizamisha Chelsea kwenye FA Cup hivi punde
Daa Chuma hichooo! Petr Cech na beki wake hawaamini kama Jovetic amefunga bao la kuongoza

MABAO mawili ya  Steven Jovetic na jingine la Samir Nasir yametosha kuzima ndoto za kocha Jose Mourihno kuitambia kwa mara ya pili Manchester City baada ya timu yake ya Chelsea kuondoshwa kwenye michuano ya Kombe la FA muda mfupi uliopita.
Jovetic alifunga bao la kwanza dakika ya 16 kwa pasi ya Edin Dzeko kabla ya Samir Nasir kuongeza la pili katika kipindi cha pili akimalizia kazi ya David Silva katika dakika ya 67 na kuipeleka Manchester City hadi Robo Fainali ya michuano hiyo.
Wiki mbili zilizopita Chelsea iliitambia City nyumbani kwao kwa kuilaza bao 1-0 na leo ilitarajiwa labda wangerejea kitendop hicho, lakini vijana wa Etihad walikuja kivingine na kuibana Chelsea na kuendelea kuweka hai matumaini ya kunyakua mataji nne msimu huu.
City tayari imetinga fainali ya Kombe la Ligi (Capital One) na inashiriki pia Ligi ya Mabingwa Ulaya na ipo kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya England.

Wigan Athletic yaifuata Sunderland FA Cup

Wigan midfielder Ben Watson (second left) powers in a goal against Cardiff in their FA Cup tie
Wigan midfielder Ben Watson
KLABU ya Wigan Athletic imeifuata Sunderland katika hatua ya Robo Fainali ya michuano ya Kombe la FA baada ya kuing'oa Cardiff City kwa mabao 2-1 katika mechi iliyomalizika muda mchache uliopita.
Wigan walipata ushindi huo ugenini kwa mabao Chris McCann katika dakika ya 18 na Ben Watson aliyefunga bao dakika ya 40, licha ya wenyeji ilipata bao la kufutia machozi katika dakika ya 27 kupitia Fraizer Campbell.
Pambano lingine la michuano hiyo kati ya Manchester City dhidi ya Chelsea limeshaanza na wenyeji City wameshafunga bao moja lililofungwa na Stevan Jovetickatika dakika ya 16 na kwa sasa mchezo huo upo ndani ya dakika ya 20.






Azam wapo tayari kuwavaa Wamakonde, KMKM kufanya maajabu kwa Wahabesh?, KMKM

Azam Fc watakaokuwa ugenini nchini Msumbiji
KMKM ipo nyumbani kurudiana na Wahabeshi

WAKATI ya Yanga na Chuoni yameshafahamika baada ya kucheza jioni ya leo, wawakilishi wengine wa Tanzania, Azam na KMKM zitakuwa kibaruani kesho kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho katika viwanja viwili tofauti.
Azam wenyewe watakuwa ugenini mjini Beira, Msumbiji kukabiliana na wenyeji wao, Ferroviario de Beira katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika wakati KMKM watakuwa uwanja wa Amaan Zanzibar dhidi ya wageni wao kutoka Ethiopia, Dedebit.
Katika mechi zao za awali wiki iliyopita Azam ilipata ushindi mwembamba nyumbani wa bao 1-0 wakati KMKM inayoiwakiliza Zanzibar kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ilifungwa mabao 3-0.
Msemaji wa Azam, Jafar Idd amesema kikosi chao kipo imara kwa ajili ya mechi ya kesho ambapo wanatarajiwa kupata sapoti kubwa ya mashabiki wa Kitanzania kutoka miji mingine ya nchi hiyo iliyopo Kusini mwa Tanzania.
Jafar alisema jiji la Beira kwa sasa gumzo kubwa ji nyota wa Azam, Salum Abubakar, John Bocco 'Adebayor' na Kipre Tchetche ambao kesho watashuka dimbani kuihakikishia Azam ikitinga raundi ya kwanza ya michuano hiyo inayoishiriki kwa mara ya pili mfululizo.
Katika mechi nyingine za michuano hiyo ya Afrika timu ya KCCA ya Uganda imesonga mbele licha ya kulala nyumbani kwa mabao 2-1 dhidi ya El Merreikh ya Sudan baada ya mechi ya awali kushinda ugenini 2-0, Kabuscop ya Angola imeing'oa Cote d'Or ya Seychelles kwa jumla ya mabao 7-2 baada ya leo kuilaza 2-1 wiki moja baada ya kuikung'uta mabao 5-1 mjini Luanda.
Nkana Red Devils ya Zambia iitandika Mbabane Swallows ya Swaziland kwa jumla ya mabao 5-4 baa ya leo kuilaza 5-2, wiki moja baada ya kulazwa 2-0 ikiwa ugenini, huku Rayon Sports ya Rwanda ikishindwa kutamba nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 na AC Leopards ya Congo na kung'olewa kwa faida ya mabao ya ugenini kwani wiki iliyopita walitoka suluhu ya 0-0 ugenini.Hizo ni mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika wakati mechi za Kombe la Shirikisho ukiacha Chuoni kung'oka pia Gaborone United ya Botswana imetolewa na Super Sports kwa jumla ya mabao 3-0 baada ya leo kulala nyumbani bao 1-0 wiki moja baada ya kufungwa ugenini 2-0, Club Kamsar ya Guinea imelazimishwa sare ya 1-1 na Douanes ya Togo na kung'olewa kwa jumla ya mabao 3-1 baada ya wiki iliyopita kulazwa 2-0 ugenini.
Nayo Cob ya Mali imefanikiwa kusonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya leo kushinda 1-0 baada ya sare ya awali ya 1-1 dhidi ya Al Ahli Tripoli, mechi nyingine zinazochezwa leo bado matokeo yake hayajapatikana mpaka sasa, ila MICHARAZO itawaeletea matokeo mara yatakapopatikana.

Sunderland yatangulia robo fainali FA England

Craig Gardner
Sunderland ikifunga bao lake pekee dhidi ya Southampton

SUNDERLAND imeendelea kuonyesha maajabu baada ya kuwa klabu ya kwanza kutinga hatua ya Robo Fainali ya Michuano ya FA baada ya kuitandika Southampton kwa bao 1-0 katika pambano lililochezwa mapema leo.
Vijana hao wa Gustav Poyet waliokuwa wakichechemea kwenye  Ligi Kuu ya England, tayari imeshatinga fainali ya Kombe la Ligi (Capital One) itakapoumana na Manchester City mwezi ujao na ushindi huo wa leo umeipa uhakika wa kuendelea kuonyesha maajabu chini ya kocha huyo.
Bao lililoizamisha Southampton katika pambano hilo lililochezwa kwenye uwanja wa Light (Stadium of Light) liliwekwa kimiani katika kipindi cha pili na Craig Gardner.
Gardner alifunga bao hilo katika dakika ya 49 na kuipa wakati mgumu wageni wao kutafuta bao la kusawazisha lakini dakika 90 zilipoisha wenyeji walikuwa washindi na kutangulia robo fainali.
Usiku huu kutakuwa na mechi nyingine za michuano hiyo Cardiff City dhidi ya Wigan Athletic na Manchester City itaikaribisha Chelsea na mechi nyingine iliyokuw aichezwe jioni hii kati ya Sheffield Wedn dhidi ya Charlton Athletic umeahirishwa kutokana na hali mbaya ya hewa.

Simba bado gonjwa, Coastal yakaa Mlandizi

* Mtibwa Sugar nayo yanyukwa nyumbani, kwingine sare tupu
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEg2BTfXkwh4BZ5f8ZQ6Ys5ZFz04K7rM7SUvMVEKPecWJHyoL_6pe1P9_Fq3AmPV0Pc1iw1uB7AqBm1WTQ9nq2JJISFutKaNXFzEqLWQWOL5g9cNxO1mG8cimYRISmeLknTq4KPU6zXFmFFi/s1600/Simba+Vs+Mbeya+City.jpg
Deo Julius wa Mbeya na Haruna Chanongo wa Simba leo wote wamehusika na mabao ya jijini Mbeya. Hii ni mechi yao ya kwanza iliyoisha kwa sare ya 2-2

VIJANA wa Msimbazi, Simba jioni ya leo imeigomea Mbeya City nyumbani kwao kukweka kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuchomoa bao na kulazimisha sareya 1-1 katika pambano kali lililochezwa kwenye uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.
Wakati Simba ikilazimisha sareugenini, Mtibwa Sugar imejikuta ikichezea kichapo toka kwa Prisons ya Mbeya, huku Mgambo JKT na  Rhino Rangers zikitoka sare ya 1-1 kama ilivyokuwa kwa Oljoro JKT dhidi ya JKT Ruvu na Coastal Union ikishindwa kuonyesha makali wa Oman kwa kulala kwa Ruvu Shooting.
Katika pambano la Mbeya, Simba walishtukizwa na bao la penati katika dakika 13 baada ya William Lucian 'Gallas' kunawa mpira  langoni mwake na Deogratius Julius kukwamisha na kudumu hadi wakati wa mapumziko licha ya kosa kosa za hapa na pale toka kwa timu zote.
Dakika tano baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, Amissi Tambwe aliisawazishia Simba bao kwa kichwa na kuwa goli lake la 15 la mshambuliaji huyo kutoka Burundi baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Haruna Chanongo aliyepiga krosi murua.
Timu ziliendelea kushambuliana na kufanya mabadiliko ya wachezaji, lakini hakuna kitu kilichobadilika na kufanya mechi kuisha kwa sare ya 1-1 na timu hizo kugawa pointi moja moja na kuiacha Simba ikibakia nafasi ya nne ikiwa na pointi 32 na Mbeya ikifikisha pointi 35 na kulingana na Yanga, lakini uwiano wa mabao umeifanya kubaki nafasi ya tatu.
Kwa sare hiyo imeikwamisha Mbeya City kukwea kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo nafasi waliyokuwa nayo katika mchezo huo kwani ingefikisha pointi 37 na kuzishinda Azam na Yanga ambao wikiendi hii wana majukumu ya kimataifa ugenini nchini Comoro na Msumbiji.
Katika mechi nyingine, Mgambo JKT ilishindwa kuendeleza ubabe katika ligi hiyo baada ya kufungana bao 1-1 na Rhino Rangers mjini Tabora. Wenyeji walianza kuandika bao dakika ya 29 kupitia Gideon Mlami na Mgambo kusawazisha kipindi cha pili dakika ya 51 na Ajali Boli. huku Oljoro JKT kubanwa  nyumbani jijini Arusha mbele ya JKT Ruvu kwa kutoka 0-0 nayo Coastal Union ikisulubiwa na Ruvu Shooting Mlandizi-Pwani kwa kulazwa bao 1-0, bao lililofungwa na Said Dilunga.
Nao Ashanti United ikiwa uwanja wa nyumbani wa Chamazi, wakilazimishwa sare na Kagera Sugar ya kutofunga bao lolote, huku Mtibwa Sugar ikiwa uwanja wa Manungu imelazwa  bao 1-0 na wageni wao Prisons ya Mbeya.

Ngassa azidi kung'ara Afrika apiga hat trick nyingine Comoro, Chuoni yang'oka Shirikisho Afrika yalala kwa Wazimbabwe

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEi11gBZHuo7IUZ3uKTJrVrdmUFUir9Z5Oc8ElaQAwQWFmHZj3LJsWXh3x8O43owD9f_7o29fg8A7vqq25rErMvJHI8g06ph2VmhSTCkbJ79-BBwiQgjqAnxZw_YyvPZoNyZUwzusu5h8FIf/s640/blogger-image-1980253589.jpg
Ngassa alipoinyanyasa Komorozine jijini Dar na leo kaifanyia hivyo hivyo kwa kupiga hat trick

WINGA machachari wa kimataifa, Mrisho Ngassa ameendelea kuweka rekodi Afrika baada ya jioni ya leo nchini Comoro kufunga hat trick nyingine na kuondoka na mpira wakati Yanga ikiilaza Komorozine de Domoni kwa mabao 5-2.
Ngassa alifunga mabao matatu katiuka mchezo wa kwanza wakati Yanga ikishinda mabao 7-0 na kuondoka na mpira uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kurudia kitendo hicho leo inamfanya kufikisha jumla ya mabao 6 na kuongoza kwenye orodha ya wafungaji wa michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mabao mengine ya Yanga katika mchezo huo wa marudiano yaliwekwa kimiani na Simon Msuvah na Hamis Kiiza 'Diego'.
Kwa ushindi huo Yanga imefuzu raundi ya kwanza kwa jumla ya mabao 12-2 na kupata nafasi ya kuvaana na mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Al Ahly ya Misri katika mechi mbili kazi inayoonekana ngumu kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Nao wawakilishi wa Tanzania Zanzibar katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika Chuoni, imehitimisha safari yake katika michuano hiyo baada ya kulazwa mabao 2-1 na How Mine ya Zimbabwe katika mchezo uliochezwa uwanja wa Amaan Zanzibar.
Chuoni walitangulia kupata bao kabla ya wageni kurejesha na kuongeza la ushindi na kufanya isonge mbele kwa jumla ya mabao 6-1 baada ya mechi ya awali Wazimbabwe hao kushinda nyumbani mabao 4-0.

Hiki ndicho kikosi cha Yanga kitakachoanza Comoro



1. Deogratias Munish "Dida" - 30
2. Mbuyu Twite - 6
3. Oscar Joshua - 4
4. Nadir Haroub "Cannavaro" - 23
5. Kelvin Yondani - 5
6. Athuman Idd "Chuji" - 24
7. Saimon Msuva - 27
8. Haruna Niyonzima - 8
9. Didier Kavumbagu - 7
10. Mrisho Ngasa - 17
11. Hamis Kizza - 20

Subs:
Barthez, Juma Abdul,Luhende, Rajab, Domayo, Dilunga n Bahanuzi

Simba, Mbeya City hapatoshi leo Sokoine

* Mbeya City kukalia kiti cha uongozi leo?
* viwanja vingine vitano kuwaka moto wikiendi hii
Ilivyokuwa hekaheka ya mechi ya kwanza kati ya Simba na Mbeya City

Simba
Mbeya City

Ashanti Utd
JKT Ruvu wapo ugenini jijini Arusha
 
Kagera Sugar watakuwa jiji Dar kuivaa Ashanti
Prisons wageni wa Mtibwa mjini Manungu

Mgambo JKT wapo Tabora kuvaana na Rhino Rangers
Oljoro JKT kuvuna nini kwa JKT Ruvu jijini Arusha?
Ruvu Shooting kuifanyia nini Coastal Union
JIJI la Mbeya leo litasimama kwa muda wakati wenyeji Mbeya City watakapoikaribisha Simba kwenye uwanja wa Sokoine likiwa ni moja ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayochezwa leo nchini.
Mechi hiyo inavuta hisia kubwa kuliko hata mechi za kimataifa ambazo timu za Yanga na Azam zilizopo ugenini zitakuwa zikiiwakilisha Tanzania katika kutafuta nafasi ya kufuzu raundi ya kwanza.
Mvuto wa mechi hiyo ya Mbeya unatokana na ukweli kuwa Simba katika mechi zake mbili zilizopita ilionekana kupepesuka, huku Mbeya City inayotajwa kuwa tishio zaidi ikiwa uwanja wa nyumbani ikiwa na kumbukumbu ya kupata sare dhidi ya Mnyama katika mechi yao ya duru la kwanza jijini Dar es Salaam.
Mashabiki wa Mbeya wanaamini Simba leo haitatoka kama walivyoifanyia Mtibwa Sugar au ilipoibana Yanga ilipoenda kucheza nao kwenye uwanja huo mwaka jana.
Hata hivyo mashabiki wa Simba wenyewe wanaamini wameenda Mbeya ili kukata mzizi wa fitina wa kutofungika kwa timu hiyo kwenye uwanja wao wa nyumbani na kutaka kuendeleza ilichokifanya Yanga kwa 'kuitengua udhu' walipoumana nao wiki mbili zilizopita jijini Dar na kuzima rekodi ya kutofungika kabisa licha ya kucheza Ligi Kuu kwa maraya kwanza msimu huu.
Makocha wa timu zote mbili wamenukuliwa wakitambiana kwamba leo ni leo, lakini kwa kuwa mpira ni dakika 90 mashabiki watakuwa na hamu ya kuona mechi hiyo itaishaje.
Simba chini ya makocha Zdrakov Lugarusic na msaidizi wake, Seleman Matola wameapa kupata ushindi ili kurejea kwenye nafasi ya tatu waliyoikalia kwa muda kabla ya Mbeya City kuirejea na kuirudisha Simba nafasi ya nne iliyokuwa inaikamata tangu duru la kwanza lilipoisha.
Kupoteza mchezo huo kunaweza kuitoa Simba kwenye kinyang'anyiro cha ubingwa msimu huu kazi inayowapa wakati mgumu vijana wa Logarusic kukaza msuli Sokoine.
Mbeya City nayo chini ya kocha Juma Mwambusi wameapa kutaka kuizima Simba ili kunyakua pointi tatu na kuzidi kusonga nafasi za juu ili kutimiza ndoto za kutaka kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu katika msimu wao wa kwanza kama walivyowahi kufanya 'kaka' zao Tukuyu Stars mwaka 1987.
Pia ushindi wowote kwa vijana wa Mwmbusi itamaanisha wanaziengua Azam na Yanga zilizopo juu yao na kukalia kiti cha uongozi angalau wiki nzima kwa kuwa itafikisha pointi 37 moja zaidi ya za Azam wanaoongoza sasa na pointi 36 na mbili zaidi ya Yanga wanaokamata nafasi ya pili kwa sasa.
Timu zote zinawategemea nyota wao kadhaa, Simba ikimtambia kinara wa mabao Amissi Tambwe, Ramadhani Singano 'Mess' na Haruna Chanongo, wakati Mbeya City inayoundwa na vijana zaidi ikiwategemea 'wauaji' wao Mwagani Yeya, Paul Nonga, Jeremiah Michael na mkongwe Stephen Mazamba.
Mbali na mechi hiyo iliyo gumzo kwa mashabiki wa soka nchini kote kwa sasa, leo pia kutakuwa na mechi nyingine tano, ambapo Ruvu Shooting itaikaribisha Coastal Union kwenye uwanja wa Mabatini-Mlandizi Pwani, huku Mgambo JKT itakuwa ugenini dhidi ya Rhino Rangers.
Mechi nyingine itazikutanisha timu za Oljoro JKT itakayokuwa uwanja wake wa nyumbani wa Sheikh Amri Abeid kuvaana na maafande wenzao wa JKT Ruvu, huku Ashanti Utd wataialika Kagera Sugar kwenye dimba la Chamazi  jijini Dar es Salaam na Mtibwa Sugar itaikaribisha Prisons-Mbeya uwanja wa Manungu.

Vita tupu Kombe la FA England

*Man City, Chelsea leo, Arsenal v Liverpool kesho

LIGI KUU ENGLAND Wikiendi hii itakuwa mapumzikoni ili kupisha michezo ya Raundi ya Tano za Kombe la FA ambapo kazi itaanza leo Jumamosi na kuendelea hadi Jumatatu.
Kubwa kwenye mechi hizo ni Big Match mbili leo Jumamosi na ile ya Jumapili ionayokumbushia mechi za Ligi Kuu ya England watu kutaka kulipizana kisasi. Leo Jumamosi, huko Etihad, Manchester City wataikaribisha Chelsea huku wakikumbuka kufungwa na Chelsea Bao 1-0, wiki iliyopita kwenye Mechi ya Ligi na Jumapili, ndani ya Emirates, Arsenal, watawaalika Liverpool ambao Jumamosi iliyopita waliinyuka Arsenal 5-1 huko Anfield kwenye Mechi ya Ligi.
Ni Kocha Yupi atalimwaga?? kati ya hawa! FA CUP
Raundi ya Tano

RATIBA:
Jumamosi Februari 15

Sunderland v Southampton
Cardiff v Wigan
Sheff Wed v Charlton
Man City v Chelsea

Jumapili Februari 16
Everton v Swansea
Sheff Utd v Nottm Forest
Arsenal v Liverpool
Jumatatu Februari 17
Brighton v Hull

Yanga na kazi nyepesi Comoro leo


WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga leo inatarajiwa kushuka dimbani ikiwa ughaibuni kwa kuumana na Komorozine ya Comoro katika pambano la marudiano la michuano hiyo.
Mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa kwenye uwanja wa Sheikh Said Mohamed International uliopo mji wa Mitsamihuli na Yanga ina kazi nyepesi ya kukamilisha ushindi mnono iliyopata katika mechi yao ya nyumbani ilipoisasambua Komorozine mabao 7-0.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Comoro zilizoripotiwa na mtandao wa klabu hiyo ni kwamba mara baada ya juzi jioni kufanya mazoezi mepesi katika uwanja mdogo wa hotel ya Retaj, Yanga ilijifua tena jana  asubuhi majira ya saa 5 ausbuhi katika Uwanja wa Sheikh Said kwa ajili ya kuuzoea tayari kwa ajili ya mchezo wa leo.
Kocha mkuu wa Young Africans Hans Van der Pluijm amesema anashukuru kikosi chake kipo vizuri kuelekea mchezo huo na hakuna mchezaji majeruhi hata mmoja hivyo anapata fursa ya kuchagua amtumie nani katika mchezo huo.
Akiongelea wapinzani timu ya Komorozine de Domoni amesema hawajaidharau kwa mechi ya leo kama watu wengi wanavyofikiria, kikubwa amewaandaa vijana wake waeze kufanya vizuri na kupata ushindi, "Kwangu mie hakuna mechi ndogo wala mchezo wa kirafiki" alisema Hans.
Young Africans itashuka dimbani kucheza mchezo huo wa marudiano ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 7-0 iliyoupata katika mchezo wa awali uliofanyika jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika mechi hiyo Mrisho Ngassa alitupia mabao matatu na kushika nafasi ya pili kwa wachezaji wanaoongoza kwa kufunga mabao mengi katika michuano hiyo, ambapo kama leo ataongeza jingine anaweza kujiweka pazuri katika kuwania kiatu cha dhahabu mwishoni ila kama Yanga itasonga mbele mbele ya Al Ahly ya Misri watakaoumana nao kwenye raundi ya kwanza.

Mario Balotelli aibeba Milan Seria A

The man: Balotelli is surrounded by his team-mates after scoring the winner over Bologna
Wachezaji wa AC Milan wakimpongeza Balotelli (45) baada ya kufunga bao pekee katika mechi ya Seria A jana usiku
MSHAMBULIAJI 'mtukutu', Mario Balotelli usiku wa kuamkia leo aliifungia bao pekee timu yake ya AC Milan na kuipa ushindi dhidi ya Bologna katika mechi ya Ligi Kuu ya Italia (Seria A).
Balotelli alifunga bao hilo dakika za lala salama likiwa ni bao lake la 10 msimu huu kwa shuti kali la mita karibu 30 na kuipa ushindi timu yake ambayo imekuwa ikichechemea kwenye ligi hiyo.
Nyota huyo anayeichezea pia timu ya taifa ya nchi hiyo alifunga dakika ya 86 akiwa ndani ya lango la wapinzani na kuifanya Milan kufikisha pointi  32 sawa na kurejea kwenye nafasi ya 10 nyuma ya Lazio.

Friday, February 14, 2014

Twiga Stars yalala 2-1 Zambia

Na Boniface Wambura, Lusaka
TWIGA Stars imepoteza mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) baada ya leo kufungwa mabao 2-1 na Zambia (Shepolopolo) kwenye Uwanja wa Nkoloma jijini Lusaka.
Hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika katika mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi Salma Mukansanga timu hizo zilikuwa suluhu.
Wenyeji ndiyo walianza kupata bao lililofungwa na Hellen Mubanga dakika ya 75. Mfungaji huyo aliyeingia kipindi cha pili nchini alimalizia wavuni mpira uliotemwa na kipa Fatuma Omari.
Dakika nne baadaye Zambia ambao walikuwa wakishangiliwa kwa nguvu na washabiki wao baada ya kufunga la kwanza, walipata bao la pili ambalo nahodha wa Twiga Stars, Sophia Mwasikili alijifunga mwenyewe.
Mwasikili alikuwa akijaribu kutoa nje mpira uliopigwa na nahodha wa Shepolopolo, Mupopo Kabange ambapo ulipishana na kipa Fatuma Omari kabla ya kujaa wavuni.
Bao la Twiga Stars lilifungwa na Donisia Daniel dakika ya 90. Beki huyo wa kushoto ambaye pia ni mchezaji wa Tanzanite alipanda mbele kuongeza mashambulizi ambapo akiwa nje ya eneo la hatari alipiga shuti lililomshinda kipa Hazel Nali.
Akizungumza baada ya mechi, Kocha wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage alisema amebaini upungufu katika kikosi chake ambao ataufanyia kazi kabla ya mechi ya marudiano ili timu yake iweze kusonga mbele.
“Kwa matokeo haya bado tuna nafasi ya kufanya vizuri kwenye mechi ya marudiano nyumbani na kusonga mbele,” alisema Kaijage.
Twiga Stars iliwakilishwa na Fatuma Omari, Fatuma Bashiru, Donisia Daniel, Fatuma Issa, Evelyn Sekikubo, Sophia Mwasikili, Vumilia Maarifa, Mwapewa Mtumwa/Amina Ali, Asha Rashid, Etoe Mlenzi/Zena Khamis na Shelida Boniface.
Timu hiyo inarejea nyumbani kesho kwa ndege ya Fastjet ambapo itatua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 7 kamili mchana.

Juan Mata afunguka kuhusu Mashetani Wekundu


368919_heroa
Mchezaji ghali zaidi kuwahi kununuliwa na klabu ya Manchester  United, Juan Mata amesisitiza kwamba ana furaha kucheza kwenye sehemu wowote uwanjani atakayopangwa na mwalimu wake na amebakia mtu mwenye furaha tangu alipojiunga na klabu hiyo mwezi uliopita.

Mhispania huyo ambaye amecheza mechi zote nne tangu alipojiunga na timu, na ameiwezesha timu yake kufunga mabao matatu na kuhakikisha inapata pointi 5, huku akichezeshwa kwenye namba tofauti na kocha David Moyes.
Moyes ameshamchezesha Mata kwenye winga zote mbili, amecheza nyuma ya mshambuliaji, lakini kiungo huyo mwenye miaka 25 hana chaguo lolote la sehemu ya kuchezeshwa anachojali ni kuisadia timu yake kushinda.
“Maisha yangu yote ya soka nimekuwa nikicheza upande wa kushoto, kulia na nyuma ya mshambuliaji,” Mata aliwaambia waandishi wa habari.
“Sijali wapi nachezeshwa na kocha wangu. Nina furaha nipo kwenye klabu kubwa sana na nina matumaini tutamaliza msimu vizuri.
“David de Gea amenisaidia kupazoea hapa, pia Chicharito, [Antonio] Valencia, na Rafael, wote wanaongea kihispania na wamenisaidia.”

TFF ya Jamal Malinzi yarejesha Kombe la Taifa kivingine

Rais wa TFF, Jamal Malinzi aliyetangaza mikakati ya kuikwamua Tanzania soka la kimataifa
MASHINDANO maalumu ya mikoa ya kuunda kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi Februari 22 hadi Machi 5 mwaka huu, huku ikiigharimu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) takribani Sh. Milioni 360.
Michuano hiyo maalumu itashirikisha mikoa wanachama ya TFF na itakuwa ikichezwa kwa mfumo wa nyumbani na ugenini kwa timu mbili za kanda moja kuchuana na inatarajiwa kutoa wachezaji bora 60 wataoweka kambi ya siku 30 Tukuyu, Rungwe mkoani Mbeya.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Rais wa TFF Jamal Malinzi amesema michuano hiyo ni maalumu kwa ajili ya kuuunda upya kikosi bora cha Stars, ili kiweze kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika mwakani nchini Morocco.
Malinzi alisema jumla ya timu 32 za Tanzania nzima zitashiriki michuano hiyo, kila mechi moja watakuwepo wasaka vipaji watano ‘Scouts’ kwa ajili ya kumulika wachezaji bora, pia mechi zote zitakuwa zikirekodiwa.
Baada ya zoezi la kuibua vipaji kwenye michuano hiyo, wasaka vipaji wote watajifungia (retreat) kwa muda wiki moja mjini Lushoto, Tanga kupitia rekodi zote za mechi na kuchagua wachezaji 60 bora, ambao watapelekwa Tukuyu, Mbeya kwa ajili ya mazoezi makali na wataalamu mbalimbali.
Wachezaji hao 60 watachujwa baada ya mwezi mmoja na kubaki 30, ambao watachanganywa na wachezaji wa sasa wa Taifa Stars na baadaye kupatikana kikosi bora kwa ajili ya mapambano ya kuwania kufuzu kwa AFCON.
Malinzi alisema wachezaji wa sasa wa Stars nao watakwenda kwenye kambi hiyo mkoani Mbeya mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) mwezi Aprili.
“Tunaamini mfumo huo utasaidia kupata vijana wapya wa kuboresha kikosi cha Stars, hatutachagua majina wala kuangalia umri kwa kuwa hiki ni kipindi cha mpito na ni muda mchache umebakia kuelekea kwenye michuano hiyo,” alisema Malinzi.
Machi 5 mwaka huu Stars itashuka dimbani kuumana na Namibia katika mechi ya kirafiki inayotambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Rais wa TFF, Jamal Malinzi akikabidhi sehemu ya vifaa vya michezo kwa ajili ya michuano maalum ya kusaka kikosi cha Stars leo (Picha kwa hisani ya Lenzi ya Michezo)

Wakati huo huo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeanza rasmi mikakati ya kuiwezesha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kufuzu kwa Fainali za mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani baada ya kupanga mpango wa timu hiyo kuweka kambi nchini Uholanzi.
Kambi hiyo itakuwa ni maalumu kwa timu hiyo kuweza kujiandaa na hatua ya kufuzu kwa fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Morocco na kushirikisha jumla ya mataifa 16 yatakayofuzu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Rais wa TFF, Jamal Malinzi amesema endapo Stars itafanikiwa kupita katika hatua ya awali ya mchujo ikiwa itapangwa kwenye hatua hiyo, wamepanga kuweka kambi nchini Uholanzi ya timu hiyo, ili kujiandaa na hatua ya pili ya makundi.
Malinzi alisema wameamua kufanya hivyo ili kurudia historia ya mwaka 1980 ya Stars kufuzu kwa mara ya mwisho michuano ya AFCON, iliyofanyika nchini Nigeria, ambapo Stars iliweka kambi Uholanzi mwaka 1979 na kufanikiwa kufuzu kwa fainali hizo.
“Tumepokea barua ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) inayotueleza kuwa mechi zetu za mchujo zitaanza kati ya mwezi Mei hadi Agosti kutokana na kiwango chetu kuwa chini ya nchi 21 bora za bara hili, hivyo muda si mrefu tunafikiria kurekebisha benchi lote la ufundi kwa pamoja na kuanza mikakati ya timu hiyo.
“Huenda timu yetu ikaanzia hatua ya mchujo kama CAF walivyotuandikia, ikifanikiwa kufuzu katika hatua ya makundi ttumepanga kuweka kambi nje ya nchi katika nchi ya Uholanzi, na huko timu itapata mafunzo ya kisasa ili kufanya vizuri kwenye hatua ya makundi,” alisema Malinzi.
Katika hatua nyingine alisema kwa sasa wameshazungumza na Balozi wa Uholanzi hapa nchini kwa ajili ya mipango yao hiyo, pia wamewataarifu wadhamini wakuu wa Stars, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chao cha Kilimanjaro Premier Lager ili kuandaa bajeti ya ziara hiyo. 

MECHI YA TWIGA STARS, ZAMBIA ‘LIVE’ ZNBC

Na Boniface Wambura, Lusaka
KIKOSI cha Twiga Stars kinashuka Uwanja wa Nkoloma, Lusaka nchini Zambia leo kuwavaa wenyeji Zambia (Shepolopolo) katika mechi ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) itakayooneshwa moja moja ‘live’ na televisheni ya Shirika la Taifa la Utangazaji la Zambia (ZNBC).

Mechi hiyo itaanza saa 9 kamili mchana kwa saa za Zambia ambapo Tanzania itakuwa saa 10 kamili jioni huku Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage akiwa tayari ametangaza ‘silaha’ zake kwa mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza.

Watakaoanza kupeperusha bendera ya Tanzania katika mechi hiyo ambayo kiingilio ni bure kwa majukwaa yote isipokuwa lile kuu ni; Fatuma Omari 1, Fatuma Bashiru 17, Donisia Daniel 2, Fatuma Issa 5, Evelyn Sekikubo 15, Sophia Mwasikili 16, Vumilia Maarifa 10, Mwapewa Mtumwa 9, Asha Rashid 14, Etoe Mlenzi 13 na Shelida Boniface 7.

Wachezaji wa akiba ni Maimuna Said 18, Fatuma Hassan 12, Zena Khamis 6, Esther Chabruma 8, Amina Ally 4, Therese Yona 11 na Happiness Hezron 3.

Sikinde yapiga mbizi baharini na kuibukia Kigamboni

Baadhi ya wapiga wa Sikinde wakiwajibika

BENDI kongwe ya muziki wa dansi, Mlimani Park 'Wana Sikinde' leo inatarajia kuvuka bahari ya Hindi na kwenda kufanya onyesho maalum la Siku ya Wapendanao 'Valentine Day' eneo la Mji Mwema Kigamboni.
Onyesho hilo litafanyika kufcuatia maombi ya wadau wa muziki wa dansi wa eneo hilo ambao wanataka kuishuhudia bendi hiyo ikifanya vitu vyake huko kwenye siku hiyo ambayo husherehekewa kote duniani Februari 14 ya kila mwaka.
Mratibu wa onyesho hilo, Michael Yona alisema kuwa amesikia maombi ya wakazi wa Kigamboni na sasa anawapelekea bendi hiyo kongwe ambayo ana uhakika itawaburudisha vya kutosha kwenye siku hiyo maarufu duniani.
"Sikinde wana nyimbo zao mpya kama Kiboyo, Nundu ya Ng'ombe, Kukatika kwa Dole Gumba, Jinamizi la Talaka, Tabasamu Tamu, Deni Nitalipa na nyingine nyingi ambazo nina uhakika itakuwa ni nafasi ya pekee kwa wakazi wa Kigamboni kuburudishwa na nyimbo hizo," alisema Yona.
Alisema kuwa nyimbo hizo ndizo zinazoandaliwa kwa ajili ya albamu mpya baada ya ile ya 'Supu Imetiwa Nazi' ambayo hadi sasa bado iko sokoni wakati wanamuziki wakiendelea kukuna vichwa ili kukamilisha vitu vipya.
Naye katibu wa bendi hiyo, Hamis Milambo alisema Sikinde alisema kuwa kwa muda mrefu haijafanya onyesho Kigamboni na kwamba ana uhakika wakazi wa eneo hilo wana hamu ya kuwaona Sikinde wakiwaburudisha.
"Kwanza kabisa ieleke kwamba Mlimani Park ni bendi ya watu wote wakiwamo wakubwa na vijana wadogo ambao naamini watakuja kuishuhudia kwenye onyesho hili la Siku ya Wapendanao," alisema Milambo.
Bendi hiyo ilirudia jina lake la zamani la Mlimani Parbk kutoka DDC Mlimani Parik baada ya kuachwa na Shirika la DDC na sasa inajitegemea.

Hassan Vocha kuwa Surprise mashabiki leo

 
MUIMBAJI mpya wa kundi la taarab lililorejea upya la Dar Modern 'Wana wa Jiji', Hassan Vocha, amewaahidi kuwafanyia 'mshangao' mashabiki wa kundi hilo watakaohudhuria utambulisho wake na wasanii wenzake unaofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Vocha na waimbaji wenzake kadhaa walionyakuliwa na kundi hilo lililowahi kutamba na vibao kama 'Pembe la Ng'ombe', 'Kitu Mapenzi' na 'Malavidavi' watatambulishwa leo 'Valantine Day' eneo la Magomeni.
Akizungumza na MICHARAZO, msanii huyo alisema ameandaa kitu 'spesho' kwa mashabiki wa muziki wa taarab katika onyesho hilo maalum.
"Kuna kitu maalum nimewaandalia mashabiki kwa ajili ya utambulisho huo ikizingatiwa onyesho litafanyika Siku ya Wapendanao', naomba waje ukumbini kujua kitu gani hicho," alisema Vocha.
Vocha aliyejipatia umaarufu mkubwa kupitia wimbo wake wenye jina hilo la 'Vocha' alichoimba na Dogo Aslay wakati akiwa Mkubwa na Wanae, alisema jukumu alililopewa kuvaa 'viatu' vya Hammer Q ni changamoto kwake.
"Najua ni changamoto kwangu, lakini kwa vile mimi ni msanii mwenye kipaji nitawapa burudani mashabiki wenye imani nami," alisema Vocha ambaye katika onyesho hilo ataimba karibu nyimbo zote alizoimba Hammer Q.
Uzinduzi huo wa Dar Modern utafanyika Travertine Hotel na kusindikizwa na makundi ya Kibao Kata na Baikoko ambapo Vocha atatambulisha nyimbo mbili alizorekodi katika albamu za kundi hilo za 'Oh My Sweet' na 'Ngoma Inapasuka'.

Thursday, February 13, 2014

News Alert! Imamu-Arusha amwagiwa 'tindikali'

IMAMU wa Msikiti wa Sawiyatu Qadiria, Hassan Bashir, akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, baada ya kumwagiwa inayodaiwa kuwa ni tindikali jana na mtu asiyefahamika baada ya mtu huyo kumwita kwa jina anayedaiwa alikuwa amevalia koti na kanzu. Inaelezwa wakati Imamu huyo anageuka ghafla ndipo alipomwagia bahati nzuri ilimpata tutawaletea habari baadae 

Tanzania, Ureno, Algeria zapaa orodha ya FIFA, Hispania bado kinara

TANZANIA imepanda kwa nafasi mbili katika orodha ya ubora wa viwango vya soka duniani kutoka nafasi ya 118 hadi nafasi ya 116, huku Hispania, Ujerumani na Argentina zikiendelea kubaki katika nazo za Tatu Bora kama ilivyokuwa katika orodha ya mwisho.
Kwa mujibu wa orodha mpya iliytotolewa leo la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) inaonyesha Ureno imepanda kwa nafasi moja toka nafasi ya tano hadi ya nne wakiporomosha Colombia, na Uswisi imepanda kwa nafasi mbili hadi nafasi ya 6 na Uruguay ikiangukwa kwa nafasi moja na kushika nafasi ya 7 juu ya Italia iliyoporomoka kwa nafasi moja pia.
Wenyeji wa michuano ya Fainali za Kombe la Dunia Brazil ilipanda kwa nafasi moja hadi namba 9 na timu inayofungia 10 Bora ya orodha hiyo mpya ni Uholanzi. Timu zilizopo kwenye 20 Bora ukiondoa 10 za kwanza ni pamoja na Belgium,Ugiriki,  Marekani, Chile, Engalnd, Croatia, Bosnia and Herzegovina, Ukraine, Ufaransa na Denmark imefunga dimba.
Kwa upande wa Afrika, Ivory Coast imeendelea kuongoza ikishika nafasi ya 23, huku Algeria ikipanda hadi nafasi ya pili Afrika kwa kukamata nafasi ya 26 na Cape Verde ikiweka rekodi ikikamata nafasi ya 27 na nafasi ya tatu barani Afrika, huku Ghana waliokuwa nafasi ya pili kwa muda mrefu nyuma ya Ivory Coast imeporomoka hadi nafasi ya 4 Afrika na Dunia ya 37.
Misri, inakamata nafasi ya 38 duniani na Afrika ikikamata nafasi ya 5 ikifuatiwa na Tunisia, kisha Cameroon, Nigeria, Mali na Burkina Faso    ikifunga dimba la 10 Bora.
Tanzania wenyewe wamepanda kwa nafasi mbili duniani kwa kushika nafasi ya 116 toka 118 iliyokuwa ikikamata awali na kwa Afrika inakamata nafasi ya 33.
Kwa upande wa CECAFA, Uganda inaendelea kuongoza ikifuatiwa na Ethiopia kisha Kenya ndipo Tanzania , Sudan, Burundi, Rwanda, Eritrea, Sudan Kusini, Somalia na Djibout

Extra Bongo yaibomoa Twanga Pepeta

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEi_thGkmsIrUaJZWJqet-LSegNzvnbsCbEG3Jit2hZQ_xSn2L7PSe0RzFpOjQHOlexM2dfpT-CY4xNZSJNvTSOiAY-j31q0A5lPppz310NhtGlGN5rptXa5P_dpG_6a-t_BOyGnsdHpPo0/s640/EXTRA5.jpg
'Mtoto karudi nyumbani' Rapa Grayson Semsekwa
UONGOZI wa wakali wa muziki wa dansi nchini Extra Bongo ‘Next Level Wazee wa Kimbembe’ umemrejesha kundini aliyewahi kuwa rapa bendi hiyo Greyson Semsekwa sambammba na kumnyakuwa mnenguaji Asha Sharapova kutoka bendi ya African Stars Twanga Pepeta.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Msemaji wa bendi hiyo Juma Kasesa, alisema, kurejea kwa Semsekwa mmoja ya wanamuziki waasisi wa Extra Bongo kutaimarisha safu ya 'kufokafoka' kuelekea kwenye uzinduzi wa albamu yao mpya ya 'Mtenda Akitendewa.'

Kwa mujibu wa Kasesa, Mtenda Akitendewa inatarajiwa kuzinduliwa Februari 22 mwaka huu kwenye Ukumbi wa Dar Live, uliopo Mbagala Zakhiem  jijini Dares Salaam.

Semsekwa alishiriki kwa kiwango katika albamu ya 'Mjini Mipango' mwaka 2009 kabla ya baadae kutimkia Twanga Pepeta na sasa amerejea kundini akiwa na rapu mpya ambazo atazimbulisha Jumamosi hii katika onyesho maalumu la Utambulisho wao litakalofanyika katika Ukumbi wa Meeda Sinza.

Alisema, wameamua kumchukua Sharapova baada ya kutambua kipaji alichonacho katika unenguaji hivyo kukidhi vigezo vya kunengua kwenye bendi hiyo inayoundwa na wanenguaji wakongwe kama Maria Salome na Otilia Boniface chini ya ukufunzi wa Super Nyamwela.

"Tunaendelea na mikakati ya kujiimarisha kwakuwa kila maboresho tunayofanya kwenye bendi pia tunazingatia maoni na ushauri wa wapenzi na wadau wa Extra Bongo ili kuendelea kuwapa burudani inayowasuuza nyoyo zao,"alisema Kasesa.

Aliwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi Jumamosi hii kwenye onyesho la bendi hiyo Meeda kuona muonekano mpya wa Semsekwa na Sharapova baada ya kutoka Twanga Pepeta.

Yanga watua Comoro tayari kwa vita

baadhi ya wachezaji wa Yanga wakishangilia moja ya mabao yao
MABINGWA watetezi wa Ligi kuu Tanzania Bara, Yanga wamefika salama mjini Demoni, nchini Comoro tayari kwa mchezo wa marudiano Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji Komorozine siku ya Jumamosi.
Taarifa kutoka nchini humo inasema kuwa kikosi hicho chenye wachezaji 19 wamefika salama tayari kwa mechi hiyo ya mkondo wa pili.
Yanga iliyoondoka mapema leo, imetua nchini humo ikiwa na matumaini makubwa ya kusonga mbele, baada ya kuichapa Komorozine mabao 7-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.
Iwapo Yanga itahitimisha vyema kampeni yake hiyo, itakutana na mabingwa watetezi, Al Ahly mwezi ujao.