STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, May 24, 2013

Baada ya kung'ara Gor Mahia, Ivo Mapunda awindwa na Tusker

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgcOsm-7zdR8dd1_VaKXsG_pBGttOec_6nguW8rxdX0f25fGFel_h1i8t__5lKCqSGd3tP8YSGwX1MS8JUGnUEQ-6eDQgXlYYQaO-VxDlPnOlnnAqByjy6zuTcYxXENkjTNjtlTc7tBatOJ/s400/IVO-MAPUNDA.jpg
Ivo Mapunda
KIPA nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ivo Mapunda anayeidakia Gor Mahia ya Kenya, amesema yupo katika harakati ya kuhamia kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Kenya, Tusker.
Hata hivyo kipa huyo aliyewahi kuichezea Bandari-Kenya kabla ya kutua Gor Mahia, alisema anasubiri kwanza kumalizika kwa mkataba wake mwishoni mwa mwaka huu kuamua hatma yake.
Alisema kocha wa Tusker, Robert Matano alimpigia simu mara baada ya kung'ara katika pambano la marudiano la Nusu Fainali ya 8 Bora ili kujua mkataba wake ukoje kabla ya kumvuta Tusker.
Mapunda aliyechaguliwa Mchezaji Bora wa pambano hilo lililoisha kwa suluhu ya kutofungana, lakini Tusker ikisonga mbele kwa ushindi wa bao 1-0 iliyopata katika mechi ya awali, alisema iwapo Tusker itamvutia kimasilahi atahamia kwa mabingwa hao wa ligi.
"Nitaangalia masilahi kwanza kama jamaa nibaki Gor Mahia au kujiunga na Tusker, ila nasubiri kwamba mkataba wangu na klabu yangu ya sasa uishe Desemba mwaka huu," alisema Mapunda.
Kuhusu mafanikio anayoyapata akiwa Kenya, kipa huyo aliyewahi kuidakia Prisons Mbeya na St George ya Ethiopia alisema yanamfariji mno baada ya kupuuzwa nyumbani akionekana kaisha.
"Nafurahia mno kupata mafanikio ugenini na kuthaminika naamini Mungu ataendelea kunisaidia zaidi na kutamba," alisema.
Mapunda ambaye amekuwa chaguo la kwanza katika kikosi cha Gor Mahia anatarajiwa kuiongoza timu yake Jumapili ikiwa ugenini katika mji wa Mumias dhidi ya Western Stima katika mechi ya Ligi.

HATIMAYE HARUNA NIYONZIMA ASAINI MIAKA MIWILI YANGA SC


Uongozi wa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Vodacom  klabu ya Young Africans leo umekata mzizi wa fitina kwa kiungo mchezeshaji kutoka nchini Rwanda Haruna Niyonzima kuendelea kuitumikia timu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili kufuatia kumalizika kwa mkataba wake awali.
Akiongea na waandishi wa habari makao ya klabu ya Yanga, katibu mkuu Lawrence Mwalusako amesema wameamua kumuongezea mkataba mchezaji huyo kufuatia kuuhitaji mchango wake kwani katika kipindi chake cha miaka miwili ameonyesha kiwango cha hali ya juu na kutoa mchango mkubwa.
 Mwalusako amesema kumekua yakiongelewa mengi juu ya mchezaji wetu Niyonzima, baadhi ya vyombo vya habari vimekua vikitoa taarifa za kupotosha juu yake ukweli leo umedhihirika kwamba Niyonzima ni mchezaji wa Yanga na ataendelea kuitumikia kwa miaka miwili.
Haruna Niyonzima alijiunga na Yanga kwa mara ya kwanza Julai 2011 akitokea katika timu ya APR nchini Rwanda ambapo katika miaka yake miwili aliyoichezea timu ya Yanga amefanikiwa kuisadia kupata makombe mawili ya ubingwa wa Ligi Kuu 2012-2013 na Kombe la Kagame 2011-2012.
Naye Niyonzima amesema anawashukuru wanachama, washabiki na wapenzi wa klabu ya Yanga kwa kuwa naye muda wote, Yanga ni nyumbani kwangu kwani najisikia furaha kuichezea timu hii na malengo yangu ni kuisadia ili iweze kufanya vizuri katika upatashindano ya kimataifa.
Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya klabu ya Yanga Abdallah BinKleb amesema palikua na propaganda nyingi juu ya Niyonzima, lakini ukweli ndio huu Niyonzima ataendelea kuitumikia klabu ya Yanga kwa miaka miwili.
"Tunautambua mchango wake alioutoa kwa miaka mwili kwani ameweza kutupatia vikombe viwili vya Ligi Kuu ya Vodacom na Kombe la Kagame hivyo tumemuongezea mkataba wa miaka miwili tena ili aendelee kutoa mchango wake na kuisadia timu katika michezo ya kimataifa" alisema BinKleb.

Credit:Global Publishers

Banana Zorro, Khadija Kopa kupamba Miss Ukonga kesho

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhWIQs31cc1ObyFSwZFkTslMrCrqe8JOHfVCu5nkNNQIMV-QitnF79eyi9AgiPQKx9mq3a7k7lemiNEE0Y6epiRyqHRbVYnrCXUJvSOY0_6ingI_jceO6O3ekt0BiFPfLJBng9Pq07XD6o/s400/IMGP0489.JPG
Banana Zorro na mmoja wa waimbaji wake wa B-Band wakitumbuiza

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhOH8NqF9z-_bsGqNP4n7EmBzCzeCozBhgE-FpTw7JPWKIK3AMrIKZOl0OcZt7XFra7Cgs0XElATkb75G19PbU0rCcdIdYf0Jb2yiqhyphenhyphenPJ38iRmtyFJ8YyEVicrcy3cSiVPESCxSnCSigU/s1600/kopa.jpg
Khadija Kopa
WASANII nyota nchini Banana Zorro na bendi yake ya B-Band pamoja na Malkia wa Mipasho, Khadija Kopa kesho wanatarajiwa kuwasinidikiza warembo 17 watakaochuana kuwania taji la urembo la Redd's Miss Ukonga 2013, litakalofanyika jijini Dar es Salaam.
Warembo hao watachuana kwenye shindano litakalofanyika kwenye ukumbi wa Wenge Garden na kusindikizwa na burudani ya wasanii hao wanaotamba nchini na nyimbo mbalimbali.
Mratibu wa shindano hilo, Rashid Kazumba aliiambia MICHARAZO kuwa jumla ya warembo 17 watachuana kuwania taji hilo sambamba na kuwania nafasi ya kuwania ushiriki wa shindano la Miss Ilala litakalofanyika baadaye.
Kazumba alisema maandalizi kwa ujumla kwa ajili ya kinyang'anyiro hicho yamekamilika na kwamba inasubiriwa tu kuona nani atakayeibuka kidedea usiku wa kesho.
Aliwataja baadhi ya warembo watakaochuana katika shindano hilo lililodhaminiwa na makampuni kadhaa nchini ni pamoja na Glory Jigge, Happiness Jackson, Flosek Mwakanyamale, Annatolia Raphael, Musnat Hassan, Gift Swai, Natasha Mohamed, Vanessa Magule, Queen John, Martha Gewe, Nancy Obasi, Mwanamkasi Bakari na Diana Joachim.



Klabu za Ligi Kuu kupigwa msasa kuhusu usajili wa TMS




Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeandaa semina ya usajili kwa njia ya mtandao (Transfer Matching System-TMS) kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom kwa ajili ya msimu wa 2013/2014.

Semina hiyo itafanyika Jumamosi (Mei 25 mwaka huu) kwenye ofisi za TFF saa 3 kamili asubuhi ikishirikisha watu wawili kutoka kila klabu ambao ni TMS Manager, na ofisa mwingine wa klabu.

Klabu za ligi hiyo zinazotakiwa kuhudhuria semina ya usajili ni Ashanti United, Azam, Coastal Union, JKT Ruvu, Kagera Sugar, Mbeya City, Mgambo Shooting, Mtibwa Sugar, Oljoro JKT, Rhino Rangers, Ruvu Shooting, Simba, Tanzania Prisons na Yanga.

Semina hiyo huenda ikazisaidia klabu za ligi hiyo ambao mara kadhaa wamekuwa wakiingia mkenge katika zoezi la usajili wa wachezaji kutokana na mfumo huo mpya kuwakanganya kama ilivyojitokeza msimu huu ulioisha katika usajili wa mchezaji Mbuyi Twitte aliyegombewa Simba na Yanga.

Banka kuitema Bandari-Kenya, huenda akarejea nyumbani au....!


Banka (kushoto) akiwa na wachezaji wenzake wa Kitanzania wanaocheza wote Bandari-Kenya
KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania anayecheza soka la kulipwa nchini Kenya, Mohammed Banka amesema hafikirii kuongeza mkataba mpya na timu yake ya Bandari Kenya bila kueleza sababu.
Banka, alisema kuna mambo mawili kichwani mwake baada ya kuisha kwa mkataba wake na klabu hiyo yenye maskani yake Mombasa, ama arejee nyumbani au kujiunga na timu nyingine.
Kiungo huyo alisema mkataba wake unatarajiwa kuisha miezi miezi mwili ijayo na hivyo hajaamua kuongeza mkataba mpya zaidi ya kutaka kuondoka klabuni hapo.
"Tunamalizia duru la kwanza Jumapili kwa kuumana na Sofapaka na mimi ndiyo namalizia mkataba wangu na sifikirii kuongeza tena zaidi ya kurudi nyumbani au kusonga mbele," alisema Banka.
Mchezaji huyo aliyekuwa miongoni mwa walioipandisha Ligi Kuu timu hiyo ambayo kwa sasa ipo nafasi ya sita kwenye msimamo wa timu 16, alisema haoni sababu ya kubaki Bandari bila kufafanua.
Hata hivyo hivi karibuni mchezaji huyo alidokeza kuna mambo hayapo sawa hasa suala la masilahi tofauti na makubaliano yaliyokuwepo kati yake na uongozi wa timu hiyo ilipopanda daraja.


TFF yasisitiza wenyeviti wa FA ndio wasimamizi wa RCL




Na Boniface Wambura
WAKATI mechi za kwanza za raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) zinachezwa wikiendi hii, Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesisitiza kuwa wasimamizi wa mechi za ligi hiyo ni wenyeviti wa mikoa wa vyama vya mpira wa miguu.

Kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Ramadhan Nassib ilikutana jana (Mei 23 mwaka huu) kupitia ripoti za makamishna kwa mechi za raundi ya kwanza ya RCL iliyomalizika wikiendi ya Mei 18 na 19 mwaka huu.

Kuhusu viwanja vinavyotumika kwa ligi hiyo, Kamati imesema vitaendelea kuwa vile vya makao makuu ya mikoa, na kwa vile vilivyokuwa vimeombwa vifanyiwe marekebisho ili viweze kukaguliwa kwa ajili ya RCL msimu ujao. Pia imeitaka mikoa kuendelea kuboresha viwanja vinavyotumika sasa, lakini vina upungufu.

Vilevile Kamati imebaini kuwa zimekuwepo pingamizi kuhusu usajili wa wachezaji ambapo imesema haiwezi kujadili pingamizi hizo kwa vile mikoa yote haikuwasilisha usajili wa wachezaji wa klabu husika uliofanyika mikoani kama ilivyoagizwa na kuelekezwa na TFF.

Hata hivyo, Kamati imeitaka mikoa ambayo klabu zao zimefanikiwa kuingia raundi ya pili kuwasilisha usajili huo haraka.

Pia Kamati imebaini kuwa zipo baadhi ya klabu ambazo zimekata rufani kuhusu usajili wa baadhi ya wachezaji, na kusisitiza kilichowasilishwa ni pingamizi kwa vile kwa mujibu wa kanuni masuala ya uwanjani hayakatiwi rufani. Hivyo, Kamati imeshauri klabu zilizokata rufani zilirejeshewe ada zilizolipa kwa ajili hiyo.

Makamishna na waamuzi wanaosimamia mechi za RCL wamekumbushwa kuwa ili mchezaji aruhusiwe kucheza mechi ni lazima awe na leseni yake (kadi ya usajili), vinginevyo asiruhusiwe kucheza mechi husika.

Mechi za RCL zinaendelea wikiendi hii ambapo zote zitachezwa Jumapili (Mei 26 mwaka huu) isipokuwa mechi kati ya Friends Rangers ya Dar es Salaam na African Sports ya Tanga itakayochezwa Jumamosi (Mei 25 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi.

Nayo mechi kati ya Abajalo ya Dar es Salaam na Kariakoo ya Lindi iliyokuwa ichezwe Jumamosi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam sasa itachezwa Jumapili kwa vile siku hiyo uwanja huo utatumika kwa mazoezi ya Taifa Stars.

Mechi nyingine za RCL zitakazochezwa Mei 26 mwaka huu ni Machava FC ya Kilimanjaro dhidi ya Mpwapwa Stars ya Dodoma kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, Stand United FC ya Shinyanga itakuwa mgeni wa Magic Pressure ya Singida kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.

Polisi Jamii ya Bunda mkoani Mara na Biharamulo FC ya Kagera zitaumana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma. Mjini Kigoma kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika ni kati ya wenyeji Saigon FC na Katavi Warriors ya Katavi.

Nayo Kimondo SC ya Mbeya itakuwa mgeni wa Njombe Mji ya Njombe katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe. Mechi za marudiano zitachezwa kati ya Juni 1 na 2 mwaka huu.

Timu zitakazofuzu kucheza raundi ya tatu zitacheza mechi za kwanza kati ya Juni 8 na 9 mwaka huu wakati mechi za marudiano zitakuwa kati ya Juni 15 na 16 mwaka huu.

Sasa ruksa kwa Dk Slaa kuoana na mchumba wake Josephine Mushumbuzi

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhraC9iZRYXVNVm9NqNkpaKtt00FJUrgjJ20tjW7uw8VZAV2l2xCsa2DxseokFhXxi8XHjbYkrN-G5Eg6GQDuB3gFAvn1GOFpzsh9m1YKJAyhTzhVERBpIPmei-IZLLqnakhleRVhkl1XA/s640/dkt+slaa.jpg
Dk Slaa (kulia) na mchumba wake, Josephine Mushumbuzi


HATIMAYE Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, imetupilia mbali rufaa iliyokuwa imekatwa na aliyekuwa mume wa Josephine Mshumbusi, ambaye ni mchumba wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Wilbroad Slaa, Mahimbo baada ya kuiona rufaa hiyo haina msingi wowote kisheria.



Hukumu hiyo ya rufaa ya  madai ya ndoa Na.32/2012 ilitolewa jana na Hakimu Aniseth Wambura ambapo alisema mahakama yake imefikia uamuzi huo wa kuitupa rufaa hiyo kwasababu haina mantiki ya kisheria.



Hakimu Wambura alisema mahakama yake imekubalina na hukumu iliyotolewa Aprili 2012 na Mahakama ya Mwanzo Sinza katika kesi ya madai talaka iliyokuwa imefunguliwa na Mshumbusi anayetetewa na wakili wa kujitegemea Philemon Mutakyamilwa  dhidi ya Maimbo ambapo mahakama hiyo ya chini ilitangaza kuwa hakukuwa na ndoa baina ya watu hao kwasababu Maimbo alikuwa ni mzinzi, simwaminifu katika ndoa yake na alikuwa akimtesa mkewe.



“Baada ya mahakama yangu kusikiliza hoja za mwomba rufaa na mjibu rufaa ,mahakama hii imefikia uamuzi wa kukubali hoja za Mshumbisi kuwa kwa tabia ile ya mbaya ya uzinzi na ukosefu wa uaminifu katika ndoa yake hapakuwepo na ndoa baina yao hivyo mahakama yake inatangaza kuwa hukumu ya mahakama ya Mwanzo Sinza ambayo iliivunja ndoa hiyo ilikuwa hukumu sahihi “alisema hakimu Wambura.



Akizungumza na mwandishi wa habari hizi baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo wakili Mutakyamilwa alisema amefurahishwa na hukumu hiyo kwani mahakama imetenda haki  kwasababu kesi hiyo ya madai ya talaka ilikuwa na msukumo wa siasa chafu zilizokuwa na lengo chafu la kumchafulia jina mteja wake(Mshumbusi) ambaye kwa sasa ni mzazi mwenzie Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.Wilbroad Slaa.
Kutokana na hali ni wzi kwamba Dk Slaa sasa wanaweza kuoana na mpenzi wake huyo waliyezaa naye mtoto mmoja.

Chegge, Mhe Temba wanaswa na Maringo 7


Mhe Temba na Chegge

Maringo Saba katika pozi
MCHEKESHAJI anayetamba kwenye kipindi cha Mizengwe, Rashid Costa 'Maringo 7' amewajumuisha wakali wa muziki wa kizazi kipya nchini, Said Chegge, Mheshimiwa Temba na 'bosi' wao Saidi Fella kwenye filamu yake anayotarajia kuitoa hivi karibuni.
Maringo 7 aliyewahi kutamba na michezo ya kuigiza ya kwenye runinga akiwa na kundi la Shirikisho Msanii Afrika, alisema filamu hiyo itafahamika kwa jina la 'Papaa' na atawashirikisha wakali hao na nyota wengine wa filamu nchini.
"Nipo katika maandalizi ya mwisho ya kukamilisha filamu yangu mpya itakayoitwa 'Papaa' ambayo mbali na kucheza mimi na nyota wengine wa filamu, pia ndani mwake kutakuwa na Said Fella, Mhe. Temba, Said Chegge na YP," alisema Maringo 7.
Maringo 7, alisema ana imani kazi hiyo itathibitisha kipaji alichonacho katika sanaa ya uigizaji na muziki, fani anazozifanya kwa wakati mmoja kwa sasa.

Salha, Hammer Q watoa albamu ya Mke na Mume

Salha Abdallah na mumewe Hammer Q
MUIMBAJI nyota wa taarab wa kundi la Dar Modern, Salha Abdallah akishirikiana na mumewe Husseni Mohammed 'Hammer Q' wamekamilisha kurekodi nyimbo tatu mpya kwa ajili ya kutoa albamu yao.
Akizungumza na MICHARAZO, Salha ambaye 'amelitosa' kundi la Five Star lililokuwa limetangaza kumnyakua hivi karibuni, alisema nyimbo mbili kati ya hizo zipo katika miondoko ya taarab na wimbo mwingine upo katika mahadhi ya mchiriku.
Salha aliyeripotiwa kupewa kipigo kikali na mumewe huyo kiasi cha kulazwa hospitalini kabla ya kusameheana, alizitaja nyimbo hizo tatu kati ya nne walizopanga kuwamo katika albamu hiyo kuwa  ni 'Tunaoana', 'Safiri Salama' na 'Nisamehe Tusonge Mbele'.
"Wimbo wa 'Nisamehe Tusonge Mbele' upo katika mahadhi ya Mchiriku na nyingine zipo katika miondoko ya taarab na kibao cha mwisho ambacho tutakirekodi baadaye ni ule wa 'Subhana Heri'," alisema Salha.
Muimbaji huyo aliyeingia kwenye fani hiyo mwaka 2008 kwa kuvutiwa na sauti tamu ya marehemu Mariam Khamis, alisema wameanza kutoa albamu hiyo lakini mipango yao ya baadaye kuja kuanzisha kundi lao ili kuepuka kuwatumikia watu.
"Tuna mipango ya kuja kuanzisha kundi letu wenyewe baada ya kufanya kazi kwa watu kwa kipindi kirefu bila ya kupata mafanikio yoyote ya maana," alisema Salha

TP Mazembe yamnyakua kocha wa Mali


https://lh6.googleusercontent.com/-VEtRhDY7qrI/UZzx8PeR2fI/AAAAAAAAlAE/izjc83pUpI8/patrice-carteron-dijon5.jpg?imgmax=800
Kocha Patrice Carteron

LUBUMBASHI, Congo DR
KAMPENI za Mali za kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zilipaa juzi Jumatano wakati kocha wao Patrice Carteron  aliposaini mkataba wa miaka miwili na klabu ya TP Mazembe ya Congo.
Mali, ambayo chini ya kocha huyo Mfaransa ilimaliza ya tatu katika fainali ya Mataifa ya Afrika nchini Afrika Kusini, ina mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Rwanda na Benin Juni 9 na Juni 16.
"Tunamtambua Patrice Carteron kama kocha wa Mali," rais wa shirikisho la soka la nchi hiyo Hamadoun Kola Cisse alisema katika mahojiano na kituo cha radio cha Ufaransa.
"Yuko katika mkataba hadi mwakani lakini kwa kwenda kusaini mkataba mwingine anajiweka matatani," Cisse alisema.
Katika muda huo huo wa mahojiano, beki wa zamani wa klabu za St Etienne na Sunderland, Carteron (42) alikuwa alikuwa akitambulishwa hadharani kwenye Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi.
"Hatuna pingamizi kwa Carteron kuiongoza Mali katika mechi zao mbili zijazo Juni licha ya kusaini mkataba nasi," mwenyekiti Moise Katumbi alisema.

JK awatia moyo Stars kwa Morocco

Rais Jakaya Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Taifa Stars jana Ikulu

Wachezaji wa Stars wakijifua kwa mazoezi

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, amewaambia wachezaji wa timu ya taifa ya soka (Taifa stars) kwamba wanaweza kuwafunga tena Morocco katika mechi yao ya marudiano ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014 mjini Marrakech kama walivyowafunga jijini Dar es Salaam katika mechi yao ya awali.
Stars watarudiana na Morocco Juni 7 katika mechi yao ya nne ya hatua ya makundi baada ya kuwashushia kipigo kilichoishangaza "dunia ya soka" cha magoli 3-1 katika katika mechi yao ya awali jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na timu hiyo wakati alipoialika Ikulu kwa ajili ya mlo wa mchana jana, Rais Kikwete alisema: "Maadamu mliwashinda mara ya kwanza, hakikisheni mnawashinda tena kwa kuwa mkishinda tunafurahi sana na mkishindwa tunanyong’onyea sana."
Rais Kikwete aliiambia timu hiyo kuwa uwezo waliouonesha katika mechi ya kwanza ya kuwania kufuzu kwa fainali hizo dhidi ya Gambia ambayo walishinda 2-0, na kisha kuisambaratisha Morocco 3-1, zinathibitisha uwezo mkubwa walionao Watanzania katika mchezo huo na kwamba cha muhimu ni kujiamini.
Aidha, amempongeza kocha wa timu hiyo Kim Poulsen pamoja na Kamati ya Ushindi ya Taifa stars kwa kuisaidia timu hiyo kwa hali na mali ili iweze kushinda na hatimaye iweze kufuzu kwa mara ya kwanza katika historia kucheza fanali za Kombe la Dunia. Stars itahitaji kucheza mechi tano kishujaa ili kwenda Brazil 2014.
Naye Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenella Mukangara alisema serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa michezo nchini ili kupambana na changamoto zinazoikabili timu hiyo ili kuiwezesha kufanya vizuri.
Kwa upande wake kocha Poulsen alimshukuru Rais Kikwete kwa kuwakaribisha na kuwatia moyo ambapo aliahidi kuifundisha vizuri timu hiyo ili kuhakikisha kuwa wanafanya makubwa.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, nahodha wa  timu hiyo, Juma Kaseja alimshukuru Rais Kikwete na kuahidi kuhamasishana kujituma kwenye mazoezi na hatimaye kutimiza ndoto za Watanzania.
Taifa Stars iko Kundi C la kufuzu kwa Kombe la Dunia 2014, ikiwa na pointi 6, moja nyuma ya vinara, Ivory Coast. Morocco ni ya tatu kwenye msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi mbili na Gambia inaburuta mkia ikiwa na pointi moja.

Yanga kujipima kwa Rayon kabla ya kwenda Darfur kutetea Kagame


Kikosi cha Yanga
MABINGWA watetezi wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Yanga wanatarajia kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Rwanda, Rayon kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza mwezi ujao.
Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako, alisema kuwa wamepokea barua ya mwaliko huo kutoka kwa mratibu wa mechi hiyo lakini bado hawajathibitisha hadi kocha Mholanzi Ernie Brandts atakapotoa maelekezo.
Mwalusako alisema kwamba mechi hiyo wakiipata itakuwa ni nzuri kwa kuwaandaa wachezaji kuelekea Sudan na vile vile ni nafasi kwa Yanga kuwapa heshima mashabiki wake wa kanda ya ziwa kuiona timu baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara.
"Ni kweli taarifa za mechi hiyo tunayo, lakini majibu rasmi hatutawapa na siku ya mchezo pia haijapangwa ila wamependekeza iwe mapema mwezi ujao," alisema Mwalusako.
Naye mmoja wa viongozi wa Rayon, Clever Kazungu, alithibitisha timu yake kupokea mwaliko huo na kusema kwamba wako tayari kuja nchini endapo watafikia makubaliano na waandaaji wa mchezo.
Kazungu alisema tayari wameambiwa kuwa watalipiwa gharama ya malazi, chakula na posho ya wachezaji kwa siku watakazokuwa hapa nchini.
Yanga itaanza kampeni za kutetea ubingwa wa Kombe la Kagame kwa kuivaa Express ya Uganda katika mechi ya kundi C itakayofanyika Juni 20 kwenye Uwanja wa Elfasher saa nane mchana wakati Simba iliyopangwa kundi A itashuka dimbani siku inayofuata kuivaa El Mereikh.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Bara watashuka tena dimbani Juni 22 mwaka huu kuikabili Ports na watakamilisha mechi za hatua ya makundi Juni 25 kwa kuvaana na Vital'O.
Simba watashuka tena kusaka ubingwa wa michuano hiyo Juni 23 kwa kupambana na APR na watamaliza dhidi ya Elman Juni 26.
Yanga pia huenda ikawavaa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Zanzibar, KMKM, katika mechi nyingine ya kirafiki inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Thursday, May 23, 2013

Shinji Kagawa aipa taji Borussia Dortmund

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEg6qnMGGtEdfljwGsrw8rCwj7Az3DybB28VZLR1sfi1mmYGfENc0OAMvIk91kA-UOfpfSkxBVypEs7biZVLGjf9QjGPv1VGFTXYprResinbb3klLzzYOUfYrXyXIVyyW2YP87McxG1lYi4/s1600/Shinji+Kagawa+wallpapers.jpeg
Shinji Kagawa katika uzi wa Manchester United

 

http://ballsybanter.com/wp-content/uploads/2012/06/Cologne-v-Borussia-Dortmund-Shinji-Kagawa-cel_2739644.jpg
Shinji Kagawa alipokuwa akiichezea Borussia Dortmund

 

KIUNGO wa kijapani anayeichezea Manchester United, Shinji Kagawa ametoa turufu yake kwa klabu yake ya zamani Borussia Dortmund kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya katika fainali itakayochezwa Jumamosi nchini Uingereza.

Kagawa aliyetua Manchester United msimu uliopita akitokea Dortmund kwa dau la Pauni Milioni 12, alisema anadhani Borussia wataifunga Bayern Munich kwenye fainali za michuano hiyo itakayochezwa katika uwanja wa Wembley.

Pia mchezaji huyo alisema mafanikio iliyopata Dortmund msimu huu kwenye michuano hiyo ya Ulaya licha ya kupoteza ubingwa wa ligi ya Ujerumani, itawachochea Man Utd kufanya vyema kwa msimu ujao wa Ligi hiyo ya Mabingwa Ulaya.

Pamoja na kupoteza taji la nyumbani Dortmund wamekuwa na mafanikio makubwa katika michuano hiyo ya Ulaya licha ya wali kutopewa nafasi kubwa kama klabu nyingine zilizong'olewa au kama ilivyo kwa mahasimu wao Bayern Munich.

Kagawa aliyecheza kwa mafanikio makubwa katika klabu hiyo ya Ujerumani, alisema Dortmund inacheza kwa kujituma na ina wachezaji ambao wanajua wajibu wao uwanjani, licha ya kuimwagia sifa pia Bayern akidai ni timu kubwa na yenye bahati katika soka.

Rio Ferdinand asaini mkataba mpya Man Utd



BEKI mahiri wa Manchester United, Rio Ferdinand amesaini mkataba mpya wa kuendelea kuichezea klabu hiyo na kuzima tetesi kwamba huenda angeachana na klabu hiyo.
Rio mwenye umri wa miaka 34 alinukuliwa akisema kuwa anapenda kuendelea kuichezea timu hiyo na ndiyo maana amesaini mkataba huo mpya wa mwaka mmoja.
"Nimesaini mkataba mpya wa mwaka mmoja," alisema.
Alihoji ni mchezaji gani ambaye asingependa kucheza kwenye klabu kubwa kama Manichester ambayo kila wikiendi zaidi ya watazamaji 74,000 wanakuwepo uwanjani kumshangilia.
Beki huyo aliteua Old Trafford mwaka 2002 akitokea Leeds kwa mkataba uliovunja rekodi wa Pauni Mil 30 na kwa kipindi chote ametwaa mataji 14 tofauti akiwa na kikosi hicho ambacho kinampoteza kocha wake kipenzi na aliyeiweka kwenye kilele cha mafanikio, Sir Alex Ferguson aliyetangaza kustaafu hivi karibuni.

Hali bado tete Mtwara, wananchi wasakwa nyumba kwa nyumba


Mwandishi wetu aliyepo Mtwara ametueleza kuwa hivi sasa baadhi ya wananchi wa eneo la Magomeni mkoani mtwara wamekimbilia katika Hospitali ya Mkoa wa Mtwara Lugula wakihofia usalama wao kutokana na vurugu za kuchomwa kwa nyumba zao pamoja na vibanda vya biashara zilizotokea leo asubuhi katika eneo hilo.

Maduka maeneo ya Magomeni yamechomwa moto ikiwamo pia mali za Askari Magereza . Mwanafunzi wa CHUNO amefikishwa hospitali Ligula na majeraha ya risasi mguuni.  
Mwanamke mwingine anayekadiriwa kuwa na miaka 25 mjamzito ameuawa kwa kupigwa risasi maiti ipo Ligula.




Kwa sasa ( jioni  hii) inaelezwa kuwa katika baadhi ya mitaa hali imetulia na ni idadi ndogo ya wananchi ndiyo inayoonekana wakitembea mitaani isipokuwa eneo la Magomeni ambako mabomu yanaendelea kusikika huku huduma za kijamii katika mji huo zikiwa zimesimama zikiwemo usafiri, huduma za kibenki na shule
Credit:Mpekuzi Huru pia unaweza kuchungulia www.mtwarakumekucha.blogspot.com kwa updates za kinachoendelea Mtwara.

Yanga yatahadharishwa Kagame Cup

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEj-wNTiS0urUo8wOMFwqWJ0vzpBnDlo2yooX-52M-cZ5UN2JNHrVtVLvE9KyyG8N_z649s5etRc43ySwdL5fZJVU8TBWcKPLFKt3GK_S7QVhss2NUWcUH1s8wiZjlN8jn6zPGsIdMulOxo/s1600/Yanga+4.jpg
Mabingwa watetezi wa Kagame, Yanga wakishangilia taji lao la mwaka jana
MABINGWA watetezi wa michuano ya Kombe la Kagame, ambao pia ni mabingwa wapya wa soka nchini Tanzania, Yanga wametahadharishwa kufanya maandalizi ya kutosha iwapo wanataka kutetea taji la michuano hiyo ambaya kwa mwaka huu itafanyika nchini Sudan.
Yanga imepangwa kundi C pamoja na timu za Express ya Uganda, Vital'O ya Burundi na Port Djibout na itaanza kibarua chake siku mbili baada ya kuanza kwa michuano hiyo kwa kuumana na Express.
Kutokana na ugumu wa michuano hiyo itakayoanza Juni 18 hadi Julai 2, wanachama wa Yanga wameanza kutahadharisha mapema viongozi na wachezajiu wao kwamba wajiandae vyema kwa ajili ya kuzidi kuwapa raha katika ushiriki wao nchini Sudan.
Ramadhani Kampira, aliyewahi kuichezea timu hiyo na kuongoza Chama cha Soka wilaya ya Kinondoni (KIFA) alisema kwa kuiangalia michuano hiyo ya Sudan ni wazi itakuwa migumu, hivyo Yanga wanapaswa kujiandaa vyema na wachezaji kwenda 'kukaza' ili warejee Tanzania na taji.
Kampira alisema, yeye binafsi anaamini Yanga ina kikosi kuzuri kinachoweza kuwapoa raha, lakini bila kujipanga ni wazi inaweza kuwasononesha wanayanga ambao wanachekelea taji la 24 la Ligi Kuu Tanzania.
"Yanga wanapaswa kufanya maandalizi mazuri, tuna hamu ya kuona klabu yetu inatwaa taji kwa mara ya tatu mfululizo na kwa mara nyingine tena nje ya ardhi ya Tanzania baada ya mara mbili kunyakua Uganda," alisema.
Kampira, alisema tahadhari hiyo haipo kwa Yanga tu, bali hata kwa watani zao Simba ambao wana rekodi ya kunyakua taji hilo mara 6 pamoja na AFC Leopards ya Kenya kwa sababu nao ni wawakilishi wa Tanzania.
"Wawakilishi wetu wote wanapaswa kujipanga, wasitarajie mteremko Sudan, klabu zilizopo kwenye michuano hiyo siyo za kubeza nazo zinahitaji taji kama ambavyo Yanga na Simba zitakuwa zikilitamani,' alisema.
Jumla ya timu 13 zinatarajiwa kuchuana katika michuano hiyo ya kusaka Klabu Bingwa wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ambapo Simba wenyewe wamepangwa kundi A na timu za APR Rwanda, Elman ya Somalia na El Merreikh.
Kundi jingine la michuano hiyo ni lile la B lenye timu za Super Falcon ya Zanzibar, El Hilal na El Ahly Shandi za Sudan na Al Nasir Juba ya Sudan Kusini.

Majambazi wajeruhi na kupora Mil 40 Dar

 Pichani ndio matundu ya risasi zilivyorindima kwenye kioo cha dereva (risasi tatu) ,mara majambazi hayo kufanikiwa kumjeruhi dereva sehemu ya bega na kufanikiwa kunyakua begi linalosadikiwa kuwa,lilikuwa na kiasi cha fedha shilingi milioni 40 na kutokomea nazo.
Pichani kulia ni Askari Usalama barabarani akichukuliwa maelezo yake kutokana kushuhudia tukio la ujambazi lililofanyika maeneo ya Sayansi mataa-Kijitonyama jijini Dar mapema leo mnamo majira ya saa tano kasoro.
 
Ambapo kwa mujibu wa mashuhuda waliokuwepo eneo la tukio wanaeleza kuwa majambazi hao walikuwa wapatao wanne wakiwa wamepanda piki piki,ghafla wakasimama na kulizunguka gari aina Vitz yenye usajili wa namba T929 CCX (pichani chini) kwa haraka,mmoja wao akiwa na mashine gun na wengine walikuwa na bastola.
 
Mmoja wao alifyatua risasi hewani kumtaka dereva asimame na ashushe vioo vya gari yake,kufuatia hali ya utata wa majibishano ya muda mfupi majambazi hao waliifyatulia risasi kadhaa gari hiyo upande wa dereva, bahati mbaya wakamjeruhi sehemu ya bega,ndipo wakafanikiwa kuondoka na begi kubwa linalosadikiwa kuwa lilikuwa na kiasi cha fedha shilingi milioni 40 (kwa mujibu wa dereva aliempeleka majeruhi hospitali).

Mara baada ya majambazi hayo kutimka wasamalia wema wakamchukua dereva huyo aliyekuwa akigugumia kwa maumivu ya jeraha lake na kumtafutia tax na hatimae kumkimbiza hospitali ya Kairuki kwa huduma ya haraka.
 Baadhi ya watu wakijaribu kubadilshana mawazo kwa kulitafakari tukio hilo la ujambazi.
 Gari iliyokuwa imevamiwa na majambazi ikikokotwa na gari la polisi mara baada ya kushindwa kuwaka.

Polisi Moro waapa kurudi tena Ligi Kuu


Kikosi cha Polisi Moro. Rambow (wa kwanza kushoto mbele)

MSHAMBULIAJI nyota wa timu ya Polisi Moro, Mokili Rambow, amesema licha ya timu yao kushuka daraja, lakini wanaamini watacheza tena Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa 2014-2015.
Rambow, ambaye ni nahodha wa timu hiyo, alisema wamekubali matokeo kwa timu yao kushindwa kuhimili vishindo vya ligi hiyo waliokuwa wakiicheza kwa mara ya kwanza waliposhuka daraja msimu wa 2008-2009 akidai kuwa ilichangiwa na 'ushamba' wa ligi kabla ya kuzinduka duru la pili wakiwa wameshachelewa.
Akizungumza na MICHARAZO, Rambow alisema kushuka kwa timu yao ni pigo na jambo linalowaumiza karibu wadau wote wa klabu hiyo ikizingatiwa waliipigania kuirudisha ligi kuu kwa miaka kadhaa, hata hivyo hawana jinsi zaidi ya kujipanga upya ili kurudi katika ligi hiyo kwa msimu ujao.
Mchezaji huyo ambaye ameifungia mabao kadhaa timu hiyo akishirikiana na wachezaji wenzake, alisema Polisi kwa sasa wanafanya tahmini kabla ya kujiopanga kwa ligi Daraja la Kwanza msimu ujao ambapo aliapa kwamba ni lazima watarejea ligi ya msimu wa 2014-2015.
"Tunajipanga kwa ajili ya kurudi ligi kuu, tunajua ni kazi pevu lakini tutafanhya kila njia kurudi Ligi Kuu kwa kweli tumeumia mno kushuka tulipotoka," alisema Rambow.
Polisi Moro, imemaliza ligi ya msimu huu waliyoicheza baada ya kupanda toka daraja la kwanza, ikiwa na pointi 25 sawa na Toto Africans na kuungana na African Lyon waliotangulia mapema wakiwa na pointi 22 tu.
Katika duru la kwanza Polisi walitolewa nishai na kuambulia pointi nne tu ikiwa na kocha wao maarufu, John Simkoko kabla ya kuachana naye na kumpa jukumu hilo nyota wa zamani wa Yanga, Pan African na Taifa Stars, Mohammed Rishard 'Adolph' aliyeipa jumla ya pointi 21, lakini hazikuwasaidia kuwaokoa wasishuke.

Bunge laahirishwa tena, kisa sakata la Mtwara

http://dewjiblog.com/wp-content/uploads/2013/02/8517823001.jpg
Spika wa Bunge, Mhe. Anna Makinda
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Anna Makinda ameliahirisha tena bunge leo asubuhi ili kupisha kamati ya uongozi ya Bunge iendelee kukutana ili kutoa maamuzi na tamko kuhusu vurugu za Mtwara.
Bunge hilo jana pia liliahirishwa kutokana na sakata hilo ambalo lilijitokeza mapema jana na kusababisha mtu mmoja kufariki dunia na uharibifu mbalimbali kutokea ikiwemo kuchomwa moto nyumba za viongozi wa serikali,chama cha mapinduzi na nyumba ya mwandishi wa habari wa TBC.
Pia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini umesimamishwa kwa muda mpaka ufumbuzi wa tatizo la vurugu hizo utakapopatiwa suluhisho.

Kesho bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya Afrika Mashariki itajadiliwa.
 

Wanachuo Mwl Nyerere kutembelea yatima

UMOJA wa Wanafunzi Wanachama wa Umoja wa Mataifa Tawi la Mwalimu Nyerere (UNC MNMA) unatarajia kuwatembelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwenye kituo cha New Hope Familiy kilichopo Ungindoni Maweni, Kigamboni Jijini Dar es Salaam siku ya Jumapili ikiwa ni sehemu ya kuwaaga wanafunzi wanaomaliza chuo hicho hivi karibuni.
Hayo yamebainishwa na Katibu aliyemaliza muda wake hivi karibuni Selemani Msuya wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii jijini Dar es Salaam.
Alisema wanachama wa UNC wanaomaliza na wale ambao wanaendelea walikubaliana kwa pamoja juu ya kuwatembelea watoto hao ikiwa ni moja ya malengo yao kushirikiana na jamii iliyokaribu na chuo chao.
Msuya alisema moja ya malengo ya vijana wanachama katika umoja wao wao ni kuhakikisha kuwa wanashirikiana na jamii iliyokaribu nao ikiwa ni kwakushiriki moja kwa moja katika shughuli mbali mbali pamoja na kutoa msaada.
“Sisi vijana wanachama wa UNC kupitia chuo cha Mwalimu Nyerere tumeamua kufanya mahafali ya kuwaaga wenzetu kwa kushiriki chakula  cha mchana na watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwani tunaamini kuwa  tutakuwa tumefanya jambo nzuri kwetu na kwa watoto hao,” alisema
Katibu huyo aliyemaliza muda wake ambaye kwa sasa ni mjumbe wa kamati ya utendaji alisema katika ziara hiyo wanatarajia kushiriki chakula cha mchana, kutoa msaada wa vifaa vya shule na kusomea pamoja na kucheza pamoja.
Alisema wana UNC wamejitolea kuchangia kiasi kidogo kulingana na uwezo wao ili kuhakikisha kuwa wanafanya sherehe hiyo ya kuwaagana kwa kushirikiana na watoto ambao wanaishi katika mazingira magumu.
Msuya huyo alisema tukio lingine ambalo litafanyika katika mahafali hayo ni kwa watoto hao ambao wanaishi katika mazingira magumu kuwapatia vyeti wahitimu ambao wanamaliza chuo hivi karibuni.
Katibu huyo ambaye amemaliza muda wake amewataka watu mbalimbali ambao wanatambua changamoto zinazowakabili watoto ambao wanaishi katika mazingira magumu kutoa misaada yao ili waweze kuunganisha na hicho kidogo walichonacho kuwapatia watoto hao.

Sheha amwagiwa tindikali Zanzibar

 
Sheha aliyemwagiwa tindikali na watu wasiojulikana akiwa hospitalini alipolazwa kwa matibabu
SHEHA wa eneo la Tumondo, visiwani Zanzibar, Mohamed Omary Said, amemwagiwa tindikali na mtu asiyejulikana na hivyo kupata maumivu makali sehemu yake ya kifua na jicho kuumia pia.

Sheha huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Mnazi mmoja mjini Unguja ambapo alipatiwa matibabu ya dharura.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mukhadam Khamis, amesema chombo kilichotumika kumwagia tindikali Sheha huyo kilipatikana eneo la tukio na kwamba polisi imekichukua kwa kukichunguza kitaalam ili kugundua aliyekuwa akikitumia kwa kuangalia alama za vidole.

Sheha huyo alimwagiwa tindikali jana usiku wakati alipotoka nje ya nyumba yake kuchota maji na ndipo mhalifu huyo alipomwagia tindikali na kwamba hakuweza kumtambua.
Miezi michache iliyopita Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga naye alimwagiwa tindikali kabla ya imamu wa msikitini mjini humo kuuwawa kwa kukatwa mapanga sikui chachje baada ya matukio ya viongozi wa Kikristo kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

Wednesday, May 22, 2013

Wanajeshi wanne wafa Nachingwea wakienda Mtwara kutuliza ghasia


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgRZcHVZ3CvZsU4ZT-KF1Whe3ITc-0bHzMl3d37SUPMrVc13MZKx6Iyfu8r9S5f6pDFDQCE_88ubI9JuNojGoqUyfGvP_uPOAUTi0P2GDoMRS7hqdPbZejXJaJ4EuGl0SWFwOV1gPFuELQ/s400/3.JPG
Wanajeshi wakipokea mwili ya askari mwenzao. Picha hii haihusiani na habari hapo chini

WANAJESHI wanne wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) waliokuwa wakielekea Mtwara kusaidia kutuliza ghasia zinazoendelea mjini humo wamefariki dunia, huku wengine 20 wakijeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali wilayani Nachingwea mkoani Lindi.
Habari zilizopatikana hivi punde na kuthibitishwa na baadhi ya mashuhuda zinasema kuwa ajali hiyo ilihusisha lori la wanajeshi hao na gari nyingine imetokea eneo la Kilimani Hewa, kilomita mbili toka kambi ya Jeshi hilo ya 41KJ wilayani humo.
Taarifa hizo zinasema kuwa jumla ya wanajeshi 31 walikuwa kwenye msafara huo na kwamba 20 wamejeruhiwa na kukimbizwa hospitali ya wilaya hiyo, huku wengine saba wakitoka salama bila ya kuwa na majeruhi yoyote.
Inaelezwa kuwa mwendo kasi na kona kali iliyopo eneo la tukio ndiyo chanzo cha ajali hiyo, ingawa Polisi bado haijathibitisha taarifa hizo kuhusiana na vifo vya wanajeshi hao wanne walioelezwa wamefariki katika ajali hiyo.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Viginia Ole Swai, amenukuliwa na kituo cha Radio One Stereo akisema huenda vumbi nalo lilichangia kutokea kwa ajali hiyo baada ya gari hizo kugongana katika ajali hiyo ambayo imepoteza uhai wa wapiganaji hao wa JWTZ wanne na wengine kujeruhiwa ambapo wapo hospitali wakitibiwa.

Azam Marine kuleta meli nyingine kali zaidi


 Muonekano wa Kilimanjaro 4
KAMPUNI ya Azam Marine, inaleta boti mpya ya Kilimanjaro 4, ambayo inatarajiwa kuwasili nchini, kuanzia mwishoni wa mwezi huu, ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 700 na kutumia muda wa dakika 70 kwa safari moja ya kati ya Zanzibar na Dar es Salaam. Hii ni boti mpya kabisa katika muendelezo wa boti za Kilimanjaro, ambayo itakidhi mahitaji ya wasafiri wa eneo hili kwa kuwa inabeba sifa zote, ambazo ni Usalama, Kasi zaidi na Unadhifu. Kaa tayari kwa mzigo mpya kutoka Azam Marine.

Pellegrini athibitika kuondoka Malaga, milango i wazi kutua Man City

http://images.gazzetta.it/Media/Foto/2009/10/30/pelle_01.JPG
Kocha Manuel Pellegrini

MENEJA wa timu ya soka ya Malaga ya Hispania, Manuel Pellegrini amethibitisha kuwa ataondoka katika klabu hiyo mwishoni mwa msimu wa Ligi Kuu ya nchi hiyo.
Duru za michezo zinasema kuwa, Pellegrini atajiunga na Manchester City kuchukua nafasi ya kocha aliyetimuliwa katika timu hiyo, Muitaliano Roberto Mancini.
Kocha huyo alithibitisha mapema leo kwamba ataondoka katika benchi la ufundi la timu hiyo aliyokuwa akiinoa tangu mwaka 2010.
Akinukuliwa na mtandao wa Marca.com wa gazeti moja la nchini humo , kocha huyo alisema yeye na klabu hiyo wanaelekea kuachana, lakini umoja wao utaendelea kuwepo hata kama watatenganishwa na miji watakayokuwepo.
"Naondoka," alinukuliwa kocha huyo aliyoifikisha Malaga kwenye Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kutolewa na  Borussia Dortmund ambayo inatarajiwa kuvaana na wapinzani wao wa Ujerumani, Bayern Munich siku ya Jumamosi katika pambano la Fainali za mwaka huu.

Mkutano wa Tenga na wanahabari haupo tena kesho

 
Rais Tenga akiwa na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah
ULE mkutano kati ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga na Waandishi wa Habari uliokuwa ufanyike kesho (Mei 23 mwaka huu) umeahirishwa mpaka hapo mtakapoarifiwa tena.
Taarifa iliyotumwa na Msemaji wa TFF, Boniface Wambura imesomeka kwamba mkutano huo wa kesho haupo kama ulivyokuwa umepangwa bila kufafanuliwa kilichosababisha kufutwa ghafla.