STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, January 13, 2014

Uganda The Cranes waanza vyema CHAN 2014


Man of the match Yunus Ssentamu celebrates his second goal against Burkina Faso
Sentamu akishangilia bao lake la pili

VINARA wa kandanda Kanda ya Afrika Mashariki, Uganda The Cranes imeanza vyema kampeni zake za kuwania ubingwa wa fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) baada ya kuisambaratisha Burkina Faso kwa mabao 2-1 katika pambano la kundi B lililochezwa usiku wa jana.
Mabao mawili kutoka kwa aliyekuwa nyota wa mchezo huo, Yunus Sentamu moja kila kipindi yalitosha kuiweka Uganda kileleni mwa kundi hilo ikifikisha pointi tatu na mabao mawili, huku Burkina Faso wakienda mpaka mkiani ikiwa haina pointi yoyote.
Sentamu alifunga bao la kwanza kwenye dakika ya 15 kabla ya kuongeza jingine dakika ya 73 na wapinzani wao kupata bao la kufutia machozi dakika mbili kabla ya kumalizika kwa pambano hilo kupitia kwa Cyrille Bayala.
Michuano hiyo itaendelea tena jioni ya leo kwa mechi za kundi C, Ghana kuvaana na Jamhuri ya Congo na Libya kukabiliana na wawakilishi wengine wa ukanda wa CECAFA, Ethiopia.

Sunday, January 12, 2014

Simba, KCC hapatoshi kesho Fainali Kombe la Mapinduzi

kikosi cha Simba
KCC ya Uganda
 KIVUMBI cha michuano ya Kombe la Mapinduzi kinatarajiwa kumalizika kesho kwa pambano la Fainali kati ya Simba dhidi ya KCC ya Uganda litakalochezwa jioni kwenye uwanja wa Amaan, visiwani Zanzibar.
Simba inaivaa KCC baada ya kuitoa nishai URA pia ya Uganda kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Mganda Joseph Owino, aliyekuwa akiichezea timu hiyo kabla ya kurejea Msimbazi na lile la Amri Kiemba.
KCC wenyewe waliwavua ubingwa Azam kwa kuwakandika mabao 3-2, licha ya kutanguliwa kufungwa 2-1 hadi wakati wa mapumziko.
Simba iliyowahi kunyakua taji hilo miaka miwili iliyopita, itakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha Kombe hilo halichukuliwi na wageni kwani tangu ilipoanzishwa michuano hiyo taji hilo halijawahi kutoka nje ya Tanzania.
Ikiwa chini ya kocha Zdrakov Lugarosic, Simba itaendelea kuwategemea wachezaji wake nyota Ramadhani Singano, Harun Chanongo, Amri Kiemba na golini atakuwa Ivo Mapunda kuhakikisha KCC hawafuruki katika mchezo huo wa fainali unaotarajiwa kuhudhuriw ana viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wale wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikizingatiwa kesho ni mapumziko kitaifa.
KCC ambayo haikuwa ikipewa nafasi kubwa, kabla ya kuja kuongoza kundi A walilokuwa na Simba katika mechi za awali siyo timu ya kubeza kwani imetoa upinzani mkubwa ikiwa haijafungwa mchezo wowote kama wapinzani wao ambao wana nyongeza ya rekodi ya kutoruhusu bao lolote langoni mwao mpaka sasa.
Timu huyo ya Jiji la Kampala inawategemea wachezaji wake kadaa nyota kama Ibrahim Kiiza na wengine ambao waliisimamisha Azam na kuwavua taji katika mechi ya Nusu Fainali ya kwanza juzi.
Uongozi wa Simba umenukuliwa jioni hii toka Zanzibar wakisema kikosi chao kipo imara tayari kuwapa raha Wazanzibar wanaosherehekea miaka 50 ya Mapinduzi na watanzania kwa ujumla ili kulibakisha taji hilo katika ardhi ya Tanzania kwa kuwazuia KCC wasiondoke nalo kama walivyofanya dada zao wa netiboli walioifunga timu ya taifa ya Tanzania kwenye fainali pia juzi.

Liverpool yatakata, Suarez nouma!

Liverpool's Steve Gerrard scores from the spot
Gerrard akitupia kambani bao la penati la Liverpool

LUIS Suarez ameendelea kuonyesha dhamira yake ya kunyakua kiatu cha dhahabu cha Ufungaji Bora wa Ligi Kuu ya England baada ya muda mfupi uliopita kufunga mabao mawili na kufikisha mabao 22 wakati akisaidia Liverpool kupata ushindi mnono ugenini wa mabao 5-3 dhidi ya Stoke City.
Suarez alifunga mabao hayo katika dakika za 32 na 71, huku wachezaji waliokuwa majeruhi nahodha Steven Gerrard na Daniel Sturridge wakifunga bao moja moja, Gerrard akifunga kwa mkwaju wa penati, huku bao la kuongoza la Liverpool likifungwa na beki wa Stoke City, Ryan Shawcross dakika ya 5 tu ya mchezo huo uliochezwa kwenye uwanja wa Britannia.
Sturridge alifunga bao la tano dakika tatu kabla ya kumalizika kwa pambano hilo akitokea benchi, huku wenyeji wakipata mabao yao ya kufutia machozi kupitia kwa  Peter Crouch, Charlie Adam na Jonathan Walters.
Kwa ushindi huo Liverpool imefikisha jumla ya pointi 42 na kurejea kwenye nafasi ya nne ikiishusha Everton na Tottenham ambazo jana zilitakata na ushindi wa mabao mawili kila moja.

Zimbabwe yaibana Morocco CHAN 2014

http://upload.wikimedia.org/wikipedia/en/8/8d/2014_African_Nations_Championship.png
TIMU ya soka ya taifa ya Zimbabwe imefanikiwa kuvuna pointi moja mbele ya Morocco baada ya kutoka nayo suluhu ya kutofungana katika pambano la kundi B la Michuano ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani iliyoanza jana nchini Afrika Kusini.
Pambano hilo lililochezwa kwenye uwanja wa Athlone, mjini Cape Town lilikuwa la vuta nikuvute kwa muda wote wa dakika 90 na kushuhudiwa timu hizo zikikosa mabao ya wazi na kufanya matokeo kuwa 0-0.
Mechi nyingine ya kundi hilo inatarajiwa kuanza hivi punde kati ya Uganda The Cranes itakayoumana na Burkina Faso kwenye uwanja huo huo wa Athlone.
Kesho katika mfululizo wa michuano hiyo iliyoasisiwa mwaka 2008,  Ghana itaumana mapema na Congo kabla ya Libya kuvaana na Ethiopia katika mechi za Kundi C na mechi za raundi ya kwanza zitamalizika Jumanne kwa mechi za kundi D kati ya DR Congo dhidi ya Mauritania na Gabon kuumana na Burundi.

Juventus haikamatiki Seria A, Roma, Napoli nazo zaua Italia

TIMU ya Juventus imeendelea kujikita kileleni baada ya kupata ushindi ugenini dhidi ya Cagliari, huku Roma na Napoli nazo zikipata ushindi wa kishindo katika mechi zao za Seria A jioni ya leo.
Juventus kwa ushindi huo wa mabao 4-1 dhidi ya wenyeji wao imeifanya ifikishe pointi 52 na kufuatiwa na Roma  yenye 44 baada ya kushinda nyumbani mabao 4-0 dhidi ya Genoa na Napoli kushinda mabao 3-0 na kujikita nafasi ya tatu ikiwa na pointi 42.
Mechi nyingine za leo katika Seria A imeshuhudia Fiorentina ikipata sare ya 0-0 ugenini dhidi ya Torino na  Atalanta ikishinda nyumbani 2-1 dhidi ya Catania.

Manchester City yaiua Newcastle kwao, na kuing'oa Chelsea kileleni

Edin Dzeko akishangilia bao lake dhidi ya Newcastle



BAO la mapema lililofungwa na Edin Dzeko katika dakika ya nane na jingine la dakika za lala salama kupitia kwa Alvaro Negredo yametosha kuipaisha Manchester City hadi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England wakiiporomosha Chelsea iliyokwea nafasi hiyo jana.
City wakiwa ugenini kuifuata Newcastle United iliweza kupata mabao hayo na kuifanya ifikishe pointi 47, moja zaidi ya ilizonazo Chelsea iliyoibamiza Hull City nyumbani kwao kwa mabao 2-0.
Dzeko alifunga bao la kwanza akimalizia kazi nzuri ya beki wa pembeni wa City, Aleksandar Kalarov kabla ya Negredo kuwaduwaza wenyeji dakika za nyongeza kwa kufunga bao la pili na kuifanya City imalize mechi hiyo ikiwa vidume, ikiwa ni mechi yao ya sita mfululizo kushinda katika Ligi.
Hata hivyo vijana hao na Manuel Pelligrini wanaweza kusalia kwa muda tu kileleni hapo kama Arsena ambayo kesho itashuka dimbani itapata ushindi ugenini dhidi ya Aston Villa katika mechi pekee ya ligi hiyo.
Hivi punde pambano la Stoke City dhidi ya Liverpool litaanza kuchezwa katika mfululizo wa ligi hiyo.

Afrika Kusini, Mali waanza vyema CHAN 2014

Wachezaji wa Bafana Bafana wakishangilia ushindi wao jana dhidi ya Msumbiji

TIMU ya taifa ya Nigeria jana ilianza vibaya michuano ya CHAN baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 toka kwa Mali huku wenyeji wa michuano hiyo inayohusisha wachezaji wanaocheza ndani ya Afrika, ikipata ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Msumbiji.
Katika mechi ya wenyeji iliyochezwa uwanja wa Cape Town, jijini Cape Town, Msumbiji iliwashtua wenyeji wao kwa kupata bao la kuongoza lililofungwa kwenye dakika ya 11 kupitia Diogo.
Bao hilo lilikuja kurejeshwa na Bernard Parker katika dakika ya 30 kwa mkwaju wa penati na kufanya hadi mapumziko timu hizo kuwa nguvu sawa  kwa bao 1-1.
Kipindi cha pili kilikuwa cha wenyeji baada ya kujipatia mabao mawili kupitia kwa Hlompho Kekana na Parker kwa mara nyingine tena na kufanya Afrika Kusini kuzoa pointi tatu na kuongoza kwenye kundi lake la A ikifuatiwa na Mali waliowazabua majirani zao Nigeria kwa mabao 2-1.
Mabao ya washindi yalifungwa na Abdoulaye Sissoko katika dakika ya 11 na Adama Troure la dakika ya 54 kabla ya Nigeria kupata bao la kufutia machozi lililofungwa na Fuad Salami.
Jioni hii kuna mechi nyingine mbili zinazoendelea ambako Zimbabwe na Morocco mpaka sasa hazijafunga zikikaribia kwenda mapumziko na mechi ya Uganda The Cranes na Burkina Faso itafanyika usiku na MICHARAZO itawaletea matokeo yake.

Tanzia! Nyota wa zamani wa Reli, Taifa Stars afariki


Boniface Njohole enzi za uhai wake (Picha: Mtanda Blogu)
MCHEZAJI wa zamani wa klabu ya Reli ya Morogoro na Taifa Stars, Boniface Njohole amefariki dunia katika kijiji cha Mngeta tarafa ya Ifakara wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro. 
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mkoani Morogoro Karibu Mtendaji wa chama cha soka mkoa wa Morogoro (MRFA) Hamis Semka alisema Njohole amefariki dunia katika kijiji cha Mngeta majira ya saa 5:30 asubuhi baada ya kuumwa kwa muda mrefu.
Hata hivyo taarifa zaidi zinasema kuwa Njohole aliyekuwa akifahamika kama Boni, alikuwa akisumbuliwa na matataizo ya Figo na alikuwa akitibiwa Moshi, kabla ya kurejeshwa nyumbani kwake Ifakara na kukutwa na mauti. 
Taarifa zaidi zinaendelea kufuatiliwa kujua mazishi na taratibu nyingine juu ya msiba wa mwanandinga huyo
MICHARAZO inatoa pole kwa ndugu, jamaa na wadau wote wa soka kwa msiba wa Boniface Njohole na kutakia moyo wa subira kwa kutambua kuwa Kila Nafsi Itaonja Mauti. Mungu Aiweke Roho ya Marehemu Mahali Pema. Ameen

TFF yamlilia Sultan Sikilo

Jeneza la Mwili wa Sultan Sikilo likiswaliwa kabla ya kwenda kuzikwa jana, jijini Dar es Salaam..
Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mtangazaji wa michezo wa Radio Abood, Sultan Sikilo kilichotokea jana alfajiri (Januari 11) jijini Dar es Salaam.

Sikilo ambaye pia aliwahi kufanyia kazi Radio Times na Radio Kheri na hadi umauti unamkuta alikuwa Mweka Hazina Msaidizi wa Chama cha Waandishi wa habari za Michezo Tanzania (TASWA) amezikwa jana jioni katika makaburi ya Kibada, Kigamboni.

Msiba huo ni mkubwa katika sekta ya habari na mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Sikilo alifanya kazi na TFF kwa kuripoti shughuli zetu nyingi za mpira wa miguu, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Sikilo, Radio Abood na TASWA na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Pia TFF imetoa ubani wa sh. 100,000 kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake.

Jamal Malinzi aanza vita dhidi ya dawa za kulevya katika soka

Rais wa TFF, Jamal Malinzi akizungumza kwenye uzinduzi wa programu ya Ishi Huru
Na Boniface Wambura
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amezindua programu ya kutoa elimu ya kupambana na matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana iitwayo Ishi Huru.
Programu hiyo iliyozimduliwa jana (Januari 10 mwaka huu) jijini Dar es Salaam iko chini ya taasisi ya Africa Inside Out inayoongozwa na Rebecca Young wakati washirika (partners) ni TFF na kampuni ya Rhino Resources ya Marekani.
Rais Malinzi amesema matumizi ya dawa za kulevya nchini yamekuwa yakiongezeka, hivyo kuwa kikwazo kwa maendeleo ya vijana ambapo ameipongeza Africa Inside Out kwa programu hiyo kwa vile itazuia vijana
wengi kujiingiza katika matumizi ya dawa hizo.
“Moja athari kubwa za matumizi ya dawa za kulevya ni kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutokana na kuchangia sindano za kujidunga dawa hizo.
“TFF tutatoa ushirikiano wa kutosha katika programu hii. Lakini pia tutaingiza Ishi Huru katika programu zetu za mpira wa miguu kwa vijana. Tutahamasisha jamii katika kupambana na dawa za kulevya,” amesema.
Katika uzinduzi huo, pia Rais Malinzi alizundua semina ya waelimishaji na kuwaeleza kuwa wamepata fursa hiyo kwa vile ni vijana wanaojituma, hivyo watafikisha vizuri ujumbe wa Ishi Huru katika shule na vituo vya vijana.

Wanawake, viongozi wa kitaifa, waalikwa Maulid Dar

MWENYEKITI Kamati ya Maandalizi ya Sherehe za Maulid kwa wanawake wa    mkoa wa Dar es Salaam, kuadhimishwa kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W),  Aisha Sururu (wa kwanza kulia), akiwaongoza wanawake wengine kuomba dua, baada ya kumaliza kikao cha maandalizi ya sherehe hizo
zitakazofanyika kesho, katika Ukumbi wa Diamond Jubilee.
***
WANAWAKE viongozi wa kitaifa na mkoa wa Dar es salaam, wameombwa
kujitokeza ili kuungana na wanawake wengine wa kiislam, katika
sherehe ya Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W).

Wito huo ulitolewa na Kamati ya Maandalizi ya sherehe hizo kwa upande
wa wanawake, na kubainisha kuwa hawataalika mgeni rasmi, badala yake ,
viongozi na wanawake wengine wawe kitu kimoja kuadhimisha siku hiyo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Aisha Sururu, alisema, sherehe itafanyika
Januari 14, katika ukumbi wa Diamond Jubilee, na kwamba
itawakutanisha wanawake waislam wa mkoa wa Dar es Salaam na mkoa
jirani wa Pwani.

"Wanawake wa hali ya chini, wamefikiria kwanini sherehe za kidini
ambazo hazina harambee, michango wala kitu chochote, tualike mgeni
rasmi? Wakaona ni vyema kutangaza ili nao kama wananchi wajumuike na
wanawake wa hali ya chini, ambao watafarijika zaidi, kuona wamekaa
mkekani pamoja na viongozi wakubwa,"alisema
Aisha.

Mwenyekiti huyo, ambaye pia ni diwani viti maalum Ilala, alisema, kwa
wale ambao hawatafikiwa kwa mualiko wa mmoja mmoja, wanaruhusiwa
kujumuika na wenzao siku hiyo ya maadhimisho.

Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W), huadhimishwa duniani  kote kila ifikapo mfungo wa sita kwa kalenda ya kiislam. ikiwa ni

kumbukumbu tangu kuzaliwa kwa kiongozi huyo wa wafuasi wa dini ya
kiislam.

Maandalizi ya sherehe hiyo kitaifa, mwaka huu yatafanyika mkoani
Kigoma, ambapo Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA), limesema
mgeni rasmi atakuwa Rais Jakaya Kikwete.

Kesho, Keshokutwa Wabongo kula shushu!

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail:  ikulumawasiliano@yahoo.com press@ikulu.go.tz              

Fax: 255-22-2113425

PRESIDENT’S OFFICE,
      THE STATE HOUSE,
       P.O. BOX 9120,  
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 
                                         
TAARIFA KWA  UMMA.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametangaza kuwa kesho, Jumatatu, Januari 13, 2014, itakuwa ni Siku ya Mapumziko (Public Holiday) kwa Watanzania wote kusheherekea miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Rais Kikwete ameutangaza uamuzi huo mjini Zanzibar ambako leo ameungana na Watanzania na Wazanzibari wote kusheherekea miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, mwaka 1964.

Mapinduzi hayo yaliyoongozwa na mwasisi wa Zanzibar na Taifa la Tanzania, Hayati Abeid Amaan Karume yalifanikiwa kuung’oa madarakani utawala dhalimu wa Sultan na kuwawezesha kwa mara ya kwanza katika historia Waafrika walio wengine kujitawala ndani ya nchi yao wenyewe.

Yalikuwa ni Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofungua njia ya kuzaliwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar – miezi mitatu baada ya Mapinduzi hayo – Aprili 26, 1964.               
Naye Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Ali Mohamed Shein ametangaza kuwa kesho itakuwa Siku ya Mapumziko Tanzania Visiwani kusheherekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Rais Shein alitangaza mapumziko hayo wakati alipohutubia wananchi kwenye Uwanja wa Michezo wa Amaan mjini Zanzibar katika kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi.

Rais Shein alitangaza mapumziko hayo wakati alipohutubia wananchi kwenye Uwanja wa Michezo wa Amaan mjini Zanzibar katika kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi.

Mwisho.
Imetolewa na;
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS
Ikulu,
es Salaam.
12 January, 2014

Manchester City kuiengua Chelsea kileleni itaivaa Newcastle Utd

KLABU tishio kwa sasa nchini England, Manchester City chini ya kocha Manuel Pellegrini leo ina nafasi ya kukalia kiti cha uongozi wa Ligi Kuu ya Engalnd iwapo itaishinda ugenini dhidi ya Newcastle United na kuinegua Chelsea iliyoing'oa Arsenal jana kwa kuicharaza Hull City.
City itakuwa ugenini kuvaana na Newcastle ina pointi 44 na iwapo itashinda mechi hiyo ya jioni ya leo itafikisha pointi 47, moja zaidi ya zile ilizonazo Chelsea iliyokaa kileleni na pointi 46, moja zaidi ya waliokuwa vinara Arsenal ambayo yenyewe itashuka dimbani kesho kuvaana na Aston Villa ugenini.
Kikosi cha Pellegrini ambayo kimecheza mechi 12 kuanzia Desemba Mosi na kufunga mabao 36 katika michuano yote inayoshiriki msimu huu, huku ikiwa na rekodi ya kushinda nyumbani hata hivyo hawatakuwa na kazi nyepesi kwa Newcastle watakaokuwa uwanja wao wa nyumbani wa St James Park kutokana na timu kupoteza mechi mbili mfululizo kutoka kwenye lindi la ushindi wiki chache zilizopita.
Manchester City wanapewa nafasi kubwa ya kushinda pambano hilo kutokana na kuwa na safu kali ya ushambuliaji ikiongozwa na Alvaro Negredo, Edin Dzeko na kiungo Yaya Toure Mchezaji Bora wa Afrika kwa mara ya tatu mfululizo.
Mbali na mechi hiyo inayofuatiliwa kwa ukaribu na mashabiki wa kandanda pia leo kuna mechi nyingine nzuri ya Stoke City itakayopikaribisha Liverpool kabla ya kesho kuhsuhudiwa Aston Villa kuialika Arsenal katika pambano ambalo kama The Gunners watashinda itadhihirisha dhamira yake ya kunyakua taji la Ligi msimu huu baada ya miaka mingi ya kulikisikia kwenye bomba tu.

RATIBA
Jumapili Januari 12 
17:05 Newcastle V Man City
19:10 Stoke V Liverpool
Jumatatu Januari 13 

23:00 Aston Villa V Arsenal

Ni Bobby Williamson au Adel Amrouche kuinoa Yanga

Bobby Williamson




Adel Amrouche


Na Sanula Athanas, Zanzibar
MAKAMU Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Clement Sanga ameweka wazi kuwa pamoja na kupokea majina ya makocha 60 walioomba kazi ya kuifundisha timu hiyo, ni makocha wawili tu ambapo Yanga wameona wanauwezo wa kuifundisha timu hiyo.
Akizungumza mjini Zanzibar juzi usiku, Sanga alisema Kocha wa Gor Mahia, Bobby Williams raia wa Scotland na Kocha wa timu ya taifa ya Kenya (Harambee Stars), Mbelgiji Adel Amrouche, ndiyo makocha pekee wenye sifa za kuinoa timu yao inayokabiliwa na mashindano ya Klabu Bingwa Afrika mapema mwezi ujao.
Sanga, aliyekuwa kisiwani hapa tangu juzi kwa ajili ya kuiomba radhi serikali ya Zanzibar kwa kutoleta timu yao kushiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi, alisema baada ya kufanya mchujo wa majina zaidi ya 60  waliyokuwa nayo makocha hao ndio wawili ndiyo wamekidhi vigezo vinavyotakiwa na klabu hiyo ya Jangwani.
 “Unajua yanazungumzwa mengi kuhusu kocha wetu ajaye, lakini ukweli ni kwamba mpaka sasa hatujapata kocha mkuu na timu itaendelea kuwa chini ya Mkwasa (Boniface) hadi pale tutakapopata,” alisema kiongozi huyo.
“Tulipata zaidi ya maombi ya makocha 60, wanaotufaa ni Bobby na kocha wa Harambee Stars (Amrouche). Tumefanya mazungumzo nao lakini kuna masharti magumu yanayotuchelewesha kwa sababu wana mikataba na timu zao,” aliongeza Sanga.
Alisema kuwa bado wapo kwenye mazungumzo kuona ni kwa namna gani wanaweza kumpata kocha mmoja wapo kati ya hao kwa ajili ya kuchukua nafasi ya kocha aliyetimuliwa, Ernest Brandts raia wa Uholanzi.
Kocha huyo alitimuliwa siku mbili baada ya kufungwa na Simba magoli 3-1 kwenye mchezo maalum wa kirafiki wa 'Nani Mtani Jembe' uliochezwa Desemba 21 mwaka jana.
Kikosi cha Yanga kwa sisi kipo chini ya Kocha Charles Mkwasa ambaye amchukuliwa pamojana Juma Pondamali kuchukua nafasi za Fred Felix 'Minziro' na Mkenya Razaq siwa ambao pia walitupiwa virago pamoja na Brandts.

Yanga ipo nchini Uturuki ilipokwenda kuweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu pamoja na ligi ya klabu bingwa Afrika.NIPASHE JUMAPILI

Waziri Miuu wa zamani wa Israel, Ariel Sharon afariki

BDEA70B3-44DF-4D1E-BDDB-A5DCEBA4F87F_w640_r1_sWaziri mkuu wa zamani wa Israel, Ariel Sharon, amefariki dunia Jumamosi akiwa na umri wa miaka 85.
Alikuwa waziri mkuu wa Israel mwaka 2001.
Amekuwa mahututi tangu mwaka 2006 kufuatia mfululizo wa matatizo ya kiharusi. 
Ariel Sharon alikuwa askari wa vita na baadae kuwa kiongozi wa nchi.
Alipokuwa mwanajeshi, alijulikana kwa ushujaa wake katika uwanja wa mapambano kwa miongo kadhaa kufuatia kuundwa kwa taifa la Israel, akijulikana hasa wakati wa vita vya jom kippur vya mwaka 1973. Katika mbinu za hali ya juu alizozionyesha, aliwaongoza wanajeshi wa Israel kuvuka mfereji wa suez, na kulikabili jeshi la misri.
Pia alijulikana na wengi kwa kuwa jabari na mbabe. Mwaka 1982, aliongoza uvamizi wa Lebanon ambao ulipelekea mauaji yaliyofanywa na wanamgambo wa Lebanon kwa mamia ya wapalestina katika kambi za wakimbizi za sabra na shatilla huko Beirut.
Kama mwanasiasa, Ariel Sharon pia alikuwa na utatanishi. Akiwa waziri, alihamasisha kuundwa kwa makazi ya walowezi wa kiyahudi kote katika maeneo ya wapalestina.
Serikali yake ilizikandamiza vurugu katika muda wa miaka michache, na kuanza kazi ya kuweka vizuizi vya usalama ambavyo hivi sasa vinawatenga waisraeli na wapalestina.
Mwaka 2006, bwana Sharon alipata mfululizo wa matatizo ya kiharusi na kuingia katika hali ya kupoteza fahamu. Nafasi yake ya waziri mkuu ilichukuliwa na Ehud Olmert.
Chanzo:VOASWAHILI.COM

Saturday, January 11, 2014

SUAREZ, PELLEGRINI WASHINDA TUZO ZA MWEZI.

MSHAMBULIAJI wa klabu ya Liverpool, Luis Suarez ametajwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Desemba wa Ligi Kuu nchini Uingereza huku meneja wa Manchester City Manuel Pellegrini akitajwa kama kocha bora wa mwezi. Suarez ambaye anakipiga katika klabu ya Liverpool alianza mwezi vibaya baada ya timu hiyo kukubali vipigo kutoka kwa Hull City, Manchester City na Chelsea lakini alionyesha kiwango cha juu baadae kwa kufunga mabao 10 katika mechi nne pekee. 


Mabao hayo alifunga katika mechi dhidi ya Norwich City ambapo alifunga manne, West Ham United mabao mawili, Totehham Hotaspurs mabao mawili na mengine mawili katika mchezo dhidi ya Cardiff City. Mabao hayo yaliisaidia Liverpool kushika usukani wa ligi katika kipindi cha Christmas iangwa baadae waliteleza mpaka nafasi ya tano katika kipindi cha mwaka mpya. Naye Pellegrini mwezi Desemba ulikuwa mzuri kwake baada ya kushinda mechi zote sita kati ya saba walizocheza huku mmoja wakitoka sare ya kufungana bao 1-1 na Southampton.

YANGA YAANZA KAMBI VEMA KWA KUICHAPA 3-0 ANKARA SEKERSPOR

Kikosi cha Young Africans kilichoanza leo dhidi ya Ankara Sekerspor
Young Africans imeanza vizuri katika kambi yake ya mafunzo nchini Uturuki baada ya kuifunga timu ya Ankara Sekerspor kwa mabao 3-0 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika pembeni kidogo ya eneo ililofikia katika mji wa Manavgat Antalya.

Kocha wa Young Africans aliwatumia wachezaji 18 jumla katika mchezo huo ambao wenyeji mara baada ya mchezo walimpongeza kwa timu yake kwa kucheza vizuri katika mchezo huo wa kirafiki.
Dakika ya 10 ya mchezo shuti lililopigwa na mganda Emmanuel Okwi lilishinda mlinda mlango wa Ankara Sekerspor ambapo aliutema mpira huo na kumkuta Didier Kavumbagu aliyeukwamisha mpira huo wavuni na kuhesabu bao la kwanza.

Timu zote ziliendelea kushambuliana kwa zamu na mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Ankara Sekerspor i0 - 1 Young Africans .
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na iliwachukua dakika moja Young Africans kujipatia bao la pili la mchezo kupitia kwa Emmanuel Okwi aliyeitumia vyema pasi ya mwisho ya kiungo Mrisho Ngasa aliywatoka walinzi wa Ankara Sekaspor na kumpasia mfungaji ambaye hakufanya makosa na kuukwamisha mpira wavuni.
Dakika ya 58 kocha Mkwasa alifanya mabadiliko, ambapo waliingia Hamis Kizza na Nizar Khalfani kuchukua nafasi za Didier Kavumbagu na kiungo Hassan Dilunga.

Hamis Kizza aliipatia Young Africans bao tatu la mchezo na la ushindi dakika ya 61 ya mchezo baada mpira aliogongewa na Domayo kuwapita walinzi wa Ankara Sekerspor na kumkuta Kizza ambaye alipiga shuti liliomgonga mlinzi wa Ankara Sekerspor wakati akiokoa na kujaa wavuni.

Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Ankara Sekerspor 0 -3 Young Africans.
Mara baada ya mchezo kaimu kocha mkuu wa Young Africans Charles Boniface Mkwasa alisema anashukuru vijana wake walicheza vizuri kwa kufuata malekezo na ndio maana wakaweza kupata ushindi huo,makosa yapo machache yaliyojitokeza na ataendelea kuyafanyia kazi.

"Mechi ilikua ni nzuri ukizingatia ndo mchezo wetu wa kwanza wa kirafiki tukiwa na siku ya tatu tangu tufike hapa Uturuki, kwa mazoezi ya jana vijana wameosha mabadiliko na leo wameweza kucheza vizuri na kuweza kupata ushindi, kikubwa naamini kwa siku zilizobakia nitaendelea kufanya marekebisho na kukifanya kikosi kuendelea kuwa bora pindi kitaporejea nchini tayari kwa mzunguko wa pili wa Lig Kuu ya Vodacom" alisema Mkwasa 

Kikosi cha Young Africans kilichocheza leo ni:
1.Juma Kaseja/Ally Mustafa "Barthez" (dk65), 2.Juma Abdul, 3.Oscar Joshua/David Luhende(dk 82), 4.Mbuyu Twite (C), 5.Kelvin Yondani, 6.Frank Domayo/Ibrahim Job(dkk 80), 7.Haruna Niyonzima/Saimon Msuva (dk72), 8.Hassan Dilunga/Nizar Khalfan (dk58), 9.Didier Kavumbagu/Hamis Kizza (dk58), 10.Mrisho Ngasa/Jerson Tegete (dk 68), 11. Emmanuel Okwi/Said Bahanuzi (dk 85)

Chelsea yaiengua Arsenal kileleni

 Eden Hazard scores for Chelsea
MABAO mawili moja kutoka kwa Ezen Hazard na jingine la Fernando Torres 'El Nino' yameiwezesha Chelsea kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 ugenini na kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England kwa muda.
Chelsea ilipata ushindi huo dhidi ya Hull City kwenye pambano lililochezwa kwenye uwanja wa Kingstons Communication na kuifanya kufikisha pointi 46, moja zaidi ya Arsenal ambao watashuka dimbani keshokutwa.
Hazard alifunga bao la kwanza dakika ya 56 akimalizia kazi nzuri ya Ashley Cole kabla ya Torres kuongeza la pili dakika ya 87 na kuwakatisha tamaa wenyeji.
Jioni hii kuna mechi nyingine zinazoendelea katika ligi hiyo na baadaye Manchester United itaikaribisha Swansea City waliowatoa nishai kwenye michuano ya Kombe la FA katika dimba hilo hilo.

Simba yavunja mwiko, Kiemba we acha tu

 
AMRI Kiemba amezidi kudhihirisha kuwa yupo kikazi zaidi kama alivyopwahi kunukuliwa na Blogu hii baada ya usiku wa jana kuhusika na mabao mawili yaliyotosha kuvunja mwiko wa URA wa kutofungwa na Simba kwenye mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi.
Kiemba, alitengeneza bao la kwanza lililofungwa na beki Joseph Owino kabla ya kuongeza jingine na kuipa Simba ushindi wa mabao 2-0 na kuivusha hadi Fainali ya michuano hiyo.
Mabao yote mawili yalifungwa kwenye kipi8ndi cha pili baada ya kipindi cha kwanza kuisha timu zikiwa hazijafungana na URA wakicheza punguyfu baada ya nyota wao Oweni Kasule kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Ramadhani Singano 'Messi'.
Kwa ushindi huo asmbao umeifanya Simba kuweka rekodi kwa kuondoa uteja kwa URAnma kutinga Fainali bila kupoteza mchezo zozote wala kufungwa bao lolote katika lango lao, limeifanya Simba sasa kukutana na KCC ya Uganda iliwatemesha taji waliokuwa watetezi, Azam.
Azam walikumbana na lkipindi cha mabao 3-2 katika mechi ya kwanza iliyochezwa jioni kwenye dimba la Amaan licha ya kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-1, mabaoi yake yakiwekwa kimiani na kinda, Joseph Kimwaga.
Fainali ya michuano hiyo itachezwa Jumatatu kwenye uwanja huo wa Amaan.

Friday, January 10, 2014

Hapatoshi Nusu Fainali Kombe la Mapinduzi leo

Kikisi cha Simba kitakachovaana na URA

Watetezi Azam watakaovaana na KCC

LEO ni kimbembe katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi wakati Azam itavaana na KCC ya Ungada wakati Simba ikishuka dimbani usiku kuivaa URA.
URA imekuwa ikiionea Simba kila wanapokutana nao kwa muda mrefu sasa iwe kwenye mashindano au mechi za kirafiki na kufanya mechi hiyo kuwa yenye mvuto zaidi kuliko ya KCC na watetezi Azam.
Hata hivyo mechi zote zinaonekana kusisimua kutokana na ukweli inazikutanisha timu za Tanzania na Uganda ambazo timu zao za taifa zimekuwa zina upinzani katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Simba ilitinga nusu fainali baada ya kuibamiza mabao 2-0 timu ngumu ya Chuoni FC ya Unguja katika mchezo wa robo fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Amaan usiku wa kuamkia jana na URA URA ikifuzu baada ya kuifunga KMKM bao 1-0 kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba juzi.
Azam ambayo haijapoteza mchezo wowote katika michuano hiyo mpaka sasa itataka kuitoa nishai KCC ili kuweza kutinga fainali na kusubiri kuona itaumana na nani Jumapili kutetea taji lake.
Simba wenyewe itawavaa URA ikimtegemea nyota wake Ramadhani Singano 'Messi' na wakati wengine walioipaisha timu hiyo kwenye michuano hiyo.
Messi alifunga mabao mawili katika mechi ya robo fainali na kuibuka mchezaji bora wa michuano hiyo, japo Mrundi Amissi Tambwe ameling'ang'ania moja ya mabao hayo akidai alifunga yeye.
Makocha wa timu zote nne zilizotinga nusu fainali wamenukuliwa visiwani humo wakitamba kuwa wapo tayari kwa vita ili kuona vikosi vyao vikitinga fainali na hatimaye kunyakua taji hilo.
Tangu michuano hiyo ilipoanzishwa, hakuna klabu kutoka nje ya Tanzania imefanikiwa kutwaa taji hilo na hivyo Simba na Azam kuwa na mtihani wa kuhakikisha zinakutana tena zenyewe kwa zenyewe kulinda rekodi.

Yaya Toure atwaa tena tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika


KIUNGO nyota wa klabu ya Manchester City na timu ya taifa ya Ivory Coast, Yaya Toure ametawazwa kwa mwaka wa tatu mfululizo kuwa Mwanasoka Bora wa Afrika.
Yaya aliwashinda Mnigeria John Obi Mikel aliyeshika nafasi ya pili na Didier Drogba.
Toure, aliyeshinda tuzo hiyo mwaka 2011 na 2012, alipata kura 373 dhidi ya 265 na 236 za Mikel na Drogba waliomfuatia.
Sherehe za utoaji tuzo hiyo na nyingine zilihudhuriwa na Maofisa mbalimbali wakiwemo Rais wa CAF, Issa Hayatou, Gavana wa Lagos, Babatunde Fashola Raji Fashola, Waziri wa Vijana na Michezo Nigeria, Alhaji Bolaji Abdullah, Wajumbe wa Kamati Kuu ya CAF na wengineo.
Kwa tuzo ya mchezaji bora anayecheza Afrika, ilienda kwa kiungo wa Misri, Mohamed Aboutrika aliwashinda  Ahmed Fathy  wa Misiri na Sunday Mba wa Nigeria.
Hiyo ilikuwa mara ya nne, Aboutrika, aliyetangaza   kustaafu soka hivi karibuni kushinda tuzo hiyo akifanya hivyo mwaka 2006, 2008 na 2012.

TUZO ZA CAF ZILIZOTOLEWA JANA:

Mchezaji Bora wa mwaka; Yaya Toure, Ivory Coast na Manchester City
Mchezaji bora wa mwaka anayecheza Afrika; Mohamed Aboutrika, Misri na Al-Ahly
Mwanasoka anayechipukia; Kelechi Iheanacho (Nigeria)
Timu bora ya mwaka; Nigeria
Timu bora ya vijana ya mwaka; Nigeria U-17 klabu bora ya mwaka; Al-Ahly (Misri)
Kocha bora wa mwaka; Stephen Keshi (Nigeria)
Refa bora wa mwaka; Haimoudi Djamel (Algeria)
Tuzo ya mchezo wa kiungwana; Mashabiki wa Nigeria
Magwiji wa CAF; Bruno Metsu, Mehdi Faria
Tuzo ya Platinum; Goodluck Jonathan (Rais wa Nigeria)
11 bora wa kuunda kombaini ya Afrika;
Kipa: Vincent Enyeama (Nigeria)
Mabeki: Ahmed Fathy (Misri), Mehdi Benatia (Morocco), Kevin Constant (Guinea)
Viungo: Jonathan Pitroipa (Burkina Faso), John Obi Mikel (Nigeria), Yaya Toure (Ivory Coast), Mohamed Aboutreika (Misri)
Washambuliaji: Emmanuel Emenike (Nigeria), Asamoah Gyan (Ghana) na Pierre-Emerick Aubameyang (Gabon).

Mara baada ya kupokea tuzo yake Yaya amewashuku kaka zake,Obi Mikel na Drogba.

Thursday, January 9, 2014

Kiemba yupo kikazi zaidi Msimbazi

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiEps_zFlpFfrIRTHTU257hsjXqtA3uCzF1EGsUAwBerMzrMu3p71BRHrvT_PAW8jmgbx_rRosYweFvnR2QgN-fg9FuvtsrJH864KdBbmabBo26I2G3mMzDW-LOY6-JuP35XAxWAxMRf5Q/s640/AMRIKIEMBASIMBA.jpg
Amri Kiemba kishangilia moja ya mabao yake
 KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Amri Kiemba, amesema kwa sasa hana muda wa kupiga blabla kwenye vyombo vya habari na badala yake anaelekeza ngumu na kuwaonyesha mashabiki wa kandanda kipi anachokifanya uwanjani.
Akizungumza na MICHARAZO kwa njia ya simu toka Zanzibar, Kiemba alisema anaamini wote ambao walikuwa na maoni tofauti dhidi yake watakuwa wamepata salama kutokana na kile anachokifanya.
Kiemba alisema kutokana na hilo kwa sasa ameamua kufunga mdomo wake kuzungumza lolote badala yake kufanya kazi kwa manufaa ya klabu yake.
"Dah kwa sasa nimeamua kukaa kimya ili nifanye kazi, naamini hivi ndivyo inavyotakiwa ili kuwafanya watu wapime kazi yangu uwanjani na siyo kwenye vyombo vya habari," alisema Kiemba.
Mchezaji huyo ambaye magoli yake mawili aliyoyafunga kwenye mechi mbili tofauti yaliisaidia Simba kuvuka hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani Zanzibar.
Kiemba alifunga bao la kwanza wakati Simba ikiilaza AFC Leopards katika mechi ya kwanza ya kundi B kabla ya kuifunga pia KMKM ya Zanzibar.
Nyota huyo wa zamani wa Kagera Sugar, Yanga, Miembeni na Moro United, alikuwa katika hatihati msimu huu kuondoka Simba kabla ya kupewa mkataba wa miaka miwili baada ya kuzima uvumi alikuwa akielekea Yanga.
Klabu hiyo ya Simba jana ilifanikiwa kuinyuka Chuoni katika mechi yao ya Robo Fainali ya Mapinduzi kwa mabao 2-0 na sasa wanakutana na timu inayowasumbua kwa muda mrefu ya URA toka Uganda.
Simba kwa miaka zaidi ya miwili ikikutana na URA imekuwa ikitepeta, japo ukali wa kocha Zdrakov Logarusic na msaidizi wake, Suleiman Matola wanatoa matumaini ya kupata dawa ya kuizima URA kab la ya kujua itavaana na nani kati ya Azam na KCC ya Uganda.

Tom Olaba akimwagia sifa kikosi cha Ruvu Shooting

http://images.supersport.com/AFC-Tom-Olaba-300.jpg
Tom Olaba

KOCHA Mpya wa klabu ya Ruvu Shooting, Mkenya Tom Olaba amekimwagia sifa kikosi cha timu yake akidai kina wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa wa soka na kudai wanampa imani ya kufanya nao vema katika Ligi Kuu.
Aidha kocha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, alisema amebaini udhaifu wa aina tatu katika kikosi hicho na kueleza ameanza kurekebisha ili kuwahi pambano lao la kwanza la duru la pili la Ligi Kuu dhidi ya Prisons.
Akizungumza na MICHARAZO, Olaba aliyetua Ruvu Shooting kuziba nafasi ya kocha Charles Boniface aliyehamia Yanga, alisema kwa siku chache tangu aanze kukinoa kikosi chake amebaini kimejaliwa 'vijana wa kazi'.
Olaba alisema asilimia kubwa ya wachezaji wa timu hiyo wana vipaji na uwezo mkubwa wa soka kitu kinachomtia moyo kwamba watafanya kazi kwa ufanisi na kuipaisha Ruvu kwenye duru la pili la ligi kuu.
"Kwa kweli ndiyo kwanza nina siku kama tata au nne tangu nianze kuinoa timu yangu, nimebaini vipaji na vijana wenye uwezo wa soka kitu kinachonitia moyo na kuamini tutafanya kazi vyema," alisema.
Olaba alisema pamoja na vipaji na uwezo wa kisoka, amebaini mapungufu matatu katika kikosi hicho na tayari ameanza kuyafanyia kazi kuyarekebisha.
"Wachezaji hawana uwezo wa kukaa na mipira, kutoa pasi na kunyang'anya mipira, kitu ambacho nimeanza kufanyia kazi mapema ili hata tukienda Mbeya kuvaana na Prisons tuwe tumekamilika, ila nimevutiwa na aina ya wachezaji walipo Ruvu kwani wanajua soka na wana vipaji," alisema.
Ruvu Shooting iliyomaliza duru la kwanza ikiwa kwenye nafasi ya saba kwa kujikusanyia pointi 17 kutokana na mechi 13, imemnyakua Olaba kwa mkataba wa muda mfupi wa miezi sita kwa ajili ya mechi za duru la pili.

TASWA kuchaguana Februari 16

KATIBU wa TASWA, Amir Mhando 'Mgosi'
UCHAGUZI Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), utafanyika Februari 16 mwaka huu jijini Dar es Salaam. 
Uamuzi huo ulifikiwa na kikao cha Kamati ya Utendaji ya TASWA kilichofanyika Dar es Salaam jana kujadili masuala mbalimbali ya chama na waandishi wa habari za michezo kwa ujumla. 
Kikao kilikubaliana kuwa uchaguzi ufanyike kwa katiba ya zamani, kwani mchakato wa katiba mpya unaweza kuchukua muda mrefu, hivyo kusababisha viongozi waliopo madarakani kuendelea kukalia viti kinyume cha katiba, jambo ambalo si sahihi. 
Kutokana na hali hiyo viongozi wapya watakaochaguliwa moja ya kazi yao kubwa itakuwa kuifanyia marekebisho makubwa katiba ya chama chetu ili iende na wakati. 
Fomu za kuwania uongozi zitaanza kutolewa Februari 10 hadi Februari 14 mwaka huu saa kumi alasiri, masuala mengine yahusiyo uchaguzi huo, ikiwemo mahali utakapofanyika yatatangazwa baada ya kikao cha sekretarieti ya TASWA na Kamati ya Uchaguzi kitakachofanyika Februari 3.

Jennifer Mgendi aachia video mpya iitwayo 'Hongera Yesu'

MUIMBAJI nyota wa muziki wa nyimbo za Injili, Jennifer Mgendi ameibuka na albamu mpya ya video iitwayo 'Hongera Yesu' yenye nyimbo saba.
Akizungumza MICHARAZO, Mgendi alisema kuwa albamu hiyo tayari imeshatua madukani na aliwataka wapenzi wa muziki huo kutonunua CD 'feki' kwani kufanya hivyo kunawavunja moyo wasanii.
Video hiyo mpya mbali na kibao cha 'Hongera Yesu' kilichobeba jina la albamu, pia ina nyimbo kama 'Nikufanyie Nini?', 'Kikulacho', 'Mimi ni Wako', 'Baraka Zangu', 'Fumbua Macho' na 'Msimamo'.
Katika nyimbo za albamu hiyo Mgendi amewashirikisha nyota wengine wa muziki wa Injili kama Bahati Bukuku, Bonny Mwaitege, Christina Matai na Martha Ramadhani.
Mbali na kutoa video, Mgendi pia ametoa albamu ya audio ya vibao hivyo, ambayo nayo tayari iko madukani.
Muimbaji huyo amewahi kutamba na albamu kadhaa zilizomtangaza vyema kwenye ulimwengu wa muziki wa miondoko hiyo ikiwamo ile ya 'Mchimba Mashimo' iliyokuwa na nyimbo kama 'Moyo Tulia', 'Nalia', 'Baba ni Wakuaminiwa', 'Niongoze Safarini' na 'Rudi Nyumbani'.
Aidha, Mgendi alisema kuwa mwaka huu anatarajia pia kuzindua filamu yake mpya ambayo hata hivyo hakupenda kuitaja jina kwa sasa kwavile bado ni mapema.