STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, June 20, 2014

Filbert Bayi yachomoa kwenda kutetea taji la Netiboli Dodoma

MABINGWA watetezi wa Ligi Daraja la Kwanza kwa mchezo wa Netiboli, Filbert Bayi na Teachers za jijini Dar es Salaam hazitashiriki michuano hiyo itakayoanza rasmi mwezi ujao mjini Dodoma.
Hata hivyo klabu hizo zimetakiwa kutoa sababu maalum za kukwepa michuano hiyo ili kuepuka adhabu ya kushushwa daraja kama kanuni za ligi hiyo zinazovyoelekeza.
Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli (CHANETA), Anna Kibira aliiambia MICHARAZO mapema leo kuwa,  uongozi wa klabu hizo ulitoa taarifa za mdomo kwamba wasingeshiriki michuano hiyo ya Dodoma.
"Hata hivyo tuliwaambia waandike barua na kutoa sababu zinazoelewekwa ili kuepuka kukumbwa na 'rungu' la kanuni dhidi ya klabu zinazokacha michuano," alisema Kibira.
Aliongeza kuwa ukiondoa timu hizo, mpaka sasa klabu 17 zimethibitisha kushiriki ligi hiyo itakayoanza Julai 12-26.
Kibira alizitaja klabu zilizothibitisha ni JKT Ruvu, Jeshi Stars, CMTU, JKT Mbweni, Uhamiaji na Polisi Dar zote zikiwa za Dar es Salaam.
Nyingine ni Polisi, Magereza na TTL zote za mkoa wa Morogoro, Polisi-Kigoma, Polisi-Mbeya, Polisi-Arusha, Mbeya City Queens, CIDT-Arusha, Polisi-Shinyanga, Polisi-Dodoma, Polisi-Mwanza na Nyanyembe ya mkoa wa Tabora.
Kibira alisema maandalizi kwa ajili ya michuano hiyo kwa ajili ya kusaka bingwa na timu nne za kuiwakilisha Tanzania Bara kwenye Ligi Kuu ya Muungano yanaendelea vyema kwa sasa mjini Dodoma.
========

Madaktari wamuonya Ronaldo, mwenyewe mbishiiii

RIO DE JANEIRO, Brazil
DAKTARI wa Cristiano Ronaldo amemuonya nyota huyo wa Ureno kuwa, kama anajitia matatizoni kuichezea Ureno kwenye Kombe la Dunia kwa hali aliyionayo na  majeruhi na kwamba anaweza kushindwa kukipiga katika klabu yake kama ataendelea kucheza huko Brazil.
Nyota huyo wa Real Madrid anasumbuliwa na majeraha ya goti na yupo katika presha ya kuingoza timu yake kwenye mechi ya Jumapili dhidi ya Marekani baada ya mchezo wa ufunguzi wa kundi lao kukubali kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya Ujerumani.
Kwa mujibu wa gazeti la El Confidencial, daktari wa Mreno huyo Jose Carlos Noronha alimwambia Ronaldo (29), kuwa: 'Liache goti lako lipumzike, ama mustakabali wako wa baadaye uwe matatizoni', hata hivyo Ronaldo aliripotiwa kujibu: 'Mimi ndiye mwenye wajibu wa kusema nicheze ama ni sicheze'.
Ronaldo alipigwa picha akifanya mazoezi huku mguu ukiwa na 'bandeji' kwenye goti la kushoto linalomsumbua.
Kumekuwa na hofu kubwa kuhusu nyota huyo wa Real Madrid kuwa fiti wakati michuano hii ikiendelea, baada ya maumivu ya paja na goti kumlazimisha kutokuwamo wakati wa maandalizi ya michuano hiyo hapo awali.
Ronaldo alikiri kuwa fiti kwa asilimia 100  katika mechi ya ufunguzi ambayo walichapwa 4-0 na Ujerumani, hata hivyo pamoja na kukiri huko cheche zake hazikuonekana na kuweza kuisaidia timu yake kubadili matokeo.
Sasa inaonekana kuwa mshindi huyo wa Ballon d'Or anasumbiliwa na goti baada ya kuonekana akipatiwa matibabu wakati wakijifua huko Campinas, Brazil.
Ronaldo alitolewa nje kwa machela kabla ya kufungwa 'bandeji' pamoja na kuwekewa barafu mguuni katika goti la kushoto ikiwa ni dakika 30 kabla ya mazoezi kumalizika, hata hivyo hakuweza tena kurejea mazoezini hadi yalipomalizika.

Suarez aiangamiza England, Tembo wa Afrika wafa Colombia

Suarez akimtungua Joe Hart



WAKATI wawakilishi tegemeo la Afrika, Ivory Coast wakiwa mguu ndani mguu nje kwenye michuano ya Kombe la Dunia, nyota wa Liverpool, Luis Suarez amethibitisha ubora wake kwa kuifungia nchi ya Uruguay mabao mawili yaliyoizamisha England katika fainali hizo zinazoendelea nchini Brazili.
Suarez aliyekosa pambano la kwanza la Uruguay dhidi ya Costa Rica na kulala mabao 3-1, alirejea uwanjani akitokea kwenye majeruhi kwa kufunga mabao hayo yaliyoilaza England 2-1.
Wayne Rooney alifunga bao lake la kwanza kwenye fainali za Dunia katika dakika ya 75, lakini halikutosha kuiokoa nchi yake ambayo sasa inasubiri majaliwa yake kutokana na matokeo ya mechi ya leo ya kundi lake kati ya Italia na Costa Rica.
Kama Costa Rica itafungwa itakuwa nafuu kwa England ikisubiri kuona mechi yao ya mwisho dhidi ya Costa Rica itaamua vipi juu ya hatma yao, ingawa dalili za wazi ni kwamba timu hiyo imeshapoteza matumaini ya kusonga mbele na kuweka rekodi ya kufungwa mechi mbili mfululizo  za makundi katika michuano hiyo mkubwa ya dunia.
Mtukutu Suarez kinara wa mabao wa Ligi Kuu ya England, alianza kuiadhibu England kwa bao la dakika ya 39 ambalo lilidumu hadi wakati wa mapumziko kabla ya Rooney kusawazisha na kuonyesha kwamba mechi ingeisha kwa sare kabla ya Suarez kuzima ndoto hizo dakika ya 86.
Katika mechi nyingine zilizochezwa jana, Ivory Coast ilijikuta ikipokea kipigo cha mabao 2-1 toka kwa Colombia na kuwaacha wapinzani wao wakitangulia hatua ya 16 Bora.
Colombia iliyoitungua timu ya Ugiriki kwa mabao 3-0 katika mechi yao ya kwanza ilitangulia kupata mabao yake katika dakika ya 64 na 70 kupitia kwa James Rodriguez na Juan Quintero kabla ya Tembo hao wa Afrika kupata bao la kutia machozi lililokuwa la kuisawazisha kuptia kwa Gervinho dakika ya 74.
Nayo Japan na Ugiriki zimeshindwa kutambiana baada ya kutoka suluhu ya bila kufungana na kutoa nafuu kwa Ivory Coast ambao wanasubiri kujua hatma yao watakapoumana na Ugiriki wiki ijayo.
Kipute cha fainali hizo kinaendelea tena kwa michezo itakayozikutanisha Italia dhidi ya Costa Rica, Uswisi dhidi ya Ufaransa na Hondurus itapepetana na Ecuador
RATIBA IPO hivi:
LEO Juni 20, 2014
 Italia    v    Costa Rica        Saa 1:00 Usiku  
 Uswis    v    Ufaransa        Saa 4:00 Usiku  
 Honduras    v    Ecuador    Saa 6:59 Usiku  

KESHO Jumamosi Juni 21, 2014
Argentina    v    Iran        Saa 1:00 Usiku  
Ujerumani    v    Ghana        Saa 4:00 Usiku
Nigeria    v    Bosnia-Herze    Saa 6:59 Usiku

Maskini Michael Wambura 'achinjwa' kimoja Simba

KAMATI ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imeikataa rufani ya Michael Wambura kupinga kuenguliwa kugombea urais katika uchaguzi wa klabu ya Simba unaotarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu.
Wambura aliwasilisha rufani yake mbele ya Kamati hiyo iliyokutana leo (Juni 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam chini ya Kaimu Mwenyekiti Wakili Mwita Waissaka kupinga uamuzi wa kumwengua katika kinyang’anyiro hicho uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya Simba kwa kufanya kampeni kabla ya muda uliopangwa.
Baada ya kupitia vielelezo, kanuni na sheria, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF imeridhika kuwa mrufani (Michael Wambura) alifanya kampeni kabla ya muda kinyume na Ibara ya 6(1)(a) na (g), Ibara ya 6(1)(l) pamoja na Ibara ya 14(3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF toleo la 2013.
Kwa mujibu wa ibara hizo, Kamati ya Uchaguzi ya Simba inayo mamlaka ya kumwengua (disqualify) mgombea anayefanya kampeni ama kukiuka maagizo halali ya Kamati ya Uchaguzi.
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF imeziagiza kamati zote za uchaguzi za wanachama wa TFF kufuata kanuni za uchaguzi kama zilivyoainishwa katika Katiba zao ili kuepusha rufani za mara kwa mara.
Uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF umezingatia Katiba ya TFF pamoja na kanuni zake, na pia Katiba ya Simba.

26 Stars waitwa kambini safari ya Botswana

WACHEZAJI 26 wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) wanatarajiwa kuingia kambini Jumatatu kwa ajili ya safari ya Gaborone, Botswana. 
Kwa mujibu wa Kocha Msaidizi wa Stars Salum Mayanga, wachezaji hao wanatakiwa kuripoti katika hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa safari hiyo inayotarajiwa kuwa Juni 24 mwaka huu, ikiwa ni maandalizi ya mechi ya kuwania Fainali za Afrika 2015 dhidi ya nchi ya Msumbiji (Mamba).
Wachezaji wanaoatakiwa kambini ni pamoja na makipa Deogratias Munishi 'Dida' na Aishi Manula, mabeki Benedictor Tinoko, Kelvin Yondani, Said Moradi, Nadir Haroub, Joram Nason, Shomari Kapombe, Oscar Joshua, Edward Charles, Aggrey Morris na Pato Ngonyani. 
Wengine ni viungo Frank Domayo, Amri Kiemba, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Said Juma, Haruna Chanongo na Himid Mao, huku washambuliaji wakiwa ni John Bocco, Simon Msuva, Kelvin Friday, Ramadhan Singano, Khamis Mcha, Mrisho Ngasa na Mwegane Yeya.
Stars itavaana na Mamba Julai 20 jijini Dar es Salaam kabla ya kurudiana nao wiki mbili baadaye mjini Maputo Msumbiji na itakayopenya hapo itatinga kundi F la mchujo wa fainali hizo za Afrika za nchini Morocco.
Katika kundi hilo Stars ikifuzu itakumbana na timu za Zambia, Niger na Cape Verde.

Tuesday, June 17, 2014

Thomas Muller awafunika wakali wengine Brazil

WAKATI Climt  Dempsey wa Marekani akiweka rekodi ya kufunga bao la mapema zaidi mpaka sasa kwenye Kombe la Dunia likikamata nafasi ya tano tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo mwaka 1930, Mjerumani Thomas Muller amewafunika wakali wengine kwa kuongoza orodha ya ufungaji mpaka sasa.
Muller anaongoza msimamo akiwa na mabao matatu aliyioyapata jana wakati wakiiangamiza Ureno kwa mabao 4-0 na kuwazidi Robin Van Persie, Karim Benzema na Arjen Robben, Neymar waliokuwa wakiongoza na mabao mawili kila mmoja wakati raundi ya kwanza ikitarajiwa kumalizka leo kabla ya timu nyingine kuanza ngwe ya pili ya makundi.
Muller alifunga mabao hayo katika pambano la kundi la kifoi ambalo lilishuhudia Mmarekani Clint Dempsey akifunga bao la mapema zaidi katika michuano ya mwaka huu ya nchini Brazili katika sekunde ya 29 tu na kukamata nafasi ya tano katika goli la mapema lililowahi kufungwa kwa muda wote wa michuano hiyo ya Kombe la Dunia.
Bao la Mmarekani huyo limepitwa na yale ya Hakan Sukur linaloongoza likiwa lifungwa Sekunde ya 11 katika michuano ya mwaka 2002, Vaclav Masek aliyefungwa sekunde ya 16 kwenye michuano ya mwaka 1962, Ernst Lehner la sekunde ya 25 kwenye michuano ya mwaka 1934 na lile la Brayan Robson la sekunde ya 27 michuano ya mwaka 1982.
Orodha ya mabao ya mapema katika Kombe la Dunia ni kama ifuatavyo;
Hakan Sukur (2002) Sekunde 11
Vaclav Masek (1962) Sekunde 16
Ernst Lehner (1934) Sekunde 25
Brayan Robson (1982) Sekunde 27
Clint Dempsey (2014) Sekunde 29
Bernard Lacombe (1978) Sekunde 30
Emile Veinante (1938) Sekunde 35
Arne Nyberg (1938) Sekunde 35
Florian Albert (1962) Sekunde 50
Adalbert Desu (1930) Sekunde 50

Chini ni Orodha ya wafungaji wanaoongoza kwa sasa katika michuano ya Brazil;
3- Thomas Müller (Germany)
2- Karim Benzema (France)
    Neymar (Brazil)
    Arjen Robben (Netherlands)
    Robin van Persie (Netherlands)
1- Lionel Messi (Argentina)
    Xabi Alonso (Spain)   
    P. Armero (Colombia)
    Mario Balotelli (Italy)       
    J. Beausejour (Chile)
   Winfried  Bony (Côte d'Ivoire)
   Gervinho (Cote d'Ivoire)
   T. Cahill (Australia)
   J. Campbell (Costa Rica)
   Edinson Cavani (Uruguay)
   S. de Vrij (Netherlands)
   Andre Ayew (Ghana)
   Clint Dempsey (USA)
   John Brooks (USA)
  Mats Hummels (Germany)

Shaaban Kisiga aibeba Morning Star

Na Adam Fungamwango
KIUNGO mchezeshaji wa Mtibwa Sugar Shaabani Kisiga, juzi aliipeleka robo fainali ya Wadau Cup timu yake ya Morning Star ya Kiwalani alipofunga bao moja na kutengeneza lingine, ilipoifunga Mwananyamala Veterani mabao 2-0.
Mechi hiyo kali ilifanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi Mwananyamala ambako michuano hiyo inafanyika.
Kisiga ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa Simba na SC Villa ya Uganda, alifunga bao kwenye dakika ya 75 kwa shuti kali baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Zokora Nyambiso.
Bao hilo liliamsha mayowe kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo baada ya kulisubiri kwa muda mrefu, kwani timu yao ilihitaji ushindi tu ili iweze kusonga mbele.
Mshambuliaji wa Ruvu Shooting Paul Ndauka aliikosesha bao Morning Star katika dakika ya 80 baada ya kupiga shuti lililopaa akibaki yeye na kipa Hamza Zongera wa Mwananyamala Veterani.
Kisiga akiwa katikati ya uwanja alitoa pasi ndefu kwa Nyeje Mussa ambaye hakufanya makosa na kuukwamisha mpira wavuni kwenye dakika ya 88, akiihakikishia timu yake ushindi.
Mbali na Morning Star, timu nyingine zilizofanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ni Mbogamboga FC, Sharobaro FC na African People zote za Mwananyamala, Kijitonyama Chipukizi, Generation ya Kinondoni.

Ruvu Star kusambaza Spirit videoni

Rogert Hegga
BENDI ya Ruvu Star imekamilisha kurekodi video zao mbili za nyimbo za 'Spirit' na 'Jua Kali' na wanatarjiwa kuanza kusambaza wiki hii ili kuwapa burudani mashabiki wa muziki wa dansi nchini.
Nyimbo hizo zilizorekodiwa video hizo ni kati ya tatu zinazoendelea kutamba kwenye vituo vya redio, wimbo mwingine ukifahamika kwa jina la 'Network Love' ambao video yake imewekwa kiporo kwa sasa.
Akizungumza na MICHARAZO mmoja wa viongozi wa Ruvu, Roger Hegga alisema nyimbo hizo zitasambazwa kuanzia kesho kabla ya bendi yao kuingia tena studio kumaliza kurekodi nyimbo tatu za mwisho za kukamilisha albamu yao ya kwanza.
Hegga alisema walipanga kuingia studio wiki hii, lakini wamesitisha zoezi hilo kupisha maandalizi ya onyesho maalum la 'Usiku wa Mwana Dar es Salaam' litakalofanyika siku ya Jumamosi, jijini Dar.
"Baadhi ya wanamuziki wa Ruvu ni wale walioshiriki albamu ya Mwana Dar es Salaam ya African Stars 'Twanga Pepeta'. hivyo kwa sasa wanamuziki hao tupo katika mazoezi ya onyesho hilo," alisema.
Alisema baada ya onyesho hilo la 'Usiku wa Mwana Dar es Salaam' wanamuziki wa Ruvu watarejea kwenye bendi yao na kufanya mazoezi ya mwisho kabla ya kuingia studio kurekodi nyimbo hizo.
Hegga, mtunzi na muimbaji nyota nchini alizitaja nyimbo hizo za mwisho za kukamilisha albamu yao ni 'Koo' uliotungwa na Khamis Kanyumbu 'Amigolas', 'Chewa Original'-Suleiman Muhumba na 'Facebook' cha mpapasa kinanda Victor Mkambi.

Taifa Stars kuinolea makali Mamba nchini Botswana

KIKOSI cha tmu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kinatarajiwa kuondoka nchini wiki ijayo kwenda Botswana kuweka kambi ya mwezi mmoja kujiandaa na mchezo dhidi ya Msumbiji kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani Morocco.
Wachezaji wote wa Taifa Stars waliruhusiwa kurejea makwao baada ya kuingia kambini juni 11 kwa ajili ya kujiandaa na safari hiyo na watakutana tena kesho.
Stars inayofundishwa na Mholanzi, Mart Nooij itaondoka nchini Juni 27 kwenda Gaborone, ambako itaweka kambi ya mazoezi hadi Julai 7 itakaporejea nchini.
Taifa Stars itamenyana na Msumbiji ‘Mambas’ katika hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco baada ya kuitoa Zimbabwe juzi kwa jumla ya mabao 3-2, ikianza kwa ushindi wa 1-0  nyumbani na kumaliza kwa sare ya 2-2 juzi mjini hapa.
Mechi yake kwanza itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Julai 19 na 20 mwaka huu, wakati mechi ya marudiano itafanyika Msumbiji kati ya Agosti 2 na 3 mwaka huu.
Stars pia inatarajiwa kuwa na mchezo wa kujipima nguvu na Uganda kabla ya kumenyana na Msumbiji.

Dk Ndumbaro amdindia Malinzi, 'amchinja' tena Wambura

Dk Ndumbaro
KAMATI  ya Uchaguzi ya Simba imemuondoa kwa mara nyingine Michael Wambura kutokana na kufanya kampeni kabla ya wakati huku akiwa ameonywa.
Pia imesisitiza uchaguzi utafanyika Juni 29 kama ilivyopangwa kwa kuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi aliyetangaza kuusimamisha, hana mamlaka hayo kikatiba.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, mwanasheria na wakili maarufu nchini, Dokta Damas Daniel Ndumbaro 'DDN' ndiye amefunga na kusema hayo.
Ndumbaro amemwaga ripoti kamili ambayo inachambua mambo yote huku ikionyesha kiasi gani Malinzi hana haki ya kusitisha uchaguzi huo kama alivyotangaza jana.
IFUATAYO NDIYO RIPOTI KAMILI YA DAKTARI HUYO WA SHERIA NCHINI:
Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club, ilifanya mkutano wake kawaida tarehe 15 Juni 2014 kujadili mambo mbalimbali ambayo yanayohusu uchaguzi mkuu wa Simba Sports Club ambao umepangwa kufanyika tarehe tarehe 29 Juni 2014. Kamati ya Uchaguzi ya Simba sports Club inapenda kuujulisha umma, hususan wapenzi wa Simba Sports Club mambo yafuatayo:

1. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club, kwa mujibu wa Ibara ya 10(6) ya Kanuni za uchaguzi za TFF toleo la mwaka 2013, ndiyo chombo pekee chenye mamlaka ya kutangaza, kubadilisha, kusimamisha au kufuta tarehe ya Uchaguzi ya Simba Sports Club. Kwakuwa Kamati haijafanya hivyo, wala hakuna mdau yoyote aliyeleta hoja ya kusimamisha uchaguzi, tunawajulisha kuwa uchaguzi wa Simba Sports Club upo pale pale kama ambayo Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilivyopanga. Maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vema na Uchaguzi utafanyika tarehe 29 Juni 2014 kama ilivyopangwa hapo awali.
2. Kamati imesikia kupitia vyombo vya habari kuwa TFF imesimamisha uchaguzi wa Simba Sports Club mpaka hapo Kamati ya Utendaji ya Simba Sports Club itakapoteua Kamati ya Maadili. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club inapenda kusema yafuatayo:
i. Mamlaka ya kusimamisha uchaguzi ni kazi ya Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club kwa mujibu wa ibara 10 (6) ya Kanuni za Uchaguzi, 2013
ii. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilipoanza mchakato wa uchaguzi ilitoa tamko kuwa: “kwasababu Simba Sports Club haina kanuni za Uchaguzi, Kamati ya Rufaa ya uchaguzi, wala Kamati za Maadili kwa mujibu wa ibara za 16 (e) na (f) ya Katiba ya Simba Mwaka 2014, vyombo husika vya TFF vitatumika”. Kulikuwa hakuna pingamizi toka kwa mtu yoyote juu ya kauli hiyo, ikiwemo TFF.
iii. Tarehe 26 Mei 2013, Rais wa TFF aliialika Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club katika chakula cha mchana. Katika mkutano huo, kauli ya aya (ii) hapo juu ilirejewa na Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilikabidhi rasmi mchakato mzima wa uchaguzi na kutoa ufafanuzi kuwa kamati husika za TFF zitahusika, jambo ambalo halikupingwa na TFF.
iv. TFF iliruhusu Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF kusikiliza Rufaa za uchaguzi za Simba, hivyo basi haiwezi kuzuia Kamati zake nyingine kusikiliza Masuala ya kimaadili. “Estopel” inawazuia TFF kufanya hivyo sasa.
v. Wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji ya Simba Sports Club, isipokuwa watatu tu, ni wagombea katika uchaguzi huu. Na hao watoto tayari wapo kwenye Kambi za Kampeni za uchaguzi hii ambazo zipo bayana kabisa. Kuiagiza Kamati ya Utendaji ya Simba iunde Kamati ya Maadili kusikiliza kesi za maadili dhidi yao wenyewe ni kukiuka msingi wa haki ya asili (natural justice). Ni dhahiri kuwa haki haiwezi kutendeka kwa wajumbe wa kamati ya utendaji ya Simba Sports Sports Club, ambao ni watuhumiwa katika masuala ya maadili, wachague majaji wa kuwahukumu. Hapo haki haitatendeka.
Ifahamike kuwa, baada ya Kamati ya Utendaji ya Simba Sports Club kuteua Kamati ya uchaguzi ya Simba Sports Club, Kamati hiyo haina mamlaka tena ya kujadili, kuingilia au kuteua chombo kingine kufanya shughuli zinazohusu uchaguzi ukizingatia kuwa wajumbe wake ni wagombea.
vi. Katika Uchaguzi Mkuu wa TFF wa Mwaka 2013, ambao ulimuingiza Jamal Malinzi Madarakani, FIFA walikuja, wakongea na pande zote na hatimaye, walisema kuwa; “tunapendekeza kuwa uchaguzi mkuu usimame ili kuunda kamati mbalimbali”. Mapendekezo hayo yalipokelewa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Bw. Deo Lyato, na hatimaye ni Kamati ya Uchaguzi ya TFF ndio iliyotangaza kusimamisha Uchaguzi na sio Sepp Blatter.
vii. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ni Kamati huru ambayo haipaswi kuingiliwa na Chombo chochote kile. Ili kulinda uhuru huo, tunalazimika kukanusha matamshi ya TFF kuhusu kusitisha Uchaguzi Mkuu wa Simba Sports Club. 
3. Malalamiko ya Kimaadili Kupelekwa FIFA.
Kwa mujibu wa Ibara ya 11 (9) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF, 2013, inatoa mamlaka kwa Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club kupeleka masuala ya maadili katika kamati ya maadili ya TFF. Tarehe 9 Juni 2014, Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilipeleka Masuala ya Maadili katika Kamati ya Maadili ya TFF. Kwakuwa TFF imekataa kusikiliza masuala ya maadili ambayo yanakiuka Kanuni za maadili, Katiba za Simba, TFF na FIFA, Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club, itapeleka Masuala ya Maadili FIFA ili haki itendeke.
4. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilijadili kuhusu vitendo vya wagombea kupiga kampeni kabla ya muda wa kampeni ulioruhusiwa. Kwa mujibu wa Mchakato wa Uchaguzi ya Simba Sports Club, muda wa kampeni unaanza tarehe 24 -28 Juni 2014. Hapo awali kamati ilibaini kuwa wagombea wawili wa nafasi ya urais; Michael Richard Wambura na Evans Aveva walifanya vitendo vya kampeni siku ya kuchukua na kurejesha fomu za kugombea. Tarehe 25 Mei 2014, Kamati iliwapa ONYO KALI la maandishi wagombea hao na kuwataarifu kuwa hatua kali zaidi zitachukuliwa dhidi yao, ikiwemo kuondolewa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi. 
Baada ya Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club kumuondoa Bw. Michael Richard Wambura katika kinyang’anyiro cha uchaguzi Mkuu wa SImba Sports Club, Bw. Wambura aliitisha Mkutano na waandishi wa habari, aliitukana Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club, na kutoa matamshi ambayo ni Kampeni.
Baadaya ya Kamati ya Rufaa ya uchaguzi ya TFF kumrejesha Bw. Wambura katika Kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa Simba, Bw. Wambura aliitisha tena mkutano wa waandishi wa habari, aliisifu kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF, kwa mara kwanza aliisifu Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club na kutoa matamshi ambayo ni wazi kuwa ni kampeni. Baadhi ya Matamshi aliyoyatoa kupitia vyombo vya habari ni kama ifuatavyo:
i. “Simba Sports Club inahitaji zaidi wadhamini na sio wafadhili”
ii. “Wafadhili kazi yao in kutoa fedha mfuko wa kushoto na kuepeleka mfuko wa kulia”
iii. “Simba ilikuwa na viwanja vitatu lakini kimoja kimeuzwa na wajanja na vimebaki viwili tu”
Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilitafakari matamshi hayo, na kubaini kuwa hiyo ni kampeni ya waziwazi wakati muda wa kampeni bado haujaanza.
Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ililipa jambo ili uzito wa kipekee kwasababu Mkosaji amekuwa na tabia ya kurudia kosa hilo hata baada ya kupewe onyo la maandishi.
HIVYO BASI: Kwa mujibu wa mamlaka ya kikanuni, hususan Ibara za: 6 (1) (a) – (g); 6 (1) (L) na 14(3) za Kanuni za uchaguzi za TFF – 2013, Bw. Michael Richard Wambura anaondolewa Katika Kinyang’anyiro cha Uchaguzi wa Simba Sports Club, 2013, kwa kosa la kurudia kufanya kampeni kabla ya muda wa kampeni ambao umepengwa."

Ratiba ya Kombe la Dunia ipo hivi

  
LEO Juni 17, 2014
16. Ubelgiji     v    Algeria        Saa 1:00 Usiku  
17. Brazil    v    Mexico        Saa 4:00 Usiku  
18. Urusi    v    Korea        Saa 6:59 Usiku      

KESHO Juni 18, 2014
20.Australia    v Uholanzi        Saa 1:00 Usiku
19. Hispania v    Chile            Saa 4:00 Usiku
18. Cameroon    v    Croatia        Saa 6:59 Usiku      

Alhamisi Juni 19, 2014

21.Colombia    v    Ivory Coast     Saa 1:00 Usiku  
23.Uruguay    v    England     Saa 4:00 Usiku
22.Japan    v    Ugiriki         Saa 6:59 Usiku    

Riyana, Slim wapiga mzigo Zenji


STAA wa filamu nchini, Riyama Ally na Slim Omary 'Kiwi' wapo Zanzibar kwa ajili ya kutengeneza filamu iitwayo 'Dhana' wakishirikiana na wasanii wa visiwani humo.
Akizungumza na MICHARAZO juzi, Kiwi alisema sehemu kubwa ya filamu hiyo imekamilika na walikuwa njiani kurejea jijini Dar es Salaam kuendelea na majukumu yao mengine.
Kiwi alisema mbali na yeye na Riyama filamu hiyo imechezwa pia na msanii maarufu visiwani humo aitwaye Eddy na wakali wengine za Zanzibar na ni 'bonge' la mseto.
"Tupo visiwani kumaliza kushiriki filamu mpya iliyozalishwa visiwani humu iitwayo 'Dhana' ni bonge la filamu kwani kisa chake kina mafunzo makubwa kwa jamii," alisema.
Kiwi alisema simulizi ya filamu hiyo linamhusu mtu mmoja ambaye anamjengea dhana mbaya mkewe kumfanyia usaliti na kuamua kulipa kisasi ambacho kinakuwa majutoa kwake.
"Hii siyo ya kuikosa kwa sababu mikasa kama hii imekuwa ikizikumba nyumba nyingi na watu kuwekeana kinyongo kwa dhana tu, bila ya uhakika wa jambo analodhania," alisema.
Msanii huyo anayetamba

Ghana yafa kiume, Nigeria yabanwa na Iran, Ujerumani dah!

Ronaldo alijitahidi mbele ya Ujeruman, lakini jahazi lao lilizama mara 4
Vita ya Nigeria na Iran ilikuwa hivi
Dempsey akishangilia bao lake dhidi ya Ghana
WAKATI Ujerumani ikitoa onyo katika Fainali za Kombe la Dunia kwa kuigagadua Ureno kwa mabao 4-0 timu za Afrika zimeendelea kuchechemea.
Ghana ilijikuta ikifa kiume mbele ya Marekani kwa kucharazwa mabao 2-1, huku wawakilishi Nigeria wakibanwa mbavu na Iran katika mchezo mwingine.
Ujeruman waliopo kundi G waliitoa nishai Ureno ikiwa na nyota wa dunia, Cristiano Ronaldo kwa kuilaza mabao 4-0 huku beki wake 'mapepe' Pepe alilimwa kadi nyekundu.
Mabao ya Thomas Muller aliyefunga 'hat trick' na jingine la Mats Hummels yalitosha kuiangamiza Ureno katika pambano la kwanza la timu hizo lililochezwa saa 1 usiku.
Baadaye saa nne Nigeria ikisakata kandanda murua ilishindwa kupata ushindi mbele ya Iran iliyotumia muda mrefu kupaki basi na kushambulia kwa pamoja.
Manane ya usiku Ghana walikuwa dimbani kukamilisha ratriba ya mechi za kwanza za kundi G kwa kuvana na Marekani na kujikuta wakilazwa mabao 2-1.
Bao la mapema la Clint Dempsey kwenye sekundi ya 31 na jingine la dakika ya 86 kupitia kwa John Brooks yalitosha kuzima ndoto za Ghana kuambulia sare.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Fulham, aliifungia Marekani inayonolewa na kocha Jurgen Klinsmann alifunga bao hilo dakika nne baada ya Ghana kuchomoa bao kupitia kwa Andre Ayew.
Michuano hiyo itaendelea tena leo kwa michezo mitatu, Algeria wataumana na Ubelgiji, huku Brazil wenyeji wa michuano hiyo watacheza mchezo wao wa pili dhidi ya Mexico na Urusi kupepetana na Korea.

Kalidjo Kitokololo atua Mashujaa Band, uongozi watamba

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Bendi ya Mashujaa Bw. Maximillian Luhanga akizungumza katika mkutano huo wakati alipomtambulisha rapa Kitokololo kushoto kutoka bendi ya FM Academia kulia ni King Dodoo mshauri wa bendi hiyo.
Kitkololo akitangaza rasmi kujiunga na bendi ya Mashujaa leo kulia ni Mkurugenzi wa Mawasiliano Bw. Maximillian Luhanga.
BENDI ya Mashujaa imemchukua rapa, Kalidjo Kitokololo ‘Kuku’ kutoka bendi ya FM Academia na kusaini naye Mkataba wa miaka miwili.
Akizungumza kwenye ukumbi wa Milenium Business Park leo , Kijitonyama, Dar es Salaam Mkurugenzi wa Mawasiliano wa bendi hiyo, Maximillian Luhanga amesema kupatikana kwa Chitokololo ni furaha kubwa kwao. 
“Kalidjo anakuwa rapa wa tatu katika bendi ya Mashujaa , baada ya Saulo John maaurufu Ferguson na Sauti ya Radi, ambao wote ni wakali, kwa marapa hao wote tunaamini bendi yetu itakuwa inatisha sana,” amesema Luhanga. 
Maxmilian Luhanga amesema Kitokololo anaanza kazi mara moja baada ya kusaini mkataba mpya.
Kwa upande wake, Kitokololo mwanamuziki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) amesema amekuja Tanzania kutafuta maisha na Mashujaa imempa ofa nzuri ndiyo maana amejiunga na bendi hiyo.
Amesema ameondoka vizuri FM Academia akiwa amewaaga vizuri wenzake ambao wameridhia kuondoka kwake.
Kitokololo amesema kwamba amejiunga na Mashujaa akimfuata King Dodo ambaye kimuziki ni baba yake , King Dodoo ndiye aliyemleta nchini kwa mara ya kwanza mwaka 2004.
Mashujaa itamtambulisha rasmi mwanamuziki huyo katika onyesho maalum litakalofanyika ukumbi wa Letasi Lounge Ijumaa wiki hii. Mashujaa pia wanatarajiwa kuwa na ratiba ndefu mara baada ya mfungo mtukufu wa ramadhani ambapo Maximillian Luhanga amewaambia mashabiki wa bendi hiyo nchini kote kukaa mkao wa kula, Kwakuwa bendi hiyo itakuwa na ziara karibu mikoa yote ya Tanzania ili kutoa burudani kwa mashabiki wao.

Sunday, June 15, 2014

Ronaldo awatoa hofu Ureno wakijiandaa kuivaa Ujerumani

Ronaldo alipokuwa akitoka uwanjani kwenye mazoezi
WAKATI nchi yake kesho ikitarajiwa kuwa na kibarua kigumu mbele ya Wajerumani katika mechi yao ya kwanza ya Kombe la Dunia, Mshambuliaji nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo amewatoa hofu mashabiki wa timu yake.
Ronaldo aliviambia vyombo vya habari nchini kwake kuwa majeraha ya goti lake la kushoto yamepona, wakati akifanya mazoezi. 
Zaidi mashabiki wapatao 10,000 walikuwepo kutizama mazoezi hayo ya wazi huko Campinas ambapo kuna wakati mwanamke mmoja alikimbia uwanjani na kujaribu kumfikia Ronaldo na kuzuiwa na walinzi kabla ya kukimbia tena mita 40 na kuwekwa chini na walinzi wengine. 
Ronaldo ambaye alicheza mchezo wa kirafiki ambao Ureno iliitandika Ireland kwa mabao 5-1, alimfuata mwanamke huyo aliwekwa chini ya ulinzi na kuweka saini katika fufala yake kabla ya wachezaji wengine wa Ureno nao kuvua fulana zao na kuwarushia mashabiki hao. 
Ureno itakwaana na Ujerumani katika mchezo wao ufunguzi utakaochezwa kesho Jumatatu na inatarajiwa nyota huyo wa Real Madrid atashuka dimbani kuiongoza nchi yake katika pambano hilo.
Nchi hizo mbili zipo kundi moja na timu za Ghana na Marekani zitakazoumana baadaye usiku wa manane hiyo kesho.

Angeline Jolie atunukiwa tuzo za Malkia Elizabeth

WACHEZA filamu Daniel Day-Lewis na Angelina Jolie, wametukuzwa na Malkia Elizabeth wa Uingereza katika orodha anayotoa kila mwaka kuwatunza watu waliotoa mchango mkubwa kwa jamii.
Daniel Day-Lewis atapewa cheo cha Sir, na Angelina Jolie atapewa cheo cha Dame kwa kampeni yake ya kupambana na uhalifu wa ubakaji wa wanawake katika maeneo ya vita, pamoja na kazi zake nyengine kwa niaba ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi, UNHCR.
Na waandishi wawili wa BBC wamepata nishani ya OBE:
Lyse Doucet, mwandishi mkuu wa BBC katika maswala ya kimataifa, na Tin Htar Swe, mhariri wa Idhaa ya BBC ya lugha ya Burma.
Stephen Sutton, kijana wa miaka 19 aliyekufa karibuni kutokana na saratani, na wakati akiugua aliongoza mchango wa karibu dola milioni 7 kugharimia utafiti dhidi ya ugonjwa huo, ametunzwa MBE, (ambayo alipokea kabla ya kufariki mwezi uliopita.)
Mtunzi wa riwaya, Hilary Mantel, aliyeandika vitabu vilivyopata zawadi ya Booker, 'Wolf Hall' na 'Bring up the Bodies', piya amepewa hadhi ya Dame.
BBC

Wagosi wa Kaya kuteta Juni 22, yafanya kufuru ya usajili

MABINGWA wa zamani wa soka nchini, Coastal Union ya Tanga inatarajiwa kufanya Mkutano Mkuu wa wanachama Juni 22 kwenye ukumbi wa Hotel ya Mkonge, jijini Tanga, huku wakiwasainisha wachezaji kadhaa wapya na wa zamani kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Afisa Habari wa klabu hiyo, Oscar Assenga mkutano huo utakuwa na ajenda kuu mbili zitakazojadiliwa na mengineyo.
Assenga alisema ajenda ya kwanza itakuwa ni kupokea taarifa na kujadili taarifa za kazi kutoka kamati mbalimbali za utendaji ndani ya klabu hiyo kwa kipindi kilichopita.
Pia alisema kutakuwa na kuthibitisha bajeti kwa mwaka wa fedha unaofuata baada ya mwaka uliopita kumalizika ambapo mkutano huo hautaruhusu wanachama wanaodaiwa madeni kuhudhuria.
“Pia tutafanya marekebisho ya katiba kwani tutaongeza kifungu cha kamati ya maadili ambacho ni muhimu ikiwa ni agizo la TFF," alisema Assenga.
Afisa Habari huyo alitoa wito kwa wanachama wa klabu hiyo waliopo sehemu mbalimbali hapa nchini kuhakikisha wanatimiza haki yao ya msingi kwa kuhudhuria kwenye mkutano huo muhimu kwa ajili ya maendeleo ya timu hiyo kongwe hapa nchini.
Mkutano huo unafanyika huku klabu hiyo ikiwa imeanza mchakato wa usajili wa wachezaji kwa msimu ujao wa Ligi Kuu ikiwasainisha wachezaji kutoka Mgambio JKT, ASAhanti United na wale iliyoikuwa nao msimu uliopita, licha ya kukimbiwa na aliyekuwa  mfadhili wao, Nassor BinSlum aliyeingia mkataba wa kuidhamini klabu ya Mbeya City kwa miaka mitatu.

Ivo Mapunda atoa darsa Kombe la Dunia

GOLIKIPA wa klabu ya Simba na timu ya taifa 'Taifa Stars', Ivo Mapunda, amesema wachezaji wa soka nchini wanapaswa kuzitumia fainali za kombe la Dunia zilizoanza juzi nchini Brazil kwa ajili ya kujifunza mambo mablimbali ya soka.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mapunda, alisema kuwa pamoja na kuwa Tanzania haishiriki kwenye fainali hizo lakini kuna nafasi kwa wachezaji kujifunza kitu kwenye michuano hiyo mikubwa Duniani.
"Hatupo kwenye fainali..., lakini tumepata fulsa ya kutazama fainali hizi kupitia luninga, tunaweza kama wachezaji kujifunza kitu kutoka kwa wenzetu," alisema Mapunda.
Alisema kuwa hata kwa viongozi wa soka nchini wanapaswa kujipanga na kuhakikisha mikakati thabiti inawekwa ili Tanzania ishiriki kwenye fainali hizo miaka ijayo.
Alisema kuwa Tanzania bado ipo nyuma kisoka ukilinganisha na nchi zinazoshiriki kwenye fainali za Dunia lakini bado ina nafasi ya kufikia kwenye uwezo wa kucheza kombe la Dunia.
"Hata hizo timu zinazoshiriki sasa hivi zilianza chini kabisa kama sisi, ila wenzetu walikuwa na mipango mizuri..., tupo nyuma sana lakini tunaweza," aliongezea kusema Mapunda.
Alisema kuwa kama hakutakuwa na mipango mizuri, Tanzania itaendelea kuwa wafuatiliaji kwenye luninga wa fainali za kombe la Dunia.

Bacary Sagna atua Manchester City kilaini akiikacha Arsenal

KLABU ya Manchester City imetangaza rasmi kumnasa beki Bacary Sagna kwa uhamisho huru kutoka klabu ya Arsenal. 
Beki huyo wa kimataifa wa Ufaransa amejiunga na mabingwa hao wa Ligi Kuu kwa mkataba wa miaka mitatu baada ya kuthibitisha juzi kuwa hataongeza mkataba na Arsenal. 
Mustakabali wa beki huyo kubakia Arsenal umekuwa mashakani kwa kipindi kirefu baada ya kushindikana kufikiwa kwa makubaliano ya mkataba mpya aliokuwa akiutaka mchezaji huyo. 
Sagna mwenye umri wa miaka 31 ameungana na kiungo wa Porto Fernando ambao meneja wa City Manuel Pellegrini alikuwa akiwahitaji katika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi. 
Kuondoka kwa Sagna kunamuacha kocha Arsene Wenger kutafuta mbadala mpya katika nafasi ya beki wa kulia huku mchezaji wa Atletico Madrid JuanFran na nyota wa Toulouse Serge Aurier wakiwa wachezaji wanaotizamiwa kuziba pengo hilo.

Jahazi la timu ya Babi, UiTM lazama Malaysia

JAHAZI la timu ya UiTM ya Malaysia anayoichezea kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Kassim 'Babi'juzi lilizamishwa baada ya kucharazwa mabao 4-0 na timu ya DRB-Hicom katika mfululizo wa Ligi Kuu ya nchi hiyo.
Kipigo hichio kilichopatikana kwenye uwanja wa ugenini wa Hang Jebat, mjini Melaka imeifanya UiTM ambayo ilianza kuonyesha matumaini kwa kupata ushindi ushindi na sare mfululizo kiasi cha kuchupa toka nafasi za mkiani hadi nafasi ya 8 kusaliwa na pointi zao 20 baada ya mechi 19.
Timu hiyo itashuka dimbani kesho kujaribu bahati yao mbele ya timu kali ya PBAPP katika mfululizo wa ligi hiyo inayoelekea ukingoni kwa sasa.
Babi alisema walizidiwa mchezao na wapinzani wao na wanajipanga kwa mechi ya kesho nyumbani ili kuibuka na ushindi na kusogea nafasi za juu.