STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, June 26, 2011

Rufita yamnasa Kibugila



BENDI ya muziki wa dansi ya Rufita Connection 'Wana Shika Hapa Acha Hapa', imepata mcharaza solo mpya ikiwa ni wiki chache baada ya Seleman Shaibu Mumba kukimbilia Twanga Pepeta.
Kwa mujibu wa rais wa bendi hiyo, Chai Jaba, mpiga solo huyo ni Abdalah Kibugila ambaye amewahi kuwa bendi mbalimbali ambapo kwa mara ya mwisho alikuwa Bwagamoyo International ya Mwinjuma Muumin.
"Seleman alikuwa mpiga solo wetu lakini ameshahama, lakini tayari tumeshapata aliyeziba nafasi yake, kazi inaendelea kama kawaida kutokana na ukweli kwamba Kibugila ni mwanamuziki siku nyingi ana uzoefu wa kutosha," alisema.
Alisema Kibugila anashiriki maonyesho ya bendi hiyo huku akizifanyia mazoezi nyimbo za bendi hiyo zikiwemo za 'Mapenzi Yanaua', 'Nilinde Nikulinde', 'Anasa', 'Shida ya Mapenzi', 'Usia', 'Acha Pupa','Mkosi Gani' na 'Mazi'.
Akielezea zaidi mipango ya bendi hiyo, Chai Jaba inajiandaa kumalizia kazi ya kurekodi nyimbo zote na kisha kuanza kushuti video na kisha zitafuatia taratibu za kuzindua albamu.
"Nina uhakika yatakwenda vizuri na inawezekana tukakamilisha kazi ya kurekodi nyimbo zetu mwezi ujao kabla ya kuendelea na kazi ya kushuti video ili tujitambulishe zaidi kwa mashabiki wa muziki wa dansi," alisema.
Aidha, alisema bendi hiyo inajiandaa kuleta wanenguaji wapya wanne kutoka Congo (DR) watakaokuja kuungana na wenzao waliopo kwa sasa ili kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji wa jukwaa.

Gilla alia na Phiri kumzibia riziki Simba



MSHAMBULIAJI chipukizi wa Simba Salim Aziz Gilla aliyetangazwa kutafutiwa timu ya kucheza kwa mkopo msimu ujao amemlaumu aliyekuwa kocha mkuu wa klabu hiyo Patrick Phiri kuwa alichangia kufifisha nyota yake kisoka.
Gilla aliyenyakuliwa na Simba kwa mkataba wa miaka mitatu mwaka 2009 baada ya kung'ara kwenye michuano ya Kombe la Taifa, alisema kutoaminiwa na Phiri kulikopelekea kushindwa kuitumikia vema Simba ndiko kulikomfanya asifurukute.
Akizungumza na MICHARAZO, Gilla alisema hata kushindwa kuitwa kwake kwenye timu za taifa, zikiwemo za vijana, inatokana na kukalishwa benchi na Phiri.
Phiri aliondoka Simba mara baada ya kumalizika kwa ligi kuu ya Bara msimu uliopita.
"Kushindwa kuaminiwa na Phiri na kunipa nafasi ya kuonyesha uwezo wangu katika kufumania nyavu umenisababishia haya yote yanayonikuta ndani ya Simba na kukosa kuitwa hata katika timu za vijana ambazo huenda ningezisaidia," alisema Gilla.
Gilla, anayekaribia umri wa miaka 21, alisema misimu miwili aliyokuwa Simba hakuwahi kupata nafasi ya kucheza dakika 90 za mchezo wowote, kitu alichodai sio kimemvuruga akili, bali kimemnyima fursa ya kuonekana kama alivyong'ara kenye Kombe la Taifa akiwa na timu ya mkoa wa Tanga.
Katika michuano hiyo, Gilla aliibuka Mchezaji Bora, huku akiteuliwa mara mbili kuwa 'nyota' wa mchezo ukiwemo ule wa kusaka mshindi wa tatu ambapo Tanga waliilaza Mwanza mabao 2-0.
Alisema hajakata tamaa kutamba kisoka, hatahivyo.
Alisema anaamini alichokutana nacho Simba ni mtihani hivyo anajipanga ili kuendeleza kipaji chake kilichomfanya aichezee Polisi Dodoma chini ya Sekilojo Chambua kabla ya kutua Simba.

Simba yaanza kwa kusuasua Kagame, Ocean View safi



MABINGWA wa kihistoria wa michuano ya Klabu Bingwa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, 'Kagame Cup' Simba ya Tanzania jana ilianza kwa kusuasua michuano hiyo baada ya kulazimishwa suluhu na Vital'O ya Burundi, katika pambano la lililofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.
Simba inayopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kutokana na kucheza nyumba na rekodi yake nzuri michuano hiyo inapofanyika Tanzania, imebakiza mechi dhidi ya Zanzibar Ocean View, Etincelles ya Rwanda na wawakilishi wa Eritrea -- Red Sea.
Nafasi nzuri zaidi ya kupata bao kwa Simba ambayo ilianza mchezo na wachezaji wanne wapya ilikuja mwishoni mwa kipindi cha kwanza wakati Haruna Moshi 'Boban' alipopiga mpira wa kwa tik tak uliogonga mwamba wa mabingwa wa Burundi hao kabla ya kuokolewa na mabeki.
Shuti la 'Boban' ambaye hajacheza kwa miaka miwili kutokana na mzozo wa mkataba kati yake na Gefle IF ya Sweden lilikuja kutokana na krosi ya Ulimboka Mwakingwe ambaye kama mpigaji huyo amerudi kikosini baada ya kuachwa msimu uliopita.
Mwakingwe aliuwahi mpira mikononi mwa mlinda mlango wa Vital'O kufuatia shambulizi kali kwenye lango la wapinzani wa Simba hao, pembeni mwa eneo la hatari kabla ya kupiga krosi.
Kikosi cha Simba yenye pointi moja sawa na Vital'O na ambayo bado ina matumaini ya kusonga mbele kutokana na kundi lake kuwa na nafasi tatu za kucheza robo-fainali, kilikuwa pia na mchezaji wa zamani Said Nassoro 'Cholo' na Walulya Derick.
Kocha wa Simba MOses Basena alisema ameshangazwa na matokeo ya kutofungana wakati Simba ilitengeneza nafasi nyingi katika mchezo huo. Na kweli.
Wakati Vital'O ilicheza kwa kujihami zaidi na kushambulia kwa kushitukiza mara nyingi, Simba ilikuwa na mlolongo wa mashambulizi langoni mwa warundi hao.
Kocha wa Vital'O Younde Kagabo alisema ameridhika na sare hiyo kutokana na timu yake kuwa na wachezaji 10 wapya uwanjani.
Katika mchezo wa kwanza mabingwa wa Zanzibar, Zanzibar Ocean View walianza kwa kishindo michuano hiyo baada ya kuilaza Etincelles ya Rwanda kwa mabao 3-2 na hivyo kuongoza kundi hilo la A linalohusisha timu tano.
Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo kwa mechi za kundi B ambapo mabingwa wa soka nchini Tanzania, Simba itakwaruzana na El Merreikh ya Sudan iliyokuja kwenye michuano hiyo baada ya mabingwa wa nchi yao, Al Hilal kujitoa ili ijiandae vema na Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi inayotarajiwa kuanza mwezi ujao.
Mechi ya Yanga na Wasudan hao ambao inakumbusha fainali za michuano hiyo za mwaka 1986 ambapo Yanga ilikomboa mabao mawili dakika mbili za mwisho wa mchezo kupitia Abubakar Salum 'Sure Boy' kabla ya kulazwa kwa mikwaju ya penati na kuliacha kombe liondoke Tanzania, itachezwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pambano jingine la leo ni la kundi C michezo inayochezwa uwanja wa Jamhuri, Morogoro kwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo, APR ya Rwanda kuumana na Ports Authority ya Djibout.

Saturday, June 25, 2011

Dialo kutoka Bondeni ana tatu mpya




MSANII aliyewahi kufanya shughuli zake nchini Afrika Kusini, Zakaria Kazi Mkombozi maarufu kama Dialo, akishirikiana na bendi yake binafsi ameachia nyimbo tatu mpya ikiwa ni maandalizi ya kupakua albamu yao ya kwanza.
Akizungumza na mtandao huu, Dialo, alizitaja nyimbo hizo ambazo zimeanza kusambazwa kwenye vituo vya redio kuwa ni 'Sudan Risen' unaozungumzia hali ya kisiasa nchini Sudan, 'Madoda Mpela' uliombwa Kizulu na 'Let Do It'.
Dialo alisema nyimbo hizo ni kati ya nyimbo zitakazokuwa kwenye albamu yao ijayo ambayo bado hawajaipa jina, ila alisema itakuwa na nyimbo 10 zilizopo kwenye miondoko ya Reggae, Afro Pop na Ragga.
"Baada ya kuwa kimya tangu niliporejea nchini kutoka Afrika Kusini, nilipokuwa nafanya shughuli zangu za muziki, nimefanikiwa kuunda bendi ambayo tumeachia kazi tatu mpya ikiwa ni maandalizi ya kupakua albamu yetu ya kwanza," alisema.
Dialo alisema mbali na kuendesha bendi ya muziki, lakini pia ameanzisha klabu ya vijana kwa ajili ya kuwapa elimu ya stadi za maisha na kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na kujikinga na ukimwi.
Alisema bendi yake ina jumla ya wasanii sita ambao ni yeye Dialo, Bob Chuwa, Dk Today, Alex, Katanga Junior (mdogo wa aliyekuwa mpiga dramu maarufu nchini, Gabby Katanga, ambaye kwa sasa ni marehemu, Yuzo na Amani.
Dialo, aliyewahi kufungwa kwa muda wa miaka mitatu nchini Afrika Kusini kwa kile alichodai kufanyiwa hila na watu aliokuwa akifanya nao kazi ya muziki nchini humo, alisema beni yao inatarajiwa kutumbuiza mjini Moshi siku ya Juni 17 mwaka huu.
Alisema onyesho hilo litafanyika kwenye ukumbi wa Glacian Sports Bar, ambapo mbali na kutambulisha nyimbo zao, lakini pia watapiga nyimbo za magwiji wengine wa muziki duniani kwa staili ya kukopi.
"Tumeanza kufanya maonyesho ambapo Juni 17 tulikuwa nyumbani Moshi, Kilimanjaro kwenye ukumbi wa Glacian Sports Bar," alisema.

Nisha: Wasanii tusiridhike mapema


MSANII anayekuja juu kwenye fani ya filamu nchini, Salma Jabu 'Nisha' amewataka wasanii wenzake kutoridhika na mafanikio ya kutamba nyumbani na badala yake kujibidiisha kujitangaza katika anga la kimataifa.
Nisha aliyeng'ara kwenye filamu kama 'Family Disaster', 'Better Day', 'Kimya' na nyinginezo, alisema kulewa sifa na mafanikio ya nyumbani kwa wasanii wengi nchini kunachangia wengi wao wasitambe kimataifa, kitu kinachopaswa wabadilike sasa.
"Wasanii nchini wanapaswa kubadilika na kujitangaza kimataifa, tusiridhike na mafanikio ya nyumbani kwani ndio yanatufanya tusipige hatua kubwa kimaendeleo kama wenzetu wa nje,' alisema Nisha, aliyejitumbukiza kwenye fani hiyo miaka mitatu iliyopita.
Nisha ambaye yupo mbioni kuibuka na filamu iitwayo 'Simu Sikioni' ya msanii nguli, Deo Shija, alisema hata yeye mwenyewe pamoja na nyota ya neema kuanza kumulikia kwa sasa nchini, hataridhika hadi atakaposimama kimataifa akichuana na wakali wa dunia katika fani hiyo.
"Ndoto zangu ni kutamba kimataifa kwa kuwa sitaridhika na mafanikio ya nyumbani, jambo ambalo kila msanii wa ukweli anatakiwa awe hivyo," alisema Nisha.
Mzanzibar huyo, alisema anaamini kama kila msanii atakuwa na kiu ya kutamba kimataifa ni wazi Tanzania itajitangaza na kutoa fursa ya Watanzania kutambulika kama ilivyo kwa Wanigeria, Wamarekani na wasanii wengine wanaotamba ulimwenguni.

Monday, April 25, 2011

Tamasha la ngumi laanzishwa Dar

MABONDIA mbalimbali wakiwemo wakongwe na chipukizi wanatarajia kujumuika pamoja katika tamasha maalum la ngumi linaloanza rasmi kesho kwenye Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam.
Tamasha hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Kinyogoli Foundation inayomilikiwa na bondia wa kimataifa wa zamani ambaye ni kocha kwa sasa, Habib Kinyogoli, awali lilipangwa kufanyika leo Jumatatu ya Pasaka, kwenye ukumbi wa Panandipanandi.
Akizungumza na MICHARAZO, mmoja wa waratibu wa tamasha hilo, Rajabu Mhamila 'Super D' alisema katika tamasha hilo, mabondia mbalimbali wakongwe na chipukizi watachuana na lengo ni kuwapa nafasi chipukizi ya kujifunza mbinu kutoka kwa mabondia hao wazoefu.
Super D ambaye pia ni bondia wa zamani na kocha wa klabu ya Ashanti, alisema yeye na Kinyogoli, wameamua kushirikiana kuandaa tamasha hilo ili kuhakikisha mchezo wa ngumi nchini unarejesha heshima yake baada ya kudorora kwa muda mrefu.
"Katika kurejesha hadhi ya ngumi nchini, tumeamua kuandaa tamasha la ngumi ambalo litakuwa likifanyika kila wiki kwenye ukumbi wa Panandi Panandi ambapo wakongwe na mabondia wanachipukia watashirikiana kupigana katika kutoa burudani," alisema Super D.
Aliongeza kuwa, mbali na michezo kadhaa ya ngumi, ikiwahusisha baadhi ya nyota wa mchezo huo kama mabondia wa ukoo wa Matumla, pia tamasha hilo litapambwa na burudani kemkem za muziki kutoka kwa wasanii ambao watakakuwa wakipokeza kwenda kutumbuiza kama njia ya kuwahamasisha watu kuhudhuria kwa wingi.

Sikinde wana mbili mpya



BENDI ya Mlimani Park 'Sikinde' imekamilisha vibao viwili ikiwa ni moja ya mikakati yake ya kujipanga upya baada ya kuondokewa na mwanamuziki wake, Shaaban Dede aliyejiunga na mahasimu wao, Msondo Ngoma.
Katibu wa bendi hiyo, Hamis Milambo, alisema kuwa bendi yao ambayo kwa wiki mbili mfululizo imekuwa kambini ikijifua, ambapo imekamilisha nyimbo mbili zilizotungwa na muimbaji wao mkongwe, Hassani Bitchuka.
"Tumeanza kujipanga upya kwa ajili ya kupakua albamu mpya na tayari tupo kambini kwa wiki ya pili sasa, ambapo tumeshakamilisha nyimbo mbili mpya zilizotungwa na Bitchuka," alisema.
Katibu huyo alisema nyimbo hizo zinazoendelea kufanyiwa mazoezi, hazijapewa majina hadi sasa na zitatambulishwa kwa mashabiki wao katika maonyesho yao ya Sikukuu ya Pasaka.
"Tutazitambulisha kwenye maonyesho yetu ya Pasaka, na hapo ndipo zitakapofahamika majina yake, ila ni kati ya nyimbo zitakazothibitisha kuwa Sikinde ni mabingwa wa muziki wa dansi nchini," alisema Milambo.
Milambo alisema baada ya maonyesho ya Pasaka, bendi yao itarejea kambini kwa ajili ya kumalizia kuzifanyia mazoezi nyimbo nyingine mpya ambazo zimeshaandikwa mashairi na waimbaji wao, Abdallah Hemba na Hassani Kunyata tayari kukamilisha idadiu ya nyimbo zinazotakiwa kwa albamu yao ijayo.
Tangu mwaka juzi, Sikinde ilipotoa albamu yao ya Supu Imetiwa Nazi, bendi hiyo haijaachia albamu nyingine zaidi ya vibao viwili vya Wanawake Wanaweza na Tunu ya Upendo vilivyotungwa na Dede maarufu kwa sasa kama 'Mzee wa Loliondo' ambaye ameenda Msondo Ngoma.

Kitabu cha Assosa chatinga mitaani





KITABU cha mwanamuziki nguli wa muziki wa dansi, Tshimanga Kalala Assosa, kiitwacho 'Jifunze Lingala' kimeingia mitaani, huku mwenyewe akijiandaa kutoa toleo la pili la kitabu hicho kinachofundisha lugha ya Kilingala na Kiswahili.
Akizungumza na MICHARAZO, Assosa, alisema kitabu hicho ambacho mbali na kufunza watu Kilingala, pia kina tafsiri ya nyimbo za wanamuziki maarufu wa Kongo na kiliingia sokoni tangu juzi huku kikigombewa kama njugu.
Assosa, alisema tangu akiingize sokoni kitabu hicho kimeshauza kopi zaidi ya 1000, huku akipokea oda kedekede toka kila pembe ya nchi kwa watu wanaokiulizia.
"Aisee kile kitabu changu nimeshakiingiza sokoni, na huwezi kuamini kimekuwa kikinukuliwa kama njugu tofauti na matarajio yangu, hali inayonifariji mno," alisema Assosa.
Mkongwe huyo aliyewahi kuzipigia bendi za Negro Succes, Orchestre Lipualipua, Fukafuka, Le Kamalee, Marquiz du Zaire, Marquiz Original, Mambo Bado, Legho Stars na sasa Bana Marquiz, alisema hakutaraji kama kingegombewa.
Alisema hakuwa na tumaini la kugombewa kwa kitabu chake kutokana na ukweli ndicho cha kwanza kwake kukitoa tangu aamue kujikita kwenye uandikaji wa vitabu, nje ya shughuli zake za muziki anaoendelea nao hadi sasa.
Aliongeza kuwa, hali hiyo unamfanya afikirie kuongeza idadi ya nakala zake, ili kukidhi mahitaji ya mashabiki wanaokiulizia ambacho ndani yake pia kina picha za wasanii wakongwe wa Kongo pamoja na yeye na familia yake.
"Kama watakuwa wanavihitaji pia wanaweza kwenda pale Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, kuna wakala anaviuza pale, au wanaweza kunipigia simu namba 0713-240735, watakipata." alisema Assosa.

Rapa wa Levent atua TOT-Plus

BENDI ya TOT-Plus ambayo sasa inaendelea na kambi yake ya mazoezi, Mwananyamala, jijini Dar es Salaam, imempata rapa mpya Dokta Steve 'Sauti ya Ng'ombe' kutoka bendi ya Levent Musica ya mjini Morogoro.
Kiongozi wa TOT-Plus, Badi Bakule, alisema rapa huyo alijiunga na tangu wiki iliyopita na anaendelea
na mazoezi kama kawaida akisubiri kutambulishwa rasmi.
"Tumemchukua rapa huyu ili kuziba nafasi ilioachwa na Jua Kali ambaye ameachana na TOT-Plus na kwenda kufanya kazi kwingine, Dokta Steve ameonyesha uwezo mkubwa hivyo anatufaa," alisema Bakule.
Bakule alisema bendi hiyo ambayo imekuwa na mazoezi kwa zaidi ya mwezi mmoja, inatarajia kutoka kambini Ijumaa Aprili 29 na kisha itajitambulisha rasmi Mei Mosi.
Alisema, rapa huyo kwa sasa amekuwa akijifua katika mazoezi makali kwenye kambi ya bendi hiyo iliopo eneo la Ujiji Mwananymala, jijini Dar es Salaam ili kuhakikisha kwamba anaibuka na vitu vipya.
"Pia tunataka azijue nyimbo zote mpya ambazo tayari tumezikalimisha na hata zile za zamani ambazo wanamuziki karibu wote wamezifanyia mazoezi kabla rapa huyu mpya hajajiunga na bendi yetu," alisema.
Kiongozi huyo alizitaja nyimbo hizo mpya kuwa ni 'Kilio cha Linda', 'Zai' 'Maisha Duni', Liwalo na Liwe','Dakika Tisa' na 'Riziki na Zengwe' ambazo baadhi yake tayari zimesharekodiwa.
Aliongeza kuwa 'Sauti ya Ng'ombe' atatoka kambini akiwa pia amemaliza kuzifanyia mazoezi baadhi ya nyimbo za zamani zilizochangia kuiweka TOT-Plus kwenye matawi ya juu.
"Kuna nyimbo kama Masimango, Mtaji wa Masikini, Elimu ya Mjinga, Mtoto Yatima, Mnyonge Mnyongeni na nyingine nyingi ambazo anatakiwa azifahamu vizuri kabla hatujatoka kambini," alisema.
Tangu imalize kampeni za Uchaguzi Mkuu mwishoni mwa mwaka jana, bendi hiyo bado haijafanya maonyesho na badala yake imeingia kambini ili kujipanga vizuri kwa ajili ya kuibuka kwa kishindo.

Stone Mayiyasika wanasa watano

BENDI ya Stone Mayiyasika 'Vijana wa Kazi' imeimarisha safu ya ushambuliaji wa jukwaa kwa kunasa wanenguaji watano akiwemo mnenguaji mahiri aliyewahi kutamba na bendi ya Twanga Pepeta, Juma Mohamed (Super Danger).
Mratibu wa bendi hiyo, Pascal Mahollelo, alisema wanenguaji hao watano wameanza mazoezi na katika maonyesho yao yote ya kusheherekea sikukuu ya Pasaka wataanza kuwatambulisha kwa mashabiki.
Alisema, mbali ya Super Danger ambaye ni mkongwe, wanenguaji wengine wapya ni wa kike na kwamba ni chipukizi ambao wameonyesha uwezo mkubwa wa kazi.
Aliwataja wanenguaji hao wa kike kuwa ni Zawadi Seif, Joselina Ngatunga (Happy), Shania Malimba na Mwanahamisi Ramadhan.
"Sisi hatuhitaji kugombana na watu ndiyo maana tumeona tuwatengeneze wetu wenyewe na nina imani mashabiki watawakubali kutokana na umahiri wao jukwaani" , alisema Mahollelo.
Alisema, utambulisho wa wanenguaji hao ungeanza kwenye maonyesho yao Sikukuu ya Pasaka.

Cloud atambia Basilisa




MSANII nyota wa filamu nchini, Issa Mussa 'Cloud', amedai filamu yake mpya ya 'Basilisa' ni funika bovu, miongoni mwa kazi zake alizowahi kuzitoa kwa hivi karibuni.
Cloud, alisema filamu hiyo iliowashirikisha wasanii kadhaa mahiri nchini, akiwemo mrembo Wema Sepetu na Ummy Wenslaunce 'Dokii', inaweza kuwa kazi bomba kwa mwaka huu wa 2011 kwa jinsi ilivyoandaliwa kwa ustadi mkubwa.
Mkali huyo aliyetamba na michezo ya kuigiza kupitia runinga kabla ya kuibukia filamu, alisema 'Basilisa' ambayo itasambazwa na kampuni ya Steps Entertainment ni bora kati ya zote alizowahi kuzitoa tangu aiingie kwenye fani hiyo.
Alisema kinachomfanya aamini hivyo ni kwa jinsi hadhithi yake ilivyo, namna alivyoshiriki na umahiri ulioonyeshwa na wasanii wenzake, acha upigaji picha wa kiwango cha hali juu na mandhari iliyotumika kurekodiwa kazi hiyo.
"Sio vibaya mtu kujisifia kwa jinsi anavyofanya kazi yake, nami naiona 'Basilisa' ni moja ya kati niliyoumiza kichwa na kushiriki kwa kiwango kikubwa, nadhani itakuwa miongoni mwa kazi bora kwa mwaka," alisema Cloud.
Msanii huyo, ambaye hushirikishwa kazi mbalimbali, alisema ndani ya filamu hiyo ameigiza katika nafasi tatu tofauti kama alivyowahi kufanya muigizaji wa Kimarekani, Eddy Murphy katika filamu yake ya 'Nutty Professor'.
Tofauti na Murphy aliyeigiza kikomedi zaidi, Cloud ndani ya filamu yake ameigiza 'siriazi' akiwa kama chizi, kiumbe wa kutisha na hali yake ya kawaida, kiasi ni vigumu kubaini kama nafasi hizo tatu tofauti zimechezwa na mtu mmoja.
Mbali na yeye (Cloud) wengine walioshiriki filamu hiyo itakayoingia sokoni mwezi ujao ni Adam Kuambiana, Dokii, Wema Sepetu, Selemani Barafu 'Mzee wa Land Rover', Single Mtambalike 'Richie', Kajala Masanja na wengineo.

Friday, April 15, 2011

Mbio za usajili zaanza Bara * Mastaa wa vigogo matumbo joto * Zilizopanda zawanyemelea







PAZIA la usajili wa wachezaji kwa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa ajili ya msimu ujao wa limefunguka kwa klabu mbalimbali kupigana vikumbo kupata saini za nyota inayowahitaji.
Ingawa, Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, halijatangaza zoezi ya usajili litaanza lini, tayari vilabu kadhaa vimeshaanza kujinadi kuwanasa wachezaji wapya na kuwafungulia milango ya kutoka wasiowahitaji kwa msimu ujao, huku Simba, Yanga na Azam zikiongoza kwenye mbio hizo.
Simba ambayo ilipoteza ubingwa kama utani kwa watani zao, imedaiwa imeshawatangazia baadhi ya wachezaji wake kuwa waangalie ustaarabu wake, huku ikiwa imeshawasainisha wachezaji kama Mwinyi Kazimoto toka JKT Ruvu, Patrick Mafisango na wengine wakiendelea kuwafukuzia.
Walioachiwa milango ya kutokea hadi sasa, ingawa haijatangazwa rasmi ni pamoja na kipa Juma Kaseja, kiungo Mohammed Banka, Mussa Hassani Mgosi, Joseph Owino, Hillary Echessa, Salum Kanoni, Anthony Matangalu, Mohammed Kijuso na David Naftal waliokuwa kwa mkopoa klabu za AFC Arusha na Majimaji Songea.
Pia katima orodha hiyo anatajwa beki Kelvin Yondan, ambaye inadaiwa yu mbioni kutua kwa mahasimu wa Simba, Yanga iliyokuwa ikimwinda kwa muda mrefu.
Inaelezwa Yanga inamtaka Kelvin kutokana na kuwepo kwa taarifa kwamba beki wake, Nadir Haroub 'Cannavaro' yu mbioni kutua Azam iliyoanza kumnyemelea tangu msimu ulioisha karibuni.
Yanga wenyewe tayari imeshawapoteza wachezaji wao wawili 'mapro', Mghana Ernest Boakye na Ivan Knezevic wanaodaiwa watakipiga msimu ujao ndani ya Azam Fc.
Ingawa, Yanga imesema inasubiri mapendekezo ya kocha wake, Sam Timbe kuimarisha kikosi chao, baadhi ya wachezaji wanaodaiwa hawatakuwa na timu hiyo msimu ujao ni pamoja na Issac Boakye wa Ghana, Nsa Job, Shamte Ally, Nelson Kimath na wengine walioonekana kuwa 'mizigo'.
Baadhi ya klabu zilizopanda daraja msimu huu zenyewe zinatajwa kuwavizia baadhi ya nyota watakaoachwa katika klabu hizo kubwa ili kuimarisha vikosi vyao kabla ya kushiriki ligi hiyo ngumu na kubwa kwa Tanzania.
Timu zilizopanda daraja toka Ligi Daraja la Kwanza ni pamoja na Villa Squad na Moro United za Dar, JKT Oljoro ya Arusha na Coastal Union ya Tanga inayorejea tena kwenye ligi hiyo.

Ligi ya Kick Boxing sasa Juni





MICHUANO ya Ligi ya Ubingwa kwa Mchezo wa Kick Boxing iliyokuwa ichezwe mwishoni mwa Machi, imesogezwa mbele hadi Juni mwaka huu.
Mratibu wa michuano hiyo, Japhet Kaseba, alisema ligi hiyo imekwama kufanyika kutokana na kutingwa na mazoezi ya maandalizi ya pambano lake la Ngumi za Kulipwa kati yake na bondia Mada Maugo.
Kaseba atapigana na Maugo, wiki ijayo kwenye ukumbi wa PTA, Dar es Salaam katika pambano lisilo na mkanda la uzito wa kilo 72 kuwania nafasi ya kupigana na bingwa wa dunia, Francis Cheka wa Morogoro.
Akizungumza na MICHARAZO, Kaseba, alisema kubanwa na mazoezi kumemfanya ashindwe kuratibu ligi hiyo na kusema, mara baada ya pambano lake atatangaza tarehe rasmi ya ligi hiyo ingawa alisema kuna uwezekano ikafanyika mwezi Juni.
"Nimeshindwa kuratibu ligi kama nilivyopanga ifanyike Machi na sasa natarajia ifanyike Juni, ingawa tarehe nitaitangaza baada ya kumaliza pambano langu dhidi ya Maugo ambalo ndilo lililonifanya niwe 'bize', nataka kumpiga nikapigane na Cheka," alisema.
Kuhusu maandalizi ya pambano hilo, Kaseba alisema anaendelea vema na ana matumaini makubwa ya kushinda pambano hilo, la raundi 10 lililoandaliwa na Double K Entertainment, litakalosimamiwa na TPBO inayoongoza na Rais wake, Yasin 'Ustaadh' Abdalla.
"Kwa kweli naendelea vema, najifua usiku na mchana kuhakikisha nakuwa fiti nimpige Maugo, ili nikavaane na Cheka kuthibitishia mashabiki wangu kuwa, sikupigwa kihalali na Cheka kwenye pambano letu la uwanja wa Uhuru," alisema Kaseba.


Mwisho

Matumla kuzichapa Dodoma




BINGWA wa zamani wa Dunia wa Ngumi za Kulipwa nchini, Rashid Matumla 'Snake Man' anatarajiwa kupanda ulingoni siku ya Pasaka kuzipiga na Mkenya, Joseph Odhiambo katika pambano litakalofanyika mjini Dodoma.
Rais wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania, TPBO, Yasin Abdallah 'Ustaadh', alisema pambano lisilo la ubingwa la uzani wa Middle, litakuwa la raundi 10.
Ustaadh, alisema lengo la pambano hilo ni kusaidia kuinua mchezo wa ngumi mkoani humo sambamba na kuwapelekea burudani wakazi wa mji huo ambao watakuwa wakisherehekea sikukuu ya Pasaka.
"Dodoma imekuwa ikipelekewa burudani za muziki, mpira na kadhalika, lakini mchezo wa ngumi kwa muda mrefu haujafanyika mjini humo na TPBO tumeamua kuwapelekea pambano hilo kubwa kama njia ya kuhamasisha mchezo huo na kuwaburudisha wakati wa sikukuu," alisema.
Alisema maandalizi ya pambano hilo litakalodhaminiwa na mfanyabiashara maarufu wa mjini humo, Moshi Semayu yamekamilika na watautangazia umma pambano hilo litafanyikia wapi, ingawa alikuwa na hamu lifanyike uwanja wa Jamhuri, mjini humo.
Aliongeza, baada ya pambano hilo la Dodoma, TPBO ilikuwa itafanya mipango ya kuandaa michezo mingine ya ngumi za kulipwa katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Singida na kadhalika kwa lengo la kuuhamasisha mchezo huo katika mikoa hiyo.
Matumla, aliyewahi kuwa bingwa wa dunia wa WBU, alisema yupo fiti kumchapa Odhiambo, ili kudhihirisha kuwa yeye bado wamo katikia mchezo huo uliomjengea sifa ndani na nje ya nchi.

Wakazi wa Udzungwa kufunzwa namna ya kutunza Mbega

SHIRIKA lisilo la kiserikali la STR8 UP Vibes imeandaa warsha maalum kwa wakazi wanaoizunguka hifadhi ya Udzungwa juu ya kuwatunza wanyama aina ya Mbega wekundu wanaopatikana kwenye hifadhi hiyo.
Warsha hiyo imepangwa kufanyika hivi karibuni, mkoani Morogoro, ambapo mbali ya kuwatunza wanyama hao lakini pia itakuwa na lengo la kutoa elimu ya kuvitunza vyanzo vya maji.
Akizungumza na Mtandao huu, mratibu wa warsha hiyo, Salum Kondo alisema kuwa, wameamua kuandaa warsha hiyo ili kuwapa elimu ya kutosha watu wote wanaoishi kando kando ya hifadhi za taifa kujua jinsi ya kuwatunza wanyama na vyanzo vya maji.
Kondo, alieleza kuwa kwa kuanzia wamemua kuanza na mkoa wa Morogoro, ambapo baadaye wataaendelea kwenye mikoa mingine iliyo na hifadhi za Taifa.
"Dhumuni letu ni kuwapa elimu watu wote wanaishi karibu na hifadhi za Taifa, lakini kutokana na umuhimu wa hifadhi za Udzungwa, tumekubaliana tuanzie huko" alisema.
Aliongeza kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la kuwauwa Mbega Wekundu, hali ambayo inaweza kusababisha wanyama hao kutoweka kabisa Duniani.
Kondo aliongeza kuwa kwa kuwa wanyama hao hupatikana, Udzungwa pekee, wameona kuna haja ya kuwalinda kwa gharama yeyote.
"Kama wakazi wa wanaizunguka hiafdhi ya Udzungwa watapatiwa elimu ya kutosha juu ya kuwatunza wanyama hao na namna ya kuwatumia kuwaingizia kipato, bila shaka wataacha kuwaua," alisema.
Kondo alisema katika Kongamano hilo litakalofanyika mkoani Morogoro linatarajia kuwashirikisha wadau mbali ikiwa ni pamoja na wanavijiji, wataalam kutoka wizara ya Maliasili na Utalii, ambapo pia kutakuwa na burudani mbalimbali zitakazowakilisha mila na tamaduni za mkoa huo.

KITABU CHA ASSOSA CHATOKA HADHARANI




Na Badru Kimwaga
MWANAMUZIKI mkongwe wa muziki wa dansi, Tshimanga Kalala Assosa, amekamilisha kitabu chake cha tafsiri ya Lugha ya Kilingala na Kiswahili kiitwacho 'Jifunze Lingala', ambapo licha ya kufunza lugha hizo mbili pia ina nyimbo kadhaa za wanamuziki wa zamani wa DR Congo (Zaire).
Kitabu hicho kilichoanza kuandaliwa tangu mwishoni mwa mwaka jana, tayari kimeshachapishwa na mwanamuziki huyo anayemiliki bendi ya Bana Marquiz anafanya mipango ya kuanza kuvisambaza ili wadau wa muziki wa lingala na wengineo waanze kukipata.
Akizungumza na MICHARAZO, Assosa, aliyewahi kutamba na bendi mbalimbali kama 'Negro Succes', 'Le Kamalee', 'Lipualipua' na 'Fukafuka', alisema kitabu hicho ni mwanzo wa kujitosa kwenye kazi ya uandikaji vitabu wenye lengo la kufundisha lugha ya Kilingala, moja ya lugha maarufu ya Congo.
Assosa, alisema msukumo wa kuandika kitabu hicho alichochapisha nakala 50,000 za awali kama majaribio ni kutokana na simu na maombi ya mashabiki wa muziki wanaofuatilia fasiri zake katika kituo cha TBC! kinachohusu miziki ya Kavasha.
"Nilikuwa napokea simu nyingi za kuwatafsiria watu baadhi ya nyimbo za nyota wa zamani wa Zaire (sasa DR Congo) na kupata wazo la kuandaa kitabu kwa mfumo wa kamusi ambao pia una nyimbo za wakali hao na tafsiri mbalimbali za maneno ya lugha hiyo," alisema Assosa.
Mtunzi na muimbaji huyo aliyefanyia kazi bendi nyingine za 'Mambo Bado', 'Legho Stars', 'DDC Mlimani Park', 'Marquiz du Zaire' na ile ya Original, alisema mafanikio ya mauzo ya kitabu hicho kitamfanya aweze kutoa muendelezo wake siku za baadae.
Assosa, alisema shukrani pekee katika maandalizi ya kitabu hicho 'toleo la kwanza' ni kwa wanachama wa klabu ya Dar Family Kavasha na Mhariri, Joseph Kulangwa aliyekihariri hadi kuweza kuchapishwa na kuandaliwa kuachiwa mtaani wakati wowote kuanzia sasa.
Mwanamuziki huyo aliyetamba kwa utunzi wa nyimbo kama 'Minou', 'Salama', 'Huba', 'Promotion' 'Masua' na 'Abisina' alizoimba kwa kushirikiana na Nyboma Mwandido, alisema pamoja na kutaka kujitosa jumla kwenye utunzi wa vitabu, bado hajaachana na kazi ya muziki akiwa na bendi yake ya Bana Marquiz ambayo inaendeela kutumbuiza kuanzia Alhamis hadi Jumapili kila wiki.

Mwisho

KASEBA, MAUGO WAPIMA UZITO KUZIPIGA KESHO PTA






MABONDIA Japhet Kaseba na Mada Maugo pamoja na watakaowasindikiza kwenye pambano lao litakalofanyika Jumamosi, wanatarajiwa kupima uzito wao leo jijini Dar es Salaam.
Upimaji huo wa uzito utafanyika kwenye ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO saa 5 asubuhi, ukihusisha pia upimaji wa afya kama moja ya kampeni ya kupambana na ukimwi michezoni.
Akizungumza na MICHARAZO asubuhi ya leo, Mratibu wa pambano hilo, Kaike Siraju, alisema mabondia wote watakaopigana Jumamosi watapimwa leo tayari kwa michezo hiyo itakayofanyika kwenye ukumbi wa PTA, jijini Dar es salaam.
Siraju, alisema mbali na Kaseba na Maugo watakaopogana kwenye pambano la kusaka mkali kati yao ili kupata tiketi ya kwenda kupigana na Francis Cheka, mabondia wengine watakaopimwa ni wale watakaosindikiza pambano hilo.
"Mabondia wanaotarajiwa kucheza siku ya Jumamosi kwenye pambano la kusaka mkali kati ya Kaseba na Maugo, watapimwa uzito na afya yao siku ya Ijumaa majira ya saa 5 asubuhi kwenye ukumbi wa Idara ya Habari-Maelezo," alisema Siraju.
Siraju, alisema maandalizi ya michezo yote ikihusisha pambano hilo la Nani Mkali la uzani wa Middle raundi 10, yamekamilika na kinachosubiriwa ni mashabiki kwenda ukumbini kupata burudani.
Michezo itakayosindikiza pambano hilo la Kaseba na Maugo, ni lile la Bingwa wa Kick Boxing wa Afrika, Kanda Kabondo atakayezipiga na Maneno Osward 'Mtambo wa Gongo', nahodha wa zamani wa ngumi za ridhaa, Joseph Martin dhidi ya George Dimoso.
Mapambano mengine ni la Yohana Robert dhidi ya Saidi Zungu, Deo Njiku atakayepigana na Issa Sewa, Fadhili Awadh atapigana na Bakari Dunda na Hassan Mandula atatwangana na Uwesu Said, Mohammed Matumla 'Snake Boy Junior' atakayeonyeshana kazi na Sadiki Momba.

Mwisho

Mafisango ambadili Humud Simba






KIUNGO aliyetua Msimbazi kwa mbwembwe na kuishia kushindwa kutamba katika timu ya Simba kutokana na majeruhi ya mara kwa mara, Abdulhalim Humoud, ametua Azam akipishana na beki Mnyarwanda Patrick Mafisango.
Humoud aliyesajiliwa na Simba msimu uliopita akitokea Mtibwa Sugar, ikiwa ni siku chache tangu ang'are kwenye pambano la kihistoria la kimataifa kati ya Tanzania na Brazil, ni miongoni mwa wachezaji wapya waliotua Azam kwa ajili ya msimu ujao.
Kwa mujibu wa taarifa za mtandao wa klabu hiyo, kiungo huyo anayependa kufananishwa na Ronaldinho Gaucho, ametua Azam akibadilishana na beki Mafisango aliyeenda Msimbazi kuimarisha kikosi chao kilichopoteza ubingwa kwa Yanga.
Wachezaji wengine wapya waliotuma Azam, ikiwa ni kati ya wachezaji 20 waliopendekezwa na kocha wao, Stewart Hall ni pamoja na aliyekuwa kipa wa Yanga,
Obren Cuckovic toka Serbia na Mwadini Ally aliyekuwa Mafunzo ya Zanzibar.
Pia wamo Waziri Salum toka Mafunzo, Ghulam Abdallah wa Chuoni Zanzibar, Zahor Pazi wa African Lyon na nyota wa Ocean View, Khamis Mcha 'Viali'.
Habari hizo zinasema kuwa hao ni sehemu ya wachezaji wapya wanaotua Azam kuungana na wachezaji wengine walioisaidia klabu hiyo kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao wameshasainishwa mikataba mipya.
Wachezaji hao kwa mujibu wa mtandao huo ni Manahodha Ibrahim Shikanda na Aggrey Moris, Malika Ndeule, Lackson Kakolaki, Erasto Nyoni, Ibrahim Mwaipopo, Seleman Kasim Selembe, Kalimangonga Ongala, Jamal Mnyate, Mrisho Ngassa na John Bocco.
Wachezaji vijana waliokuwa wamepandishwa kwenye kikosi hicho toka timu ya vijana na kubakishwa ni Himid Mao, Salum Aboubakar na Jamal Mnyate, wakiongezewa nguvu na kipa Daudi Mwasongwe aliyepandishwa toka Azam Academy.
Makipa Vladmir Nhyonkulu na Jackson Chove pamoja na wachezaji wengine kama saba walioichezea timu hiyo wapo katika hatihati ya kuendelea kubaki katika kikosi hicho kinachosukwa kwa ajili ya kuongeza upinzani kwa msimu ujao wa ligi kuu nchini.

Mwisho

Tundaman ni Bora Tuachane tu



MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya toka kundi la Tip Top Connection, Khaleed Ramadhan 'Tundaman', ameachia kibao kipya kiitwacho 'Bora Tuachane', akiwa mbioni kufyatua wimbo mwingine akiwashirikisha Mapacha wa kundi la P Square la Nigeria.
Nyimbo hizo mbili ni maandalizi ya kufyatuliwa kwa albamu yake mpya itakayokuwa ya nne kwa msanii huyo aliyetumbukia kwenye sanaa ya muziki mwaka 2007 akitokea kwenye soka.
Akizungumza na MICHARAZO, Tundaman, alisema kibao hicho cha 'Bora Tuachane' ambacho kinatarajiwa kusambazwa hivi karibuni ni simulizi la kweli linalomhusu yeye.
"Wakati albamu yangu ya Hali Yangu Mbaya ikitamba sokoni, nimeanza maandalizi ya kufyatua albamu mpya ya nne, ambapo nimeachia ngoma inakwenda kwa jina la 'Bora Tuachane' ambao ni simulizi la kweli linalonihusu mimi mwenyewe," alisema Tundaman.
Msanii huyo, mwenye mtoto mmoja wa kike aitwae Khairat, alisema kama zilivyo nyimbo zake za nyuma, kibao hicho kipo katika mahadhi ya 'kulalamika' na kutamba kitabamba kutokana na ujumbe uliopo na midundo yake inayovutia.
Aliongeza mbali na kibao hicho, pia ana wimbo mwingine mpya ambao ataimba kwa kushirikiana na wasanii wawili mapacha wa Nigeria, P Square.
"Kibao kingine ninachokiandaa ni The All One, ambacho nimewatumia mistari P Square ili waweke sauti zao, kabla ya kuja kuchanganywa, mie nitaimba kiswahili na wao wataimba kwa lugha ya Kiingereza, lengo likiwa ni kusaka hadhi ya kimataifa," alisema.
Tundaman, aliyewahi kuzichezea timu za Friends Rangers na Yanga kabla ya kuhamia kwenye muziki, hadi sasa ana albamu tatu, ambazo ni Neila iliyomtambulisha rasmi kwenye ulimwengu wa muziki huo, Nipe Ripoti alioshirikiana na Spark na Hali Yangu Mbaya, aliyoachia hivi karibuni.

Coast Modern wapika albamu ya nne



BAADA ya kutamba na albamu yao ya 'Damu Nzito', kundi mahiri la muziki wa taarab la Coast Modern 'Watafiti wa Mipasho', limeanza maandalizi ya albamu yao mpya ya nne ikiwa imeshakamilisha nyimbo zipatazo tatu hadi sasa.
Mkurugenzi wa kundi hilo, Omar Tego 'Special One' aliiambia MICHARAZO kuwa, nyimbo tatu kati ya nne zinazolengwa kuwepo kwenye albamu hiyo ijayo zimeshakamilika kutungwa na kufanyiwa mazoezi tayari kupelekwa studio kurekodiwa.
Hata hivuo Tego alikataa kuzitaja nyimbo hizo kwa madai ni mapema mno na pia kuhofia asiibiwe 'idea' na wapinzani wake katika muziki huo wa taarab nchini.
"Tupo katika maandalizi ya kufyatua albamu yetu mpya itakayokuwa ya nne kwa Coast Modern, tayari tumekamilisha nyimbo tatu na tumesaliwa na mmoja, kuhitimisha nyimbo zitazotakiwa kabla ya kuzipeleka studio kurekodiwa," alisema Tego.
Tego alisema kwa jinsi walivyojipanga, huenda albamu hiyo ikakamilika na kuwa mitaani kabla ya Julai, kwani karibu kila kitu kimekamilisha wanachosubiri ni kuingia studio.
Alisema wataichelewesha kidogo albamu hiyo kutoka hadi Julai kwa nia ya kutoa nafasi ya albamu yao ya sasa ya 'Damu Nzito' kuendelea kutamba kwenye soko la muziki huo.
"Unajua tumeachia 'Damu Nzito' muda mfupi tu uliopita, hivyo ili kuipa nafasi ya kufanya vema sokoni, ndio maana tumepanga kuitoa albamu yetu ya nne kabla ya Julai," alisema Tego.
Kabla ya albamu hiyo ya 'Damu Nzito' kundi hilo la Coast Modern, liliachia albamu mbili zilizotikisa muziki wa mwambao nchini za 'I'm Crazy For You' na 'Kupendwa Isiwe Tabu' iliyokuwa na kibao kilichotamba cha 'Chongeni Fenicha Sio Maneno' ulioimbwa na Tego.
Aidha Tego, alisema kundi lao linaendelea kuzitambulisha nyimbo zao mpya na zile za albamu zao zilizopita katika maonyesho yao, ambapo kila Ijumaa huwa kwenye ukumbi wa Kiburugwa Inn, Mbagala na Jumamosi ufanya makamuzi yao Bashnet Hall, Mtoni Mtongani, jijini Dar es Salaam.

Mwisho

Katundu ana Nadhiri ya Mapenzi Msondo






MTUNZI na muimbaji mahiri wa bendi ya Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki', Juma Katundu ameibuka na kibao kipya kiitwacho 'Nadhiri ya Mapenzi', ambacho kimekamilisha idadi ya nyimbo sita za albamu mpya ya bendi hiyo inayoandaliwa kwa sasa.
Akizungumza na MICHARAZO, Shaaban Dede 'Mzee wa Loliondo', alisema Msondo imeongeza nyimbo mbili mpya ambazo zinakamilisha idadi ya nyimbo za albamu yao ijayo, kikiwemo kibao chake kiitwacho 'Suluhu' na hicho cha Katundu ambacho kinaendelea kufanyiwa mazoezi.
Dede, alisema kibao chake kingine kinachokemea Dawa za Kulevya, nacho kipo tayari isipokuwa hana hakika kama kitakuwa kwenye albamu hiyo ijayo ya Msondo Ngoma, moja ya bendi kongwe ya muziki wa dansi nchini.
"Kwa kifupi ni kwamba Msondo imekamilisha nyimbo nyingine mbili mpya, moja ukiwa ni wangu uitwao 'Suluhu' na kingine kimetungwa na Juma Katundu, kinaitwa 'Nadhiri ya Mapenzi'," alisema.
Dede, aliyetua hivi karibuni katika bendi hiyo akitokea Mlimani Park 'Sikinde' alisema pamoja na kukamilika kwa nyimbo hizo sita za albamu yao ijayo, bado wanamuziki wa bendi hiyo wanaendelea kutunga vibao vingine vinavyoendelea kufanyiwa mazoezi ili vipigwe ukumbini.
"Wanamuziki tunaendelea kutunga nyimbo nyingine kwa ajili ya kudhihirisha kuwa Msondo ni Baba ya Muziki kutokana na kuundwa na wanamuziki wanaojua majukumu yao, vibao hivyo vitakuwa vikipigwa kwenye maonyesho yetu ya ndani na nje ya jijini la Dar," alisema Dede.
Msondo, iliyokuwa na desturi ya kufyatua albamu mpya kila mwaka, kwa mwaka uliopita ilishindwa kufanya hivyo kwa kile kilichoelezwa na meneja wake, Said Kibiriti, maelekezo ya wasambazaji wa kazi zao waliotaka watoe nafasi kwa albamu yao ya 'Huna Shukrani' ifanye vema sokoni.
Albamu zilizofuatana pamoja kwa miaka karibu 10 mfululizo ni 'Cheusi Mangala', 'Demokrasi ya Mapenzi', 'Ndoa Ndoana', 'Kilio cha Mtu Mzima', 'Piga Ua Talaka Utatoa', 'Kaza Moyo', 'Ajali', 'Kicheko kwa Jirani' na 'Huna Shukrani' inayoendelea kutamba iliyoachiwa mwaka juzi.

Mwalubadu: Kujituma kumenipa tuzo 2010







ANAFAHAMIKA zaidi kama 'Mwalubadu', ingawa jina lake halisi ni Athuman Mussa Masangula, mmoja wa wachekeshaji mahiri nchini ambaye kipaji chake kilianza kuonekana tangu akiwa darasa la nne katika Shule ya Msingi Mgulani, jijini Dar es Salaam.
Mwalubadu alisema alianza kushiriki maigizo shuleni kwa kuigiza sauti za walimu wake na baadhi ya viongozi maarufu, huku akishiriki pia katika uchezaji ngoma na michezo mbalimbali.
Alikiendeleza kipaji chake hata alipokuwa Shule ya Sekondari Mzalendo, iliyopo Moshi, Kilimanjaro ambapo alikuwa akikodishwa kwa ajili ya kunogesha sherehe mbalimbali za harusi na kipaimara na kuzidi kupata umaarufu zaidi hadi alipomaliza masomo yake na kurejea Dar.
Alijiendeleza kielimu kwa kusomea masomo ya IT ngazi ya cheti pale Chuo Kikuu Mlimani, kitengo cha Kompyuta, huku akijishughulisha na masuala ya sanaa kupitia kundi la Katavi lililowahi kutamba na michezo ya kuigiza kiup[itia kituo cha ITV.
Baadhi ya michezo aliyoshiriki akiwa na kundi hilo yaliyomtambulisha kwa mashabiki ni 'Jabali', 'Miale' na 'Tunduni' kabla ya kuangukia kwenye filamu akiigiza 'Copy' mwaka 2007 na kufuatiwa na nyingine zikiwemo za vichekesho zilizomjengea jina kubwa nchini.
Mwalubadu ambaye kwa sasa ni mtangazaji wa kituo cha Radio cha Ebony FM iliyopo, Iringa, alisema alijikuta akipenda sanaa ya uigizaji na hasa vichekesho kwa kuvutiwa na Steve Urkel, aliyetamba na 'Family Matters' na Brian Deacon, aliyeigiza filamu kadhaa ya Yesu.
Alisema kujibidiisha na kujifunza kwa waliomtangulia kwenye fani ndiko kulikomfanya anyakue tuzo ya Mchekeshaji Bora wa mwaka 2010, kupitia mtandao wa Filamu Central.
Mkali huyo anayependa kucheza soka, muziki na kuangalia filamu za vichekesho, alisema pamoja na mafanikio aliyoyapata kwenye fani hiyo, bado hajaridhika na anajibidiisha zaidi ili zweze kuwa msanii wa kimataifa, akimiliki kampuni yake mwenyewe sambamba na kujiendeleza kielimu.
Baadhi ya kazi za filamu alizoshiriki na kumjengea jina kubwa katika fani hiyo nchini ni pamoja na 'Sheria', 'Lango la Jiji', 'Inye' na 'Kaka Ben' za vichekesho, huku filamu za kawaida ni 'The Strangers', 'Swahiba', 'Solomba' na nyinginezo.
Mbali na kuchekesha, Mwalubadu pia ni mtunzi na mwandishi wa filamu hizo, moja ya kazi yake binafsi ni 'King Mwalubadu'.
Mkali huyo aliyezaliwa Januari 10, miaka kadhaa iliyopita akiwa mtoto wa tatu wa familia ya Mzee Mussa Masangula, alisema hakuna jambo la furaha kwake kama siku alipoanza kutangaza katika kituo cha Ebony Fm, huku tukio la huzuni ni kufiwa na baba yake mzazi, kitu alichodai akisahau.

Mwisho

Jahazi, Manchester Musica kuonyeshana kazi 'Usiku wa Naksh'

ONYESHO la 'Usiku wa Naksh Naksh wa Mwambao na Mastaa wa Muziki na Filamu', litakuwa ni pambano lisilo rasmi la kundi la Jahazi Modern Taarab na bendi ya Manchester Musica.
Kwa mujibu wa mraribu wa onyesho hilo litakalofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Travertine, Abdallah Mensah, makundi hayo mawili yataonyeshana umwamba mbele ya mashabiki watakoenda kulishuhudia.
Mensah, alisema tayari makundi hayo yameshaanza kutoleana tambo juu ya kufunikana siku ya onyesho hilo, ambalo litahusisha mastaa wengine kibao wa muziki akiwemo Prince Mwinjuma Muumin, aliyepo Africana Stars 'Twanga Pepeta'.
"Japo ni onyesho la kutoa burudani kwa kushirikisha wasanii mbalimbali nyota wa muziki na filamu, lakini ni kama mpambano wa Jahazi Modern Taarab na Manchester Musica, moja ya bendi zinazokuja juu kwa sasa nchini kwenye muziki wa dansi," alisema Mensah.
Wengine watakaopamba onyesho hilo litakalofanyika Mei 8 ni pamoja na Malkia wa Mipasho nchini, Khadija Kopa, Mwanaidi Shaaban, Hassani Ally, Maua Tego, Thabit Abdul na kundi la Kanga Moja 'Ndembendembe.'
Pia wasanii wa kundi la TMK Wanaume Family, Said Fella, Said Chegge pamoja na wakali wa filamu ambao bado wameweka kapuni kwa sasa nao watajumuika pamoja kuwapa wakazi wa jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake burudani ya aina yake kwa wakati mmoja.
"Unaweza kuona mchanganyiko uliopo siku ya onyesho hilo, utakavyoweza kuwapa burudani zaidi ya moja kwa wakati mmoja, maana mbali ya taarab na dansi, pia wasanii mbalimbali wa filamu na muziki wa kizazi kipya watakuwepo kutoa burudani kabambe," alisema Mensah.
Mensah, alisema kwa sasa anahaha kusaka wadhamini wa onyesho hilo, ili kulizidishia manjonjo kabla ya kufanyika kwake.

Mwisho

Madee kudondosha nyingine



MSANII mahiri wa muziki wa kizazi kipya nchini, Hamad Ally 'Madee', anatarajia kuachia hewani ngoma nyingine mpya baada ya wiki mbili zilizopita 'kudondosha' audio na video ya kibao kipya cha 'Napeleka Benki'.
Ingawa Madee hakuweza kuweka bayana kibao kipi kitakachofuata baada ya 'Napeleka Benki', lakini alisema wiki ijayo ataachia kazi nyingine mpya wakati akiendelea na maandalizi ya kupakua albamu yake mpya na ya nne.
Kiongozi huyo wa kundi la Tip Top Connection, alisema moja kati ya nyimbo zake saba alizokamilisha itaachiwa kuzidi kuitambulisha albamu hiyo mpya itakayokuwa na nyimbo nane.
"Natarajia kuachia wimbo mwingine mpya baada ya 'Napeleka Benki', sijui itakuwa ipi kati ya 'Nisikilize', 'Siku ya Mwisho', 'Mtasubiri', 'Pendo', 'Hifla', 'Amka' au 'Siri Zote Ninazo Mimi'," alisema Madee.
Madee alisema nyimbo zote za albamu hiyo ya nne tangu alipoingia kwenye fani ya muziki zimerekodiwa katika studio mbili tofauti za MJ Production na Bongo Records chini ya watayarishaji Makochali, Master J na P Funk.
Ingawa bado hajaipa jina albamu yake ijayo iitwe vipi, lakini hiyo itakuwa ni albamu ya nne kwa Madee baada ya awali kutamba na 'Kazi ya Mola', 'Hip Hop Haiuzi' na 'Pesa'.Msanii huyo aliyesherehekea siku yake ya kuzaliwa mwanzoni mwa wiki hii, aliwahi kutangaza kutaka kustaafu muziki, ili apumzike na kujiendeleza kimasomo, lakini kwa ushauri wa watu wake wa karibu pamoja na mashabiki wa muziki aliamua kufuta wazo hilo lililokuwa alifanye mwaka juzi.

Ray kumbe ni 'Handsome wa Kijiji'

WAKATI filamu yake ya 'Second Wife' ikiendelea kutesa mitaani kwa sasa, msanii mkali wa filamu nchini, Vincent Kigosi 'Ray' amekamilisha kazi yake nyingine mpya iitwayo 'Handsome wa Kijiji', ambayo kwa mara ya kwanza ameigiza kama mtu dhalili aishie kijijini tofauti na alivyozoeleka.
Filamu hiyo iliyokamilika wiki iliyopita imerekodiwa maeneo ya Bagamoyo, mkoani Pwani, baada ya ushauri wa mashabiki wake waliodai wamechoshwa kila mara kumuoa akiigiza kama mtu tajiri anayeishia kifahari mjini, na hivyo kumlazimisha kutekeleza wazo hilo na kwenda 'bush'.
Kazi hiyo mpya ambayo imewashirikisha wakali kadhaa wa fani hiyo nchini kama Ben Blanco, Mzee Magali, Tash, Hashim Kambi, Irene Paul na wengine ipo kwenye uhariri tayari kupelekewa sokoni.
Katima ujumbe kwa mashabiki wake, Ray, amewataka amewataka wadau wa filamu kukaa mkao wa kula kushuhudia picha ya aina yake ambayo, ndani yake ameigiza kwa jina la Hamza.
"Wadau wa kiwanda cha filamu Tanzania napenda kuwafahamisha kuwa filamu yenu mpya ya kipekee na yenye manjonjo mengi sasa yakamilika," sehemu ya ujumbe wa Ray kupitia mtandao wake unasomeka hivyo.
Pia unaongeza; Nawashukuru sana kwa kuweza kufuatilia mchakato mzima wa sinema yenu ya Handsome wa Kijiji subirini sana wadau mzigo huu maana kampuni ya Rj Company imekuja tofauti kabisa na watu walivyozoea."
Filamu hiyo ni ya tatu kwa Ray ndani ya mwaka huu, baada ya awali kuachia 'Family Disaster' na kisha 'Second Wife' iliyopo sokoni kwa sasa ikiendelea kufanya vema kati ya kazi zilizotoka mwezi uliopita.