 |
Samuel Ruhuza (kulia) |
Na Suleiman Msuya
ALIYEWAHI kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha NCCR Mageuzi
Samuel Ruhuza amesema uelewa mdogo na posho wanaopokea wajumbe wa Bunge
la Katiba ndicho chanzo kikubwa kinachosababisha kutohairishwa kwa bunge
hilo linaloendelea Mkoani Dodoma.
Ruhuza alisema hayo wakati
akizungumza na mwandishi wa habari hii jijini Dar es Salaam ambaye
alitaka kujua nini mtazamo wake juu ya Bunge la Katiba.
Alisema
uelewa wa katiba ni changamoto kwa wananchi walio wengi ila inatia shaka
pale ambapo wawakilishi wao katika bunge lao wanakuwa na uelewa mdogo
zaidi na kinyume chake ni kutoa kauli za kashfa na sio za kujenga hoja
ambazo zinaweza kuleta katiba nzuri.
Katibu Mkuu huyo wa zamani
alisema kwa asilimia kubwa ya wajumbe wa bunge hilo wanaonekana ni watu
ambao wanafikiria maslahi yao jambo ambalo linaweza kupatikana kwa
katiba isiyo na tija kwa wananchi na nchi kwa ujumla.
Alisema wapo
wajumbe hasa wa chama tawala (CCM) ambao wanaonekana kuwa wameambiwa
maneno ya kusema jambo ambalo si haki kutokana na ukweli kuwa kilichopo
kwenye rasimu ni maoni ya wananchi na sio chama.
“Mimi nimekuwa
nikifuatilia tangu Bunge hilo lilivyo anza tatizo kubwa ni baadhi ya
wajumbe hasa kutoka CCM wanaonekana kuwa hawajaenda pale kama wao ila
wapo kutokana na msimamo wa chama jambo ambalo sahihi.”, alisema Ruhuza.
Ruhuza
alisema pamoja na uelewa mdogo juu ya utengenezaji katika posho pia ni
sababu kubwa ambayo inachangia kutohairishwa kwa bunge hilo ambalo
limekosa mvuto kwa jamii ya Watanzania.
Alisema iwapo posho
isingekuwepo ni dhahiri baadhi ya wajumbe ambao sio wanachama wa CCM
wasingeendelea kujadili lakini ni ukweli kuwa 300,000 sio ndogo kwa siku
hivyo ni vigumu kuikataa kama huna uzalendo na nchi yako.
Aidha
alisema katika kuthibitisha hilo ni katika suala la muda wa wabunge
kuwepo katika madaraka kwa kipindi cha miaka kumi na tano ambapo
wamekiondoa na kusahau kuwa Rais yeye ana kikomo cha uwepo wa nafasi
hiyo.
Ruhuza alisema ni wazi kuwa wabunge wengi waliopo katika bunge
hilo wanatetea maslahi yao na sio jambo ambalo linaweza kukosekana au
kupatikana katiba ambayo itakuwa na maslahi kwa jamii.
Katibu huyo
alisema ni vigumu rasimu ya katiba iliyopendekezwa na tume ya katiba
kukubalika kwa wanasiasa kutokana na ukweli kuwa inagusa maslahi ya
wanasiasa wengi ambao wapo katika Bunge la Muungano kutokana na
mazingira yasiyovutia watu wengi.
Alisema rasimu inataka kuwepo kwa
wabunge wawili kila mkoa na kuondolewa kwa viti maalum hivyo ni wazi
kuwa wajumbe waliowengi wataendelea kuipinga kwa kila njia kwa dhana
kuwa fulani akiingia madarakani atampatia nafasi.
Kuhusiana na
sintofahamu iliyopo juu ya idadi ya serikali ambazo zimependekezwa
alisema ni vema wananchi na viongozi wote wakatambua kuwa muungano
hauwezi ukawa kwa kila kitu hasa muungano wa Tanganyika na Zanzibar
ambao ulizaa Tanzania.
Alisema ni ngumu kuamni kuwa muungano upo
wakati ni wazi kuwa Rais wa Zanzibar analindwa na mwanajeshi kama
anavyolindwa Rais wa Muungano.
Katibu huyo wa zamani alisema ni
vigumu kwa wazanzibar kukubaliana na rasimu iliyopo kwani inawanyanganya
madaraka ambayo wamepewa na Katiba ya Zanzibar iliyopo sasa.
Ruhuza
alitoa rai kwa Watanzania kutambua kuwa wao ndio wanatakiwa kusimamia
maslahi yao wenyewe kwani wanasiasa hawawezi kuwa sahihi kwa kila jambo
ambapo alitolea mfano katika suala hilo la katiba wananchi wamekuwa
wakiambiwa mambo ambayo hayana tija kwa maslahi yao.