STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, March 28, 2014

Ashanti, Oljoro nani kulia Chamazi, vita ipo J'pili

Oljoro JKT
Ashanti United
VIBONDE vya Ligi Kuu Tanzania Bara, Ashanti United na Oljoro JKT kesho zinatarajiwa kupepetana katika pambano pekee kwa siku ya Jumamosi, huku kila moja ikiwa inahitaji ushindi ili kufufua matumaini ya kuendelea kusalia kwenye ligi ya msimu ujao.
Timu hizo zinazofuata toka mkiani zikiwa juu ya Rhino Rangers inayoburuza mkia na pointi zake 13 zitaumana kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Ni ushindi pekee kwa kila timu utafufua matumaini ya kuendelea kucheza ligi ya msimu ujao, vinginevyo huenda wakajiweka pabaya zaidi kushuka daraja kama walivyo wenzao wa Rhino ambao watashuka dimbani  Jumapili dhidi ya JKT Ruvu.
Ashanti inayonolewa na kocha Abdallah Kibadeni ina pointi 18 ikiwa nafasi ya 12, huku wapinzani wao wakiwa chini yao na pointi 16 kila moja ikiwa imecheza mechi 22.
Kila timu inahitaji ushindi ikizingatiwa zimetoka kuchezea vichapo katika mechi zao zilizopita, Ashanti ikizamishwa mabao 2-0 na Ruvu Shooting na Oljoro ikizabuliwa na Azam.
Timu hizo zilizobadilisha makocha baada ya kuyumba kwenye duru la kwanza, zimekuwa kama homa ya vipindi kwa viwango vyao kupanda na kushuka kulingana na aina ya mechi.
Kivumbi zaidi cha ligi hiyo kitakuwa Jumapili ambapo viwanja sita vitawaka moto kwa kuzikutanisha timu 12 zikiwamo tatu zinazowania taji la ubingwa wa ligi hiyo linaloshikiliwa kwa sasa na Yanga.
Azam watakuwa kwenye uwanja wa Taifa kuivaa Simba, ikihitaji ushindi ili kuujongelea ubingwa huo na pia kuiombea mabaya Yanga watakaokuwa ugenini mjini Tanga kupepetana na Mgambo JKT iteleze katika mechi yake hiyo itakayopigwa uwanja wa Mkwakwani.
Azam ina pointi 50, nne na ilizonazo Yanga licha ya kuwa mbele kwa mchezo mmoja na timu yoyote ikiteleza itatoa nafasi kwa mwenzake kuubeba ubingwa huo kwa msimu wa 2013-2014.
Mbeya City waliopo nafasi ya tatu na pointi 42 wakiwa nao wanauota ubingwa watakuwa uwanjwa wa Sokoine kuumana na ndugu zao Prisons wanmaougulia kipigo cha mabao 5-0 walichopewa na Yanga juzi.
Ushindi wowote kwa Mbeya utamaanisha unaiweka pabaya Simba katika mbio zake kutaka kuambulia angalau nafasi ya tatu kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Simba wana pointi 36 na wamesaliwa na mechi nne, ambazo kama watashinda zote itafikisha pointi 48 zilizopitwa na Azam tayari.
Simba itavaana na Azam ikiwa inauguza kipigo cha bao 1-0 ilichopewa na Coastal Union mwishoni mwa wiki iliyopita kqwenye uwanja wa Taifa.
Mabingwa hao wa soka wa 1988 wenyewe watawafuata Mtibwa Sugar kuumana nao katika mchezo utakaochezwa uwanja wa Manungu, huku timu zote zikiwa hazina nafasi ya ubingwa wala hofu ya kushuka daraja.
Michezo nyingine ya Jumapili ni pamoja na Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting katika pambano linalosubiriwa kwa hamu kubwa mjini Bukoba, ambapo Msemaji wa Ruvu Masau Bwire ametamba kwamba wanaenda Kaitaba kuvuna pointi tatu.
Hata hivyo Bwire anatamba akitambua wazi kuwa Kagera Sugar huwa wagumu kwene uwanja wao wa nyumbani.
Timu hizo mbili zinafukuzana kwenye nafasi ya tano na sita zikitofautishwa na pointi moja, Kagera wakiwa na pointi 32 na Ruvu wenyewe wana pinti 31.

TMK, Tip Top kuzindua Yamoto

WASANII nyota toka makundi ya Tip Top Connection na TMK Wanaume Family wanatarajiwa kupamba uzinduzi wa video za Yamoto na Inno za kundi jipya linalooundwa na chipukizi toka Kituo cha Mkubwa na Wanawe.
Kundi hilo linaloundwa na wasanii Dogo Aslay, Beka, Maromboso na Bella, litazinduliwa Jumapili Masaki na nyota wa Tip Top wakiongozwa na Madee huku TMK litakuwa chini ya Chegge.
Kwa mujibu wa mmoja wa mabosi wa wasanii hao, Said Fella 'Mkubwa' aliliambia MICHARAZO uzinduzi wa kundi hilo utaenda sambamba na utambulisho wa kazi mpya za wasanii hao.
"Tunatarajiwa kuwatambulisha rasmi na kuzindua kundi la Moto linaloundwa na wasanii wanne walioibuliwa na Mkubwa na Wanae watakaosindikizwa na makundi ya Tip Top na TMK," alisema Fella.
Fella alisema makundi hayo yote yatakuwa na wasanii wao wote nyota na kuwataka mashabiki wa muziki kujitokeza kwa wingi Jumapili ili kupata burudani murua.

Mashali, Kaseba kupima uzito leo

Kaseba na Mashali wakishoo
MABONDIA Japhet Kaseba na Thomas Mashali na wengine watakaowasindikiza katika pambano lao la kuwania ubingwa wa UBO Afrika wanatarajiwa kupima uzito wao siku ya Ijumaa jijini Dar.
Kwa mujibu wa taarifa ya mmoja wa waratibu wa pambano hilo, Ibrahim Kamwe mabondia hao watapima uzito kuanzia saa 3 asubuhi kwenye ukumbi wa hoteli ya National iliyopo eneo la Keko.
Mbali na Mashali na Kaseba watakaopambana katika pambano la raundi 10 uzito wa LightHeavy (kilo 79), pia mabondia wengine watakaopima uzito na afya zao ni Allan Kamote ambaye atapigana na Karage Suba katika pambano la kuwania taji la kimataifa ya UBO.
"Mabondia wote wameshataarifiwa na wanatakiwa kuwahi mapema siku ya Ijumaa, National Hotel ili kupima afya na uzito wao kabla ya Jumamosi kuonyeshana kazi kwenye ukumbi wa PTA," alisema.
Kamwe aliwataja wengine watakaochuana katika michezo hiyo iliyoandaliwa na promota Ally Mwazoa, ni pamoja na Fredy Sayuni dhidi ya Rajab Mahoja watakaowania ubingwa wa taifa wa PST.
Baina Mazola atacheza na Bakari Dunda,Issa Omar ataonyeshana kazi na Zuberi Kitandula, Juma Fundidhidi ya Haji Juma, Shabaan Mtengela vs Jumanne Mohamed, Jocky Hamis dhidi ya Said Chaku

Subira ya Shaa mwezi ujao

Shaa katika pozi
'AUDIO' na VIDEO ya wimbo mpya wa msanii, Sarah Kais 'Shaa' unaofahamika kama 'Subira' unatarajiwa kuachiwa rasmi mapema mwezi ujao.
Wimbo huo uliobadilishwa jina kutoka 'Sifa Ujinga' hadi kuwa 'Subira' ni kazi ya pili ya mshindi huyo wa zamani wa Coca Cola Pop Star chini ya familia ya Mkubwa na wanae inayongozwa na Said Fella.
Akizungumza na MICHARAZO, Fella alisema wamepanga kutoa 'audio' na video ya wimbo huo mwezi ujao baada ya kurekodiwa mapema tangu Februari mwaka huu.
Fella alisema waliamua kuuzuia wimbo huo kutoka mapema ili kutoa nafasi ya kazi ya msanii huu iitwayo 'Sugua Gaga' kuendelea kutamba kwenye soko la muziki kutokana na ukali wake.
"Kazi mpya ya Shaa tutaiachia rasmi mapema mwezi ujao ikiwa ni 'audio' na video yake, hivyo mashabiki wajiandae kupata uhondo," alisema Fella waliyeingia mkataba na Shaa kwa muda wa miezi sita.
Kabla ya kutua Mkubwa na Wanae, Shaa alikuwa akifanya kazi chini ya umeneja wa Master J.

Ac Milan yazinduka, Juve moto chini

http://news.bbcimg.co.uk/media/images/73837000/jpg/_73837135_carlos-tevez-getty.jpg
Tevez akishangilia moja ya mabao yake

KLABU ya AC Milan imezinduka nchini Italia baada ya juzi kuikwanyua Fiorentina kwa mabao 2-0 nyumbani kwao, huku usiku wa jana wapinzani wao wa jiji la Milan, InterMilan walilazimishwa sare ya 0-0 na Udinese.
Milan ambaye imekuwa na matokea mabaya kwenye Ligi Kuu ya Seria A, walipata ushindi huo kupitia magoli yaliyofyungwa na Mexes dakika ya 23 kabla ya Mario Balotelli kufunga kipindi cha pili katika dakika ya 64 na kuipaa pointi tatu mabingwa hao wa zamani wa Ulaya.
Katika mechi nyingine za ligi hiyom, Juventus wakiwa nyumbani walipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Parma na kuzidi kujiweka karibu na kutetea taji la ubingwa wa ligi hiyo.
Magoli  yote mawili yalitupiwa kambani na Carlos Tevez katika dakika ya 25 na 32 na kuwapa pointi zinazowafanya wafikishe 81 na kusaliwa na mechi nane mkononi ambapo kama akishinda mechi tatu ikiwamo ya Jumapili dhidi ya Napoli atatawaza kuwa bingwa. Wageni walimpoteza Amauri aliyeonyesha kadi nyekundu.
Matokeo ya mechi nyingine za ligi hiyo;

Chievo     3 - 0     Bologna
Cagliari     1 - 0     Hellas Verona
Genoa     2 - 0     Lazio
Atalanta     2 - 0     Livorno   
Fiorentina     0 - 2     Milan
Catania     2 - 4     Napoli  
Juventus     2 - 1     Parma
Sassuolo     1 - 2     Sampdoria
Inter Milan 0-0 Udinese

Askofu Mhogolo afariki dunia

ASKOFU wa Dayosisi ya Central Tanganyika, Godfrey Mhogolo amefariki dunia nchini Afrika Kusini, alikokuwa amekwenda kwa matitabu. 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kanisa la Angilikana Dodoma jana, ilisema kuwa Askofu Mhogolo kabla ya kufikwa na mauti alikuwa akitibiwa katika hospitali ya Milpark huko Johanesburg, Afrika Kusini. Askofu Mhogolo alikuwa askofu wa tano wa dayosisi ya Central Tanganyika na atazikwa katika viwanja vya kanisa Kuu la Roho Mtakatifu Mjini Dodoma.  
Hata hivyo Mchungaji Michael Nchimbi alisema mipango ya mazishi inaendelea na taarifa zitatolewa baadaye. 
matukio na vijana

Golden Bush kupeleka makali yao Kilombero

Kikosi cha Golden Bush
Makocha wa Golden Bush, Madaraka Seleman na Herry Morris waliosimama wakiteta na wachezaji wao katika moja ya mechi zao
 MABINGWA wa kandanda wa soka la maveterani, Golden Bush Veterani inatarajiwa kupeleka makali yake wilaya ya Kilombero Morogoro kumenyana na Kilombero Veterani katika mechi inayochezwa kesho.
Kwa mujibu wa Msemaji wa klabu hiyo, Onesmo Waziri 'Ticotico' kikosi cha Golden Bush kitaondoka kesho asubuhi kikiwa na wachezaji 25 wakiongozwa na mkuu wa msafara,  Waziri Mahadh 'Mandieta'.
Ticotico alisema kikosi chao kitashuka dimbani jioni ya kesho kwenye uwanja wa Ruaha kuumana na wenyeji wao watakaokuwa wakiongozwa na nahodha wa zamani wa Simba, Mustafa Hozza.
Ticotico alitamba kuwa wanaenda Kilombero kuendeleza ubabe wao ambao umewafanya kukimbiwa na wapinzani na kwamba wenyeji wao wajiandae kwa kipigo.
Alisema kikosi chao chini ya kocha Madaraka Seleman 'Mzee wa Kiminyio' kitaongozwa na nahodha wao Wisdom Ndhlovu a.k.a Mwakalinga.

TFF kuuendeleza uwanja wao wa Tanga

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeanza mchakato wa kuendeleza uwanja wake uliopo eneo la Mnyanjani jijini Tanga.
Rais wa TFF, Jamal Emil Malinzi alisema shughuli inayoendelea kwa sasa ni kupima udongo (soil test) na kuandaa michoro kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha michezo (Sports Complex) ukiwemo uwanja wa mpira wa miguu na majukwaa yake.
Amesema TFF imetuma maombi rasmi kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kuomba eneo la kujenga kituo cha michezo ikiwemo uwanja wa mipira wa miguu na majukwaa yake.
“Pia Mkuu wa mkoa ameombwa kuingilia kati kuwaondoa wafanyabiashara waliovamia uwanja wa mpira wa miguu wa Jamhuri (King George Memorial ground) mjini Moshi,”amesema Malinzi.
Amesema TFF inawakumbusha viongozi wa vyama vya mikoa ambao hawajaomba maeneo ya kujenga vituo vya michezo vikiwemo viwanja vya mpira wa miguu, waongeze jitihada za kufanya hivyo na shirikisho hilo litawaunga mkono.
“TFF inachukua fursa hii kuvipongeza vyama vya mpira wa miguu ambavyo ama tayari vimeshachukua hatua au viko mbioni kuchukua hatua kutafuta na kuendeleza maeneo kwa ajili ya matumizi ya mpira wa miguu. TFF inaahidi kuunga mkono juhudi hizi na pale itakapohitajika kuongeza nguvu haitasita kufanya hivyo,”amesema.

Wednesday, March 26, 2014

Beki Coastal achekelea kuidungua Simba Taifa


Hamad Juma akichuana na Messi siku ya pambano la Coastal na Simba Taifa
MFUNGAJI wa bao pekee la Coastal Union ya Tanga lililoizamisha Simba kwenye uwanja wa Taifa, Hamad Juma anasema mpaka sasa haamini kama ni yeye aliyewalaza mapema vijana hao wa Msimbazi.
Hata hivyo beki huyo wa pembeni, aliyepandishwa kikosi cha kwanza toka timu ya vijana msimu huu, amesema anajisikia fahari kubwa kuwalaza mapema mashabiki wa Simba walioamini wangeshinda.
Akizungumza na MICHARAZO, Hamad alisema kila akikaa na kufikiria alichokifanya kwenye uwanja wa Taifa, hushindwa kujiamini kama ni yeye kutokana na ukweli wapinzani wao walisheheni nyota watupu.
Hamad alisema maamuzi aliyoyafanya mara baada ya beki wa Simba, Omar Salum kuzembea kuokoa mpira hakutarajia, lakini yaliweza kuwapa bao pekee lililoipa Coastal pointi tatu muhimu.
"Huwa nashindwa kuamini kama ni mimi niliyefunga bao lile na kuizamisha Simba, hata hivyo nashukuru kwa kusaidia Coastal na kuweka rekodi ya kuifunga timu kubwa kama ya Simba," alisema.
Alisema ushindi huo ulikuwa muhimu kwao ikizingatiwa kocha wao Yusuph Chipo aliwaamini vijana na kuwapanga katika pambano hilo timu yao ikitoka kufungwa mabao 4-0 na Azam.
Beki huyo alifunga bao hilo dakika ya 44 na kudumu hadi mwisho na kuifanya Simba ipoteze mechi ya nne katika ligi ya msimu huu na kuiacha ikibakia kwenye nafasi ya nne ya msimamo wa ligi hiyo.
Simba pia ilishapoteza mechi nyingine tatu mbele ya Azam, Mgambo JKT na JKT Ruvu na kutishia kukosa uwakilishi wa nchi kwa mara ya pili mfululizo kutokana kutanguliwa na Azam, Yanga na Mbeya City.

Yanga yaiua Prisons Taifa, Azam haishikiki

Yanga
Azam wanaozidi kuukomalia ubingwa unaoshikiliwa na Yanga
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga imezidi kufufua matumaini ya kutetea taji hilo baada ya jioni hii kuibugiza Prisons-Mbeya kwa mabao 5-0.
Pambano hilo lililochezwa kwenye uwanja wa Taifa, lilishuhudia Yanga wakienda mapumziko wakiongoza kwa mabao 2-0.
Bao la kwanza la Yanga liliwekwa kimiani na Mganda Emmanuel Okwi kwa mkwaju wa faulo katika dakika ya 21 kabla ya Mrisho Ngassa kuongeza la pili dakika ya 38 akimalizia krosi ya Husseni Javu.
Kipindi cha pili Yanga ilicharuka na hasa baada ya kufanya mabadiliko ya wachezaji na kuweza kujiandikia bao la tatu lililofungwa dakika 68 na mtokea benchi, Hamis Kiiza 'Diego'.
Kiiza alifunga bao hilo akiuwahi mpira uliotemwa na kipa wa Prisons baada ya Simon Msuva kumimina krosi murua langoni mwa 'Wajelajela' na Mganda huyo kufunga kilaini.
Nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro' aliiandikia Yanga bao la nne katika dakika ya 78 kwa mkwaju wa penati baada ya mabeki wa Prisons kumuangusha Husseni Javu, aliyeng'ara katika mchezo huo aliyoingia kipindi cha kwanza kuchukua nafasi ya Jerryson Tegete.
Dakika chache kabla ya kumalizika kwa pambano hilo, Kiiza kwa mara nyingine aliiongezea Yanga bao la tano baada ya Hussen Javu kufanya kazi nzuri kwa kufumua shuti langoni mwa wapinzani wao.
Kwa ushindi huo Yanga wamefikisha pointi 46 kutokana na kucheza mechi 21, wakiendelea kusalia nafasi ya pili nyuma ya Azam ambao jioni hii wameibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mgambo JKT katika pambano lililochezwa jijini Tanga.
taarifa toka Tanga zinasema kuwa Azam walipata mabao yake kupitia kwa John Bocco na Brian Umony na kuifanya timu hiyo kuendeleza rekodi yao ya kutopoteza mchezo wowote katika ligi ya msimu huu na kukaa kileleni wakiwa na pointi 51 licha ya kucheza mchezo 22.

Tuzo za Wanamichezo Bora Juni 27

http://www.fullshangweblog.com/wp-content/uploads/2013/02/kapo4.jpg
Shomari Kapombe Mwanamichezo Bora wa 2012
 TUZO za Wanamichezo Bora Tanzania zinazotolewa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) zitafanyika Juni 27, mwaka huu katika ukumbi ambao utatajwa baadaye mjini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya tuzo, Rehure Nyaulawa amesema leo kwamba baada ya kikao cha juzi cha Kamati yake juhudi za pamoja baina ya Kamati yake na Kamati ya Utendaji kuzungumza na wadhamini mbalimbali wakubwa na wadogo kwa nia ya kufanikisha tuzo hizo zimeanza.
“Kamati yetu kwanza inawaomba radhi viongozi wa vyama vyote vya michezo kutokana na tuzo kushindwa kufanyika mwaka jana na hilo kwa mujibu wa taarifa ya uongozi wa TASWA iliyowasilishwa kwenye kikao chetu, ilitokana na sababu mbalimbali lakini kubwa ni kujitoa dakika za mwisho kwa baadhi ya kampuni zilizokuwa zimethibitisha kudhamini tuzo hizo,”. Hata hivyo, Nyaulawa ameomba wendelee kutoa ushirikiano mwaka huu na kwa kuanzia watawatumia barua rasmi za kuomba majina ya wanamichezo wao waliofanya vizuri kuanzia Januari 2013 hadi Aprili mwaka huu, ambapo matarajio yao wanamichezo wasiopungua 40 watapewa tuzo. Amesema kwamba kamati pia imeamua kwamba kila mwaka tuzo hizo zijena ujumbe maalum kwa wanamichezo, ambapo kwa kuanzia tuzo za mwaka huu ujumbe wake utakuwa ni: ‘Wanamichezo Tupige Vita Ujangili’. “Tunaamini wale wote wataowania, wale watakaoshinda tuzo hizo na wanamichezo wote wakiwemo waandishi wa habari za michezo tutashirikiana na jamii kwa ujumla kwa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha vita dhidi ya ujangili kwa namna tutakavyomudu,”amesema. Amesema pia katika kuhakikisha tuzo za mwaka huu zinakuwa bora kwa maslahi ya wanamichezo wote hapa nchini, kamati imeteua baadhi ya viongozi wa kiserikali kuwa washauri wa kamati katika masuala mbalimbali na sasa wanasubiri majibu yao ili waweze kuwatangaza rasmi.

29 waanza kambi ya Stars marekebisho Tukuyu


Na Mwandishi maalumu, Tukuyu
WACHEZAJI 29 kati ya 34 waliochaguliwa katika programu maalumu ya marekebisho ya timu ya Taifa inayoendeshwa na TFF wameshaanza mazoezi makali katika Wilaya ya Rungwe, Mbeya.

Wachezaji hao, ambao wametokea katika mikoa mabali mbali, waliingia kambini siku ya Jumamosi huku wakiongozwa na Mwalimu Salum Mayanga akisaidiwa na Patrick Mwagata, ambaye ni kocha wa makipa, Meja Joakim Mashanga ambaye ni daktari wa team na Fred Chimela ambaye ni Meneja Vifaa.


Timu ya Taifa, Taifa stars, inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager kwa mwaka wa pili mfululizo sasa, inatarajiwa kupata mabadiliko makubwa sana ndani ya miezi miwili ijayo ili ipatikane timu bora itakayoshiriki katika mechi za kufuzu kupata tiketi ya kucheza Kombe la Afrika.

Mashetani Wekundu wafa tena, Arsenal yabanwa Everton yapeta

Edin Dzeko
Edin Dzeko akiwatungua Manchester United
Wilfried Bony
Hekaheka langoni mwa Arsenal

Everton's Ross Barkley
Shhhhh!
  JAHAZI la Manchester United limezidi kuzama baada ya usiku wa kuamkia leo kukandikwa mabao 3-0 kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Old Trafford na mahasimu wao wa jiji la Manchester, Manchester City.
Mabao ya Edin Dzeko aliyefunga mawili katika sekundu chache baada ya kuanza kwa mchezo huo na jingine la dakika 26 na lile la Yaya Toure dakika za 'jioni' yaliwafanya vijana wa David Moyes kushindwa kujua wamekumbwa na nini msimu huu.
Ushindi huo umeipeleka City hadi nafasi ya pili ikiiengua Liverpool itakayoshuka dimbani leo kuumana na Sunderland, kutokana na kufikisha pointi 66 baada ya kucheza mechi 29, mechi mbili pungufu na vinara wa ligi hiyo Chelsea wanaoongoza wakiwa na pointi 69.
Katika mechi nyingine, Arsenal ikiwa nyumbani ilinyang'anywa tonge mdomoni baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Swansea City kwenye uwanja wa Emirates.
Wageni walitangulia kupata bao dakika ya 11 kupitia kwa Wilfried Bony kabla ya wenyeji kuja kusawazisha katika kipindi cha pili kupitia kwa Lucas Podolski katika dakika ya 73 na kuongeza jingine kupitia kwa Olivier Giroud.
Hata hivyo wakati Arsenal ikijiandaa kushangilia ushindi mchezaji wake Mathieu Flamini alijifunga katika harakati za kuokoa shambulizi langoni mwake na kuwapa sare Swansea na kugawa pointi moja moja.
Nao Everton wakiwa ugenini waliwaduwaza wenyeji wao Newcastle Utd kwa kuwakandika mabao 3-0, mabao yaliyowekwa kimiani na Barkley, Lukaku na Osman.
Kwa ushindi huo umeifanya Everton kufikisha pointi 57 na kupanda nafasi ya tano na kuishusha Tottenham Hotspur yenye pointi 56 ambayo inarudi katika nafasi ya sita.
Kivumbi cha ligi hiyo kitaendelea tena usiku wa leo kwa michezo miwili, Liverpool itakayoumana na Sunderland na West Ham Utd itaikaribisha Hull City.

Bayern Munich nouma yatetea taji Ujerumani kwa aina yake

 http://www.sportsarena.com.sg/di/library/omnisport/11/68/bayernmunich_1um7biac60yco14kixp752v0gm.jpg?t=-616441876w=570

MABINGWA watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Bayern Munich imefanikiwa kutetea taji lake la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) usiku wa jana baada ya kuwafunga Hertha Berlin kwa mabao 3-1.
Watetezi hao wametwaa taji hilo la 23 wakiwa wameshinda mechi 10 mfululizo na pia wakiwa wamecheza mechi 52 ya mashindano yote bila kupoteza.
Mabo ya washindi katika pambano hilo lililochezwa mjini Berlin, yalifungwa na  Toni Kroos, Mario Goetze na Frank Ribery na kuifanya Bavarians kunyakua taji hilo ikiwa na mechi saba mkononi kabla ya kumaliza msimu wa Bundesliga.

Tuesday, March 25, 2014

Watatu wadakwa na 'unga', nyara za TTCL Lindi

Kamanda wa Polisi mkoa wa Lindi,Kamishna msaidizi Renatha Mzinga
Watuhumiwa wakiwa mikononi mwa polisi
Waya zilizokamatwa kwa mtuhumiwa Abdul Mahamud ambazo zimeyeyushwa zinasadikiwa kuwa za kampuni ya simu(TTCL)
..Baadhi ya madawa waliyokamatwa kwa Mtuhumiwa Salum Shaban Mapande
Na Abdulaziz Video, Lindi 
WATU watatu wanashikiliwa na Polisi Mkoani Lindi kwa tuhuma za kukutwa  na madawa ya kulevya aina ya heroin pamoja na Miundo mbinu ya Kampuni ya simu (TTCL) kinyume na Sheria.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Kamishna msaidizi Renatha Mzinga amesema leo kuwa kwa ushirikiano mkubwa waliopewa na wanajamii wamefanikiwa kumkamata Bw Salum Shaban Mapande(32)Mkazi wa Dar es sallam akiwa na madawa ya kulevya kete 42 kubwa na ndogo 104 zenye uzito wa Gram 58 na pesa taslim tsh 2,827,500 zinazosadikika kuwa za mauzo ya madawa hayo 
Watuhumiwa wengine waliokamatwa ni pamoja na mwanafunzi wa Chuo cha Utalii mjini Lindi, Masudi Mohamed(19) aliyekutwa na kete 35 za bangi huku Abdul Mahamud na Halfan Salum waliokutwa na nyaya za kampuni ya simu TTCL Zenye Uzito wa kg 5.
Kamanda Mzinga alisema mkoa wa Lindi umeanza kampeni kubwa ya kupambana na uhalifu mbalimbali ikiwemo kupambana na wimbi la uingizaji na uuzaji wa madawa ya kulevya ambalo kwa sasa kuna ongezeko kubwa la utumiaji na uuzaji wa madawa hayo ikiwemo pombe haramu ya gongo.
Aidha Kamanda Mzinga ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa huo kujidhatiti na kufichua wahalifu wakiwemo wauza madawa ya kulevya ambapo Jeshi lake litatoa ushirikiano na usiri kwa watakaotoa taarifa zinazoashiria Uvunjifu wa Amani ikiwemo za Usalama barabarani.
Matukio na Vijana

Breaking Newz: RC Mara aanguka ghafla na kufariki

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhbPVGH0kLaqzzGwCgm726E5L95gHbG_mDaef9wmO82-Q0lpd1-mOyWXZ-PTlBEmDNHjqlcBi-15RKMB5mT_SvjzOsI_90ppINqe6gajrvEnYGTbIMpHcghInX30rtWkznYVf7xkMZyr2hC/s640/Sensa%2010.jpg
RC Tupa (aliyesimama) enzi za uhai wake
HABARI zilizotufikia hivi punde zinasema kuwa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, John Tupa ameanguka ghafla na kutokwa na povu wakati akitoka nje ya ofisi ya Mkuu wa Wilaya (DC) Tarime kuelekea kupanda gari yake tayari kuanza ziara ya Tarime.
taarifa hizo zinasema kuwa, RC huyo aliwahishwa hospitali ya Wilaya, lakini kwa bahati mbaya amepoteza uhai wake.
Tunaendelea kufuatilia na tutawafahamisha zaidi...!
MICHARAZO inawapa pole ndugu, jamaa na familia nzima ya Rc Tupa kwa msiba huo...Kwa Hakika Kila Nafsi Itaonja Mauti...BWANA Ametoa na Yeye Ametwaa Jina Lake Lihimidiwe.

TFF yataka majina mabingwa wa mikoa kabla ya Machi 30


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) linavikumbusha vyama vya mpira wa miguu vya mikoa kuwa vinatakiwa kuwasilisha majina ya mabingwa wao kufikia Machi 30 mwaka huu.
Majina ya mabingwa yanatakiwa kuwasilishwa pamoja na usajili wa wachezaji waliotumika kwenye ligi ya mkoa. Kila klabu inaruhusiwa kuongeza wachezaji watano kutoka ndani ya mkoa husika, ambapo unatakiwa uthibitisho wa usajili huo.
Mpaka sasa ni vyama viwili tu ndivyo vimeshawasilisha mabingwa wao. 
Vyama hivyo ni Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) ambapo bingwa wake ni Kiluvya United, na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Lindi (LIREFA) ambapo bingwa ni Kariakoo SC.

Kalapina atoa mpya kiulayaulaya

Karama Masoud 'Kalapina' akionyesha manjonjo yake jukwaani
NYOTA wa muziki wa Hip Hip nchini, Karama Masoud 'Kalapina' amefyatua 'single' mpya  iitwayo 'Hip Hop is Alive' aliomshirikisha msanii  'Q Chilla' ambayo anatarajia kuuachia rasmi kesho.
Akizungumza na MICHARAZO, Kalapina anayetoka kundi la Kikosi cha Mizinga alisema wimbo huo umerekodiwa katika studio za Rubby Records chini ya mtayarishaji wake Jallaman.
Kalapina alisema tofauti na alivyozoeleka kuimba hip hip ngumu, safari hii amekuja kivingine akiimba hip hip laini inayoweka kuchezeka akiwa amelenga soko la kimataifa zaidi.
"Huu ni ujio mpya wa Kalapina, nimelenga soko la kimataifa kwa kuimba wimbo huo kwa staili ya Ulaya na sijaegemea Marekani au Nigeria kama ilivyo kimbilio la wasanii wengi kwa sasa, na nitaachia hadharani kuanzia kesho Jumatano," alisema.
Kalapina alisema ameamua kubadilika kidogo ili kufanya muziki wake usikilizwe na watu wa rika lote na kuweza kuwarusha wasikilizaji wake na lengo lake kubwa ni kutaka kufungua soko la muziki wake anga la kimataifa badala ya kukomalia nyumbani tu.

Timu ya Watoto wa Mitaani yaenda Brazil

  https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEi-_8-_Pi8v83y40ogZfYaU-TnhwkTqBDPtblA7ofd5DJ-6KhCtG-h5Zc0BdkZlWCO-JmXfTz1vkPBXM9NxnCRxvk0HJUHPqB2MglnkrBOIcgUOXB1MlstOZxAxkEIHaQgqbOm_MsmLgE4/s1600/531480_458178010866718_1145297429_n.jpg
TIMU ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania kutoka Kituo cha Mwanza imeondoka leo (Machi 26 mwaka huu) kwenda Brazil kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia kwa Watoto wa Mitaani.
John Kadutu ambaye ni mjumbe wa Bodi ya kituo hicho, na pia mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) akiwakilisha klabu za Mkoa wa Mwanza ndiye kiongozi wa msafara wa timu hiyo ya Tanzania.
Michuano hiyo ya siku 10 inayoshirikisha watoto wa mitaa (wavulana na wasichana) inaanza keshokutwa (Machi 28 mwaka huu). Nchi 19 zinashiriki michuano hiyo itakayofanyika katika Jiji la Rio de Janeiro.
Mbali ya Tanzania, nchi nyingine zinazoshiriki michuano hiyo kwa upande wa wavulana ni Argentina, Burundi, India, Kenya, Liberia, Marekani, Mauritius, Misri na Pakistan. Kwa wasichana ni Afrika Kusini, Brazil, El Salvador, Indonesia, Msumbiji, Nicaragua, Philippines, Uingereza na Zimbabwe.
Mwaka 2010 mashindano hayo yalifanyika Durban, Afrika Kusini ambapo pia Tanzania ilishiriki.

Diamond, Lady Jaydee watisha Kili Music Awards


'Sukari ya Warembo' Diamond Platnumz
Lady Jaydee 'Comando' a.k.a Anaconda
WANAMUZIKI nyota nchini, Nassib Abdul 'Diamond Platinum' na Judith Wambura Mbibo 'Lady jaydee' a.k.a Comando au Anaconda wameteuliwa mara nyingi kuwania tuzo za muziki za Kili Music zilizotangazwa leo.
Diamond ameingia katika vipengele 6 vya kinyan’ganyiro cha tuzo za muziki nchini, maarufu kama Kilimanjaro Tanzania Music Awards 2014, huku Binti Machozi akiteuliwa mara 7.
Wimbo bora wa mwaka;
1 Number one-Diamond,
2 Joto hasira-Lady Jaydee Ft Prof Jay,
3 I love u-Cassim Mganga,
4 Yahaya-Lady JayDee,
5 Kidela -Abdu Kiba Feat Ali Kiba 
6 Muziki gani-Ney ft Diamond.


Wimbo bora wenye vionjo vya asili ya Kitanzania;
1 Kwejaga nyangisha-Batarokota,
2 Nalonji-Kumpeneka,
3 Bora Mchawi-Dar Bongo massive,
4 Tumbo lamsokota-Ashimba,
5 Aliponji –Wanakijiji 
6 Agwemwana-Cocodo African music band.

Wimbo bora wa kiswahili –Bendi;
1 Ushamba mzigo-Mashujaa Band,
2 Shamba la Bibi -Victoria Sound,
3 Chuki ya nini -FM Academia,
4 Yarabi nafsi -Mapacha Watatu
5 Kiapo mara 3 -Talent Band.

Wimbo bora wa Reggae;
1 Niwe na wewe-Dabo,
2 Hakuna Matata-Lonka,
3 Tell Me-Dj Aron ft Fidempha,
4 Bado nahitaji-Chikaka ft Bless p & Lazzy B
5 Bongo Reggae-Warriors from the east.

Wimbo bora wa Afrika Mashashariki;
1 Tubonge-Jose Chamelleone,
2 Nakupenda Pia-Waire Ft Allain,
3 Badilisha-Jose Chamelleone,
4 Kipepeo-Jaguar
5 Kiboko Changu-Aman FT Weizal and Radio.

Wimbo bora wa Afro pop;
1 Number one-Diamond,
2 Joto hasira-Jay Dee,
3 Kidela-abdul kiba ft Ali Kiba,
4 I love you-Kassim,
5 Tupogo-Ommy Dimpoz Ft J Martins
6 Roho yangu-Rich Mavoko.

Wimbo bora wa Taarab;
1 Wasi wasi wako-Mzee Yusuf,
2 Asiyekujua Hakuthamini-Isha Ramadhani & Saida Ramadhani,
3 Nipe stara -Rahma Machupa,
4 Sitaki shari-Leyla Rashid,
5 Fahari ya Mwanamke-Khadija Kopa,
6 Mambo bado-Khadija Yusuf
7 Kila muomba Mungu -Mwanahawa Ali.

Wimbo bora wa Hip hop;
1 Bei ya mkaa-Weusi,
2 Nje ya box-Nick wa pili ft Joh Makini na Gnako,
3 Siri ya mchezo-Fid q ft Nature,
4 2030-Roma
5 Pesa-Mr Blue Ft Becka Title.

Wimbo bora wa R&B;
1 Listen-Belle 9,
2 Closer -Vanessa Mdee,
3 So crazy-Maua ft Fa,
4 kama huwezi-rama dee ft jay dee
5 Wa ubani-Ben Pol ft. Alice

Wimbo bora wa kushirikisha/kushirikiana;
1 Music Gani-Ney Mitego ft Diamond,
2 Joto Hasira-Lady JayDee ft. Prof Jay,
3 Kidela -Abdul Kiba ft. Ali Kiba,
4 Bila Kukunja Goti-Mwana FA na AY ft. Jay Martins
5 Tupogo-Ommy Dimpoz ft. Jay Martins.

Wimbo bora wa Ragga/Dancehall;
1 Nishai-Chibwa Ft Juru,
2 Sex girl-Dr Jahson,
3 My sweet-Jettyman Dizano,
4 Feel Alright-Lucky Stone,
5 Wine-Princess Delyla.

Wimbo bora wa Zouk /Rhumba;
1 Yahaya-Lady Jaydee,
2 Yamoto-Mkubwa na wanawe,
3 Msaliti-Christian Bella,
4 Nakuhitaji-Malaika Band
5 Narudi kazini-Beka.

Mwimbaji bora wa kike -kizazi kipya;
1 Vanessa Mdee,
2 Lady Jaydee,
3 Linah na 4 Maua

Mwimbaji bora wa kiume -kizazi kipya
1 Ben Pol,
2 Rich Mavoko,
3 Diamond,
4 Ommy Dimpoz
5 Cassim Mganga.

Mwimbaji bora wa kike –Taarab;
1 Khadija Kopa,
2 Isha Ramadhani,
3 Khadija Yusuf,
4 Mwanahawa Ali
5 Leyla Rashid,

Mwimbaji bora wa kiume –Taarab wanashindana
1 Mzee Yusuf,
2 Hashimu Saidi
3 Mohamedi Ali aka Mtoto Pori.

Mwimbaji bora wa kiume –Bendi;
1 Jose Mara,
2 Kalala Junior,
3 Charz Baba,
4 Khalid Chokoraa
5 Christian Bella,

Mwimbaji bora wa kike -Bendi
1 Luiza Mbutu,
2 Catherine (Cindy) 
3 Ciana.

Msanii bora wa -Hip hop;
1 FID Q,
2 Stamina,
3 Young killer (Msodoki),
4 Nick wa pili,
5 Gnako.

Msanii bora chipukizi anayeibukia;
1 Young Killer(Msodoki),
2 Walter Chilambo,
3 Y Tony,
4 Snura
5 Meninah,

Rapa bora wa mwaka –Bendi kuna
1 Kitokololo,
2 Chokoraa,
3 Furguson,
4 Canal Top
5 Totoo ze Bingwa.

Mtumbuizaji bora wa kike wa Muziki.
1 Khadija Kopa,
2 Vanessa Mdee,
3 Isha Ramadhani,
4 Luiza Mbutu
5 Catherine (Cindy)

Mtumbuizaji bora wa kiume wa Muziki
1 Diamond,
2 Christian Bella,
3 Rich Mavoko,
4 Ommy Dimpoz
5 Abdu Kiba.

Mtayarishaji bora wa nyimbo wa mwaka –Taarab;
1 Enrico,
2 Ababuu Mwana ZNZ
3 Bakunde

Mtayarishaji bora wa nyimbo wa mwaka -Kizazi kipya
1 Marco chali-Mj Records,
2 Man Water-Combination Sound,
3 Mazoo-Mazoo Records,
4 Sheddy Clever-Burnz Records
5 Nahreel -Home Town Record.

Mtayarishaji bora wa nyimbo wa mwaka –Bendi;
1 Allan Mapigo,
2 C9,
3 Enrico,
4 Amoroso
5 Ababuu Mwana ZNZ,

Mtunzi bora wa mwaka –Taarabu,
1 Mzee Yusuf,
2 El-Ahad Omary,
3 El-khatib Rajab,
4 Kapten Temba,
5 Sadiki Abdul
6 Nassoro Seif,

Mtunzi bora wa mwaka -kizazi kipya,
1 Belle 9,
2 Ben Pol,
3 Diamond,
4 Rama dee
5 Rich mavoko.

Mtunzi bora wa mwaka –Bendi
1 Christia Bella,
2 Jose Mara,
3 Chaz Baba,
4 Nyoshi Saadat
5 Kalala Junior

Mtunzi bora wa mwaka -Hip hop,
1 Nikki wa Pili,
2 Young Killer(Msodoki),
3 Roma,
4 FID Q
5 G- Nako.

Video bora ya muziki ya mwaka;
1 Number One-Diamond,
2 Yahaya-lady Jaydee,
3 Joto hasira-Lady Jaydee Ft Prof Jay,
4 Uswazi takeaway-Chege Ft Malaika,
5 Mama Yeyo-Gnako Ft Ben Pol.

Bendi bora ya mwaka;
1 FM Academia,
2 Mapacha Watatu,
3 African Stars ‘Twanga Pepeta’,
4 Akudo Impact,
5 Malaika Band,
6 Mashujaa Band,

Kikundi cha mwaka cha Taarab ni
1 Jahaz Modern Taarab,
2 Mashauzi Classic
3 Five Stars

Kikundi cha mwaka cha kizazi kipya;
1 Makomandoo
2 Navy kenzo,
3 Weusi
4 Mkubwa na wanawe

(CHANZO: www.saluti5.com).

Easy Man kuweka Mashetani wake videoni

Easy Man  katika 'kichupa' chake cha Kasoro Wewe
MSANII anayetajwa kama 'mfalme' wa mchiriku nchini kwa sasa, Is'haka Salehe 'Easy Man',  anatarajiwa kurekodi video ya wimbo wake mpya uitwao 'Mashetani'.
Easy Man alisema wimbo huo ambao ni wa pili kwake baada ya kutesa na 'Kasoro Wewe', alisema kazi ya kurekodi video hiyo inatarajiwa kuanza keshokutwa chini ya kampuni moja iliyopo maeneo ya Temeke.
"Kuanzia Alhamisi natarajia kuanza kazi ya kurekodi video ya wimbo wangu wa 'Mashetani' na baada ya hapo nitaingia tena studio kwa ajili ya kurekodi wimbo mwingine ambao nitauachia kabla ya Mei mwaka huu," alisema Easy Man.
Msanii huyo alisema ana imani video ya wimbo wake wa 'Mashetani' unafunika kama ule wa 'Kasoro Wewe', huku akikatishwa tamaa baada ya kushindwa kuingia kwenye kinyang'anyiro cha Tuzo za Muziki wa Kili Music alizokuwa akiziombea awemo safari hii.

Kamati ya Sheria TFF kukutana juu ya Katiba

Rais wa TFF, Jamal Malinzi
KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inatarajia kukutana mwishoni mwa wiki kupitia taarifa ya utekelezaji wa agizo la wanachama kurekebisha katiba zao. TFF ilitoa agizo kwa wanachama wetu kufanyia marekebisho katiba ikiwemo kuingiza Kamati ya Maadili. Mwisho wa utekelezaji wa agizo hilo ulikuwa Machi 20 mwaka huu. Hivyo, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji itapokea taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo kutoka kwa Sekretarieti, na baadaye kutoa mwongozo wa hatua inayofuata.

Japanese ataka wasanii wa kike kujifunza kupiga ala

Japanese (kulia) akiwa na wanamuziki wenzake wa Jambo Survivors
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgxe5Rtm0ti7byoMQu71Qu2RCeP9KEud2GUkrLmeGrxVLRPJp1gKactUXZTOHXJoo7jhXXQbSZTnLG8klbNhVehA7oIbPN1esGX21SAjpyExhcK1wLO_mtK85shSRI2zmvGELH-iAE88iw/s1600/FIL0.JPG
Marehemu Asia Daruwesh enzi za uhai wake akionyesha umahiri wake katika kinanda
MUIMBAJI nyota wa zamani wa African Revolution na Double M Sound, Amina Ngaluma 'Japanese' amewataka wasanii wenzake wa kike kujibidiisha kujifunza kupiga ala za muziki badala ya kuishia kuimba tu.
Japanese alisema wasanii wengi wa kike wamekuwa wakikwepa kujifunza kupiga ala au kujifunza vitu zaidi ya uuimbaji na kuwafanya waachwe nyuma na wasanii wa kiume.
Alisema imefika wakati wanawake wenzake kuacha uvivu na badala yake kukamilia ala mbalimbali ili wawe wanamuziki kamili na kuweza kusimama pamoja na wanamuziki wa kiume wanaoonekana kutawala anga la muziki nchini.
"Mimi natunga, napanga muziki, napiga gitaa na ala nyingine, kitu ambachio natamani wasanii wa kike wengine wafuate nyayo ili kuondoa dhana muziki ni wa wanaume tu na sisi kazi yetu kuimba tena wakati mwingine kuitikia tu," alisema.
Alisema pia angependa kuona idadi ya wiambaji wa kike nchini inaongezeka maradufu kama ilivyokuwa miaka ya 1980-2000 waimbaji wa kike walipokuwa wengi na wengine kama marehemu Asia Daruwesh akiwa mahiri katika kupapasa kinanda kwa ustadi mkubwa.

Yanga, Azam vitani tena kesho VPL

Yanga SC
Azam Fc
KLABU za Azam na Yanga ambazo zinachuana kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, zinashuka tena viwanjani kesho (Machi 26 mwaka huu) kuwania pointi tatu. Azam yenye pointi 47 itakuwa mgeni wa Mgambo Shooting katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Mgambo Shooting ipo katika nafasi ya kumi na moja kwenye msimamo wa VPL ikiwa na pointi 19.
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Yanga na Tanzania Prisons kuanzia saa 10.30 jioni. Yanga ipo nyuma ya Azam kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 47. Hata hivyo, timu hiyo ina mchezo mmoja mkononi. Tanzania Prisons ambayo ipo chini ya Kocha David Mwamaja hivi sasa ina pointi 22 ikiwa katika nafasi ya kumi. Timu tatu za mwisho katika ligi hiyo itakayomalizika Aprili 19 mwaka huu zitashuka kurudi Ligi Daraja la Kwanza (FDL). Ligi itaendelea tena Jumamosi (Machi 29 mwaka huu) kwa mechi kati ya Ashanti United na Oljoro JKT itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam. Jumapili (Machi 30 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Mbeya City na Tanzania Prisons (Uwanja wa Sokoine), Kagera Sugar na Ruvu Shooting (Uwanja wa Kaitaba), Mtibwa Sugar na Coastal Union (Uwanja wa Manungu), JKT Ruvu na Rhino Rangers (Uwanja wa Azam Complex), Azam na Simba (Uwanja wa Taifa) na Mgambo Shooting na Yanga (Uwanja wa Mkwakwani).

Mahakama yaagiza Yanga ikatwe kuwalipa akina Malashi

Steven Malashi na Wisdom Ndlovu wanaoidai Yanga
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limepokea amri ya Mahakama Kuu (Kitengo cha Kazi) kukamata Sh. Milioni 106 za klabu ya Yanga kutokana na mapato ya mlangoni kwenye mechi zake ili kuwalipa waliokuwa wachezaji wake, Stephen Malashi na Wisdom Ndlovu.
Taarifa ya TFF imesema kwamba, tayari wameanza utekelezaji wa amri hiyo ambapo katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) dhidi ya Rhino Rangers iliyochezwa Machi 22 mwaka huu mjini Tabora walizuia Sh. 9,221,250 ambazo ndizo zilizokuwa mgawo wa Yanga katika mchezo huo ulioingiza jumla ya sh. 38,655,000.
Wachezaji hao walifungua kesi kortini kupinga mikataba yao na klabu hiyo kuvunjwa bila kulipwa haki zao za kimkataba. Malashi na Ndlovu walishinda kesi hiyo, hivyo korti kuwapa tuzo hiyo ya sh. milioni 106.
Tunawakumbusha wanachama wetu (klabu za Ligi Kuu, vyama vya mpira wa miguu vya mikoa na vyama shiriki) kuzingatia mikataba wanayoingia na watendaji wao wakiwemo wachezaji, makocha na maofisa wengine.
“Iwapo wanataka kuvunja mikataba ya ajira wafuate taratibu kwa vile hakuna mkataba ambao hauelezi jinsi ya kuvunjwa iwapo upande mmoja unataka kufanya hivyo,”imesema taarifa ya TFF.