STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, June 7, 2013

Kaseba atamba kumnyuka Mmalawi kesho

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjFKxyn1zY5N0LdqD-e-U0vmTvTHRxMFaw14h7F1xRM5apKF6x1EdSsAEfYW5qjbiA4G1nJXaEGwTOENecckOdcCgwcNJN2_uZE5wh4UL_reh1bBEAcHHCNlBFXVJhst64EnmZwbvAOksE/s640/Japhet+Kaseba.jpg
Japhet Kaseba
 
 
Baadhi ya Mabondia watakaomsindikiza Kaseba atakapovaana na Mmalawi kesho
BONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchinim, Japhet Kaseba kesho anatarajiwa kupanda ulingoni kuzichapa na mpinzani wake kutoka Malawi, Rasco Chimwanza akiahidi kupata ushindi katika pambano hilo litakalofanyika kwenye ukumbi wa DDC Magomeni Kondoa, Dar es Salaam.
Mabondia hao wawili walipimwa uzito na afya zao leo zoezi lililosimamiwa na Anthony Ruta, Ibrahim Kamwe, Pendo Njau na Dk John Lugambila na kugundulika kuwa wote wapo fiti tayari kuonyeshana kazi kesho.
Katika upimaji huo, Kaseba amejinadi atamsambaratisha mpinzani wake katika raundi za mapema za mchezo huo.
Kaseba na Mmalwi huyo watasindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi ambapo Juma Fundi atapigana na Hassani Kiwale maarufu kama Moro Best,Joseph Onyanyo wa Kenya ataonyeshana kazi na Seba Temba wa Morogoro, huku Issa Omar 'Peche Boy'atavaana na Juma Seleman na michjezo mingine kadhaa.

Kim Poulsen aahidi ushindi ugenini kesho dhidi ya Morocco

Kocha Kim Poulsen

Kikosi cha Stars

Na Boniface Wambura, Morocco
TIMU ya taifa, Taifa Stars inatupa karata yake ya pili ugenini kwenye mechi za mchujo za Kombe la Dunia kwa kesho (Juni 8 mwaka huu) kuikabili Morocco (Lions of the Atlas) kwenye Uwanja wa Grand Stade hapa Marrakech, Morocco.

Ilipoteza ya kwanza ugenini dhidi ya Ivory Coast mwaka jana, na kushinda mbili mfululizo nyumbani dhidi ya Gambia na Morocco. Mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 3 usiku kwa saa za Morocco ni ya pili kwa Stars katika uwanja huo ambapo mwaka juzi ilifungwa mabao 3-1.

Washabiki wa Morocco wanaonekana kuikatia tama timu yao yenye pointi mbili tu nyuma ya Ivory Coast inayoongoza kundi hilo la C ikiwa na pointi saba ikifuatiwa na Tanzania yenye sita. Huo ni mtazamo wa washabiki, lakini kwa upande wa timu inaonekana imepania kujichomoa katika nafasi za chini.

Kwa upande wa Kocha wa Stars, Kim Poulsen amesema timu yake imepania mechi hiyo, lengo likiwa ni kuona inapata matokeo mazuri baada ya dakika 90 za mechi hiyo itakayokuwa chini ya refa Daniel Frazier Bennett wa Afrika Kusini.

Amesema timu yake itacheza kwa umakini na uangalifu kwa vile wanajua wapinzani wao wakicheza mbele ya washabiki wao watakuwa katika shinikizo za kushinda, jambo ambalo wamejiandaa kukabiliana nalo.

Kwa upande wa maandalizi, Kim amesema Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wadhamini wa timu hiyo Kilimanjaro Premium Lager wameiandaa vizuri kwani iko kambini kwa wiki tatu sasa na kupata mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan iliyochezwa wiki iliyopita nchini Ethiopia.

Stars iliifunga Morocco mabao 3-1 zilipokutana Machi 24 mwaka huu jijini Dar es Salaa. Lakini zilipokutana hapa Marrakech mara ya mwisho mwaka 2011, Morocco iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Kim amesisitiza kuwa kikosi chake kimepania kufanya vizuri katika michuano hii ya mchujo ya Kombe la Dunia, ha hiyo inathibitishwa na matokeo ya timu kadri inavyoendelea kucheza mechi za mashindano.

“Moja ya mipango yetu katika mechi hizi za Kombe la Dunia ni kushinda nyumbani, hilo hadi sasa tumelifanya kwa asilimia 100. Lakini ili tukae vizuri zaidi tumekuja hapa Morocco kwa lengo la kupata matokeo mazuri, ingawa tunajua mechi itakuwa ngumi,” amesema kocha huyo raia wa Denmark.

Kwa hapa Marrakech mechi hiyo imekuwa haizungumzwi mara kwa mara, na kubwa ni kuwa Wamorocco wengi wanaamini kuwa timu yao ambayo hadi sasa ina pointi mbili haina nafasi ya kusonga mbele katika hatua inayofuata ya michuano hiyo.


Arsenal yaridhia Wenger kumsajili Rooney


http://i.dailymail.co.uk/i/pix/2012/12/21/article-2251594-165E1B03000005DC-807_634x569.jpg
Wayne Rooney

http://static.guim.co.uk/sys-images/Football/Pix/pictures/2009/8/1/1249153548354/Arsene-Wenger-001.jpg
Kocha Arsene Wenger

KLABU ya Arsenal ya England imempa ruksa Meneja wake Arsene Wenger kumnunua mshambuliaji wa Manchester United, Wayne Rooney  endapo atahisi kuwa mchezaji huyo anahitajika kwenye klabu hiyo.
Mkurugenzi mtendaji wa Arsenal, Ivan Gazidis amenukuliwa na gazeti la The Sun akisema kuwa klabu yake ina uwezo wa kumnunua, Wayne Rooney kwa paundi milioni 25 na kumlipa mshahara wa paundi 200,000 kwa wiki sawa na anaolipwa kwenye klabu ya Manchester United kwa sasa .
Gazidis aliongeza kuwa, iwapo kocha wao (Wenger) atapeleka maombi ya kutaka kumnunua mchezaji huyo  bodi ya wakurugenzi haitakuwa na sababu ya kuyakataa kwa vile wanao uwezo wa kumnunua na kumlipa  mshahara huo mnono.
Rooney amekuwa kwenye wakati mgumu ndani ya klabu ya Manchester siku za karibuni juu ya hatma yakee Old Trafford baada ya kupeleka maombi ya kutaka kuuzwa mwishoni mwa msimu ulioisha hivi karibuni, huku klabu yake ikinyakua taji kwa kuwapokonya mahasimu wao Manchester City.
Hata hivyo duru za kimichezo zinasema kuwa, Rooney anajiandaa kubadilisha uamuzi wake wa kutaka kuondoka Old Trafford kwa kusalia baada ya kocha Sir Alex Ferguson kustaafu akitajwa hakuwa na uhusiano mzuri naye kwa siku za karibuni.
Tangu ilipotangazwa nia yake ya kuondoka United, klabu kadhaa zimekuwa zikipigana vikumbo kumnyemelea mshambuliaji huyo tegemeo wa timu ya taifa ya England zikijiandaa kumnunua zikiwemo Arsenal na PSG , lakini wakisubiri kupata maafikiano na klabu yake ya sasa ya United.

Miss Kigamboni, Sinza, Mbeya kupatikana leo


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEi9yOYtTf6fzueqNlsH73yKCUSBSeVTNa7vumcj64AoXUic6tYCJnyfg5B8WormJKggH2bCA5_4zblvWCiaMWq_oCQT0Ks2fHyyi4M8WA7PtIoC3659MnuhVZp8ONatHK0g4f2gnIm8QcM/s1600/fm8.jpg
Bendi ya FM Academia itakayopamba shindano la Redd's Miss Kigamboni

MREMBO atakayefanikiwa kutwaa taji la kitongoji cha Kigamboni mwaka huu "Redd's Miss Kigamboni 2013" katika shindano litakalofanyika leo usiku kwenye ukumbi wa Navy Beach, Kigamboni atajinyakuliwa zawadi ya Sh.500,000, imeelezwa.
Maandalizi ya shindano hilo yamekamilika na warembo 12 kutoka sehemu mbalimbali jijini Dar es Salaam watapanda jukwaani kuwania taji hilo.
Akizungumza jana, mratibu wa shindano hilo, Somoe Ng'itu, alisema kuwa mrembo atakayeshika nafasi ya pili katika shindano hilo atapata zawadi ya Sh.300,000, mshindi wa tatu Sh.250,000 huku wawili watakaotangazwa kushika nafasi ya nne na ya tano kila mmoja ataondoka na Sh.200,000.
Somoe alisema kuwa warembo wengine saba waliobaki kila mmoja atapata kifuta jasho cha Sh.100,000.
Alisema bendi ya FM Academia maarufu Wazee wa Ngwasuma itatumbuiza katika shindano hilo ambalo kiingilio cha viti maalum ni Sh.10,000 na viti vya kawaida ni Sh. 5,000.
Warembo watano watakaoshika nafasi za juu kwenye shindano hilo watapata nafasi ya kushiriki kinyang'anyiro cha Redd's Miss Temeke baadaye mwaka huu.
Taji la Redd’s Miss Kigamboni linashikiliwa na Edda Sylivester ambaye pia ndiye mshindi wa kanda ya Temeke na alishika nafasi ya tatu katika shindano la Redd’s Miss Tanzania mwaka jana.
Aidha, shindano la Redds Miss Sinza pia litafanyika leo ambapo warembo 12 wanaowania taji la hilo watakapopanda jukwaani kwenye ukumbi wa Meeda Club kushindania taji hilo.
Mashindano hayo ambayo yamepangwa kuanza saa 1.00 usiku, yatashuhudia Redds Miss Tanzania, Brigitte Alfred akivua taji lake la kwanza katika usiku huo ambao utakuwa na burudani za kila aina. Mbali ya kuwa Miss Sinza, Brigitte  pia anashikilia taji la Redds Miss Tanzania.
Mratibu wa mashindano hayo, Majuto Omary alisema jana kuwa maandalizi yameshakamilika na bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' itatumbuiza siku kwa mara ya kwanza na kutoa zawadi kwa wakazi wa Sinza na vitongoji vyake.
Wakati huo huo, Furaha Eliab anaripoti kutoka Mbeya kuwa warembo 12 kutoka katika wilaya mbalimbali za mkoa wa Mbeya watachuana kuwania taji la Redd’s Miss Mbeya yatakayofayika kesho.
Akizungumza na waandishi wa habari, muandaaji wa mashindano hayo, Gabriel Mbwile, alisema kuwa mashindano hayo yatafanyika kesho kwenye viwanja vya City Pub vya jijini Mbeya na yatapambwa na msanii wa kizazi kipya, Bob Junior, maarufu kama Rais wa Masharobaro.
Alisema mshindi wa kwanza atajinyakulia zawadi ya Sh. milioni 1, mshindi wa pili Sh.750,000 na wa tatu Sh.500,000.

Thursday, June 6, 2013


WAPINZANI WA MIYEYUSHO, MASHALI WAFAHAMIKA KUPIGANA NAO TAMASHA LA USIKU WA MATUMAINI UWANJA WA TAIFA

Bondia Thomas Mashali (kulia) akitia saini ya dole gumba kwenye mkataba wa kupambana kwa ajili ya kuchangia elimu siku ya Tamasha la Usiku wa Matumaini litakalofanyika Julai 7, mwaka huu katika uwanja mpya wa Taifa jijini Dar. Mashali atacheza na Bondia Patrick Amote kutoka Kenya. Tamasha hilo litawashilikisha wasanii mbalimbali pamoja na wabunge. Kushoto ni Rais wa TPBO, Yasin Abdallah.
Bondia Francis Miyeyusho (kulia) akisaini mkataba kwa ajili ya mpambano wake na Bondia Shadrack Muchanje kutoka Kenya katika Tamasha la Usiku wa Matumaini. Kushoto ni Rais wa TPBO, Yasin Abdallah.
Thomas Mashali akipokea sehemu ya fedha za maandalizi kwa ajili ya mpambano wake na Bondia Patrick Amote katika Tamasha la Usiku wa Matumaini.
Bondia Francis Miyeyusho (kulia) akipokea sehemu ya fedha za maandalizi kwa ajili ya mpambano wake na Bondia Shadrack Muchanje kutoka Kenya.

Ajali nyingine mbaya jijini Mbeya, 17 wanusurika kufa kiajabu





Daladala ambayo ilikuwa inatoka Mbalizi kwenda Songwe  yenye namba za usajili T 635 ALS ikiwa imeharibika vibaya Baada ya Ajali kutokea Eneo la Ifisi Mbalizi Mbeya
Hapa ndipo eneo ambalo Daladala iliingia wakati ilijaribu kulipita Gari lengine akiwa mwendo kasi na kuukutana na Tela la Mafuta
Daladala upande wa nyuma
 Lori aina ya Scania yenye namba ZA usajili T378 AGD likiwa limepaki Baada ya ajali hiyo kutokea

Mabaki ya daladala
Wananchi mbalimbali wakiwa wanashuhudia ajali hiyo iliyo tokea Ifisi Mbalizi Mbeya
Hivi ndivyo Daladala inavyo onekana upande wa Mbele baada ya Ajali kutokea


 Dereva wa daladala ambaye ndiye aliye sababisha ajali hiyo Nikutusya Mwanja akiwa anapelekwa chumba cha matibabu ya Haraka.

 
 Baadhi ya Majeruhi waliokuwemo katika ajali hiyo
Wakazi mbalimbali wakiwa katika Hospitali ya Ifisi Mbalizi Mbeya kutazama ndugu zao waliopata ajali.
Askari wa usalama barabarani wakiandikishana Dhamana na ndugu wa Dereva wa Daladala ili apate dhamana ya kutibiwa
*****************


WATU  17 wamenusurika kifo baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuharibika vibaya kufuatia ajali iliyohusisha Gari la abiria aina ya Toyota Hiace na Scania.
Ajali hiyo imetokea  leo majira ya Saa Saba Mchana katika eneo la Ifisi nje ya Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Ifisi(ICC) Mbeya Vijijini.
Mashuhuda  wa ajali hiyo wamesema gari la abiria Toyota Hiace lenye namba za usajili T 635 ALS likiendeshwa na Nikutusya Mwanja likitokea Mbalizi kuelekea Songwe iliingia kwenye Trela la Scania lililokuwa likitokea Tunduma kuelekea Dar Es Salaam.
Wamesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari ndogo ambapo Dereva alikuwa akijaribu kulipita gari lingine lakini mbele akakutana na Lori ambalo alipojaribu kulikwepa akaingia kwenye Trela lake na kupinduka vibaya.
Trela hilo lenye namba za usajili T 675 ACT likiwa linavutwa na Kichwa chenye namba za usajili T 378 AGD halikuweza kuumia sana kutokana na kwenda kwa mwendo mdogo ambapo majeruhi wote wamekimbizwa katika Hospitale teule ya Ifisi kwa matibabu zaidi.
Muuguzi Msaidizi wa Hospitali Teule ya Ifisi Elimath Sanga amethibitisha kupokelewa kwa majeruhi 17 na kwamba kati ya majeruhi hao 3 hali zao siyo nzuri sana ingawa majina yao hayakuweza kupatikana.
Ameongeza kuwa majeruhi wengi wameumia sehemu za kichwani na miguuni na kwamba baada ya kumaliza kupatiwa huduma ya kwanza wataangalia ni wangapi wanaweza kuruhusiwa na wengine kulazwa.
Hata hivyo habari kutoka eneo la tukio zimesema kuwa Kondakta wa gari dogo aliyefahamika kwa jina moja la Ayubu alitoweka mara baada ya kutokea kwa ajali ingawa haifahamiki kama ni kurukwa kwa akili au ni kukimbia kesi.

Uholanzi yaingia Tano Bora, Tanzania yapaa FIFA

WAKATI Tanzania ikizidi kupaa katika viwango vya ubora wa soka duniani kutoka nafasi ya 116 hadi 109 ikiwa na maana imepanda nafasi saba, nchi ya Uholanzi imefanikiwa kuingia kwenye Tano ya orodha mpya iliyotangazwa na Shirikisho la Kimataifa la Soka, FIFA, huku nchi ya England ikiporomoka kwa nafasi mbili.
Katika orodha mpya nafasi nne za juu imeendelea kubaki vile vile kama ilivyokuwa mwezi uliopita ambapo Hispania ianongoza , ikifuatiwa na Ujerumani kisha Argentina na Croatia.
Ureno ya Cristiano Ronaldo imeshuka kwa nafasi mopja hadi nafasi ya sita, ikifuatiwa na Colombia, Italia, England na Ecuador.
Kwa ukanda wa Afrika Ivory Coast wameendelea kuongoza orodha ikiwa nafasi ya 13 duniani ikifuatiwa na Ghana iliyopo nafasi ya 21 duniani na Mali (23).
Ukanda wa Afrika Mashariki na kati, Uganda inaongoza ikishika nafasi ya 24 Afrika na 93 duniani ikifuatiwa na Ethiopia, kisha Tanzania iliyopanda kwa nafasi saba hadi nafasi ya 109 duniani na 32 Afrika.
Inayofuata baada ya Tanzania ni Kenya iliyolala jana 1-0 kwa Nigeria, kisha Burundi, Rwanda, Sudan, Eritrea, Sudan Kusini, Somalia na Djhibout inayoshika mkia.

Khadija Kopa amlilia mumewe akiwa Rukwa

Baadhi ya viongozi na wananchi wa mkoa wa Rukwa na Mpanda wakimsindikiza kuapanda ndege msanii wa taarab na malkia wa mipasho Tanzania ''Khadija Omar kopa'' kwenye uwanja wa ndege wa mpanda baada ya kupewa taarifa ya kufiwa na mumewe Jafari Ali Yussuf aliyefariki Dunia leo alfajiri kutokana na ugonjwa, Bi Khadija Kopa alikua akitokea kwenye Maadhimnisho ya siku ya Mazingira Duniani kitaifa yaliyoadhimishwa Namanyere Mkoani Rukwa jana.
Mkuu wa mkoa Rukwa Eng. Stalla Manyanya (kushoto) akimfariji msanii na taarab na malkia wa mipasho Tanzania, Khadija Omar Kopa alipokua kwenye chumba maalum cha kupumzikia wageni kwenye uwanja wa ndege wa Mpanda baada ya kupewa taarifa ya kufiwa na mumewe Jafari Ali Yussuf aliyefariki Dunia leo alfajiri kutokana na ugonjwa, Bi Khadija Kopa alikua akitokea kwenye maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani kitaifa yaliyoaadhimishwa Namanyere Mkoani Rukwa jana.
 
Chanzo:Masai Nyota Mbofu

Hatimaye Ngwair apumzishwa nyumba yake ya milele

BAADA ya siku kadhaa zilizokuwa na kila aina ya harakati, ugumu na majonzi makubwa, hatimaye mwili wa msanii Albert Mangweha 'Ngwair' umepumzishwa leo katika nyumba yake ya milele katika makaburi ya eneo la Kihonda Morogoro.


Kabla ya kuzikwa, wananchi wa Morogoro walipata fursa ya kuuaga mwili wake kwenye uwanja wa Jamhuri, ambapo
Umati mkubwa wa wananchi ulijitokeza kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Ngwair aliyefariki nchini Afrika Kusini, wiki iliyopita. 
Wasanii wengi kutoka Dar es Salaam nao wamehudhuria mazishi hayo.
16f11344cea711e2813a22000a1f8f34_7
75e8603ecea511e29ecd22000aaa08de_7
4406673ccea511e2850422000a1f9a85_7
“Marehemu Albert Mangweha azikwa kishujaa sana ni umati usioelezeka mungu akulaze mahali pema peponi,” ameandika Izzo B kwenye Instagram.

Naye Lady Jaydee kupitia Twitter ameandika: Mpk hapa tulipomsindikiza panatosha. Mungu amrehemu, kazi tumeimaliza. Life goes on.”
e1147594cea211e2a86422000a1f9839_7
ee9d94facea411e2a9ea22000ae81462_7
f18745b2cea411e2aa3022000a9e2931_7



Aidha msanii aliyekuwa na Ngwair nchini Afrika kusini Mgaza Pembe maarufu kama M to the P, naye alifanikiwa kutimba nchini na kumuaga 'swahiba' wake kabla ya kuzikwa baada ya awali kufichwa ukweli kuhusu kiofo cha mwenzake.

M to the P aliyekuwa amelazwa hoi hospitalini wakati Ngwair akiaga dunia, aliwasili nchini baadaya kupata ukweli wa mwenzake baadaya awali kufichwa kuwa ametangulia Dar wakati yeye alipokuwa hoi hospitalini na alishindwa kujizuia kumlilia rafikiye huyo wakati akiuaga mwili wa Ngwair leo mchana.
Inaelezwa alipewa taarifa na rafikie wa kike aitwaye Maggie baada ya kumdodosa sana ukweli kuhusu Ngwair na namna waliokuwa wakimtembelea hospitali alikolazwa walivyotoweka ghafla.
Chanzo:Mpekuzi Huru

Binti Michael Jackson anusurika kujiua, kisa...!


http://www.aceshowbiz.com/images/wennpic/paris-jackson-immortalized-handprint-ceremony-03.jpg
Binti wa MJ, Paris Jackson anayedaiwa kutaka kujiua

BINTI wa nyota wa zamani wa miondoko ya Pop duniani, Michael Jackson ambaye kwa sasa ni marehemu, Paris, 15,  amenusurika kujiua na kulazwa kwa sasa hospitali moja iliyopo mjini Carfornia.
Hata hivyo taarifa zilizonukuu mtandao wa kituo cha runinga cha ABC kinasema kuwa Paris anaendelea vyema kwa mujibu wa msemaji wa familia baada ya kupatiwa huduma na madaktari waliompokea.
Inaelezwa kuwa, binti huyo amekuwa katika sononi kubwa tangu baba yake alifariki Juni 2009 na ndicho kinachoelezwa kilimfanya kutaka kujiua.
Paris ni binti mkubwa wa nyota huyo wa zamani wa muziki duniani, ndugu zake wengine wakiwa ni Prince Jackson na Blanket ambaye ni binti mdogo kuzaliwa kati ya watoto hao watatu wa Wacko Jacko.

Haya ni baadhi ya magari aina ya Polaris Rangers RZR zitakazotambulishwa mbio za Puma Rally 2-13








http://www.totalmotorcycle.com/ATV-Quad/2010ATVmodels/2010-Polaris-RangerRZRSc.jpg

Taifa Stars yawatoa hofu Watanzania mechi dhidi ya Morocco

http://www.michezoafrika.com/NewsImages/Taifa-Stars-vs-Morocco.jpg
Thomas Ulimwengu akiwatoka wachezaji wa Morocco katika mechi ya awali iliyochezwa jijini Dar

BAADHI ya wachezaji wa timu ya soka ya taifa, TaifaStars wamewataka watanzania wasiwe na hofu yoyote dhidi ya pambano lao na wenyeji wao Morocco kwa kuahidi kuibuka na ushindi licha ya kucheza ugenini.
Stars inatarajiwa kuvaana na Morocco usiku wa Jumamosi nchini humo katika mechi ya mkondo wa pili kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazili.
Katika mechi ya kwanza ilioyochezwa Machi mwaka huu, Stars iliisambaratisha Morocco kwa mabao 3-1 na kuzidi kung'ang'ania nafasi ya pili katika kundi lao la C ikiwa na pointi 6, moja nyuma ya vinara, Ivory Coast ambayo itakuwa ugenini wikiendi hii kucheza na Gambia.
Licha ya kutambua ugumu wa mechi hiyo ya Jumamosi dhidi ya Morocco baadhi ya wacheza wa Stars wamewatoa hofu watanzania kwa kutamba kuwa ni lazima wawazime kwa mara nyingine Morocco japo wapo nyumbani kwao.
Mmoja wa wachezaji hao aliyezungumza na MICHARAZO kutoka Morocco ni Zahoro Pazi aliyerejeshwa katika kikosi hicho, alisema haoni sababu ya watanzania kuwa na mchecheto dhidi ya mechi hiyo kutokana na namna wachezaji wa Stars walivojiandaa.
Pazi alisema wachezaji wote wana ari na morali kubwa ya kuhakikisha wanaipa Stars ushindi mbele ya wenyeji wao kwa nia ya kujiweka nafasi nzuri kabla ya kuvaana na Ivory Coast katika mechi ijayo.
"Tunaendelea vyema na tunapenda kuwaambia watanzania nyumbani wasiwe na hofu, tutapigana kiume kuwapa raha na tunaamini Morocco watakaa Jumamosi hata kama watatucheza usiku," alisema.
Naye Himid Mao, alisema ushidni Jumamosi ni lazima kwa namna walivyofanya maandalizi na kujiamini kuwa wanaweza kurudia walichokifanya Tanzania kwa Morocco kwakuwalaza mabao 3-1.
Stars ambayo haijawahi kushiriki Fainali hizo za Kombe la Dunia, inahitaji ushindi ili kurejea nyumbani kuwasubiri Ivory Coast kabla ya kumalizia mechi za kundi lake Septemba mwaka huu dhidi ya Gambia ambao mpaka sasa wanaburuza mkia wakiwa na pointi moja tu.

Ruvu Shooting yamnyakua Mfungaji Bora FDL

http://www.greatfootball.com.ua/tanzania/logo-big/ruvu_shooting_stars.gif

BAADA ya kuwanyakua wachezaji wawili kwa mpigo Cosmas Lewis toka Azam na Elias Maguli kutoka Prisons-Mbeya,  maafande wa Ruvu Shooting imefanikiwa kumnasa mshambuliaji mwingine nyota, Jerome Lembeli kutoka kwa timu iliyopanda daraja ya Ashanti United.
Lembeni aliyewahi kuichezea Moro United na kutamba kwenye timu ya taifa ya vijana U17 ametua Ruvu kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kusainishwa juzi na uongozi wa klabu hiyo.
Msemaji wa Ruvu, Masau Bwire alisema kunyakuliwa kwa mshambuliaji huyo aliyeifungia Ashanti mabao 16 wakati wakiirejesha ligi kuu  kuna kusuidia kuimarisha safu ya ushambuliaji wa timu yake ambayo msimu uliopita haikuwa na bahati hasa ilipompoteza Abdallah Seif Karihe aliyepo Azam.
Bwire alisema rekodi za kuvutia za Lembeli ndizo zilizowafanya wamsajili katika muendelezo wao wa kuimarisha kikosi chao kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu 2013-2014.
Limbeli ndiye aliyeifungia Tanzania katika michuano ya U17 bao pekee walipotwaa ubingwa wa Dunia na pia alikuwa mfungaji wa pili katika michuano ya U17 ya Copa Coca Cola iliyofanyika Afrika Kusini akifunga mabao matano moja pungufu la mfungaji bora toka Nigeria.
Pia amekuwa akitoa mchango mkubwa katika  timu za taifa za Serengeti Boys na ilemya U20 tangu alipoanza kuitwa, mbali na kuichezea timu ya taifa mara kadhaa ilipokuwa chini ya kocha Marcio Maximo kabla ya kurejea kwao Brazili.
"Kwa sifa hizo katika kufumania nyavu tumeona ni vyema tuwe naye na tumemsajili kwa mkataba wa miaka miwili tukiamini atatoa mchango mkubwa kwa kikosi cha timu yetu ambacho kimepania msimu ujao iwe tishio baada ya msimu huu kuteleza," alisema Bwire.
Klabu mbalimbali za soka kwa sasa zipo katika harakati za kuimarisha vikosi vyao baada ya kumalizika kwa msimu wa 2012-2013 ambapo ilishuhudiwa timu za majeshi zikichechemea na kuziacha timu za kiraia zikitamba ambapo Yanga ilikuwa bingwa, ikifuatiwa na Azam, Simba,Kagera Sugar, Mtibwa Sugar na Coastal Union zilizomaliza kwenyue Sita Bora.

CHANETA yateua katibu mkuu wa muda

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhPSKf8_wO8O8dSbKi_p0N0JZB5cEPqF9bBLrUQPAKeKW-W7pigpA4aLHh5l5WTWkDRtVLQKJHTkDWW3iyucmYpTe5S4qaub6iAXgJXs4QgUQq1w4q22gF_uGq31xjaE7j60qTteQGClfW0/s1600/9+netiboli.jpg

CHAMA cha netiboli chini (CHANETA) kimemteua Maimuna Mrisho kuwa katibu mkuu wa muda wa chama hicho hadi pale atakapopatikana wa kuajiriwa.
Uteuzi huo umefanywa na kamati ya utendaji ya chama hicho katika kikao kilichofanyika Juni mosi mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Katiba ya CHANETA, katibu huyo atakaa madaraka kwa muda wa miezi sita, hadi pale chama hicho kitakapopata katibu mkuu wa kuajiriwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa CHANETA, Anna Kibira alisema uteuzi huo umepitishwa na wajumbe wa kamati ya utendaji wakati wakiendelea na mchakato wa kupata katibu mkuu wa kuajiriwa.
Mbali na hilo, Kibira alisema katika kikao hicho pia walipitisha wajumbe wa kamati mbalimbali ambazo ni Kamati ya Mashindano, Kamati ya Shule na Vyuo, Kamati ya Ufundi na Mafunzo, pamoja na Kamati ya Fedha na Mipango.
Alisema mbali na kamati hizo, pia waliteuwa walezi watano wa chama na washauri watano ambao watashirikiana na uongozi katika utendaji wa kazi za chama hicho.
Alifafanua zaidi kuwa CHANETA pia likutana na chama cha netiboli cha Zanzibar (CHANEZA) Juni 2 kujadili mambo yahusuyo umoja wa michezo wa vyama hivyo.
Alisema moja ya maazimio waliokubaliana ni pamoja na kukitambua chama cha netiboli cha kimataifa (IFN), Netiboli Afrika (CANA) na chama cha netiboli cha Afrika Mashariki (EANA).
Alisema mambo mengine waliyokubaliana ni pamoja na kuteua timu ya taifa ya Muungano, ambayo itajumuisha wachezaji wa pande zote mbili, ikiwamo pia kuteua makocha wa timu hizo kutoka pande hizo.
Alisema kutokana na makubaliano hayo wameunda kamati ya pamoja ambayo itasimamia utekelezaji wa maazimio hayo ambayo itakuwa chini ya wenyeviti, watendaji wakuu, waweka hazina, na mjumbe mmoja kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na la Zanzibar, BMTZ.
Wakati huo huo, timu za Jeshi Stars, JKT Mbweni na Filbert Bayi zimetakiwa hadi kufikia Juni 10 ziwe zimethibitisha ushiriki wa mashindano ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki.

Chanzo:NIPASHE

Deluxe Modern Taarab yafyatua 3 mpya

Mwanahawa Ally 'Chipolopolo'
KUNDI jipya la muziki wa taarab la High Class maarufu kama Deluxe Modern 'Watoto wa Kujaribu' limekamilisha nyimbo mbili mpya na kufanya ifikishe jumla ya nyimbo tatu wanazoziandaa kwa ajili ya albamu yao ya kwanza.
Akizungumza na MICHARAZO asubuhi ya leo, Mkurugenzi wa kundi hilo Mwanahawa Ally 'Chipolopolo' alisema nyimbo hizo ni 'Acha Kazi Ufanye Kazi' na 'Mwenye Kunirusha Roho Huwezi'.
Mwanahawa alisema nyimbo hizo zimeungana na wimbo wao wa kwanza uitwao 'Riziki Ina Wakati' ambao umekuwa gumzo tangu ulipoanza kusikika hewani kwenye maonyesho yao ya kila wiki.
"Tumekamilisha nyimbo tatu ambao ni maandalizi ya kupakua albamu yetu ya kwanza, baada ya 'Riziki Ina Wakati' sasa tumeibuka na 'Acha Kazi Ufanye Kazi' na 'Mwenye Kunirusha Roho Huwezi," alisema.
Mwanahawa mtoto wa mwanamuziki wa zamani wa bendi za Urafiki Jazz, Bima Lee, Shikamoo Jazz na Msondo Ngoma anasema wamepanmga mpaka kufikia wakati wa sikukuu ya Idd wawe wameikamilisha albamu yao na kuizindua pamoja na kulizindua kundi lao lenye wasanii tisa.
"Tumepanga kabla ya Septemba tuwe tumeikamilisha albamu yetu na kuzindua kundi hilo ambalo maskani yake ni Keko," alisema Mwanahawa  aliyewahi kuyafanyia kazi makundi la Dar Modern, Zanzibar Stars na King's Modern.

Khadija Kopa afiwa na mumewe



MUIMBAJI nyota wa muziki wa taarab nchini,  Khadija Omar Kopa, amefiwa na mumewe kipenzi Jaffari Ally.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa MICHARAZO na muimbaji wa Five Star, Husseni Mohammed 'Hammer Q' ni kwamba Jaffar alifariki usiku wa kuamkia leo akiwa hospitalini.
Marehemu alikuwa anasumbuliwa na matatizo katika mfumo wa upumuaji na mpaka mauti yanamfika alikuwa amelazwa katika hospitali ya Lugalo jijini Dar es Salaam. 
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. AMEN.

Wednesday, June 5, 2013

Busara Agro Machinery kutambulisha magari mapya mbio za PUMA Rally Juni 14

Wadhamini wa mbio hizo za magari za Juni 14
Na Seleman Msuya
KAMPUNI ya Busara Agro Machinery Tanzania imesema itafungua mashindano ya mbio za magari za jijini Dar es Salaam kwa kutumia magari yao ya Polaris Range RZR ili kuweza kuyatambulisha magari hayo hapa Tanzania.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Mhandisi Oded Kit wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi huyo alisema lengo lao ni kuhakikisha kuwa magari hayo yanatambulika katika mashindano ambapo watakuwa wakifanya maandalizi ya kushiriki mashindano mbalimbali ambayo yatakuwa yakiandaliwa hapa nchini.
Alisema wameshashiriki katika mashindano yaliyopita hivi karibuni ya Arusha Enduro ambapo pia walikuwa kama wafunguzi wa njia ya mashindano lengo likiwa ni kutambulisha magari yao ambayo yamekuwa yakishiriki mashindano ya kimataifa.
Mhandisi Kit alisema Polaris Range RZR ni magari ambayo yanakimbia na imara hivyo wana uhakika kuwa yatafanya vizuri kwa siku za karibuni.
Alisema kampuni yao imedhamiria kuwawezesha madereva ambao wanahitaji kushiriki mashindano ambapo wametoa punguzo la asilimia 30% ya bei ya magari hayo ambayo yanatoka nchini Marekani.
Kit alisema mashindano ya magari yanahitaji maandalizi ya kutosha kuanzia dereva mwenyewe gari, na mahitaji mengine kutokana na ukweli kuwa ni kazi ngumu na ya kuhatarisha maisha.
“Tumesikia kilio chao hivyo tunawaomba waje ili waweze kupata magari imara kwa bei ndogo ambayo tumetoa punguzo la asilimia 30% hivyo tunaamini mtu yoyote akitaka anaweza kununua”, alisema.
Kwa upande wake Fundi Mkuu wa Busara Agro Machinery Denis Gastelleir alisema katika kuonyesha ubora wa magari yao wanatarajia kuwa na magari matatu ambayo yatashiriki katika mashindano ya magari ya PUMA ambayo yatafanyika kuanzia 14 hadi16 mwezi huu kwa kulometa 400 hapa jijini Dar es Salaam.
Alisema magari hayo ambayo yanatokea nchini Marekani yamekuwa yakishiriki katika mashindano mbalimbali kama Dakar Rally na mengine mengi yanayofanyika hapa duniani.
Katika hatua nyingine Kampuni ya mafuta ya PUMA Tanzania imejitolea kudhamini mashindano yam bio za  magari zitakazofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 14 hadi 16.
Hayo yamesemwa na Rais wa Chama Cha Magari Tanzania Nizar Jivan wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii jijini Dar es Salaam.
Alisema pamoja na kampuni hiyo ya mafuta ya PUMA pia zipo kampuni zingine ambazo zimejitokeza kudhamini mashindano hayo ambayo yatashirikisha madereva kutoka katika nchi mbalimbali za Afrika.
Rais huyo alizitaja kampuni tanzu katika kudhamini mashindano hayo kuwa ni pamoja na SUNVIC Express, D.B Shapriya , A TO Z, NIC, CMC, Automobile Ltd, Knight Support, M/S Busara Agro Machinery, New Africa Hotel, Monster Energy Drink, Hari Singh and Sons Ltd, Waljis Travel Bureau and Tazara Reailway.
Jivan alisema hadi sasa ni madereva 25 ambao wamethibitisha kushiriki katika mashindano hayo ambapo 18 ni Watanzania na 7 wanatoka nje ya nchi ambapo amewataka madereva wengine wenye sifa wajitokeze ila.
“Tarehe 14 hadi 16 tunatarajia kuwa na mashindano ya kukimbiza magari ambayo yatakuwa ni ya kilometa 400 na yatafanyika hapa Dar es Salaam ambapo tutatumia barabara mbalimbali tukianzia Tazara”, alisema.
Rais huyo alisema katika mashindano hayo kutakuwa na magari mbalimbali kama Subaru Impreza R14, Mistubish Evolution X, Subaru Impreza N12, Mistubishiu Evolution 8, Subaru Impreza MY04, Subaru Impreza MY03, Mistubish Evolution IX, Subaru Impreza MY06, Subaru LEGACY, Mistubish Galant VR4, Toyota CelicaGT-4, Mistubish EvolutionIV, Subaru Impreza GC8, Range Rover, Toyota Land Cruser, VW Beetle, Nissan 240Z na Toyota Spinter.
Naye Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mafuta ya PUMA ambao ndio wadhamini wa kuu wa  mashindano hayo Philippe Consaletti alisema wao wamejipanga kuendelea kudhamini mashindano hayo kama moja ya sehemu ya faida yao ambayo wanaipata hapa nchini.
Consaletti alisema katika kutekeleza hilo wanatarajia kudhamini mashindano ya mwaka ujao ambapo wameahidi kuwa yatafanyika mkoani Arusha wakati ukifika.
Kwa upande wake Kamanda wa Usalama Barabarani Kamishna Mohammed Mpinga amewahakikishia madereva na raia ambao watakuwa katika maeneo ambayo magari yatapita kuwa usalama utakuwepo.
Mpinga aliwataka raia kuzingatia na kufuata utaratibu ambao utakuwa unatumika ili kuepusha kero mbalimbali ambazo zinaweza kutokea.

Mabondia Francis Miyeyusho,Mashali kupamba usiku wa matumaini Taifa


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEinRhjpHSbCg9922iuKEu7yRGuZPivlZYKf5raXPv4zYh46zFQoJQ0-1Sh6iLAKEVHIbv3u3aFQ0lHTdlr_OU9lIuCGjNoDBHEDotXfejWXg0vtj6VvPMB_uhMfTLKiCj0cwmyJUrBGp-GB/s640/miyeyusho3.JPG
Francis Miyeyusho

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgtcm3L7pzcbja7bSnx_bJy-ImxGoBHRqZqfw5QUsg3g5ocnIaLOkRpz-LEPJGDUySKvqg1G_zJ11McXXzRECzzEm3xIIYxJrvk0zRrkugyCJ2Hx9PHrLbn-wMfi2SGRUeXMUb8SU9J0cg/s1600/IMG_5146.JPG
Thomas Mashali

MABONDIA nyota nchini Francis Miyeyusho na Thomas Mashali wanatarajiwa kupigana na mabondia kutoa nchi jirani za Kenya na Uganda katika kulinogesha Tamasha la Usiku wa Matumaini linalotarajiwa kufanyika Julai 7 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Tamasha hilo litakalofanyika kwa mara ya pili tangu kuanzishwa kwake linaratibiwa na kampuni ya Global Publishers na litasimamiwa na Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO).
Akizungumza na MICHARAZO, Rais wa TPBO-Limited, Yassin Abdallah 'Ustaadh' alisema  Miyeyusho bingwa wa Afrika wa uzani wa Bantam na Mashali bingwa wa Afrika Mashariki na Kati uzito wa Kati ndiyo watakaopamba usiku huoi utakaokuwa na burudani mbalimbali siku hiyo.
Ustaadh alisema mabondia hao wa Tanzania watapanda ulingoni siku hiyo kwenye uwanja wa Taifa kuzipigana na mabondia kutoka Kenya na Uganda ambao majina yao yatarajaiwa kuanikwa hivi karibuni.,
"Tumewateua mabondia Francis Miyeyusho na Thomas Mashali ili waweze kupambana na mabondia toka nje ya nchi kati ya Kenya na Uganda na kwa sasa tunaendelea na mawasiliano na vyama vya mchezao huo vya nchi hizo ili kupata majina ya wapinzani wa mabondia wetu," alisema Ustaadh.
Ustaadh alisema mabondia hao wa Tanzania hawatawaangusha Watanzania siku ya tamasha hilo ambalo mwaka jana lilishuhudiwa bondia Francis Cheka akimkimbia kwenye ulingo, bingwa wa Taifa wa PST, Japhet Kaseba.
Kama ilivyokuwa mwaka jana tamasha hilo la 'Night of Hope', lina lengo la kusaka fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni kwa wanafunzi wa kike nchini.

FM Academia kupamba Miss Kigamboni Ijumaa


Katika harakati za kumpata mrembo wa taifa atakayewakilisha nchi katika mashindano ya urembo ya dunia, baadhi ya vitongoji vya DSM vinaendelea na maandalizi ya kupata warembo wake ambapo vitongozi wa SINZA na KIGAMBONI vitapata warembo wake Ijumaa wiki hii yaani Juni 7, ambapo kwa shindano la Kigamboni bendi ya FM Academia 'Wazee wa Ngwasuma' wanatarajiwa kupamba kwa kutoa burudani. Shindano hilo la Redds' Miss Kigamboni 2013 linaratibiwa na mwanadada Somoe Ng'itu anayeoonekana hapo pichani juu.

Uchaguzi Mkuu wa BFT sasa Julai 7


Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga
UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT) ambao awali ulitangazwa ungefanyika mwishoni mwa Mei, sasa umepangwa kufanyika Julai 7, jijini Mwanza.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolea na BFT ikisainiwa na Katibu Mkuu wake, Makore Mashaga uchaguzi huo ufanyika sambamba na michuano ya Majiji ambayo nayo iliahirishwa mpaka Julai badala ya Mei kama ilivyokuwa imepangwa.
Taarifa hiyo inasema kuwa nafasi zitakazowaniwa katika kinyang'anyiro hicho ni Urais, Makamu wake, Katibu Mkuu, Mhazini na Wajumbe 9 wa Kamati ya Utendaji wa shirikisho hilo zitakazohusisha Kamati za Mipango na Fedha, Waamuzi na Majaji, Mashindano na Vifaa, Walimu, Ufundi na Utafiti, Kamati ya Uhusiano, Habari na Masoko,  Wanawake, Kamati ya Maendeleo ya Mikoa na Taasisi za Umma.
Kamati ya Tiba na Kamati za Maendeleo ya Vijana na Wachezaji.
Fomu za uchaguzi huo zimeshaanza kutolewa tangu leo Jumanne (04/06/2013) katika Ofisi za Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na zoezi litaendelea hadi Julai 7, ambapo ada za fomu hizo zimepangwa kulingana na nafasi ambayo mgombea atajitokeza kuiwania.
Kwa fomu ya kuwania nafasi ya Rais, ada yake ni Tsh. 150,000/=, Makamu wa Rais, Katibu Mkuu na Mweka Hazina kila moja ni Tsh. 100,000/=, wakati kwa nafasi ya Ujumbe kila fomu itauzwa kwa Tsh. 50,000/=
BFT imetoa wito kwa  watanzania wenye uwezo wa kuongoza michezo kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi kama zilivyoelezwa hapo juu.