STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, May 22, 2012

Ramadhani Singano: Messi wa Simba anayemzimia Boban

<
KIPAJI kikubwa cha soka alichonacho hasa kumiliki mpira, kupiga chenga, mbio na kufunga, kimemfanya kinda la timu ya Simba, Ramadhani Singano kufananishwa na nyota wa Barcelona, Lionel Messi. Wadau wa soka hasa wa klabu ya Simba humfahamu zaidi kwa jina la Messi kuliko majina yake halisi, wakimlinganisha kiuchezaji na nyota huyo wa Argentina anayetajwa kama mwenye kipaji cha pekee duniani. Licha ya kufurahia jina hilo, Singano anakiri hajafikia hata robo ya umahiri wa Messi anayemhusudu na kumuiga uchezaji wake. Singano, aliyewapoteza wazazi wake akiwa na miaka 11, alisema anamshukuru Mungu kwa kumjalia kipaji hicho, ila anaamini ana kazi kubwa ya kufika alipo 'wajina' wake. Hata hivyo, Messi aliyeanza kucheza kama beki enzi za soka la chandimu, alisema nidhamu, mazoezi, kujituma na kumtumainia Mungu kutamfikisha mbali kisoka. "Naamini nikijituma zaidi, nikazingatia nidhamu na kumtanguliza Allah, katika kila kitu, nitafika mbali kwani najiamini naweza," alisema. Messi, alizichezea timu za Ubatani na Bombom kabla ya kuonwa na Simba B, alisema japo hana muda mrefu katika soka, anashukuru mafanikio aliyopata. "Soka limenisaidia mengi kimaisha na kiuchumi, ila sipendi yaandikwe, lakini kufahamika, kuheshimiwa na kumudu kuwasaidia ndugu na jamaa zangu, ni vitu vya kujivunia," alisema. Pia, alisema kutwaa mataji, medali na tuzo mbalimbali akiwa na Bombom na Simba B, ikiwemo kuwa Mchezaji Bora mara tatu katika michuano ya Rolling Stone, Uhai Cup na Copa Coca Cola 2009 ni mengine yanayomfariji. "Mwaka jana pekee nimetwaa mataji mawili ya Uhai na Kinesi nikiwa Simba B na msimu huu nimesherehekea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara nikiwa na Simba," alisema. Messi, anayemzimia na kuvutiwa na soka la Haruna Moshi 'Boban', alisema hakuna tukio la furaha kwake kama alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mchezaji bora wa michuano ya Uhai-2009. "Furaha niliyokuwa nayo ilinifanya nigawe fedha za zawadi kwa wachezaji wenzangu wa Simba B, nakumbuka nilitoa Sh. 150,000 kati ya 400,000," alisema. Kwa matukio ya huzuni, Messi alisema ni kuwapoteza wazazi akiwa mdogo na kunusurika kufa kwa ajali ya gari alipotoka kumzika baba yake mjini Tanga mwaka 2003. Mchezaji huyo anayependa kula mihogo ya kuchemsha, ugali kwa bamia na kunywa juisi ya Parachichi, alisema hupenda kutumia muda wake mwingi kufanya ibada na kuangalia 'muvi' hasa za filamu za Jean Claud van Damme. Aliwashukuru makocha wake, Ahmed Mohammed Kibonge, Teddy na Bosco waliokivumbua na kukiendeleza kipaji chake kiasi cha leo kuonekana 'lulu'. "Nawashukuru mno hasa Kibonge aliyetambua kipaji changu wakati anasoma Shule ya Sekondari Al Farouk na kunipeleka katika timu yake ya Bombom." Alisema, Simba B ilivutiwa naye baada ya kung'ara katika mechi dhidi ya Bombom na kusajiliwa katika kikosi hicho mwaka 2009 na kuja kupandishwa timu ya wakubwa msimu huu akiwa na wenzake wanne. Messi, anayemudu karibu nafasi zote dimbani, japo hufarahia kucheza kama mshambuliaji, alisema hawezi kuzisahau mechi mbili akiwa na Simba dhidi ya Azam na Kiyovu Sport ya Rwanda katika Kombe la Shirikisho Afrika. "Nazikumbuka kwa vile zilizokuwa mechi kubwa za kwanza kwangu na namna nilivyoonyesha kiwango cha hali ya juu nikisaidia moja ya mabao mawili ya ushindi dhidi ya Azam katika Ligi Kuu," alisema. Mkali huyo anayeota kucheza soka la kulipwa nje ya nchi na kuanzisha asasi ya kusaidia yatima na wenye matatizo, alisema soka la Bongo lipo juu, ila baadhi ya wachezaji hawajitambui na kuchangia kulikwamisha. Alisema huenda kukosa misingi bora ya soka ni tatizo kwa wachezaji nchini, ila aliwataka wazinduke na kutambua soka ni ajira yao hivyo walitumikie kwa ufanisi ili wafike mbali kama nyota wa mataifa mengine ni tatizo. Pia, alidai tabia ya wadau kuwaingilia kazi makocha na kuwakatisha tamaa wachezaji ni tatizo jingine, sawa na kukosekana kwa wadhamini katika soka la vijana. Alisema angekutana na Rais, licha ya kumuomba aboreshe miundo mbinu na huduma za jamii, angemsihi pia atumie nafasi yake kushawishi wawekezaji na wafadhili kuangalia soka la vijana na timu nyingine ndogondogo. Ila yeye angelikuwa ni Rais, angeboresha huduma za jamii hasa elimu na kuwekeza katika michezo akidai ni njia nzuri ya kusaidia ajira kwa wengi. Kuhusu Stars, alisema timu hiyo inashindwa kufanya vema kutokana na tabia ya u-Simba na u-Yanga inayoendekezwa na wadau wakiwemo hata wachezaji, pia kuingiliwa kazi kwa makocha wa timu hiyo. "Tunaweza kufuzu fainali za Afrika na Dunia, kama wadau wataacha u-simba na u-yanga unaowaathiri hata wachezaji, pia makocha waachiwe wafanye kazi na timu ziandaliwe vema," alisema. Shabiki huyo wa Manchester United anayechizishwa na nguo za rangi yoyote, alisema anaamini kila mmoja akitimiza wajibu wake katika klabu au timu ya taifa, Tanzania zitaweza kutamba kimataifa. Ramadhani Yahya Singano, alizaliwa Desemba 31, 1992 akiwa ni mtoto wa mwisho wa familia ya watoto sita wa Yahya Singano mwenyeji wa Tanga akitanguliwa na kaka wanne na dada mmoja. Shule ya Msingi alisoma Mgulani kati ya mwaka 2000-2006 kabla ya kusoma kama yatima katika Shule ya Sekondari Al Farouk alipozidi kung'ara katika soka baada ya awali kuanza kucheza akiwa darasa la nne. Chandimu alilichezea timu ya G Spar Kavela, kabla ya kutua Ubatani akicheza nao michuano ya mchangani kisha kusajiliwa Bombom na baade Simba B. Kwa upande wa timu za taifa, alianza kuchezea timu za vijana U17 na U20 tangu 2010 kabla ya wiki iliyopita kuitwa Taifa Staras na kocha Kim Poulsen. --------------------

Doyi Moke: Kipa wa zamani aliyejitosa kwenye biashara ya madini

TANGU alipostaafu baada ya kucheza kwa mafanikio makubwa, kipa wa zamani wa timu za Majimaji ya Songea, Simba na Yanga, Doyi Moke, amewekeza nguvu zake katika biashara za kununua na kuuza madini katika nchi za Afrika. Nyota huyo aliyeibebesha taji la ubingwa wa Ligi ya Muungano, Majimaji mwaka 1997, alisema amejikita katika shughuli hiyo kwa fedha za soka. Alisema japo soka halikumpa fedha nyingi, lakini kidogo alichopata aliweka akiba inayomfanya leo aishi maisha mazuri akifanya biashara hiyo ya madini akishirikiana na nduguze. Moke, mzaliwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, aliyeanza kucheza soka tangu Shule ya Msingi na kucheza soka la kulipwa akiwa na miaka 17 tu katika timu ya Muungano ya Bukavu, anauza madini chini ya kampuni yake. Kampuni hiyo inaitwa GFK Limited, yeye akiwa ndiye Mkurugenzi akinunua madini kama almasi na dhahabu toka Kongo na kuuza Tanzania na nchi nyingine za Afrika na kumfanya awe mtu wa kusafiri. Moke alisema kabla ya kufanya biashara hiyo alijikita katika biashara nyingine mara alipotundika daluga mwaka 2003 hata hivyo hazikumlipa kama biashara yake ya sasa. Mkali huyo aliyewahi kuwika pia na timu za Aspwara, Rayon za Rwanda na Afya Sport ya Goma, alisema ni vema wachezaji wa sasa wakawa makini na kile wanazovuna katika soka kwa ajili ya manufaa ya ya baadae. "Tulipokuwa tukicheza fedha hazikuwepo kama leo, hata hivyo baadhi yetu tulikuwa na fikra za mbali ndio maana leo tunaishi vema, kwa wanaocheza sasa ni wajibu wao kukumbuka kesho yao kwa kujiwekea akiba," alisema. ALIPOTOKA Doyi Moke alizaliwa Oktoba 4, 1967 Bukavu nchini Zaire, sasa Kongo akiwa ni mtoto wa sita kati ya 10 wa familia yao. Shule ya Msingi aliisoma College Alfajiri kisha Atenend Banda Sec kabla ya kusomea Diploma ya Lugha ya Kifaransa. Kisoka alianza kucheza tangu kinda akidakia timu za shule na kutwaa nao mataji ya mashindano ya shule nchini mwao, akimtaja kocha Gabie Mugimbi kuwa ndiye aliyekivumbua kipaji chake. Moke alikiri alimvutiwa kisoka na nyota wa zamani wa Ufaransa Michel Platin na kuitaja klabu yake ya kwanza ya kulipwa kuwa ni Muungano aliotwaa nao taji la Ligi ya Mkoa wa Bukavu mwaka 1987. Baada ya kung'ara na timu hiyo kocha wa zamani wa Yanga, Raoul Shungu alimuona na kumpeleka Rwanda kuichezea ASPWARA 1989 kabla ya kutua Rayon Sport kwa muda na kurudi Kongo kuichezea Afya ya Goma. Alitua baadae Vital'O ya Burundi na kufanya mambo makubwa akiwapiku makipa wanne aliowakuta kikosi ikiwemo mmoja, Ramadhani Ally aliyemsusia jezi alipopewa nafasi mara ya kwanza kikosini. Alisema anakumbuka kocha alimpa nafasi katika mechi dhidi ya wapinzani wao Port Louis walioifunga mabao 2-0 na kujihakikishia namba akiipa ubingwa na kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika 1992. Alisema aliachana na Vital'O mwaka 1995 aliposhuhudia mchezaji mwenzake, Kamala Jeff akipigwa risasi na waasi wa Burundi mpakani mwa nchi hiyo na Kongo na kuamua kuachana na soka ili aende Afrika Kusini kusaka maisha. "Hata hivyo nilipofika Tanzania nikielekea 'Bondeni', nilikutana Mackenzie Ramadhani aliyenishawishi kuendelea na soka na kunikutanisha na kocha Nzoysaba Tauzany, aliyenisajili kuichezea timu yake ya Majimaji," alisema. Alisema hakuamini alipopokelewa kama 'Mfalme' mjini Songea na viongozi wa mkoa akiwemo RC, ambaye kwa sasa ni Spika wa Bunge, Anne Makinda akitaja dau alilosajiliwa likiwa Sh 700,000. Baada ya kuipa ubingwa wa Muungano kutokana na kumaliza Ligi ya Tanzania Bara wakiwa watatu nyuma ya Yanga na Simba, mwaka 1999 alihama na kutua Simba alioichezea kwa mafanikio kabla ya kusajiliwa Yanga. Alisema aliamua kuachana na Simba baada ya 'kuzikwa' fedha zake za usajili na mmoja wa viongozi (jina kapuni) na kuhamia Yanga mwishoni mwa mwaka 2000 na kuichezea hadi mwaka 2003 alipoenda Rayon Sport na kustaafu huko. Alisema tangu alipostaafu amekuwa mshauri kwa klabu ya Yanga na wachezaji wanaocheza sasa, pia akimpiga tafu shemejie, Henry Kalekwa anayemiliki timu ya Sofapaka ya Kenya. Moke anayependa kula wali kwa kisamvu na kunywa bia ya Safari, alisema kati ya klabu zote alizochezea, Vital'O na Yanga ndizo bomba kwake. Alisema mbali na kuichezea, pia yeye ni mshabiki mkubwa wa Yanga, Arsenal na TP Mazembe, huku akidai anapenda kuogelea na kubadilishana mawazo. HUJUMA Moke aliyemtaja Mbwana Samatta anayecheza TP Mazembe kama 'nembo' ya Tanzania katika soka la kulipwa kwa kipaji kikubwa alichonacho, alisema ndani ya soka amekumbana na mambo mengi. Alitaja mojawapo ni tuhuma alizodai kubambikiwa klabu ya Simba akidaiwa kuihujumu timu hiyo dhidi ya Yanga katika mechi iliyochezwa mwaka 2000 ambapo Yanga walishinda 2-0 kwa mabao ya 'Bwana Harusi' Idd Moshi. "Jambo hilo linaniuma hadi sasa na ndilo lililonifanya niichukie Simba kwa vile uongozi uliamua kunipakazia baada ya kuumbua kwa wanahabari juu ya kunizika fedha zangu za usajili," alisema. Juu ya mechi ngumu, Moke, alisema ni ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2001 akiichezea Yanga na Highlander ya Zimbabwe lililochezwa Harare ambapo Yanga ilishakata tamaa baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 nyumbani. "Naikumbuka kwa namna nilivyowaapia wanayanga waliokata tamaa na kutishwa na kauli ya kocha wa Highlander aliyetutaka tusisumbuke kuwafuata kwao kwa maana tulikuwa tunajisumbua tu," alisema. Alisema hata hivyo aliwapa moyo wenzake na kwenda kufanya vitu adiumu uwanjani na kuisaidia Yanga kushinda mabao 2-0 na kusonga mbele. Moke aliyemhofia Mohammed Husseni 'Mmachinga', alisema soka la Bongo, litasonga mbele iwapo nyota wa zamani watapewa nafasi za kuongoza klabu na FA badala ya 'wavamizi' wanaotambia elimu zao kubwa. Alisema wengi wa viongozi waliojipenyeza kwenye soka wanafanya hivyo kwa kusaka masilahi ikiwemo umaarufu wa kugombea nafasi za kisiasa, huku wakiliacha soka likiporomoka. "Ni kweli elimu ni kitu cha muhimu, ila wachezaji wa zamani wana umuhimu katika kuinua soka la Tanzania, watumiwe kama wenzetu wanavyowatumia wachezaji wao," alisema. Moke anayesikitishwa na kifo cha baba yake kilichotokea akiwa na miaka 13 tu, ameoa na ana watoto wawili, pia aliwashukuru mama yake mzazi kwa jinsi alivyomlea na kumuongoza hadi kufika alipo, sambamba na Rashid Haradee na marehemu Tauzany. Aliwaasa wachezaji kujituma na kutambua soka ni ajira lao, sambamba na kuzipigania klabu na timu za taifa pale wanapozichezea ili kuzisaidia na kujitangaza vema kimataifa. --------------------

Stanley Msungu: 'Seneta' anayemzimia Ramsey Nouah

INGAWA filamu ya 'Second Wife', aliyoigiza na 'Ray' ndio inayoonekana kama iliyomtambulisha kwa mashabiki, ukweli ni kwamba msanii Stanley Msungu, alishaanza kuonyesha makeke yake kitambo kirefu katika fani hiyo ya uigizaji. Msanii huyo anayefahamika kisanii kama 'Seneta Msungu', tangu akiwa shuleni alikuwa mahiri katika fani hiyo sambamba na uchezaji wa ngoma na uimbaji na alishauza sura katika michezo kadhaa ya runinga kupitia kituo cvha ITV akiwa na kundi la Amka Sanaa. Miongoni mwa michezo hiyo iliyodhihirisha kipaji cha msanii huyo ambaye pia ni mahiri katika muziki akiwa ameshafyatua nyimbo tatu mpaka sasa ili kutoa albamu kamili ni pamoja na 'Lulu', 'Safina' na 'Dunia'. Mwenyewe alisema michezo hiyo ilimpa uzoefu wa kutosha katika uigizaji na haikuwa ajabu kwake kuamua kujiengua katika kundi hilo na kutumbukia kwenye uigizaji za filamu kazi yake ya awali kabisa ikiwa ni Last Minutes iliyotoka miaka minne iliyopita. "Baada ya kujiona nimeiva na hali ilivyokuwa katika kundi letu, niliamua kujiengua na kujitosa kwenye filamu na kazi ya kwanza kucheza ni Last Minutes kabla ya kufungukiwa neema kwa kucheza filamu zinazokaribia 30 kwa sasa," alisema. Msungu, aliyetumbukia kwenye uigizaji kutokana na kuvutiwa na Ramsey Noauh wa Nigeria, alisema baada ya Last Minutes, alicheza filamu za Peace of Mind, Devorce, Devil's Kingdom, Moses, Ndoa Yangu, I Hate My Birthday, The Shell, Shortcut na sasa akitamba na Rude, moja ya kazi binafsi za mwanadada Jenifer Kyaka 'Odama'. Mkali huyo, aliyewahi kung'ara katika soka akiichezea timu yake ya shule na zile mtaani, alisema kati ya kazi zote alizocheza, filamu za Moses, Devil's Kingdom aliyoigiza na marehemu Steven Kanumba na Ramsey Nouah, Rude na Second Wife ndizo kali kwake. Alisema wakati alipoitwa kwenda kucheza filamu ya Devil's Kingdom alikaribia kuzimia kutokana na kushindwa kuamini kama angeigiza na Ramsey Nouah anayemhusudu mno. "Sio siri Kanumba ni kama alinifanyia 'surprise' kwa kunipa taarifa ya ghafla kwenda kuigiza na hata nilipofika na kuonana uso kwa uso na Ramsey sikuamini. Kwa kweli namzimia mno huyu jamaa na anaweza kazi," alisema. KIFO Msungu, aliyezaliwa mwaka 1979 wilayani Lushoto, mkoani Tanga akiwa mtoto wa kwanza kati ya sita wa familia yao, alisema wakati tukio la kukutana na Ramsey likiwa ni furaha kwake, kwa upande wa huzuni yapo mambo makuu mawili. Moja alisema kifo cha wazazi wake, na kunusurika kwake kuuwawa kwa risasi katika tukio la uhalifu lililowahi kutokea eneo la Kigamboni. Alisimulia, Msungu alisema alishawishiwa na rafiki zake aliokuwa akiwaonea wivu kwa namna walivyokuwa 'mambo safi' na kumueleza kama anaweza aungane nao kusaka fedha bila kujua kama walikuwa wezi. "Siku moja wananiambia niambatane nao kwenda kuvuna fedha na kuibukia TIPPER ambako kabla sijajua kilichoendelea tulijikuta tukivamiwa na kuwekwa chini ya ulinzi na askari wenye silaha. Kwa kweli nilitahayari mno," alisema. Alisema askari aliyemwelekezea silaha, alimwambia akisogea hatua moja tu, angemlipua risasi, lakini kwa ujasiri na kukata kwake tamaa, alimwambia askari yule kama ni risasi basi ampige ya kichwa ili afe mara moja. "Nilimweleza mie sikuwa mhalifu ila niliwafuata wenzangu bila kujua kama ni wezi, hivyo ni bora aniue kwa kunitwanga risasi ya kichwa badala ya kwingine nikihofia kuwapa tabu wadogo zangu niliokuwa nawatunza," alisema. Alisema aliyatamka hayo huku akitembea kuelekea baharini akiamini askari yile angemuua, cha ajabu alikuja kuzinduka keshoye akiwa majini alfajiri bila jeraha lolote ilihali mwanzoni aliamini alikuwa amekufa. Alidai tangu tukio hilo, alishika adabu na kuwaepuka rafiki zake hao na kuamua kuhangaika kwa kutumia vipaji vyake vya uigizaji na muziki. Msungu anayependa kula ugali kwa bamia au wali kwa njegere na kunywa juisi, alisema japo hajanufaika sana na sanaa, lakini anashukuru fani hiyo imemsaidia kwa mengi kimaisha. "Sina cha kujivunia, ila nashukuru sanaa imenisaidia kwa mengi na jinsi fani inavyozidi kukua naamini nitafika mbali kimaisha, na kutimiza ndoto za kuwa mtayarishaji na kumiliki kampuni binafsi ya filamu," alisema. MUZIKI Msungu, anayezishabikia timu za Yanga, Barcelona na Liverpool, akiwazimikia nyota wa timu hizo, Haruna Niyonzima, Lionel Messi na Luis Suarez, alisema baada ya kutamba kwenye filamu sasa amehamishia makali kwenye muziki. Alisema mpaka sasa amepakua nyimbo tatu, ya kwanza ikiendelea kutesa kwenye runinga unaoitwa 'Unanitesa' alioimba na Milan wa Bana Marquiz, 'Nalia' na mapema wiki hii alirekodi kibao kiitwacho 'Mikosi'. "Lengo langu kabla ya mwisho wa mwaka huu niwe nimeshatoa albamu kamili itakayokuwa na nyimbo nane za miondoko mchanganyiko ya Zouk na Kwaito," alisema. Alidokeza atakuwa akisambaza video za nyimbo hizo tu kabla ya kutoa 'audio' baadae ili kuepuka 'kuchakachuliwa' na baadhi ya wajanja wanaiba kazi za wasanii. Msungu anayewakubali waigizaji kama Sajuki, marehemu Kanumba, Ray, Gabo, Odama, Riyama Ally na Jackline Wolper, alisema ili wasanii wa Tanzania wafike mbali ni lazima wapendane, kushirikiana na kuwa wa moja. "Sio siri wasanii wengi nchini hatupendani na tunaendekeza majungu na unafiki vitu ambavyo sio vizuri kwa maendeleo ya sanaa zetu," alisema. Alisema, pia ni vema wasanii hasa watayarishaji na waigizaji wa filamu kuwa wabunifu kwa kutunga visa vinavyorandana na mazingira ya Tanzania. "Tubuni kazi zinazoendana na uhalisi wa maisha wa watanzania, pia serikali itusaidie na kuturuhusu kutumia maeneo yatakayoitangaza nchi," alisema. Alisema wasanii wanapotaka kuigiza katika maeneo yatakayotoa uhalisia wa simulizi la kazi zao, hupata usumbufu na kuchangia kazi nyingi kulipuliwa na kutokuwa na uhalisia wa mambo. Msungu aliyepania kuja kuwasaidia vijana wenye vipaji, alisema kuna haja pia ya serikali kusaidia kukomesha wizi wanaofanyiwa wasanii katika kazi zao, sambamba na kutazama sanaa kama eneo la kupatia pato la taifa. Mkali huyo anayechizishwa na nguo za rangi ya kahawia (brown), hajaoa ila ana watoto wawili ambao mmoja anasoma mjini Morogoro na mwingine Kigamboni anapoishi yeye. Mwisho

Bango la TFF kuhusu mapinduzi ya wazee wa Yanga

TAARIFA YA TFF KUHUSU MAPINDUZI YALIYOFANYIKA KATIKA KLABU YA YANGA SIKU YA JUMAPILI

Malawi njiani kuja kuivaa Stars

TIMU ya soka ya taifa ya Malawi inatarajia kuwasili nchini keshokutwa Alhamisi kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya wenyeji wao Taifa Stars itakayofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Angetile Osiah, alisema jana jijini kuwa kikosi hicho cha Malawi kinatarajia kuja na msafara wa watu 27 na maandalizi ya mechi hiyo yako kwenye hatua za mwisho. Osiah alisema kuwa wanaamini mechi hiyo ya Jumamosi itakuwa ni kipimo sahihi kwa wachezaji wa Taifa Stars ambao wanakabiliwa na mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia hatua ya makundi dhidi ya Ivory Coast huko jijini Abdijan. Aliongeza kuwa wachezaji wa Taifa Stars walioko kambini wanaendelea na mazoezi chini ya kocha wao mpya, Kim Poulsen, na wote wanajua umuhimu wa mchezo huo wa kirafiki. "Tunafahamu Stars inakabiliwa na mechi ya ushindani, Malawi pia ni kipimo kizuri kwao, wenzetu wako juu katika viwango vya FIFA, ni mechi itakayotusaidia," aliongeza Osiah. Hata hivyo, wachezaji watatu kati ya 25 walioutwa Stars kwa sasa wanakosa kushiriki katika programu ya mazoezi inayoendelea ya kocha Kim Piulsen kutokana na kutokuwepo nchini. Wachezaji ambao hawako kambini ni pamoja na Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, ambao watatua nchini Jumatatu Mei 27 wakitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanakoichezea TP Mazembe huku mwingine akiwa ni Haruna Moshi 'Boban' ambaye alikwenda Kinshasa kumzika kiungo wa Simba, marehemu, Patrick Mafisango, aliyezikwa juzi. Katika mechi ya kwanza ya kuwania tiketi ya kucheza fainali hizo za Dunia zitakazofanyika Brazil mwaka 2014, Taifa Stars iliyokuwa chini ya kocha aliyemaliza mkataba wake, Jan Poulsen, ilitoka sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Mechi hiyo ya Jumamosi ndio utakuwa mchezo wa kwanza kwa Kim kuiongoza Taifa Stars huku akiwa na matokeo mazuri na timu ya vijana ya umri chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes. Chanzo:NIPASHE

Sita Simba hatarini kupigwa panga

HATMA ya wachezaji sita wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba ya jijini Dar es Salaam, iko shakani baada ya mikataba ya kuichezea klabu hiyo kumalizika huku kikao cha Kamati ya Usajili kilichofanyika juzi usiku kikishindwa kufikia maamuzi ya kuwapa mikataba mipya. Nyota hao ambao kanuni zinawaruhusu kufanya mazungumzo na klabu yoyote sasa ni pamoja na Ally Mustapha 'Barthez', Uhuru Suleiman, Juma Jabu, Juma Nyosso, Derick Walulya na Gervais Kago, ambaye ni kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati. Uhuru alithibisha kuwa hana mkataba na Simba hivi sasa na yoyote anayemuhitaji milango iko wazi kumfuata. "Ila Simba ni zaidi, wamenisaidia sana (wakati alipovunjika mguu) siwezi kuwasahau," alisema kiungo huyo. Hata hivyo, wachezaji Mganda Walulya na Kago tayari wameshatupiwa virago na msimu ujao hawatavaa jezi tena za klabu hiyo, habari hizo zilisema. "Kago si mbaya ila ameshindwa kuendana na mfumo unaotumika sasa katika timu yetu ila bado timu yake ya taifa (Jamhuri ya Afrika ya Kati) inamuhitaji, Walulya amekuwa mzito na anashindwa kumudu kasi ya washambuliaji anaowakaba," alisema mmoja wa viongozi wa kamati ya usajili. Kiongozi huyo alisema kuwa kamati inaendelea kufanyia kazi ushauri kutoka katika benchi la ufundi la timu hiyo ili kuziba nafasi zenye mapungufu na hatimaye kufanya vizuri kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) yanayotarajiwa kufanyika hapa nchini kuanzia mwezi ujao. Aliwataja wachezaji wapya waliosajiliwa kuwa ni mshambuliaji Abdallah Juma kutoka JKT Ruvu, kiungo mmoja wa DC Motema Pembe huku pia Simba ikipanga kwenda Uganda kumfuata Mussa Mude ambaye pia anawaniwa na Azam na Santos ya Afrika Kusini. Kamati ya Usajili ya Simba inaongozwa na mwenyekiti wake, Hanspope Zacharia, ambaye Ijumaa iliyopita alitarajia kumsainisha marehemu Patrick Mafisango, lakini mipango hiyo haikutimia kufuatia ajali iliyotokea asubuhi ya siku hiyo na kuchukua uhai wa kiungo huyo mkabaji aliyekuwa na uraia wa Rwanda. Wachezaji nyota wengine waliobaki akiwemo Juma Kaseja, Emmanuel Okwi, Mwinyi Kazimoto, Shomary Kapombe, Kevin Yondani, Haruna Moshi 'Boban', Salum Machaku, Felix Sunzu, Nassor Masoud 'Chollo', Amir Maftah na yosso kutoka Simba B waliopandishwa wote mikataba yao bado haijaisha. Chanzo;NIPASHE

TFF yawagomea wanachama wa Yanga, yadai haitambuii mapinduzi yao dhidi ya Nchunga

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema kuwa msimamo wake ni kuwa halitatambua maamuzi yoyote yanayofanywa na wanachama wake ambayo yako nje ya taratibu na maelekezo yaliyoainishwa katika katiba ya klabu hiyo. Kauli hiyo ya TFF imekuja kufuatia mkutano wa wanachama wa Yanga uliofanyika juzi Jumapili kwenye makao makuu ya klabu hiyo ambapo walitangaza kuwa wamemuondoa madarakani Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Lloyd Nchunga, kwa madai kwamba ameshindwa kuwaongoza na anavunja katiba yao. Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kuwa wanachama wote wanatakiwa kuheshimu na kulinda katiba za klabu yao na hawana budi kufuata katiba hizo katika kufanya mabadiliko ya uongozi endapo wana sababu ya kutekeleza maamuzi hayo. Osiah alisema kuwa hakuna mwanachama (klabu au vyama vya michezo) ambaye atafanya mabadiliko bila kufuata katiba na mabadiliko hayo yakatambuliwa. "Wasivuke taratibu kuanzia chini halafu wakafikiri wakija huku kwetu tutawatambua, tunasisitiza kuwa msimamo wetu ni kutotambua uongozi ambao utateuliwa kwa muda, hiyo ni kwa mujibu wa ibara ya 12 (2) ya TFF inavyoeleza," alisema Katibu huyo. Aliwataka wanachama kuwa na subira na kuwaeleza kwamba hakuna katiba inayokataa mabadiliko ya uongozi na wafahamu kwamba hakuna matatizo au migogoro itakayotatuliwa nje ya katiba. Alieleza kuwa tayari shirikisho limeshakutana na viongozi wa Yanga na kuwaeleza kwamba wakutane na upande wa pili ili kumaliza matatizo yao kwa njia ya busara kwa lengo la kuhakikisha wanajipanga kusajili wachezaji wenye uwezo na kufanya maandalizi ya kutetea ubingwa wao wa mashindano ya Kombe la Kagame yanayotarajiwa kuanza Juni 23 hadi Julai 8 mwaka huu. Naye mwenyekiti wa Yanga, Llyod Nchunga, alikielezea kilichofanywa na wanachama wa Yanga waliokutana Jumapili si jambo sahihi na anaeleza kuwa mkutano huo ulikuwa ni kama 'sinema'. Mwenyekiti huyo aliendelea kusema kuwa wanachama wake wanatakiwa kuwa na subira endapo wanaitakia mafanikio klabu hiyo kongwe hapa Afrika Mashariki. Alisema kuwa Julai 15 sio mbali na Kamati yake ya Utendaji ilipanga siku hiyo kwa kuzingatia taratibu zilizoelezwa katika katiba yao kwa uongozi kuitisha Mkutano Mkuu. Aliongeza kuwa mkutano huo aliouitisha ni Mkutano Mkuu wa mwaka na agenda zake zimeelezwa katika Ibara ya 21 ya katiba ya Yanga. Aliwataka wanachama kuendelea na maandalizi ya kujitokeza katika mkutano huo aliouitisha huku akisema kwamba uongozi uko kwenye mchakato wa zoezi la usajili wa wachezaji na kusaka mrithi wa kocha Mserbia Kostadin Papic. Kwa mujibu wa katiba ya Yanga Ibara ya 17, Mkutano Mkuu ni ule tu ulioitishwa kwa kufuata utaratibu na ndio wenye mamlaka ya kufanya maamuzi. Na miongoni mamlaka ya mkutano huo kama yalivyoelezwa katika Ibara ya 19 kipengele cha (13) na (15), ni kubatilisha mamlaka ya mwanachama na pia kumsimamisha au kumfukuza mwanachama.

Mr Nice akamailisha albamu, atamba itamtoa

MSANII anayefurukuta kurejesha makali yake ya zamani, Lucas Mkenda 'Mr Nice' amekamilisha albamu yake mpya itakayofahamika kwa jina la 'Tabia Gani'. Albamu hiyo inatarajiwa kuingizwa sokoni muda wowote kuanzia sasa, itakuwa na nyimbo nane zilizoandaliwa chini ya mtayarishaji nyota, Lamar wa Fishcrab Records. Akizungumza na MICHARAZO, Mr Nice alisema albamu hiyo imekamilika na sasa wanafanya mipango ya kuiigiza sokoni baada ya kutambulishwa na vibao viwili vya 'Tabia Gani' na 'Nionje' alioimba na Muimbaji Bora wa Kiume nchini, Barnaba. Mr Nice alizitaja nyimbo zitakazokuwa katika albamu hiyo kuwa ni 'Tabia Gani' yenyewe, 'Nionje', 'Kupata', 'Maneno Maneno', 'Mfalme', 'Nionaje', 'Amini' na 'Ulisemaje'. "Kaka nimekamilisha ile albamu yangu mpya ya kunirejesha upya katika ulimwengu wa muziki baada ya kimya cha muda mrefu, itakuwa na nyimbo nane na kwa sasa najipanga na wasimamizi wangu ili kuiingiza sokoni," alisema. Mr Nice, alisema kwa namna albamu hiyo ilivyoandaliwa na Lamar, huenda akarejesha heshima na makali yake yaliyomfanya abatizwe jina la 'Mfalme wa TAKEU'. "Ni moja ya kazi yenye kiwango cha hali ya juu, si unajua makali ya Lamar na ukichanganya na vionjo vyangu vya 'TAKEU Reloaded', sina shaka itabamba sokoni," alisema. Mr Nice, aliyevuma miaka saba iliyopita na nyimbo matata kama 'Fagilia', 'Kikulacho', 'Friday Night', 'Bwana Shamba' na nyingine, ameibuka upya baada ya kushindwa kusimama hata alipojitosa kwenye muziki wa Injili alipotoa albamu ya 'Fungu la Kukosa'.

Viuno vya Shilole hadharani

NYOTA wa filamu aliyetumbukia kwenye fani ya muziki, Zuwena Mohammed 'Shilole' amefyatua wimbo mpya uitwao 'Viuno kwa Viuno' ameanza kuusambaza jana Jumatatu. Kisura huyo, alisema kibao hicho ambacho ni cha tatu kwake baada ya awali kuachia 'Lawama' na 'Dume Dada' vinavyokimbiza nchini kwasasa, ameshirikiana kuimba na wakali Kalidjo Kitokololo wa Fm Academia na Rich Mavoko. Shilole, alisema amepanga kuusambaza katika vituo mbalimbali vya redio leo ili uanze kuchezwa hewani, huku akijipanga kuachia nyimbo nyingine kwa ajili ya kuhitimisha albamu aliyopanga iwe na nyimbo sita au nane. "Nimekamilisha kibao kipya kiitwacho 'Viuno kwa Viuno ambao nadhani nitaanza kuusambaza redioni siku ya Jumatatu (jana ili uanze kurushwa hewani," alisema. Shilole, alisema anaamini kama ilivyokuwa kwa nyimbo zake mbili za awali, hata 'singo' hiyo itawabamba mashabiki kutokana na namna ulivyoandaliwa na kazi kubwa iliyofanywa nae na wasanii alioshirikiana nao. "Nataka kuwathibitishia mashabiki wangu, sijavamia fani, bali nauweza muziki kwa vile ni kipaji cha kuzaliwa licha ya kwamba naonekana ni mkali zaidi katika filamu," alisema. Mwanadada huyo, ambaye hujishughulisha na ujasiriamali, alisema mbali na kujipanga kutoa albamu pia anaendelea na maandalizi ya kupakua filamu zake binafsi.

Warembo Redd's Miss Bagamoyo waanza kambi Dar

WAREMBO 10 waliojitokeza kushiriki kinyang'anyiro cha kumsaka kisura wa Bagamoyo 'Redd's Miss Bagamoyo 2012', wameanza rasmi kambi ya mazoezi jijini Dar. Mkurugenzi wa Asilia Decoration inayoratibu shindano hilo, Awetu Salim, alisema warembo hao wameanza kambi katika ukumbi wa Meridian Hotel, iliyopo Kinondoni tayari kujiwinda na mchuano huo utakaofanyika Juni 15, mjini Bagamoyo, Pwani. Awetu, alisema kambi hilo ilianza Jumapili na itaendelea hadi siku ya shindano hilo litakalofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Sanaa, TaSUBA- Bagamoyo. Mratibu huyo aliwataja baadhi ya warembo hao watakaokuwa chini ya mkufunzi wao Sadah Salim kuwa ni Julieth Jeremiah, Rose Lucas, Beatrice, Rachel, Celine Wangusu na Maria. Aliongeza, kwa kushukuru kujitokeza zaidi kwa wadhamini akiitaja kampuni ya Kishen Enterprises ilijitokeza hivi karibuni kuwapiga tafu katika shindano lao. Awetu, alisema wadhamini hao wapya wameungana na wale wa awali ambao baadhi ni Twanga Pepeta', Kiu Investment, Asilia Boutique & Hair Dressing, Dr Osborn na Dk Kalenga. Juu ya burudani itakaowasindikiza warembo hao, mratibu huyo aliitaja bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' ndio watakaotumbuiza ukumbini siku ya onyesho lao.

Kumekucha Miss Kurasini 2012

WAREMBO 16 wanatarajiwa kupanda katika jukwaa la ukumbi wa Equator Grill jijini Dar es Salaam Ijumaa ya May 25 katika shindano la kumsaka Miss Kurasini 2012. Mkurugenzi wa ZUM Fashion & entertainment,inayoandaa shindano hilo Zuwena Mustapha alisema jana kwamba maandalizi kwa ajili ya shindano hilo yanaendelea vema na kwamba mwaka huu wataendeleza historia ya kutoa mrembo bomba atakayetikisa hadi ngazi ya Taifa. Alisema mpaka sasa wameshapatikana wadhamini 14 kwa ajili ya kusaidia shindano hilo ambalo linatarajiwa kuwa bomba, huku likiambatana na burudani kabambe.Taji la kitongoji hicho linashikiliwa na Top Model wa Miss Tanzania 2011, Mwajabu Juma (pichani). “Leo napenda kuwaambia kuwa hadi sasa tunajumla ya wadhamini 14 ambao wamejitokeza kudhamini shindano hilo, lakini bado milango ipo wazi kwa yeyote anaependa kutuzamini na kusaidia warembo wetu wa kurasini kupata zawadi nono na shindano kuwea zuri,”alisema Mustapha. Mustapha alisema wadhamini wakuu wa shindano hilo ni Nameems Wear wakisaidiwa na kampuni ya bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Redds, Dodoma wine, Clouds FM, Lady Pepeta, Father Kidevu Blog, Jambo Leo, Aucland Tours & Safaris, Candy Bureau de Change, Flexip, PJ Amusement, Renzo Salon na Madishisha Video Production. Aliwataja warembo waliopo kambini na kunolewa na Mwajabu Juma akisaidiwa na Malkia wa vipaji wa Miss Tanzania 2011, Rose Hurbert ni Mariam Sadic (19), Johari Juma (20),Linda Deus (20),Irene Sostheness 20),Neemadoree Sylvery(29),Edna Magige (22), Lindanancy Joseph(20), Elizabeth Mkende (19), Betty Peter (22), Jennifer Njabili (18), Lilian Joseph (20), Farida Mrope (23),Christina Moses (20), Angle Gasper (19), Flaviana Maeda(22) na Sia Kimambo (19).

Monday, May 21, 2012

Matibabu ya Sajuki nchini India shakani, kisa...!

IMEELEZWA kwamba upungufu wa damu na kudhoofika mwili kupita kiasi kumemfanya mtayarishaji na mcheza filamu mashuhuri nchini, Salum Juma Kilowoko ‘Sajuki’, kushindwa kufanyiwa upasuaji mapema nchini India alikokwenda kwa matibabu. Sajuki ambaye aliondoka nchini Jumapili iliyopita na kufikia katika Hospitali ya Saifee iliyopo Mumbai, nchini India, anakopatiwa matibabu, ameanza kuongezewa damu na kupewa vyakula ambavyo vitaweza kuupa mwili wake nguvu ili kukabiliana na zoezi la upasuaji. Kwa mujibu wa rafiki wa karibu wa Sajuki, Denis Sweya ’Dino’ ambaye alizungumza na gazeti hili muda mfupi baada ya kuwasiliana na mke wa Sajuki, Wastara, alisema hali ya msanii huyo imezidi kutengemaa kila kukicha na kuwaomba Watanzania kumuombea zaidi kwa Mungu aweze kurudi haraka katika hali yake. Sajuki anasumbuliwa na tatizo la uvimbe pembeni ya ini, ambapo wataalamu wa afya wanadai kuwa ni dalili za ugonjwa wa Hepatoma (kansa ya ini). Taarifa za awali zinaeleza kwamba Sajuki alianza kwa kupata uvimbe sehemu tofauti katika mkono wake mmoja, lakini baadaye tatizo hilo lilihamia ndani na kuanza kupata maumivu makali pembeni ya ini. Katika mahojiano yake na gazeti moja la wiki, Sajuki alikaririwa akisema madaktari walibaini ana uvimbe pembeni ya ini tatizo ambalo limekuwa likinisumbua kwa muda mrefu. Kutokana na hali hiyo, wadau mbalimbali wa filamu wakiwemo wasanii waliweza kumchangia nyota huyo kiasi cha fedha ambacho alitakiwa kukipata ili kuweza kufanyiwa matibabu nje ya Tanzania. Tanzania Daima inamtakia kila la kheri Sajuki. CHANZO:TANZANIA DAIMA

Boban azuiwa Airport akimsafirisha Mafisango, kisa...!

Michael Momburi, Kinshasa SAFARI ya mwisho ya kiungo wa Simba, Patrick Mafisango kuonekana duniani, inakamilishwa leo wakati sanduku lenye mwili wake litakapoteremshwa kaburini baadaye jioni. Mafisango alifariki alfajii ya Alhamisi iliyopita baada ya gai lake kuacha njia na kuingia mtaroni. Alikuwa akitoka Maisha Club kurudi nyumbani. Kiungo huyo aliyeacha mke na watoto watatu, aliagwa juzi kwenye Viwanja vya Klabu ya Sigara, Chang'ombe Dar es Salaam. Msafara wa uliosindikiza mwili wa Mafisango ulitua jijini hapa jana saa 6.10 mchana na kulakiwana mashabiki wengi wa kike huku askari wa usalama ndani ya Uwanja wa Ndege wahapa wakishindwa kujizuia na kumwaga machozi. Mafisango atazikwa leo kwenye makaburi ya Kinkole yaliyoko karibu na Uwanja wa Ndege wa Kinshasa. Baada ya mwili wa mchezaji huyo kutua, askari wa uhamiaji pamoja na wahudumu wa afya wanaokagua kadi za chanjo kwa wasafiri ndani ya uwanja wa ndege walianza kuuliza kwamba ni nani huyo lakini walipoelezwa bado hawakuelewa kwa vile mchezaji huyo hakuwahi kutamba na timu yoyote ya Kinshasa. Kiungo wa DC Motema Pembe, Mussa Hassan Mgosi alikuwa miongoni mwa waombolezaji. Mkuu wa msafara wa Simba, Itang'are alipotoa nakala za magazeti ya Tanzania na kuwaonyesha waliacha kazi zao na kuuzingira mwili huo huku wanawake wakishindwa kujizuia nakuanza kumwaga machozi kwa jinsi walivyoona gari lake lilivyochakaa baada ya ajali hiyo. Askari hao walitumia takribani dakika 10 kuangalia jeneza la mchezaji huyo huku wengine wakikimbia ofisi zao na kwenda kuliangalia na walisaidia kulitoa nje kuwakabidhi ndugu ingawa walizuia kabisa kupiga picha eneo la uwanja. Licha ya barabara nyingi kuwa chakavu kwenda Lemba nje ya kidogo ya jiji alikokuwa akiishi marehemu, mwili wake ulibebwa kwa gari ndogo ukiongozwa na ving’ora ingawa msafara huo uliingiliwa na 'daladala'. Msafara mzima ulikuwa na magari manane. Nyumbani kwa marehemu, kulikuwa na wanawake wengi waliokuwa wakimlilia mchezaji huyo wa Rwanda na ilitumia karibu saa nzima kuwatuliza kabla ya Mzee Kinesi kumkabidhi baba mlezi wa Mafisango, Papaa Pierre mwili wa mchezaji huyo kisha kumwelezea tukio zima la ajali na hali ilivyokuwa Tanzania. Pierre alishindwa kujizuia na kuanza kulia kwa sauti ya juu. Mwili huo wa mchezaji huyo ambaye hapa anafahamika kwa jina la Patrick Tabu Ete ambayo ndiyo majina halisi ya wazazi wake, haukukaa sana nyumbani hapo kutokana na nafasi kuwa ndogo na waliuhamishia kwenye Uwanja wa mpira wa Terrain ambao Mafisango alianzia kucheza soka ili kutoa nafasi ya mashabiki kumuaga zoezi linaloendelea hadi leo mchana. Ingawa anaonekana si maarufu sana jijini hapa kama ilivyo Lubumbashi na Rwanda, mchezaji huyo picha zake zilikuwa zimebandikwa kwenye magari mbalimbali ya vijana na hadi jana jioni hakuna mke wake aliyekuwa amewasili wala mtoto. Pierre alisema; “Msibahuu unauma sana, hakuna jinsi ninavyoweza kuelezea lakini nashukuru Wanasimbana Tanzania kwa kumpa heshima stahili mwanangu, hii ni kazi ya Mungu, tumpumzishe aende kwa amani.” Ujumbe wa Shirikisho la Soka la Rwanda, Ferwafa pamoja na familia na wageni mbalimbali mashuhuri walitarajiwa kuwasili usiku wa kuamkia leo kwa shughuli hiyo. Katika hatua nyingine, nguo za Mafisango zimeyeyuka kiaina huku Haruna Moshi ‘Boban’ akionja joto ya jiwe kwenye Uwanja wa Ndege wa hapa. Ndugu wa Mafisango waliokuwa wakiishi naye jijini Dar es Salaam walidai kupakia nguo hizo kwenye ndege na walipofika Kinshasa hazikuonekana huku wahudumu wakidai zitakuwa zimesahaulika Nairobi. “Sisi tuliziweka sehemu ya mizigo lakini tunashangaa hapa hazionekani wanasema labda zimebaki Nairobi, kule ndani ya begi lake vilikuwa vitu vyake vyote mpaka zile nguo alizopatia ajali yaani sijui itakuwaje,” ndugu mmoja alimueleza Papaa Pierre ambaye ni baba mlezi wa Mafisango. Lakini wahudumu wa ndege iliyosafirisha mizigo hiyo wameahidi kwamba leo Jumapili huenda nguo hizo zikapatikana kama kweli zilikwama Nairobi. Wakati huo huo, Haruna Moshi aliyesindikiza mwili wa marehemu, alizuiwa kwa zaidi ya nusu saa na maofisa wa uhamiaji ndani ya Uwanja wa Ndege wa Kinshasa kwa madai kuwa pasi yake ya kusafiria si halali. Maafisa hao walikuwa wakidai pasi hiyo ya dharura anayotumia Boban hairuhusu kuingia nchini Congo bali kwenye nchi za Afrika Mashariki lakini baadaye wakalainika na kumruhusu. “Huyu anarudi Dar es Salaam hawezi kuingia Congo na hii karatasi nyie ondokeni, huyu gari lile pale anarudi nalo mpeni kila kilicho chake,”alisema Afisa mmoja akimwambia mkuu wa msafara wa Simba Mzee Kinesi. Lakini baadaye maafisa hao walipoona picha za Boban kwenye magazeti ya Tanzania yaliyoripoti ajali ya Mafisango walilainika na kuamua kumruhusu Boban aingie ingawa alishachanganyikiwa na kutaka kulia huku akigoma kwenda licha ya kwamba askari hao haswa wa kiume walimsukuma mara kadhaa. “Sasa mimi niende wapi wakati ubalozi wenu umenipa visa na kuniruhusu nije kuwawakilisha wachezaji wenzangu kwenye mazishi ya ndugu yetu,”alisikika Boban akimwambia askari mmoja. Hata hivyo baadhiya askari walisikika waziwazi wakiomba kitu kidogo ili wamuachie Boban apite kwani alisahau hata karatasi yake ya chanjo jijini Dar es Salaam. Habari hii kwa hisani ya Michael Momburi kupitia ShafiiDauda.Blogspot.com

TPBO yamlilia Mafisango, waipa pole Simba

OGANAIZESHENI ya Ngumi za Kulipwa nchini, TPBO, imetuma salamu za rambirambi kwa klabu ya soka ya Simba kutokana na msiba wa kiungo wao nyota, Patrick Mutesa mafisango aliyefariki wiki iliyopita kwa ajali ya gari. Rais wa TPBO, Yasin 'Ustaadh' Abdallah, alisema wameshtushwa na kifo cha ghafla cha mchezaji huyo aliyekuwa kiigizo chema kwa wachezaji vijana nchini na kuungana na ndugu, jamaa na wadau wa klabu ya Simba kwa msiba huo. Ustaadh, alisema wadau wa ngumi hasa wanaopenda kuhudhuria michezo mbalimbali ya soka, wanajua namna gani Simba imepata pigo kwa kufiwa na kiungo huyo rais wa Rwanda ingawa mwenyeji wa DR Kongo. "TPBO tunaupa pole uongozi wa Simba na wadau wote wa klabu hiyo na soka kwa ujumla kwa kuondokewa na Patrick Mafisango, kama wadau tunaungana nao katika majonzi na kuwatakia moyo wa subira," Ustaadh alisema. Aliongeza kwa kuwataka wachezaji wenzake ambao anafahamu itawachukua muda mrefu kusahau kifo cha Mafisango kumuenzi mwenzao kwa kuiheshimu kazi yake aliyoifanya enzi za uhai wake kwa kuipa Simba mafanikio zaidi. "Najua ni vigumu wadau wa Simba kusahau msiba wa Mafisango, lakini TPBO tunaamini nnia pekee ni kumshukuru Mungu kwani kazi yake haina makosa na pia kumuenzi kwa kuipa Simba mafanikio zaidi," alisema. Patrick Mutesa Mafisango, aliyezikwa jana nyumbani kwao, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, alifariki usiku wa kuamkia Alhamisi baada ya kupata ajali ya gari akitokea Maisha Club 'kujirusha'. Kiungo huyo aliyewahi kung'ara na timu za TP Mazembe, APR, Azam kabla ya kutua Simba akiichezeapia timu ya taifa ya Rwanda 'Amavubi', amefariki akitokea kuisaidia Simba kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara 2011-2012. Mwisho

Mil. 150 kudhamini tuzo za TASWA

KAMPUNI ya Bia ya Serengeti (SBL) jana imetangaza kudhamini tuzo za Mwanamichezo Bora wa Tanzania wa mwaka 2011 kwa Sh. milioni 150. Tuzo hizo zinaandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) na mwaka huu zitatolewa Juni 14 kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee (VIP). Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa SBL, Teddy Mapunda, alisema kuwa lengo la kudhamini tuzo hizo ni kutaka kuona michezo na wanamichezo hapa nchini inakua na kujitangaza ndani na nje ya nchi. Alisema kampuni yake inaona fahari kuendelea kudhamini tuzo za TASWA ikiwa ni mwaka wa tatu mfululizo, hivyo mwaka huu wameongeza udhamini zaidi ili kuziboresha. Alisema tuzo hizo zitafanyika Juni 14 mwaka huu ukumbi wa Diamond Jubilee (VIP) Dar es Salaam na kwamba wana matumaini makubwa zitakuwa bora kuliko zilizopita. Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto aliwashukuru Serengeti na kusema udhamini huo ni ishara ya namna kampuni hiyo inavyothamini wanamichezo nchini na kwamba umeongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka Sh. milioni 80 ambazo walitoa mwaka jana. Pinto alisema kuwa milango bado iko wazi kwa kampuni nyingine kwa sababu bajeti nzima ya shughuli hiyo iliyopangwa ni Sh. milioni 370. Alisema kuwa mchakato wa kupata washindi wa tuzo hizo unasimamiwa na kamati maalumu iliyoteuliwa na TASWA na wanaamini inafanya kazi zake kwa uadilifu. Kwa miaka mitano iliyopita walioshinda Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa TASWA walikuwa ni Samson Ramadhani (2006), Martin Sulle (2007), Mary Naali (2008), ambao wote ni wanariadha, wakati 2009 na 2010 alikuwa ni mcheza netiboli Mwanaidi Hassan. Mshindi wa mwaka jana, Mwanaid, ambaye alizawadiwa gari aina ya Toyota Cresta (GX 100), ndiye mfungaji aliyeisaidia timu ya taifa ya netiboli, Taifa Queens, kumaliza ikiwa ya pili kwenye mashindano ya mchezo huo ya Afrika yaliyofanyika nchini hivi karibuni.
Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando 'Mgosi'

Ngumi nazo zikumbukwe kama ilivyo kwa soka

INGAWA soka linatajwa kama mchezo unaopendwa na wengi duniani na hata nchini Tanzania, hata hivyo mchezo wa ngumi nao haupo nyuma kwa kuwa na mashabiki wengi. Kwa hapa nchini ukiondoa miaka ya hivi karibuni ambapo soka kurejesha heshima yake, mchezo wa ngumi ndio uliokuwa ukiongoza kwa kushabikiwa na watu wengi kiasi cha vijana wengi kuota kuwa mabondia. Hii ilitokana na mafanikio makubwa waliyopata mabondia wetu hasa wa ngumi za kulipwa kama akina Rashid Matumla, Rodger Mtagwa, Joseph Marwa, Mbwana Matumla na wengineo. Kabla ya mabondia hao kutamba katika ngumi za kulipwa kuna wakali wengine waliong'ara katika ngumi za ridhaa na kuiletea Tanzania medali katika mashindano mbalimbali ya kimataifa. Iwapo nitataka kuiandika orodha ya nyota walioiletea sifa katika ngumi enzi hizo, huenda nafasi isitoshe lakini baadhi yao ni akina Titus Simba, Habib Kinyogoli, Emmanuel Mlundwa, Bakar Seleman 'Match Maker' na wengine. Hata baada ya kuondoka kwa wakali hao na kuja kizazi cha akina Matumla, bado ngumi zimekuwa zikiendelea kutamba kwa kushuhudia mabondia kama Francis Cheka , Karama Nyilawila na wengine wakiitangaza vema Tanzania. Mataji ya kimataifa waliyotwaa katika mchezo huo likiwemo la hivi karibuni ya IBF-Afrika anaoushikilia Cheka, au ubingwa wa Dunia wa WBF ulioachwa kutetewa na Nyilawila ni mifano ya mafanikio machache ya mchezo wa ngumi. Hata hivyo pamoja na mafanikio hayo, bado mchezo huo haujapewa kipaumbele kama ilivyo kwa soka ambapo licha ya kusuasua na kutokuwa na tija ya kutosha linapewa hadhi ya kipekee nchini. Mchezo huo umekuwa na viwanja vya kutosha vya kuzalisha nyota wa baadae vikiwemo vya kimataifa ambavyo vimezidi kuwatia wazimu mashabiki wake, hali ikiwa ni tofauti kwa michezo mingine hususani ngumi. Mafanikio pekee ya kujivunia katika soka ni kufika fainali za Afrika za mwaka 1980 kwa timu ya taifa na klabu za Simba kutinga fainali za CAF-1993 na kufika nusu fainali za Klabu Bingwa Afrika mwaka 1974 na kucheza hatua ya makundi kwa Simba na Yanga mwaka 1998 na 2003. Pengine kwa mafanikio makubwa iliyopata mchezo wa ngumi kimataifa nilidhani kuna haja ya kuwepo uwanja au ukumbi maalum wa kufanyikia mashindano ya michezo huo kama soka ilivyo na viwanja vyake. Kitambo kidogo watu wa ngumi walikuwa na hakika wakienda ukumbi wa Arnatoglo au Relwe Gerezani, wangesuuza mioyo yao kwa kuwaangalia mabondia wakipasha misuli na wakati mwingine wakichuana mashindanoni. Mabondia wetu kwa sasa wamekuwa wakitangatanga na kutumia ama 'gym' zao zilizopo uchochoroni katika mazingira mabaya kukuzia vipaji vyao wakati wenzao wa soka wanatanua katika viwanja kadhaa vilivyopo nchini. Hata wanapokuwa na mipambano yao, utasikia kama sio Diamond Jubilee, ambao hata hivyo kwa sasa hautumiwi sana, basi ni PTA, Friends Corner au DDC Keko. Yaani hakuna ukumbi maalum wa kufanyikia mapambano ya ngumi kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia katika mataifa mengine kama Marekani yenye kumbi za uhakika kama Madson Square Garden au MGM Grand. Ni vigumu kujilinganisha na Marekani, lakini nadhani kama kungekuwa na kumbi maalum au eneo maalum la kukutanishia mabondia ingesaidia kuwapoa uhakika mabondia na mapromota wao katika kukuza mchezo huo. Inawezekana Tanzania kuwa na kumbi za kisasa na zenye ubora zitakazotoa ushawishi kwa mapromota hata wa nje kuleta mapambano makubwa kucheza nchini kama uwanja wa Taifa ulivyozileta timu kubwa za soka nchini. Nani aliyekuwa akiota siku moja Brazil ingeweza kuja kucheza Tanzania? Lakini kwa kuwa na uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000 tuliwaona akina Robinho, Kaka na wengine kisha tukawaona akina Yaya Toure, Solomon Kalou, Didier Drogba na wengine wa Ivory Coast. Hivyo ni changamoto kwa serikali, vyama vinavyosimamia ngumi na wadau wote wa ngumi kupigania jambo hili la kuwepo kwa uwekezaji mzuri katika ngumi ili kuufanya mchezo huo uwe na hadhi kulingana na thamani yake. Nadhani kujengwa kwa kumbi au eneo litakalokuwa kama kitovu cha kuwakutanishia mabondia na la kufanyikia mapambano ya ngumi sio tu itawasaidia mabondia kufika mbali, lakini itawavuta watu wa nje kuja nchini. Kuja kwa kutasaidia kuitangaza Tanzania kimataifa katika sekta ya Utalii na hivyo kuliingizia taifa pato kubwa, kama ambavyo Brazil, New Zealand au Vancouver Whitecap ya Canada walivyokuja nchini kisoka. Mwisho

Twiga Stars yakiona cha moto kwa Banyana Banyana

WIKI moja tangu iangushiwe kipigo cha mabao 4-1 na madada wenzao wa Zimbabwe, kwa mara nyingine tena timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Tanzania, Twiga Stars jana ilikumbana na kipigo kingine kizito toka kwa 'wababe' wa Afrika Kusini, Banyana Banyana. Katika mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa, Twiga Stars ilicharazwa mabao 5-2 na wageni wao katika mechi zao za kujiandaa na michezo yao ya kufuzu fainali za Afrika. Twiga itacheza mechi yake ya kufuzu dhidi ya Ethiopia mjini Addis Ababa Mei 26, wakati Banyana itakuwa ugenini Zambia siku hiyo hiyo. Katika mechi ya jana iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Banyana walipata goli la kwanza katika dakika ya 23 kupitia kwa Patricia Modise aliyeuwahi mpira uliorudishwa nyuma na beki wa Twiga, Mwanaidi Tamba, na kufanya matokeo ya 1-0 hadi wakati wa mapumziko. Banyana Banyana iliongeza bao la pili kupitia tena kwa Modise tena aliyepachika wavuni kwa kichwa akiunganisha krosi ya Gabisile Hlumbane, Twiga ilizinduka na kujipatia bao la kwanza kupitia kwa Fatuma Bushiri aliifungia Twiga Stars kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa na mwamuzi wa FIFA, Judith Gamba, baada ya Mwanahamis Omary 'Gaucho' kuangushwa na Janine van Wyk katika dakika ya 63. Wageni walipata goli la tatu katika dakika ya 73 kupitia kwa Sanah Mollo aliyeingia kuchukua nafasi ya Andiswe Mgloyi baada ya mabeki wa Twiga kujichanganya. Asha Rashid 'Mwalala' alifanya matokeo yawe 3-2 katika dakika ya 77 kufuatia pasi ya Fatuma Mustapha, lakini dakika mbili baadaye Banyana walipata goli la nne lililofungwa na Sanah tena. Na dakika nne kabla ya mechi kumalizika beki Janine van Wyk aliwafungia Banyana goli la tano kwa mpira wa 'fri-kiki' iliyokwenda moja kwa moja wavuni. Mara ya mwisho wakati timu hizo zilipokutana katika fainali za Mataifa ya Afrika nchini Afrika Kusuni, Twiga ililala 2-1. Kikosi cha Twiga Stars jana kilikuwa: Fatuma Omary, Fatuma Khatibu, Mwajuma Abdallah, Fatuma Bushiri, Mwanaidi Tamba, Everine Sekikobo, Esther Chabruma 'Lunyamila', Mwanahamisi Omary 'Gaucho', Asha Rashid 'Mwalala', Mwapewa Mtumwa na Fatuma Mustapha. Banyana: Roxanne Barker, Nodhano Vilakazi, Amanda Sister, Janine van Wyk, Zamandosi Cele, Amanda Dlamini, Mary Ntsweg, Patricia Modise, Gabisile Hlumbane, Rafilde Jane, Andiswe Mgloyi.

Licha ya bahati, lakini tulistahili taji-Cole

BEKI wa Chelsea, Ashley Cole amesisitiza kwamba uwezo wao, sio bahati, ndio kilichowapa ubingwa wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya katika fainali usiku wa kuamkia jana. Cole, ambaye alifunga moja ya penalti za wakati wa kupigiana "matuta", alikiri kwamba Chelsea ilikuwa na bahati ilikuwa kwao katika fainali wakati Bayern Munich wakipotena zafasi nyingi nzuri za kushinda lakini mwisho wa mechi wao walikuwa washindi waliostahili. Aliiambia Sky Sports 1: "Maneno yamenikauka. Tulipaswa kuwa tumeshafungwa kutokana na nafasi nyingi walizitengeneza. "Tulikuwa na bahati, unahitaji bahati katika michuano hii kama unataka kuwa bingwa. Leo tulikuwa na bahati lakini pia tulistahili kushinda leo." Alipoulizwa hadhani kwamba bahati yao ilikuwa inaelekea kupotea baada ya Bayern kupata penalti dakika tano katika muda wa dakika 30 za nyongeza, mchezaji huyo wa kimataifa wa England aliongeza: "Hapana, kutokana na wachezaji tulionao tulifikiria, 'ok ni penalti lakini bado muda upo', na pale Petr alipookoa kiufundi yale ndiyo yunayoamini daima." Ubingwa ulimaanisha kwamba mara hii bahati ilikuwa upande wa Cole katika fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa baada ya kupoteza mechi za fainali wakati akiichezea Arsenal mwaka 2006 na Chelsea 2008. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31, ambaye wakati akihamia katika klabu hiyo inayomilikiwa na tajiri alituhumiwa kuwa alifuata pesa na akapachikwa jina la "Cash-ley" Cole alisema: "Hii ndiyo sababu niko hapa." (Mail)

Nchunga 'angolewa' Yanga kwa mabavu

MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Llyod Nchunga 'ameondolewa' madarakani na kundi la wanachama zaidi ya 700 waliokutana jana kwenye mkutano wao wa dharura. Wanachama hao waliokutana kwenye makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, walikubaliana kumuondoa madarakani Nchunga, kwa madai ya kushindwa kuiongoza Yanga na pia kukiuka katiba kwa kutoitisha Mkutano Mkuu tangu alipochaguliwa mnamo mwaka juzi. Hata hivyo, maamuzi hayo ili yaweze kupata baraka kisheria yatapelewa katika ofisi za Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo wa Manispaa ya Ilala ambapo Yanga ndipo imesajiliwa. Akitangaza maamuzi ya wanachama hao baada ya kuwauliza na wao kuitikia kwa sauti ya juu kwamba ha
Picha za matukio za mkutano wa wanachama wa Yanga waliokutana jana klabuni kwao na kumuengua madarakani Nchunga. wamtaki Nchunga, Katibu wa Baraza la Wazee, Ibrahim Akilimali, alisema kuwa wamefikia maamuzi hayo kutokana na uongozi waliouchagua kushindwa kuiongoza Yanga na kuruhusu 'ufisadi' kufanyika ndani ya klabu yao. Akilimali alisema kuwa wamekosa imani na Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo na baada ya kuona wameshindwa uongozi waliowapa na waliwataka waondoke ili kuepusha aibu ambayo hivi sasa inawakabili hasa kufuatia kupoteza ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na kufungwa magoli 5-0 na watani wao Simba. "Tulimshauri atupe timu ili tuweze kuiandaa vyema kumvaa mtani, alikubali, lakini baadaye akatuita sisi ni wahuni na majina mengi yasiyofaa, sasa kwa hili tunasema kuanzia sasa Nchunga na wenzake si viongozi tena wa Yanga," alisema Akilimali na kushangiliwa na wanachama ambao walikutana kwenye uwanja wao wa Kaunda huku kukiwa na amani. Alisema kuwa makundi yaliyoko ndani ya klabu hiyo ndiyo yamewafikisha walipo na wamekubaliana waungane na kumaliza tofauti zao ili Yanga iwe moja. Mkutano huo kwa kauli moja pia ulipitisha jina la Rais wao zamani, Abbas Tarimba, kuwa mshauri wa Kamati ya Usajili ambayo itaanza kazi leo na kuhakikisha wanasajili wachezaji wenye uwezo na hatimaye kutetea ubingwa wao wa Kombe la Kagame. Wanachama hao waliazimia kutowaruhusu viongozi waliobaki kwenye Kamati ya Utendaji kuingia kwenye jengo hilo kwa sababu hawana imani nao tena. Pia Akilimali alisema kuwa hivi sasa Yanga inapaswa kuitisha mkutano wa uchaguzi kufuatia wajumbe wa Kamati ya Utendaji kujiuzulu na kubakia watano. Yusuph Mzimba, alisimama kwenye mkutano huo na kuwataka wanachama wa Yanga wabadilike na kutorudia makosa waliyoyafanya kwenye uchaguzi uliopita kwa kumchagua kiongozi huyo. Mzimba alisema kwamba wasikubali tena kutumika na kuchaguliwa viongozi wasiojua maana ya utawala. "Yanga ibadilike, sio kama ilivyokuwa huko nyuma," alisema Mzimba na kupigiwa makofi. Alisema Nchunga ameshindwa kusoma alama za nyakati kwa kufahamu kwamba sasa wanachama hawamtaki na hivyo alitakiwa mapema kujiuzulu hatimaye kulinda heshima yake. Wanachama kuanzia 500 wanaweza kuomba mkutano mkuu na kutoa maamuzi lakini ikiwa chini ya mkutano ulioitishwa na uongozi. Hata hivyo, Nchunga alikaririwa jana akisema kwamba mkutano huo ni batili kwa sababu haukuwa mkutano wa wanachama kama wazee walivyoubadili 'kihuni', bali ulipaswa kuwa ni baina ya uongozi na wazee wa klabu. Hadi kufikia jana Kamati ya Utendaji ya Yanga imebakia na viongozi wanne huku nane wakiwa wameshajiuzulu hivyo waliobaki hawawezi kukutana na kutoa maamuzi yoyote. Wajumbe ambao kuanzia juzi waliwasilisha barua za kujiuzulu ni pamoja na Paschal Kihanga, Mzee Yusuph na Mohammed Bhinda, ambaye alipokelewa kwa shangwe kwenye mkutano huo wa wanachama na kuahidi leo ataweka wazi sababu zilizoepelekea yeye kufikia maamuzi hayo. Mzee Yusuph katika barua yake amesema kuwa amefikia maamuzi hayo baada ya kuona wameshindwa kusimamia na kuiendesha klabu hiyo katika misingi ya weledi, uwazi na uwajibikaji. Wajumbe wengine waliojiuzulu ni Ally Mayai, Sarah Ramadhani, Seif Ahmed 'Magari', Abdallah Binkleb na Davis Mosha, wakati Theonest Rutashoborwa alifariki na kuipunguzia nguvu kambi ya uongozi.

Sh50m awaits Epiq Bongo Star Search 2012

The winner of this year Epiq Bongo Star Search (EBSS) 2012 will pocket Shs 50 million, Zantel Vice President-Commercial, Ahmed Mokhles announced on Friday. Speaking during the launching ceremony held at the Serena Hotel, Mokhles said that they have decided to increase the winner prizes from Shs 40 million of last year aiming to make the search competitive and reward the winners. Mokhles said that they are proud to be associated with a successful Tanzanian talent competition focusing on discovering and promoting new musical talent among the youth. He said that through Epiq Nation related products aimed at the youth, they believe this year’s contest will be very energetic, full of color and pomp and many surprises. He explained that Zantel has incorporated a fashion aspect to this year’s competition whereas local and young designers will be given an opportunity to dress the contestants and will be assessed by professional fashion designers. “We all now BSS has changed lives of many young people and would like to see this continue under our firm stewardship and are creating additional segments to the show such as fashion to give opportunities to more youths and benefit from this one o a kind partnership,” added Mokhles. Benchmark Production Managing Director, Rita Paulsen elaborate her happiness during the launch “This is very unique day in Tanzania Music industry as we officially launch epiq bongo star search 2012 with avibrant new sponsor who has come up with a fresh look towards bongo star search.” Epiq Bongo Star search will continue with its usual format of having auditions from all major towns around the country an thisi year it will be extended to eight regional that are Zanzibar, Lindi, Mbeya, Mwanza, Arusha, Tanga, Dodoma and Dar es Salaam.

Saturday, May 19, 2012

Doyi Moke awataka Yanga watulie

KIPA nyota wa zamani wa klabu za Majimaji-Songea, Simba na Yanga, Doyi Moke, amewasihi wanachama wa timu ya Yanga kumaliza matatizo yao kwa kukaa mezani na kuzungumza. Aidha, kipa huyo raia wa JK Congo na aliyewahi kuzidakia pia timu za Rayon Sport ya Rwanda na Vital'O ya Burundi, alisema wanayanga wanapaswa kukumbuka kuwa mbele yao kuna kibarua cha kutetea taji la Kombe la Kagame la klabu bingwa za Afrika Mashariki na Kati hivyo watulizane mapema. Akizungumza kwenye mahojiano maalum, mkali huyo ambaye kwa sasa ni mfanya biashara madini alisema Yanga watajuta mbeleni wasipokaa mezani. "Nadhani hali inayoendelea Yanga haileti ishara njema, pande zinazotofautiana zikae chini na kuzungumza, kuendelea kulumbana bila kupata muafaka ni kuiweka pabaya timu yao wakati wanakabiliwa na michuano ya Kombe la Kagame linaloanza Juni," alisema. Alisema hadhani kama kuendelea kujadili kipigo cha mabao 5-0 walichopewa na watani zao Simba au kupokonywa taji la ligi kuu itaisaidia klabu hiyo wakati matokeo hayo hayawezi kubadilika. Baadhi ya wanachama wa Yanga wamekuwa wakishinikiza mwenyekiti Lloyd Nchunga ajiuzulu mara moja, na katika kuhakikisha hilo wameitisha mkutano mkuu kesho klabuni huku mwenyekiti akiwa ametaja Julai 15 kuwa siku ya mkutano mkuu rasmi wa mwaka.
Doye Moke enzi akicheza soka nchini Tanzania

Mashujaa, Mashauzi kung'arisha Miss Tabata

BENDI zinazotamba nchini kwa sasa Mashujaa na Mashauzi Classic zitatumbuiza kwenye kinyang'anyiro cha kumtafuta mrembo wa Tabata kitakachofanyika Juni Mosi katika ukumbi wa Da West Park, Tabata. Mratibu wa shindano hilo, Godfrey Kalinga alisema wameamua kuweka burudani yenye ladha tofauti ili kukidhi kiu ya watu mbalimbali watakaohudhuria shindano hilo. Kalinga alisema siku hiyo pia itatumika kusherehekea miaka 10 tangu kuasisiwa kwa shindano la Miss Tabata. "Shindano la mwaka huu litakuwa ni la aina yake kwa sababu utakuwa ni mwaka wetu wa 10 tangua kuanza kuandaa Miss Tabata... ndio maana tunaleta burudani nyingi," alisema mratibu huyo wa Bob Entertainment na Keen Arts. Alisema warembo waliyowahi kushinda mataji mbalimbali ya shindano hilo, pia wamealikwa kusherehekea miaka 10 ya Miss Tabata. Shindano hili limedhaminiwa na Dodoma Wine, Redds, Integrated Communications, Fredito Entertainment, Multichoice Tanzania, Screen Masters, Kitwe General Traders, Step In Electronics, Brake Point, Atriums Hotel na Lady Pepeta. Warembo 10 wa kwanza watafuzu kushiriki Miss Ilala na baadaye Miss Tanzania. Mrembo anayeshikilia taji la Tabata kwa sasa ni Faiza Ally. Warembo wa Tabata wamekuwa wakifanya vizuri katika mashindano ya Miss Tanzania ambapo 2010 Consolata Lukosi alishinda nafasi ya tatu kabla ya kutangazwa kuwa balozi wa kinywaji cha Redds.
Visura watakaochuana kinyang'anyiro cha Miss Tabata 2012

'Ticotico' wa Simba aanzisha klabu binafsi ya soka, kuteta leo

ALIYEWAHI kuwa Katibu wa Kamati ya Fedha ya klabu ya Simba, Onesmo Waziri 'Ticotico' ameanzisha klabu ya soka iitwayo 'Golden Bush Fc', ambayo imeshasajiliwa rasmi tayari kwa ajili ya ushiriki wa michuano mbalimbali. Akizungumza na MICHARAZO, Ticotico, mmoja wa 'membaz' wa zamani wa Friends of Simba, alisema klabu yake imesajiliwa ndani ya wilaya ya Kinondoni na itakuwa na makao makuu yake eneo la Mabibo, Dar es Salaam. Alisema mpaka sasa timu hiyo imeanza kukusanya wachezaji chini ya kocha wa muda, nyota wa zamani wa timu ya Yanga, Waziri Mahadh 'Mandieta'. Ticotico, alisema katika kuhakikisha klabu yake inajiendesha kisasa ikiwa na ufadhili wa kutosha wameitisha mkutano na wadau wa soka wilayani Kinondoni, ili kujadili na kutoa mawazo yao. Mkutano huo unatarajiwa kufanyika leo Jumamosi mchana, kwenye majengo ya ofisi ya TANLAP, Kinondoni Biafra. Ticotico aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa klabu ya Red Coast iliyotamba Ligi ya TFF-Kanda, alisema lengo la kuanzisha klabu hiyo ni kuendeleza soka nchini sambamba na kuwasaidia vijana wenye vipaji vya mchezo huo. "Katika kuendeleza soka nchini nimeamua kuanzisha klabu itakayoitwa Golden Bush, ambayo imeshasajiliwa na Jumamosi tunatarajia kufanya mkutano au tuseme kongamano la wadau wa soka kupata mawazo namna ya kuifanya iwe klabu ya kipekee Kinondoni," alisema. Mwisho

KWAHERI JEMBE MAFISANGO TUTAKUKUMBUKA DAIMA

MAISHA UPITA, LAKINI MEMA NA MAZURI YA MTU HAYASAHAULIKI. TUTAKUKUMBUKA DAIMA PATRICK MUTESA MAFISANGO KWA UHAMIRI WAKO DIMBANI. KAPUMZIKE KWA AMANI BABA!

Jezi ya Mafisango yataifishwa SIMBA, Wengi wamlilia!

KLABU ya soka ya Simba imeamua 'kuitaifisha' jezi namba 30, aliyokuwa akiitumia kiungo wao wa kimataifa kutoka Rwanda, mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Patrick Mutesa Mafisango kama njia ya kumuenzi. Uongozi wa Simba umesema kuanzia sasa hautaitumia tena jezi hiyo kama heshima ya mchezaji huyo aliyefariki usiku wa kuamkia juzi, jijini Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Simba, Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage aliyasema hayo jana wakati akiwahutubia waombolezaji waliofika kuuaga mwili wa marehemu Mafisango kwenye viwanja vya TCC-Chang’ombe, Dar es Salaam, kabla ya kupelekwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl JK Nyerere, ili kusafirishwa leo kwenda kwao Kongo kwa ajili ya mazishi yanayofanyika kesho Jumapili. Heshima, aliyopewa Mafisango inafanana ya ile ya kiungo wa zamani wa kimataifa wa Cameroon, Marc Vivien Foe na klabu yake, Manchester City ya England alipofariki Juni, 2003, ambapo jezi yake namba 23 ilitunzwa moja kwa moja. Kiungo huyo aliyekuwa ameitwa saa chache kujiunga na timu yake ya taifa ya Rwanda 'Amavubi' kwa kipindi alichoichezea Simba alijijengea jina kwa umahiri aliokuwa nao dimbani, kiasi cha kusamehewa hata alipofanya utovu wa nidhamu hivi karibuni kambi ya timu hiyo. Rage alisema msiba huu ni mkubwa kwa Simba kwa kuwa mchezaji huyo alikuwa ni muhimili mkubwa kwa timu hiyo akiwashauri wachezaji na kuwa nao karibu ndani na nje ya uwanja. “Mafisango alikuwa na mchango mkubwa kwa Simba na mara ya mwisho klabu kukumbumbwa na msiba mzito namna hii ilikuwa ni mwaka 1978 ambapo Simba ilimpoteza mchezaji wake mahiri Hussein Tidwa na ukweli ni kwamba wachezaji hawa tutawaenzi miaka yote na ndio sababu ya kutotumia tena jezi namba 30 kwa kuvaliwa na mchezaji yoyote,” alisema Rage. Rage alisema licha ya umahiri wa Mafisango Dimbani pia alikuwa mchezaji ambaye alitoa mchango mkubwa na hasa wachezaji wawapo nje ya nchi kutokana na umahiri wake wa kujua lugha mbalimbali ambapo alikuwa akiwasaidia wachezaji wenzake. “Ni pengo kubwa kwa kuwa mchezaji huyo alikuwa akijua lugha nyingi ikiwemo Kiswahili, Kingereza na Kifaransa na kuwasaidia wachezaji walipokuwa nje ya nchi tutamkubuka sana Mafisango,” aliongeza. Kutokana na machungu ya msiba huo Rage alishindwa kumaliza kusoma risala fupi ya marehemu mara baada ya kuishiwa nguvu na kumwaga machozi na kupelekea Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Godfrey Nyange ‘Kaburu’ kumsaidia kusoma risala hiyo. “Mfisango ni mchezaji ambaye alikuwa akijituma nje na ndani ya uwanja na kabla ya kutua Simba Marehemu aliwahi kucheza soka katika timu mbalimbali ikiwemo Tp Mazembe ya DRC, APR ya Rwanda , Azam na Simba za Tanzania na pia alikuwa Nahodha wa timu ya Taifa ya Rwanda ‘Amavubi’ alisema Kaburu. Wakati wa kutoa heshima za mwisho katika uwanja wa Sigara maelfu ya watu walijitokeza uwanjani hapo wakiongozwa na mchungaji Tito Kihame ambaye aliongoza ibada ya kuuga mwili wa marehemu, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenella Mukangara na viongozi mbalimbali wa serikali na viongozi kutoka klabu mbalimbali za hapa nchini. Mukangara aliwataka wachezaji wa Tanzania kujituma na kuwa na moyo kama ambao alikuwa nao Marehemu Mafisango kwa kujituma na kuwa na jitihada za zaidi nje na ndani ya uwanja kama ambavyo marehemu alivyokuwa akifanya. “Kifo chake ni pigo kubwa kwa Simba na Watanzania kwa ujumla na tunamshukuru kwa kuvuka mipaka na kuona umuhimu wa kuja na kucheza Tanzania na pia wachezaji wa Simba wasikate tamaa cha muhimu waendeleze kile ambacho alikiacha marehemu,” alisema Mukangara. “Ukweli ni kwamba katika familia ya soka hapa nchini tumepoteza mtu muhimu sana na tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa amani,” alisema Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania TFF Angetile Osiah. “Sisi Simba ni watani zetu na tunakuwa pamoja katika shida na hivyo basi mimi kama kiongozi wa Yanga nimeiwakilisha klabu nzima na tutaendelea kuwa bega kwa bega na watani zetu katika kipindi hiki kigumu ila mchezaji Mafisango alikuwa ni mchezaji hodari uwanjani hivyo basi anastaili kuigwa na wachezaji wengine,” alisema Selestine Mwesigwa katibu Mkuu wa Yanga. Nao wachezaji mbalimbali kutoka timu ya Taifa Taifa Stars walijitokeza na kubeba jeneza la mchezaji mwenzao na kuliingiza katika viwanja vya Sigara wachezaji hao Juma Kaseja, Jonh Bocco, Mwinyi Kazimoto, Shabani Nditi, Amiry Maftah, Nurdin Bakari, Agrey Moris na Juma Nyoso. Profesa Philemon Sarungi akimsaidia Rage Mara baada ya nyota hao kuufikisha mwili wa marehemu katika sehemu husika ambayo ilipangwa Kazimoto na Kaseja iliwalazimu watu wa ziada kujitokeza na kuwapa sapoti mara baada ya kushindwa kutembea na kuwapeleka katika eneo husika ambalo walikuwa wamepangiwa kukaa. Naye Msemaji wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga alisema msafara wa leo kwenda Kongo kuusafirisha mwili wa Mafisango, Haruna Moshi 'Boban' atawakilisha wachezaji wa klabu hiyo huku kwa uongozi atakuwa Mjumbe wao wa kamati ya utendaji Joseph 'Mzee Kinesi' Itang’are. Kamwaga alisema mwili huo ungeondoka asubuhi ya leo ukiambatana na mtoto wa marehemu Crespo Tabu Mutesa, mwenye umri wa miaka mitano na mchezaji wa Yanga Haruna Niyonzima ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Rwanda.