STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, July 14, 2011

Banka yu tayari wa lolote Simba



KIUNGO nyota wa timu ya Simba na timu ya taifa, Taifa Stars, Mohammed Banka, amesema ingawa hajapata taarifa rasmi ya kutemwa ndani ya kikosi hicho, lakini yupo tayari kwa lolote mradi alipwe chake kwa kuvunjwa mkataba alionao na klabu hiyo.
Aidha amedai kusikitishwa na lawama anazotupiwa kwa kushindwa kung'ara kwenye pambano la fainali za Kombe la Kagame dhidi yao na Yanga, wakati ilifahamika kuwa ametoka majeruhi kitu ambacho hata kocha Moses Basena alikuwa akifahamu.
Akizungumza na MICHARAZO mapema leo, Banka alisema hana taarifa za kuachwa na Simba kama baadhi ya vyombo vya habari vilivyoripoti jana, lakini kama jambo hilo ni kweli hana jinsi zaidi ya kukubaliana na mapendekezo ya viongozi wake.
Banka alisema kitu cha msingi ni klabu ya Simba imlipe chake kwa kuvunja mkataba wao, ili akatafute maisha pengine, ingawa alisema amesikitishwa na kushutumiwa kwa kuwa miongoni mwa walioikosesha Simba taji la saba la michuano ya Kagame.
"Kwa kweli sijapewa taarifa yoyote rasmi zaidi ya kusoma kwenye vyomvo vya habari, lakini kama uongozi umeazimia hivyo, sitakuwa na jinsi zaidi ya kusubiri kulipwa changu kwa kuvunjwa mkataba nitafute mahali pa kwenda," alisema.
Aliongeza, kucheza kwake chini ya kiwango katika mechi ya Simba na Yanga katika fainali za Kagame ilitokana na kutoka kuwa majeruhi, kitu ambacho hata mwenyewe alishtuka alipoagizwa na kocha Basena kuingia dimbani.
"Kocha aliniambia kabla ya mechi atanichezesha kipindi cha pili ili kuangalia maendeleo yangu ya kupona majeraha, hivyo alivyoniambia niingie nilishangaa, lakini kama mchezaji ninayezingatia nidhamu sikuweza kumbishia, ila Simba wasinielewe vibaya," alisema Banka.
Kiungo huyo alisema anaamini mchango wake ndani ya Simba ni mkubwa kuliko lawama anazopewa sasa, lakini kwa kuwa soka ndivyo lilivyo anajiandaa kutafuta maisha mahali pengine kwa kuamini 'riziki' yake imeisha ndani ya klabu hiyo.
Banka, pamoja na Mussa Hassani Mgosi na Athumani Idd 'Chuji' walitajwa kuwa miongoni mwa waliopendekezwa kutemwa ndani ya Simba kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa kutokana na kuonyesha kiwango duni kwenye Kombe la Kagame, ambapo Simba ilifungwa na Yanga bao 1-0.

Mwisho

Bujibu kuchapana na Mtambo wa Gongo


WAKATI michuano ya Ligi ya Kick Boxing iliyotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu ikiahirishwa hadi Desemba, mabondia wakongwe wa ngumi za kulipwa nchini, Maneno Osward na Ernest Bujiku wanatarajiwa kupamba ulingoni kupigana.
Maneno Osward maarufu kama Mtambo wa Gongo atapigana na Bujiku katika moja ya mapambano ya ngumi yatakayoshindikiza pambano la Kick Boxing kati ya Amour Zungu wa Zanzibar dhidi ya Mchumia Tumbo litakalofanyika Julai 30 kwenye ukumbi wa DDC Keko, Dar es Salaam.
Kaseba alisema, mbalio na pambano la Osward na Bujiku siku hiyo pia mabondia wa kike, Jamhuri Said wa Tanzania atapimana ubavu na Rukia Kaselete wa Kenya katika pambano jingine la Kick Boxing.
Alisema michezo mingine itakayosindikiza mipambano hiyo ni kati ya Fadhila dhidi Demu wa Kisarawe, Dragon Kaizum atakayepigana na Faza Boy, Idd dhidi ya Dragon Boy, Lion Heart dhidi ya Begeje na michezo mingine ya ngumi za kulipwa.
Kaseba alisema michezo hiyo inafanyika ili kuwapa burudani wakazi wa Dar es Salaam ambao walikuwa wakijiandaa kushuhudia ligi ya Kick Boxing ambayo imeahirishwa hadi Desemba kwa ajili ya kufanya maandalizi ya kutosha.
"Tumeamua kuahirisha ligi ya Kick Boxing hadi Desemba kutoa muda kwa mabondia kujiandaa na kufanya katika kiwango cha kimataifa, hivyo ili kutowanyima raha wadau wa mchezo huo tumeandaa michezo kadhaa ya Kick Boxing na ngumi za kulipwa siku ya Julai 30 itakayofanyika kwenye ukumbi wa DDC Keko," alisema Kaseba.
Alisema Bujiku na Osward kila mmoja kwa sasa yupo katika maandalizi makali ya kuonyeshana umwamba wakikumbushia enzi zao wakitamba kwenye mchezo huo.

Mwisho

Waajiri wapigwa msasa kuishi na wafanyakazi wa majumbani



WAAJIRI wa wafanyakazi wa ndani watakiwa kutowabagua na kuwanyanyasa watumishi wao wa ndani na badala yake kuishi nao kwa wema kutokana na ukweli wao ni watu wa karibu na wasiri wakubwa wa familia zao.
Wito huo umetolewa kwenye semina ya siku moja iliyoandaliwa na Asasi ya kiraia ya KIWOHEDE kwa lengo la kujenga mauhusiano mema baina ya waajiri na watumishi wa kazi za ndani ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakichukuliwa kama vijakazi.
Mgeni rasmi wa semina hiyo, Sheikh Shughuli Sheikh, ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Malapa Kata ya Buguruni na Mwezeshaji wa semina hiyo Edda Kawala, walisema kuna umuhimu wa waajiri kuwaona wafanyakazi wa majumbani kama sehemu ya familia zao.
Sheikh, alisema kutokana na mchango na umuhimu wa wafanyakazi wa ndani ambao ni tegemeo la waajiri katika kusaidiwa kazi za nyumbani ni vema watumishi hao wakapewa heshima na kuthaminiwa kama wanafamilia.
"Wao ndio wanaowapikieni, kuwafulieni na kazi nyingine za ndani, hivyo ni wasiri na watu muhimu katika familia zenu hivyo ni vema kukaa nao kwa wema mkiwajali na kuwathamini tofauti na baadhi yenu mnavyowafanyia," alisema Sheikh.
Naye Mwezeshaji alisema lengo la semina hiyo ni kuona waajiri na wafanyakazi hao wa ndani wanakuwa na mauhisiano mema, pamoja na kila mmoja kuhakikisha wanakuwa na mikataba au makubaliano yanayolinda haki na hadhi ya kila mmoja.
Alisema KIWOHEDE, imebaini zipo baadhi ya nyumba au waajiri wamekuwa wakiwabagua watumishi wao na kuwanyima haki zao stahiki na kuchangia kuwepo kwa uhasama na kuifanya kazi hiyo kudharaulika mbele ya jamii.
Washiriki wa semina hiyo wengi wao wakiwa ni akinamama, walisema kuna mambo mengine hawakuwa wanayajua juu ya haki za msingi za watumishi hao na semina hiyo imewafungua macho na kuahidi kuwa 'mabalozi' mema warejeapo makwao.
Semina hiyo ilielekeza umri stahiki wa wafanyakazi wanaopaswa kuajiriwa kwa kazi za majumbani, haki za msingi stahiki za watumishi hao na namna ya uwajibikaji wa kila mmoja kati ya waajiri na wafanyakazi hao.

Mwisho

Tanzania yapongezwa kuridhia mkataba wa ILO


SERIKALI ya Tanzania imepongezwa kwa kuwa miongoni mwa nchi zilizopitisha Mkataba wa Kimataifa wa Kutambuliwa kwa Wafanyakazi wa Majumbani, iliuyopitishwa kwenye Mkutano wa 100 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Kadhalika Rais Jakaya Kikwete amepongezwa kwa hutuba aliyoisoma kwenye mkutano huo juu ya serikali ya Tanzania kuwatambua wafanyakazi hao kama watumishi halali wanaoostahiki hakio zote wa waajiriwa, akiombwa kuhakikisha utekezaji unafanyika.
Mratibu wa Shirika la Wafanyakazi wa Majumbani Kanda ya Afrika (IUF), Vick Kanyoka, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam alieleza maazimio ya mkutano wa ILO uliofanyika mwezi uliopita mjini Geneva, Uswisi.
Kanyoka, alisema kitendo cha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zilizopigia kura ya kupitisha mkataba huo wa 189 wa kuwatambua wafanyakazi wa majumbani ni ushindi kwa wafanyakazi wote ambao kabla ya hapo walikuwa wakichukuliwa kama watumwa.
Aliongeza IUF, inaipongeza Tanzania na Rais Jakaya Kikwete aliyehutubia kwenye mkutano huo Juni 15 mwaka huu na kuiomba serikali hiyo itekeleze kwa vitendo mkataba huo ili wafanyakazi wa majumbani kupata haki na kuthaminiwa kama wafanyakazi wengine.
Alisema ingawa sheria ya kuwalinda na kuwatetea wafanyakazi majumbani ipo, lakin i utekelezaji wake umekuwa ni tatizo na ndio maana IUF inaiomba Tanzania kuhakikisha jambo hilo linapata ufanisi ili kuleta usawa miongoni mwa watumishi hao.
"IUF tunaipongeza Tanzania na Rais wake kwa kuridhika kupitishwa kwa mkataba wa 189 wa kutambulika kwa wafanyakazi wa majumbani, uliopitioshwa Juni 16 mwaka huu ambapo ulipitishwa kwa kura 396, huku 16 zikiukataa miongoni mwa mataifa yaliyoukataa likiwa ni Uingereza," alisema Kanyoka.
Mratibu huyo alisema ni kutekelezwa kwa vitendo kwa mkataba huo kutatoa fursa ya waajiri kuwathamini na kuwajali watumishi hao kwa kuingia nao mkataba na kuwalipa haki zao stahiki kma ilivyo kwa watumishi wengine.
Alisisitiza ni muhimu wafanyakazi hao kusaidia kufanikisha uitekelezaji huo kwa kuwa wa kwanza kuhakikisha wanaingia mikataba na makubalino na waajiri wao kabla ya kuanza kazi ili watakapofanyiwa kinyume iwe rahisi kutetewa na kupata haki zao.

Mwisho

Saturday, July 9, 2011

Ligi ya Kick Boxing yaiva

MICHUANO ya Ligi ya Kick Boxing inatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu jijini Dar es Salaam kwa mabondia wa kike na wa kiume kuumana kuwania ushiriki wa fainali za taifa zitakazofanyika baadaye mwaka huu.
Kwa mujibu wa mratibu wa michuano hiyo, Japhet Kaseba, alisema michuano hiyo itafanyika Julai 31 kwenye ukumbi wa DDC Mlimani, Mwenge jijini Dar es Salaam.
Kaseba, alisema kabla ya kufanyika kwa michuano hiyo anatarajiwa kukutana na mabondia washiriki kwa lengo la kuwapa darasa dhidi ya mchezo huo ambao safari hii utashirikisha wakongwe na chipukizi ikiwa ni mikakati ya kuendeleza mchezo huo.
"Michuano yetu ya ligi ya Kick Boxing itafanyika mwishoni mwa mwezi huu kwenye ukumbi wa DDC Mlimani, ambapo mabondia mbalimbali wake wa waume chipukizi na wakongwe wataonyesha kazi safari hii," alisema.
Kaseba alisema kwa sasa anaendelea na mipango ya kusaka wadhamini kwa ajili yua kulipiga tafu shindano lao ambalo limekuwa kikifanyika kwa mwaka wa tatu sasa katika njia ya kurejesha msisimko wa michuano hiyo iliyompa mataji ya Afrika na Dunia.
Katika hatua nyingine bingwa wa Kick Boxing wa Uganda, Moses Golola, alifanikiwa kumchakaza bondia toka Sudan, Abdul Quadir Rahim mwishoni mwa wiki jijini Kampala, akisisitiza ana hasira ya kutaka kupigana na Kanda Kabongo wa Tanzania.
Golola aliyepigwa na Kabongo katika pambano la kuwania ubingwa wa Afrika, alisema ushindi wake wa KO ya raundi ya pili dhidi ya Msudan ni salamu kwa Kabongo kuwa ajiandae kwa ajili ya kisasi siku wakikutana ambapo huenda ikawa ndani ya mwaka huu.

Klabu za ngumi kupepetana Ilala

KLABU za ngumi za ridhaa za Amana na Matimbwa ni miongoni mwa klabu zaidi ya tano zinazotarajiwa kuonyeshana kazi katika mfululizo wa michuano maalum ya mchezo huo inayoendelea wilayani Ilala jijini Dar es Salaam.
Klabu zingine zitakazopambana katika michezo itakayofanyika mwishoni mwa wiki hii ikiratibiwa na taasisi ya Kinyogoli Foundation ni Ashanti, Big Right na zingine ambazo hazikuweza kufahamika mapema.
Mratibu wa michuano hiyo, Rajab Mhamila 'Super D' alisema michezo hio itafanyika Jumamosi kwenye ukumbi wa Panandipanandi, Ilala Bungoni.
Super D, alisema maandalizi ya michezo hiyo yamekamilika ikiwemo vikosi vya timu zote kuendelea kujifua.
Aliwataja baadhi ya mabondia watakaoziwakilisha klabu zao kuwa ni Ibrahim Class, Khalfan Othman, Kassim Sambo na Saidi Ally kwa upande wa Amana, wakati Matimbwa itawakilishwa na Mohamed Matimbwa, Mohamed Muhani, Edson Joviki na Mohamed Kumbilambali.
Kwa upande wa Ashanti, Super D alisema itawakilishwa na mabondia kama Uwesu Manyota, Ramadhani Kimangale, Mark Edson na wengine na mipambano yao itachezwa kwa raundi nne nne kila mmoja.
Aliongeza kwa kutoa wito kwa wadau wa ngumi kujitokeza kuzisaidia klabu shiriki na mabondia vifaa vya michezo na mahitaji yao mengine ili kuwatia moyo wa kuupenda mchezo huo.

Wednesday, June 29, 2011

Hapa na pale za Micharazo



Villa Squad yaangukia wadau

UONGOZI mpya wa klabu ya soka ya Villa Squad, umekiri una kazi ngumu katika kuiongoza klabu hiyo kutokana na hali mbaya kiuchumi iliyonayo na kuwaangukia wadau wa soka wa wilaya ya Kinondoni kujitokeza kuisaidia kwa hali na mali.
Villa iliyorejea Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kushuka daraja mwaka 2008, ilipata viongozi wake mwishoni mwa wiki katika uchaguzi mkuu uliohusisha nafasi za makamu mwenyekiti na wajumbe wa kamati ya utendaji tu.
Makamu Mwenyekiti, Ramadhani Uledi, alisema kwa jinsi hali ilivyo mbaya kiuchumi katika klabu hiyo wanalazimika kuwaomba viongozi, wanasiasa na wakazi wa wilaya yao kuisaidia kwa hali na mali klabu yao ili kuhimili vishindo vya ligi hiyo wasirudie makosa ya mwaka 2008.
Uledi, alisema Villa kwa sasa ni kama 'jicho' kwa wakazi wa Kinondoni kutokana na kuwa timu pekee kushiriki Ligi Kuu baada ya awali kuteremka daraja na hivyo ipewe sapoti ikisaidiwa ili irudi 'mchangani'.
"Pamoja na kuwashukuru wanachama kutuchagua kuiongoza Villa, tulikuwa tunaomba tupewe sapoti ya kutosha kwa wadau wa soka na wakazi wa Kinondoni kuiunga mkono kwa kuisaidia kwa hali na mali ili imudu mikikimikiki ya ligi kuu na tusirejee makosa ya 2008 tuliposhuka daraja," alisema Uledi.
Aliongeza uongozi wao ulitarajiwa kupanga siku ya kukutana kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali pamoja na kuteua kamati za kuusaidia uongozi wao katika maandalizi ya ushiriki wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao inayotarajiwa kuanza Agosti 20 mwaka huu.
***

Yanga waituliza Ruvu Shooting


BAADA ya Ruvu Shooting kuitemea cheche Yanga kwa kumchukua beki wao Oscar Joshua bila kufuata taratibu, uongozi wa Yanga umewatuliza ukisema watamalizana nao tu.
Yanga imeipoza Ruvu kwa kusema isubiri mapesa ya mchezaji huyo kwani hata wao wanajua kuwa ametokea kwao.
Msemaji wa Yanga Louis Sendeu amesema, uongozi wao unafahamu kuwa Joshua hajaokotwa jalalani ila kuna timu ametoka, hivyo haiwezi kumsajili bila kufuata taratibu.
"Hili ni suala la muda tu, sisi tutakutana na viongozi wa Ruvu Shooting na tutamalizana tu, hala hakuna tatizo," alisema Sendeu.
Yanga imeamua kupoza makali hayo, baada ya Ruvu kuwa mbogo na kusema kuwa itapinga sehemu yoyote yule mchezaji wao huyo kwenda Yanga kwa sababu hawakumchukua kihalali.
Viongozi wa Ruvu waliripotiwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari, walisema kuwa mchezaji huyo ana mkataba na timu yao.
Kabla hata Yanga haijamalizana na Ruvu, tayari mchezaji huyo ameanza kuitumikia timu hiyo kwenye michuano ya Kagame.
Mchezaji huyo mwenye uwezo wa kucheza beki na kiungo amejiunga na Yanga akitokea Ruvu Shooting ambako nako alichukuliwa kutoka Toto African ya Mwanza.
***

Mcuba kuwasaka 10 Bora ngumi taifa


MABONDIA wa timu ya taifa ya ngumi waliopo kambi ya mazoezi jijini Dar es Salaam wanatarajiwa kuchuana wenyewe kwa wenyewe ili kuchujwa na kupatikana mabondia 10 watakaoiwakilisha nchi kwenye michuano ya 'All African Games'.
Michuano hiyo ya Afrika inatarajiwa kufanyika kati ya Septemba 3-18 mjini Maputo Msumbiji.
Mchujo wa mabondia wa Tanzania unatarajiwa kufanywa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mcuba Pimintel Hutardo ambaye anatarajia kuwashindanisha wachezaji wake kusaka wakali 10.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania, BFT, Makore Mashaga, alisema kocha Hutardo atawachuja mabondia hao katika michezo itakayofanyika kwenye kumbi mbalimbali za jijini Dar es Salaam ukihusisha mapambano 20.
Mashanga alisema baada ya mchujo huo mabondia 10 watakaosalia wataendelea kujifua pamoja na kwenda kucheza mechi za majaribio katika nchi kadhaa ambazo Tanzania imapata mialiko na kuzitaja ku ni pamoja na England, India, Scotland na Mauritius.
Katibu huyo alisema sababu ya kocha kuendesha zoezi hilo la mchujo kwa kushindanisha mabondia hao wenyewe ni kupata wachezaji wenye uwezo wa kuisaidia Tanzania kwenye michuano hiyo ya Afrika ambayo inatarajiwa kushirikisha karibu nchi 55.
***

Kinondoni yaapa Pool Taifa


MABINGWA watetezi wa michuano ya taifa ya Pool ya 'Safari Lager National Pool Championship 2011' yaliyoanza kutimua vumbi Juni 30, wametamba kutetea vema ubingwa huo waliouchukuwa mwaka jana mkoani Arusha.
Katibu mkuu wa chama cha pool cha Kinondoni (KIPA), Zaharo Ligalu aliwaambia makatibu wakuu juzi wa klabu 10 zitakazoshiriki mashindano hayo kuwa wamejipanga vema kuhakikisha hawapotezi ubingwa huo.
Ligalu aliyasema hayo wakati wa upangaji wa ratiba ya mashindano hayo kwenye ukumbi wa Meeda Club uliopo Sinza Jijini Dar es salaam.
Alisema kuwa licha ya ushindani mkubwa ambao wanategemea kuupata kutoka kwa mikoa mingine lakini hakuna sababu ya kuchukuwa tena ubingwa huo kutokana na Kinondoni kusheheni vipaji vya wachezaji wa mchezo huo.
"Makatibu wenzangu wa klabu naomba niwambie kuwa tumejipanga kuhakikisha ubingwa unarudi tena Kinondoni, hivyo endeleeni kuwaandaa wachezaji wenu vizuri ambao nina imani ndiyo watakaosaidia Kinondoni kutetea vema ubingwa wetu,"alisema Ligalu.
Alisema kuwa kikubwa ambacho kitafanikisha kutetea ubingwa huo ni ushirikiano wa pamoja wa wadau wote wa mchezo huo wa Kinondoni.
Klabu zinazoshiriki mashindano hayo ngazi ya mikoa kwa upande wa Kinondoni ni Shoko, Topland, Meeda, 4 wayz, Madrid, Mkwajuni, Ubungo Terminal, Jaba, Bahama mama na Mlalakuwa.
Fainali za taifa ambazo Kinondoni itatetea taji lake zitafanyikia kwenye ukumbi wa Kilimani mkoani Dodoma.

===========
Akudo, Mapacha Wa3 uso kwa uso


BENDI za muziki wa dansi za Akudo Impact na Mapacha Watatu, zinatarajia kufanya onyesho la pamoja linalolenga kudumisha urafiki baina ya wanamuziki wa bendi hizo mbili.
Mratibu wa onyesho hilo, Mkurugenzi wa kampuni ya Biggy One Entertainment, Abubakar Mwanamboka, alisema bendi hizo zitaonyeshana kazi kesho kwenye ukumbi wa Vatican, Dar.
"Lengo letu ni kutaka kuonyesha kwamba bendi za muziki wa dansi zinaweza kushirikiana na kuondoa mawazo yaliyojengeka miongoni mwa baadhi ya watu kuwa wanamuziki wa bendi mbili hawawezi kushirikiana," alisema.
Alisema, majigambo kati ya bendi moja na nyingine siyo ugomvi bali ni njia ya kuvuta mashabiki na kwamba kampuni yake imeandaa onyesho hilo ili kudhihirisha kuwa wanamuziki wanaweza kushirikiana katika kazi yao.
Mratibu huyo alisema, mbali na bendi hizo mbili kutoa burudani kwenye onyesho hilo, piaatakuwepo msanii wa muziki wa kizazi kipya H. Baba ambaye naye atafanya vitu vyake.
Aliongeza onyesho hilo la Akudo na Mapacha ni la kwanza kuratibiwa na kampuni yake.
Akudo Impact imekuwa ikitamba na albamu ya kwanza ya 'Impact' wakati Mapacha Watatu nayo ikitamba na albamu ya kwanza ya 'Jasho la Mtu' na sasa bendi hizo kila moja iko kwenye maandalizi ya albamu ya pili.


Mwisho

Sunday, June 26, 2011

MCHANYATO WA MICHARAZO

Tisa wamwagwa Mtibwa Sugar

KLABU ya soka ya Mtibwa Sugar, imetangaza kuwatema wachezaji wake 9 akiwemo mkongwe Faustine Lukoo na kipa Soud Slim waliomaliza mkataba wa kuichezea klabu hiyo.
Kwa mujibu wa Msemaji wa klabu hiyo, Thobias Kifaru, baadhi ya wachezaji wengine waliopewa mkono wa kwaheri katika mashamba ya Manungu, Morogoro ni winga Julius Mrope aliyeenda Yanga na Obadia Mungusa aliyesajiliwa na Simba.
Kifaru, aliwataja wachezaji wengine ni Yusuph Mgwao, Yona Ndabila anayeenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, Mganda Boban Zilintusa waliyeshindwa kumtumia kwa kukosa ITC, ambaye walimsajili na kushindwa kumtumia kwa kukosa ITC, na Lameck Dayton.
"Tumeacha jumla ya wachezaji tisa, akiwemo mkongwe Faustine Lukoo baada ya kumaliza mikataba ya kuitumikia klabu yetu na wengine kuhamia klabu zingine za Ligi Kuu, ila Ndabila aliyekuwa na mkataba aliomba kusitisha kwa vile anataka kwenda kucheza soka nje," alisema.
Hata hivyo Kifaru hakuweka bayana juu ya wachezaji Salum Machaku na kipa Shaaban Kado ambao wametajwa kutua kwa watani wa jadi wa soka la Tanzania, Simba na Yanga kwa msimu ujao wa ligi kuu.
Machaku anayeichezea pia timu ya taifa, Taifa Stars imedaiwa amesajiliwa Simba na Kado anayechezea timu za vijana U20 na ile ya wakubwa tayari imethibitishwa amenyakuliwa na Yanga kwa ajili ya msimu ujao utakaoanza Agosti 20 mwaka huu.
***

Fainali Pool Taifa zaiva


FAINALI za taifa za mchezo wa pool za 'Safari Lager National Pool Champioship 2011' zinatarajia kuanza mwezi ujao.
Kwa mujibu wa Meneja wa bia ya Safari Lager, Oscar Shelukindo, fainali hizo zitafanyika kati ya Julai 27-30 kwenye ukumbi wa Kilimani mkoani Dodoma.
Shelukindo alisema, fainali hizo zitatanguliwa na mashindano ya ngazi za mikoa yatakayoanza Juni 30 hadi Julai 17, ikishirikisha mikoa 14 ya Tanzania Bara.
Alisema mara baada ya mashindano hayo kukamilika katika ngazi za mikoa kila mkoa utaunda kombaini ya wachezaji kwa ajili ya kuwakilisha kila mkoa katika ngazi ya fainali hizo za taifa.
Shelukindo alisema bingwa wa fainali hizo atanyakulia Sh.mil. 5, mshindi wa pili ataondoka na mil. 3, mshindi wa tatu Mil. 2 na mshindi wa nne Mil 1.
Aliongeza fainali hizo ambazo zitahusisha na wachezaji mmoja mmoja wanaume na wanawake, bingwa kwa upande wa wanaume atazawadiwa Sh.Sh.500,000, mshindi wa pili Sh.250,000, mshindi wa tatu Sh.200,000 na mshindi wa nne Sh.100,000
Kwa upande wa wanawake bingwa atapewa Sh.350,000, mshindi wa pili Sh.200,000, mshindi wa tatu Sh.150,000 na mshindi wa nne Sh.50,000.
Aliongeza kwa kuzitaja zawadi kwa upande wa ngazi ya mikoa kuwa bingwa atajinyakulia Sh. 700,000, mshindi wa pili ataondoka na Sh.350,000, mshindi wa tatu atazawadiwa Sh.200,000 na mshindi wa nne Sh150,000.
Kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja ngazi ya mikoa (wanaume) bingwa atajinyakulia Sh.350,000, mshindi wa pili Sh.200,000, mshindi wa tatu Sh.150,000 na mshindi wa nne Sh.100,000,
Kwa upande wa wanawake bingwa atapewa Sh.250,000, mshindi wa pili Sh.150,000, mshindi wa tatu Sh.100,000 na mshindi wa nne Sh.50,000.
Mikoa itakayoshiriki ni mabingwa watetezi Kinondoni, Ilala na Temeke, Shinyanga, Mwanza, Kagera Mbeya, Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Dodoma, Iringa, Manyara na Morogoro.
***

Toto Afrika yazionya Kagera, Mtibwa Sugar


KLABU ya soka ya Toto Afrika ya Mwanza imezitaka klabu zinazotaka kuwasajili nyota wao kutotumia mlango wa nyuma na badala yake zionane nao na kufanya mazungumzo.
Uongozi wa Toto, umesema umelazimika kutoa tahadhari hiyo kutokana na kuwepo kwa taarifa zinazoripotiwa na vyombo vya habari juu ya timu za Kagera Sugar na Mtibwa Sugar kuwanyakua wachezaji wao wawili nyota bila ya wenyewe kujua lolote.
Wachezaji walioufanya uongozi huo kucharuka mapema ni mshambuliaji, Husseni Sued anayedaiwa kutua Kagera Sugar na kiungo Mohammed Soud aliyevumishwa kunyakuliwa na klabu ya Mtibwa ya Morogoro.
Katibu wa klabu hiyo, Salum Kaguna, alinukuliwa hivi karibuni akisema kuwa, hawana taarifa zozote za wachezaji hao kunyakuliwa na timu hizo kwa vile hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanywa hadi ssa baina yao na klabu hizo.
Kaguna, alisema ni vema klabu zinazowataka wachezaji ziende mezani kuzungumza kwa sababu nyota hao wana mikataba na hivyo hawatakuwa radhi waondoke kienyeji.
"Hatuzuii wachezaji wetu kuondoka kama wamepata timu, muhimu ni taratibu zifuatwe, mfano Soud anayetajwa kutua Mtibwa, yeye ana mkataba wa miaka mitatu ya Toto akiwa ametumikia miaka miwili na kubakisha mmoja utakaoisha mwakani," alisema Kaguna.
Viongozi wa Mtibwa na Kagera hawakupatikana kuweka bayana kinachoendelea juu ya harakari zao za kuwanyakua wachezaji hao na onyo hilo la uongozi wa Toto Afrika ambayo imekuwa ikijinadi imepania kufanya kweli msimu ujao katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
***

TAVA yapongezwa, yashauriwa


CHAMA cha Mpira wa Wavu nchini, TAVA, umepewa 'kifyagio' kwa kujitahidi kurejesha hadhi ya mchezo huo, lakini kikashauriwa kuwekeza nguvu zao ngazi za chini hususani katika mashule ili kuzalisha nyota wa baadaye watakaoisaidia Tanzania kimataifa.
Kifyagio na ushauri huo umetolewa na mchezaji nyota wa zamani wa klabu ya Jeshi Stars, Ibrahim Christopher 'Michael Power' alipozungumza na MICHARAZO na kusema uongozi wa TAVA umekuwa ukijitahidi katika hali ya mazingira magumu kuinua tena mchezo huo nchini.
Christopher, alisema kukosekana kwa wadhamini ni tatizo lililochangia kuufanya mchezo wa wavu kudodora, lakini jitihada za viongozi wa chama chao umesaidia kuendesha michuano ya kitaifa na kimataifa jambo la kupongezwa.
Alisema hata hivyo bado TAVA inapaswa kuelekeza nguvu zao katika ngazi za chini kusaka nyota wa baadae ikiwezekana kuendesha michuano katika shule za msingi na sekondari ili kuwapa morali vijana kujitosa kwenye mchezo huo.
"Kwa kweli TAVA inafanya kazi katika mazingira magumu kwa kutokuwa na wafadhili wala wadhamini, lakini bado naiomba waelekeza nguvu zao kwa vijana toka ngazi za chini ili waje kuchukua nafasi zetu kuendelea mchezo huu," alisema.
Nyota huyo aliyeisadia Mzinga ya Morogoro kutwaa taji la Ligi ya Muungano lililofanyika mjinio Tanga, alisema kadhalika wachezaji na viongozi wa zamani wa mchezo huo wanapaswa kujitokeza kuusaidia uongozi wa sasa katika kuhakikisha wavu inarejesha makali yake.
"Viongozi na wachezaji wa zamani wamejiweka kando, wanapaswa kutoka mafichoni kusaidiana na TAVA kurejesha makali ya mchezo huo," alisema.
***


'Wazee wa Kizigo' wapata meneja


BENDI ya Extra Bongo 'Wazee wa Kizigo', imepata meneja ambaye atabeba jukumu la kusimamia shughuli zote za bendi hiyo ili isonge mbele kufikia malengo ya kuwa matawi ya juu.
Kiongozi wa bendi hiyo Rogert Hegga, alimtaja meneja huyo mpya kuwa ni Mujibu Hamis aliyewahi kuifanya kazi katika bendi za FM Acdeamia na Mashujaa Musica.
Hegga alisema, kwa vile Mujibu ni mzoefu wa kazi hiyo kwa muda mrefu, ana uhakika mchango wake utakuwa mkubwa ndani ya Extra Bongo ambayo inazidi kupanda chati kila kukicha.
"Fitina za muziki anazijua sana na sisi tunaamini kwamba tukiwa naye kwenye bendi yetu ya Extra Bongo tutaendelea kupiga hatua zaidi ili kufikia malengo ambayo tumejiwekea," alisema Hegga.
Alisema, Extra Bongo haikuwa na meneja hali ambayo ilikuwa inachangia baadhi ya shughuli za bendi kukwama na kwamba sasa amempata Mujibu ambaye atatumia uzoefu wake kusimamisha maendeleo ya Extra Bongo.
Katika hatua nyingine kiongozi huyo alisema, Extra Bongo imeanzisha ushirikiano wa maonyesho ya pamoja na vikundi mbalimbali vya burudani ili kujenga urafiki kati ya wanamuziki wake na wasanii wa vikundi hivyo.
Alisema ushirikiano huo ulianza wiki iliyopita kwa kufanya onyesho la pamoja na vikundi vya Baikoko, Kiti Tigo, Werawera na Khanga Moja ambavyo vina umaarufu miongoni mwa mashabiki wa burudani.

Sikinde yabakisha mbili albamu mpya





BENDI kongwe ya muziki wa dansi ya Mlimani Park 'Sikinde' imebakisha nyimbo mbili kabla ya kukamilisha albamu mpya itakayokuwa na nyimbo sita.
Katibu wa bendi hiyo, Hamis Milambo, alisema hadi sasa bendi yao imekamilisha nyimbo nne ambazo zilitarajiwa kutambulishwa jana kwa mashabiki wao katika onyesho maalum la uzinduzi wa vyombo vyao.
Milambo alizitaja nyimbo hizo nne zilizokamilika kuwa ni 'Jinamizi la Talaka', 'Mihangaiko ya Kazi', 'Kinyonga' na 'Deni Nitalipa'.
"Tumekamilisha nyimbo nne ambazo tutazitambulisha kwa mashabiki wetu na mbili za mwisho tayari zimeshaandikwa mashairi ingawa hazijapewa majina yake," alisema Milambo.
Alisema nyimbo hizo za awali zimetungwa na waimbaji wao mahiri akiwemo mkongwe, Hassani Rehani Bitchuka na wengineo.
Tangu ilipopakua albamu ya 'Supu Imetiwa Nazi', Sikinde haijapakua albamu nyingine tena mpya na hivi karibuni iliondokewa na mtunzi na muimbaji wake nguli, Shaaban Dede aliyetua kwa mahasimu wao, Msondo Ngoma ambapo ameshaibuka na nyimbo mbili mpya.
Nyimbo hizo ni 'Suluhu' uliowekwa kwenye albamu mpya ya Msondo na kingine cha 'Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya' uliowekwa kiporo kwa albamu ijayo ya bendi hiyo.

Jumbe ahidi Talent kufanya makubwa Kilwa Masoko

MWANAMUZIKI nyota wa bendi ya Talent 'Wazee wa Kuchechemea', Husseni Jumbe, amejigamba kuwa atafanya makamuzi ya haja kwenye onyesho la bendi yake litakalofanyika Jumatano ijayo mji wa Kilwa Masoko, mkoani Lindi.
Jumbe na bendi yake wanatarajia kwenda kutambulisha albamu yao mpya na ya pili iliyokamilika hivi karibuni katika onyesho litakalofanyika Jumatano ijayo (Juni 29) kwenye ukumbi wa Kilwa PM Resort.
Akizungumza na MICHARAZO, Jumbe, alisema wamepania kwenda kuwapa burudani wakazi wa mji huo kutokana na kwamba hiyo itakuwa ni mara yao ya kwanza kwenda mjini Kilwa.
Alisema katika onyesho hilo Talent itatambulisha albamu yao ya awali ya 'Subiri Kidogo' na ile moya iitwayo 'Shoka la Bucha' ambayo imekamilika hivi karibuni ikiandaliwa kupakuliwa video zake.
"Tumejiandaa vya kutosha kuwapa burudani wakazi wa Kilwa katika onyesho letu la Juni 29, tunaamini tutakidhi kiu ya muda mrefu ya mashabiki wa muziki wa eneo hilo," alisema Jumbe.
Jumbe, alizitaja nyimbo watakazozitambulisha katika onyesho hilo lililoratibiwa na mmiliki wa ukumbi huo, Yohana Miwa, kuwa ni 'Shoka la Bucha', 'Usiku Haulaliki', 'Kiapo Mara Tatu', 'Kilio cha Swahiba' na zile za albamu yao iliyopita ya 'Subiri Kidogo' iliyozinduliwa Novemba, 2010.
Mkongwe wa dansi alisema pia katika onyesho hilo watawapigia mashabiki watakaohudhuria nyimbo za albamu zake binafsi za 'Mapenzi ya Siri' na 'Kwetu ni Wapi', pamoja na vibao alivyowahi kung'ara navyo akiwa na bendi za DDC Mlimani Park na Msondo Ngoma.

Extra Bongo kujitambulisha Morogoro



BAADA ya ziara ya mafanikio kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani, bendi ya Extra Bongo 'Next Level', inatarajia kuzuru mkoani Morogoro kwa maonyesho maalum matatu ya kuinadi nyimbo mpya ikiwemo 'Watu na Falsafa' uliotungwa na Ramadhan Masanja 'Banzastone' katika miji ya Kilombero, Ifakara na Kilosa.
Ikiwa mkoani Lindi Extra Bongo ilitumbuiza katika ukumbi wa Lindi Oceanic Hoteli, Mtwara katika ukumbi mpya wa Safari Pub na Pwani katika ukumbi wa Maendeleo mjini Utete ambapo maonyesha hayo yalipata wapenzi wengi.
Akizungumza na MICHARAZO, mkurugenzi wa bendi hiyo, Ally Choki alisema kufuatia mafanikio waliopata kwenye mikoa hiyo ya kusini mwa Tanzania, wapenzi wa mkoa wa Morogoro wameitaka bendi ikatumbuize huko.
Alisema, Julai Mosi Extra Bongo itatumbuiza katika ukumbi wa Jamos Centre uliopo Ifakara kabla ya kwenda Kilombero katika ukumbi wa K2 Centre na kisha mjini Kilosa ambako itakuwa katika ukumbi wa Babilon Luxury Centre.
"Tunakwenda Morogoro baada ya kupata mafanikio katika ziara yetu mikoa ya kusini, tunaamini ziara hii inaweza kupanua milango zaidi ya Extra Bongo kupata mialiko ndani na nje ya Dar ili kusaidia wanamuziki kunufaika," alisema.
Chuki alisema hii ni mara ya pili kwa Extra kufanya ziara mkoani Morogoro, lakini alisema awali ilitumbuiza katika ukumbi uliopo mjini na kwamba hatua ya kwenda hadi wilayani ni mwanzo wa bendi yake kutembelea nchi nzima.
Wakati hayo yakiendelea, Choki alisema kabla ya kwenda Morogoro, leo bendi hiyo itafanya vitu vyake katika ukumbi wa Rufika, Tabata Segerea.

Msondo Ngoma wasaka jina la albamu yao



LICHA ya kukamilisha nyimbo zote sita zitakazokuwepo kwenye albamu yao mpya ijayo, uongozi wa bendi ya Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki', bado haujajua albamu hiyo mpya iitwe kwa jina gani.
Msondo ambayo leo inatarajiwa kuendelea na makamuzi yao kwenye ukumbi wa TCC-Chang'ombe, Temeke, imesema inaendelea kutafakari waipe jina gani albamu hiyo ijayo.
Msemaji wa bendi hiyo, Rajabu Mhamila 'Super D', alisema wanamuziki wao wanaendelea kuumiza vichwa kutafuta jina litakalobeba albamu hiyo itakayochukua nafasi ya ile ya mwaka juzi ya Huna Shukrani'.
Super D, alisema hata hivyo siku si nyingi mashabiki wao wao watafahamu jina la albamu hiyo ambayo baadhi ya nyimbo zimekuwa zikitambulishwa kwenye maonyesho yao ndani na nje ya jijini la Dar es Salaam.
"Albamu yetu ijayo bado haijafahamika itaitwaje kwa vile wanamuziki wanaendelea kuumiza vichwa kutafuta jina lake, ila nyimbo zote sita zimeshakamilika na kuanza kutambulishwa kwa mashabiki wetu," alisema.
Alizitaja nyimbo za albamu hizo na watunzi wake kwenye mabano kuwa ni 'Lipi Jema' na 'Baba Kibebe' (Eddo Sanga), 'Dawa ya Deni (Isi'haka Katima), 'Suluhu' (Shaaban Dede), 'Nadhiri ya Mapenzi' (Juma Katundu) na 'Kwa Mjomba Hakuna Urithi (Huruka Uvuruge).

Mapacha Wa3 wajikomboa zaidi




BENDI mpya ya muziki wa dansi ya Mapacha Watatu 'Wazee wa Kuchakachua', imendelea kujikwamua kwa kufanikiwa kupata vyombo vipya vya muziki vyenye thamani ya shilingi milioni 36.
Mmoja wa Wakurugenzi wa bendi hiyo, Khalid Chokoraa alisema wamefanikiwa kununua vyombo kwa juhudi zao wenyewe na kuungwa mkono na baadhi ya mashabiki wao.
Chokora alisema, sasa bendi hiyo inatarajia kuzindua vyombo hivyo leo Jumapili katika ukumbi wa Mzalendo Pub, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam ambapo wamealikwa watu mbalimbali akiwemo Asha Baraka.
"Tutazindua vyombo vyetu Jumapili ambapo tumewaalika Wakurugenzi wa bendi mbalimbali na wadau wa muziki wa dansi akiwemo Asha Baraka, Ally Choki, Martin Kasyanju, Mama Sakina na wengine wengi," alisema.
Mkurugenzi huyo alisema vyombo hivyo vitaanza kutumika rasmi kwenye onyesho la pamoja na bendi ya Akudo Impact ambalo linatarajiwa kufanyika Julai 2 katika ukumbi wa Vatican Sinza, jijini Dar es Salaam.
Mapacha Watatu ina albamu ya kwanza ya 'Jasho la Mtu' na sasa iko kwenye maandalizi ya albamu ya pili ikiwa imekamilisha nyimbo za 'Tangulia Shambani', 'Sumu ya Mapenzi remix', 'Mtoto wa Paka' na 'Usia wa Babu'.
Bendi hiyo ilianza kama kundi likiwa na vijana watatu ambao ni Khalid Chokoraa, Jose Mara na Kalala Junior lakini wamepiga hatua kwa kuanzisha bendi ambayo ina wanamuziki ya 10.
Baadhi ya wanamuziki hao ni Allen Kisso (solo), Jimmy London (besi), Sele Tumba (tumba), Erasto Mashine (kinanda), Mariam Bessie, Mariam Zidane, Juddy Chakachua, Mariam na Sabrina Pazi ambao wote ni wanenguaji.

Dede alia na uvivu wa mawazo katika dansi



MWANAMUZIKI mkongwe nchini, Shaaban Dede 'Mzee wa Loliondo' amewaasa wanamuziki wenzake wa dansi kutobweteka na mafanikio machache waliyonayo katika sanaa zao na badala yake waumize vichwa kubuni mambo mapya kama wanavyofanya wale wa muziki wa taarab.
Dede, alisema anawafagilia wanamuziki wa taarab kwa kubuni kitu kilichouinua muziki huo nchini toka taarab asilia hadi kuwa ya kisasa ikichezeka na kupendwa na mashabiki wengi.
Alisema kuwekwa kwa rhumba na rapu katika muziki wa taarab kumeupandisha chati na kuonyesha jinsi gani wanamuziki wa dansi walivyo na changamoto ya kuumiza vichwa kuhimili ushindani wanaoupata toka kwa miondoko hiyo ya mwambao na muziki wa kizazi kipya.
"Lazima wanamuziki waumize vichwa, wasibweteke kwa kuona muziki wetu unakubalika na watu wengi, hilo linaweza kutufanya tubaki tulipo wakati wenzetu wakisonga mbele kama ambavyo taarab walivyofanya," alisema Dede.
Dede anayeifanyia kazi Msondo Ngoma, alisema kwa kuwa wanamuziki wanaojiandaa kuwarithi wakongwe katika muziki wa dansi wanapaswa kuacha kulemaa na kasumba ya kuiga kazi za nje na badala yake wakajikita katika kutafuta vyao kama ambavyo miaka ya nyuma bendi zilivyotofautiana kimipigo na kuzoa mashabiki lukuki.
Alisema tabia ya bendi kuwa na ladha yake ya kimuziki na kujitofautisha na wengine ndio iliyozifanya Sikinde na Msondo hadi leo kuwa na mashabiki wao binafsi, kitu ambacho bendi zingine za kisasa zinapaswa kufuata mkumbo huo.

Rufita yamnasa Kibugila



BENDI ya muziki wa dansi ya Rufita Connection 'Wana Shika Hapa Acha Hapa', imepata mcharaza solo mpya ikiwa ni wiki chache baada ya Seleman Shaibu Mumba kukimbilia Twanga Pepeta.
Kwa mujibu wa rais wa bendi hiyo, Chai Jaba, mpiga solo huyo ni Abdalah Kibugila ambaye amewahi kuwa bendi mbalimbali ambapo kwa mara ya mwisho alikuwa Bwagamoyo International ya Mwinjuma Muumin.
"Seleman alikuwa mpiga solo wetu lakini ameshahama, lakini tayari tumeshapata aliyeziba nafasi yake, kazi inaendelea kama kawaida kutokana na ukweli kwamba Kibugila ni mwanamuziki siku nyingi ana uzoefu wa kutosha," alisema.
Alisema Kibugila anashiriki maonyesho ya bendi hiyo huku akizifanyia mazoezi nyimbo za bendi hiyo zikiwemo za 'Mapenzi Yanaua', 'Nilinde Nikulinde', 'Anasa', 'Shida ya Mapenzi', 'Usia', 'Acha Pupa','Mkosi Gani' na 'Mazi'.
Akielezea zaidi mipango ya bendi hiyo, Chai Jaba inajiandaa kumalizia kazi ya kurekodi nyimbo zote na kisha kuanza kushuti video na kisha zitafuatia taratibu za kuzindua albamu.
"Nina uhakika yatakwenda vizuri na inawezekana tukakamilisha kazi ya kurekodi nyimbo zetu mwezi ujao kabla ya kuendelea na kazi ya kushuti video ili tujitambulishe zaidi kwa mashabiki wa muziki wa dansi," alisema.
Aidha, alisema bendi hiyo inajiandaa kuleta wanenguaji wapya wanne kutoka Congo (DR) watakaokuja kuungana na wenzao waliopo kwa sasa ili kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji wa jukwaa.

Gilla alia na Phiri kumzibia riziki Simba



MSHAMBULIAJI chipukizi wa Simba Salim Aziz Gilla aliyetangazwa kutafutiwa timu ya kucheza kwa mkopo msimu ujao amemlaumu aliyekuwa kocha mkuu wa klabu hiyo Patrick Phiri kuwa alichangia kufifisha nyota yake kisoka.
Gilla aliyenyakuliwa na Simba kwa mkataba wa miaka mitatu mwaka 2009 baada ya kung'ara kwenye michuano ya Kombe la Taifa, alisema kutoaminiwa na Phiri kulikopelekea kushindwa kuitumikia vema Simba ndiko kulikomfanya asifurukute.
Akizungumza na MICHARAZO, Gilla alisema hata kushindwa kuitwa kwake kwenye timu za taifa, zikiwemo za vijana, inatokana na kukalishwa benchi na Phiri.
Phiri aliondoka Simba mara baada ya kumalizika kwa ligi kuu ya Bara msimu uliopita.
"Kushindwa kuaminiwa na Phiri na kunipa nafasi ya kuonyesha uwezo wangu katika kufumania nyavu umenisababishia haya yote yanayonikuta ndani ya Simba na kukosa kuitwa hata katika timu za vijana ambazo huenda ningezisaidia," alisema Gilla.
Gilla, anayekaribia umri wa miaka 21, alisema misimu miwili aliyokuwa Simba hakuwahi kupata nafasi ya kucheza dakika 90 za mchezo wowote, kitu alichodai sio kimemvuruga akili, bali kimemnyima fursa ya kuonekana kama alivyong'ara kenye Kombe la Taifa akiwa na timu ya mkoa wa Tanga.
Katika michuano hiyo, Gilla aliibuka Mchezaji Bora, huku akiteuliwa mara mbili kuwa 'nyota' wa mchezo ukiwemo ule wa kusaka mshindi wa tatu ambapo Tanga waliilaza Mwanza mabao 2-0.
Alisema hajakata tamaa kutamba kisoka, hatahivyo.
Alisema anaamini alichokutana nacho Simba ni mtihani hivyo anajipanga ili kuendeleza kipaji chake kilichomfanya aichezee Polisi Dodoma chini ya Sekilojo Chambua kabla ya kutua Simba.

Simba yaanza kwa kusuasua Kagame, Ocean View safi



MABINGWA wa kihistoria wa michuano ya Klabu Bingwa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, 'Kagame Cup' Simba ya Tanzania jana ilianza kwa kusuasua michuano hiyo baada ya kulazimishwa suluhu na Vital'O ya Burundi, katika pambano la lililofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.
Simba inayopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kutokana na kucheza nyumba na rekodi yake nzuri michuano hiyo inapofanyika Tanzania, imebakiza mechi dhidi ya Zanzibar Ocean View, Etincelles ya Rwanda na wawakilishi wa Eritrea -- Red Sea.
Nafasi nzuri zaidi ya kupata bao kwa Simba ambayo ilianza mchezo na wachezaji wanne wapya ilikuja mwishoni mwa kipindi cha kwanza wakati Haruna Moshi 'Boban' alipopiga mpira wa kwa tik tak uliogonga mwamba wa mabingwa wa Burundi hao kabla ya kuokolewa na mabeki.
Shuti la 'Boban' ambaye hajacheza kwa miaka miwili kutokana na mzozo wa mkataba kati yake na Gefle IF ya Sweden lilikuja kutokana na krosi ya Ulimboka Mwakingwe ambaye kama mpigaji huyo amerudi kikosini baada ya kuachwa msimu uliopita.
Mwakingwe aliuwahi mpira mikononi mwa mlinda mlango wa Vital'O kufuatia shambulizi kali kwenye lango la wapinzani wa Simba hao, pembeni mwa eneo la hatari kabla ya kupiga krosi.
Kikosi cha Simba yenye pointi moja sawa na Vital'O na ambayo bado ina matumaini ya kusonga mbele kutokana na kundi lake kuwa na nafasi tatu za kucheza robo-fainali, kilikuwa pia na mchezaji wa zamani Said Nassoro 'Cholo' na Walulya Derick.
Kocha wa Simba MOses Basena alisema ameshangazwa na matokeo ya kutofungana wakati Simba ilitengeneza nafasi nyingi katika mchezo huo. Na kweli.
Wakati Vital'O ilicheza kwa kujihami zaidi na kushambulia kwa kushitukiza mara nyingi, Simba ilikuwa na mlolongo wa mashambulizi langoni mwa warundi hao.
Kocha wa Vital'O Younde Kagabo alisema ameridhika na sare hiyo kutokana na timu yake kuwa na wachezaji 10 wapya uwanjani.
Katika mchezo wa kwanza mabingwa wa Zanzibar, Zanzibar Ocean View walianza kwa kishindo michuano hiyo baada ya kuilaza Etincelles ya Rwanda kwa mabao 3-2 na hivyo kuongoza kundi hilo la A linalohusisha timu tano.
Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo kwa mechi za kundi B ambapo mabingwa wa soka nchini Tanzania, Simba itakwaruzana na El Merreikh ya Sudan iliyokuja kwenye michuano hiyo baada ya mabingwa wa nchi yao, Al Hilal kujitoa ili ijiandae vema na Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi inayotarajiwa kuanza mwezi ujao.
Mechi ya Yanga na Wasudan hao ambao inakumbusha fainali za michuano hiyo za mwaka 1986 ambapo Yanga ilikomboa mabao mawili dakika mbili za mwisho wa mchezo kupitia Abubakar Salum 'Sure Boy' kabla ya kulazwa kwa mikwaju ya penati na kuliacha kombe liondoke Tanzania, itachezwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pambano jingine la leo ni la kundi C michezo inayochezwa uwanja wa Jamhuri, Morogoro kwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo, APR ya Rwanda kuumana na Ports Authority ya Djibout.

Saturday, June 25, 2011

Dialo kutoka Bondeni ana tatu mpya




MSANII aliyewahi kufanya shughuli zake nchini Afrika Kusini, Zakaria Kazi Mkombozi maarufu kama Dialo, akishirikiana na bendi yake binafsi ameachia nyimbo tatu mpya ikiwa ni maandalizi ya kupakua albamu yao ya kwanza.
Akizungumza na mtandao huu, Dialo, alizitaja nyimbo hizo ambazo zimeanza kusambazwa kwenye vituo vya redio kuwa ni 'Sudan Risen' unaozungumzia hali ya kisiasa nchini Sudan, 'Madoda Mpela' uliombwa Kizulu na 'Let Do It'.
Dialo alisema nyimbo hizo ni kati ya nyimbo zitakazokuwa kwenye albamu yao ijayo ambayo bado hawajaipa jina, ila alisema itakuwa na nyimbo 10 zilizopo kwenye miondoko ya Reggae, Afro Pop na Ragga.
"Baada ya kuwa kimya tangu niliporejea nchini kutoka Afrika Kusini, nilipokuwa nafanya shughuli zangu za muziki, nimefanikiwa kuunda bendi ambayo tumeachia kazi tatu mpya ikiwa ni maandalizi ya kupakua albamu yetu ya kwanza," alisema.
Dialo alisema mbali na kuendesha bendi ya muziki, lakini pia ameanzisha klabu ya vijana kwa ajili ya kuwapa elimu ya stadi za maisha na kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na kujikinga na ukimwi.
Alisema bendi yake ina jumla ya wasanii sita ambao ni yeye Dialo, Bob Chuwa, Dk Today, Alex, Katanga Junior (mdogo wa aliyekuwa mpiga dramu maarufu nchini, Gabby Katanga, ambaye kwa sasa ni marehemu, Yuzo na Amani.
Dialo, aliyewahi kufungwa kwa muda wa miaka mitatu nchini Afrika Kusini kwa kile alichodai kufanyiwa hila na watu aliokuwa akifanya nao kazi ya muziki nchini humo, alisema beni yao inatarajiwa kutumbuiza mjini Moshi siku ya Juni 17 mwaka huu.
Alisema onyesho hilo litafanyika kwenye ukumbi wa Glacian Sports Bar, ambapo mbali na kutambulisha nyimbo zao, lakini pia watapiga nyimbo za magwiji wengine wa muziki duniani kwa staili ya kukopi.
"Tumeanza kufanya maonyesho ambapo Juni 17 tulikuwa nyumbani Moshi, Kilimanjaro kwenye ukumbi wa Glacian Sports Bar," alisema.

Nisha: Wasanii tusiridhike mapema


MSANII anayekuja juu kwenye fani ya filamu nchini, Salma Jabu 'Nisha' amewataka wasanii wenzake kutoridhika na mafanikio ya kutamba nyumbani na badala yake kujibidiisha kujitangaza katika anga la kimataifa.
Nisha aliyeng'ara kwenye filamu kama 'Family Disaster', 'Better Day', 'Kimya' na nyinginezo, alisema kulewa sifa na mafanikio ya nyumbani kwa wasanii wengi nchini kunachangia wengi wao wasitambe kimataifa, kitu kinachopaswa wabadilike sasa.
"Wasanii nchini wanapaswa kubadilika na kujitangaza kimataifa, tusiridhike na mafanikio ya nyumbani kwani ndio yanatufanya tusipige hatua kubwa kimaendeleo kama wenzetu wa nje,' alisema Nisha, aliyejitumbukiza kwenye fani hiyo miaka mitatu iliyopita.
Nisha ambaye yupo mbioni kuibuka na filamu iitwayo 'Simu Sikioni' ya msanii nguli, Deo Shija, alisema hata yeye mwenyewe pamoja na nyota ya neema kuanza kumulikia kwa sasa nchini, hataridhika hadi atakaposimama kimataifa akichuana na wakali wa dunia katika fani hiyo.
"Ndoto zangu ni kutamba kimataifa kwa kuwa sitaridhika na mafanikio ya nyumbani, jambo ambalo kila msanii wa ukweli anatakiwa awe hivyo," alisema Nisha.
Mzanzibar huyo, alisema anaamini kama kila msanii atakuwa na kiu ya kutamba kimataifa ni wazi Tanzania itajitangaza na kutoa fursa ya Watanzania kutambulika kama ilivyo kwa Wanigeria, Wamarekani na wasanii wengine wanaotamba ulimwenguni.

Monday, April 25, 2011

Tamasha la ngumi laanzishwa Dar

MABONDIA mbalimbali wakiwemo wakongwe na chipukizi wanatarajia kujumuika pamoja katika tamasha maalum la ngumi linaloanza rasmi kesho kwenye Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam.
Tamasha hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Kinyogoli Foundation inayomilikiwa na bondia wa kimataifa wa zamani ambaye ni kocha kwa sasa, Habib Kinyogoli, awali lilipangwa kufanyika leo Jumatatu ya Pasaka, kwenye ukumbi wa Panandipanandi.
Akizungumza na MICHARAZO, mmoja wa waratibu wa tamasha hilo, Rajabu Mhamila 'Super D' alisema katika tamasha hilo, mabondia mbalimbali wakongwe na chipukizi watachuana na lengo ni kuwapa nafasi chipukizi ya kujifunza mbinu kutoka kwa mabondia hao wazoefu.
Super D ambaye pia ni bondia wa zamani na kocha wa klabu ya Ashanti, alisema yeye na Kinyogoli, wameamua kushirikiana kuandaa tamasha hilo ili kuhakikisha mchezo wa ngumi nchini unarejesha heshima yake baada ya kudorora kwa muda mrefu.
"Katika kurejesha hadhi ya ngumi nchini, tumeamua kuandaa tamasha la ngumi ambalo litakuwa likifanyika kila wiki kwenye ukumbi wa Panandi Panandi ambapo wakongwe na mabondia wanachipukia watashirikiana kupigana katika kutoa burudani," alisema Super D.
Aliongeza kuwa, mbali na michezo kadhaa ya ngumi, ikiwahusisha baadhi ya nyota wa mchezo huo kama mabondia wa ukoo wa Matumla, pia tamasha hilo litapambwa na burudani kemkem za muziki kutoka kwa wasanii ambao watakakuwa wakipokeza kwenda kutumbuiza kama njia ya kuwahamasisha watu kuhudhuria kwa wingi.

Sikinde wana mbili mpya



BENDI ya Mlimani Park 'Sikinde' imekamilisha vibao viwili ikiwa ni moja ya mikakati yake ya kujipanga upya baada ya kuondokewa na mwanamuziki wake, Shaaban Dede aliyejiunga na mahasimu wao, Msondo Ngoma.
Katibu wa bendi hiyo, Hamis Milambo, alisema kuwa bendi yao ambayo kwa wiki mbili mfululizo imekuwa kambini ikijifua, ambapo imekamilisha nyimbo mbili zilizotungwa na muimbaji wao mkongwe, Hassani Bitchuka.
"Tumeanza kujipanga upya kwa ajili ya kupakua albamu mpya na tayari tupo kambini kwa wiki ya pili sasa, ambapo tumeshakamilisha nyimbo mbili mpya zilizotungwa na Bitchuka," alisema.
Katibu huyo alisema nyimbo hizo zinazoendelea kufanyiwa mazoezi, hazijapewa majina hadi sasa na zitatambulishwa kwa mashabiki wao katika maonyesho yao ya Sikukuu ya Pasaka.
"Tutazitambulisha kwenye maonyesho yetu ya Pasaka, na hapo ndipo zitakapofahamika majina yake, ila ni kati ya nyimbo zitakazothibitisha kuwa Sikinde ni mabingwa wa muziki wa dansi nchini," alisema Milambo.
Milambo alisema baada ya maonyesho ya Pasaka, bendi yao itarejea kambini kwa ajili ya kumalizia kuzifanyia mazoezi nyimbo nyingine mpya ambazo zimeshaandikwa mashairi na waimbaji wao, Abdallah Hemba na Hassani Kunyata tayari kukamilisha idadiu ya nyimbo zinazotakiwa kwa albamu yao ijayo.
Tangu mwaka juzi, Sikinde ilipotoa albamu yao ya Supu Imetiwa Nazi, bendi hiyo haijaachia albamu nyingine zaidi ya vibao viwili vya Wanawake Wanaweza na Tunu ya Upendo vilivyotungwa na Dede maarufu kwa sasa kama 'Mzee wa Loliondo' ambaye ameenda Msondo Ngoma.

Kitabu cha Assosa chatinga mitaani





KITABU cha mwanamuziki nguli wa muziki wa dansi, Tshimanga Kalala Assosa, kiitwacho 'Jifunze Lingala' kimeingia mitaani, huku mwenyewe akijiandaa kutoa toleo la pili la kitabu hicho kinachofundisha lugha ya Kilingala na Kiswahili.
Akizungumza na MICHARAZO, Assosa, alisema kitabu hicho ambacho mbali na kufunza watu Kilingala, pia kina tafsiri ya nyimbo za wanamuziki maarufu wa Kongo na kiliingia sokoni tangu juzi huku kikigombewa kama njugu.
Assosa, alisema tangu akiingize sokoni kitabu hicho kimeshauza kopi zaidi ya 1000, huku akipokea oda kedekede toka kila pembe ya nchi kwa watu wanaokiulizia.
"Aisee kile kitabu changu nimeshakiingiza sokoni, na huwezi kuamini kimekuwa kikinukuliwa kama njugu tofauti na matarajio yangu, hali inayonifariji mno," alisema Assosa.
Mkongwe huyo aliyewahi kuzipigia bendi za Negro Succes, Orchestre Lipualipua, Fukafuka, Le Kamalee, Marquiz du Zaire, Marquiz Original, Mambo Bado, Legho Stars na sasa Bana Marquiz, alisema hakutaraji kama kingegombewa.
Alisema hakuwa na tumaini la kugombewa kwa kitabu chake kutokana na ukweli ndicho cha kwanza kwake kukitoa tangu aamue kujikita kwenye uandikaji wa vitabu, nje ya shughuli zake za muziki anaoendelea nao hadi sasa.
Aliongeza kuwa, hali hiyo unamfanya afikirie kuongeza idadi ya nakala zake, ili kukidhi mahitaji ya mashabiki wanaokiulizia ambacho ndani yake pia kina picha za wasanii wakongwe wa Kongo pamoja na yeye na familia yake.
"Kama watakuwa wanavihitaji pia wanaweza kwenda pale Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, kuna wakala anaviuza pale, au wanaweza kunipigia simu namba 0713-240735, watakipata." alisema Assosa.

Rapa wa Levent atua TOT-Plus

BENDI ya TOT-Plus ambayo sasa inaendelea na kambi yake ya mazoezi, Mwananyamala, jijini Dar es Salaam, imempata rapa mpya Dokta Steve 'Sauti ya Ng'ombe' kutoka bendi ya Levent Musica ya mjini Morogoro.
Kiongozi wa TOT-Plus, Badi Bakule, alisema rapa huyo alijiunga na tangu wiki iliyopita na anaendelea
na mazoezi kama kawaida akisubiri kutambulishwa rasmi.
"Tumemchukua rapa huyu ili kuziba nafasi ilioachwa na Jua Kali ambaye ameachana na TOT-Plus na kwenda kufanya kazi kwingine, Dokta Steve ameonyesha uwezo mkubwa hivyo anatufaa," alisema Bakule.
Bakule alisema bendi hiyo ambayo imekuwa na mazoezi kwa zaidi ya mwezi mmoja, inatarajia kutoka kambini Ijumaa Aprili 29 na kisha itajitambulisha rasmi Mei Mosi.
Alisema, rapa huyo kwa sasa amekuwa akijifua katika mazoezi makali kwenye kambi ya bendi hiyo iliopo eneo la Ujiji Mwananymala, jijini Dar es Salaam ili kuhakikisha kwamba anaibuka na vitu vipya.
"Pia tunataka azijue nyimbo zote mpya ambazo tayari tumezikalimisha na hata zile za zamani ambazo wanamuziki karibu wote wamezifanyia mazoezi kabla rapa huyu mpya hajajiunga na bendi yetu," alisema.
Kiongozi huyo alizitaja nyimbo hizo mpya kuwa ni 'Kilio cha Linda', 'Zai' 'Maisha Duni', Liwalo na Liwe','Dakika Tisa' na 'Riziki na Zengwe' ambazo baadhi yake tayari zimesharekodiwa.
Aliongeza kuwa 'Sauti ya Ng'ombe' atatoka kambini akiwa pia amemaliza kuzifanyia mazoezi baadhi ya nyimbo za zamani zilizochangia kuiweka TOT-Plus kwenye matawi ya juu.
"Kuna nyimbo kama Masimango, Mtaji wa Masikini, Elimu ya Mjinga, Mtoto Yatima, Mnyonge Mnyongeni na nyingine nyingi ambazo anatakiwa azifahamu vizuri kabla hatujatoka kambini," alisema.
Tangu imalize kampeni za Uchaguzi Mkuu mwishoni mwa mwaka jana, bendi hiyo bado haijafanya maonyesho na badala yake imeingia kambini ili kujipanga vizuri kwa ajili ya kuibuka kwa kishindo.

Stone Mayiyasika wanasa watano

BENDI ya Stone Mayiyasika 'Vijana wa Kazi' imeimarisha safu ya ushambuliaji wa jukwaa kwa kunasa wanenguaji watano akiwemo mnenguaji mahiri aliyewahi kutamba na bendi ya Twanga Pepeta, Juma Mohamed (Super Danger).
Mratibu wa bendi hiyo, Pascal Mahollelo, alisema wanenguaji hao watano wameanza mazoezi na katika maonyesho yao yote ya kusheherekea sikukuu ya Pasaka wataanza kuwatambulisha kwa mashabiki.
Alisema, mbali ya Super Danger ambaye ni mkongwe, wanenguaji wengine wapya ni wa kike na kwamba ni chipukizi ambao wameonyesha uwezo mkubwa wa kazi.
Aliwataja wanenguaji hao wa kike kuwa ni Zawadi Seif, Joselina Ngatunga (Happy), Shania Malimba na Mwanahamisi Ramadhan.
"Sisi hatuhitaji kugombana na watu ndiyo maana tumeona tuwatengeneze wetu wenyewe na nina imani mashabiki watawakubali kutokana na umahiri wao jukwaani" , alisema Mahollelo.
Alisema, utambulisho wa wanenguaji hao ungeanza kwenye maonyesho yao Sikukuu ya Pasaka.

Cloud atambia Basilisa




MSANII nyota wa filamu nchini, Issa Mussa 'Cloud', amedai filamu yake mpya ya 'Basilisa' ni funika bovu, miongoni mwa kazi zake alizowahi kuzitoa kwa hivi karibuni.
Cloud, alisema filamu hiyo iliowashirikisha wasanii kadhaa mahiri nchini, akiwemo mrembo Wema Sepetu na Ummy Wenslaunce 'Dokii', inaweza kuwa kazi bomba kwa mwaka huu wa 2011 kwa jinsi ilivyoandaliwa kwa ustadi mkubwa.
Mkali huyo aliyetamba na michezo ya kuigiza kupitia runinga kabla ya kuibukia filamu, alisema 'Basilisa' ambayo itasambazwa na kampuni ya Steps Entertainment ni bora kati ya zote alizowahi kuzitoa tangu aiingie kwenye fani hiyo.
Alisema kinachomfanya aamini hivyo ni kwa jinsi hadhithi yake ilivyo, namna alivyoshiriki na umahiri ulioonyeshwa na wasanii wenzake, acha upigaji picha wa kiwango cha hali juu na mandhari iliyotumika kurekodiwa kazi hiyo.
"Sio vibaya mtu kujisifia kwa jinsi anavyofanya kazi yake, nami naiona 'Basilisa' ni moja ya kati niliyoumiza kichwa na kushiriki kwa kiwango kikubwa, nadhani itakuwa miongoni mwa kazi bora kwa mwaka," alisema Cloud.
Msanii huyo, ambaye hushirikishwa kazi mbalimbali, alisema ndani ya filamu hiyo ameigiza katika nafasi tatu tofauti kama alivyowahi kufanya muigizaji wa Kimarekani, Eddy Murphy katika filamu yake ya 'Nutty Professor'.
Tofauti na Murphy aliyeigiza kikomedi zaidi, Cloud ndani ya filamu yake ameigiza 'siriazi' akiwa kama chizi, kiumbe wa kutisha na hali yake ya kawaida, kiasi ni vigumu kubaini kama nafasi hizo tatu tofauti zimechezwa na mtu mmoja.
Mbali na yeye (Cloud) wengine walioshiriki filamu hiyo itakayoingia sokoni mwezi ujao ni Adam Kuambiana, Dokii, Wema Sepetu, Selemani Barafu 'Mzee wa Land Rover', Single Mtambalike 'Richie', Kajala Masanja na wengineo.