STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, January 6, 2017

Rais wa Caf katika kashfa kama ya Blatter

Rais wa Caf, Issa Hayatou
WALIOSEMA kuwa, mwenzako akinyolewa nawe tia kichwa maji, hawakukosea kabisa.
Miezi kadhaa tangu aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Duniani, FIFA, Sepp Blatter kuingia kwenye kashfa nzito ya Rushwa kiasi cha kumlazimu ajiuzulu nafasi yake kabla ya kufungiwa, mzimu wa tuhuma hizo sasa umehamia kwa mshirikisha wake mkubwa, Issa Hayatou Rais wa Shirikisho la Soka Afrika, CAF.
Mamlaka zinazosimamia Mashindano mbalimbali nchini Misri zimethibitisha kuwa Rais huyo wa CAF, atafikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka kutokana na tuhuma za rushwa zinazomkabili zikiwemo zile za utoaji haki za matangazo ya ligi mbalimbali.
Mamlaka hizo zimebainisha kuwa Hayatou alikiuka kipengele namba vifungu (A), (B), (C), (D), (E) za sheria za uhifadhi na ulinzi wa mashindano, baada ya kukiuka matakwa ya kazi yake na kuwapa haki za matangazo kampuni ya Lagardere Sports pekee pasipo kuweka wazi ili kampuni nyingine zenye uwezo pia zijitokeze.
Ripoti inasema kuwa Hayatou aliwapa Lagardere haki za matangazo kwa miaka 12 kuanzia mwaka 2017 mpaka mwaka 2028. CAF ilisaini kandarasi na Lagardere mwezi June 2015, ikiwa ni takribani mwaka mmoja kabla makubaliano ya haki hizo hayajakwisha. Ni sahihi pia kusema kuwa CAF iliwapa haki hizo Lagardere mwaka  2008 mpaka 2016, ikimaanisha kampuni hiyo imepewa mzigo huo kwa miaka 20.
Haki hizi hazikuwa kwa upande wa urushwaji matangazo kwa njia ya satellite peke yake bali hata kwa wenye matumizi ya tovuti, na sio kwa Misri na Afrika peke yake, bali dunia kwa ujumla.
Mamlaka hizo za mashindano ya Misri, zimeomba  CAF kuchukua hatua za haraka kutokana na kifungu cha sheria namba 20 kilichopo kwenye sheria za mashindano, ikiwemo kuvunja mkataba uliopo kati yake na Lagardere kutokana na matokeo iliyonayo kwa Misri.
Mamlaka hiyo pia imetoa ruksa kwa kampuni ya BeIn media pamoja na kampuni nyingine zilizoomba haki ya kurusha matangazo mubashara kuendelea kufanya hivyo hasa kwa ajili ya mashindano ya mataifa ya Afrika, 2017 AFCON itakayoanza January 14.
CAF iabadili pia namna haki za matangazo za mashindano mbalimbali zinavyouzwa nchini Misri katika mantiki ya kugawanya vifurushi vinavyohakikisha kutengeneza mazingira yatakayovutia mahsindano hayo kurushwa na vituo.
Mamlaka za mashindano zinaweka wazi kuwa CAF ina mlengo wa kuhakikisha inalinda na kusimamia sheria za mashindano na pia inatakiwa  kufuata hivyo kulingana na makubaliano yaliyopo kati ya serikali ya Misri na CAF.
Na kwa taarifa zinazoendelea kutoka ni kuwa CAF ina mpango wa kuhamisha makazi yake kutoka nchini Misri, lakini mamlaka ya mashindano imesema kuweza kufanya hivyo asilimia 75 ya wanachama ambao ni nchi 54 wanatakiwa kupiga kura kukubali kwenye mkutano mkuu kutokana na sheria za CAF kifungu namba 1.
FIFA ambalo Hayatou aliwahi kuongoza kwa muda kama Rais baada ya Blatter kutangaz kujiuzulu mapema mwaka uliopita, lilikumbwa na kashfa kubwa kiasi cha kufanya chaguzi mkuu mara mbili katika msimu mmoja.

Msuva aiaibisha Simba mapema Kombe la Mapinduzi 2017

Simon Msuva
Hekaheka wakati wa pambano la Simba na Yanga Oktoba 1, 2016 lililoisha kwa sare ya 1-1.
HATA kabla ya Watani wa Jadi, Simba na Yanga hazijajua kama zitakutana kwenye mechi za nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi 2017 kule visiwani Zanzibar, tayari Vijana wa Jangwani wameipiga bao Simba.
Tena aliyeiopiga bao ni kijana mmoja mfupi hivi, ambaye amekuwa akipata wakati mgumu mbele ya mashabiki wa Jangwani kila Yanga inapocheza jijini Dar es Salaam. Mashabiki wasio na ustaarabu wala kuheshimu mchango wa nyota wao, Simon Msuva wamekuwa wakimtusi na kumtolea kejeli winga huyo, lakini ukirejea kwa kile anachjokifanya uwanjani utajua Msuva ni nani!
Winga huyo anayeongoza orodha ya ufungaji bora katika Ligi Kuu Bara kwa sasa akiwa sambamba na Amissi Tambwe anayecheza naye pale Jangwani na Shiza Kichuya wa Wekundu wa Msimbazi ni balaa.
Katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, Msuva ameifanyia mbaya Simba hata kama ya kukutana nao baada ya kufunga mabao manne ambayo ni moja zaidi ya iliyonao wapinzani wao hao kutoka Mtaa wa Msimbazi.
Katika mechi mbili tu za Kombe la Mapinduzi, Msuva amefunga mabao hayo, huku kikosi kizima cha Simba kikiwa kimecheza mechi tatu mpaka sasa, lakini kikiwa na mabao matatu tu, yaliyofungwa na Mzamiru Yassin mawili na Juma 'Ndanda' Liuzio.
Kwa lugha nyepesi unaweza kusema kuwa Msuva ameibwaga Simba kwa mabao 4-3 hata kabla timu yake na Wekundu wa Msimbazi hazijashuka uwanjani wikiendi hii kusaka tiketi ya kukutana ama kukwepana pale Unguja.
Msuva alianza kwa kufunga mabao mawili walipoikamua Jamhuri ya Pemba kwa mabao 6-0, kabla ya kuongeza mengine walipoizamisha Zimamoto na kama sio kukosa umakini katika mechi hiyo ya pili jamaa angetupia hat trick kwani alipata nafasi ya kupiga penalti, lakini akashindwa kukwamisha kimiani.
Bila ya shaka mashabiki wa Simba kokote walipo kwa sasa watakuwa wanajiuliza itakuwa vipi kama chama lao litakutana na Yanga katika michuano hiyo kwa mziki mnene iliyonayo wapinzani wao hao.
Katika mechi yao ya pili, Yanga iliwakosa washambuliaji wake wote wa kati baada ya Donald Ngoma na Amissi Tambwe kutocheza kabisa, lakini katika mechi yao ya kesho dhidi ya Azam huenda majembe hayo yakawepo.
Simba kwa upande wao makali yake kwa sasa yanabebwa na viungo wake wajanja, Mzamiru, Mohammed Ibrahim na Pastory Athanas, huku wakipigwa tafu na Liuzio ambaye katika mechi ya tatu ya Simba dhidi URA Uganda alianza sambamba na Laudit Mavugo ambaye amekuwa na hali mbaya klabuni.
Je, Msuva ataendelea kuikimbiza Simba ama Simba itatafuta upenyo wa kuukacha mziki wa Jangwani na kusubiri kujua majaliwa yao kwenye fainali ya michuano hiyo Januari 13? Tusubiri tuone.

Hebu msikieni Gerard Pique na ulalamishi wake

Wachezaji wa Barcelona wakimlalamikia mwamuzi katika mechi yao ya jana dhidi ya Atheltico Club
Beki Gerard Pique akisikitika akiwa nyavuni wakati timu yake ikipokea kipigo cha mabao 2-1.
KUMBE wepesiiii. Barcelona wameuanza mwaka vibaya baada ya kujikuta wakitunguliwa mabao 2-1 na Athletico Club, huku beki wake Gerard Pique akitupa lawama kwa waamuzi wa pambano hilo.
Pique amedai kuwa waamuzi nchini Hispania wanawapendelea mahasimu wao wakuu, Real Madrid baada ya klabu hiyo kuchapwa katika mchezo wa Kombe la Mfalme uliochezwa usiku wa jana.
Barcelona walilalamikia penalti mbili, moja iliyomhusisha Neymar na nyingine Pique, ambazo zilikataliwa katika mchezo huo wa mkondo wa kwanza hatua ya timu 16 bora, ingawa baadae wenyeji Bilbao walipoteza wachezaji wawili kwa kadi nyekundu Raul Garcia na Ander Iturraspe.
Akihojiwa beki huyo wa kimataifa wa Hispania alisema penalti hizo zilikuwa za wazi kabisa, lakini anadhani wanajua kwanini wanafanyiwa hivyo.
Pique aliendelea kudai kuwa waamuzi wamekuwa wakiwakwamisha kwa kuonyesha upendeleo kwa Madrid akitolea mfano wa mechi yao ya jana dhidi ya Sevilla ambayo walishinda mabao 3-0.

Pep Guardiola mzuka mtupu Kombe la FA

Kocha Guardiola
 
UKISIKIA mzuka unapanda ndiko huku bwana! Menaja wa klabu ya Manchester City, Pep Guardiola amesema ana hamu kubwa ya kusimamia mchezo wake wa kwanza wa michuano ya Kombe la FA wakati kikosi chake kitakapovaana na West Ham United usiku wa leo Ijumaa.
Man City iliyopo nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England baada ya kushushwa na Tottenham Hotspur iliyoinyoa Chelsea kwa mabao 2-0, itavaana na Wagonga Nyundo hao wa London katika mchezo wa mzunguko wa tatu.
City wanatarajiwa kukwaana na West Ham katika Uwanja wa London baadae leo usiku na wakati akihojiwa Kocha Guardiola alisema michuano hiyo ni muhimu kwa sababu timu za chini zinaweza kuzifunga timu kubwa ndio maana inakuwa na msisimko.
Kocha huyo aliendelea kudai kuwa ana hamu kubwa na mchezo huo, lakini utazikutanisha timu zote za Ligi Kuu hivyo utakuwa mgumu.
Michezo mingine ya michuano hiyo maarufu na mikongwe barani Ulaya itachezwa wikiendi hii na Jumatatu kama ratiba inayoonyesha chini;     

    07.01. 15:30    Manchester United    Reading       
    07.01. 18:00    Accrington    Luton       
    07.01. 18:00    Barrow    Rochdale       
    07.01. 18:00    Birmingham    Newcastle Utd       
    07.01. 18:00    Blackpool    Barnsley       
    07.01. 18:00    Bolton    Crystal Palace       
    07.01. 18:00    Brentford    Eastleigh       
    07.01. 18:00    Brighton    Milton Keynes Dons

    07.01. 18:00    Bristol City    Fleetwood Town       
    07.01. 18:00    Everton    Leicester       
    07.01. 18:00    Huddersfield    Port Vale       
    07.01. 18:00    Hull City    Swansea       
    07.01. 18:00    Ipswich    Lincoln City       
    07.01. 18:00    Millwall    Bournemouth       
    07.01. 18:00    Norwich    Southampton       
    07.01. 18:00    QPR    Blackburn       
    07.01. 18:00    Rotherham    Oxford Utd       
    07.01. 18:00    Stoke City    Wolves       
    07.01. 18:00    Sunderland    Burnley       
    07.01. 18:00    Sutton    AFC Wimbledon       
    07.01. 18:00    Watford    Burton       
    07.01. 18:00    West Brom    Derby       
    07.01. 18:00    Wigan    Nottingham       
    07.01. 18:00    Wycombe    Stourbridge       
    07.01. 20:30    Preston    Arsenal
    08.01. 14:30    Cardiff    Fulham       
    08.01. 16:30    Liverpool    Plymouth       
    08.01. 18:00    Chelsea    Peterborough       
    08.01. 18:00    Middlesbrough    Sheffield Wed

    08.01. 19:00    Tottenham    Aston Villa       
    09.01. 22:45    Cambridge Utd    Leeds

Mashetani Wekundu kumbe hawatanii kwa Griezmann

WAMEPANIA aisee! Klabu ya Manchester United inadaiwa imeanza kufanya mazungumzo ya kumuwania straika wa kimataifa wa Ufaransa, Antoine Griezmann, huku ikielezwa kuwa inatarajiwa kumpa ya mshahara wa pauni 220,000 kwa wiki ili kumshawishi kutua Old Trafford.
Duru za michezo zinadai kuwa, Mashetani Wekundu tayari wameanza mazungumzo na wawakilishi wa nyota huyo wa Atletico Madrid na imeahidi mshahara wake utafikia ule anaolipwa kiungo Paul Pogba aliyepo ndani ya klabu hiyo ya EPL.
Griezmann ameshawahi akikaririwa akieleza jinsi anavyoihusudu United na Mourinho katika mahojiano yake huko nyuma. Kama wakifikia makubaliano hayo United inadaiwa italazimika kutoa kitita cha pauni milioni 86 ili kutengua kitenzi katika mkataba wa mshambuliaji huyo ambaye amekuwa akizitoa udenda klabu nyingi barani Ulaya kwa soka lake murua.

Kocha Mourinho kiroho safi ongezeko la timu WC

AMEKUBALI. Kocha wa klabu ya Manchester United, Jose Mourinho 'Special One', amekuwa kocha wa kwanza kuunga  mkono mapendekezo ya kuongeza timu kufikia 48 katika Kombe la Dunia akiamini kuwa wachezaji watalindwa vyema.
Rais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Gianni Infantino ana matumaini mpango wake kuwa na makundi 16 yenye timu tatu kuanzia michuano ya mwaka 2026 utapitishwa wakati wa kikao cha kamati ya utendaji ya shirikisho hilo wiki ijayo.
Muungano wa Klabu Ulaya ambao United pia ni mjumbe wake, tayari wameshaonyesha kutounga mkono pendekezo hilo, lakini Kocha Mourinho yeye anaunga mkono.
Akihojiwa kuhusiana na suala hilo, Mourinho alisema anaunga mkono kwa vile ana uhakika FIFA itazingatia maslahi ya wachezaji kwa kutowachezesha mechi nyingi zaidi kuliko sasa.

Msuva mkimchekea tu, kabeba mwanangu!

Msuva Kulia akiwajibika katika mechi za Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam. Timu hizo kesho zitavaana kwenye Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar.
UMEIANGALIA orodha ya Wafungaji Bora wa sasa wa michuano ya Kombe la Mapinduzi? Jina la Simon Msuva bila shaka ndilo linaloongoza kwa sasa akiwa ametupia kambani mabao manne.
Sasa kama hujui, idadi hiyo ya mabao aliyonayo sasa ndiyo iliyompa tuzo Mwaka 2015 alipochaguliwa kuwa Mfungaji Bora akiwafunika wakali wengine.
Msuva kwa sasa anaongoza orodha hiyo na kama kesho Jumamosi atatupia tena kambani kuna uwezekano mkubwa wa kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao mengi kwenye michuano hiyo iliyoasisiwa 2007.
Michuano ya Mapinduzi kwa mwaka jana wa 2016, Peter Lwasa wa URA ndiye aliyekuwa Mfungaji Bora akitupia kimiani mabao matatu.
Msuva amekiri kwamba kiu yake katika michuano ya mwaka huu ni kuona anaibuka Mfungaji Bora na hata kunyakua Mchezaji Bora na kuisaidia pia Yanga kubeba taji lao la pili la michuano hiyo inayoendelea visiwani Zanzibar.
Mpaka sasa Msuva amafukuziwa kwa karibu na wachezaji wawili, Abdul-Samad Kassim wa Jang'ombe Boys aliyepiga hat trick ya kwanza katika michuano hiyo na Bokota Labama wa URA-Uganga wenye mabao matatu kila mmoja.
Kwenye michuano ya mwaka huu Mfungaji Bora na Mchezaji Bora atazawadiwa kila mmoja kitita cha Sh. 1 milioni moja kama atakachopewa Kipa Bora, Mchezaji Bora Chipukizi, Mwamuzi Bora na Kocha Bora, fedha ambazo zimetolewa na mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Khamis Chuma.

Orodha ya Wafungaji;

4 Simon Msuva                     (Yanga)
3 Bokota Labama                    (URA)
   Abdul Kassim 'Hasgut' (Jang'ombe)
2 Khamis Makame         (Jang'ombe)
   Donald Ngoma                  (Yanga)
   Mzamiru Yassin                 (Simba)
1 Seif Hassan 'Banda'             (Taifa)
   Juma Liuzio                      (Simba)
   Laudit Lufunga  o.g           (Simba)
   Thabani Kamusoko            (Yanga)
   Bakar Mahadhi                  (Yanga)
   Shaaban Idd                      (Azam)

   Salum Songoro                    (KVZ)

Hiki ndicho kikosi bora cha Afrika 2016

Pierre-Emerick Aubemeyang wa Gabon

Sadio Mane wa Senegal
MASTRAIKA waliokuwa wakichuana kwenye Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika kwa mwaka 2016, Pierre-Emerick Aubameyang, Riyad Mahrez na sadio Mane ndio wanaouunda safu ya ushambuliaji ya Kikosi cha Timu Bora ya Afrika ya Mwaka 2016.
Kikosi hicho kilitangazwa jana kwenye sherehe za utoaji tuzo za Caf ambapo kipa Mganda, Dennis Onyango ndiye pekee toka Ukanda wa Afrika Mashariki aliyeingia kikosini.
Kwa mujibu wa Caf kikosi hicho kipo hivi;
Kipa: Dennis ONYANGO (Uganda & Mamelodi Sundowns)
Mabeki: Serge AURIER (Cote d’Ivoire & Paris Saint-Germain), Aymen ABDENNOUR (Tunisia & Valencia), Eric BAILLY (Cote d’Ivoire & Manchester United), Joyce LOMALISA (DR Congo & AS Vita)
Viungo: Khama BILLIAT (Zimbabwe & Mamelodi Sundowns), Rainford KALABA (Zambia & TP Mazembe), Keegan DOLLY (South Africa & Mamelodi Sundowns),
Mastraika: Pierre-Emerick AUBAMEYANG (Gabon & Borussia Dortmund), Sadio MANE (Senegal & Liverpool), Riyad MAHREZ (Algeria &Leicester City).


Wachezaji wa Akiba: Aymen MATHLOUTHI (Tunisia & Etoile du Sahel), Kalidou KOULIBALY (Senegal & Napoli), Salif COULIBALY (Mali & TP Mazembe), Islam SLIMANI (Algeria & Leicester City), Mohamed Salah (Egypt & Roma), Kelechi IHEANACHO (Nigeria & Manchester City), Alex IWOBI (Nigeria and Arsenal).

Simba yabanwa, Yanga ikiisubiri nusu fainali Mapinduzi Cup


Benchi la Simba likifuatilia moja ya mechi zao za Mapinduzi Cup 2017
Yanga kabla ya mechi yao ya Jamhuri Pemba
NA RAHMA WHITE, Z'BAR
SIMBA, jana usiku ilishikwa shati na Watoza Ushuru wa Uganda, URA, lakini kesho Jumamosi kutakuwa na kazi kubwa itakayozikutanisha timu za Yanga na Azam ili kuamua hatma ya Kundi B katika Kombe la Mapinduzi 2017.
Michuano hiyo inayoendelea usiku wa leo kwa pambano moja tu la Kundi A kati ya Taifa Jang'ombe 'Wakombozi wa Ng'ambo dhidi ya KVZ, inachezwa kwenye Uwanja wa Amaana, Zanzibar na jana Simba ilitoka suluhu na URA.
Kwa matokeo hayo Simba imeendelea kuongoza kundi A ikiwa na pointi saba baada ya kushushwa kwa muda katika nafasi hiyo na Jang'ombe Boys ambayo jioni ya jana ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya KVZ.
Katika pambano hilo la mapema, Abdul Samad Kassim Hasgut alikuwa mchezaji wa kwanza kwa msimu huu kufunga hat trick wakati wakiizamisha KVZ ambayo ilitangulia kupata bao dakika ya tano tu kupitia Salum Songoro.
Hata hivyo kazi ipo kesho asikuambie mtu, Yanga na Azam zitavaana kuamua nani aongoze kundi ili kuelekea mechi za njusu fainali zitakazopigwa wiki ijayo.
Yanga inaongoza msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi sita huku Azam ikiwa nyuma yao na pointi zao nne na Jamhuri ni ya tatu ikiwa na pointi moja ambapo mapema jioni ya kesho itavaana na Zimamoto ambayo imeshaaga mashindano hayo mapema kwa kupigwa mechi zao mbili za awali.
Pambano la Yanga na Azam linavuta hisia kubwa kutokana na ushindani uliopo baina ya timu hiyo, japo safari hii Azam inaonekana wanyonge kwa kufanya vibaya katika Ligi Kuu Bara na juzi kati ilibanwa mbavu na Jamhuri na kutoka nao suluhu. Jamhuri ilitunguliwa na Yanga mabao 6-0 katika mechi yao ya kwanza na wengi walidhani Azam ingefuata nyayo hizo, lakini ikajikuta ikiomba pambano limalizike kwa namna Jamhuri walivyowakimbiza uwanjani.
Matokeo yoyote kwa Yanga mbali na kipigo yataifa uongozi wa kundi hilo na kusikiliza mechi za keshokutwa Jumapili za Kundi A ili kujua itavaana na nani kwenye hatua ya nusu fainali.
Jumapili vinara wa Kundi A, Simba itavaana na Jang'ombe Boys iliyopo nafasi ya pili majira ya usiku na mapema jioni ya siku hiyo URA iliyopo nafasi ya tatu itamaliza kazi dhidi ya Taifa Jang'ombe.
Matokeo yoyote ya kundi hilo yanaweza kuzifusha timu za Simba, Jang'ombe Boys, URA  na hata Taifa jang;ombe kucheza nusu fainali na moja yao itakuwa na nafasi ya kuvaana na Yanga ambayo katika mechi mbili za awali imeshinda kwa mabao nane huku wavu wao ukiwa haujaguswa tofauti na wapinzani wa kundi hilo la A.
Mechi za wikiendi hii za kukamilishia hatua ya makundi za michuano hiyo ndizo zitakazoamua timu zipi tatu za mwisho za kuungana na Yanga iliyotangulia mapema kucheza nusu fainali.

Mambo yalivyo Kombe la Mapinduzi 2017

Des 30, 2016
Taifa Jang'ombe 1-0 Jang'ombe Boys (Seif Hassan 'Banda')

Jan 01, 2017
URA 2-0 KVZ  (Bokota Labama  57', 90')
Taifa Jang'ombe 1-2 Simba (Mzamiru 27', Liuzio 41'; Lufunga 76 Og)

Jan 02, 2017
Azam 1-0 Zimamoto (Shaaban Idd 79')
Yanga 6-0 Jamhuri (Msuva 19', 40', Ngoma 23', 37', Kamusoko 59', Mahadh 85')

Jan 03, 2017
URA 1-2 Jang'ombe Boys (Bokota Labama 31'; Khamis Makame '19', 51')
KVZ 0-1 Simba (Mzamiru 44')

Jan 04, 2017
Yanga 2-0 Zimamoto (Msuva 11', 21')
Azam 0-0 Jamhuri

Jan 05, 2017
KVZ 1-3 Jang'ombe Boys (Salum Songoro 5'; Abdul Kassim 20', 35', 45)
Simba 0-0 URA

Ratiba ilivyo sasa


Leo Ijumaa

Taifa Jang'ombe v KVZ Saa 2:30 usiku

Kesho Jumamosi

Jamhuri v Zimamoto Saa 10:00 jioni
Azam v Yanga Saa 2:30 usiku

Jumapili Jan 08, 2017

Simba v Jang'ombe Boys Saa 10:00 jioni
Taifa Jang'ombe v  URA Saa 2:30 usiku

Jan 10, 2017
Nusu Fainali

Mshindi A v Wa Pili B Saa 10:00 jioni
Mshindi B v Wa Pili A Saa 2:30 usiku

Jan 13, 2017

Mshindi NF1 v Mshindi NF2 Saa 2:30

Msimamo
Kundi A:
                         P  W  D  L  F  A  Pts
1. Simba           3   2   1   0  3  1   7
2. Jang'ombe     3   2   0  1   5  3   6
3.  URA             3   1   1  1   3  2   4
4. Taifa              2   1   0  1   2  3   3
5. KVZ               3   0   0  3   1  6   0

Kundi B
                       P  W  D  L  F  A  Pts
1. Yanga           2   2   0  0  8  0  6
2. Azam            2   1  1   0  1  0  4
3. Jamhuri        2   0   1   1  0  6  1
4. Zimamoto     2   0   0   2  0  3  0

Wafungaji:
4 Simon Msuva         (Yanga)
3 Bokota Labama     (URA)
   Abdul Kassim 'Hasgut' (Jang'ombe)
2 Khamis Makame    (Jang'ombe)
   Donald Ngoma      (Yanga)
   Mzamiru Yassin     (Simba)
1 Seif Hassan 'Banda' (Taifa)
   Juma Liuzio            (Simba)
   Laudit Lufunga  o.g (Simba)
   Thabani Kamusoko(Yanga)
   Bakar Mahadhi        (Yanga)
   Shaaban Idd            (Azam)

Orodha ya Mabingwa wa Mapinduzi
Mwaka     Bingwa            Mshindi wa Pili
2007         Yanga SC          Mtibwa Sugar
2008         Simba SC          Mtibwa Sugar
2009         Miembeni          KMKM
2010         Mtibwa Sugar    Ocean View
2011         Simba SC          Yanga SC
2012         Azam FC           Simba SC
2013         Azam FC           Tusker FC
2014         KCCA                Simba SC
2015         Simba SC          Mtibwa Sugar
2016         URA                  Mtibwa Sugar
2017          ??                          ??

Mahrez ndiye Baba lao Afrika, Onyango amrithi Samatta


Mahrez akiwa na tuzo yake ya Mchezaji Bora wa Afrika 2016
Akiwa kazini Leicester
Kipa Dennis Onyango wa Uganda aliyemrithi Samatta
RIYAD Mahrez amembwaga straika wa kimataifa wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang katika kinyang'anyiro cha Tuzo za Mchezaji Bora wa Afrika 2016 baada ya Mualgeria huyo kunyakua tuzo hiyo kwa mara ya kwanza.
Tuzo hizo za Wanasoka waliofanya vema kwa mwaka 2016 zilifanyika usiku wa kuamkia leo mjini Abuja, Nigeria na kusindikizwa na burudani toka kwa wasanii mbalimbali akiwamo Diamond Platinumz na Rayvan.
Mahrez anayekipiga Leicester City ametwaa tuzo hiyo kwa kupigiwa kura 361 akimzidi Aubameyang aliyekuwa akitetea tuzo hiyo aliyevuna pointi 313 na Sadio Mane wa Senegal akiambulia nafasi ya tatu na pointi 186.
Hiyo ni tuzo ya pili Afrika kwa Mahrez kwani hivi karibuni alitwaa tuzo ya Mwanasoka wa Afrika wa BBC 2016.
Mahrez na tuzo yake ya BBC

Kwa upande wa Mchezaji Bora wa Afrika Wanaocheza barani humu, nafasi hiyo ilitwaliwa na kipa Dennis Onyango aliyewafunika washindani wake, Khama Brilliat anayecheza naye Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Rainford Kalaba wa TP Mazembe.
Mganda huyo ametwaa tuzo hiyo akimpokea Mtanzania anayekipiga Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta aliyeitwaa mwaka jana nchini humo akiwa na klabu ya TP Mazembe ya DR Congo.
Uganda iliendelea kutisha baada ya timu yao ya taifa, The Cranes kushinda tuzo ya Timu Bora ya Taifa, huku Mamelodi Sunsdowns ikiwa Klabu Bora ya Mwaka ya Afrika na Kocha wa klabu hiyo Pitso Mosimane akitwaa tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka.
Tuzo nyingine zimeenda kwa Kelechi Iheanacho kama Mchezaji Mwenye Kipaji na Alex Iwobi anayeichezea Arsenal akitwaa tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Afrika, wote hao wanatokea Nigeria, huku Mwanasoka Bora wa Kike nafasi ikienda kwa Asisat Ashoala kutoka Nigeria.
Tuzo ya Gwiji wa Afrika ilienda kwa wakali wawili wa zamani wa Laurent Pokou wa Ivory Coast na Emilienne Mbango wa Cameroon, huku timu ya wanawake ya Nigeria ikishinda kuwa Timu Bora ya Soka la Wanawake.
Mwamuzi Bakary Gassama wa Gambia alipiga 'hat trick' ya kuwa Mwamuzi Bora wa Afrika kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kufanya hivyo pia mwaka 2014 na 2015 kabla ya jana usiku mjini Abuja, Nigeria kutwaa tuzo hiyo tena naye  Rais wa Shirikisho la Soka la Guinea Bissau, Manuel Lopes Nascimento alitwaa tuzo ya Kiongozi Bora wa Soka wa barani Afrika.

Orodha ya Washindi wa Tuzo za CAF 2016

Mchezaji Bora wa Afrika wa Mwaka
Riyad Mahrez (Algeria & Leicester City)

Mchezaji Bora wa Mwaka Anayecheza Afrika
Dennis Onyango (Uganda & Mamelodi Sundowns)

Mchezaji Bora wa Kike wa Mwaka
Asisat Oshoala (Nigeria & Arsenal)

Chipukizi Mwenye Kipaji cha Aina Yake
Kelechi Iheanacho (Nigeria & Manchester City)

Chipukizi Bora wa Mwaka
Alex Iwobi (Nigeria & Arsenal)

Kocha Bora wa Mwaka
Pitso Mosimane (Mamelodi Sundowns)

Klabu Bora ya Mwaka
Mamelodi Sundowns

Timu Bora ya Taifa ya Mwaka
Uganda The Cranes

Timu Bora ya Taifa ya Wanawake
Nigeria

Mwamuzi Bora wa Mwaka:
Bakary Papa Gassama

Friday, September 9, 2016

Wilshere mbona mtamu, subirini tu muone-Wenger

http://www.telegraph.co.uk/content/dam/football/2016/04/07/jack-wilshere8-large_trans++qVzuuqpFlyLIwiB6NTmJwfSVWeZ_vEN7c6bHu2jJnT8.jpgMBONA freshi tu! Kocha wa klabu ya NEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amedai kuwa Jack Wilshere anaweza kuitumikia klabu hiyo kwa kipindi kirefu mbele ya safari huku akisisitiza kuwa kiungo huyo hana chochote cha kumuonyesha zaidi ya kuwa fiti. Wilshere ameenda kwa mkopo wa msimu mzima katika klabu ya AFC Bournemouth dakika za mwisho kabla ya dirisha la usajili majira ya kiangazi halijafungwa ikiwa kama sehemu ya mikakati ya kujijenga upya kufuatia kusumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara katika misimu miwili iliyopita.
Akizungumza kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Southampton, Wenger alipuuza habari kuwa amekuwa haelewani na kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24 ambaye amekuwa akimtaja kuwa na uwezo mkubwa.
Kocha Wenger alisema alizungumza na Wilshere naye alimwambia hadhani kama ataweza kupata muda wa kutosha kucheza akibakia hapo kwa vile anataka  kucheza zaidi msimu huu baada ya kupona majeruhi yake.
Wengeraliendelea kudai kuwa alimruhusu kuondoka kwasababu alikuwa hawezi kumuahidi muda wa kutosha wa kucheza kama alivyotaka mwenyewe.

Ronaldo kamili gado kuanza mambo La Liga

http://www.ronaldo7.net/news/2014/04/824-cristiano-ronaldo-fitness-drills.jpgUSIYEMPENDA Kaja. Ndivyo ambavyo Osasuna watakuwa wanawaza sana, baada ya kuwepo kwa taarifa kwamba nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo yupo fiti na kesho huenda akashuka uwanjani kuvaana nao.
Straika huyo amebainisha kuwa atarejea uwanjani Jumamosi hii katika mchezo dhidi ya Osasuna.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 amekuwa akijiuguza goti lake katika majeruhi aliyopata katika mchezo wa fainali ya michuano ya Ulaya hali iliyomfanya kukosa mechi ys Super Cup ya Ulaya na zingine walizocheza Madrid katika La Liga msimu huu. Akihojiwa kuhusiana na hali yake inavyoendelea, nahodha huyo wa Ureno amesema yuko tayari kurejea uwanjani na anatarajia kucheza katika mchezo dhidi ya Osasuna.
Madrid wameshinda mechi zao zote mbili za la Liga walizocheza msimu huu, kwa kuzifunga Real Sociedad na Celta Vigo.

Buriani Kocha Mohammed Hassan Msomali

Kocha Mohammed Hassan 'Msomali' enzi za uhai wake hivi karibuni
Msomali wa kwanza kushoto waliochuchumaa enzi za uhai wake akikipiga Cosmopolitan
ALIYEKUWA Kocha mkongwe na mwenye mafanikio makubwa nchini, Mohammed Hassan 'Msomali' (74) amezikwa leo mjini Morogoro baada ya kufariki dunia jana mchana nyumbani kwake mjini humo.
Marehemu aliyewahi kuzichezea Yanga, Cosmo na Taifa Stars kwa mafanikio makubwa kabla ya kuzinoa timu za Tumbaku, Mseto, Pan Africans na Moro United sambamba na timu za Mkoa wa Morogoro na Taifa Stars, atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika soka la Tanzania.
Ukiondoa kuwa miongoni mwa walioisaidia Cosmo kubeba taji la Ligi ya Tanzania mwaka 1968 wakiipoka Simba (enzi za Sunderland) iliyokuwa ikimiliki taji kwa miaka miwili tangu kuanzishwa kwa Ligi hiyo mwaka 1965, pia ndiye kocha wa kwana kubeba taji kwa timu za mkoani.
Alifanya hivyo mwaka 1975 akiwa na Mseto ya Morogoro na kubeba tena akiiongoza Pan Africans mwaka 1982.
Kocha huyo ndiye aliyewaibua nyota mbalimbali waliowahi kutamba na kuendelea kuwa kiigizo chema kwa wanasoka wa kisasa kama Zamoyoni Mogella, Malota Soma, John Simkoko, Omar Hussein, na kikosi cha dhahabu cha Pan Africans wakiongozwa na kipa Juma Pondamali, Sunday Manara, Mohammed Mkweche, Mohammed Yahya 'Tostao' Mohammed Rishard Adolph, Jafar Abdulrahman, Ally Katolila na wengine.
Mwaka jana kocha huyo aliyekuwa kiungo mahiri na aliyeiwakilisha Tanzania kwenye michezo ya Afrika (All Africa Games) mwaka 1973 ilipofanyikia Nigeria, alienda kuhiji Makka kwa maana hiyo mautio yamekumta akiwa ni ALHAJI.
Innalillah Waina Illaiy Rajiun. Tangulia mzee wetu Mohammed Msomali, nasi tu nyuma yako. Blog hii ya Micharazo Mitupu inatoa pole kwa ndugu, jamaa, familia na rafiki wa marehemu Msomali sambamba na wadau wa soka kwa kuwakumbusha kuwa kila nafsi itaonja mauti.Tumuombee katika safari yake ya Ahera nasi tukijiandaa kwa safari hiyo kwa vile hatujui saa, siku wala mwaka.

Sikia hii kutoka Chadema kuhusu jeshi la Polisi


Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho Kinondoni Dar es Salaam leo mchana, wakati akitoa madai ya kushikiliwa kwa wafuasi wa chama hicho zaidi ya 70 wasiofahamika na wengine 10 katika vituo mbalimbali vya polisi jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kujihusisha na masuala ya Umoja wa Kupinga Udikiteta (Ukuta), bila ya kufikishwa mahakamani. Kushoto ni Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene.
Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho Kinondoni Dar es Salaam leo mchana, wakati akitoa madai ya kushikiliwa kwa wafuasi wa chama hicho zaidi ya 70 wasiofahamika na wengine 10 katika vituo mbalimbali vya polisi jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kujihusisha na masuala ya Umoja wa Kupinga Udikiteta (Ukuta). Kulia ni Mwenyekiti Baraza la Umoja wa Vijana Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi na kushoto ni Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Mkutano na wanahabari ukiendelea.

Na Dotto Mwaibale
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kinakusudia kufungua maombi katika Mahakama Kuu ya kuiomba mahakama hiyo kuiamuru Polisi kuwafikisha mahakamani watu wanaoshikiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi jijini Dar es Salaam.
Hatua hiyo inatokana na chama hicho kudai kuwa kuna watu 10 ambao wanashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi (Central) na Kituo cha Oysterbay vya Dar es Salaam kwa zaidi ya wiki mbili bila kupewa dhamana ya polisi au kufikishwa mahakamani.
Kauli hiyo ya Chadema imetolewa na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu yake yaliyo mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam leo mchana.
Akifafanua kuhusu Habeas Corpus alisema, ni mamlaka iliyonayo Mahakama Kuu ya kuamuru mamlaka yoyote ya kiserikali inayomshikilia mtu kumpeleka mtu huyo mahakamani.
Lissu alisema, vijana hao walikamatwa katika mikoa mbalimbali kwa makosa aliyodai kuwa ni kujihusisha na haraka za kinachoitwa Umoja wa Kupambana na Udikteta (UKUTA) pamoja na masuala mengine ya kisiasa.
“Kama ikifika Jumanne hawajapelekwa mahakamani au hawajapewa dhamana ya polisi, tutakwenda Mahakama Kuu kufungua maombi ya habeas corpus, imuite IGP au DCI au Ma-RPC au wakuu wa vituo wanakoshikiliwa hao waeleze kwanini wanawashikilia hao watu kwa zaidi ya wiki mbili,” alisema Lissu.
Lissu alisema tayari wameshaanza maandalizi ya hati hizo ambazo zitapelekwa Mahakama Kuu ili iweze kuwaita kati ya Mkuu wa Polisi (IGP), Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Makamanda wa Polisi wa Mikoa au Wakuu wa Vituo vya Polisi wanakoshikiliwa watu hao.
Alifafanua kuwa alionana na watu hao ambao wamedai mbali na kushikiliwa lakini pia wamepigwa na kuteswa huku wakidai kuwa wamekuwa wakichukuliwa usiku na kupelekwa katika eneo lililopo Mikocheni ambako wanateshwa na kurudishwa polisi.
Alisema jeshi la polisi linakiuka sheria na haki za binadamu kwa kuwashikilia watu hao kwa muda mrefu bila kuwapa dhamana au kuwafikisha mahakamani kwa ajili ya kusomewa mashitaka.

Nyie vipi, Ngoma? Mambo yapo kwa Bocco baba'ake

http://www.cecafafootball.org/wp-content/uploads/2014/03/john-bocco.jpg
John Bocco akishangilia moja ya mabao yake
Na Tariq Badru

KUELEKEA raundi ya nne ya Ligi Kuu Bara, nahodha wa Azam, John Bocco 'Adebayor' amewafunika mapro wa kimataifa wa klabu za Simba na Yanga katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu.
Bocco ambaye yupo jijini Mbeya akiwa na kibarua cha kuiongoza tena timu yake kusaka pointi tatu ugenini dhidi ya Wagonga Nyundo wa jiji hilo, mpaka sasa ana mabao matatu akiongoza orodha ya wafungaji.
Straika huyo ngongoti amewaacha mbali kina Amissi Tambwe, Donald Ngoma wa Yanga ambao msimu uliopita walitisha kwa kutupia kambani ambao mpaka sasa hawana bao hata lile la kuotea katika msimu huu wa ligi hiyo.
Mbali na nyota hao wa Yanga, Bocco pia amemzima Laudit Mavugo aliyetabiriwa mapema kusumbua nchini kutokana na rekodi yake ya mabao nchini Burundi ambapo baada ya mechi tatu za ligi hiyo ametupia mabao mawili akiwa na Simba.
Straika mwingine wa kimataifa wa Simba aliyeachwa solemba na Bocco ni Frederick Blagnon mwenye bao moja, huku mapro wengine wa wazawa waliopo klabu tofauti 16 za ligi hiyo wakiwa hawana chao mbele ya Bocco.
Bocco ambaye hana hulka ya kujisifu wala kuzungumza sana kwenye vyombo vya habari amekuwa akisema mwanzo alioanza nao ni kudra za Mungu anayemshukuru na ameapa kupambana akishirikiana na wenzake kurejesha taji la Ligi Kuu Azam.
Azam ndiyo inayoonga msimamo wa ligi kwa sasa ikilingana kila kitu na Mbeya City watakaovaana nao kesho kwenye Uwanja wa Sokoine, zote zikiwa na pointi saba na mabao matano ya kufunga na kufungwa moja, wakifuatiwa na Simba yenye pointi kama hizo na mabao matano ya kufungwa ila imefungwa mabao mawili.
 

Orodha kamili ya wafungaji ipo hivi kwa sasa;
3- John Bocco                            (Azam)
2- Rashid Mandawa        (Mtibwa Sugar)
    Rafael Daud                   (Mbeya City)
    Laudit Mavugo                      (Simba)
1- Federick Blagnon                  (Simba)
    Shiza Kichuya                       (Simba)
    Subianka Lambert                (Prisons)
    Omar Mponda                     (Ndanda)
    Shaaban Kisiga         (Ruvu Shooting)
    Hood Mayanja              (African Lyon)
    Wazir Junior                 (Toto African)
    Mudathir Yahya                      (Azam)
    Abdallah Seseme                ( Mwadui)
    Victor Hangaya                    (Prisons)
    Frank Msese              (Ruvu Shooting)
    Shomari Ally               (Mtibwa Sugar)
    Shija Mkina                         (Ndanda)
    Deus Kaseke                          (Yanga)
    Simon Msuva                         (Yanga)
    Juma Mahadhi                       (Yanga)
    Haruna Shamte              (Mbeya City)               
    Salim Mbonde             (Mtibwa Sugar)
    Bahati Ngonyani                 (Majimaji)
    Ramadhani Chombo        (Mbeya City)
    Omar Ramadhan             (Mbeya City)
    Emmanuel Kichiba                  (Mbao )
    Ally Ramadhani           (Kagera Sugar)
    Adam Kingwande              (Stand Utd)
    Ibrahim Ajib                          (Simba)
    Abdulrahman Mussa   (Ruvu Shooting)
    Kipre Balou                             (Azam)

Wanaume wa Manchester kumalizana mchana kweupe Jumamosi


Pep Guardiola
ACHANA na kelele zote ulizosikia kuelekea kwenye pambano la kukata na shoka baina ya Manchester United dhidi ya wapinzani wao Manchester City. Mwisho wa yote ni kesho Jumamosi wakati miamba hiyo itakapokwaruzana mchana kweupee.
Itakuwa vita ya makocha Jose Mourinho wa Man United dhidi ya Pep Guardiola ambao wote wametua katika timu zao hizo hivi karibuni na tayari wameshauwasha moto wa kutosha katika mechi tatu za Ligi Kuu ya England (EPL).
Macho na masikio ya wapenzi na mashabiki wa soka duniani kote mwishoni yataelekezwa kwenye mchezo huo mkali wa kumaliza ubishi kwa mahasimu hao wa jiji la Manchester.
Mchezo huo utakaokuwa ukipigwa kwenye Uwanja wa Old Trafford, nyumbani kwa Man United una ladha nyingi za kusisimua kuanzia thamani ya pambano lenyewe na hata nyota wanaotarajiwa kuonyeshana kazi majira ya saa 8:30 mchana.
Katika mchezo huo timu hizo  zitaingia uwanjani zikiwa na rekodi nzuri ya kuanza vyema msimu mpya wa ligi wakiwa wameshinda mechi zao tatu za mwanzo. Hata hivyo pamoja matokeo hayo, United wao watakwenda katika mchezo wa kesho wakiwa na rekodi nzuri zaidi dhidi ya City katika mechi 171 walizowahi kukutana huko nyuma, ambapo wameshinda 71 dhidi ya 49 za wapinzani wao. Mchezo wa mwisho United kuitambia City ulikuwa ni ule uliofanyika Machi mwaka huu katika Uwanja wa Etihad ambapo United walishinda bao 1-0. Mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa mgumu ni wa kwanza kukutana kwa mameneja wote wawili toka mwaka 2013 katika mchezo wa Super Cup ya Ulaya kati ya Chelsea na Bayern Munich ambapo Guardiola aliibuka kidedea kwa kushinda kwa matuta baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2.
Mameneja hao wana historia ndefu kwani wameshawahi kukutana mara 16 wakiwa na timu tofauti katika kipindi cha miaka saba iliyopita. Kulinganisha na historia ya timu hizo, upande huu ni tofauti kidogo kwani katika mara hizo 16 walizokutana Guardiola ndio ameibuka kidedea kwa kushinda mechi saba, wakitoa sare mechi sita huku Mourinho yeye akishinda mechi tatu pekee.
Wakati Kocha Mourinho akiwa Inter Milan walikutana na Guadiola aliyekuwa Barcelona mara nne, mbili Guardiola akishinda, sare moja huku Mourinho naye akiambulia ushindi mara moja. Wakati Mourinho akiwa Real Madrid walikutana na Guardiola aliyekuwa Barcelona tena mara 11, tano kati ya hizo Guardiola akiibuka kidedea, sare nne na Mourinho akiambulia ushindi mara mbili katika kipindi chote alichokuwa Hispania. Mara ya mwisho mameneja hao kukutana ilikuwa Agosti 30 mwaka 2013, ambapo Guardiola akiwa na Bayern Munich aliibuka kidedea kwa changamoto ya mikwaju ya penati baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Chelsea ya Mourinho.
Klabu zote zitawategemea nyota wao wanaokimbiza kwenye orodha ya ufungaji, Man United ikiwa na Zlatan Ibrahimovic wakati wenzao wakitambia Raheem Starling na Duran Nolito wenye mabao mawili kila moja, kinara, Kun Aguero hatacheza pambano hilo kwa vile kafungiwa na FA kwa utovu wa nidhamu.
Kadhalika Man City itawakosa wakali wake kadhaa kwa sabau nyingine ikiwamo kuwa majeruhi akiwamo nahodha, Vincent Kompany, Bacary Sagna, Leroy Sane, Ilkay Gundogan, huku Man United ikimkosa Henrikh Mkhitaryan  aliye majeruhi na kuna uwezekano mkubwa wa Marcus Rashford kulianza pambano hilo kama Mourinho ataamua kusikiliza maombi ya mashabiki wengi wa klabu hiyo iliyopo nafasi tatu.
Katika mechi zao za mwisho, Manchester United ilipata ushindi mwembamba ugenini dhidi ya Hull City, bao likitupiwa kambani na kinda hilo, wakati wapinzani wao walishinda nyumbani kwa mabao 3-1 dhidi ya West Ham na kukaa kileleni.


Ratiba kamili ya EPL kwa wikiendi hii ipo hivi;

Kesho Jumamosi
14:30 Man United    v Manchester City
17:00 Arsenal          v Southampton
17:00 Bournemouth v West Brom
17:00 Burnley          v Hull
17:00 Middlesbroughv Crystal Palace
17:00 Stoke City      v Tottenham
17:00 West Ham      v Watford
19:30 Liverpool        v Leicester City
 

Jumapili
18:00 Swansea        v Chelsea
 

Jumatatu Septemba 12
22:00 Sunderland    v Everton

 

Friday, August 19, 2016

Duh! Liverpool yaukacha Uwanja wao wa Anfield mwezi mzima


LIVERPOOL iliyoanza vema Ligi Kuu ya England msimu huu kwa kuikandika Arsenal kwa mabao 4-3 inatarajia kucheza mechi zake tatu zinazofuata ikiwa ugenini kitu ambacho si cha kawaida.
Sababu inayoifanya Liverpool isicheze kwenye Uwanja wao wa Anfield kwa mwezi mzima na kucheza mechi tatu mfululizo za EPL ugenini ni kwa sasa ni kutokana na ombi lao wenyewe la kutaka uwanja wao ukarabatiwe.
Mechi inayofuata kwa Liverpool ni kesho Jumamosi ikivaana na Burnley ugenini, lakini imebainika kuwa wametaka hivyo ili kupisha kukamilika kwa ujenzi wa upanuzi wa Jukwaa Kuu la Uwanja wao wa Anfield.
Jukwaa hilo limepanuliwa na kuongezwa ngazi 3 juu za kukalia mashabiki, kupanua ukumbi wa Wachezaji kuingia na kutoka uwanjani kutoka vyumba vya Kubadili Jezi, mabenchi ya wachezaji wa akiba na Jopo lao la Ufundi kutengenezwa upya. Pia sehemu maalum kwa walemavu itatengenezwa upya sambamba na kuboreshwa kwa miundo mbinu ya watazamaji.
Jukwaa Kuu la Anfield litaongeza viti 8,500 na kuufanya Uwanja huo sasa uingize jumla ya Watazamaji 54,000.
Mechi ya kwanza kabisa kwa Liverpool kukanyaga Anfield Jijini Liverpool msimu huu itakuwa Septemba 10 watakapovaana na Mabingwa Watetezi Leicester City.

Arsene Wenger awapa moyo mashabiki Arsenal

Kocha Arsene Wenger
KWISHA habari yake. Kocha Arsene Wenger anayetajwa kama mmoja ya makocha wabahili katika kununua wachezaji, amelegea baada ya kusisitiza kuwa,  yuko tayari kutumia fedha kununua nyota wapya ndani ya Arsenal kabla Dirisha la Uhamisho halijafungwa Agosti 31.
Hadi sasa, katika kipindi hiki cha Uhamisho kilichoanza rasmi Julai Mosi, Arsenal imeshagomewa na Jamie Vardy wa Mabingwa wa England Leicester City wakati Ofa yao kumnunua Straika wa Lyon Alexandre Lacazette imegomewa na Klabu hiyo ya France na pia nia yao kumchukua Sentahafu wa Valencia ya Hispania Shkodran Mustafi imegota mwamba.
Matukio hayo yamewafanya Mashabiki wa Arsenal kuamini Wenger na klabu hawana nia kutumia Fedha ikibidi.
Akihojiwa nini kinajiri kuhusu Mustafi, Wenger alijibu: “Naamini ni bora tusizungumzie kuhusu wachezaji binafsi, lakini sisi tunafanya kazi kwa bidii. Nyie mnaamini kabisa kuwa sipo tayari kutumia Fedha lakini nakuhakikishia tupo tayari kutumia Fedha!”

Mavugo kimeeleweka, kuivaa Ndanda Taifa

Mavugo
Na Tariq Badru
UHONDO unakolea. Klabu ya Simba imepata hati ya uhamisho wa kimataifa  (ITC) za mastraika wake wawili wa kigeni, Laudit Mavugo na Frederic Blagnon.
ITC hizo zimetua leo Ijumaa mchana baada ya kukamilisha uhamisho wao na sasa wanaweza kuanza majukumu yao Msimbazi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyopostiwa kwenye mitandao na Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele ni kwamba ITC  zimetua nchini leo mchana kutoka katika mashirikisho ya soka ya Burundi na Ivory Coast.
Blagnon Fredric Goue ametokea klabu ya Africa Sports ambao ni wapinzani wa jadi wa ASEC Mimosas ya nchini Ivory Coast.
Wakati Mavugo yeye anatokea klabu ya Vital'O ya Burundi na kupatikana kwa hati hizo kunamaliza utata wa uhamisho wa Mavugo ambaye kulitokea kwa maneno toka kwa uongozi wa klabu ya Vital’O kuwa bado ana mkataba wa mwaka mmoja jambo ambalo lilikanushwa na Mavugo.
Mavugo amewakuna mashabiki wa Simba baada yab kupiga mpira mwingi kwenye mechi ya Tamasha la Simba Day dhidi ya AFC Leopards ya Kenya na ile mechi ya URA.

Usain Bolt kashindikana Olimpiki, ashinda tena

https://ssl.gstatic.com/onebox/media/olympics/photos/o16/live/RIOEC8J0568SG_768x432.JPGKASHINDIKANA. Mwanariadha kutoka Jamaica, Usain Bolt, amedhihirisha kwamba yeye ni mwamba wa mbio za fupi baada ya kushinda Mita 200 katika michuano ya Olimpiki inayoelekea ukingoni mjini Rio de Jeneiro, Brazil.
Bolt ameshinda mbio hizo na kujinyakulia medali ya Dhahabu ikiwa ni mara ya pili baada ya kunyakua ya michuano ya Mita 100.
Bolt aliweza kushinda mbio hizo kwa urahisi kwa kutumika Sekunde 19.79 na kwa sasa anahitaji kushinda mbio za mita 400 za kupokezana vijiti ili kukamilisha medali ya tatu ya dhahabu kama alivyofanya katika michuano iliyopita.
Mapema wiki hii alidhihirisha kuwa ni mwamba wa mbio fupi pale aliposhinda mbio za mita 100 na kunyakuwa medali ya dhahabu.
Kwa upande wa Marekani imeweza kujinyakulia medali nyingine nne za Dhahabu ikiwemo ya mwanariadha wake Ashton Eaton.
Huku mkimbiaji kutokea nchini Kenya aliyekuwa ametangaza kustaafu, Ezekiel Kemboi, ameeleza kwamba ameahirisha kustaafu mara baada ya kunyang`anyway medali aliyokuwa ameshinda katika mbio za kuruka viunzi na maji.
Medali hiyo iliyochukuliwa na Mfaransa mara baada ya kukata Rufaa kwenye Mita 3000 imemfanya Kemboi kusema kuwa watakutana tena London 2017 kwenye michezo ya Olimpiki ili kuweza kudhihirisha kwamba alikuwa akistahili medali hiyo.

Pogba kuanza mambo yake Man United

KAZI imeanza. Kiungo mpya wa klabu ya Manchester United, Paul Pogba leo Ijumaa anatarajiwa kuanza kuitumikia timu yake hiyo kwa mara ya kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Southampton.
Pogba aliyeondoka klabuni hapo kwa mlango wa nyuma mwaka 2012 kwenda Juventus amerejea tena Man United kwa ada ya Pauni Milioni 89 iliyovunja rekodi ya dunia, alishindwa kuanza katika mchezo uliopita dhidi ya Bournemouth.
Kilichomkwamisha nyota huyo wa Ufaransa kukipiga kwenye mchezo huo ambao Man Un ited ilishinda mabao 3-1 ni kwa sababu ya kutumikia adhabu ya mechi moja aliyotoka nayo Italia katika Ligi ya Serie A.
Akihojiwa kuhusu mchezo wa leo usiku, Pogba alisema anajisikia yuko fiti na amekuwa akifanya mazoezi kwa siku 10, lakini hata hivyo itategemea meneja wake Jose Mourinho atakavyoona inafaa.
Pogba aliendelea kudai kuwa ameshazoea hali hiyo kwani amekuwa akifanya mazoezi hata wakati alipokuwa likizo hivyo anajiona yuko sawa.
Man United itaivaa Saints ikitegemea safu yake kuongozwa na nyota wao mpya, Zlatan Ibrahimovic aliyeanza kwa makeke ndani ya klabu hiyo inayoongoza msimamo kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Hata hivyo mapema leo mchana Kocha Mourinho aliwahakikishia mashabiki wa Man United kuwa kiungo Paul Pogba atawavaa Southampton.
Kocha Mourinho alisema Pogba amefanya mazoezi kwa siku 11 na imekuwa rahisi kumbadili Pogba kwa vile ni kijana aliyekulia OT na anamjua kila mtu.
Alipoulizwa kama yeye anaweza kusaidia kurejesha ile hali ya timu kuiogoga Man United iliyokuwepo enzi za Sir Alex Ferguson, Mourinho alijibu: “Sio mimi. Ni timu, ndio. Na mashabiki pia. Nadhani kila kitu kinaanza hapo, uhusiano kati ya timu na mashabiki.”
Aliongeza: “Ikiwa humo Old Trafford, mashabiki wa upinzani, maelfu kadhaa wanakuwa na kelele kubwa kupita Mashabiki zaidi ya 70,000, basi sisi tupo mashakani. Inamaanisha uhusiano kati ya timu na mashabiki wake. Kukiwepo uhusiano, basi ule ukweli wa kutisha tukiwa nyumbani utarudi. Kila kitu kinaanza na uhusiano huo wa timu na mashabiki wake. Ikiwa mashabiki watahusiana na timu, wanataka nao kucheza na wakicheza, wapinzani hawana nafasi!”
Kwa taarifa yako tu ni kwamba Southampton imekuwa ikizoa pointi tatu kwenye Uwanja wa Old Trafford kwa misimu miwili sasa wakifungamana na Norwich City, Swansea City na West Bromwich Albion.


Mtamkoma! Kessy ruksa kukipiga Jangwani msimu huu

Kessy akiwajibika kwenye mechi ya Ngao ya jamii dhidi ya Azam
Na Rahma Kimwaga
YANGA inayojiandaa kupaa kwenda zao DR Congo huenda ikawa inatabasamu kwa furaha baada ya beki waliyekuwa wakimpigania kutoka Simba, Hassan Kessy kupewa uhalali wa kuanza kuitumikia timu hiyo katika Ligi Kuu Bara msimu huu.
Kessy aliyekuwa akiwekewa zengwe na Simba, licha ya ukweli ilishamaliza naye mkataba na ilionyesha wazi kutomhitaji baada ya kumfungia mechi tano za mwishoni mwa msimu uliopita kwa kitendo cha kunmchezea rafu Edward 'Rddo' Christopher aliyekuwa akiichezea Toto Africans aliyesajiliwa Kagera Sugar kwa sasa.
Kamati ya Sheria na Haki za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)  lilipitisha jina la Kessy kuichezea Yanga sambamba na usajili wa klabu nyingine kwa msimu wa 2016-2017.
Kamati hiyo imepitisha jina la Hassan Ramadhani ‘Kesi’ kuitumikia Yanga kuanzia msimu huu 2016/17 baada ya kuona kuwa hana tatizo katika usajili badala yake madai ambayo pande husika zinaweza kudaiana wakati mchezaji anaendeleza kipaji chake.
Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Richard Sinamtwa imepitia usajili wa timu zote na kujiridhisha kwamba suala la mchezaji Hassan Kessy limeegemea kwenye madai na si usajili ambako Simba ndiye mdai kwa kumtuhumu mchezaji huyo kuwa alianza kuitumikia Young Africans kabla ya kumaliza mkataba wake Simba SC. Mkataba wake ulifika mwisho, Juni 15, 2016.
Kama ni madai Simba inaweza kuendelea kumdai Kessy au Young Africans wakati mchezaji huyo anatumika uwanjani kwa mwajiri mpya. TFF inafuatilia na kuangalia haki ya Simba namna ya kupata haki yake baada ya kuwasilisha madai kuhusu kuvunja mkataba na mwajiri wake wa zamani.
Kanuni hazimzuii mchezaji kuendelea kucheza kwa hoja ya madai badala yake suala hilo linaweza kumalizwa wakati mashindano yanaendelea. Kamati inaendelea kupitia malalamiko na pingamizi za wachezaji wengine na inatarajiwa kutoa taarifa rasmi kuhusu wachezaji wote wakati wowote kuanzia sasa.
Katika hatua nyingine Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limezionya timu shiriki za ligi hiyo kutochezesha wachezaji wa kigeni kama hawana vibali vya kuishi, kufanya kazi na leseni inayomruhusu kucheza ligi husika kwa mujibu wa sheria za nchi na kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Vibali vya kuishi na kufanya kazi vinatolewa na Idara ya Uhamiaji Tanzania (Uhamiaji) wakati leseni ya kucheza inatolewa na TFF.
Vilevile TFF imeziagiza klabu kulipia ada za ushiriki kwa kila timu; leseni za wachezaji, ada za wachezaji na ada za mikataba.
Mchezaji hatapewa leseni ya kucheza kama uongozi wa timu hautakamilisha taratibu za malipo.
TFF pia imezikumbusha timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwamba hazitapewa leseni ya mchezaji yeyote ambaye timu haikuleta mkataba wakati wa maombi ya usajili, hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 68 vipengele vya 1, 2, 3 na 8 ya Ligi Kuu ya Tanzania toleo la 2016/2017.
Kila timu inatakiwa kuleta nakala tatu za mkataba wa mchezaji, ili kamati ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji iweze kupitia na TFF iweze kuidhinisha mikataba hiyo. Baada ya hapo timu na mchezaji, watakuja kuchukulia mikataba hiyo hapa TFF. Ni matarajio yetu kuwa kila klabu itatimiza wajibu wake ili kuondoa migogoro kati ya timu na mchezaji na mchezaji na timu. Tunategemea kupata ushirikiano.