STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, May 8, 2014

Man City yanusa ubingwa England, Sunderland yaendeleza maajabu yake

Dzeko akifunga bao
Dzeko akishangilia moja ya mabao yake na wachezaji wenzake wa Man City
Fabio Borini akishangilia bao lake lililoisaidia Sunderland kunusurika kushuka daraja
WAKATI Sunderland ikijihakikisha kusalia kwenye Ligi Kuu ya England baada ya kuitwanga West Bromwich kwa mabao 2-0, Manchester City imejiweka katika nafasi nzuri ya kunyakua taji la ligi hiyo baada ya kupata ushindi mnono nyumbani dhidi ya Aston Villa.
Manchester City iliyorejea kileleni ikiitoa Liverpool ilipata ushindi wa mabao 4-0 na kuwafanya wafikishe jumla ya pointi 83, mbili zaidi ya Liverpool huku ligi ikitarajiwa kumalizika mwishoni mwa wiki ambapo itahitaji ushindi kurejesha taji hilo kwenye himaya yao toka kwa wapinzani wao Manchester United waliolitema taji hilo walilowapokonya msimu uliopita.
Ikicheza kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Etihad, Manchester City ilipata mabao yake kupitia kwa  Edin Dzeko aliyefunga mabao mawili katika dakika za 64 na 72, Stevan Jovetic na Yaya Toure.
Katika mechi nyingine iliyochezwa pia jana, Sunderland ikiwa nyumbani iliweza kupata ushindi wake wanne mfululizo kwa kuilaza West Brom kwa mabao 2-0 na kujinasua kwenye janga la kushuka daraja ikiwaachgia kasheshe wapinzani wao, West Brom, Norwich City na Hull City.
Mabao yaliyoivusha salama Sunderland katika msimu huu baada ya kusota mkiani kwa muda mrefu yalifungwa na Jack Colback katika dakika ya 13 na Fabio Borini dakika ya 31 na kuifanya timu hiyo kufikisha jumla ya pointi 38 ambazo haziwezi kufikiwa na timu ya Norwich iliyopo nafasi ya 18 ikiwa na pointi 33 ligi ikiwa imesaliwa na mzungumzo mmoja tu siku ya Jumamosi.
Msimu wa Ligi Kuu ya England utakamilishwa siku hiyo ya Mei 11 kwa mechi kati ya Cardiff City vs Chelsea, Fulham vs Crystal Palace, Hull City vs Everton, Liverpool vs Newcastle United, Manchester City vs West Ham United, Norwich City vs Arsenal, Southampton vs Manchester United, Sunderland vs Swansea City, Tottenham Hotspur vs Aston Villa na West Bromwich vs Stoke City.
Timu za Fulham na Cardiff City zenyewe tayari zimeshaaga ligi hiyo na inasubiri timu moja ya mwisho za kurudi nao Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.

Tuesday, May 6, 2014

Pep Guardiaol apata mtetezi Bayern Munich

WINGA wa Bayern Munich, Arjen Robben anaona kwamba mambo yamekuzwa mno tangu walipotolewa katika nusu fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid.
Mabingwa hao waliokuwa watetezi walitolewa kwa jumla ya mabao 5-0, na kusababisha mbinu za ufundishaji za kocha Pep Guardiola kupingwa kufuatia kipigo cha 4-0 nyumbani katika mechi yao ya marudiano.
Wakiwa wameshatwaa ubingwa wa Bundesliga mapema zaidi katika historia msimu huu, kikosi cha Guardiola kinawania taji la pili la Kombe la 'FA' (DFB-Pokal), dhidi ya Borussia Dortmund katika fainali na Robben anaona kwamba hawastahili kusakamwa kama vile hamna walichofanya.

Uchaguzi Mkuu Simba Waiva, Hanspope ndiyo basi tena!

Zakaria Hanspope
MSAJILI wa Klabu na Vyama vya Michezo Nchini jana aliipitisha katiba ya klabu ya Simba lakini ikiwa imeondolewa kipengele cha 26 (4) kilichokuwa kimefanyiwa marekebisho na wanachama wa klabu hiyo ambao walifanya mkutano mkuu wao Machi 16 mwaka huu kwenye ukumbi wa Bwalo la Maafisa wa Polisi, Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Kugonga mwamba kwa kipengele hicho kunamaanisha kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba wa kuteuliwa, Zacharia Hanspoppe, hataweza kuwania uongozi ndani ya klabu hiyo.
Kipengele hicho kinachoelezea sifa ya mgombea kwamba ni lazima asiwe mtu aliyewahi kufungwa/ kutiwa hatiani kwa kosa la jinai, ndiyo kilimuondoa Hanspoppe aliyekuwa anawania uenyekiti katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2010 ambao ulimuweka madarakani Mwenyekiti, Ismail Aden Rage na wenzake.
Akizungumza jana jijini, Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kwamba kipengele hicho hakikufika kwa msajili na kiliondolewa na Kamati ya Katiba ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa sababu inapingana na katiba ya shirikisho hilo linalosimamia mchezo huo nchini.
Kamwaga alisema kuwa kukamilika kwa katiba hiyo ni fursa kwa klabu yao kutangaza tarehe mpya ya kufanya uchaguzi utakaowaweka madarakani viongozi wapya.
Kamwaga alisema kuwa marekebisho mengine ambayo yalifanyiwa marekebisho na wanachama wa Simba yamepitishwa mojawapo ni kiongozi wa juu sasa atajulikana kwa jina la Rais badala ya Mwenyekiti na kutakuwa na Makamu wa Rais.
Alisema kuwa mabadiliko yaliyopitishwa ni pamoja na kuundwa kwa Kamati ya Rufaa, Kamati ya Maadili na pia ndani ya kata moja sasa inaruhusiwa kuwa na tawi zaidi ya moja lakini liwe na wanachama kuanzia 50 na wasiozidi 250.
Pia Kamwaga alisema kwamba kati ya wajumbe watano wa watakaochaguliwa, nafasi moja itakuwa ni kwa mjumbe mwanamke na hiyo wamelenga kuleta mawazo ya jinsi hiyo ndani ya uongozi.
"Kuundwa kwa kamati hizi kunaashiria kwamba matatizo yetu ndani ya Simba yanaweza kumalizwa na kamati hizi kabla ya kuvuka ngazi nyingine," alisema Kamwaga.
Alieleza kwamba kufuatia katiba hiyo kusajiliwa, Kamati ya Uchaguzi ambayo iko chini ya Mwenyekiti wake, Damas Ndumbaro, inatarajia kukutana leo jioni kwa ajili ya kupanga tarehe ya uchaguzi na mchakato mzima utakaohusisha zoezi hilo.

Tanki la mafuta lateketea na kuleta hopfu Singida

BAADHI ya  wananchi wakipiga picha wakati tanki la mafuta la kampuni ya B. Clarke Haulege Construction, Tanki hilo ni mali ya Bw. Bundala Kapela wa Igunga ni namba T634 BCZ lenye vyumba vinne na uwezo wa kubeba lita 40.000 za mafuta ya Petroli lililipuka majira ya Saa 11:00 katika barabara kuu ya Dodoma Mwanza eneo la Shelui mkoani Singida wakati breki za tanki hilo upande wa kushoto zilipojam na kusababisha moto.
Jambo lililomfanya dereva wa roli lenye namba za usajiri T 164 CGF aina ya Scania lililokuwa likivuta tanki hilo kusimamisha na kukata haraka tanki hilo huku akiondoa haraka injini ili kuepusha madhara zaidi ambayo yangeweza kutokea.
Katika tukio hilo lililosababisha usumbufu mkubwa kwa abiria na msururu wa magari kushindwa kupita katika eneo hilo kutokana na moto mkubwa uliochanganyika na moshi kutishia usalama wa watumiaji wengine.
Hata hivyo baada ya moto kupungua kiasi askari wa usalama barabarani waliamuru magari yaanze kupitia pembeni mwa barabara hiyo ili kuendelea na safari. Hakuna mtu aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa katika tukio hilo.
 Angalia matukio zaidi ya picha hapo chini. 
(PICHA FULLSHANGWE-SHELUI-SINGIDA) 5 4 3 2 111 
Msururu wa magari ukiwa mkubwa katika eneo hilo baada ya kushindwa kupita kutokana na moto mkubwa uliokuwa ukiwaka. 10 
Wananchi na wasafiri mbalimbali wakitoka kuangalia tukio hilo. 8 
Askari wa usalama barabarani akihakikisha mambo yanakwenda sawana usalama unaimarishwa katika eneo hilo.

Liverpool yaduwazwa ugenini, ubingwa kwao ni majaliwa sasa!

Hekaheka uwanjani kati ya Crystal Palace na Liverpool jana
Liverpool wakipongezana baada ya kufunga moja ya mabao yao matatu

Suarez akioyesha makali yake kabla ya kufuga bao la tatu la Liverpool
MBIO za kuelekea kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England baada ya miaka 24 kupita kwa Liverpool imekutana na vikwazo baada ya usiku wa jana kung'ang'aniwa na timu ya Crystal Palace na kutoka sare ya mabao 3-3, huku Suarez akizidi kutikisa nyavu akifikisha bao la 31.
Liverpool waliokuwa ugenini walifanikiwa kuongoza zaidi ya nusu ya mchezo huo wakiwa mbele kwa mabao 3-0, lakini cha ajabu mabao yote yalikuja kurejeshwa na wenyeji na kufanya wagane pointi moja moja, ambazo zinawarejesha Liverpool kileleni lakini wakiweka rehani matumaini yao ya ubingwa msimu huu.
Wageni walianza kuandika bao la kuongoza lililofungwa na Joe Allen katika dakika ya 18 kwa kumalizia kazi nzuri ya nahodha wake, Steven Gerrard na kudumu hadi wakati wa mapumziko.
Dakika nane baada ya kuanza kwa kipindi cha pili Daniel Sturridge aliifungia Liverpool bao la pili kabla ya dakika mbili baadaye Suarez kufunga bao lake la 31 katika msimu huu na kuifanya timu yake iongoze kwa mabao 3-0.
Hata hjivyo wenyeji walicharuka na kurejesha mabao hayo kupitia kwa Delaney aliyefunga dakika ya 79 na Gayle aliyefunga mabao mawili katiika dakika ya 81 na 88 na kuiduwaza Liverpool ambao wamesaliwa na mchezo mmoja,huku wapinzani wao,Manchester City waliowaoindoa kileleni kwa sare hiyo ya jana wamesaliwa na mechi mbili wakiwa na pointi 80.
Ligi hiyo itaendelea tena leo kwa pambano moja kati ya Manchestert United iliyotoka kupokea kipigo cha baoa 1-0 toka kwa Sunderland itakapoumana na Hull City.

Network Love ya Ruvu Stars videoni

Kiongozi wa Ruvu Stars, Khamis Amigolas
BENDI ya muziki wa dansi ya Ruvu Stars keshokutwa inatarajia kuanza kurekodi video za nyimbo zao tatu ambazo zinaendelea kutamba kwenye vituo mbalimbali vya redio nchini.
Akizungumza na MICHARAZO mmoja wa viongozi wa bendi hiyo ya maafande wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Rogart Hegga 'Katapila' alisema kuwa video hiyo itahusisha nyimbo zao za 'Network Love', 'Spirit' na 'Jua Kali' ambazo ndizo zilizolitambulisha kundi hilo kwa mashabiki wa muziki baada ya kusukwa upya likiwahusisha wanamuziki mahiri nchini.
Baadhi ya wanamuziki walionyakuliwa na kundi hilo ili kulisuka upya ni pamoja na Hegga, Khamis Kayumbu 'Amigolas', Khadija Mnoga 'Kimobitel', Jojo Jumanne, Victor Nkambi na rapa Msafiri Diouf.
Hegga alisema kazi hiyo ya kurekodi video hizo itaanza wiki hii na zoezi hilo litakapomalizika wataingia studio kumalizia nyimbo zao tatu za mwisho za kukamilisha albamu yao ya kwanza waliyopanga kuizindua baadaye mwaka huu.
"Tumesitisha zoezi la kumalizia nyimbo zetu tatu za kuhitimisha albamu ili kurekodi video za nyimbo za awali na kazi hiyo itafanywa katikati ya wiki chini ya kampuni moja ya jijini Dar es Salaam," alisema Hegga.
Alisema nyimbo za mwisho walizokuwa wameanza kurekodi ni 'Kioo' utunzi wake kiongozi mkuu wa bendi hiyo, Khamis Amigolas, 'Chewa Original' wa Seleman Muhumba na 'Facebook' wa Mkuu wa Jukwaa, Victor Nkambi ambaye pia ni 'mpapasa' kinanda mahiri nchini.

Matumla, Miyeyusho kuyeyushana Jumamosi PTA

Miyeyusho na Matumla wakiwa katika pozi. Wawili haowatapigana siku ya Jumamosi pale PTA
MABONDIA Francis Miyeyusho 'Chichi Mawe' na mtoto wa bingwa wa zamani wa dunia, Rashid Matumla, Mohammed Matumla 'Snake Boy Jr' watapanda ulingoni siku ya Jumamosi kuchapana katika pambano lisilo la ubingwa.
Aidha, mabondia hao wanatarajiwa kupima uzito na afya zao siku ya Ijumaa kwenye ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni kabla ya kuvaana siku inayofuata kwenye ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam.
Mabondia hao awali walipangwa kupigana Aprili 26, lakini likasogezwa mbele ili kupisha pigano la Miyeyusho dhidi ya Mthailand Sukkasem Kietyngyuth ambaye alimchapa Miyeyusho kwa TKO ya raundi ya kwanza.
Akizungumza na MICHARAZO, Rais wa TPBO-Limited inayosimamia pambano hilo, Yasin 'Ustaadh' Abdallah alisema pambano hilo lipo kama lilivyopangwa siku ya Mei 10.
Ustaadh alisema mabondia wote wapo kambini kujiandaa kwa ajili ya pambano hilo la kukata mzizi wa fitina baina yao baada ya kuwapo kwa tambo za muda mrefu. Miyeyusho amejichimbia mjini Bagamoyo na mpinzani wake yuko jijini Dar.
Rais huyo wa TPBO-Limited alisema maandalizi ya pambano hilo lililoandaliwa na promota Ally Mwazoa na litakalokuwa na michezo kadhaa ya utangulizi, yanaendelea vizuri.
Ustaadh alisema mapambano ya utangulizi siku hiyo yatakuwa kama ifuatavyo; Simon Zablon dhidi ya Keis Amary (kg 60), Mane Patrick dhidi ya  Sadiq Abdul (kg 50), Kassim Gamboo dhidi ya Kassim Rajab (Kg55), Azizi Abdallah atapigana na Ide Mnali (kg 60) na mkongwe Rashid Ally dhidi ya Suma Ninja (kg 60).

Monday, May 5, 2014

SIMANZI! Kidume Sheikh Ilunga Hassan Kapungu afariki dunia

Sheikh Ilunga Hassan Kapungu enzi za uhai wake.
MMOJA wa Wanaharakati na viongozi machachari wa Kiislam,  Sheikh Ilunga Hassan Kapungu amefariki dunia usiku wa kuamkia leo kwa ugonjwa wa Kisukari jijini Dar es Salaam. 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Sheikh Mohammed Kassim, Marehemu Sheikh Ilunga ambaye kwa siku za karibuni alikuwa akiandamwa kutokana na DVD zenye hotuba zake za kusisimua za kiharakati zilizokuwa zikiwaamsha waislam kutambua na kutetea haki zao  amezikwa leo majira ya saa 10 jioni baada ya mwili wake kuswaliwa msikiti wa Kichangani. Magomeni.
Inna Lillah Waina Illah Rajiun, Sheikh Ilunga katangulia nasi tu nyuma yake kwa sababu Kila Nafsi ni Lazima Itaonja Mauti.

Juventus mabingwa wapya Italia

http://cdn.bleacherreport.net/images_root/slides/photos/003/467/801/hi-res-454028537-gianluigi-buffon-of-juventus-fc-celebrates-victory-at_crop_650x440.jpg?1386971109MABINGWA watetezi wa Italia, Juventus ambao usiku huu wataingia uwanjani kupepetana na Atalanta wamejihakikishia ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo, Seria A baada ya wapinzani wao Roma kupoteza 4-1.
Kipigo hicho kimeifanya Roma kusaliwa na pointi 85 na michezo miwili ambapo hata kama wakishinda mechi hizo hawataweza kuzifikia pointi ilizonazo Juve ambazo ni 93 na kuwafanya kibibi cha Turin kuingia uwanja wa nyumbani wakiwa tayari mabingwa wa Seria A.
Katika mechi nyingine za jana nchini humo, AC Milan iliwashikika adabu wapinzani wao wa jiji la Milan, Inter Milan kwa kuwalaza bao 1-0, huku Parma wakishinda nyumbani mabao 2-0 dhidi ya Sampdoria, Udenese ikishinda pia nyumbani mabao 5-3 dhidi ya Livorno, Torino ikiiduwaza  Chievo Verona kwa kuwalaza bao 1-0 na Genoa na Bologna zilishindwa kutambiana kwa kutofungana.

Suarez ashinda tena tuzo England

http://thebeastbrief.com/wp-content/uploads/fbl-eng-pr-man_city-liverpool_yat6982_33846537.jpgNYOTA ya neema imeendelea kumuangazia Mshambuliaji mahiri wa klabu ya Liverpool, Luis Suarez baada ya kutajwa tena kuwa Mchezaji bora wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini Uingereza. 
Strika huyo kutoka Uruguay, aliyefunga mabao mabao 30 (kabla ya mechi ya usiku huu)msimu huu katika Ligi Kuu na kuiwezesha timu yake kufukuzia taji la ubingwa toka walipofanya hivyo mwaka 1990. 
Suarez, 27, alipata asilimia 52 ya kura zilizopigwa na waandishi hao akimshinda nahodha wake Steven Gerrard, huku Yaya Toure wa Manchester City akishika nafasi ya tatu. 
Mshambuliaji huyo hiyo ni tuzo ya pili baada ya wiki iliyopita alitajwa kama mchezaji bora na Chama cha wachezaji wa Kulipwa nchini humo (PFA) anatarajiwa kupokea zawadi yake hiyo katika sherehe za chakula cha usiku zitakazofanyika jijini London Mei 15.

Sunday, May 4, 2014

Ruvu Shooting kama Azam yatema sita

Kikosi cha Ruvu kitakachopanguliwa wachezaji sita kutokana na pendekezo la kocha Tom Olaba
KOCHA mkuu wa Ruvu Shooting, Tom Olaba amependekeza wachezaji sita watemwe katika kikosi chake kitakachoshirikishi Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu ujao kutokana na utovu wa nidhamu.
Msemaji wa timu hiyo, Masau Bwire, aliiambia MICHARAZO kuwa, kocha Olaba katika ripoti yake ya msimu wa 2013/14 wa ligi hiyo, amependekeza wachezaji sita watemwe kutokana na utovu wa nidhamu na kushuka kwa kiwango cha soka.

Bwire hakuwa tayari kuweka wazi majina ya wachezaji hao hata hivyo. 
“Tutawataja muda ukifika,”amesema Bwire huku rungu hilo likionekana wazi litawakumba wachezaji waliotoroka kambini na kukimbilia Oman kwa ajili ya kufanya majaribio na wale waliotoroka kambini wakati timu ya 'maafande' hao wa Pwani ikijiandaa na mechi iliyopita dhidi ya Azam FC.
Aidha, katika mikakati ya kukisuka upya kikosi chao cha U-20 na timu ya wakubwa, uongozi wa umesema kutakuwa na majaribio ya wachezaji kati ya Mei 15 na 28 kwenye makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Mlandizi, Pwani.

“Mwenyekiti wa klabu, Kanali Nguge ameomba yeyote mwenye uwezo wa kucheza mpira, umri stahiki wa mpira, umbo na nidhamu kutoka sehemu yoyote nchini aje kushiriki majaribio hayo,” amesema Bwire.

Diamond, Jaydee wafunika tuzo za Kili Music Awards 2014

Diamond aliyeng'ara tuoz za Kill akimpita hata 20 Percent aliyetamba mwaka juzi

Comandoo Jide kama kawa
1. USIKU wa jana kulikuwa na utoaji wa tuzo za muziki ambapo kama kawaida Diamond amerejea kwa kishindo kwa kunyakua tuzo lukuki, sambamba na Jady Jaydee na Mzee Yusuph. Jisomee mwenyewe washindi wa tuzo hiyo kisha upime ukali wa wasanii hao watatu waliotajwa hapo juu.

WIMBO BORA WENYE VIONJO VYA ASILI YA TANZANIA - Bora Mchawi, Dar Bongo Massive
2. MSANII BORA CHIPUKIZI ANAYEIBUKA - Young Killer 
3. WIMBO BORA WA ZOUK - Yahaya, Lady Jaydee
4. WIMBO BORA WA AFRO POP - Number One, Diamond Platnumz
5. WIMBO BORA WA RAGGA / DANCEHALL - Nishai Chibwa Ft Juru
6. WIMBO BORA WA RAGGAE - Niwe na wewe, Dabo
7.WIMBO BORA WA TAARAB - Wasiwasi wako, Mzee Yusuf
8. KIKUNDI CHA MWAKA CHA TAARAB - Jahazi Modern Taarab
9. MWIMBAJI BORA WA KIKE  TAARAB - Isha Ramadhani
10. MWIMBAJI BORA WA KIUME TAARAB - Mzee Yusuf
11. WIMBO BORA WA KISWAHILI BENDI - Ushamba mzigo, Mashujaa Band
12. MWIMBAJI BORA WA KIKE BENDI - Luiza Mbutu
13. MWIMBAJI BORA WA KIUME BENDI - Jose Mara
14. RAPA BORA WA MWAKA BENDI - Furguson


15. BENDI YA MWAKA - Mashujaa Band
16. MWIMBAJI BORA WA KIKE, KIZAZI KIPYA - Lady Jaydee
17. MWIMBAJI BORA WA KIUME, KIZAZI KIPYA - Diamond
18. KIKUNDI CHA MWAKA CHA KIZAZI KIPYA - Weusi
19. WIMBO BORA WA RNB - Closer, Vanessa Mdee
20. WIMBO BORA WA HIP HOP - Nje ya Box, Nick wa Pili Ft Joh Makini & Gnako
21. MSANII BORA WA HIP HOP - Fid Q
22. WIMBO BORA WA KUSHIRIKISHA / KUSHIRIKIANA - Muziki Gani, Nay wa Mitego ft Diamond
23. WIMBO BORA WA AFRIKA MASHARIKI - Tubonge, Jose Chameleone
24. MTUNZI BORA WA MWAKA TAARAB - Mzee Yusuf
25. MTUNZI BORA WA MWAKA BENDI - Christian Bella
26. MTUNZI BORA WA MWAKA KIZAZI KIPYA - Diamond
27. MTUNZI BORA WA MWAKA HIP HOP - Fid Q
28. MTAYARISHAJI BORA WA NYIMBO WA MWAKA, TAARAB - Enrico
29. MTAYARISHAJI BORA WA NYIMBO WA MWAKA, BENDI - Amoroso
30. MTAYARISHAJI BORA WA NYIMBO WA MWAKA, KIZAZI KIPYA - Man Water, Combination Sound
31. HALL OF FAME, INDIVIDUAL - Hassan BItchuka
32. HALL OF FAME, INSTITUTION - Masoud Masoud
33. VIDEO BORA YA MUZIKI YA MWAKA - Number One, Diamond
34.WIMBO WA MWAKA - Number One. Diamond
35. MTUMBUIZAJI BORA WA KIKE WA MUZIKI - Isha Ramadhani
36. MTUMBUIZAJI BORA WA KIUME WA MUZIKI - Diamond

Friday, May 2, 2014

Kiwewe, Matumaini wapona kwa Injili

WACHEKESHAJI Robert Augustino 'Kiwewe' na Tumain Martin 'Matumaini' wameamua kugeukia muziki wa Injili wakijiandaa kuachia albamu yao iitwayo 'Nimepona'.
Akizungumza na MICHARAZO hili, Kiwewe anayetamba na kipindi cha 'Ze Comedy Show' alisema kuwa albamu hiyo itakuwa na nyimbo sita na imeshakamilika ikisubiri kuachiwa mtaani.
Kiwewe alisema wameamua kumtumikia Mungu kwa kuimba kama njia ya kumshukuru kwa yote aliyowatendea tangu walipoanza kujipatia umaarufu kupitia fani ya uigizaji.
"Tumeamua kumtumia Mungu kwa njia ya huduma ya nyimbo na tunaomba mashabiki wetu watuunge mkono mara albamu hiyo itakapoingia sokoni wakati wowote kuanza sasa," alisema.
Hata hivyo Kiwewe aliweka bayana kwamba pamoja  na kuimba muziki wa Injili, yeye hajaokoka kama 'patna' wake Matumaini ambaye kwa sasa ni Mlokole akisali Mito ya Baraka.
"Sijaokoka kwa sababu siyo kila aimbaye muziki wa Injili ameokoka, ila Matumaini yeye kaokoka," alisema.
Matumaini mwenyewe alisema albam,u hiyo wameirekodia katika studuio za Levon, zilizopo Kibamba jijini Dar na kuzitaja nyimbo zilizopo katika albamu hiyo kuwa ni 'Nimepona', 'Amani ya Bwana', 'Msukule', 'Nitakutangaza Bwana', 'Mungu' na 'Anaweza Yesu' na amepanda kuiachia wiki mbili zijazo.

Mabweni Shule ya Sekondari yateketea kwa moto

MABWENI saba ya wavulana wa Shule ya Sekondari Ivumwe, mkoani hapa, inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), yameteketea kwa moto na kuteketeza vifaa mbalimbali vya wanafunzi wa shule hiyo.

Moto huo ulizuka jana majira kati  ya saa tatu na nne asubuhi wakati wanafunzi hao wakiwa madarasani kuendelea na masomo yao.

Akitoa taarifa mbele ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi taifa, Abdallah Majura Bulembo, aliyefika mkoani hapa kujionea janga hilo, Mkuu wa shule hiyo, Emmery Muhondwa, alisema mbali na kuteketeza mabweni hayo, hakuna madhara ya kibinadamu.

Mwalimu Muhondwa alisema moto huo uliteketeza vitanda 93, magodoro 186, mashuka 372, blanketi 186, mabegi 186, matranker 186 pamoja na vitabu na madaftari, vyote vikiwa na jumla ya  thamani ya sh milioni 30.

“Katika kukabiliana na hali hiyo, tumewahamishia wanafunzi katika madarasa yaliyokuwa yanatumiwa na kidato cha sita ili walale humo, tumeazima magodoro 169 kutoka Shule ya Sekondari ya Loleza na tunawasiliana na wazazi ili wawanunulie nguo za kushindia na za shule huku tukiendelea kukarabati mabweni,’’ alisema Mwalimu Muhondwa.

Mwenyekiti wa jumuiya hiyo taifa, Bulembo, aliwapa pole wanafunzi na kuwataka wawe wavumilivu katika kipindi hiki.

Pia alitoa mchango aliouita wa dharura wa sh milioni tatu  kwa ajili ya ukarabati wa mabweni na mahitaji mengine ya haraka na kuahidi kuwashirikisha wadau wengine wa elimu ili kuwasaidia wanafunzi hao.

Mbali na mchango huo, alitoa tamko kuzitaka shule zote zinazomilikiwa na jumuiya hiyo kuwa na bima ya moto.

“Kuanzia sasa, suala la bima ya moto ni la lazima kwa shule zote za jumuiya ya wazazi wa CCM. Baraza Kuu tutakutana kwa dharura mjini Dodoma Mei 17, mwaka huu na tutakachokipata tutakileta haraka kwenu ili kusaidia janga hili la moto,’’ alisema Bulembo.

Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo, Dk. Victoria Kanama, alimshukuru mwenyekiti huyo kwa mchango wake.

“Tutahakikisha tunakarabati mabweni haya ndani ya mwezi mmoja na kufanya jitihada za kuongeza ufanisi wa ufaulu katika shule yetu,” alisema Dk. Kanama.

Ivumwe, ni kati ya shule zenye sifa ya kufaulisha ambapo katika mtihani wa utamilifu (Mock), kidato cha sita mwaka huu, shule hiyo imeshika nafasi ya pili kati ya shule 26 zilizokuwa na watahiniwa 30 Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Udaku Special

Bomu lingine laua watu 10 Nigeria


mlipuko
USIKU wa kuamkia leo Maafisa nchini Nigeria wametoa taarifa kuhusu mlipuko uliotokea na kuua watu 19 katika kituo cha basi katika mji mkuu wa taifa hilo Abuja.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa idara ya kushughulikia mikasa na hali ya dharura- FEMA- Abbas G Idriss, watu 60 walijeruhiwa vibaya lakini 6 kati yao wametibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani pia magari sita yameharibiwa katika mlipuko huo.
Mlipuko huo umetokea katika eneo la Nyanya ambao uko karibu na kituo cha basi ambako zaidi ya watu sabini waliuwawa katika shambulizi la tarehe14 mwezi Aprili.
nyanya 
Ripoti za awali zimesema kuwa watu kadhaa wameuwawa na wengine wengi kujeruhiwa,Waandishi wanasema kuwa mlipuko huo umesababishwa na bomu lililotegwa ndani ya gari,Mmoja wa walioshuhudia kisa hicho amesema aliona miili 20 ya watu waliouwawa.
Mpaka sasa hakuna kundi lililodai kuhusika katika shambulizi hilo lakini kundi la wanamgambo wa kiislamu la Boko Haram limewahi kutekeleza mashambulizi kama hayo mjini Abuja,Mengi ya mashambulizi ya Boko Haram yamekuwa yakitokea katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Bomu la tarehe 14 Aprili lilizua hofu kwamba huenda wanamgambo hao wameanza kupanua maeneo wanayoendeleza harakati zao.

Yanga yatoa ufafanuzi sakata la usajili wa akina Domayo Azam

Didier-Kavumbagu-na-Frank-Domayo-wakisaini-kuichezea-klabu-ya-Azam-FCUongozi wa klabu ya Young Africans unapenda kuwajulisha wanachama wake, wapenzi wa soka na wadau kwa ujumla kuwa taarifa za kuhama kwa wachezai wake Didier Kavumbagu na Frank Domayo kwenda kujiunga na Azam FC zisiwakatishe tamaa, ni mapenzi ya wachezaj wenyewe kwani walishakubaliana na uongozi kila kitu juu ya kuendelea kuitumikia Yanga kabla ya siku mbili hizi kuonekana wakiwa wamejiunga na wana ramba ramba.
Yanga tayari ina wachezaji watatu wenye mikataba inayoendelea na kama kanuni za VPL kwa wachezai wa kimataifa kuwa watatu zitatumika wachezaji Haruna Niyonzima, Hamisi Kizza na Emmanuel Okwi ndio watakaoendelea, hivyo uongozi uliomba mwongozo kwa TFF juu ya taratibu zitakazotumika kwa msimu ujao kabla ya kuwasainisha Kavumbagu na Twite.
Awali uongozi wa Yanga ulikuwa kwenye mazungumzo na wachezaji hao tangu mwanzoni mwa msimu wa 2013/2014 juu ya kuongezewa muda wa mikataba yao ili waweze kuendelea kuitumika Yanga kwa ajili msimu mpya ujao 2014/2015.
Didier Kavumbagu na Mbuyu Twite ambao mikataba yao ilikuwa mwishoni waliongea na uongozi tangu mapema mwaka jana mwezi wa Septemba juu ya kuweka sahihi zao na kuendelea kuitumikia Yanga na kukubaliana mambo yote ya msingi kikubwa kilichokuwa kinasubiriwa ni maamuzi ya TFF juu ya usajili wa wachezaji wa kigeni msimu mpya wa 2014/2015 kwani Azimio la Bagamoyo linapaswa kuanza kutekelezwa msimu huu
Uongozi wa Yanga uliandikia TFF barua mapema kuomba kupewa mwongozo wa kanuni zitakazotumika kwenye usajli kwa wachezaji wa kimataifa kwa msimu mpya kufuatia Azimio la Bagamoyo kuelekeza msimu huu kila timu inapasa kuwa na wachezaji watatu wa kigeni, mpaka sasa uongozi wa Yanga haujapata majibu juu ya utaratibu utakaotumika kwenye msimu wa Ligi Kuu ijayo.
Hivyo makubaliano ya wachezaji Didier Kavumbagu, Mbuyu Twite na uongozi wa Yanga SC yalikua yakisubira majibu ya TFF juu ya kanuni zipi zitakazotumika kwenye usajili msimu wa 2014/2015 kwa wachezaji wa kigeni na katika hali ya kushangaza Kavumbagu akaonekana tayari ameshasaini kuichezea timu ya Azam FC.
Kuhusu Frank Domayo aliyeripotiwa jana kujiunga na Azam FC pia alikuwa katika makubaliano ya kuongeza mkataa tangu mwezi Julai 2013, alikubaliana na uongozi juu ya mambo yote ya msingi na kilichobakia ilikuwa ni kuweka sahihi kwenye mkataba mpya, lakini Domayo alisema hawezi kusaini mpaka siku atakapokuja mjomba wake ambaye ndie wakala wake na ahadi hiyo iliendelea kwa muda wa mwaka mzima kabla ya jana kusikia ameshasaini timu nyngine.
Habari hizi zimewashitua wapenzi, wanachama na washabiki wa Young Africans lakini ukweli ni kuwa wachezaji wenyewe walishindwa kuwa wakweli kwa viongozi na mwisho wa siku walikua na mipango yao ya kuondoka, hivyo uongozi ulijtahid kadri ya uwezo wake lakini wachezaji wanaonekana hawakua tayari kuendelea kuichezea Yanga SC.
Taarifa kamili kuhusu mipango ya timu kwa msimu ujao pamoja na ripoti ya kocha mkuu Hans pamoja na benchi lake la Ufundi zitatolewa hivi karibuni baada ya benchi la ufundi na uongozi kukaa kwa pamoja na kuafikiana mipango ya msimu ujao.
Aidha uongozi wa Yanga SC unawaomba wanachama wake, wapenzi na washabiki wasiwe na wasi wasi juu ya kuondoka kwa wachezaji hao kwani Yanga bado ina nafasi wachezaji wengi wenye vipaji na itaendelea kuboresha kikosi chake kwa kuzingatia maelekezo ya kocha mkuu Hans katika usajli wa msimu ujao

Bonite Bottlers wagawa runinga kwa wateja wao

KAMPUNI ya vinywaji baridi ya Bonite Bottlers Ltd jana ilikabidhi zawadi za luninga mpya za kisasa aina ya Sony LED zenye upana wa inchi 32 kwa washindi 29 wa shindano la Jionee Mwenyewe Kombe la FIFA la Dunia.
Katika promosheni hiyo iliyozinduliwa mapema mwezi uliopita, Coca-Cola itapeleka Watanzania 14 kwenda kushuhudia mechi ya robo fainali ya Kombe la FIFA la Dunia nchini Brazil mwezi Julai. Vile vile Coca-Cola itatoa mipira 8,000 yenye nembo ya FIFA World Cup na fulana 30,000.
Waliobahatika kushinda luninga na kukabidhiwa zawadi zao jana ni Paulina Mushi, Gabriel Warance (mwanafunzi), Moun Johnson (IT Technician), Rispa Waziri, Sophia Paulo, Abela Solomon, Chediel G. Mziray, Asha Ramadhan, Godfrey Mollel na Jackson Shayo (wafanyabiashara) na Simon Mrema (mchimba madini).
Washindi wengine ni Faidha Elidaima, Costantine Urio, Magreth Mshana, Enna Mbwambo, Emmanuel Tarimo, Julius Kimaro, Amir Ali, Emmanuel Mwasha, Gerald Swai, Joseph Mushi na Martine Temu wakazi wa mji wa Moshi.
Akizungumzia ushindi wake Gabriel Warance ambaye ni mwanafunzi jijini Arusha alishukuru Mungu kwa kumuwezesha kushinda luninga. Vile vile aliishukuru kampuni ya Bonite kwa kuleta promosheni hiyo ambayo imewawezesha wale watakaobahatika kushinda kubadili maisha yao kwa namna fulani.
Washindi wengine pia hawakusita kuonyesha furaha yao na kusema kwamba wataendelea kushiriki kwa lengo la kuendelea kushinda zawadi zaidi. “Hii ni nyota njema kwangu na naamini Mungu aliyeniwezesha kushinda zawadi hii ana uwezo wa kunipa tiketi ya kwenda Brazil kushuhudia 'laivu' fainali za Kombe la FIFA la Dunia,” alisema Godfrey Mollel ambaye ni mfanyabihashara.
Akizungumza baada ya kukabidhi zawadi kwa washindi, Meneja Mkuu wa Mauzo wa Bonite Bottlers, Christopher Loiruk aliwashukuru wateja wa Coca-Cola na wananchi kwa ujumla kwa kuendelea kuburudika na vinywaji vya Coca-Cola.
“Kombe la FIFA la Dunia ndiyo mchezo wenye mashabiki wengi zaidi duniani. Kwa kushirikisha wateja wetu katika promosheni hii, Coca-Cola itawawezesha mashabiki wa soka nchini Tanzania kuungana na wengine duniani kote kusherehekea kwa pamoja burudani ya Kombe la Dunia 2014,” anasema Loiruk
Washindi wamepatikana kwa kunywa vinywaji vya Coca-Cola na kupata vizibo viwili vyenye kutengeneza neno Brazil pamoja na kizibo cha ushindi. Kizibo cha ushindi kina picha ya kitu ambacho mteja ameshinda (TV, mpira au fulana) wakati kizibo cha ushindi wa zawadi ya tiketi kina nembo ya ndege kikiashiria safari ya kwenda Brazili kushuhudia moja kwa moja mechi ya Kombe la Dunia.

Sevilla, Benfica zafuzu fainali za UEFA Ueropa League

Stephen M'Bia akiifungia Sevilla bao muhimu lililowapeleka fainali za Europa League
Wachezaji wa Benfica wakifurahia kufuzu fainali za Europa kwa mara ya pili mfululizo
KLABU za Benfica ya Ureno na Sevilla zimefanikiwa kufuzu fainali za Ligi Ndogo ya Ulaya (UEFA Ueropa League) baada ya kupata matokeo ya kusisimua ugenini dhidi ya Juventus na Valencia.
Benfica imepenya hatua hiyo kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuidindia Juventus mjini Turin na kutoka suluhu ya kutofungana na kufuzu kwa jumla ya mabao 2-1 yaliyopatikana kwenye mechi yao ya kwanza wiki iliyopita nchini Ureno.
Wareno hao ambao waliokuwa pungufu wachezaji wawili baada ya Enzo Perez  kupewa kadi ya pili ya njano na kufuatiwa na nyekundu dakika ya 67 na baadaye na Markovic kupewa nyekundu ya moja kwa moja dakika ya 89 sambamba na Vucinic wa Juventsu, hawajawahi kunyakua taji hilo licha ya kucheza fainali mbili za michuano hiyo sasa itavaana na Sevilla ya Hispania ambayo iliwaduwaza wenyeji wao Valencia kwa kufunga bao dakika za jioni wakati wenyeji wakionekana wameshatinga fainali za michuano hiyo.
Stephen M'Bia alifunga kwa kichwa bao muhimu kwa timu yake dakika chache kabla ya pambano hilo kumalizika na kuivusha Sevilla katika fainali hizo zitakazofanyika Mei 14 mjini Turin, Italia ambazo zitakuwa za tatu kwa timu hiyo baada ya kufanya hivyo mara mbili 2006 ilipotwaa ubingwa na na 2007.
Kabla ya hapo matumaini ya Sevilla yaliyeyuka baada ya wenyeji kuongoza kwa mabao matatu mpaka zikiwa zimesalia dakika 20 za mwisho.
Mabao ya Sofiane Feghouli katika dakika ya 14 na jingine la kujifunga kwa kipa wa Sevilla Beto katika dakika ya 26na lililowanyong'onyesha wageni katika dakika ya 70 kupitia kwa Jemery Flamin, liliwapa matumaini wageni kutinfa fainali hizo kabla ya M'bia kuwakata maini kwa bao hilo la jioni.
Matokeo ya mwisho yalikuwa 3-3, lakini Sevilla imefuzu kutokana na kupata ushindi wa mabao 2-0 nyumbani na hivyo bao la ugenini ilililopata limekuwa na faida kwao na sasa itavaana na Benfica.

Thursday, May 1, 2014

Msajili airejesha katiba ya Simba irekebishwe

Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo
Na: Genofeva Matemu – Afisa Mawasiliano Serikalini (WHVUM)
SERIKALI kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imemaliza kupitia Rasimu ya Katiba ya klabu ya Simba kwa ajili ya kuidhinisha katiba hiyo na kuifanya klabu hiyo kuendelea na taratibu za uchaguzi mkuu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Michezo Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. Leonard Thadeo alipokutana na waandishi wa habari kujibu hoja mbalimbali za waandishi leo jijini Dar es Salaam.
Akijibu moja ya hoja iliyomtaka kufafanua Wizara imefikia wapi katika upatikanaji wa Katiba ya Klabu ya Simba Bw. Thadeo amesema kuwa upitiaji wa Katiba umemelizika na kuonekana kuwa na mapungufu machache yanayohitaji kurekebishwa ili Wizara iweze kuidhinisha katiba hiyo.
“Mchakato wa upitiaji wa Katiba ya klabu ya Simba umemalizika jana lakini kumekuwepo na mapungufu machache yanayohitaji kurekebishwa ili Wizara iweze kuidhinisha Katiba hiyo” amesema Bw. Thadeo.
Akifafanua zaidi Bw. Thadeo amesema kuwa mapungufu hayo yanalenga zaidi upande wa kisheria ambapo mtu anaweza kutafsiri neno vibaya hivyo kupata maana tofauti na Katiba ilivyokusudia hivyo kuitaka klabu hiyo kufanya marekebisho hayo mapema na kurejesha Katiba hiyo Wizarani kwa ajili ya kuidhinishwa.
Aidha Bw. Thadeo amewataka waandishi wa habari pamoja na wanachama wa klabu ya Simba kuwa na subira ili waweze kupata Katiba itakayokidhi malengo ya klabu yao kwani mchakato wa upitiaji wa Katiba ulihitaji umakini.

Azam yazidi kuibomoa Yanga, yambeba Domayo

Kavumbagu na Domayo walitotua Azam baada ya mikataba yao Yanga kumalizika
BAADA ya kufanikiwa kumnyakua mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga, Didier Kavumbagu, klabu ya Azam imeendelea kuibomoa Yanga kwa kumsajili kiungo wa klabu hiyo ya Jangwani, Frank Domayo.
Domayo ambaye pia ni kiungo wa timu ya Taifa (Taifa Stars) ameingia mkataba wa miaka miwili na mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Bara.
Kiungo huyo aliyejijengea umaarufu mkubwa klabuni hapo msimu huu akimuweka benchi nahodha wa timu ya taifa ya Rwanda, Haruna Niyonzima, amesajiliwa kutokana na kupendekezwa na kocha wa Azam, Mcameroon Joseph Omog.
"Domayo ameshasaini. Ni katika kukamilisha maelekezo ya kocha," alisema Katibu Mkuu wa Azam, Nasoro Idrisa.
Kusajiliwa kwa Domayo, kijana mdogo mwenye kipaji, kumekuwa ni pigo kubwa kwa Yanga, ambayo tayari msimu huu imevuliwa taji lake la ubingwa wa Tanzania Bara kwa matajiri hao wa Chamazi.
Azam ambao wametwaa ubingwa wa Bara kwa mara ya kwanza msimu huu wameanza usajili mapema ili kuunda kikosi cha kitakachoshiriki mashindano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika mapema mwakani.
Wachezaji wengine wanaotajwa kutakiwa na Azam ni pamoja na washambuliaji wa Simba, Amissi Tambwe na Ramadhani Singano.
Hata hivyo, nyota hao wawili bado wana mikataba na klabu yao ambayo mwakani haitashiriki tena michuano ya kimataifa.
Katika hatua nyingine Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeanza uchunguzi juu ya kitendo cha viongozi wa Azam kuvamia kambi ya Stars mjini Mbeya na kumsainisha Domayo kwa kilichoelezwa ni kwenda kinyume na taratibu za usajili.
Hata hivyo Azam siyo ya kwanza kufanya hivyo kwani Yanga na Simba walishawahi kufanya misimu iliyopita na haikufanywa uchunguzi wowote kwa nia ya kuchukulia hatua waliohusisha na ukiukwaji huo.

Atletico Madrid moto, yaiua Chelsea kwao yaifuata Real fainali Ulaya

Chelsea wakishangilia bao lao lililofungwa na Fernanndo Torres
Atletico wakipambana kuwania kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya
MEI 24 mjini Lisbon, Ureno itakuwa Fainali ya timu za jiji la Madrid, baada ya Atletico Madrid kuwafuata wapinzani wao wa jiji hilo Real Madrid kufuatia kutoa kipigo cha mabao 3-1 kwa Chelsea katika pambano la marudiano la Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Chelsea ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Stanford Bridge ilishindwa kuhimili makali ya wapinzani wao na kukubali kuondolewa kwa mara ya kwanza na timu za Hispania katika hatua hiyo baada ya kutandikwa huku wakishuhudiwa na gwiji wa zamani wa Argentina, Diego Maradona.
Vijana wa Mourinho walitangulia kupata bao la kuongoza lililofugwa na nyota wa zamani wa Atletico, Fernando Torres katika dakika ya 36 kabla ya wageni kusawazisha kupitia kwa Adrian dakika moja kabla ya kwenda mapumziko.
Kipindi cha pili kilikuwa kibaya kwa Chelsea baada ya Atletico kupata bao la pili lililofungwa kwa penati na Diego Costa katika dakika ya 60 kabla ya Tuiran kuongeza bao la tatu dakika ya 72 na kuihakikishia Atletico kutinga fainali za michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 20 iliyopita.
Timu hiyo sasa itakutana na mahasimu wao, Real Madrid iliyowavua taji Bayern Munich juzi kwa kuicharaza mabao 4-0 nyumbani kwao na kufuzu hatua hiyo kwa jumla ya mabao 5-0 baada ya mechi ya kwanza mjini Madrid kupata ushindi wa bao 1-0.