STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, January 3, 2013

Thomas Mashali kuuanza mwaka dhidi ya Mkenya

 
Bondia Thomas Mashali
BONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchini Thomas Mashali anatarajiwa kupanda ulingoni Januari 12 katika ukumbi wa Friends Corner Manzese Jijini Dar es Salaam kutetea Ubingwa wa Afika  Mashariki.
 
Akiongea na waandishi wa habari Mratibu wa pambano hilo Aisha mbegu alisema mashali atapambana kuzipiga na Mkenya Bernard Mackoliech mpambano utakaokuwa wa raundi 10.
 
Alisema maandalizi yamekamilika ikiwa pia na kutumiwa tiketi kwa bondia huyo mkenya ambaye anatarajiwa kuwasili januari nane kwa ajili ya kupima uzito na kupanda ulingoni.
 
“tunataraji mpambano utakuwa mkali wa kukata na shoka ukizingatia mashali ameweka kambi kwa muda mrefu nje ya mkoa lakini pia Mackoliech ni bondia mahiri ambaye anasaka rekodi ya kwenda kucheza nje ya nchi”,alisema Aisha.
 
Alisema nafasi iko wazi kwa watu wanaotaka kudhamini ili kuhakikisha mpambano huo unafanikiwa ukizingatia ndio mpambano wa kwanza kwa mwaka 2013 na pia mashali anavutia mashabiki wengi.
 
Kwa upande wake rais wa TPBO amesema mapambano ya utangulizi yanatarajiwa kuwa manne na mabondi tayari wamesaini mikataba na watatangazwa hivi karibuni.
 
Bondia Thomas Mashali anatetea ubingwa huo wa Afrika mashariki na kati ambao aliupata baada ya kumpiga Mganda Medi Sebyala Jijini Dar es salaam mpambano uliohudhuriwa na mashabiki lukuki.
 
Mwisho.

Tangulia Sajuki, kweli wewe ulikuwa mpiganaji

Sajuki enzi za uhai wake nilipomtwanga picha nyumbani kwake Magomeni kwa Macheni


KWA kipindi cha miaka miwili mfululizo, Juma Juma Kilowoko maarufu kama Sajuki, aliweza kupigana na kupambana na maradhi yaliyokuwa yakimsumbua tangu mwaka 2010.
Pamoja na kwamba alianza kuugua tangu mwaka 2010, hakuna aliyekuwa anafahamu kutokana na kufanya usiri mkubwa akijiuguza mwenyewe na familia yake, lakini mambo yalipomzidi ndipo mapema mwaka jana alijitokeza hadharani na kuweka bayana kabla ya Mei kupelekwa India kufanyiwa upasuaji.
Tangu alipotoka India, kila aliyemuona kwa siku za karibuni aliamini amefanikiwa kuyashinda mauti, kwa vile alijichanganya na kuendelea na shughuli zake, lakini kumbe Mungu alikuwa na siri kubwa nyuma ya matukio yake kwani alimpa fursa ya kuuaga salama mwaka 2012 na kuuona mwaka mpya wa 2013 kabla ya saa chache akamchukua na kutuachia majonzi watanzania walio wengi.
Sajuki, mmoja wa waigizaji, watunzi, waongozaji na wazalishaji wa filamu nchini aliyekuwa mtu wa watu amesaliwa saa chache kabla ya kupelekwa kwenye makazi yake ya milele katika makaburi ya Kisutu, jijini Dar er Salaam baada ya kuaga dunia jana asubuhi hospitalini Muhimbili.
Binafsi nilipata taarifa hizo nikiwa nyumbani kwangu, KImara King'ongo nikijiuguza Malaria na mafua makali yaliyonishika tangu Desemba 31 mwaka jana.
Nilishtuka kwa vile zilikuja ghafla mno, japo nilikuwa nafahamu Sajuki, alikuwa kalazwa Muhimbili baada ya kuzidiwa alipokuwa kwenye ziara ya kuwashukuru Watanzania na kuchangisha fedha za kupelekwa tena India jijini Arusha.
Sikuwa na kitu kingine cha kusema zaidi ya Alhamdulillah kulingana na mafundisho ya dini yetu na kumalizia kwa Innalillah Wainaillah Rajiun, kama Mtume Muhammad SAW aliyotuelekeza kila tunapokumbwa na Msiba tuseme hivyo kwa maana kwamba 'Sisi ni waja wa Mwenyezi Mungu na kwake hakika tutarejea'.
Pamoja na kwamba Sajuki ametutoka tungali tukimuhitaji katika fani yake na namna alivyokuwa akionyesha anavyothamini kazi kuliko hata afya yake, lakini Mungu ana mapenzi zaidi na tunapaswa kumshukuru.
Namkumbuka Sajuki, aliyenidokeza jina hilo lilitokana na muunganiko wa majina ya kaka yake aitwae Salum na lake la Juma na lile la ukoo yaani Kilowoko na kuzaa SAJUKI, kwa ucheshi, utani na kujiamini kupita kiasi alikojaliwa na maanani.
Mara ya kwanza kukutana naye nakumbuka ilikuwa mwaka 2009 nyumbani kwake Magomeni Mapipa nilipoenda kufanya mahojiano naye ambapo aliweza kuweka bayana ndoto aliyokuwa nayo tangu utotoni ya kuja kuwa muigizaji mchekeshaji kama Amri Athuman maarufu kama King Majuto.
"Nilitamani sana kuwa mchekeshaji kama King Majuto, lakini filamu za Sylvester Stallone 'Rambo' na ubabe wake zilibadilisha upepo na kujikuta kwenye filamu za kawaida na hasa zile za mapugano na ubabe," aliniambia nilipozungumza naye huku jirani yake akiwepo Soud Ally maarufu kama Chomba au Akuhi.
Sajuki, ambaye majina yake kamili ni Juma Juma Issa Kilowoko, alisema hamu yake ya kufika mbali katika sanaa ya uigizaji ndiyo iliyomfanya apite kundi moja hadi jingine hadi kuangukia Kaole Sanaa, lililomtangaza vema kupitia michezo iliyokuwa ikirushwa na kituo cha runinga cha ITV.
Alisema mchezo wake wa kwanza ndani ya kundi hilo lililotoa nyota kibao wa filamu nchini ni Baragumu wa mwaka 2005 na kufuatia na michezo mingine hadi mwaka 2008 alipojitoa kundini na kujikita zaidi katika filamu, kazi yake ya kwanza ikiwa ni Revenge.
"Baada ya kupita makundi kadhaa tangu nikiwa mjini Songea nilipozaliwa, hatimaye nilitua Kaole Sanaa, lililoniivisha kabla ya kuachana nao kusaka masilahi zaidi na kujikita katika filamu," alisema.
Mbali na Revenge filamu zingine alizocheza Sajuki ni pamoja na Dhambi, Mboni Yangu, Two Brothers, Behind the Scene, Round, Shetani wa Pesa, Hero of the Church na nyinginezo.
Wakati nilipokuwa nazungumza naye alikuwa akijiandaa kutoa filamu mbili binafsi za Vita na Briefcase zilizowashirikisha nyota kadhaa nchini akiwemo mshindi wa pili wa BBA, Mwisho Mwampamba.
Sajuki alisema fani ya filamu imemnufaisha kwa mambo mengi ikiwemo kimaisha, lakini kubwa ni kufanikiwa kumuoa mke mrembo na muigizaji mwenzake, Wastara Issa Juma 'Stara'.
"Kufanikiwa kumpata Wastara na kumuoa kwangu ni jambo kubwa na la kuvutia mno kati ya mafanikio kibao niliyoyapata katika fani hii ya filamu nchini," alisema.
Mkali huyo, aliyekuwa akipenda kucheza na watoto na shabiki wa muziki wa 'Quito', alisema kama kuna kitu kinachomkera katika sanaa hiyo ni tabia za 'Wauza Sura' wanaojiingiza kwenye skendo chafu zinazowachafua wasanii wote wa tasnia hiyo mbele ya jamii.
Alisema wasanii wenye kusaka umaarufu kwa lazima wanamnyima raha kwa vile jamii inadhani wasanii wote wana silka na tabia kama za wauza sura hao wanaojirahisi na kujidhalilisha.
Kuhusu rushwa ya ngono, Sajuki mtoto wa nne kati ya watano wa Mzee Juma Issa Kilowoko, alisema wanaojihusisha nao wanafanya hivyo kwa kujitakia kwa sababu hakuna anayelazimishwa kutoa mwili wake iwapo ana uwezo na kipaji kikubwa katika sanaa hiyo.
"Rushwa ya ngono kwa watoto wakike ni kujitakia kwa vile wana akili na ufahamu wa kujua athari za kufanya hivyo na watayarishaji wanaolazimisha hawafai na wanapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria," alisema Sajuki.
Sajuki, alinidokeza kuwa hakuna kitu kilichomtia simanzi na kumsikitisha kama tukio la ajali ya pikipiki iliyompata akiwa na mkewe, Wastara Juma enzi wakiwa wachumba.
Nyota huyo ambaye ameacha mjane na mtoto mmoja wa kike, aliishukuru familia yake na Vincent Kigosi 'Ray' kwa kumfikisha alipokuwapo alisema ajali hiyo sio inayomuuma, ila kitendo cha kulazimika kuidhinisha fomu hospitalini ili Wastara akatwe mguu wake uliokuwa umeharibika kwa ajali hiyo.
"Kwa kweli kile kitendo cha kuidhinisha kukatwa kwa mguu kwa Wastara kinaniuma hadi leo, lakini sikuwa na jinsi ila kufanya hivyo ili kumuokoa," Sajuki aliniambia kwa masikitiko katika mahojiano hayo.
Hata hivyo alidai alikuwa akijisikia fahari mno kuoana na kisura huyo ambaye kwa sasa anao mguu wa bandia, kwa vile wamesaidiana kuanzisha kampuni yao binafsi ya Wajey Films Production.
Sajuki alizaliwa miaka 27 iliyopita huko Songea na kusoma hadi elimu ya sekondari katika shule za Songea na Luwiko, alikoanza kuonyesha kipaji chake cha sanaa katika matamasha mbalimbali ya shule kabla ya kujitosa kwenye makundi.
Mungu ailaze mahali pema roho ya marehemu Sajuki anayezikwa kesho katia makaburi ya Kisutu.


Mwisho

Kado azivuruga Yanga, Mtibwa

Kado akitambulishwa na viongozi wa Coastal Union hivi karibuni

KLABU za Yanga na Mtibwa Sugar zimeendelea kuzozana kuhusiana na mchezaji Shaaban Kado baada ya kipa huyo kusaini mkataba wa kuichezea Coastal  Union ya Tanga kwa mwaka mmoja.
Kipa huyo ambaye aliichezea Mtibwa kwa mkopo katika mzunguko wa kwanza wa msimu akitokea Yanga, amekuwa chanzo cha malumbano baina ya klabu hizo; ambapo ‘Wanajangwani’ wanadai kuwa wana haki ya kumuuza kokote kwavile ni mchezaji wao halali huku ‘wakata miwa’ wa Mtibwa wakisisitiza kuwa anapaswa kuendelea kubaki kwao kwavile walimtwaa kwa mkataba wa kuichezea hadi mwisho wa msimu.
Hata hivyo, akizungumza jana, Kado alisema kuwa tayari ameshasaini mkataba wa mwaka mmoja kuichezea Coastal iliyowahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara mwaka 1988.
“Ni kweli nimesaini mkataba wa mwaka mmoja katika klabu ya Coastal… na nimeshaanza kufanya nao mazoezi,” alisema Kado.
Akieleza zaidi, kipa huyo alisema: “Kulikuwa na mvutano kati ya Yanga na Mtibwa juu yangu, lakini kila kitu kuhusiana na hilo nimewaachia wao. Naamini watamalizana,” alisema Kado.
Mratibu wa Mtibwa, Jamal Bayser, alisema jana kuwa wameshangazwa na kitendo cha Yanga kumuuza mchezaji huyo il-hali walikubaliana kuichezea timu yao (Mtibwa) hadi mwishoni mwa msimu huu wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Bayser alisema kuwa tayari klabu yake imewasilisha malalamiko katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusiana na suala la kipa huyo ambaye aliwahi kuichezea Mtibwa kabla ya kuuzwa Yanga na baadaye kurejea tena klabuni hapo kwa mkopo.
“Inashangaza sana kuona klabu zinasajili wachezaji kinyume na utaratibu. Kulingana na makubaliano yetu na Yanga, Kado anatakiwa kuitumikia Mtibwa hadi mwishoni mwa msimu huu,” alisema Bayser.
“Tumeshaandika barua TFF, maana tulikubaliana na na Yanga, tena tukaweka mkataba kimaandishi. Sasa tunasubiri TFF watoe maamuzi,” aliongeza mratibu huyo.
Alipotafutwa na gazeti hili jana kuzungumzia suala hilo, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema kuwa kwa sasa hawana muda wa kuzungumzia suala hilo kwavile Kado si mali yao tena kwa sasa.
“Kado ni mali ya Coastal Union kwa sasa, siwezi kuzungumzia suala la mchezaji huyo maana siyo mali yetu tena (Yanga),” alisema Mwalusako.
Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kuwa sakata la mchezaji huyo limepelekwa kwenye Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF ili lipatiwe ufumbuzi.


Chanzo:NIPASHE

Golden Bush Veterani, Wahenga Fc kurudiana Januari 12

Kikosi cha Golden Bush Veterani ambacho kinatarajiwa kurudiana na Wahenga Fc Januari 12

BAADA ya kukaribisha mwaka kwa kipigo cha aibu cha mabao 4-3 kutoka kwa wapinzani wao, timu ya soka ya Golden Bush Veterani, imekata rufaa na sasa watarudiana na wapinzani wao Wahenga Fc Januari 12.
Tayari pande zote zimekuwa zikitoleana tambo mbalimbali Wahenga wakisisitiza kuwa waliamua kutoa zawadi ya mwaka mpya kwa watani zao kwa kuwapa kipigo hicho, huku Golden Bush kikisisitiza kuwa waliotewa na kwamba mechi hiyo ya kisasi wataifumua Wahenga mabao 7-0.
Golden Bush tayari kimeweka hadhaarani kikosi kitakachoshuka dimbani siku ya mechi hiyo ambapo golini atakuwepo Hamza, kipa wa timu yao ya vijana huku kulia atasimama Chidi Rasta, kushoto Abuu Ntiro, Mmalawi Wisdom Ndhlovu atacheza kama beki namba nne na mkoba atakuwa Majaliwa.
Kiungo nama sita atacheza Yahya Issa, wingi ya kulia atasimama mlezi wao, Onesmo Wazir 'Ticotico' na Katina Shija atazungusha dimba la juu, Herry Morris atacheza kama mshambuliaji wa kati na Kapeta atacheza namba 10 na Said Swedi Panucci atacheza wingi ya kushoto.
Pamoja na Golden Bush kujinasibu kushinda mchezo huo wa marudiano, Wahenga wamekejeli wakieleza kuwa wao hawana hofu yoyote kwa sababu soka wanalijua japo wachezaji wao hawana majina makubwa kama ya wapinzani wao ambao katika mechi zao mbili za awali walitoka sare ya 1-1 na kisha kuwanyuka mabao 4-2 kabla ya kuwazima wiki mwishoni mwa wiki kwa mabao hayop 4-3 mechi zote zikichezwa kwenye uwanja wa TP Afrika, Sinza Dar es Salaam.

Je, nani atakayeiobuka na ushindi? Tusubiri kuona hiyo Januari 12.

HALI HALISI ILIVYO NYUMBANI KWA MAREHEMU SAJUKI


Mke wa marehemu, Juma Kilowoko 'Sajuki', Wastara Juma (aliyejifunika nguo) akiwa na simanzi nzito kwa kumpoteza mumewe.
Mzee Kilowoko ambaye ni baba mzazi  wa marehemu 'Sajuki' akiwasiliana na ndugu na jamaa msibani hapo.
Mama  mzazi  wa marehemu Sajuki (wa kwanza kushoto) akiwa na majonzi.
Dada wa Wastara aitwaye Marian (aliyesujudu) akilia kwa uchungu.
 
Bibi wa marehemu Sajuki akiwasili msibani.
Pichani juu ni baadhi ya taswira za waombolezaji wakiwa nyumbani kwa marehemu Juma Kilowoko 'Sajuki', Tabata- Bima jijini Dar es Salaam. Sajuki amefariki dunia jana asubuhi akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo alikuwa akitibiwa.
(PICHA NA HAMIDA HASSAN / GPL)

Chelsea hoi wa QPR, Liverpool yazidi kupeta

Wachezaji wa QPR wakimpongeza Shaun Wright Phillips aliyefunga bao pekee lililoiangusha Chelsea jana usiku.

WAKATI Liverpool ikiendeleza wimbi la ushindi kwa kuisambatarisha timu ya Sunderland kwa mabao 3-0, Chelsea walijikuta wakiteleza nyumbani kwao uwanja wa Stanford Bridge kwa kudunguliwa bao 1-0 na 'vibonde' wa Ligi Kuu ya England, QPR inayonolewa na kocha Harry Redknapp.
Chelsea ilikumbana na kipigo hicho kutokana na bao la nyota wake wa zamani Shaun Wright-Phillips aliyefunga katika dakika ya 78 kutokana na kazi nzuri ya Mmorocco Adel Taarabt.
Kipigo hicho kimeiacha Chalsea kwenye nafasi ya nne ikiwa na pointi 38 ikishindwa kuipiku Tottenham waliowazidi pointi moja wanaokamata nafasi ya tatu nyuma ya Manchester City na Manchester United.
Liverpool wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumba waliinyoa Sunderland kwa mabao 3-0, mabao wawili yakitupiwa kambani na Luis Suarez, huku bao la awali likifungwa na Raheem Sterling akimalizia kazi ya Suarez.
Katika mechi nyingine ya mfululizo wa ligi hiyo Newcastle United imeendeleza wimbi la vipigo kwa kulala nyumbani kwao mabao 2-1 toka kwa Everton.

SAJUKI  KUZIKWA KESHO MAKABURI YA KISUTU

Sajuki akichapa mzigo enzi za uhai wake
Sajuki na mkewe Wastara enzi za uhai wake
Baba yake Sajuki... Mzee Kilowoko akiwasiliana na ndugu na jamaa kwa simu wakati akiwa kwenye msiba wa mwanawe, Tabata jijini Dar es Salaam jana. Familia imeamua Sajuki azikwe makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam kesho Ijumaa.

Wasanii wa vichekesho, Mtanga (kushoto) na Kiwewe (aliyejishika goti) wakiwa na waombolezaji wengine katika msiba wa Sajuk.

Waombolezaji wakiwa nyumbani kwa marehemu Sajuki
Tutakukumbuka milele Sajuki... msanii nyota wa filamu za Kibongo, Suzan Lewis 'Natasha' akiwa kwenye msiba wa Sajuki mapema leo kushiriki maandalizi ya shughuli za mazishi, eneo la Tabata jijini Dar es Salaam 
Baadhi ya waombolezaji wa msiba wa Sajuki waliofika mapema Tabta

Piga pale...! Sajuki (kulia) akiwa katika maandalizi ya filamu yake ya Vita wakati wa enzi za uhai wake.


Waombolezaji wakiwa na majozni tele katika msiba wa Sajuki, Tabata jijini Dar es Salaam.
HATIMAYE ule utata kuhusiana na mahala pa kumzika msanii Juma Kilowoko 'Sajuki' umepatiwa jibu baada ya baba yake kukubali kuwa azikwe jijini Dar es Salaam.

Kutokana na uamuzi huo, sasa msanii huyo aliyekuwa nyota na kipenzi cha wengi enzi za uhai wake atazikwa kesho 
saa 7:00 mchana baada ya swala ya Ijumaa kwenye makaburi ya Kisutu.

Awali, baba wa msanii huyo alitaka mwanawe akazikwe kwao mkoani Songea. Hata hivyo, baada ya kuketi na kujadili kwa kina na familia yake, akaamua kutangaza kuwa mwanawe huyo kipenzi atazikwa jijini Dar es Salaam ili kutoa nafasi kwa rafiki zake wengi aliokuwa akishirikiana nao katika kazi zake za kila siku za kisanii kupata nafasi ya kushiriki mazishi yake.

Mzee Kilowoko ametoa msimamo huo mpya leo hoo hii, ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kutangaza awali kuwa mwanawe atakwenda kuzikwa Songea.

Sajuki amefariki leo asubuhi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa katika wodi ya wagonjwa mahututi na kupumua kwa msaada wa mashine kabla ya kuaga dunia mishale ya saa 1:00 asubuhi.



Mashabiki wa filamu za Kibongo nchini watamkumbuka marehemu kwa filamu zake kama 'Round', 'Shetani wa Pesa', 'Hero of the Church', 'Vita' na 'Briefcase, 'Revenge', 'Dhambi', 'Mboni Yangu', 'Two Brothers', na'Behind the Scene'.
Sajuki alizaliwa mwaka 1986 Songea mkoani Ruvuma, ameacha mke na mtoto mmoja.

Tuesday, January 1, 2013

KABURU, WENZAKE WAHOJIWA UPORAJI FEDHA ZA SIMBA

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange 'Kaburu'

MAKAMU Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na katibu mkuu wa klabu hiyo, Evodius Mtawala ni miongoni mwa watu waliohojiwa na Jeshi la Polisi jana kusaidia uchunguzi mkali kuhusiana na ujambazi uliosababaisha kuporwa kwa Sh. milioni 10.59 za klabu hiyo zilizotokana na mgawo walioupata katika mechi yao ya kirafiki dhidi ya Tusker ya Kenya kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi.
Akizungumza na jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela, alisema kuwa wameshawahoji Kaburu, Mtawala na watu wengine kadhaa ili kupata maelezo muhimu yatakayosaidia kupatikana kwa ukweli kuhusiana na kilichotokea.
"Tumewahoji viongozi hao wawili wa Simba (Kaburu na Mtawala) ili kujua taratibu za uhifadhi na utunzwaji wa fedha na mali za klabu yao... maana inastusha kusikia mtu mmoja anakwenda nyumbani kwake na mali ya klabu, tena buila ulinzi wowote ule," alisema Kenyela.
"Tumeamua pia kuwahoji ili kujua hasa ni nini kilichotokea kuanzia Uwanja wa Taifa maana tulibaini kuwa wao (Kaburu na Mtawala) ndiyo waliosaini na kupokea mgawo wa Simba kule uwanjani (Taifa),"  aliongeza.
Kataka hatua nyingine, Kenyela alisema kuwa Mhasibu wa Klabu hiyo, Erick Sekiete na watu wengine wawili, Said Pamba na Stanley Phillipo (23) waliokuwa wakishikiliwa na Polisi kuhusiana na tukio hilo waliachiwa kwa dhamana jana.
Sekiete na wenzake hao, walivamiwa wakati wakiwa katika eneo la Sinza kwa Remmy baada ya kuteremka katika gari aina ya Toyota Premio yenye namba za usajili T869 BKS iliyokuwa ikiendeshwa na Pamba.
Katika tukio hilo, ilidaiwa kuwa Sh. milioni 7.59 na dola za Marekani 2,000 (Sh. milioni tatu) zilizotokana na mgawo wa klabu hiyo katika mechi yao dhidi ya Tusker FC ya Kenya kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ziliporwa baada ya Sekiete (28) kuvamiwa na majambazi sita katika eneo la  Sinza kwa Remmy jijini Dar es Salaam ambapo risasi kadhaa zilipigwa hewani. Tukio hilo lilitokea saa 3:20 usiku.
Kamanda Kenyela alieleza kuwa Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alimdhamini Sekiete huku Phillipo akidhaminiwa na ndugu yake aitwaye Julius Kiwale.
Kamanda Kenyela alisema kuwa Pamba, ambaye alikuwa dereva wa gari lililowabeba Sekiete na Phillipo, alidhaminiwa na Kasim Pamba.
“Wanatakiwa waripoti katika Kituo cha Polisi Magomeni Jumatano (kesho),” aliongeza Kenyela.


Chanzo;NIPASHE
----------

KALA JEREMIAH KUTOKA NA ALBUM YAKE MPYA


Baada ya kufanya vizuri katika baadhi ya redio na televisheni kwa ngoma yake ya Dear GodKala Jeremiah sasa ameweka wazi kwamba siku ya tarehe 20 mwezi huu anatarajia kutoka na album yake mpya inayokwenda kwa jina la Pasaka.

GOlden Bush yaaga mwaka 2012 kwa aibu yanyukwa na Wahenga

LICHA ya kuwatumia nyota wa zamani wa klabu kubwa za soka nchini za Simba, Yanga na Mtibwa, timu ya soka ya Golden Bush Veterani jana uliuaga mwaka 2012 na kuukaribisha kinyonge mwaka 2013 baada ya kutandikwa mabao 4-3 na wapinzani wao wakubwa, Wahenga Fc katika pambano maalum la kirafiki.
Pambano la timu hizo lilifanyika jana jioni kwenye uwanja wa TP Afrika, Sinza Dar es Salaam ambapo Golden Bush, ilijikuta ikipelekwa puta na Wahenga iliyokuwa aikiongozwa na kipa wa zamani wa Yanga na Mtibwa, Mengi Matunda.
Japo Golden Bush, iliyowatumia nyota kama Yahya Issa, Athuman Machuppa, Abuu Ntiro, Waziri Mahadhi, Said Swedi na nduguye Salum Swedi 'Kussi', Nico Nyagawa, Heri Morris, Katina Shija na wengineo iliweza kuongoza kwa mabao 2-1 hadi wakati wa mapumziko, lakini ilishindwa kuepuka kipigio katika mchezo huo.
Golden Bush ilianza kujipatia bao la kuongoza katika dakika ya 18 baada ya Heri Morris kufumua shuti kali lililomshinda kipa wa Wahenga, David 'Seaman' kabla ya Said Swedi kuifungia timu hiyo bao la pili kwa kichwa akiuynganisha krosi pasi ya Nico Nyagawa.
Hata hivyo katika dakika ya 31 Wahenga walipata bao lao la kwanza kupitia kwa mchezaji wao aitwae God aliyeusukumia mpira wavuni kwa shuti karibu na lango lwa Golden Bush.
Kipindi cha pili kilishuhudiwa kwa Golden Bush ikifanya mabadiliko makubwa katika kikosi chao ikiwamo kumtoa Onesmo Waziri 'Ticotico' aliyekuwa akisumbua mbele licha ya kucheza akiwa majeruhi, lakini mabadiliko hayo hayakuwasaidia baada ya Wahenga kutumbukiza wavuni bao la kusawazisha katika dakika ya 65 kupitia Frank 'Super Et'oo'.
Wakati Golden Bush wakitafarakari jinsi walivyofungwa bao hilo, Wahenga walipata bao jingine la tatu lililofungwa kwa njia ya penati na kipa David Seaman katika dakika ya 78 baada ya mmoja wa wachezaji wa timu hiyo kuchezewa rafu ndani ya lango la Golden Bush.
Jahazi la Golden Bush lilizidi kuzama katika dakika ya 82 wakati Wahenga walipojipatia bao lao la nne lililofungwa na beki aliyepanda mbele kusaidia mashambulizi Shomar aliyewatoroka mabeki wa Golden Bush ambao katika mechi ya jana walionekana kuyumba kusiko kawaida.
Hata hivyo zikiwa zimesalia dakika nne, Golden Bush ilijipatia bao lao tatu la kujifutia machozi, lililofungwa kwa ,mpira wa adhabu ndogo na Salum Swedi 'Kussi' baada ya Machota kuchezewa vibaya na mabeki wa Wahenga nje ya eneo la hatari.
Mara baada ya pambano hilo, Mlezi wa Golden Bush, Onesmo Waziri 'Ticotico' alisema wamekikuibali kipigo cha wapinzani wao, licha ya kwamba alimtupia lawama mwamuzi wa pambano hilo, Ally Mayay kwamba 'aliwauma' na kuahidi kuomba pambano la marudiano na wapinzani wao hao ili kukata mzizi wa fitina.
"TUmekubali kipigo, lakini tutaomba mechi ya marudiano, tunaamini leo tumefungwa kwa sababu mwamuzi alikuwa 'wao', hatuamini kama hawa jamaa wana uwezo wa kuwafunga wakati hivi karibuni tuliwanyuka mabao 4-2 baada ya awali kutokana nao sare ya 1-1," alisema Ticotico.
Hata hivyo baadhi ya watazamaji wa mchezio huo wakieleza kipigo walichopewa Golden Bush kilikuwa halali kutokana na kuzidiwa ujanja na Wahenga, huku wakiwapoingeza walioandaa pambano hilo kwa kuwapa burudani ya kuagia mwaka na kuwashuhudia nyota waliotamba zamani katika klabu mbalimbali nchini ambao walikuwa hawajui wapo wapi kwa sasa baada ya kutoweka kwenye ligi kuu.

NYota wa zamani wa soka wataka 2013 uwe wa mapinduzi katika kandanda

Mecky Mexime


NYOTA wa zamani wa soka nchini wamewataka wadau wa mchezo huo kujipanga ili kuhakikisha mwaka 2013 unakuwa wenye tija na mafanikio kwa mchezo wa kandanda baada ya mwaka uliopita wa 2012 kutokuwa na cha kujivunia.
Wakizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa pambano maalum la kuuaga 2012 na kuukaribisha 2013 wachezaji hao wakiongozwa na nahodha wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mecky Mexime, walisema mwaka uliopita ujlikuwa na matukio ya kuumiza katika soka kwa timu za Tanzania kushindwa kung'ara.
Hivyo wakataka mwaka 2013 uwe wa mapinduzi ili Tanzania iweze kurejesha makali yake ya miaka ya nyuma ilipotikisa soka la Afrika.
"Awali ya yote tunashukuru kuweza kukutana wachezaji wa zamani ambao tulipoteana kitambo, lakini kubwa ni kutaka kuona mwaka 2013 unakuwa wa mapinduzi katika soka ili Tanznaia itambe kimataifa," alisema Mexime ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya Mtibwa Sugar.


Katina Shija

Madaraka Seleman
Wengine waliotoa  maoni yao kutaka mwaka 2013 uwe na mabadiliko katika michezo hususani soka ni Yahya Issa, Nico Nyagawa, Madaraka Seleman 'Mzee wa Kiminyio', Katina Shija, Wazir Mahadhi, Zubeir Katwila, kipa Steven Marashi, Onesmo Waziri 'Ticotico', Abuu Ntiro na wengine ambao walikuwa wakiichezea timu ya Golden Bush Veterani waliokuwa wakiumana na Wahenga Fc na kukubali kipigio cha aibu cha mabao 4-3.

KOCHA MFARANSA ATUA SIMBA AAHIDI MAKUBWA

Kocha wa Simba, Mfaransa Liewig akizungumza na waandishi baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana
HATIMAYE kocha mpya wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig ametua nchini  na kuahidi kuiletea mafanikio makubwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Liewig aliyekuja kutwaa nafasi iliyoachwa wazi na Mserbia Milovan Cirkovic, amesema 'Wanamsimbazi' watarajie mambo mazuri kutoka kwake, lakini kwa sharti la kumpa ushirikiano katika kila hatua wakati atakaposaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo na kuanza kibarua chake.
"Nimefurahishwa sana na mapokezi haya... najihisi kuwa nina deni kubwa. Naamini nitapata ushirikiano wa kutosha na baada ya kuzoeana na wachezaji, naamini Simba itafika mbali katika kila michuano," alisema kocha huyo.
Miongoni mwa watu waliofika uwanjani kumpokea kocha huyo ni Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, ambaye aliwaongoza mamia ya mashabiki wa Simba kumpokea kwa maandamano ya magari na pikipiki za bodaboda na bajaji.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinaeleza kuwa kocha huyo atasaini mkataba wa kuifundisha klabu hiyo kwa miezi 18 na tukio hilo litakamilishwa leo asubuhi.

Monday, December 31, 2012

Majeraha yamzuia Cheka kurudiana na Mmalawi

Bondia Francis Cheka 'SMG'


BINGWA anayeshikilia mataji manne tofauti likiwemo la IBF, bondia Francis Cheka 'SMG' hataweza kupambana kwa mara nyingine tena na Mmalawi, Chiotra Chimwemwe kutokana na kuumia katika pambano lao la kwanza lililochezwa jijini Arusha wiki iliyopita.
Cheka na Chimwemwe walitarajiwa kuvaana mjini Addis Ababa, Ethiopia katika pambano maalum la kusindikiza mkutano wa Viongozi Wakuu wa nchi za Afrika, Januari 26.
Mabondia hao wangepigana kuzindikiza pambano la kimataifa kati ya Oliver McCall wa Marekani dhidi ya Sammy Retta wa Ethiopia kuwania ubingwa wa uzito wa juu IBF (IBF AMEPG).
Rais wa IBF/USBA, Onesmo Ngowi, alisema nafasi ya Cheka imechukuliwa na mkali mwingine nwa ngumi za kulipwa nchini katika uzito wa juu, Alphonce Mchumiatumbo, ingawa haijafahamika atapigana na nani.

Ngowi alisema mapambano mengine siku hiyo ya Januari 26 ni pamoja na lile la Mkenya, Daniel Wanyonyi dhidi ya Issac Hlatswayo wa Afrika Kusini watakaowania ubingwa wa IBF AMEPG uzito wa Welterweight
Pambano jingine litawakutanisha Manzur Ali wa Misri dhidi ya Harry Simon wa Namibia watakaowania taji la IBF AMEPG uzito wa Light heavyweight.

Minziro atamba Yanga moto ule ule

Fred Minziro (kulia) katika moja ya majukumu yake uwanjani

KOCHA Msaidizi wa klabu ya Yanga, Fred Felix Minziro, ametamba kwamba moto waliomalizia nao kwenye duru la kwanza la Ligi Kuu Tanzania Bara, ndiyo watakaoanza nao katika duru lijalo, huku akisisitiza lazima Yanga iwe bingwa 2012-2013.
Aidha kocha huyo ametamba kwamba timu yao imejipanga ili kuhakikisha wanatetea taji lao la Kombe la Kagame katika michuano itakayofanyika hivi karibuni nchini Rwanda.
Akizungumza na MICHARAZO kabla ya kupaa na timu kwenda Uturuki, Minziro, beki wa kimataifa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, alisema ubora wa kikosi alichonacho na namna  wanavyojiandaa, inampa imani ya kuamini kwamba Yanga itawavua ubingwa wa ligi watani zao, Simba msimu huu.
Minziro, alisema Yanga itaendeleza moto ule ule waliomalizia nao duru la kwanza la ligi hiyo iliyowatoa nafasi za kati mpaka kileleni ikiwaengua waliokuwa vinara Simba na Azam, ili mwisho wa msimu klabu yao iwe mabingwa wapya wa Tanzania.
"Hatudhani kama tutaanza kinyonge kama ilivyokuwa katika duru la kwanza, tupo katika maandalizi kabambe ili kuhakikisha tunaendeleza moto na kasi yetu ili kurejesha taji tuliloporwa na watanbi zetu, Simba," alisema Minziro.
Minziro, alisema japo anatambua duru lijalo litakuwa lenye ushindani mkubwa, lakini wao wamejiandaa vya kutosha kuhakikisha wanafanya vema, huku akisisitiza kuwa maandalizi yao yanalenga pia kwenda kutetea taji lao la Kombe la Kagame njini KIgali.
"Macho na akili zetu zote tumezielekeza kwenye duru la pili la ligi pamoja na michuano ya Kagame, tungependa kwenda kutetea taji ugenini, tunajiamini na wachezaji wana ari kubwa ya kufanya hivyo," alisema Minziro.
Yanga inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 29, tano zaidi ya Azam waliopo nafasi ya pili na sita zaidi ya watani zao Simba wanaoshika nafasi ya tatu, ilitwaa taji hilo la Kagame Julai, 2012 kwa kuilaza Azam mabao 2-0 katika mchezo fainali zilizochezwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mtanzania kuwania taji la Jumuiya ya Madola


BONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchini, Fadhili Majia ameteuliwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC) kupigana na Isaac Quaye wa Ghana kuwania nafasi ya kupigana na bingwa Kevin Satchell wa Uingereza.
Mabondia hao wanatarajia kupigana katika pambano hilo la uzani wa Fly Februari 22 mwakani kwenye mji wa Accra, Ghana ambapo mshindi wa mechi hiyo ya mchujo atapata fursa ya kupigana na Satchell anayeshikilia taji hilo la Jumuiya ya Madola.
Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC) Onesmo Ngowi ambaye ni mmoja wa wakurugenzi wa CBC, alisema wajumbe wa bodi hiyo walimpigia kura Majia baada ya yeye kulipendekeza na hiyo kuibuka kidedea.
Ngowi, alisema hiyo itakuwa ni mara ya kwanaa kwa Majia kuwania mkanda huo wa Jumuiya ya Madola ambao huziunganisha nchi zote zilizotawaliwa na Uingereza.
"Bondia Mtanzania Fadhil Majia amepeta fursa ya kuteuliwa kucheza mechi ya mchujo dhidi ya Mghana, Isaac Quaye Februari 22, 2013 ili kuwania nafasi ya kupigana na bingwa wanayeshikilia taji la CBC, Kevin Satchell wa Uingereza," alisema Ngowi.
Katika hatua nyingine, Ngomi alisema CBC, imepitisha azimio la kuruhusu ubingwa wa baraza hilo katika Bara la Afrika.
Ubingwa huo utakuwa unajukikana kama 'CBC Africa Zone' na tayari wapo mabondia kadhaa wa nchi za Afrika ya Magharibi ambao wameshandaa mapambano mwakani.
"Napenda kuwahamasisha mapromota wa Tanzania kuchangamkia fursa hizi adimu na kuandaa mapambano ya ubingwa wa 'CBC Africa Zone' kwa manufaa ya mabondia wetu," alisema Ngowi ambaye pia ni Rais wa IBF Afrika/USBA.
***

Julio afichua siri Msimbazi


KOCHA msaidizi wa timu ya vijana chini ya miaka 17 Serengeti Boys, Jamhuri Kihwelo 'Julio', aliyerejeshwa Msimbazi kama kocha msaidizi, amefichua siri ya wachezaji wa Simba akidai wengi wao wana matatizo ya kutokuwa na pumzi na stamina ya kutosha.
Julio, alisema kutokana na kupewa jukumu la kuwanoa vijana hao kama kocha wa viungo wa Simba atarekebisha tatizo, ili timu yao iweze kufanya vema katika duru lijalo la ligi kuu pamoja na uwakilishi wa nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Beki huyo wa zamani wa Simba na Taifa Stars, alisema pamoja na mambo mengine yaliyoiponza Simba kwenye duru lililopita, amegundua tatizo kubwa kwa kikosi hicho ni kukosekana kwa stamina na pumzi za kutosha kwa nyota wa timu hiyo.
Alisema kutokana na kubaini tatizo hilo, amejipanga kuwanoa wachezaji hao ili wawe 'ngangari'.
Julio alisema anadhani tatizo hilo ndilo lililoigharimu Simba kwenye duru la kwanza kwa wachezaji wake kushindwa kumudu dakika zote 90 za mchezao badala yake kuonekana tishio dakika 45 za kwanza na kuwa 'urojo' dakika 45 za pili na kupata matokeo mabaya.
"Nimegundua wachezaji wengi wa Simba wana tatizo la pumzi na stamina, hivyo nitajitahidi kurekebisha tatizo kabla ya kuanza kwa duru la pili la ligi ili vijana wawe ng'ang'ari," alisema.
Julio amerejeshwa Msimbazi sambamba na aliyekuwa kocha mkuu wa zamani wa timu hiyo, Moses Basena ili kumsaidia kocha mpya wa klabu hiyo, Patrick Liewig  anayechukua nafasi ya Mserbia , Circokiv Milovan aliyetupiwa virango Simba.
Kwa sasa Julio na vijana wake wanaendelea kujifua kwa mazoezi ya ufukweni wakati wakisubiri kuanza kufanya mazoezi ya uwanjani mara atakapowasilia kwa Mfaransa Liewig, aliyepewa mkataba wa muda mrefu ili 'kupimwa' kiwango chake.

Kocha wa Simba sasa kutua leo Yanga wafika salama Uturuki


UONGOZI wa Simba umedai kuwa kocha mpya wa timu yao, Mfaransa Patrick Lieweg atawasili kwenye Uwanja wa Kiamataifa wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) leo saa 7:15 mchana akitokea mjini Baho, Ufaransa.
Ujio wa kocha huyo umekuwa wa danadana tangu ilipotangazwa awali angetua Desemba 27, lakini safari hii uongozi umethibitisha kuwa atatua leo mchana bila kupepesa macho.
Akizungumza na MICHARAZO jana, Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage alisema kuwa kocha huyo atatua kurithi mikoba ya aliyekuwa kocha wao, Mserbia Milovan Cirkovic, ambaye wamelazimika kumfungashia virago baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
“Kulikuwa na tatizo la usafiri wa ndege katika nchinnyingi za Ulaya kipindi hiki cha bararidi kali barani humo ndiyo maana alikuwa anakosa ndege za kumleta Tanzania,” alisema Rage.
Simba, ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi hiyo, walilazimika kuvunja mkataba na Cirkovic kutokana na kilichodaiwa na uongozi wa klabu hiyo kuwa kocha huyo alikuwa ‘anaikamua’ kiasi kikubwa mno cha fedha.
Hata hivyo, baada ya kuvunja mkataba na kocha huyo aliyewapa ubingwa msimu uliopita, ‘Wekundu wa Msimbazi’ tayari wameingia mkataba na makocha wawili wapya, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na Mganda Mosses Basena.
Kwa mujibu wa Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, baada ya kutua kwa Lieweg, uongozi wa klabu hiyo utatangaza mfumo mpya wa benchi la ufundi la timu yao.
Katika hatua nyingine msafara wa mabingwa wa Kombe la Kagame, Yanga umefika salama nchini Uturuki na unatarajiwa kuanza programu zao nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa za mtandao wa klabu hiyo, kikosi hicho kilifika salama jana asubuhi na leo kilitarajiwa kuanza kujifua kabla ya kuanza kucheza mechi kadhaa za kirafiki na wenyeji wao zikiwa maalum kwa ajili ya duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara na utetezi wao wa Kombe la Kagame litakalofanyika nchini Rwanda.

Golden Bush, Wahenga kuuaga mwaka Tp Afrika


TIMU ya soka ya Golden Bush jioni ya leo inatarajiwa kushuka dimbani kumenyana na Wahenga Fc katika pambano maalum la kuuaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2013.
Pambano la timu hizo mbili zinazoundwa na wachezaji nyota wa zamani nchini, litafanyika kwenye uwanja wa TP Afrika, Sinza Dar es Salaam kuanzia majira ya jioni.
Timu hizo zitakutana katika pambano hilo huku zikiwa na kumbukumbu ya kukutana hivi karibuni kwenye dimba la uwanja huo.
Wahenga wanakumbuka kipigo cha mabao 4-2 ilichopewa na wapinzani wao siku chache baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika michezo iliyochezwa hivi karibuni.
Golden Bush inayomilikiwa na mmoja wa wanachama wa zamani wa Friends of Simba, Onesmo Wazir 'Ticotico', itashuka dimbani leo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-2 iliyopata siku ya Jumamosi dhidi ya vijana nwa Chuo Kikuu.
Ticotico aliyeshindwa kuonyesha makeke yake katika pambano la Jumamosi kutokana na kuumia dakika 9 tu baada ya pambano hilo kuanza, alisema anaamini leo akijaliwa atashuka dimbani kuwaongoza wenzake kuendeleza 'dozi' yao ya mabao manne iliyokuwa inaitoa kabla ya kutibuliwa na vijana hao wa Chuo Kikuu.
"Nilikamia mechi ya Jumamosi, lakini nikashindwa kwa kuumia mapema, ila Jumatatu (leo) naweza kushuka dimbani kuwavaa wahenga," alisema Ticotico.
Katika mechi yao ya Jumamosi, Golden Bush ilipata mabao yake kupitia nyota wa zamani wa Yanga, Moro United na Prisons Mbeya, Herry Morris na Omar Msangi na inatarajiwa kushuka dimbani leo ikiwa na nyota wake kama Steven Marashi, Yahya Issa, Salum Swedi 'Kussi', Said Swedi 'Panucci', Herry Morris, Athuman Machuppa, Machotta, Majaliwa, Omar Msangi, Ticotico, Katina Shija na wakali wengine.
Wahenga wenyewe inatarajiwa kuwa chini ya nyota wa zamani wa Majimaji, Simba na Taifa Stars, Madaraka Seleman 'Mzee wa Kiminyio'.


Lampard aipaisha Chelsea


Frank Lampard akishangilia moja ya mabao yake aliyofunga jana


LONDON, England
FRANK Lampard alionyesha thamani yake kwa  Chelsea baada ya kufunga magoli mawili ‘makali’ yaliyoipa ushindi wa ugenini wa mabao 2-1 dhidi ya Everton jana na kukwea hadi katika nafasi yake ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England.
Huku kukiwa na uvumi mwingi kuhusiana na hatma yake ndani ya Chelsea, alionyesha kiwango cha juu na kufunga mabao yote huku goli la Everton likifungwa na Steven Pienaar.
Ushindi wan ne mfululizo wa Chelsea chini ya kocha Rafael Benitez umeiinua hadi kubakiza pointi nne tu kabla ya kuifikia Manchester City inayoshika nafasi ya pili, huku Chelsea ikiwa na mechi moja mkononi.
-----

Mhasibu Simba aporwa mamilioni ya fedha Sinza

Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage


ZAIDI ya Sh. milioni 10 za klabu ya Simba zimeporwa baada ya Mhasibu wa klabu hiyo, Erick Sekiete (28) kudai kuvamiwa na majambazi sita katika mtaa wa Sinza kwa Remmy na kuporwa kiasi hicho cha pesa juzi saa 3:20 usiku.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela alisema kuwa Sh. milioni 7.59 na dola za Marekani 2,000 ambazo Simba walizipata baada ya makato ya mapato ya mechi yao dhidi ya Tusker FC ya Kenya iliyomalizika kwa wenyeji Simba kuchapwa 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
“Simba ilipata mgawo wa Sh. milioni 10.6 na dola za Marekani 2,000 (Sh. milioni tatu) kutokana na mapato ya kiingilio cha mechi yao dhidi ya Tusker. Baada ya makato, walibakiwa na Sh. milioni 7.59 ambazo Sekiete alikabidhiwa,” alisema Kamanda Kenyela.
Alisema kuwa baada ya kukabidhiwa fedha hizo, Sekiete na mwenzake Stanley Phillipo (23) ambaye alidaiwa kuwa ni mwanafunzi, walipanda kwenye gari aina ya Toyota Premio yenye namba za usajili T869 BKS lililokuwa likiendeshwa na Said Pamba na kwamba walipofika eneo hilo, dereva aliwashusha na kwamba wakaanza kutafuta teksi.
Aliendelea kueleza kuwa muda mfupi baada ya kushushwa, Sekiete na Philipo waliamua kuvuka upande wa pili wa barabara ya iendayo Kijitonyama ili wachukue teksi lakini ghafla  walilitekwa na watu sita walioshuka kutoka kwenye pikipiki tatu.
“Mmoja wa watu walioshuka kwenye pikipiki alikuwa na bastola... alifyatua risasi hewani wakati wenzake wakipora begi lenye fedha kutoka kwa mhasibu,” alisema Kenyela.
Aliendelea kufafanua kuwa wakati watu hao wakimnyang’anya begi Sekiete walikuwa wakitamka maneno ya kejeli kwa uongozi wa Simba.
Aliyanukuu maneno hayo kwa kusema; “Mnafungwa halafu mnazingua, na kwa kuwa viongozi wenu wanakula pesa za klabu, nasi hizi tunaziiba.”
Kamanda Kenyela alisema kuwa baada ya watu hao kupora fedha hizo, walitokomea kusikojulikana na hadi sasa, Jeshi la Polisi linawashikilia watu watatu akiwamo Sekiete kuhusiana na tukio hilo.
Watu wengine wanaoshikiliwa na jeshi hilo katika Kituo cha Polisi Magomeni ni Pamba na Philipo ambao walikuwa pamoja na Sekiete kwenye gari.
“Sisi (Jeshi la Polisi) tulishaonya watu kusafirisha kiasi kikubwa cha fedha bila ulinzi, tunawashikilia watu hawa watatu kwa sababu huenda walipanga kuiba fedha hizo,” aliongeza.
“Mazingira ya kuporwa kwa fedha hizo yanatia shaka huenda kuna kitu kilikuwa kimepangwa ili fedha hizo ziibwe. Iweje mtu akahifadhi nyumbani kwake kiasi kikubwa cha fedha kama hicho?” alihoji Kamanda Kenyela.
“Kwa sasa mtu yeyote atakayeripoti kuporwa fedha kiasi kikubwa kama hiki na alikuwa akisafirisha pasipo na ulinzi, tutaanza naye.
“Tunawashikilia wawa watatu kwa uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo. Tunaomba ushirikiano kutoka watu wenye taarifa juu ya waliohusika na tukio hili.”
Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage alinukuliwa jana akidai amesikitishwa na taarifa za kuporwa kwa fedha za klabu yao.
“Mhasibu wetu anaishi Sinza. Alizichukua zile fedha za klabu akazihifadhi nyumbani kwake ili leo (jana) azipeleke benki,” alisema Rage.


Masawe Mtata ana Love position

MCHEKESHAJI mahiri wa kipindi cha 'Ze Comedy Show', Rogers Richard a.k.a. Masawe Mtata, amefyatua filamu mpya iitwayo 'Love Position', akijiandaa pia kupakua nyimbo mpya kwa ajili ya albamu yake ijayo.
Msanii huyo anayefahamika pia kwa jina la Dokta Kicheko, alisema tayari filamu hiyo ya kimapenzi ipo mtaani baada ya kuitoa wiki iliyopita akiwa ameigiza na wasanii kadhaa wenye majina na chipukizi.
Masawe Mtata, alisema filamu hiyo ya 'komedi' imekuja wakati akiwa katika harakati zake za kupakua albamu mpya ya muziki wa kizazi kipya baada ya kutamba na nyimbo kadhaa ukiwemo wa 'Siwezi Kulala'.
"Nimekamilisha na kuiachia filamu yangu mpya iitwayo 'Love Position', huku nikiwa mbioni kukamilisha albamu yangu ya tatu itakayokuwa na nyimbo nane," alisema.
Msanii huyo alisema albamu hiyo inakuja baada ya awali kutamba na albamu za 'Say Ye' au 'Unanipenda Mimi' na 'Mirinda Nyeusi' iliyofahamika pia kama 'Kicheko.com'.
Mchekeshaji huyo, alisema wakati filamu yake hiyo mpya ikiendelea kupokelewa na mashabiki wake, pia anajipanga kuandaa kazi nyingine mpya ili iwe kama 'funguo' kwa mwaka 2013 alioutabiri utakuwa na ushindani mkubwa kisanii nchini.

Saturday, December 29, 2012

RIDHIWANI APONDA MFUMO UENDESHAJI YANGA ADAI AFADHALI WA SIMBA

Ridhiwani akihutubia Waandishi asubuhi ya leo Kiromo Hotel

Na Mahmoud Zubeiry, Bagamoyo
MWENYEKITI wa Kamati ya Kusaidia timu za soka za vijana za taifa, Ridhiwani Kikwete, amesema mfumo wa uendeshwaji wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam ni mbovu kwa sababu unategemea mfuko wa mtu mmoja.
Akizungumza wakati anatoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Hoteli ya Kiromo, Bagamoyo mkoani Pwani, Kikwete alisema kwamba Yanga inahitaji kubadilika kutoka mfumo huo.
Kikwete alisema ni afadhali mfumo wa uendeshwaji wa Simba SC, ambao desturi yao ni kuchangishana.
“Nilijaribu kufanya uchunguzi wa mfumo wa uendeshwaji wa klabu ya Yanga, nikashangazwa ni mfumo mbaya, kwa sababu unategemea mfuko wa mtu mmoja, afadhali Simba wao huwa wanachangishana,”alisema.
Ingawa hakumtaja mtu ambaye mfuko wake unategemewa Yanga, lakini wazi ni Mwenyekiti wa klabu hiyo, Alhaj Yussuf Mehboob Manji.
Kwa ujumla katika hotuba yake, Kikwete alisema haridhishwi na mfumo wa uendeshwaji wa soka ya Tanzania na kwamba unahitaji mabadiliko.
Kikwete aliushauri uongozi wa TASWA upiganie nafasi ya uwakilishi ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kusisitiza juu ya umuhimu wa waandishi nchini kutambua haki zao.
Lakini pia Kikwete aliwaasa waandishi kuepuka uandishi wa kinazi wa Simba na Yanga na badala yake kuzama ndani zaidi katika kuripoti, sambamba na kuripoti michezo yote, badala ya kuegemea kwenye soka pekee.
“Vyombo vya habari lazima viwe na wataalamu tofauti wa kuripoti michezo tofauti, huyu akiegemea kwenye soka, mwingine aegemee kwenye mchezo mwingine, ili kuhakikisha tunafikisha ujumbe vema kwa jamii,” alisema mtoto huyo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Ridhiwani ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, NEC akiiwakilisha Wilaya ya Bagamoyo alisema kwamba ipo haja ya TASWA kuendesha semina kadhaa za kuelimisha Waandishi wa Habari kuweza kuripoti michezo mbalimbali nchini.  
Aidha, katika mkutano huo, wanachama walielimishwa kuhusu uanzishwaji wa Saccos na kuridhia kuanza kwa mchakato wa kuundwa kwa chama cha ushirika wa akiba na mikopo kwa Taswa. Walipendekezwa wajumbe waunde timu ya mpito.

CHANZO:BIN ZUBEIRY

KOCHA  SIMBA KUTUA LEO KUSHUHUDIA MECHI YAO NA TUSKER


KOCHA mpya wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba SC, Mfaransa Patrick Liewig anatarajiwa kuwasili leo nchini na atakuwapo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuishuhudia timu hiyo ikimenyana na mabingwa wa Kenya, Tusker FC.
Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga amesema kwamba, awali kocha huyo alitarajiwa kuawasili nchini juzi, lakini ilishindikana baada ya kukosa nafasi kwenye ndege na sasa mashabiki wa timu hiyo wamtarajie leo.
Alisema kocha huyo ambaye anakuja kurithi mikoba ya Mserbia Profesa Milovan Cirkovick, atakishuhudia kikosi cha Simba kikicheza mechi hiyo kabla ya kuendelea na taratibu nyingine ikiwemo kusaini mkataba wa kazi na baadaye kuanza kutumikia kibarua chake kipya.
Liewig ni kocha wa zamani wa Akademi ya Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa, ASEC Mimosas ya Ivory Coast na Club Africain ya Tunisia, Patrick Liewig na ana Stashahada ya Juu ya ukocha na Shahada ya tatu ya ualimu wa soka ya vijana aliyotunukiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Ufaransa, Gerard Houiller na amehudhuria pia kozi za ufundishaji mazoezi ya viungo Juni mwaka 1999 katika Chuo Kikuu cha Dijon.
Kwa upande wa uzoefu, Liewig alifanya kazi PSG kuanzia mwaka 1989 hadi 1999 kama Kocha Mkuu wa akademi na kuna wakati alikuwa akishirikishwa pia katika programu za timu A, ingawa majukumu yake zaidi yalikuwa ni kwa Under 20, Under 18 aliowawezesha kutwaa Kombe la French Junior Gambardella na Under 16.
Kuanzia mwaka 1989 hadi 1990:  alikuwa Meneja Mkuu wa Tomislav IVIC, 1990 hadi 1991 alikuwa Msaidizi wa Henri Michel, 1991 hadi 1994 alikuwa Msaidizi wa Artur Jorge, 1994 hadi 1996 alikuwa Msaidizi wa Luis Fernandez, 1996 hadi 1998: alikuwa Msaidizi wa Ricardo Gomez, 1998 hadi 1999 alikuwa Msaidizi wa Alain Giresse.
Liewig pia alifundisha Al Wahda FC ya Abu Dhabi kuanzia 1999 hadi 2001, ambayo aliipa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na Kombe la Ligi.
Januari mwaka 2003 alikuwa Msimamizi wa Chama cha Soka UAE katika fainali za Afrika za U20 nchini Burkina Faso.
Kuanzia mwaka 2004 hadi 2009 alikuwa Kocha wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast aliyoipa mataji matatu ya Ligi Kuu ya nchini humo mfululizo, 2004, 2005 na 2006, Super Cup ya nchini humo 2005, 2007, 2008 na 2009 na akaiwezesha kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mara tatu, mara moja akiifikisha Nusu Fainali.
Amekuwa Kocha bora wa Ivory Coast miaka mitatu mfululizo, 2004, 2005 na 2006 na tangu Septemba mwaka jana hadi Juni mwaka huu, alikuwa kocha wa Club Africain ya Tunisia
Kuelekea mchezo wa leo, Simba itamenyana na Tusker FC ambayo ilianza vema ziara yake nchini, baada ya kuichapa Yanga 1-0 katika mchezo ulipigwa kwenye Uwanja wa Taifa Jumatano.
Simba SC na Tusker zinatarajiwa kukutana pia kwenye Kundi la Mapinduzi visiwani Zanziabr hivi karibuni, kwani zimepangwa kundi moja, A pamoja na Bandari ya Unguja na Jamhuri ya Pemba.
Aidha, katika Kundi B, washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Bara, Azam FC ya Dar e Salaam pia, imepangwa na Mtibwa Sugar ya Morogoro, Coastal Union  ya Tanga na Miembeni ya Unguja.
Michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambayo ni maalum kwa ajili ya kuherehekea Mapinduzi matukufu ya Zanzaibar, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 2, hadi kilele cha miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, mwakani, huku ikishirikisha timu kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo iliyotolewa na Kamati Maalum ya Kusimamaia michuano hiyo, inaonesha kuwa katika mchezo wa kwanza utakaochezwa siku ya ufunguzi itakuwa ni kati ya Bandari kutoka Unguja ambayo itacheza na Jamhuri kutoka kisiwani Pemba ambao ni wawakilishi wa Zanzibar katika Kombe la Shirikisho Barani Afrika, pamabanolitakalochezwa katika uwanja wa Mao Tse Tung mjini Unguja, huku usiku wa siku hiyo hiyo katika Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja pambano la ufunguzi rasmi katika mashindano hayo likiwakutanisha mabingwa wa soka nchini Tanzania, Simba SC ambao watapambana na mabingwa wa soka nchini Kenya, Tusker.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo jumla ya timu nane zitashiriki katika mashindano hayo ambayo yamejipatia umaarufu mkubwa visiwani hapa, timu hizo zimegawanya katika makundi mawili ambayo ni kama ifuatavyo:
Awali michuano hiyo ilitarajiwa kuanza kisiwani Pemba tarehe 1 Januari, lakini kutokana na kujitoa katika mashindano kwa klabu ya Al-Ahly ya Misri kutokana na klie kilichoelezwa sababu za kiusalama, mechi zote sasa zitachezwa kisiwani Unguja na ufunguzi ukipangwa kuanza tarehe 2 badala ya tarehe 1 januari.
Bingwa wa michuano hiyo ataondoka na zawadi ya kombe na fedha taslim Tsh.Milioni kumi (10,000,000), mshindi wa pili Milioni tano (5,000,000), pamoja na zawadi nyengine ambazo zimegawanywa katika makundi tofauti ikiwemo zawadi ya mfungaji bora, mchezaji bora, mwamuzi bora, kipa bora, mwandishi wa habari bora, timu bora na zawadi nyinginezo.