 |
| Mwina Kaduguda (kushoto) akiwa na aliyekuwa mwenyekiti wake, Hassan Dalali walipokuwa wakiukabidhi uongozi wa sasa wa Simba, chini ya mwenyekiti wake Ismail Rage |
KATIBU
Mkuu wa zamani wa Simba, Mwina Kaduguda ameyataka makundi yanayosigana
ndani ya klabu hiyo kukaa pamoja na kumaliza tofauti zao kabla ya
kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaoatarajiwa kufanyika hivi karibuni.Kaduguda
alisema lengo la makundi hayo kukaa meza moja ni kujenga umoja na
mshikamano kwa lengo la kupata viongozi bora wanaokubalika.
Aidha
amewakumbusha wanachama wa klabu hiyo kuhakikisha wanachagua viongozi
ambao wataiwezesha Simba kuwa moja na itakayokuwa na uwezo wa kunyakua
ubingwa wa Afrika.
Akizungumza kwenye
kituo cha radio Clouds Fm leo mchana, Kaduguda alisema uzoefu alionayo katika
kuongoza soka ndani ya klabu hiyo na kwingine umemfanya kuitambua
kinachokwaza soka la Tanzania kusonga mbele mojawapo ikiwa ni mifarakano
ya kuendekeza makundi.
Kaduguda
aliyewahi kuwa Katibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kipindi
ikiitwa FAT, alisema ndani ya Simba kuna makundi ambayo yamekuwa
yakiwagawa wanachama kila upande ukitaka kundi lao litoe kiongozi kitu
alichodhani kinapaswa kudhibitiwa mapema.
Alisema
ni vyema makundi yaliyopo kukaa meza moja kwa nia ya kuijenga Simba
kuelekea kwenye uchaguzi kwa kuiwezesha klabu hiyo kupata viongozi bora
watakaoivusha mahali ilipo na kuja kutamba Afrika, la sivyo inaweza
kukutwa na yaliyozikuta Gor Mahia au AFC Leopard za nchini Kenya,
zilizopotea kwenye umaarufu wao wa soka kabla ya kuibuka tena.
"Hakuna
siri ndani ya Simba kuna makundi
kama ya Simba Taleban, Friend's of Simba na Banyamulenge ambalo hata
hivyo limelegalega, nashauri wanayounga mkono makundi hayo yakae pamoja
na kumaliza tofauti na kujadiliana kiongozi gani anayewafaa kuwaongoza."
Kaduguda
alisema na kuongeza, pia makundi hayo yanapaswa kutowapuuza au kuwabeba
watu kwa sababu ya haiba yao au uwezo wa kiuchumi, akieleza hata wasio
na uwezo wa kifedha wana haki na nafasi kubwa ndani ya klabu hiyo.
Pia
aliwakumbusha wanachama wa klabu hiyo kuwa makini katika uchaguzi huo
ili kuipa Simba viongozi makini na bora watakaoiwezesha klabu yao
kutamba kimataifa badala ya kuwabeba watu ambao watakuja kuwanyima raha
kwa miaka minne ijayo.
Klabu ya Simba
inaelekea kufanya uchaguzi mkuu baada ya uongozi wa sasa chini ya
Mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage kumaliza muda wao mwezi ujao.
Hata
hivyo uchaguzi huo bado haujatangazwa rasmi na Kamati ya Uchaguzi
ya klabu hiyo kwa sababu ya kusubiri kupitishwa kwanza kwa Katiba yao
mpya na ofisi ya Msajili ili kuweka hadharani mchakato kamili ya
kinyang'anyiro hicho.