STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, May 28, 2014

Marehemu Recho kuzikwa kesho Dar, soma historia yake fupi

Msanii Rachel Haule 'Recho' enzi za uhai wake
Msanii Recho enzi za uhai wake
Recho akiwa na mchumba wake enzi za uhai wake
STAA wa filamu za The Passion, Vanesa in Dillema, Bed Rest, Unpredictable, Rachel Haule 'Recho' aliyefariki wakati wa kujifungua anatarajiwa kuzikwa siku ya Alhamis kwenye makaburi ya Kinondoni, jijini Dar badala ya kusafirishwa kwenda kuzikwa kwao mkoani Ruvuma kama ilivyokuwa imeelezwa awali.
Kwa mujibu wa taarifa toka Bongo Movie na kuthibitishwa na Rais wa Umoja huo, Steve Nyerere, marehemu Recho sasa hatasafirishwa kwenda kuzikwa Songea badala yake atazikwa Dar na shughuli za kuagwa zitafanyika viwanja vya Leaders kabla ya kuzikwa Kinondoni yeye na kichanga chake na msiba hupo nyumbani kwa marehemu Sinza Palestina.
"Tymekubaliana marehemu azikwe Dar na shughuli nzima za kuaga miili ya marehemu itafanyika viwanja vya Leaders kuanzi  saa 4 asubuhu kabla ya saa nane kwenda kuzikwa makaburi ya Kinondoni, " Steve Nyerere alisema hivi punde alipozungumza na MICHARAZO.
Recho alifariki asubuhi ya jana muda mchache baada ya kujifungua kwa njia ya upasuaji ambapo kichanga chake nacho kilipoteza maisha, ameondoka wakati Bongo Movie ikiwa bado hawajasahau machungu ya kuondokewa na muigizaji na muongozaji mahiri, Adam Kuambiana aliyefariki wiki iliyopita.
Enzi za uhai wake Recho aliwahi kufanya mazungumzo na MICHARAZO MITUPU na kuweka bayana historia ya maisha yake namna alipojikuta akiingia kwenye fani hiyo aliyoipenda tangu akiwa mdogo.
Mwenyewe alisema alianza kuonyesha kipaji cha sanaa tangu akiwa Shule ya Msingi Ndugumbi, lakini hakuweza kupata nafasi ya kutambulika hadi miaka miwili iliyopita alipoibuliwa na filamu iitwayo 'The Passion'.
Filamu hiyo ilimsaidia mwanadada huyo kuweza kufahamika na kupata tenda ya kucheza kazi nyingine zilizosaidia kumtangaza vema na kumuinua kimaisha.
Recho, alisema kabla ya kutoka na filamu hiyo aliwahi kujiunga na kundi la sanaa la  Lumila Arts na alivutiwa kisanii na waigizaji Blandina Chagula 'Johari' na Genevieve Nnaji wa Nigeria.
Mwanadada huyo aliyeuza sura katika kazi nyingine kama Candy, Life to Life, Rude, Mtihani, Time After Time, Confussion, Mwalimu Nyerere na Mke Mwema, alisema anashukuru fani hiyo ilimsaidia kwa mambo mengi kimaisha.
MOja ya aliyokuwa akijivunia ni kuweza kufahamika na kujiingizia kipato cha kila siku, akiweza pia kufungua maduka matatu katika mikoa mitatu.
Aliyataja maduka yake hayo yanayohusika na kuuza DVD na nguo za wanawake na watoto yapo Arusha, Songea na Dodoma.
Recho aliyekuwa akipenda kula ugali kwa dagaa na wali kwa maharage na kunywa kinywaji cha Savanah, alisema fani ya filamu kwa sasa inalipa na kuwataka wasanii wenzake kuchapa kazi na kuepukana mifarakano pamoja na kujihusisha na matendo yanayowachafua mbele ya jamii.
Msanii huyo aliyekuwa na ndoto za kutamba kimataifa na kupanua miradi yake ya biashara, alisema hakuna tukio la furaha kwake kama alipoanza kuuza sura katika filamu na kusikitishwa na kifo cha mama yake mdogo aliyemlea tangu akiwa mdogo.
Nyota huyo aliyekuwa hajaolewa ingawa alikuwa mchumba wa George Segunda, alidai angetamani sana kama angekuja kuzaa watoto wasiozidi watatu, ingawa bahati haikuwa yake kwa kupoteza uhai akitekeleza 'sunna' hiyo ya kuiongeza dunia.
Kihistoria, Rachel Haule alizaliwa Aprili 4, 1988 mjini Songea akiwa mtoto wa mwisho kati ya watoto watano wa familia yao. Alisoma Shule ya Msingi Ndugumbi kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari ya bweni iitwao Hanga Montesory ya mjini Songea.
Mara alipohitimu masomo yake ya sekondari alijiunga na Chuo cha Uhazili cha Magogoni kusomea Ukatibu Mhutasi kabla ya kutumbukia kwenye masuala ya sanaa ya uigizaji aliyoendelea kuifanya mpaka mauti yalipomkuta.
Kwa hakika kifo kinauma, kifo kinaumiza...tulimpenda sana marehemu Recho, lakini aliyemuumba alipenda zaidi tunamuombea kwa Mungu roho yake iwekwe mahali pema yeye katangulia sisi tu nyuma yake.

Yaya Toure azidi kuleta utata Manchester City

MUSTAKABALI wa kiungo mahiri wa Manchester City, Yaya Toure kusalia katika klabu hiyo imezidi kuleta utata.
Kiungo huyo amesema itakuwa heshima kwake kuichezea Paris Saint-Germain-PSG na kukuza uvumi juu ya mustakabali wake na klabu hiyo. 
Wakala wa mchezaji huyo wiki iliyopita alisisitiza mteja wake hakufurahishwa na mabingwa hao wa Ligi Kuu nchini Uingereza baada ya kueleza kusononeshwa kwake na jinsi klabu hiyo ilivyoshindwa kumpa pongezi katika siku yake ya kuzaliwa. 
Toure aliunga mkono madai hayo na kubainisha atatoa taarifa rasmi kuhusiana na mustakabali wake baada ya Kombe la dunia na sasa amedokeza kuwa na nia ya kujiunga na PSG ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu nchini Ufaransa. 
Nyota huyo amesema kwa jinsi PSG walivyojijenga na kuwa na nguvu barani Ulaya itakuwa heshima kwake kuwa sehemu ya timu hiyo siku moja kama wataona anafaa. 
Toure amekuwa mchezaji muhimu kwa City msimu huu akiwa amefunga mabao 20 katika ligi na kusaidia mengine tisa na kuifanya timu hiyo kunyakuwa taji la Ligi Kuu.

Stars yaizamisha Malawi ikiifuata Mighty Warriors kumaliza kazi

Kiemba akishangilia bao lake
TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, jana ilikuwa na maandalizi mazuri ya mechi yao ya marudiano dhidi ya Zimbabwe baada ya kuifunga Malawi 1-0 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kiungo wa klabu ya Simba, Amri Kiemba alifunga goli pekee lililoamua mechi hiyo na kuipa Stars ushindi wa pili mfululizo tangu ilipokumbana na kipigo cha aibu cha 3-0 kutoka kwa Burundi katika mechi ya kuadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na pia kujiandaa na michuano ya Mataifa ya Afrika 2015.
Stars inajiandaa na mechi yake ya marudiano dhidi ya Zimbabwe katika hatua ya awali ya mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya kufuzu kwa fainali za Mataifa Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Morocco. Katika mechi yake iliyopita kwenye jijini Dar es Salaam, Stars ilishinda 1-0 kwa bao la mshambuliaji John Bocco 'Adebayor' na itahitaji japo sare jijini Harare katika wikiendi ya kati ya Mei 30-31 na Juni 1. Ikivuka hatua hiyo itaingia raundi ya pili ya mchujo ambako itakutana na mshindi baina ya Sudan Kusini na Msumbiji.
Mshindi atafuzu kwa hatua ya makundi ya kufuzu. Endapo Tanzania itatinga hatua ya makundi ya kuwania kufuzu itaingia katika Kundi F la kufuzu ambalo linaundwa na timu za Zambia, Niger, Cape Verde.
Timu mbili kutoka kila kundi la kuwania kufuzu kati ya makundi saba yaliyopo, pamoja na mshindi wa tatu mmoja aliyefanya vizuri zaidi, wataungana na mwenyeji Morocco kwa ajili ya fainali hizo za Mataifa ya Afrika 2015 nchini Morocco.
Mechi ya jana iliyoshuhudiwa na mashabiki wachache mno waliokata tiketi na kuingia uwanjani, ilianza kwa wachezaji wote na marefa kukusanyika kwenye duara la katikati ya Uwanja wa Taifa na kuwa kimya kwa dakika moja kumkumbuka Balozi wa Malawi nchini, Flossy Gomile-Chidyaonga, aliyefariki hivi karibuni.
Winga Simon Msuva alikuwa katika nafasi nzuri ya kuifungia Stars goli la dakika ya kwanza lakini, akiwa ndani ya boksi, alipaisha na kushika kichwa asiamini kilichousibu mguu wake wa kulia.
Kiungo mkongwe Kiemba aliifungia Stars goli akimalizia pasi tamu ya mchezaji 'kiraka' Shomari Kapombe katika dakika ya 36. Mpira wa bao ulianzia kwa nyota wa Malawi, Gabadinho Mhango aliyenyang'anywa na Kapombe kisha mchezaji huyo wa AS Cannes akaanza kupigiana gonga moja moja na winga chipukizi Friday wakipita kwenye wingi ya kulia kusini mwa Uwanja wa Taifa kabla ya mpira kutua kwenye mguu wa kulia wa mfungaji aliyekuwa ndani ya boksi la wageni.
Bao hilo lilidumu hadi wakati wa mapumziko. Kipindi cha pili kilianza kwa Stars kuonekana kuelewana zaidi wakicheza soka la pasi fupi fupi na za haraka lakini tatizo la umaliziaji mbovu liliwanyima wenyeji ushindi mnono zaidi.
Dakika nne kabla ya mechi kumalizika kipa Deogratias Munishi 'Dida', aliinusuru Stars kufungwa goli la kusawazisha baada ya kupangua kishujaa shuti kali la ndani ya boksi kutoka kwa mtokeabenchini Rodric Gonani.
Katika hali ya kushangaza, Kapombe alikuwa amevaa jezi namba 19 ya Kelvin Friday huku winga huyo kinda wa mabingwa wa Tanzania Bara, Azam FC akivaa jezi namba 20 inayovaliwa na Kapombe.
Mechi hiyo iliyokosa mashamsham kutokana na mahudhuria madogo, ilichezeshwa na refa Mtanzania Israel Nkongo akisaidiwa na Hamis Chang'walu na Erasmo Jesse.
Vikosi vilikuwa: Stars: Deogratias Munishi 'Dida', Himid Mao, Edward Charles, Said Morad, Joram Ngezeke/ Kelvin Yondani (dk.72), Shomari Kapombe, Simon Msuva/ Ramadhani Singano (dk.46), Erasto Nyoni/ Frank Domayo (dk.76), Kelvin Friday/ Said Juma (dk.73), Amri Kiemba/ Mwinyi Kazimoto (dk.73) na Khamis Mcha.
Malawi: Richard Chipuwa, Moses Chabvula/ Francis Mulimbika (dk.79), Limbikani Mzava/ Bashiri Maunde (dk 57), John Lanjesi, Foster Namwera, Phillip Masiye, Young Chimodzi JR, Gabadinho Mhango, Chimango Kaira, Joseph Kamwendo/ Frank Banda (dk.67) na Atusaghe Nyondo/ Robin Ngalawe (dk.37)..
NIPASHE

Kipre Tchetche, Casillas, Mwmbusi ndiye Bora Tanzania 2013-2014

Kipa Hussen Sharrif 'Casillas' akiwajibika uwanjani

KIipre Tchetche
MSHAMBULIAJI nyota wa Azam, Kipre Tchetche na kipa Hussein Sharrif 'Casillas' wamefanikiwa kushinda tuzo za Wachezaji Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara iliyoisha.
Tuzo hizo zilitolewa usiku wa kuamkia leo ambapo Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi alinyakua tuzo ya Kocha Bora msimu wa 2013/2014.
Casillas anayeichezea Mtibwa Sugar alishinda tuzo ya Kipa Bora, huku Tchetche akinyakua tuzo ya Mchezaji Bora na Amissi Tambwe akiwa Mfungaji Bora.
Wachezaji wote hao kila mmoja alizawadiwa kitita cha Sh. Mil. 5.2.

Zawadi nyingine zilizotolewa ni pamoja na Sh. Mil. 75 iliyokwenda kwa Azam waliotwaa ubingwa, Yanga walizoa Sh. Mil. 35, huku Mbeya City ikitwaa Sh. Mil. 26 na Simba waliokuwa wa nne walitwaa Sh. Mil. 21.

Tuesday, May 27, 2014

AC Milan kumtema Seedorf, Pipo kumrithi

Clarence Seedorf
KLABU ya AC Milan imedaiwa inajiandaa kumtimua kazi Kocha wake wa sasa Clarence Seedorf na nafasi yake huenda ikachukuliwa na kocha wa timu ya vijana na nyota wa zamani wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Italia (Azzurri) Filippo Inzaghi.
Kwa mujibu wa taarifa kutuka Italia zinasema kuwa, Seedorf aliyeinoa timu hiyo kwa muda wa miezi minne tu kati ya mkataba wake wa miaka miwili na nusu atafungashiwa virago kwa nia ya kuimarisha klabu hiyo imekuwa na msimu mbaya siku za karibuni kabla ya Mholanzi huyo kuisaidia kuindoa maeneo ya mkiani mwa Ligi Kuu ya nchi hiyo, Seria A.
Seedorf, 38, aliyeitumikia klabu hiyo kwa miaka 10 alipewa jukumu la kuinoa timu hiyo Januari mwaka huu kuchukua nafasi ya Massimiliano Allegri aliyefurushwa baada ya mkataba wake kusitishwa kutokana na mwenendo mbaya wa timu katika michuano iliyokuwa ikishiriki.
Pamoja na klutokuwa kocha mzoefu Mholanzi huyo aliiwezesha timu hiyo kushinda mechi 11 kati ya 19 ilizocheza Milan na kumaliza kwenye nafasi ya nane, tofauti na mtangulizi wake aliyeshinda mechi tano tu kati ya 19 za duru la kwanza.
Hata hivyo timu hiyo inayomilikiwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Italia, Silvio Berluscoini imekwama kushiriki hata michuano ya Ligi Ndogo ya Ulaya kutokana na kuangushwa na pointi moja tu, hali iliyowafanya wamiliki wake kutaka kuipanga upya mabingwa hao wa zamani wa Ulaya kurejesha hadhi yake msimu ujao.
.

Mbeya City wateleza Sudan, Wakenya waongoza kundi lao


WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya CECAFA Nile Basin Cup,Mbeya City chini ya kocha mkuu Juma Mwambusi wamefungwa mabao 2-1 na AFC Leopard ya Kenya katika mchezo uliopigwa usiku wa jana mjini Khartoum.
Bao la Mbeya City lilifungwa na kiungo mshambuliaji,Deus Kaseke, huku washindi wakitangulia kufunga mabao yao .
Ushindi huo unawafanya AFC Leopard wajikite kileleni mwa kundi B baada ya kufikisha pointi 6.

Stars, Malawi kupepetana leo Taifa, kiingilio buku 5

TIMU ya soka ya taifa, Taifa Stars jioni ya leo inatarajiwa kushuka dimbani kurudiana na The Flames ya Malawi katika mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11 kamili jioni.


Stars na Malawi zinavaana leo ikiwa ni wiki moja na ushei tangu zilipoppetana mjini Mbeya na kushindwa kutambiana zikijiandaa na mechi zao za kuwania kufuzu Fainali za Afrika za mwaka 2015 zitakazofanyika nchini Morocco.
Stars iliyopiga kambi yake Tukuyu mkoani Mbeya imewasili jijini Dar es Salaam  saa 4 asubuhi kwa ndege ya Air Tanzania tayari kwa mechi hiyo kujiandaa na mechi yao ya marudiano dhidi ya Zimbambwe itakayochezwa wikiendi hii mjini Harare.


Kiingilio katika mechi hiyo kitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani. Kwa upande wa VIP B na C kiingilio kitakuwa sh. 10,000 wakati kwa VIP A itakuwa ni sh. 20,000.


Hiyo itakuwa ni mechi ya mwisho ya majaribio kwa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kabla ya kwenda jijini Harare kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors).


Malawi (Flames) inayonolewa na mchezaji wake wa zamani Young Chidmozi nayo itakuwa inacheza mechi ya mwisho ya majaribio kabla ya kwenda N’djamena kuikabili Chad.

Video ya Shaa yakamilika

VIDEO ya staa wa zamani wa kundi la WAKILISHA, Sarah Kais 'Shaa' iitwayo 'Subira' imekamilika na wakati wowote itaanza kurushwa hewani.
Meneja wa msanii huyo, Said Fella alisema video hiyo iliyorekodiwa na kampuni ya Visual Lab, chini ya Adam Juma imekamilika na kwa sasa wapo katika hatua ya mwisho ya kuanza kuisambaza tayari kwa kurushwa hewani.
Alisema video hiyo imepigwa katika maeneo mbalimbali ya jijini Dar es Salaam na haitofautiani sana na ile ya 'Sugua Gaga' ambayho imemweka matawi ya juu msanii huyo.
"Video imekamilika kupigwa picha kwa sasa inarekebishwa kidogo kabla ya kuanza kusambazwa na mashabiki wa Shaa wajiandae kupata burudani zaidi na ile ya 'Sugua Gaga'," alisema.
Aliongeza, kukamilika kwa video ya wimbo huo ni mwanzo wa maandalizi ya kazi nyingine mpya za msanii huyo aliyekuwa mmoja wa washiriki na mshindi wa shindano la Coca Cola Pop Star lililofanyika mwanzoni mwa miaka ya 2000 na yeye Witness na Langa Kileo (marehemu) waliibuka kidedea kwa Tanzania na kwenda kuchuana na wasanii wenzao wa makundi ya nchi za Kenya na Uganda.

Sikinde kutambulisha mpya TZF Kigogo

Waimbaji wa Sikinde, Abdallah Hemba, Hassan Bitchuka
Bitrchuka (kushoto) akiimba huku Adolph Mbinga akicharaza gitaa
BENDI kongwe ya muziki wa dansi ya Mlimani Park 'Wana Sikinde' keshokutwa inatarajiwa kutambulisha nyimbo mpya kwa mashabiki wa  Kigogo ikiwa ni kwa mara ya kwanza ndani ya mwaka huu.
Katibu wa bendi hiyo, Hamis Milambo aliliambia gazeti hili kuwa, Sikinde itatambulisha nyimbo hizo zitakazokuwa katika albamu yao ijayo na zile za  zamani.
Milambo alisema mashabiki wa muziki wa dansi wamekuwa wakituma maombi ya kupelekewa burudani na wao wameitikia na watafanya hivyo Jumatano.
"Sikinde inatarajiwa kufanya onyesho maalum la kutambulisha nyimbo mpya za albamu yetu ijayo pamoja na kukumbushia vibao vya zamani kwa mashabiki wetu wa Kigogo walioililia bendi yao kwa muda mrefu," alisema.
Milambo alitaja nyimbo zitakazotambulishwa kuwa ni 'Jinamizi la Talaka', 'Kibogoyo', 'Tabasamu Tamu', 'Deni Nitalipa', 'Za Mkwezi' na Nundule' ambazo zinamaliziwa kurekodiwa albamu mpya ya bendi hiyo iliyotoa albamu ya mwisho mwaka 2011.
Nyimbo za zamani zitakazopigwa katika onyesho hilo kwa mujibu wa Milambo ni 'Kassim', 'Selina', 'Salam kwa Wazazi', 'Mv Mapenzi', 'Supu Imetiwa Nazi', 'Maisha Mapambano', 'Edita', 'Naomi' na 'Clara'.
"Yaani itakuwa bandika bandua kwa nia ya kusuuza nyoyo za mashabiki wetu ambao walitukosa kwa muda mrefu," alisema.

Utata pambano la Nyilawila, Mbelwa kuamuliwa na jopo

Said Mbelwa na Karama Nyilawila wakichuana Jumamosi kabla ya kutibua pambano lao
WAKATI hatma ya mshindi wa pambano la kimataifa kuwania mkanda wa UBO ikitarajiwa kuamuliwa chini ya jopo la mashirikisho ya ngumi Tanzania na UBO, Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPB)-Limited) imelaani kitendo kilichofanywa na bondia Said Mbelwa kumpiga Karama Nyilawila nje ya ulingo.
Mbelwa alimsukuma na kutupa nje ya ulingo mpinzani wake kabla ya kumrukia miguu miwili wakati wa pambano lao lililochezwa kwenye ukumbi wa Friends Corner, Manzese kwa kilichodaiwa kukerwa kupigwa kichwa na mpinzani wake.
Kitendo hicho kilipelekea pambano hilo kuvunjika katika raundi ya 8 kati ya 10 zilizokuwa zichezwe na mpaka sasa wasimamizi wa pambano hilo wameshindwa kumtangaza mshindi.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST), Anthony Rutta aliiambia MICHARAZO kwa njia ya simu jana kuwa wameshindwa kutangaza mshindi mpaka jopo la wadau wa ngumi wakutane kujadili tukio hilo kwa kina.
"Tunamsubiri  Rais wa PST, Emmanuel Mlundwea ambaye ni Mwakilishi wa UBO-Afrika, arejee toka Thailand na kuitisha kikao cha jopo la wadau wa ngumi ikihusisha vyama vya PST, TBBO na TPBC kujadili kilichotokea na kutoa maamuzi kwa sasa nahofia kusema lolote," alisema Rutta.
Alipoulizwa juu ya kanuni na sheria kwa bondia anayeanzisha fujo kwenye ulingoni kwa namna yoyote na kuvuruga pambano adhabu yake huwa ni nini, Rutta alisema huwa si chini ya kifungo cha miezi 6 cha kutocheza ngumi.
"Atalkayebainika anaweza kufungiwa kati ya miezisita na miaka miwili na mpinzani wake kupewa ushindi kulingana na itakavyobainika nani mkosa," alisema.
Hata hivyo, Rais wa TPBO-Limited, Yasin Abdallah 'Ustaadh' waliosimamia pambano ya utangulizi siku ya pambano hilo la Nyilawila na Mbelwa alilaani tukio hilo na kuelekeza lawama zake kwa Mbelwa kuwa hakufanya uungwana.
"TPBO tunalaani kilichofanywa na Mbelwa, kwani siyo uungwana hata kama mwamuzi na mpinzani wake hawakumtendea haki kwenye ulingoni, mambo haya ndiyo yanayovuruga mchezo wetu na kuonekana wa kihuni," alisema.
Ustaadh alisema pia anashangazwa mtandao wa UBO kutoa taarifa mechi hiyo haina mshindi wakati mwakilishi wake, Emmanuel Mlundwa yupo nje ya nchi na hakuwepo kwenye pambano hilo.
"Sidhani kama ni sahihi, Mlundwa hakuwepo ukumbini, ila mtandao wao umetoa ripoti kuwa mchezo hauna mshindi, nani aliyetoa taarifa hizo wakati mwakilishi yupo Thailand," alisema Ustaadh na kuoingeza;
"Kama ingekuwa ni  sisi TPBO moja kwa moja trungemtangaza Nyilawila kuwa mshindi kwa sasa kilichofaywa na mpinzani wake kipo nje ya kanuni na sheria ya ngumi na TPBO tunalaani kwai inatuvurugia sana ngumi zetu," alisema.

Wakazi King'ongo wachimbwa mkwara, kisa michango ya Ulinzi

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa King'ongo, Demetrius Mapesi
UONGOZI wa Serikali ya Mtaa wa Kimara-King'ongo, kata ya Saranga wilaya ya Kinondoni umewachimba mkwara wakazi wake ambao watashindwa kulipa Sh 3,000 kwa ajili ya Ulinzi Shirikishi ukisema ni suala muhimu kwa taifa.
Mkwara huo umetolewa na Mwenyekiti wa mtaa huo, Demetrius Mapesi katika mkutano uliowahusisha wajumbe wa nyumba 10 na baadhi ya wakazi wa mtaa huo uliohudhuriwa na Mkuu wa Kituo cha polisi Kimara Mwisho, Mfaume Msuya.
Mapesi alisema suala la ulinzi shirikishi ni la lazima kwa kila mkazi wa eneo hilo na wale wasioweza  kushiriki kulinda watalazimika kulipa kiasi hicho cha fedha kitakachohusisha kila kaya kwa ajili ya  kuwalipa walinzi watakaoshiriki kufanya doria usiku.
Mwenyekiti huyo alisema kumekuwa na kusuasua kwa zoezi hilo kutokana na wakazi wengi kutolipa  fedha hizo kwa kisingizio cha kuwa na walinzi wao katika maduka na nyumba zao, kitu alichodai hata wao wanalazimika kulipa fedha hizo la sivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Alisema moja ya hatua ni kuwafikisha polisi kabla ya kuburuzwa mahakama ya Jiji ambako watakutana na na adhabu ya kifungo pamoja na fidia kisichopungua Sh 50,000.
"Wenyewe mmesikia ripoti ya kamati ya ulinzi ambayo kati ya walinzi 20 waliokuwa wakilinda awali  wamesalia wanne tu kutokana na kusuasua kupatikana kwa malipo ya kuwalipa posho, sasa  tunaweka wazi kwamba suala hili siyo hiari, ni  lazima na atakayekiuka atachukuliwa hatua," alisema.
Alisema kuwa, ulinzi huo umekuwa ukisaidia kuweka mtaa wao salama dhidi ya wahalifu na kuwataka  wananchi kuuunga mkono uongozi wao, kwani ni kwa faida yao kwani uhalifu ukipungua inawapa  nafasi ya kufanya shughuli zao kwa ufanisi na kwa amani.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo aliwakanganya wananchi kwa kueleza kila kichwa kitalazimika kulipa kiasi hicho cha fedha wakiwamo wapangaji na wenye nyumba wanaoishi katika mtaa huo.
Katika kusisitizia mkwara huo, Mkuu wa Kituo cha Kimara, Mfaume Msuya alisema kituo chake  kimejenga eneo kubwa la kuweza kuwasweka wale watakaofikishwa hapo kwa ajili ya kosa hilo la  kutolipa fedha hizo za ulinzi shirikishi.
"Wasiolipa waleteni kwangu, nitawahifadhi kabla ya kuwafikisha mahakamani na ninashukuru kwa sasa  eneo la Kimara uhalifu umepungua kwa sababu ya ulinzi shirikishi kwa sasa kesi nyingi ni za fumanizi  na masuala ya mapenzi, kwa nini tuwachekee wanaokwamisha ulinzi huo," alisema Afande Msuya na  kufafanua kuwa sheria namba 82 ya ulinzi ndiyo itakayowashughulikia wakwepaji hao.

Masai ya Wapi anayejitoa kundini?!

Masai katika pozi
Masai Nyota Mbof

WAKATI akiwa mbioni kuachia video ya wimbo wake mpya uitwao 'Masai ya Wapi' alioimba na Christian Bella, mchekeshaji maarufu nchini, Gilliad Severine 'Masai Nyota Mbofu' ametangaza kujiengua Al Riyami Production.
Akizungumza na MICHARAZO, Masai anayetamba na nyimbo za 'Rungu na Mukuki' na 'Yero Masai' aliouachia hivi karibuni, alisema ameamua kujiengua Al Riyami inayoendesha vichekesho vya 'Vituko Show' kutokana na kutoridhishwa na hali ya mambo na sasa atajitegemea hadi atakapotua kundi au kampuni nyingine ya uigizaji.
Masai alisema kuondoka kwake hakuna maana kama kuna ugomvi na yeyote ila ameamua kubadilisha upepo na kujikita zaidi kwenye  muziki, japo ataendelea kucheza filamu kwa yeyote atakayemhitaji.
Kuondoka kwa Masai kumezidi kulidhoofisha kundi hilo kwani kabla ya hapo wakali kama akina KItale, Mzee Majuto, Kingwendu, Ringo na Gondo Msambaa nao walijeingua kwa nyakati tofauti, huku wasanii wengine wakipunguzwa kundini humo kwa sababu mbalimbali.
Kuhusu kazi yake mpya, Masai alisema kwa sasa anajiandaa kuitoa hadharani video ya wimbo wa 'Masai ya Wapi'.
Alisema amepanga kutoa video tu wa wimbo huo bila 'audio' yake kwa sababu zake na kwamba kazi hiyo mpya ameimba kwa kushirikiana na Christian Bella.
"Wakati video ya wimbo wangu wa 'Yero Masai' ikianza kubamba katika runinga, nipo katika maandalizi ya mwisho ya kukamilisha na kuiachia video nyingine ya wimbo wa 'Masai ya Wapi', huu sitatoa 'audio' yake," alisema Masai.

10 kuwania taji la Miss B'moyo 2014, Mapacha Wa3 kunogesha

Washindi wa Miss Bagamoyo kwa mwaka jana wakiwa katika pozi
BENDI ya muziki wa dansi ya Mapacha Watatu wanatarajiwa kuwasindikiza warembo 10 watakaokuwa wakiwania taji la urembo la wilaya ya Bagamoyo 'Miss Bagamoyo 2014' katika shindano litakalofanyika siku ya Jumamosi wilayani humo.
Mratibu wa shindano hilo, Awetu Salim, Mkuregenzi wa Asilia Decoration, aliliambia MICHARAZO
kuwa, shindano hilo litafanyika kwenye ukumbi wa hoteli Palme Tree Village wilayani humo na maandalizi yote yamekamilika na warembo wanaendelea na kambi yao mjini humo kujiandaa na mchuano huo.
Awetu alisema warembo hao watakaosindikizwa na burudani toka bendi ya Mapacha Watatu chini ya Khaleed Chuma 'Chokoraa' na Jose Mara watachuana kurithi taji hilo linaloshikiliwa kwa sasa na Elizabeth Pertty aliyetwaa katika shindano la mwaka jana (2013).
Mratibu huyo aliwataja warembo watakaochuana hiyo Jumamosi kwa jina moja moja kuwa ni; Faith, Dora, Glory, Susan, Khadija, Princess, Nkyali, Manka, Amina na Zena.
"Shindano la Miss Bagamoyo 2014 litafanyika siku ya Jumamosi ya Mei 31 jumla ya warembo 10 watachuana kuwania taji hilo na nafasi za ushiriki wa michuano ya Miss Pwani 2014, tayari tumefanikiwa kupata wadhamini kadhaa baadhi ni Chama cha Wavuvi wilaya ya Ukerewe, Duran Sound, Palme Tree Village, D'z Restaurant and Take Away," alisema Awetu.
Awetu alisema warembo watatu wa kwanza licha ya kupata zawadi, lakini wataingia kwenye kinyang'anyiro cha kushiriki shindano la Miss Pwani litakalofanyika baadaye mwaka huu.

Simanzi tena:Rachel 'Recho' Haule wa Bongo Movie afariki

MUIGIZAJI aliyekuwa anazidi kuja juu katika Bongo Movie, Rachel Haule 'Recho' afariki asubuhi hii Muhimbili Hosp, Dar es Salaam baada ya kujifungua kwa upasuaji, ambapo mtoto alifariki tangu jana.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na muigizaji mwenzake, Zuwena Mohammed 'Shilole', Recho alikumbwa na mauti hayo na kwa sasa wanajipanga kukutana Leaders kwa ajili ya kujua taratibu za mazishi za msanii mwenzao ambaye alikuwa katika hali mbaya tangu alipofanyiwa upasuaji kiasi cha kukimbizwa ICU kabla ya kukumbwa na mauti asubuhi hii.
Kifo cha Recho kimekuja ndani ya wiki moja baada ya kufariki kwa msanii mwingine wa Bongo Movie Adam Kuambiana , huku pia fani ya sanaa ikishuhudiwa ikimpoteza mwanamuziki Amina Ngaluma 'Japanese' aliyefariki nchini Thailand aliyezikwa siku ya Jumamosu.
MICHARAZO inatoa pole kwa ndugu, jamaa na familia ya marehemu Recho na Bongo Movie kwa ujumla kwa kuwataka kuwa na subiora katika kipindi hiki kigumu kwa kutambua kuwa kila Nafsi itaonja Mauti, yeye katangulia sisi tu nyuma yake.

Friday, May 16, 2014

Du! Luis Suarez azidi kuvuna tuzo England

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Liverpool Luis Suarez amezidi kuongeza tuzo katika kabati lake la kuhifadhia tuzo zake, baada ya kuteuliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Uingereza msimu wa 2013-2014.
Nyota huyo aliyefunga mabao 31 na kutoa pasi 12 za mabao katika mechi 33 za ligi alizocheza, huku timu yake Liverpool ikizidiwa kidogo na Manchester City katika mbio za ubingwa, poia ndiye mfungaji bora wa ligi hiyo. 
Suarez, ambaye pia ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Wachezaji wa PFA na Mchezaji Bora wa Waandishi wa habari za Soka msimu huu, ameshinda tuzo ya nne msimu huu pamoja na ile ya kiatu cha dhahabu. 
Tuzo hiyo Suarez imekuja ikiwa ni saa chache baada ya meneja wa Liverpool Brandan Rodgers naye kutunukiwa tuzo ya kocha bora wa mwaka na Chama cha Makocha wa Ligi nchini humo. 
Rodgers amekuwa na msimu mzuri akiiongoza timu hiyo ya Merseyside kumaliza nafasi ya pili kwenye ligi. 
Kocha wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson ndiye alimkabidhi tuzo hiyo kocha huyo mwenye umri wa miaka 41, ambayo hutokana na kura zinazopigwa na makocha kutoka timu za madaraja yote manne.
Kabla ya hapo mshambuliaji huyo alikuwa na wakati mgumu kutokana na matukio ya utovu wa nidhamu yaliyomsababisha kufungiwa kucheza mechi kadhaa na kutoza faini kwa kumbagua Patrick Evra na kung'ata beki wa Chelsea.

HUYU NDIYE AMINA NGALUMA 'JAPANESE'


MIEZI miwili iliyopita nilifanya mahojiano na Amina Ngaluma kuhusu shughuli zake za muziki akiwa ughaibuni, Mashariki ya Mbali nchini Thailand ambapo alieleza mambo mengi kuhusu safari yake na ndoto zake katika tasnia ya muziki aliyoianza tangu akiwa kinda.
Mwanamuziki huyo aliyefariki jana nchini Thailand, atakumbukwa kwa kiu yake ya kufika mbali kisanii.
MICHARAZO inakuweka makala ya mwanamuziki huyo kama alivyozungumza na blogu hii na iliyotumika pia kwenye gazeti la NIPASHE, kujua historia yake kama njia ya kumuenzi mwanamuziki huyo aliyekuwa mcheshi wa kila mtu.
ISOME:

MASHABIKI wa muziki wanamfahamu kwa jina la Japanese, ingawa majina yake halisi ni Amina Kassim Ngaluma, mmoja wa waimbaji mahiri wa kike wa muziki wa dansi nchini anayefanya kazi ughaibuni.
Japanese, aliyewahi kuziimbia bendi mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa sasa anafanya shughuli zake za muziki akiwa na bendi ya Jambo Survivors iliyopo Thailand, Mashariki ya Mbali barani Asia.
Mwanadada huyo anakiri licha ya kipaji cha muziki cha kuzaliwa, lakini alijikuta akipenda kuwa mwanamuziki kwa kuvutiwa na muimbaji nyota wa zamani wa Kongo, Mbilia Bell.
Anasema sauti na uimbaji wa Mbilia ulikuwa ukimkuna na kutamani kuwa kama muimbaji huyo, hivyo kuja kuangukia mikononi mwa nyota wa taarab nchini, Bi. Shakila Said, aliyemnoa kwenye uimbaji.
"Siyo siri nilimzimia mno Mbilia Bell, nikatamani kuwa kama yeye na kwa bahati nikaangukia mikononi mwa Bi Shakila aliyeninoa na kuwa hivi nilivyo kupitia kundi la JKT Taarab," anasema.
Anasema hata hivyo alipata wakati mgumu kwa vile mama yake hakupenda awe mwanamuziki badala yake kutaka afanye kazi za ofisi, tofauti na baba yake aliyemuunga mkono hadi leo ukubwani.
Japanese anasema baada ya kuiva kwa Bi Shakila pale JKT Taarab alihamia katika muziki wa dansi akianzia Less Mwenge-Arusha kisha   kukimbilia Kenya alipojijengea jina akizipigia bendi mbalimbali.
"Niliizipigia bendi za Sayari iliyokuwa chini na Badi Bakule 'Mkandarasi', Sky Sound iliyoongozwa na Mwinjuma Muumin, kisha Mangelepa ya Evanee kabla ya kurejea Tanzania," anasema.
Anasema aliporejea nchini alijiunga na African Revolution 'Tamtam' iliyomjengea jina kabla ya kwenda Double M Sound kisha TOT-Plus kabla ya kuhamia Jambo Survivors alionao mpaka sasa.
Japanese anaitaja bendi ya African Revolution kama ilimtambulisha katika ulimwengu wa muziki, ila bendi ya mafanikio na maendeleo kwake ni Jambo Survivors iliyomuinua kiuchumi toka alipokuwapo.

MKALI
Japanese aliyekuwa mahiri kwa mchezo wa Netiboli alioucheza kwa mafanikio kabla ya kutumbukia kwenye muziki, pia ni mahiri kwa utunzi wa nyimbo baadhi ya tungo zake ziliwahi kutikisa muziki wa Tanzania.
Baadhi ya nyimbo alizotunga mwanadada huyo mwenye ndoto za kuja kumiliki bendi binafsi akishirikiana na mumewe ambaye pia ni mwanamuziki Rashid Sumuni ni; 'Mapendo', 'Manyanyaso Kazini', 'Ukewenza', 'Wajane' na Mwana Mnyonge'.
Pia alishawahi kupakua albamu binafsi iitwayo 'Jitulize' aliyoizindua mkoani Morogoro ikiwa na nyimbo sita baadhi ni 'Jitulize', 'Uombalo Hutopata', 'Pete ya Uchumba', 'Mapenzi ya Kweli' na 'Tulia Wangu'.
Japanese anayefurahia tukio la kufunga ndoa na mumewe Rashid Sumuni na kulizwa na kifo cha kaka yake, Mashaka Ngaluma aliyeuwawa na majambazi kwa kupigwa risasi akiwa kazini kwake.
"Kwa kweli matukio haya ndiyo yasiyofutika kichwani mwangu, nilipofunga ndoa na mume wangu kipenzi, Rashid Sumuni na siku kaka yangu alipouwawa kwa risasi akiwa kazini," anasema.

MAFANIKIO
Japanese asiyefuatilia soka aliota kuja kuwa Daktari ila muziki ukaja kumbeba jumla, ingawa hajutii kwa namna fani hiyo ilivyomsaidia kwa mambo mengi ya kujivunia.
Anasema mbali na kupata rafiki wengi, kutembea nchi mbalimbali duniani na kujifunza tamaduni tofauti, pia muziki umemwezesha yeye na mumewe kumiliki miradi kadhaa ya kiuchumi, nyumba na magari.
Hata hivyo anasema bado hajaridhika hadi atakapoanzisha bendi yao ya Skwensa hapa nchini itakayokuwa ikipiga mahotelini na kurekodi kazi zake katika studio yao binafsi.
Pia angependa kuwasaidia waimbaji wa kike ili kusaidia kuongeza idadi yao katika muziki wa dansi alikodai imekuwa ikizidi kupungua kwa sababu wengi wao hawapendi tabu wala kujifunza muziki.
"Waimbaji wa kike hawapendi dansi kwa ugumu wake hivyo huona bora wajikite kwenye muziki wa kizazi kipya, ila kujifunza muziki wa dansi hasa upigaji ala husaidia kujitangaza kimataifa," anasema.

JUMBE
Japanese alizaliwa Nov 29, mjini Morogoro akiwa ni mtoto wa tatu kati ya tisa wa Baba Kassim Ngaluma na Mama Khadija Abdallah, watatu kati yao wakiwa wameshatangulia mbele ya haki ya kubakia sita tu.
Mkali huyo yupo Jambo Survivors inayopiga muziki wake katika hoteli iitwayo Banthai Beach Resort & SPA akiwa na Hassan Shaw, Eshter Lazaro, Ramadhani Kinguti, Yuda Almasi na mwana BSS Edson Teri.
Mwanadada huyo anasema kwa hapa nchini anawazimia wanamuziki  Hussein Jumbe na Nyota Waziri.
"Hawa ndiyo wanaonikosha na umahiri wao katika muziki," anasema.
Japanese anayewataka wanamuziki wenzake kuwa wabunifu ili kwenda na mabadiliko ya dunia na kuiomba serikali kuutupia macho muziki wa dansi anamshukuru Mungu kwa kumsaidia kufika alipo.
Pia anawashukuru wazazi wake kwa sapoti kubwa anayompa, mumewe Rashid Sumuni pamoja na mwalimu wake Shakila Said bila kuwasahau wote walio bega kwa bega katika fani yake kwa ujumla.

Zimbambwe usiku wa leo, Samatta waja kuibeba Stars

Samata (kati) na Ulimwengu (kulia) wakiwa na Kiemba . Nyota hao watatua keshjo kuisaidia Stars kuiangamiza Zimbabwe
TIMU ya soka ya taifa ya Zimbabwe inawasili usiku wa kuamkia Jumamosi (Mei 17 mwaka huu) ikiwa na msafara wa watu 27 kwa ajili ya mchezo wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa Afrika mwaka 2015 nchini Morocco Jumapili, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Timu hiyo itatua saa 7.30 usiku kwa ndege ya Ethiopian Airlines na itafikia hoteli ya Sapphire Court iliyopo Mtaa wa Lindi, Dar es Salaam.

Zimbabwe itafanya mazoezi siku hiyo jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam tayari kwa mechi hiyo itakayochezwa Jumapili saa 10:00 jioni kwenye uwanja huo huo.
Wakati huo huo: Wachezaji wa kimataifa wa Tanzania wanaochezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanatarajiwa kuwasili Jumamosi mchana (Mei 17 mwaka huu) kujiunga na Taifa Stars kwa ajili ya mechi dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors).
Washambuliaji hao watatokea moja kwa moja Sudan ambapo kesho (Mei 16 mwaka huu) TP Mazembe itacheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya timu ya huko.
Ujio wa washambuliaji hao utafanya wachezaji wote kutoka nje walioitwa na Kocha Mart Nooij kuwa wamepatikana kwa ajili ya mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Afrika ambalo fainali zake zitachezwa mwakani nchini Morocco. Mchezaji mwingine wa nje ambaye tayari ameripoti Stars ni Mwinyi Kazimoto anayecheza nchini Qatar.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linamshukuru Mmliki wa TP Mazembe ambaye pia ni Gavana wa Jimbo la Katanga, Moise Katumbi kwa kuwaruhusu wachezaji hao kujiunga na Taifa Stars kwa vile mechi dhidi ya Zimbabwe ipo nje ya kalenda ya FIFA.
Naye Kocha Nooij atakuwa na mkutano na Waandishi wa habari kesho (Mei 16 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi kwenye kambi ya Taifa Stars iliyopo katika hoteli ya Accomondia.

Simanzi! Amina Ngaluma Japanese afariki ughaibuni

Amina Ngaluma Japanese enzi za uhai wake
TASNIA ya muziki wa dansi imezidi kupata pigo baada ya nyota wa zamani wa bendi za African Revolution 'Tamtam', TOT-Plus na Double M Sound, Amina Ngaluma 'Japanese kufariki dunia.
Mtunzi na muimbaji huyo aliyekuwa akiitumikia bendi ya Jambo Survivors amefariki dunia mchana wa jana akiwa ughaibuni nchini Thailand alipokuwa akifanya shughuli zake za muziki na bendi hiyo.
Taarifa ambazo MICHARAZO ilizipata mapema, zilisema kuwa marehemu alikumbwa na mauti baada ya kuugua ghafla kichwa na kubainika alikuwa na uvimbe uliopasuka na damu kuchanganyika na ubongo.
Baadhi ya wasanii waliowahi kufanya nao kazi, walisema kuwa walipewa taarifa na mume wa marehemu, Rashid Sumuni ambaye ni mcharaza gitaa kuwa mkewe amefariki ughaibuni.
Kifo cha Ngaluma kimetokea wakati wadau wa muziki wa dansi wakiwa hata hawajasahau msiba mzito uliowapata baada ya gwiji Muhidini Mwalimu Gurumo 'Kamanda' kufariki mwezi uliopita.
Mungu ailaze mahali Pema Peponi Roho ya Amina Ngaluma 'Japaness' ambaye alifanyiwa mahojiano na blogu hii miezi michache iliyopita akieleza mipango yake ya kuja kuanzisha bendi na mumewe.
Kwa hakika kila nafsi itaonja mauti, na siku zote kifo hutenganisha wapendanao na kukatisha ndoto za waja, ila kwa kuwa ni kazi ya Mola tunabidi kumshukuru Maanani kwani yeye alimpenda zaidi.

Tuesday, May 13, 2014

Nyota wa zamani Simba kutimkia Afrika Kusini

David Naftari
BEKI wa zamani wa AFC Arusha na Simba, David Naftar anajiandaa kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya kufanya majaribio baada ya mkataba wake na Bandari Kenya ukielekea ukingoni.
Mchezaji kiraka huyo anayemudu nafasi nyingi uwanjani, alisema ataenda kwenye majaribio hayo mara baada ya kumalizika kwa duru la kwanza la Ligi Kuu ya Kenya iliyosaliwa raundi tatu kabla ya kuisha.
Akizungumza na MICHARAZO kutoka Kenya anakocheza soka la kulipwa katika klabu ya Bandari, Naftari alisema mipango hiyo ya kwenda Afrika Kusini inafanywa na wakala wake.
"Japo sijaambiwa nitaenda kujaribiwa katika klabu gani, lakini nitaondoka baada ya ligi kusimama, kwa sasa tumebakisha mechi tatu kabla ya duru hilo kumalizika," alisema.
Kuhusu mktaba wake na Bandari, Naftari alisema unafikia tamati Agosti mwaka huu na tayari viongozi wake wameonyesha nia ya kutaka kumuongezea, lakini mwenyewe hajafanya maamuzi bado.
"Uongozi wa Bandari unaonyesha bado unanihitaji, lakini nataka kwanza niende majaribuni nikirudi nitajua la kufanya kwani mkataba unaisha mwezi wa nane," alisema.
Mchezaji huyo alisema kwa kuwa soka ni maisha yake, daima huwa anapigana kuzidi kusonga mbele zaidi na alipo ndiyo maana hataki kurejea Tanzania kucheza baada ya kuchoshwa na mizengwe.
Naftari alikuwa miongoni mwa wachezaji walioibeba Bandari baada ya kipa Ivo Mapunda, Mohammed Banka na Thomas Mourice waliorejea nchini na Meshack Abel wanaendelea kuichezea mpaka sasa.

Rodgers wa Liverpool, Tony Pullis watwaa tuzo England

RODGERS AKIKABIDHIWA TUZO YAKE
KOCHA wa Liverpool, washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Engalnd, Brendan Rodgers ameshinda tuzo ya kocha bora kuliko wote nchini England.
Tuzo hiyo maarufu kama LMA hutolewa baada ya makocha katika madaraja yote nchini humo kupiga kura kumchagua nani ni bora zaidi.
PULLS AKIPEWA TUZO
Pamoja na Liverpool kushika nafasi ya pili lakini Rodgers amekuwa kocha wa Liverpool kushinda tuzo hiyo.
Wakati kocha huyo wa Liverpool akibeba tuzo hiyo ya juu zaidi, Tony Pulls wa Crystal Palace amekuwa kocha bora wa Ligi Kuu England.
Hii maana yake, Rodgers ni bora kwa England kwa kujumuisha na ligi zote ikiwemo Ligi Kuu England wakati Pulls ni kocha wa ligi hiyo moja tu.

Machaku asema hana mkataba JKT Ruvu zinazomtaka zimfuate

MSHAMBULIAJI nyota wa JKT Ruvu, Salum Machaku 'Balotelli' amesema hana mkataba wowote na timu hiyo na hivyo kuiacha milango wazi kwa klabu yoyote inayomhitaji kuzungumza naye.
Machaku aliyewahi kutamba na timu za Simba, Mtibwa Sugar na Polisi Morogoro, alisema yupo tayari kutua katika klabu yoyote itakayokuwa ikimhitaji mradi waridhiane katika suala la masilahi.
Mshambuliaji huyo aliyemaliza msimu huu akiwa na mabao manne alisema kwa sasa amekaa tayari kupokea maombi kutoka kwa timu yoyote ili kuweza kujiunga nayo au ikiwezekana kubaki JKT.
Alipoulizwa kama timu yake ya zamani ya Polisi Moro iliyorejea Ligi Kuu ikimfuata ili kumrejesha kikosini, alisema angefurahia kwa sababu hakuondoka kwa ugomvi katika timu hiyo iliposhuka daraja.
"Nipo tayari kurudi Polisi Moro, ni timu ninayoiheshimu, pia maisha yangu yanategemea soka sina cha kuchagua wala kubagua ila nimefurahi kuona wamerejea tena ligi kuu," alisema.
Machaku, mmoja wa watoto wa nyota wa zamani wa muziki wa dansi aliyewahi kutamba na bendi za Dar International na DDC Mlimani Park, Salum Machaku, alisema anaamini ligi ya msimu ujao itakuwa ngumu kuliko ya msimu huu ambayo haikutabirika kirahisi.
"Ligi ya msimu huu ilikuwa ni noma, siyo kwa timu za juu wala mkiani. Hapakuwa na iliyokuwa na uhakika wa itakachovuna hadi dakika za mwisho," alisema.

Hiki ndicho kikosi cha Black Stars, wamo Essien, Boateng

KIUNGO nyota wa AC Milan, Michael Essien na Kevin-Prince Boateng wamejumuishwa kwenye kikosi cha awali cha wachezaji 26 kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia.
Kikosi hicho kitapunguzwa na kubaki wachezaji 23 baada ya mchezo wa kirafiki na Uholanzi Mei 31, ambacho ndiyo watakwenda Brazil.
Essien na Boateng wameitwa baada ya kurejea kwenye soka ya kimataifa mwaka jana, kufuatia awali kuomba kujipumzisha kuichezea timu hiyo.
Nchi ya Ghana imepangwa kundi moja na timu za  Marekani, Ujerumani na Ureno likitajwa kuwa ni moja ya makundi ya kifo katika fainali za mwaka huu zitakazoanza mwezi ujao nchini Brazili.

Kikosi kamili cha Black Stars ni kama kifuatavyo:
Makipa: Stephen Adams (Aduana Stars), Fatau Dauda (Orlando Pirates), Adam Kwarasey (Stromsgodset)
 
Mabeki: Harrison Afful (Esperance), Jerry Akaminko (Eskisehirspor), John Boye (Stade Rennes), Samuel Inkoom (Platanias), Jonathan Mensah (Evian Thonon Gaillard), Daniel Opare (Standard Liege), Jeffrey Schluup (Leicester City), Rashid Sumaila (Mamelodi Sundowns)
 
Viungo: David Accam (Helsingborg), Afriyie Acquah (Parma), Albert Adomah (Middlesbrough), Emmanuel Agyemang Badu (Udinese), Kwadwo Asamoah (Juventus), Christian Atsu (Vitesse Arnhem), Andre Ayew (Olympique Marseille), Michael Essien (AC Milan), Rabiu Mohammed (Kuban Krasnodar), Sulley Muntari (AC Milan), Mubarak Wakaso (Rubin Kazan)
 
Washambuliaji: Jordan Ayew (Sochaux), Kevin Prince Boateng (Schalke 04), Asamoah Gyan (Al Ain), Abdul Majeed Waris (Valenciennes).

Homa ya Dengue yampitia Pentangone wa Twanga

MUIMBAJI wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta', Ramadhani Mhoza 'Pentagone' ameongeza idadi ya wasanii waliokumbwa na ugonjwa mpya wa homa ya Dengue baada na kulazwa hospitalini kutokana na kuugua ugonjwa huo unaofanana na Malaria.
Pentagone alikumbwa na ugonjwa huo wiki iliyopita na kulazwa hospitalini kwa siku tatu kabla ya kupata nafuu na kuruhusiwa kwenda kujiuguzia nyumbani kwake, ambako kwa sasa anaendelea vyema.
Akizungumza na MICHARAZO akiwa mapumziko nyumbani kwake, Pentagone, alisema hakuwa anajua lolote kuhusu ugonjwa huo mpya hadi alipokimbizwa hospitalini baada ya kuumwa kichwa, kuhisi uchovu na kuumwa kwa viungo vya mwili na alipopimwa na madakatari aligundulika kuambukizwa homa hiyo mpya inayozidi kushika kasi kwa sasa nchini.
Pentagone alisema anashukuru kwa sasa anaendelea vyema japo bado hana nguvu na anaamini wakati wowote atarejea tena jukwaani kuungana na wanamuziki wenzake.
"Namshukuru Mungu naendelea vyema, nilikuwa hoi hospitalini kutokana na hii homa mpya iitwayo Dengue, kwa sasa sina nguvu tu mwilini, lakini naendelea vyema," alisema.
Kuugua kwa Pentagone kumefanya idadi ya wasanii waliokumbwa na homa hiyo kufikia watatu kwa sasa baada ya awali mwanadada Rehema Chalamila 'Ray C' kuthibitishwa kuugua ugonjwa huo na kulazwa hospitali sawa na ilivyomkuta pia, Mukhsen Awadh 'Dk Cheni na muigizaji mkongwe ambaye kwa sasa ni mtangazaji wa Times Fm, Susan Lewis 'Natasha'.
Ugonjwa huo unaelezwa kuambukiwa na mbu aina ya Aedes unafanana kwa kiasi kikubwa na ugonjwa wa Malaria kwa dalili zake na watu wanaohisi kuupata wanahimizwa kuwahi hospitalini kupata matibabu.