STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, July 6, 2013

TFF yataja wakaoshiriki kozi ya ukocha ya FIFA

MAKOCHA wa mpira wa miguu na walimu 28 kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) na shule za msingi na sekondari, wameteuliwa kuhudhuria kozi ya FIFA inayoanza kesho Hombolo mkoani Dodoma.
Taarifa ya TFF iliyotolewa jana ilisema kozi hiyo itakayomalizika Julai 20 itakuwa chini ya ukufunzi wa Rogasian Kaijage ambaye pia ni kocha wa timu ya taifa ya wanawake (Twiga Stars).
Kozi hiyo itatoa nafasi kwa walimu hao kuongeza ujuzi kwenye soka, taarifa ilisena na kuwataja washiriki wa kozi hiyo kuwa ni:
Abdul Mikoroti (Shule ya Msingi Nzasa), Baltazar Kagimbo (Shule ya Msingi Tabata Jica), Baraka Baltazar (Shule ya Msingi Muhimbili), David Kivinge (Shule ya Msingi Temeke) na Dismas Haonga (Tambaza Sekondari).
Wengine ni Exuperus Kisaka (Shule ya Msingi Mavurunza) na Hadija Kambi (Shule ya Msingi Karume).
Wengine ni pamoja na Hamis Chimgege (Shule ya Msingi Tusiime) na Hobokela Kajigili (Shule ya Msingi Buguruni).
Wengine zaidi ni Issack Mhanza (Shule ya Msingi Airwing), Job Ndugusa (Shule ya Msingi Upanga), John Sebabili (TFF), Lutta Rucharaba (Shule ya Msingi Montfort) na Maua Rahidi (Shule ya Msingi Uhuru Wasichana).
Taarifa ya TFF iliwataja washiriki zaidi wa kozi hiyo kuwa ni Michael Bundala (TFF), Mussa Kapama (Shule ya Msingi Bunju ‘A’), Priscus Silayo (Shule ya Msingi J.K. Nyerere), Peter Manyika (TFF) na Rajabu Asserd (Shule ya Msingi Mtoni Kijichi).
Wengine ni Raphael Matola (TFF), Raymond Rupia (St. Anne Maria Academy), Renatus Magolanga (Ulongoni Sekondari), Ruth Mahenge (Shule ya Msingi Chang’ombe), Said Pambaleo (TFF), Sebastian Nkoma (TFF), Titus Michael (TFF) na Wane Mkisi (Jangwani Sekondari).

Fainali za Airtel Rising Stars kurushwa live Supersport

Baadhi ya timu shiriki za michuano hiyo zikichuana uwanjani
FAINALI za michuano ya Airtel Rising Stars kwa wavulana na wasichana zinazofanyika leo kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam, zitaonyeshwa na kituo cha televisheni cha Supersport kuanzia saa 7:30 mchana.
Akizungumza jijini jana, Afisa Habari wa Shirikisho la soka (TFF), Boniface Wambura, alisema nusu fainali za mashindano hayo zilizofanyika jana zilihusisha timu za wasichana za Kinondoni iliyocheza na Kigoma wakati Temeke ilicheza na Ilala wakati kwa upande wa wavulana Mwanza ilicheza na Ilala huku Kinondoni ikiumana na Morogoro.
"Fainali kwa upande wa wasichana itaanza saa saba mchana na fainali ya wavulana yenyewe itaanza saa tisa na nusu alasiri hivyo wadau wa soka na mashabiki wajitokeze kwa wingi kuangalia fainali hizi," alisema Wambura.
Alisema kuwa maandalizi kwa ajili ya fainali hizo za leo yamekamilika ambapo wanategemea kuona vipaji vipya vya vijana.
Mashindano hayo ya soka ya vijana yanayofanyika kila mwaka yamedhaminiwa na kampuni ya huduma za simu ya Airtel.

RAIS KIKWETE KUCHEZESHA MECHI YA WABUNGE‏ SIMBA, YANGA

Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, amekubali kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Usiku wa Matumaini litakalofanyika kesho Jumapili katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam. Aidha, Rais atahutubia katika tamasha na pia atakuwa refa wa mechi za wabunge wa Yanga na Simba.
Mbali na pambano hilo tamasha hilo lenye lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa kike wa Sekondari, kutakuwa pia na mipambano ya ngumi baina ya Wabunge na wasanii wa Bongo Movie.
Pia litakuwepo pambano la soka baina ya timu ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya 'Bongofleva' na Bongo Movie sambamba na burudani nyingine ya muziki toka kwa wasanii mbalimbali wakiwemo wa muziki wa Injili na dansi. 

AIRTEL YATOSHA KUWAPA NYUMBA WATEJA WA AIRTEL

 Meneja Uhusiano wa Airtel Jackson Mmbando akiongea na waandishi wahabari (hawapo picha a Nyumba 3,  iliyofanyika  katika ofisi za Airtel jijini Dar Es Salam ,akifuatiwa na meneja masoko wa Airtel bi Anethy Muga.
Meneja Uhusiano wa Airtel Jackson Mmbando akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani)  nyumba watakayojishindia washindi wa Airtel Yatosha Shinda Nyumba 3 iliyozinduliwa leo  katika ofisi za Airtel Morrocco jijini Dar Es Salam ,akifuatiwa na meneja masoko wa Airtel bi Anethy Muga.

Warundi kuichezesha Stars na Waganda Jumamosi ijayo


Kikosi cha Stars
SHIRIKISHO la soka barani Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Burundi kuchezesha mchezo wa kwanza wa mchujo kwa ajili ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani (CHAN) kati ya Taifa Stars na Uganda.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, Afisa Habari wa Shirikisho la soka (TFF), Boniface Wambura, aliwataja waamuzi hao kuwa ni mwamuzi wa kati Thierry Nkurunziza na wasaidizi wake Jean Claude Birumushahu na Pascal Ndimunzigo.
Wambura alisema mwamuzi wa akiba ni Pacifique Ndabihawenimana wakati kamishna ameteuliwa kuwa Gebreyesus Tesfaye kutoka Eritrea.
Tesfaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Eritrea na mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya CHAN.
Kikosi cha Taifa Stars ambacho kipo kambini kwa sasa kitaumana na Uganda Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kabla ya kurudiana ugenini wiki mbili baadae.
Endapo Stars itafanikiwa kupata matokeo mazuri kwenye michezo hiyo miwili dhidi ya Uganda itakuwa imefuzu kushiriki kwa mara ya pili kwenye mashindano hayo.
Wakati huo huo, CAF pia imemteua Mtanzania Leslie Liunda kuwa Kamishna wa mechi kati ya Burundi na Sudan itakayochezwa jijini Bujumbura, Afisa Habari wa Shirikisho la soka (TFF), Boniface Wambura alisema.
Mechi hiyo ya kwanza ya mchujo ya CHAN itafanyika kesho Julai 7.

Miyeyusho azidi kujifua ili amtwange Mkenya Tamasha la Matumaini


 Bondia Francis Miyeyusho (kushoto) akiwa katika mazoezi kwenye Gym ya Lazima Ukae, iliyopo Mwananyamala jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wake wa kirafiki na Bondia Shadrack  Muchanje kutoka nchini Kenya. Mabondia hao watapanda ulingoni kuonyeshana umwamba siku ya Tamasha la Matumaini litakalofanyika kesho Jumapili  kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambalo litakuwa ni la raundi sita. Miyeyusho yeye amecheza mapambano 38 huku mpinzani wake, akiwa amecheza mapambano 14 hadi sasa.
 Panchi zikiendelea.....
 Miyeyusho akipozi......
Panchi zikiendela...Lazima akae siku hiyo.....

Friday, July 5, 2013

Zahoro Pazi aahidi Simba, akiri utoto ulimfanya aikache

http://www.ippmedia.com/media/picture/large/Zahoro.jpg
Zahoro Pazi katika uzi wa JKT Ruvu
MSHAMBULIAJI mpya wa Simba, Zahoro Pazi ameahidi kuifanyia makubwa klabu hiyo iliyoingia naye mkataba wa miaka mitatu, huku akisema utoto aliokuwa nayo uliomfanya asijiunge na timu hiyo miaka mitatu iliyopita umeisha.
Pazi aliyesajiliwa na Simba akitokea JKT Ruvu aliyokuwa akiichezea kwa mkopo kutoka Azam, aliwahi kusainishwa mkataba wa miaka minne msimu wa mwaka 2010 ili kujiunga na timu hiyo, lakini akakataa kujiunga nayo baada ya kutishwa na familia.
Anasema watu wa familia yake walimtishia kwamba angejiunga na Simba angeenda kuua kipaji chake kwani 'angepigwa misumari' na hivyo kuamua kubaki Mtibwa Sugar, jambo alililodai lilitokana na akili za kitoto na kutegemea ushauri wa watu wengine.
Pazi, mtoto wa kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyetamba na timu mbalimbali ndani na nje ya nchi, Idd Pazi 'Father' alisema kwa sasa amekuwa na maamuzi binafsi ndiyo maana amesaini kuichezea Simba kwa miaka mitatu.
Alisema kutua kwake Simba kuna changamoto kubwa zinazomfanya apigane ili apate namba na pia kuifanyia makubwa kama alivyofanya baba yake wakati akiidakia timu hiyo.
"Sina miujiza kwa kutua kwangu Simba, lakini naahidi nitajituma na kucheza kwa moyo wangu wote ili kuipa mafanikio timu hiyo na kutouangusha uongozi na benchi zima la timu hiyo walioniamini na kunisajili," alisema Pazi.
Mshambuliaji huyo anayecheza pia kama winga, alisema anaamini Simba ya msimu ujao itakuwa moto wa kuotea mbali chini ya King Abdallah Kibadeni mmoja wa makocha waliochangia kukuza na kuendelea kipaji chake alipokuwa Mtibwa Sugar.
"Chini ya Kibadeni, Simba itarajie makubwa ni bonge la kocha na mtu ambaye siwezi kumsahau kwa jinsi alivyosaidia kukiendeleza kipaji changu nilipotua timu ya vijana Mtibwa," alisema.
Pazi aliyewafanyiwa majaribio ya kucheza soka la kulipwa na klabu ya Bloemfontein Celtic mapema mwaka huu na kufaulu japo alichwa baada ya Mzimbabwe Roderick Mutuma kupewa nafasi yake kwa vile nafasi iliyokuwa ikiwania ni moja, alisema anajisikia fahari kucheza timu aliyoichezea baba yake.

Yanga kwenda Kanda ya Ziwa bila nyota wake saba

Wachezaji wa Yanga inayoondoka jijini Dar kwenda Kanda ya Ziwa
MABINGWA wa Soka wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga leo wanatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam na kuelekea Mwanza kwa ajili ya kucheza mechi ya kirafiki wa kimataifa dhidi ya timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Uganda, KCC mchezo utakaofanyika kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba jijini humo.
Hata hivyo Yanga itaondoka bila ya nyota wake saba walioko katika kikosi cha timu ya Taifa (Taifa Stars) ambacho kimeshaingia kambini  kwa ajili ya kujiandaa kuikabili timu ya taifa ya Uganda (Cranes) katika mchezo wa kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).
Wachezaji wa Yanga walioko kwenye kikosi cha Taifa Stars ni pamoja na Athumani Iddi (Chuji), Ally Mustapha 'Barthez', Frank Domayo, Simon Msuva, David Luhende, Kelvin Yondani na Nadir Haroub 'Cannavaro'.
Afisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema kuwa kikosi hicho kitaondoka kwa ndege leo mchana.
Kizuguto alisema kuwa wakiwa huko watacheza mechi mbili, ya pili ikichzwa Jumapili kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga dhidi ya Waganda hao.
Kizuguto alimtaja kiungo wa kimataifa wa timu hiyo, Haruna Niyonzima kuwa vilevile hatakuwapo kwenye ziara hiyo kutokana na kukabiliwa na matatizo ya kifamilia nchini kwao  Rwanda.

Tamasha la Matumaini kurindima Jumapili

 http://api.ning.com/files/X378Xfy1meuzEX8xHlBh-qQB8hV-1a9IRTU-sWUlJ2vVfLOTpjokDf51r7zq*IPOR8Llw33BkDDIl5dVaYmxQm*gckOwOa6v/ngumi.jpg
WANAMICHEZO, wanamuziki, wasanii wa filamu na wabunge wamezidi kutambiana kuelekea Tamasha la Usiku wa Matumaini litakalofanyika keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuchangia mfuko wa elimu nchini.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, baadhi ya washiriki wa tamasha hilo walisema wamejiandaa vyema huku kila upande ukitamba kufanya vizuri.
Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan, ambaye pia ni kipa wa timu ya wabunge alisema kikosi chao kinachoendelea na mazoezi jijini Dar es Salaam kiko vizuri na wana ukakika wa kuendelea kuifunga Yanga kama walivyoifunga mwaka jana.
Mratibu wa tamasha hilo, Abdallah Mrisho alisema kutakuwa pia na burudani kutoka kwa bendi za DDC Mlimani Park na Msondo, taarab ya Mzee Yusuf na muziki wa kizazi kipya kutoka kwa Diamond Platinumz, Chege, H.Baba na Mkenya Prezzo.
"Pia kutakuwa na muziki wa injili kutoka kwa wasanii Upendo Nkone, Solomon Mukubwa, Anastazia Mukabwa, Flora Mbasha na Asha Mwaipaja wa Mbeya," alisema Mrisho.
Mbali na wabunge wa Simba na Yanga kuvaana katika soka, pia kutakuwa na mechi nyingine kati ya wasanii wa Bongo Movie dhidi ya Bongo Fleva na mapambano ya ngumi kati ya mbunge Zitto Kabwe na Vicent Kigosi (Ray), Jacqueline Wolper dhidi ya mbunge Halima Mdee na Aunt Ezekiel dhidi ya mbunge Ester Bulaya.

Christian Bella jukwaani tena na Diamond Musica

Christian Bella
BAADA ya kufanya onyesho lao kwa kishindo, mwimbaji Christian Bella atashiriki tena onyesho la pili leo na bendi ya Diamond Musica Original ikiwa ni mwendelezo wa mikakati ya kujiandaa kumchukua ili ajiunge na bendi hiyo inayokuja kwa kasi.
Onyesho la kwanza kati na mwimbaji huyo na bendi ya Diamond Musica Original lilifanyika Ijumaa iliyopita na kupata mashabiki wengi waliojitokeza kulishuhudia na sasa limeandaliwa jingine litakalofanyika leo na huenda likamshirikisha pia Ndanda Kosovo.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa bendi hiyo, Ally Ocs, maonyesho hayo yanalenga kumkaribisha Bella na kisha uongozi wa bendi utafanya naye mazungumzo ili kuona uwezekano wa kumchukua jumla mwimbaji huyo.
"Kama nilivyowahi kusema siku za nyuma Ndanda Kosovo tulishamchukua na huenda akawapo kwenye onyesho letu kwani wakati wowote anatarajia kurejea kutoka kwao Kongo alikokwenda kusalimia kabla ya kuanza kazi rasmi katika bendi yetu," alisema Ocs.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa katika onyesho atatambulishwa pia mnenguaji Mariam Bessie aliyechukuliwa kutoka bendi ya Mapacha Watatu inayoongzwa na Khalid Chokoraa na Jose Mara.
"Tumedhamiria kuingia kwenye muziki wa ushindani, hivyo hatuna budi kujipanga kisawasawa na hilo litawezekana kwani hadi sasa mambo yetu yanakwenda vizuri ikiwa ni pamoja na kuwachukua wanamuziki wenye majina makubwa," alisema.
Diamond Musica Original iko kwenye maandalizi ya albamu ya kwanza ikiwa imekamilisha baadhi ya nyimbo kama: 'Hatua',  'Shilingi', 'Upole wa Mapenzi', 'Fimbo la Mwaka', 'Kibali cha Mapenzi' na 'Deceiption'.

Kichanga chashangaza madaktari China kwa kubeba mimba

Madaktari wa nchini China walishangazwa kuona mtoto wa mwaka mmoja ana ujauzito.
Mtoto Kang Mengru wa nchini China alipelekwa hospitali baada ya wazazi wake kushtushwa na hali ya tumbo lake kuzidi kuwa kubwa siku hadi siku.
Baada ya mtoto huyo kufanyiwa kipimo cha ultrasound, madaktari waligundua kuwa mtoto huyo wa kike alikuwa amebeba kitoto kichanga kwenye tumbo lake ambacho kilikuwa kikiendelea kukua.
Madaktari wanaamini kuwa mama wa mtoto huyo alikuwa na mimba ya watoto wawili mapacha na pacha mmoja alijitokeza ndani ya tumbo la pacha mwenzake.
Hali kama hiyo ya kichanga kuzaliwa ndani ya kichanga kingine ni nadra sana kutokea na humtokea mwanamke mmoja katika wanawake 500,000.
Mtoto Kang atafanyiwa upasuaji kukiondoa kichanga hicho tumboni

Saida Karoli kutambulisha mpya Igunga, Nzega

Saida Karoli
MSANII nyota wa muziki wa asili, Saida Karoli ambaye alivumishiwa kifo hivi karibuni anatarajiwa kujitokeza hadharani kwa mara ya kwanza kufanya maonyesho maalum ya kudumisha amani yatakayofanyika mkoani Tabora.
Karoli aliyewahi kutamba na nyimbo mbalimbali kama 'Chambua kama Karanga' na nyingine atafanya onyesho la kwanza siku ya Jumapili katika shamrashamra za kusherehekea sikukuu ya Sabasaba mjini Igunga na kutambulisha nyimbo zake mpya kwa mashabiki wa mji huo.
Kwa mujibu wa mratibu wa maonyesho hayo, Livenus Madaraka, onyesho la pili la mwanadada huyo litafanyika Julai 9 katika mji wa Nzega, akiwadhihirishia mashabiki wake kwamba yu hai na anaendeleza 'makamuzi' kama kawaida.
Mratibu huyo alisema amewataka wale ambao bado hawajaamini kama Saida Karoli anadunda wajitokeze katika maonyesho hayo ambapo msanii huyo ameahidi kufanya makubwa katika kuwapa burudani mwanzo mwisho.
"Mwenyewe ameahidi kukata kiu ya mashabiki wake kwa kuwapa burudani kabambe na kuzitambulisha nyimbo zake mpya na zile za zamani zilizompatia umaarufu mkubwa ndani na nje ya Tanzania," alisema Madaraka.

Thursday, July 4, 2013

FIFA yaifungia Cameroon kujihusisha na soka


SHIRIKISHO la Kandanda Duniani, FIFA limeifungia nchi ya Cameroon kwa muda usiojulikana nchi ya kufuatia serikali ya nchi hiyo kujiingiza katika maswala ya chama cha soka nchini humo.
Kwa mujibu wa tangazo la FIFA, hatua ya kufungiwa kwa nchi hiyo imetokana na maamuzi ya kamati ya dharura ya shirikisho hilo iliyokutana na kuamua kusimamisha kwa muda chama cha soka cha Cameroon FECAFOOT na uamuzi huo umeanza kutekelezwa mara moja kwa sababu serikali inaingilia maswala ya chama cha soka.

Tumuombeeni Mzee Mandela

Mzee Mandela akiwa hospitalini
TAARIFA zilizotangazwa na kituo cha runinga cha Al Jazeera zinasema kuwa hali ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela imezidi kuwa tete ikidaiwa anapumua kwa kutumia mashine maalum.
Inaelezwa Mzee Mandela ameshindwa kupumua yeye mwenyewe na hivyo kulazimisha madaktari kumvika mashine hiyo ili kumsaidia kupigania uhai wake na kusababisha simanzi kubwa kwa ndugu, familia na wananchi wa taifa hilo tajiri Afrika na duniani kwa ujumla.
Mzee Mandela aliyekimbizwa hospitali zaidi ya siku 25, ambako wakati hali yake ikiwa hivyo familia yake imekuwa katika mzozo wa kugombea mahali pa kumzikia.

Jumuika na Mapacha Watatu kuianza wikiendi yako

Brazili yarejea 10 Bora ya FIFA, Tanzania yaporomoka

Brazil waliorejea 10 Bora ya orodha ya viwango vya soka ya FIFA
Stars iliyoporoka toka nafasi ya 109 hadi 121

MABINGWA wa Fainali za Kombe la Mabara, Brazil imechupa hadi nafasi ya 9 katika orodha mpya ya viwango vya soka Duniani vilivyotolewa na Shirikisho la Kandanda Duniani, FIFA.
Brazil imechupa katika nafasi hiyo ikiwa imerejea kwenye 10 Bora baada ya awali kuporomoka kiwango siku chache baada ya kunyakua taji hilo kwa kuizodoa Hispania kwa mabao 3-0 katika fainali iliyochezwa kwenye ardhi yake ya nyumbani.
Hata hivyo orodha hiyo mpya ya viwango imeiacha kileleni Hispania, ikifuatiwa na timu za Ujerumani, Colombia,Argentina na Uholanzi zikikamilisha orodha ya timu tano bora za dunia.
Italia ambao walifika hatua ya nusu fainali kwenye kombe la Mabara wanashika nafasi ya sita mbele ya Ureno walio kwenye nafasi ya saba huku Croatia, Brazil na Ubelgiji  zikihitimisha 10 Bora
Vinara wa soka Afrika, Ivory Coast wameendelea kuwa kileleni mwa msimamo wa orodha ya nchi za Afrika ikishika nafasi ya 13 duniani ikifuatiwa na wapinzani wa karibu Ghana waliopo nafasi ya 24 ulimwenguni na ya pili Afrika.
Taifa la Mali lenyewe lipo nafasi ya tatu ikikamata namba 28 duniani, kisha Algeria na Nigeria zilizohitimisha 5 Bora ya Afrika.
Kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Uganda kama kawa wameendelea kukomaa kileleni huku kwa Afrika ikiwa nafasi ya
19 na dunia ya 80 ikiwa imepanda kwa nafasi 13 toka orodha iliyopita waliokuwa nafasi ya 93 duniani na Afrika ya 24. 
Ethiopia bado wamesalia nafasi ya pili kwa ukanda wa CECAFA ikishika nafasi ya  25 Afrika na 90 kwa dunia ilihali Tanzania ipo nafasi ya 35 Afrika ikipanda nafasi mbili toka 32 ya awali na duniani wapo nafasi ya 121 wakiporomoka toka 106 mwezi uliopita.

Temeke kupata kipusa wake kesho katika Redd's Miss Temeke 2013


 Mratibu wa shindano la Redd’s Miss Temeke Benny Kisaka akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu shindano la Redd’s Kanda ya Temeke linalotarajiwa kufanyika katika ukumbi wa TCC Club Chang'ombe Julai 5. Kulia ni Mkuu wa Itifaki wa Kamati ya Miss Tz, Albert Makoye.Mkuu wa Itifaki wa Kamati ya Miss Tanzania, Albert Makoye akizungumza kuhusu fainali ya Redd's Miss Temeke. 
Na Mwandishi Wetu
MREMBO atakayetwaa taji la Redds Miss Temeke 2013, linalofanyika Ijumaa Julai 5, mwaka huu ataondoka na zawadi za jumla ya Sh. Milioni 3,250,000 ikiwa ni zawadi kubwa zaidi kutolewa katika mashindano yote ya urembo, yaliyofanyika mwaka huu.
Mshindi huyo, atapata ofa ya mwaka mzima kutoka RIO gym & Spa, iliyopo Quality Center, kutumia vifaa vyote ndani ya gym hiyo ambayo gharama yake ni Milioni 1,400,000, pia atajinyakulia simu ya kiganjani yenye thamani ya Sh 700,000 , dinner set kutoka AKO Catering yenye thamani ya Sh,150,000 sanjari na pesa taslim Sh. Milioni 1, hiyo jumla yake ni Milioni 3,250,000.
Mshindi wa pili katika mashindano hayo ambayo mgeni rasmi atakuwa Mbunge wa Jimbo la Temeke, Abas Mtemvu atajinyakulia kitita cha Sh.800,000 pesa taslim na dinner set ambayo thamani yake ilikuwa bado haijathibitishwa na mdhamni wa zawadi hiyo wakati mshindi wa tatu ambao wote kwa pamoja ni wawakilishi wa Miss Temeke, yeye atajipatia fedha taslimu Sh 700,000.
Sh , 400,000 zitakwenda kwa mshindi wa nne na atakayeshika nafasi ya tano yeye ataibuka na Sh 300,000. 

Washiriki wengine ambao hawatabahatika kuingia katika nafasi ya tano bora, wote watapewa Sh,200,000 kwa maana ya kifuta jasho. Tumelenga zawadi za fedha zaidi, hii ni kutokana na ugumu wa maandalizi kwa warembo ambao hugharamika zaidi, kiasi nasi kuona kuna kila namna ya kuwapunguzia maamivu hayo.
Shindano hilo, linatarajiwa kuwa na burudani ya kipekee kutoka kwa mshindi wa tungo bora ya Bongo Fleva ya Kili Music mwaka huu, Ben Paul sanjari na Twanga Pepeta ambayo mwishoni mwa wiki, ilizindua albamu yake ya 13 kwa mafanikio makubwa.

 Warembo watakaopanda jukwaani Julai 5 ni kutoka Kigamboni, Kurasini na Chang'ombe ambao wanawania taji linaloshikiliwa na Miss Tanzania namba tatu, Edda Sylvester walikuwa chini ya wakufunzi Suzy Mwenda na Shadya Mohamed wakati kwenye kucheza nako walikuwa na walimu wawili Super Bokilo na Charles.
Warembo hao ni pamoja na Axsaritha Vedastus, Darling Mmary, Esther Muswa,  Hyness Oscar, Irene Rajab, Jamila Thomas, Latifa Mohamed, Margreth Gerald, Margreth Olotu, Mey Karume, Mutesi George, Naima Ramadhan, Narietha Boniface , Stella Mngazija na Svtlona Nyameyo .       
Shindano hilo limedhaminiwa na kinywaji cha Redd's, Dodoma Wine, Gazeti la Jambo Leo, Cloud’s Media, Blogu ya Wananchi (Le Mutuz), Fredito Entertainment, CXC Africa tours & Safaris, RIO Gym & Spa, 100.5 Times FM na Kitwe General Traders. 

Mbali ya wadhamini hao pia Redds Miss Temeke imechangiwa katika ufanikishaji na Mbunge wa Jimbo hilo, Abbas Mtemvu na mwanamichezo maarufu nchini Geofrey Nyange Kaburu hasa kwa upande wa zawadi.
Temeke, imewahi kutoa warembo kadhaa miaka ya nyuma waliopata mafanikio katika mashindano hayo, mitindo na kazi nyingine hasa kupata uzoefu wa kujiamini katika njanja mbalimbali. Miongoni mwao ni Miriam Odemba(1997) aliyepata kuiwakilisha Tanzani katika fainali za mitindo zilizofanyika Nice Ufaransa na kupata mkataba wa Elite Model Look, baadaye kufakinikiwa kutwaa nafasi ya pili ya Miss Earth World, zilizofanyika China. 

Pia, Temeke ilimtoa Happines Millen Magesse(2001), na kutwaa taji la Miss Tanzania na kwa sasa anang'ara sana katika tasnia ya mitindo katika nchi za Marekani, Afrika Kusini na barani Afrika kwa ujumla. 
2003 Temeke ilimtoa Miss Tanzania, Sylvia Bahame na 2006 kuwatoa Jokate Mwegelo na Irene Uwoya. Jokate alitwaa taji la Miss Temeke mwaka huu na pia kushika nafasi ya pili Miss Tanzania na pia kushinda taji la ubalozi wa Redd's na gazeti la Citizen. 
Irene Uwoya ambaye alikuwa mshindi wa pili Temeke alishika nafasi ya nne kwenye Miss Tanzania mwaka huo. Genevieve Mpangala mwaka 2010 alitwaa taji la Miss Temeke baadaye kushinda taji la Miss Tanzania. 
Nafasi nyingine za juu zilizowahi kutwaliwa na warembo kutoka Temeke ni pamoja na Irene Kiwia, mshindi wa nne Miss Tanzania mwaka 2000, Regina Mosha mshindi wa nne Miss Tanzania mwaka 2002, Cecylia Assey mshindi wa pili Miss Tanzania 2004, Queen David mshindi wa tatu mwaka 2007 na Edda Sylvester mshindi wa tatu Miss Tanzania akiwa anashikilia taji la Redds Miss Temeke. 
BMP Promotions inayoandaa mashindano haya kwa mwaka wa 18 sasa, inatanguliza shukrani zake wadhamini wetu kwa miaka hiyo, sanjari na vyombo vyote vya habari kwa ujumla wake, kwani ndio waliofanikisha kuandaa Miss Temeke kwa ufanisi katika muda wote huo, shukrani sana.

Adhana kurushwa ktk runinga kwa mara ya kwanza UK


Waumini wa Kiislam wakiwa kwenye ibada ya swala

WAKATI mwezi mtukufu wa Ramadhani ukikaribia kuanza, nchini Uingereza kituo kimoja cha runinga kimetangaza kuanza kurushwa hewani moja kwa moja adhana ya swala ya asubuhi.
Chaneli ya 4 ya televisheni nchini humo, imesema itaanza kurushwa hewani adhana hiyo ya asubuhi 'live' kuwaamsha waumini wa kiislam ili kuwahi swala.
Justine Bower mkurugenzi wa masuala ya umma wa chaneli ya 4 ya televisheni ya nchi hiyo amesema kuwa, kanali hiyo itakuwa ikirusha moja kwa moja adhana ya asubuhi kwa ajili ya wananchi wa Uingereza.  Ameongeza kuwa, waumini wa dini ya Kiislamu wapatao milioni mbili na laki nane nchini humo wataanza mfunguo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani siku chache zijazo. 
Bower amesema kuwa kanali hiyo pia itakuwa ikirusha hewani adhana kupitia mtandao wa kanali hiyo.
Alipoulizwa wamejiandaa vipi kukabiliana na ukosoaji kwa hatua hiyo, Justine Bower amesema kuwa, karibu asilimia 5 ya wananchi wa nchi hiyo wako katika pilika pilika za kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani. 
Amesema kuwa, mwezi wa Ramadhani hufungwa na waumini wa dini ya Kiislamu kila mwaka, na nitawashangaa watu watakaostaajabishwa na uwepo wa utambulisho huo wa kidini.
Mfungo huo ambao unatarajiwa kuanza kati ya Julai 8 na 9 ni kati ya nguzo tano za dini ya kiislam ambapo waumini hujizuia kula na kunywa mchana pamoja na kujikithirisha kufanya mambo mema kwa nia ya kutaka radhi za Allah Subhana Wataala.
 
(Radio Tehran  via  Wavuti)

Kaimu Rais mpya Misri aapishwa

Kaimu Rais Mpya wa Misri, Adly Mansur
KAIMU Rais mpya wa Misri ameapishwa kuchukua nafasi ya Rais Mohammed Mosri aliyeondolewa madarakani na jeshi la nchini kufuatia wiki kadhaa ya maandamano.
Jaji mkuu wa mahakama ya juu zaidi ya kikatiba, Adly Mansur, ameapishwa nchini Misri kuwa rais wa muda baada ya jeshi kumng'oa madarakani rais aliyechaguliwa na raia kwa njia ya kidemokrasia na kushinda kwa wingi wa kura, Mohammed Mosri.
Viongozi duniani wamepokea kwa tahadhari matukio yanayojiri huko Misri. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amewaambia waandishi kwamba anaangalia kwa umakini hatua iliyochukuliwa na jeshi la Misri.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Uingereza , William Hague, amesema Uingereza haiungi mkono uvamizi huo wa kijeshi lakini haina budi kuitambua hatua hiyo na kusogea mbele. Hata hivyo alikataa kulishutumu jeshi kwa kumpindua Morsi akisema ni uvamizi ulioungwa mkono na watu wengi. Mfalme Abdalla wa Saudia ametuma ujumbe wa hongera kwa kaimu rais wa Misri akisema kwamba uteuzi wake unajiri katika wakati muhimu.
Mkuu wa jeshi Generali Abdul Fattah al-Sisi alitoa tangaza hilo kupitia televisheini Jumatano jioni, katika kile Morsi, alisema ni mapinduzi ya kijeshi.
Generali Sisi alisema kuwa Morsi,ambaye ni rais wa kwanza kuchaguliwa amekosa kutimiza mahitaji ya watu.
Kaimu rais huyo mpya ameahidi kurejesha hali ya amani nchini humo wakati akielekea kuitisha uchaguzi mkuu hapo baadaye.
Ishara ya mapenzi iliyochorwa angani kwa kutumia ndege za kijeshi kuwataka wananchi kupatana
Hatua hiyo inakuja baada ya siku nyingi ya maandamano, dhidi ya rais Morsi wa chama cha Musolim Brotherhood, ambaye inaelezwa anashikiliwa katika kambi moja ya kijeshi nchini humo.
Waandamanaji walimtuhumu yeye na chama chake kwa kusukuma ajenda ya kiisilamu kwa taifa hilo na kukosa kusuluhisha matatizo ya kiuchumi yanayokumba taifa hilo.
Chama cha Muslim Brotherhood kimesema kuwa bwana Morsi pamoja na washauri wake wako chini ya kifungo cha nyumbani na hawana mawasiliano ya nje.
Hapo awali mkuu wa majeshi alisema kuwa katiba ya nchi hiyo imeahirishwa na kwamba jaji mkuu wa taifa hilo atachukuwa mamlaka ya rais.
Maelfu ya waandamanaji wanaompinga bwana Morsi mjini Cairo walisherehekea kwa shangwe na vifijo kufuatia taarifa hiyo ya jeshi lakini wale wanaomuunga bwana Morsi wanasemekana kubaki kimya huku wakisubiri matukio yatakayofwata.
Rais Obama amesema kuwa ana wasiwasi mkubwa kuhusiana na matukio yaliyopo nchini Misri huku katibu mkuu wa umoja wa mataifa Banki Moon akitaka kuwe na utulivu.

BBC

Wednesday, July 3, 2013

Kesi dhidi ya maafisa wa Chadema yatupiliwa mbali

Mwita Waitara

KWA mara nyingine Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Singida, ilitupilia mbali kesi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) iliyokuwa ikiwakabili, Mwita Waitara, Afisa sera na utafiti Makao Makuu na Mshauri wa Chama hicho Dk Kitila Mkumbo,

Kesi hiyo ilitupiliwa mbali baada ya Mashahidi wa Serikali kushindwa kuthibitisha aina ya matusi yaliyodaiwa kutolewa na washitakiwa, waliyomtukana Naibu Katibu Mkuu, Mwigulu Mchemba, yaliyodaiwa kutolewa na Washitakiwa.

Sababu nyingine ya kutupilia mbali kesi hiyo ilielezwa kuwa ni upande wa serikali walishindwa kumleta shahidi muhimu katika kesi hiyo Nchemba, aliyedaiwa kutukanwa ili athibitishe kwamba yeye ndiye aliyetukanwa na namna ambavyo matusi hayo yalimuathiri.

“Washatakiwa hawana kesi ya kujibu kwa kuwa mashahidi wa serikali wameshindwa kuthibitisha aina ya matusi yaliyodaiwa kutolewa na washtakiwa”.alisema Masham Hakimu wa Mahakama hiyo.

“Upande wa serikali walishindwa kumleta shahidi muhimu katika kesi hiyo Mwigulu Nchemba aliyedaiwa kutukanwa ili athibitishe kwamba yeye ndiye aliyetukanwa na namna ambavyo matusi hayo yamemuathiri”.alisema Hakimu.

Alisema, Kushindwa kwa Nchemba kufika mahakamani ni kuonyesha kwamba ama hajui kwamba alitukanwa au hakuona kosa lolote alilotendewa na hivyo Mahakama haiwezi kutoa uamuzi kwa mambo ya kuhisiwa, alisema hakimu huyo.

Awali Washtakiwa hao, walidaiwa kutenda kosa hilo Julai 14, mwaka jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Ndago wilayani Iramba, ambapo Chadema kilikuwa na mkutano wa hadhara.

Wakati ikisomwa hukumu hiyo, alikuwepo Wakili wa Washitakiwa, Tundu Lisu, ambapo Hakimu Masham alisema washatakiwa hawana kesi ya kujibu kwa kuwa mashahidi wa serikali walishindwa kuthibitisha aina ya matusi yaliyodaiwa kutolewa na washitakiwa.

Kesi hiyo ambayo imekuwa ikisuasua mara nyingi kwa upande wa serikali kushindwa kuleta mashahidi mahakamani na kusababisha kesi hiyo kuahirishwa mara kwa mara, iliibua minong’ono jambo ambalo imedaiwa lilikuwa likimkera Hakimu wa kesi hiyo.

Wadau wa mambo ya kisheria wamekuwa wakihoji maswali mengi yasiyokuwa na majibu kwamba, inakuwaje baadhi ya viongozi wa Chama tawala wanawashaiwishi watu kufungua kesi zenye maslahi yao binfasi halafu siku ya kesi hawafiki? Je ni njia ya kuwasumbua watu au ni kuwapuuza Mahakimu?

Wengi wao wamekuwa wakiwatafsiri kuwa wanafanya hivyo wakijua wao ni chama tawala hivyo wanafanya ili kuwakomoa na kuwapa usumbufu wanaotuhumiwa kwa maana ya kuwafanya wazibe midomo ya kuwatetea wananchi?

Mwananchi ambaye alikuwepo mahakamani hapo na yeye akiwa na kesi alisema, anawashauri mahakimu wakate kudharauliwa na Viongozi wa Sampuli hizo, amabo wanawashikiza watu wafungue kesi kwa kulinda heshima zao, halafu wahusika hawafiki mahakani.

Amedai, kwanza kitendo hicho kinawadharirisha wananchi ambao wanabebwa kama debe tupu likisubiri hewa liwekwe kitu, ambapo wahusika wanaoona kesi zinawaendea kombo wanajificha na hivyo kuwaacha wao kama chama wakiadhrika.

Mama ambaye alikuwa mahakani hapo akiwa na kesi ya Miradhi alisema, tabia inayofanywa na viongozi hao, inachezea muda na fedha ambayo ni kodi ya wananchi, lakini akadai badala ya Mahakimu hao kufanya kazi ya kusikiliza kesi za wananchi zenye msingi wa kuwasaidia, wanapoteza muda kwa mambo yasiyo na maana.

Aidha Mwanaharakati aliyeomba asitajwe alisema, baadhi ya Viongozi na Watanzania wasipofuta mawazo ya kufanywa watumwa Punda au Ng’ombe, baadhi ya wanasisa watawachezea hivyo wasikubali kuwafanya vihongwe, huo wao wakijificha kwenye mapambano mfano kesi hizo.