STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, February 25, 2015

Mtanzania ajiunga chuo cha soka Senegal

Mtanzania Nasry Daud Aziz atakayejiunga na kituo hiki cha Senegal
MWANASOKA chipukizi Nasry Daudi Aziz aliyezaliwa Agosti 21, 2001 amechaguliwa kujiunga na kituo cha kukuza vipaji cha Aspire Football Dream kilichopo katika mji wa Dakar nchini Senegal.
Mradi wa  Aspire nchini ulianza mchakato wa kusaka vijana mwezi Machi - Mei, 2014 ambapo vijana wengi walijitokeza na kuchaguliwa vijana 14 ambao walikwenda katika mchujo mwingine uliofanyika nchini Uganda uliowashirikisha vijana zaidi ya 50.
Kijana huyo ni miongoni mwa wachezaji 17 waliochaguliwa kati ya vijana 34 walikuwepo nchini Senegal kwa muda wa mwezi mmoja, ambapo kulikuwa na vijana wengi kutoka nchi mbalimbali barani Afrika na Amerika ya Kusini.
Kituo cha Aspire kilichopo Dakar nchini Senegal ni miongoni mwa vituo viwili vinavyoongozwa na mtoto wa mfalme wa Qatar na timu ya Barcelona, kituo kingine kipo mjini Doha.
Nasry Daud Aziz anatarajiwa kuondoka nchini Februari 28 mwaka huu kuelekea Dakar ambapo atakua kwenye kituo hicho kwa mkataba wa miaka miatano.
 Kutoka nchini Tanzania Nasry anakua ni kijana wa tatu kujiunga na kituo hicho, wengine ni Matine Taganzi na Orgenes Morrel ambaye aliitwa kwenye timu ya Taifa Stars maboresho na kocha Mart Nooj.

Cheki video mpya ya Belle 9 ft Joh Makini - Vitamin Music

Mwili wa Christopher Alex hatimaye wapumzishwa Dodoma

IMG-20150224-WA0007
Makazi ya milele ya Christopher Alex
Na Rahma Junior, Dodoma
MWILI wa kiungo nyota wa zamani wa timu ya Simba, Christopher Alex, aliyefariki dunia Jumapili iliyopita katika Hospitali ya Mirembe mkoani Dodoma, umezikwa jana kwenye makaburi ya Nkuhungu.
Mwili wa Alex ulifanyiwa ibada ya maziko nyumbani kwa mama yake Massawe, Martha Matonya chini ya  Mchungaji wa Kanisa la Anglikan, Parishi ya Chamwino, Mch. David Matonya na ilihudhuriwa wa mamia ya waombelezaji, wakiwamo waliokuwa wachezaji wenzake kwa nyakati tofauti.
Baadhi ya wachezaji walioshiriki kumsindikiza marehemu Alex ni Ulimboka Mwakingwe, Boniface Pawasa, Kelvin Mhagama, Amani Mbarouk, Juma Kaseja na Juma Ikaba aliyecheza naye kwenye timu ya CDA-Dodoma, ambaye sasa ni kocha wa timu hiyo.
Klabu ya Simba iliwakilishwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa timu hiyo, Ally Sulu, ambaye pia alizungumzia malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na baadhi ya waombolezaji kwamba klabu zimekuwa na kawaida ya kuwatelekeza wachezaji pindi wanapokuwa wamemaliza kuzitumikia.
Naye Pawasa, alisema siyo tu klabu vya mpira wa miguu bali Watanzania wengi wanafurahia mtu akiwa mchezaji, anapomaliza muda wa kucheza na ikatokea ameugua au kupatwa majanga, wanamtelekeza.
“Wasanii wengine mathalani wa filamu wanashuhudiwa wakisaidiwa hata wanapokuwa kwenye matatizo ya kujitakia. (Tulipaswa kumjali) Alex alifunga penalti ya mwisho katika michuano ya Klabu Bingwa barani Afrika dhidi ya timu ngumu ya Zamalek ya Misri mwaka 2003,” alisema Pawasa.
Marehemu Christopher Alex atakumbukwa kwa kufunga penati ya mwisho iliyowavua ubingwa wa Ligi ya mabingwa Afrika Zamalek mwaka 2003 na kuvunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na Yanga katika michuano hiyo tangu 1998 walipotinga hatua ya makundi kwa timu za Tanzania.
Simba ilishinda nyumbani bao 1-0 kabla ya kufungwa idadi kama hiyo katika mechi ya marudiano nchini Misri na kufikia hatua ya kupigiana penati na Sinmba kufuzu.

Andy Murray aanza vema michuano ya Dubai Open

MUINGEREZA Andy Murray ameanza vizuri kampeni zake za kutwaa ubingwa wa mashindano ya Dubai baada ya kuibuka na ushindi wa seti 6-4 7-5 dhidi ya Gilles Muller.
Mscotland huyo, mwenye umri wa miaka 27, alipata ushindi huo kwa kutumia saa moja na dakika 45, na sasa atacheza na Joao Sousa katika raundi ya pili, ikiwa ni wiki mbili baada ya kumshinda Mreno huyo katika mashindano ya Australian Open.
Bingwa anayeongoza kwa ubora Novak Djokovic naye alianza vizuri mashindano hayo baada ya ku
mchakaza Mcanada Vasek Pospisil 6-4 6-4 katika mchezo wa rundi ya kwanza.
James Ward ambaye ni Muingereza anayeshikilia nafasi ya pili kwa ubora, alijikuta akishindwa kufanya kweli baada ya kushindwa mara mbili katika hatua ya kufuzu na kupoteza kwa 6-4 6-4 dhidi ya Muhispania Feliciano Lopez, anayeshikilia nafasi ya 13 kwa ubora duniani.
Muingereza huyo sasa atakwenda Glasgow kujiunga na timu ya Uingereza itakayocheza mchezo wa Davis Cup dhidi Marekani, utakaofanyika kuanzia Machi 6-8 huko Emirates.
Murray anatarajia kukawia kujiunga na wenzake huko Scotland endapo ataendelea kufanya vizuri huko Dubai baada ya leo kuanza vibaya mchezo huo katika jaribio lake la kwanza, lakini alifanya vizuri na kuibuka na ushindi katika seti hiyo ya kwanza.
Djokovic anashiriki kwa mara ya kwanza tangu alipotwaa taji la Australian Open Februari mosi na anaangalia kuwa mtu pekee wa 12 kushinda taji la 50.

Luis Enrique kuendelea kumtumaini Messi katika penati

Joe Hart
Joe Hart akiojkoa mkwaju wa penati ya Messi usiku wa jana
Lionel Messi watches on as Hart does brilliantly to save his last-minute penalty  
Messi akiwa haamini kama mkwaju wake umezuiwa na kipa wa Man City
Hart celebrates saving the last-gasp penalty as Pedro holds his head in his hands and Messi lies on the floor
Messi akiwa amelala chini baada ya kukosa penati
MENEJA wa klabu ya Barcelona, Luis Enrique amesisitiza kuwa Lionel Messi ataendelea kuwa mpiga penati wa timu hiyo pamoja na kukosa penati yake ya nne msimu huu katika mchezo dhidi ya Manchester City juzi.
Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina alikuwa na nafasi ya kuipa ushindi Barcelona wa mabao 3-1 katika dakika za majeruhi lakini Joe Hart alifanikiwa kuokoa mchomo wake.
Messi pia amekosa penati katika mchezo dhidi ya Levante, Septemba mwaka jana na Brazil wakati akiitumikia timu yake ya taifa Oktoba lakini Enrique anaamini kuwa nyota huyo bado ni mpigaji mzuri na anamuamini.
Kocha huyo amesema wale wote wanaokosa penati ni wale wenye uthubutu wa kufanya hivyo na Messi bado ataendelea kuwa mpigani wao.
Katika mchezo huo wa mkondo wa kwanza uliofanyika katika Uwanja wa Etihad, Barcelona ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-1, ikiwa ni siku chache ikitoka kupokea kipigo cha bao 1-0 nyumbani Camp Nou dhidi ya Malaga katika Ligi Kuu ya Hispania (La Liga).
Kukosa penati hiyo ya juzi imemfanya Messi kulingana na Cristiano Ronaldo, Luis Figo and Andy Shevchenko katika michuano hiyo ya Ulaya wakitanguliwa na Ruud Van Nistelrooy aliyekosa mabao manne na Thierry Henry anayeongoza kwa kukosa penati tano.
Pia ni penati ya 13 kwa mkali huyo wa mabao wa Cataluna kati ya mikwaju 59 aliyopiga akiwa na klabu ya Barcelona, huku kwa upande wa nchi yake ya Argentina Messi amekosa mbili kati ya 12 alizopiga

Azam, Yanga zaenda ugenini zikiwa na matumaini

Azam Fc watakaokuwa ugenini nchini Sudan
Yanga wao watakuwa vitani nchini Botswana
WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, Azam na Yanga zimeondoka nchini zikiwa na matumaini makubwa ya kushinda mechi zao za wikiendi hii za ugenini katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Azam waliondoka jana kuelekea Sudan watakuwa na kibarua kizito mbele ya wenyeji wao El Merreikh waliowafumua kwenye uwanja wa Chamazi, mabao 2-0 wakati Yanga wenyewe waliondoka alfajiri ya leo wakiwa na morali mkubwa baada ya ushindi wao wa mabao 2-0 dhidi ya Maafande wa BDF XI ya Botswana watakaorudiana nao Jumamosi.
Yanga waliowaacha baadhi ya nyota wake akiwamo Mbrazil, Andrey Coutinho kutokana na kuwa majeruhi, imeenda Botswana wakiwa na amani kutokana na mwenendo mzuri wa timu yao katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara ikipata ushindi mfululizo na kuongoza msimamo wa ligi hiyo kwa pointi nne mbele zaidi ya watetezi Azam ambao mechi zao mbili za mwisho waliambulia sare tupu.
Uongozi wa Yanga kupitia Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Jerry Muro amesema Yanga inaenda ugenini ikiwa imepania kusonga mbele licha ya kutambua pambano lao litakuwa gumu kwa vile BDF watakuwa nyumbani na wana hasira ya kufungwa mabao 2-0.
Muro alisema vijana wake wote 20 waliopo kwenye msafara wao wameapa kupambana kuhakikisha wanapata ushindi ugenini ili kusonga mbele ya kuvaana ama na Sofapaka ya Kenya au Platnum ya Zimbabwe ambao walishinda mabao 2-1 katika mchezo baina yao wiki mbili zilizopita mjini Nairobi.
Upande wa Azam kupitia Meneja wake, Jemedari Said, alisema kuwa wanaenda Sudan wakiwa na nia ya kukamilisha malengo yao ya kufuzu raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Jemedari, nyota wa zamani wa Majimaji-Songea na klabu nyingine alisema kuwa Azam wanaenda Sudan wakitambua kuwa watakabaliwa na mechi ngumu kwa vile El Merreikh siyo timu ya kubezwa hata kama waliwafunga mabao 2-0 katika mechi ya kwanza nyumbani.
Meneja huyo aliongeza kuwa Azam inayoiwakilisha Tanzania kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa baada ya miaka miwili mfululizo kushiriki Kombe la Shirikisho, imepania kufika mbali kwenye michuano hiyo ili kufuta dhana kwamba timu za Tanzania ni wasindikizaji tu katika michuano ya kimataifa.
Mabingwa watetezi hao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, watashuka dimbani keshokutwa, watahitaji sare ya aina yoyote ili kujihakikisha kusonga mbele na kukutana na ama timu ya Lydia Ludic B.A ya Burundi au Kabuscorp do Palanca ya Angola ambazo zilishindwa kufunga katika mechi mechi yao ya mkondo wa kwanza iliyochezwa nchini Burundi.
Wawakilishi wengi wa Tanzania visiwani, KMKM waliofungwa mabao 2-0 na Al Hilal na POlisi Zanzibar walifumuliwa mabao 5-0 na Maunama ya Gabon watashuka dimbani mwishoni mwa wiki kukamilisha ratiba ya mechi zao za michuano hiyo ya kimataifa ya Afrika.
Mabingwa wa Zanzibar, KMKM watahitajika kuwafunga wa Sudan mabao 3-0 ili kufuzu, huku Polisi wakihitajika kushinda mabao 6-0 kitu kinachoonekana kuwa ndoto ikizingatiwa wawakilishi wa Zanzibar hawajawahi kuvuka raundi ya awali tangu nchi hiyo ilipotambuliwa rasmi na Shirikisho ya Soka Afrika (CAF) mnamo Desemba mwaka 2004.

Suarez aiangamiza Manchester City, Juve yaiua Dortmund

Suarez akishangilia bao lake la pili
Suarez akishangilia bao la kwanza

Lionel Messi akipambana kabla ya kukosa penati dakika za lala salama
MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa Liverpool, Luis Suarez amewadhihirishia Waingereza kuwa yeye bado ni moto wa kuotea mbali baada ya kufunga mabao mawili yaliyoiangamiza Manchester City kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Etihad, mjini Manchester katika mechi ya mkondo wa kwanza ya mtoano wa 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.
Suarez aliyeibeba Liverpool msimu uliopitwa kabla ya kuuzwa kwa 'hasira' na klabu hiyo kwa Barcelona kutokana na tukio lake la utovu wa nidhamu alililolifanya katika Fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil, aliiwezesha timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kujiweka nafasi nzuri ya kutinga Robo Fainali katika mechi yao ya marudiano baadaye mwezi ujao mjini Barcelona.
Nyota huyo wa kimataifa wa Uruguay, alianza kuwashtua wenyeji ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England baada ya kufunga bao la kwanza dakika 16 akiwa ndani ya  'boksi' la lango la Manchester City kabla ya kuongeza jingine katika ya 30 akimalizia kazi nzuri ya Lionel Messi na kuifanya Barcelona iende mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili Manchester City ambao baadhi ya wachezaji wake walinukuliwa wakitamba haiwahofii Barcelona, walijitutumia na kupata bao la kufutia machozi lililofungwa na Sergio 'kun' Aguero katika dakika ya 69 kabla ya beki wake Gael Clichy kutolewa nje ya uwanja kwa kadi nyekundu katika dakika ya 74 baada ya kupewa kadi ya pili ya njano kutokana na kumchezea rafu Dani Alves.
Lionel Messi aliinyima Barcelona kuondoka na ushindi mnono zaidi baada ya mkwaju wake wa penati kuokolewa na kipa Joe Hart dakika za lala salama. Hiyo ilikuwa ni penati ya nne kwa Messi kukosa kati ya saba alizopiga katika msimu huu.
Kipigo hicho kinaifanya Manchester City kuwa na kazi yaziada ya kuhakikisha inapata ushindi usiopungua mabao 2-0 iwapo inataka kusonga mbele katia michuano hiyo iliyopenya hatua ya 16 Bora kibahati, vinginevyo mechi ya Machi 18 itakayochezwa Camp Nou huenda ikawa ndiyo ya kuagia michuano hiyo.
Katika pambano jingine la hatua hiyo ya mtoano, Juventus wakiwa uwanja wa nyumbani mjini Turin, Italia waliizabua Borussia Dortmund ya Ujerumani kwa mabao 2-1 na kuzidi kumpa wakati mgumu kocha Jurgen Klopp ambaye kikosi chake kimekuwa na matokeo mabaya msimu huu kwenye ligi ya nyumbani ya Bundesliga.
Carlos Tevez na Alvaro Morato ndiyo walioinusisha Juventus harufu ya kucheza robo fainali baada ya kila mmoja kufunga bao katika muda usiozidi nusu saa huku, wageni wakifuta machozi kwa bao la Marco Reus.
Tevez alitangulia kufunga katika dakika ya 13 kabla ya wageni wao kulisawazisha kupitia kwa Reus dakika tano baadaye na Morata kuongeza la pili dakika ya 42 akimaliza pasi nzuri ya Paul Pogba na kuifanya Juventus kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kabla ya mechi yao ya marudiano itakayochezwa nchini Ujerumani Machi 18.

Kocha Spurs awaonya nyota wake pambano la Fiorentina

KOCHA wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino amewaonya wachezaji wake akiwataka kuichukulia pambano lao la marudiano ya Ligi Ndogo ya Ulaya wakiwa ugenini dhidi ya Fiorentina ya Italia kama pambano la fainali.
Pochettino amewataka wachezaji wake wasiweke akili zao kwa pambano la Fainali za Kombe la Ligi (Capital One) dhidi ya Chelsea litakalochezwa Jumapili kwenye uwanja wa Wembley na kujisahau mbele ya Fiorentina iwapoa wanataka kutinga 16 Bora.
Spurs itavaana Chelsea kwa mara ya kwanza kwenye uwanja wa Wembley tangu mwaka 2008 na kocha huyo amesisitiza wachezaji wake waelekeze nguvu kwa pambano hilo lakini wasisahau 'fainali' nyingine dhidi ya Fiorentina ambao walitoka nao sare ya 1-1 wiki iliyopita.
Pochettino alisema: Alhamisi (leo) litakuwa pambano gumu mno. Nafikiri itakuwa ni fainali ya kwanza kwetu kabla ya Jumapili, Fiorentina ni timu pekee ambayo itaweza kutuvusha hatua nyingine ya michuano ya Ligi Ndogo ya Ulaya."
"Tunajua tunahitajika kufunga baada ya sare ya 1-1 na tunajiamini. Tunajiamini na tunapaswa kuchukua tahadhari kwa mchezo hio wa Alhamisi. Tunapaswa kupambana ili tushinde na wachezaji wanapaswa kufanya hivyo," alisema kocha huyo kuyoka Argentina.
Kocha huyo aliongeza kuwa; "Hii ni fainali nyingine na tunahitaji kufanya maamuzi (ya nani acheze) kwa sababu tumetoka kucheza mechi ngumu dhidi ya Fiorentina na West Ham,".
Spurs ambao mwishoni mwa wiki walinusurika kipigo nyumbani kwa kutoka nyuma na kurudisha mabao mawili dhidi ya West Ham Utd na kutoka sare ya 1-1 watavaana na Fiorentina katika mjini ya Frolence wakihitajika kushinda au kupata sare ya mabao zaidi ya mawili ili kutinga 16 Bora ya michuano hiyo ambayo leo pi itashuhudiwa mechi kadhaa za marudiano kabla ya kujulikana timu 16 zitakazosonga mbele.
Mojha ya pambano linalosubiwa kwa hamu ni lile la Liverpool dhidi ya Besiktas ya Uturuki ambao katika mechi ya mkondo wa kwanza uwanja wa Anfied, Liverpool ilishinda bao 1-0 la mkwaju wa penati ya 'kulazimisha' ya Mario Balotelli.

Fainali za Qatar ni faida kwa Waingereza-Phil Neville

NYOTA wa zamani wa kimataifa wa Uingereza, Phil Neville amesema kuandaliwa kwa michuano ya Kombe la Dunia kati ya Novemba na Desemba mwaka 2022 nchini Qatar ni jambo zuri kuwahi kutokea kwa nchi yake.
Kikosi kazi cha Shirikisho la Soka la Dunia-FIFA kilipendekeza michuano hiyo kuhamishwa wakati wa majira ya baridi kwasababu ya joto kali nchini Qatar.
Wakati wadau wengi wakikosoa uamuzi huo, Neville yeye anafikiri michuano hiyo itakuwa na faida kubwa kwa matumaini ya Uingereza kunyakuwa taji hilo.
Neville anaamini katika kipindi hicho wachezaji wanakuwa bado wako vyema na tayari kwa ajili ya kupambana na timu bora duniani. Mapendekezo hayo ambayo yanatarajiwa kufikishwa mbele ya kamati ya utendaji ya FIFA itakayokutana jijini Zurich, Machi mwaka huu, tayari inaungwa mkono na Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA), Michel Platini, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), Concacaf na Shirikisho la Soka la Asia (AFC).

John Riise athibitisha kumuaga Gerrard

http://sillyseason.com/sites/default/files/styles/article_top/public/article_images/riise_gerrard_reut960_1212152704.jpg?itok=zL9GLXlT
Riise akiwa na nahodha wake wa zamani, Gerrard
John Arne Riise enzi akiitumikia Liverpool
LONDON, England
BEKI wa kushoto wa zamani wa kimataifa wa Norway, John Arne Riise amethibitisha kushiriki pambano maalum la kumuaga Nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard akiungana na nyota wengine wa klabu hiyo ya Anfield.
Mechi hiyo maalum inatarajiwa kuchezwa Machi 29 kwenye uwanja wa Anfield, ikiwarejesha nyota wa zamani wa Liverpool waliwahi kucheza na nahodha huyo ili kuaga kabla ya mwanasoka huyo wa kimataifa wa Uingereza ajahamia klabu yaLA Galaxy ya Marekani mwishoni mwa msimu huu.
Kupitia akaunti yake ya Instagram, Riise alithibitisha kuwa atakuwa miongoni mwa watakaokuwapo Anfield kumuaga Gerrard katia pambano hilo litakalohusisha kikosi cha sasa cha Liverpool na kikosi cha zamani cha mabingwa hao wa zamani wa England na Ulaya.
Nyota wengine watakaoshiriki pambano hilo ni Fernando Torres 'El Nino', Xabi Alonso, Pepe Reina, Javier Mascherano na Luis Suarez ambao wameshathibitisha kucheza pambano hilo, huku Riise akimtaja pia Luis Garcia naye atakuwapo.
"Najisikia fahari kubwa kwa kuwalikwa kwenye pambano la hisani la Steven Gerrard la Machi 29, sio la kusubiri kushuhudia magwiji waliocheza pamoja kushuka tena dimbani ," aliandika Riise.

Monday, February 23, 2015

Mzigo mpya wa Izzo Bizness ft Shaa-Kidawa

Irene Uwoya aibarishia Kisoda kufunika 2015

https://40.media.tumblr.com/49d4dc38db37ae6d8398d8d9c5ab75c0/tumblr_n6yqbutuDQ1rtmw2wo1_500.jpg
Irene Uwoya
MSANII nyota wa filamu, Irene Uwoya, amesema kuwa anaamini filamu yake ijayo ya 'Kisoda' itakuwa funika bovu kuliko 'Apple' ambayo aliitoa mwaka mmoja uliopita.
Akizungumza na MICHARAZO, Irene anayefahamika kama 'Oprah' au Mama Krish, alisema kuwa kwa namna filamu hiyo ilivyotengenezwa kwa ubora wa hali ya juu ya kushirikisha nyota mbalimbali wa Tanzania na wale wa kimataifa ana imani ya kufunika 2015.
Irene alisema ingawa siyo vema kuanza kujisifia kabla hata filamu hiyo haijainguia sokoni, lakini anawataka mashabiki wake kuisubiri kuipokea kabla ya Pasaka kuweza kuthibitisha maelezo yake.
"Huwa sina utamaduni wa kupenda kujifagilia, lakini mashabiki wangu waisubiri 'Kisoda' waone utofauti, naamini itafunika kuliko hata 'Apple'," alisema Irene ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Apple Film Production.
Irene alisema kuna mambo yaliyokwamisha filamu hiyo kutoka mapema kama alivyokuwa amepanga, lakini mara baada ya kuhaririwa itaachiwa na kufanyiwa uzinduzi wake kabla ya Pasaka inayotarajiwa kuadhimishwa mwanzoni mwa Aprili.

Twiga Stars waingia kambini kujiwinda kimataifa

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiAZV4PJLK51AfIOWLOo-LS5q0FtMrlxask2Emm9hlzaIXdFSfvk8D33r9A9WSNUG4UKAQzsdUe81YTuke-D4AvaFFQMl-HBoHd_nOp0iXI0NJsfzUIYWQH-LL_wbKgMm7NLqRX0BLqbOQ/s1600/KAIJAGE.JPG
Kocha wa Twiga Stars
http://api.ning.com/files/STHDuz-8NrUpchIxJtAG7Yhc*bs7v9f6guq0lMwxNXrwwbY8mQyceglvUwtFfk9Y9Lg8A7-*-yAlwpgOnTx01kmvHI749vQs/TWIGA.JPG
Baadhi ya nyota wa Twiga Stars walioitwa kambini
KIKOSI cha wachezaji 30 kilichoitwa na Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Wanawake Tanzania (Twiga Stars), Rogasian Kaijage kimeingia kambini tayari kwa maandalizi ya mchezo wa kufuzu Fainali za Mataifa Afrika dhidi ya Zambia utakaodfanyika mwezi ujao.
Kaijage ametangaza programu yake ya  mazoezi itakayochukua takribani wiki nne (4) ili kuhakikisha wachezaji wanakua tayari kwa ajili ya mchezo huo utakaochezwa kati ya Machi 21, 22 mwaka huu, huku akipanga kucheza mchezo mmoja wa kirafiki kabla ya kuelekea Lusaka Zambia kwenye mchezo wa awali.
Twiga Stars ambayo imeingia kambini jana Jumapili na itakuwa kwenye Hosteli za Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF zilizopo Karume,  imefuzu moja kwa moja katika hatua ya pili kucheza na Zambia kufuatia kuwa na matokeo mazuri katika msimamo wa viwango vya soka la wanawake barani Afrika.
Wachezaji walioitwa na kuingia kambini ni pamoja na Asha Rashid 'Mwalala', Esther Chaburuma 'Lunyamila', Fatuma Bushiri, Fatuma Hassan, Fatuma Mustapha, Fatuma Omari, Eto Mlenzi, Mwajuma Abdallah, Sofia mwasikili, Zena Khamis, Mwanahamis Omar, Fatuma Khatibu, Fadhira Hamad, Anastazia Anthony, Shelder Boniface.
Wengine ni Thereza Yonna, Happines Hezron, Amina Ally, Donizia Daniel, Fatuma Issa, Vumilia Maarifa, Maimuna Hamisi, Najiati Abbasi, Stumai Abdallah, Ziada Ramadhani, Zuwena Aziz, Irene Joseph, Dawa Haji Vuai, Belina Julius na Amina Ramadhani.

Mwili wa Mez B kuzikwa leo mjini Dodoma

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEimP0azU_N4UKy6iarXropB_bWlOXWyV6TN5j6W57e0WoMdC59awKdXuKv1AnvZJsNTfAnaLl4hqWKSUST5yF0bw1uTgBWXiPY-qT4tXAdnHOjdm9QuoqHdYBs2IVm5TJMJYuzSB7BZJzk/s1600/Mez-B1.jpg 
http://laurent.antibi.perso.sfr.fr/WEBSITE/SiteV2/Mez%20B%20-%20Kama%20Vipi.jpg 
MWILI wa msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya, Moses Bushagama maarufu kama Mez B aliyefariki dunia Ijumaa iliyopita wakati akikimbizwa hospitalini unatarajiwa kuzikwa leo katika Makaburi ya Wahanga wa Treni yaliyopo Mailimbili  mjini Dodoma.
Taarifa iliyotolewa na mama yake  Mez B, Merry Katambi alisema  shughuli ya kumuaga mwanae itafanyika Viwanja vya Nyerere Square Mjini hapa.
Mazishi hayo kwenye viwanja vya Nyerere yataambatana na ibada ya kumuombea na yanatarajiwa kuanza saa saba mchana.
"Mwanangu tutamzika Jumatatu (leo) katika Makaburi ya wahanga wa Treni Mailimbili ila ibada pamoja na kuuga mwili wa marehemu zitafanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere’’ 
Mez B alikuwa ni mwanzilishi wa kundi la Chemba Squard ambapo alikuwa pamoja na Dar Master, Noorah na Albert Mangwea huku akitamba na nyimbo za 'Kikuku cha Mama Rhoda', 'Nimekubali' na 'Kama Vipi iliyomjengea jina kubwa kwa mashabiki wa muziki kabla ya 'kuzimika'.

Mourinho 'alianzisha' tena England, kisa sare na Burnley

http://news.bbcimg.co.uk/media/images/74475000/jpg/_74475524_74474959.jpgKOCHA Jose Mourinho wa klabu ya Chelsea, ameanzisha tena vita ya maneno na chama cha soka England, FA kufuatia kudai kuwa kampeni dhidi yake ya kuhakikisha hachukui ubingwa msimu huu inaendelea na kweli itawagharimu klabu yake.
Mourinho ameyasema hayo baada ya kutoka sare ya 1-1 na Burnley kwenye uwanja wa nyumbani wa Stamford Bridge ambapo amelaumu maamuzi ya mwamuzi Martin Alkinson.
Alkinson alimuonesha kadi nyekundu kiungo wa Chelsea, Nemanja Matic na atakosa mechi ya jumamosi ya fainali ya kombe la ligi dhidi ya Tottenham baada ya kadi nyekundu ya dakika ya 69.
Mourinho anadai Ashley Barnes alitakiwa kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya Martic na kulikosababisha kiungo wake amsukume mshambuliaji huyo wa Burnley na kuambulia kadi nyekundu.
Pia alitakiwa kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kitendo cha kumsukuma Branislav Ivanovic.
Mourinho anaamini haki haikutendeka ambapo walinyimwa penalti mbili kwani Michael Kightly aliunawa mpira wa shuti la Ivanovic katika dakika ya 33′ na nahodha wa Burnley Jason Shackell alimsukuma Diego Costa eneo la hatari dakika chache kabla ya mapumziko.
Chelsesa bao ipo kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 60, wajkifuatiwa kwa mbali na Manchester City ambao walitoa kipigo cha 'Paka Mwizi' kwa Newcastle United kwa kuizabua mabao 5-0 na kufikisha pointi 55.

Kocha Southampton kumuadhibu Sadio Mane, kisa...!

Southampton forward Mane battles for the ball with Liverpool midfielder Philippe Coutinho (right)
Sadio Mane akichuana na Coutinho katika mechi yao ya jana dhidi uya Liverpool na kulala nyumbani 2-0
MENEJA wa klabu ya Southampton, Ronald Koeman anakusudia kumuadhibu Sadio Mane kufuatia mshambuliaji huyo kuchelewa kufika katika mechi waliyopoteza 2-0 dhidi ya Liverpool usiku wa jana.
Mane alikuwepo katika kikosi kilichowakabili wakali wa Merseyside kwa kufika baada ya nusu saa kupita kutoka muda waliopanga kufika, saa saba mchana.
Pia mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Senegal anakabiliwa na adhabu nyingine ya kutozingatia muda.
“Alichelewa kwa dakika 25-30 kabla ya mechi”, amethibitisha Koeman.
“Tuna kanuni na maelekezo kwa wachezaji. Kila mtu anaweza kuchelewa siku moja asubuhi, lakini huwezi kuchelewa kufika saa saba wakati unacheza dhidi ya Liverpool.
“Hakutoa maelezo? Maelezo hayo ni baina ya kocha na mchezaji, lakini alichelewa.
‘Siwezi na sikubaliani na hilo. Kama ni kulipa faini alipe tu”

Mdudu wa sare ahamia Azam, yabanwa na Prisons

Azam waliolazimishwa sare isiyo na mabao na Prisons-Mbeya
MDUDU wa sare aliyekuwa ameiganda Simba, amehamia kwa mabingwa watetezi, Azam baada ya kulazimishwa sare ya kutokufungana na maafande wa Prisons-Mbeya ikiwa ni siku chache kuambulia sare nyingine kama hiyo na Ruvu Shooting Stars.
Sare hiyo ya pili mfululizzo kwa Azam imetoa nafasi kwa vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga kutanua pengo lake la uongozi hadi kuwa pointi nne licha ya timu zote mbili kucheza mechi 15 kila mmoja.
Yanga inaoongoza ikiwa na pointi 31 baada ya kuvuna pointi 6 jijini Mbeya kwa kuzichapa Prisons na Mbeya City kwa mabao 3-0 na 3-1, wakati Azam kwa kupoteza pointi nne wamekusanya pointi 27.

Pambano hilo la Azam an Prisons lilichezwa usiku kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi na sare hiyo isiyo na mabao imewapa afueni maafande wa Prisons waliofikisha pointi 12 baada ya kucheza mechi 15.

Sunday, February 22, 2015

Liverpool yaua, Spurs, Everton zabanwa nyumbani

Hivi ndivyo vita vya Liverpool na wenyeji wao Soputhmapton ilivyokuwa Victor Wanyama akichuana na Jordan Hendeson

WAKATI klabu ya Tottenham Hotspur ikilamizika kupigana kiume kurejesha mabao mawili ili wasife nyumbani mbele ya West Ham Utd, Liverpool wameendelea kutoa dozi kwa kuicharaza Southampton kwa mabao 2-0 katika mfululzii wa Ligi Kuu ya England.
Spurs ikiwa nyumbani ilitanguliwa kufungwa mabao 2-0 kabla ya kuyarejesha baadaye na kuambulia sare ya mabao 2-2, shukrani za pekee zieende kwa Harry Kane aliyefunga bao la kusawazisha baada ya awali kukosa penati na mpira kumrudia na kuutumbukiza wavuni.
Katika mchezo mwingine timu ya mkiani ya Leicester City ilijitutumua na kulazimisha sare ya ugenini ya mabao 2-2 dhidi ya Everton kabla ya hivi punde Liverpool kuandikisha ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Southampton.
Mabao ya Phillipe Coutinho katika dakika ya tatu na jingine la kipindi cha pili lililofungwa na Raheem Sterling liliwapa vijogoo hao wa Anfield kupata ushindi huo uliowafanya wafikishe jumla ya pointi 45 na kulingana Spurs ingawa wameshindwa kuiengua Southampton katika nafasi ya tano wakati ligi ikiwa ipo raundi ya 26.
Katika pambano hilo wenyeji walilalamika kunyimwa penati mbili za wazi baada ya wachezaji wao kufanyiwa madhambi langoni mwa Liverpool.

Mwadui Fc ndiyo mabingwa wa FDL2014-2015

Kocha wa Mwadui, Jamhuri Kihwelu 'Julio
http://shaffihdauda.co.tz/wp-content/uploads/2015/01/DSC_4165.jpg
Mabingwa wa FDL,. Mwadui Shinyanga walioizabua Wana Kimanumanu kwa bao 1-0
'KOCHA Jamhuri Kihwelu 'Julio'amedhihirisha kweli yeye ni bab'Kubwa baada ya kuiongoza timu yake ya Mwadui Shinyanga kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Africans Sports ya Tanga na kunyakua ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL).
Mwadui imeibuka na ushindi huo katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi na kuzima ngebe za wapinzani wao waliotamba awali kushinda pambano hilo kudhihirisha kuwa Mwadui ni 'vibabu'.
Hata hivyo tambo hizo za Wana Kimanumanu zilizimwa kwa bao tamu la kichwa lililofungwa na Kelvin Sabato 'Kiduku' na kuwapa taji Mwadui ambao waliongoza katika kundi lao la ligi daraja la kwanza na kupanda Ligi Kuu msimu wa 2015-2016 mwaka mmoja baada ya kubaniwa na TFF msimu uliopita.
Mbali na Mwadui, nyingine zilizopanda ligi hiyo msimu ujao kuchukua nafasi ya timu nne zitgakazoshuka katika Ligi ya msimu huu inayozidi kushika kasi ni Africans Sports, Toto Africans na Majimaji-Songea.

Mnyama afa Shinyanga, Stand Utd yaifanyizia

Kikosi cha Simba
BAADA ya kufanikiwa kuondoa 'gundu' kwa Polisi Moro na kudai walikuwa wameianza rasmia Ligi Kuu, klabu ya Simba leo ametolewa nishai ugenini mjini Shinyanga kwa kukubali kipigo cha bao 1-0.
Kipigo hicho kimetolewa kwa Simba na timu ya Stand United katika pambano tamu lililochezwa kwenyue uwanja wa Kambarage na kuzima mbwembwe za vijana wa Msimbazi huku mashabiki wao wakiibua zogo.
Zogo hilo lililosababisha pambano hilo kusimama kwa muda ilitokana na imani kwamba lango la wapinzani wao lilikuwa limefukiwa 'vitu' ambavyo vilikuwa vikiwafanya vijana wao kushindwa kufunga mabao.
Bao pekee lililowaua Simba ya kocha Goran Kopunovic, liliwekwa kimiani na Mnigeria Absalim Chiibibele likiwa ni bao lake la tano msimu huu katika dakika ya 11 na kuwafanya Simba kuhaha kurirejesha bila mafanikio.
Kwa kipigo hicho Simba imesaliwa na pointi pointi 20 baada ya mechi 16 wakati Stand imefikisha pointi 18 baada ya mechi 16 pia na itavaana na Kagera Sugar katika mechi yao ijayo mjini Shinyanga.

Yanga 'watamu' kama Mcharo! Yaifumua Mbeya City

Simon Msuva aliyeanza kufungua neema ya mabao Mbeya leo
Mrisho Ngassa  akadhihrisha amerejea upya Jangwani
Amissi Tambwe akamaliza udhia kwa kufunga bao la tatu
MABAO matatu kutoka kwa Simon Msuva, Mrisho Ngassa na Amissi Tambwe yameiwezesha Yanga kupata ushindi wa pili mfululizo jijini Mbeya baada ya kuicharaza Mbeya City kwa mabao 3-1.
Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ulichezwa kwenye uwanja wa Sokoine na kuiwezesha Yanga kuibuka na ushindi huo mnono ulioifanya izidi kujizatiti kileleni ikiwa na pointi 31 baada ya mechi 15.
Simon Msuva alianza kufunga katika kipindi kwanza kabla ya Ngassa 'kuzawadiwa' bao mara baada ya kipindi cha pili kutokana na mbwembwe za kipa David Burhan wa Mbeya City kumpoza.
Kipa huyo Bora wa msimu wa 2012-2013, alirudishiwa mpira na Steven Mazanda na badala ya kuupiga mbele alijaribu kumpiga chenga Ngassa aliyeunasa kilaini na kutumbukiza wavuni kaundika bao la pili la Yanga.
Amissi Tambwe aliunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Haruna Niyonzima na kuiandikia bao la tatu, wakati huo tayari wenyeji alishapata bao la kufutia machozi kupitia kwa Peter Mapunda.
Bao hilo la Mapunda limeitibua rekodi ya kipa Ally Mustafa 'Barthez'ambaye alikuwa amecheza muda wa dakika 704 bila kuruhusu wavu wake kutikiswa. Dakika hizo ni 630 za mechi sita na 74 za leo kabla ya Mapunda kumtungua kufuatia mabeki wake kushindwa kuokoa.
Kwa ushindi huo Yanga imejikita kileleni ikiwa na pointi 31 baada ya mechi 15 ikijiandaa kuondoka nchini kwenda Botswana kurudiana na BDF XI katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Simanzi! Christopher Alex hatunaye duniani!

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgTo5gnxm0hxL2vl32ZTdKTWURp8bI9AhqxaS4u79wBsu7mcRP0Bn9ulEdWLFZaFH-QzfMXd4561SJIzpTRzFR-0cOFzLUd4bEqUojYVciaPBRvmiskU_my2Mc8MEQgDkCBkGg0-aT8C85u/s1600/426453_235934163168144_100002546855024_482737_173110702_n.jpg
Christopher Alex (wa tatu toka kulia) enzi za uhai wake akiwa na kikosi kilichoing'oa Zamalek mwaka 2003
KIUNGO nyota wa zamani wa klabu ya Simba na timu ya taifa, Taifa Stars, Christopher Alex Massawe amefariki dunia asubuhi ya leo.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo MICHARAZO imezipata mapema zinasema kuwa, kiungo huyo aliyekuwa akiugua kwa muda mrefu amefariki akiwa kalazwa katika Hospitali ya Milembe, iliyopo mkoani Morogoro.
Alex, anayekumbukwa kwa kupiga penati ya mwisho ya Simba iliyowavua ubingwa Zamalek ya Misri katika pambano la Ligi ya Mabingwa kati yao iliyochezwa mwaka 2013, alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya kifua.
Mama mzazi wa Alex amethibitisha kutokea kwa kifo hicho ambaye alikuwa akiishi naye na kumuuguza kwa msaada wa wasamaria wema wakiwamo wadau wa soka.
Wakati klabu yake ya zamani ikiwa 'ímemsusa', mashabiki wa klabu hiyo na wengine wa soka walikuwa bega kwa bega na mama huyo kwa kuchangia fedha za matibabu, harambe kubwa ikiendeshwa na kituo cha Cloud's FM
Marehemu Christopher Alex, alizaliwa Septemba 12, 1975, na kupata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Uhuru na kumaliza katika shule ya Chamwino huko Dodoma mwaka 1993.
Alianza kucheza mpira kwenye timu ya daraja la nne ya Chamwino Utd na baadaye daraja la tatu akiwa na kikosi cha Aston Villa nayo ya Dodoma.

Mwaka 1999-2001, aliitumikia klabu ya CDA ya Dodoma, kabla ya kutimkia klabu ya Reli ya Morogoro mwaka 2002, na baadaye kujiunga na Wekundu wa Msimbazi Simba.
Marehemu ameacha mtoto mmoja aitwaye Alex.
MICHARAZO inatoa pole kwa ndugu, jamaa na familia nzima ya marehemu Alex kwa msiba huo na kuwaombea Subira kwa Mungu kwa kukumbuka kuwa 'Kila Nafsi Itaonja Mauti'
Mungu aiweke roho ya marehemu Alex Mahali Pema Ameen!

Bingwa wa FDL kujulikana leo Chamazi

http://shaffihdauda.co.tz/wp-content/uploads/2015/01/DSC_4165.jpg
Mwadui Shinyanga
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhX4CPi_gLzDiNDFJxODqQK-bun_Lz_-fqogmOSBafonpNyQztxKsciMrA9kx7T2CAkfa14juJT5WVK1BxZPxkqTuD40uPWHMTtpatpKUHMvQpdWau2Aw3yYJfbYrgwYFAnwHWaIEFpT7c/s1600/sports.JPG
Africans Sports 'Wana Kimanumanu'
FAINALI za kusaka Bingwa wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL), zinafanyika leo kwa pambano kati ya Mwadui Shinyanga dhidi ya Africans Sports mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi kuanzia majira ya saa 10 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Awali mchezo huo wa fainali ulikuwa umepangwa kufanyika kwenye dimba la Uwanja wa Taifa, lakini kutokana na sababu zilizopo nje ya uwezo wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF imepelekea mchezo huo kuhamishiwa Chamazi.
Mchezo huo wa fainali utaanza saa 10 kamili jioni, na utaonyeshwa moja kwa moja na kituo cha Azam TV ili kuwapa nafasi wapenzi na wadau wa soka waliopo mbali na hasa mikoani kuweza kushuhudia mchezo huo.
Bingwa wa Fainali ya Ligi Daraja la Kwanza atazawadiwa Kombe pamoja na medali, huku mshindi wa pili akipata kikombe na medali pia.
Viingilio vya mchezo huo ni tsh.5,000 kwa jukwaa kuu na tsh. 3,000 kwa majukwaa ya mzunguko.

Mo Farah aweka rekodi ya dunia

http://e0.365dm.com/15/02/660x350/mo-farah-birmingham-indoor-two-mile-record_3267495.jpg?20150221163812
Mwanariadha Mo Farah akimaliza mbio na kuweka rekodi mpya Birmingham
LONDON, England
MWANARIADHA Muingereza Mo Farah amevunja rekodi ya dunia ya mbio za ndani za Maili Mbili katika mbio za Birmingham Indoor Grand Prix.
Farah, 31, aliondoka uwanjani baada ya kumaliza mbio hizo kwa kutumia dakika 3.40 akiivunja rekodi iliyotanguliwa iliyowekwa na Muethiopia Kenenisa Bekele.
Hiyo ni rekodi ya kwanza kuwekwa na mwanariadha huyo bingwa mara mbili wa Olimpiki.
"Hii ina maana kubwa kwangu, " alisema Farah. "Napenda kuliwakilisha taifa langu, kutoa kitu fulani kwa watu wote. Siamini. "
Maandalizi ya kabla ya kuanza kwa mbio hizo za Jumamosi yalitawaliwa na malumbano dhidi ya mchezaji mwenzake Muingereza Andy Vernon.
Farah alidai kuwa Vernon alihoji uraia wake baada ya bingwa huyo mara mbili wa Olimpiki kushinda mbio za Ulaya za mita 10,000 mwaka 2014, huku Vernon akielezea kuwa huo ulikuwa ni upotoshaji mkubwa.
Pamoja na suala hilo lakini Farah hakutetereka kwani alitawala mbio hizo zilizofanyika jijini Birmingham, na kuwaacha Mkenya Paul Koech na Mmarekani Bernard Lagat na kushinda mbio hizo.
"Ni (malumbano na Vernon) ndio yaliyonihamasisha mimi, nilitaka kufanya hivyo, " alisema Farah.

Simba, Yanga Azam katika vita nyingine VPL

Kikosi cha Simba kitakachokuwa mjini Shinyanga,

Azam watakuwa uwanja wa nyumbani wa Chamazi
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhErXyx1Zkj3OCoFFiXSN67k52f3gi-xri1jU6EVAQNSzUHaLOE-aGYio6UwnJav0_qsoTFjW-lII6MoCyTEDN6NO6aDEosezFiW3YLR8VtXdxto3puBagAfzT7oBKaY4iLz98CetK57ihU/s1600/IMG_0916.JPG
Kikosi cha Yanga kilichopo ugenini jijini Mbeya kuvaana na Mbeya City
VIGOGO vya Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, Yanga na Azam zitakuwa kwenye viwanja tofauti kwa ajili ya kusaka pointi tatu muhimu katika mbio za kuwania ubingwa wa ligi hiyo.
Vinara Yanga wenyewe watakuwa kwenye uwanja wa Sokoine kwa mara nyingine tena kupepetana na wenyeji wao Mbeya City, ikiwa ni siku chache baada ya kugawa dozi ya mabao 3-0 dhidi ya Prisons.
Simba walioanza kushika kasi katika ligi hiyo baada ya kuchechemea kwa muda mrefu, pia ipo ugenini mkoani Shinyanga kwa ajili ya kupepetana na Stand United  kwenye uwanja wa Kambarage.
Mabingwa watetezi Azam watakuwa uwanja wa nyumbani wa Azam Complex, Chamazi kuikaribisha Prisons-Mbeya baada ya katikati ya wiki kubanwa mbavu na Ruvu Shooting na kutoka suluhu ya 0-0.
Yanga watakuwa na hamu ya kuendeleza rekodi yao ya kushinda mfululizo, ingawa Mbeya City ambayo imekuwa haina msimu mzuri safari hii ikiwa imeapa kumaliza uteja kwa wapinzani wao hao.
Mbeya City iliyopanda ligi kuu msimu uliopita, haijawahi kuifunga Yanga zaidi ya kulazimisha sare au kuambulia vipigo, kitu ambacho Kocha wake, Juma Mwambusi anaamini leo watavunja mwiko.
Hata hivyo Yanga imetamba kutaka kutoa dozi kwa lengo la kuongeza morali kabla ya kuondoka nchini kwenda Botswana kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya BDF XI.
Yanga inayoongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 28, mbili zaidi ya Azam yenye 26 itarudiana na BDF wiki ijayo mjini Gaborone baada ya wiki iliyopita kuwacharaza mabao 2-0.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro alisema hawaoni cha kuwazuia kuvuna pointi nyingine tatu jijini Mbeya wakati kikosi chao kimeandaliwa vema na kina morali mkubwa.
Muro alisema anafahamu Mbeya City ni timu ngumu na itataka kutumia vema uwanja wa nyumbani, lakini Yanga imejipanga kutoka na pointi zote ili kujikita zaidi kileleni kabla ya kwenda Botswana.
Wakati Yanga na Mbeya wakiwindana hivyo, Simba wenyewe wakiwa na furaha ya ushindi wa mabao 2-0 iliyopata ugenini mjini Morogoro dhidi ya Polisi wataivaa Stand United wakiwa na tahadhari kubwa.
Stand Utd imetoka kuwatoa nishai Mgambo JKT kwa kuicharaza mabao 4-1, kitu ambacho kinaonyesha namna gani wameanza kuizoea ligi hiyo wanayoicheza kwa msimu wao wa kwanza.
Katika pambano hilo kila timu itakuwa ikitegemea nyota wake, Simba ikitambia akina Emmanuel Okwi, Dan Sserunkuma, Eliasi Maguri na wengine huku Stand ikimtegemea Mnigeria Abasalim Chiibibele na Heri Mohammed wenye mabao manne kila mmoja katika ligi hiyo.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Oktoba 4, mwaka jana timu hizo zilizoshindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1 kwenye uwanja wa Taifa.
Angalia msimamo wa Ligi Kuu ulivyo:

                                P   W    D    L    F    A   GD Pts
01. Yanga               14  08   04  02  18  07  11  28
02. Azam                14  07   05  02  22  12  10  26
03. Kagera Sugar    16  06   06  04  13  11  02  24
04. Simba               14  04   08  02  15  11  04  20
05. Ruvu Shooting  15  05   05  05  10  11  -1   20
06. Mtibwa Sugar    15  04   07  04  15  15  00  19
07. Coastal Union   16   04  07   05  11  11  00  19
08. Polisi Moro        16  04   07   05  12  14  -2  19
09. JKT Ruvu          15  05  04  06   14   15  -1  19
10. Ndanda Fc        16  05  04   07  14   18  -4  19
11. Mbeya City       14  04  05  05   09   11  -2   17
12. Mgambo JKT    14  05  02  07   08    15  -7  17
13.Stand Utd         15  03  06   06   13   18  -5  15
14. Prisons            14  01  08   05   10   15  -5   11
Wafungaji:
8-
Didier Kavumbagu(Azam)

7- Rashid Mandawa (Kagera Sugar)
6-
Samuel Kamuntu (JKT Ruvu), Ame Ali (Mtibwa), Simon Msuva (Yanga),
5-
Danny Mrwanda (Yanga), Kipre Tchetche (Azam)
4- Rama Salim (Coastal),  Emmanuel Okwi (Simba), Nassor Kapama, Jacob Massawe (Ndanda), Heri Mohammed, Abasalim Chiibibele (Stand Utd) , Malimi Busungu (Mgambo)
3- Ally Shomari (Mtibwa), Frank Domayo (Azam), Atupele Green (Kagera)
2-
Shaaban Kisiga, Dan Sserunkuma, Elias Maguli (Simba), Salum Kanoni, (Kagera Sugar) Aggrey Morris (Azam),  Najim Magulu, Jabir Aziz (JKT Ruvu), Amissi Tambwe, Jerry Tegete, Mrisho Ngassa, Andrey Coutinho (Yanga), Ibrahim Kihaka (Prisons), Mussa Mgosi (Mtibwa), Mussa Said (Stand Utd), Ally Nassor (Mgambo), Nicolaus Kabipe (Polisi),Yahya Tumbo (Ruvu Shooting)