STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, July 4, 2014

Wambura wenzake wapigwa 'stop' Simba

UONGOZI wa klabu ya soka ya Simba umetangaza rasmi kumsimamisha uanachama aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Urais katika uchaguzi uliofanyika Jumapili, Michael Wambura, pamoja na wengine 70 kutokana na kwenda kufungua kesi kwenye mahakama za kawaida za nchi, imeelezwa jijini Dar es Salaam jana.
Akizungumza kwenye makao makuu ya klabu hiyo yaliyoko mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini jana, Rais wa Simba, Evans Aveva, alisema kuwa maamuzi ya kumsimamisha Wambura na wenzake yametolewa na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao walikutana kwa mara ya kwanza juzi.
Aveva alisema kuwa kamati hiyo imechukua maamuzi ya kuwasimamisha kwa kufuata ibara ya 11 (1) (b) ya katiba ya Simba na kuongeza kuwa hatma yao itajulikana katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa klabu unaotarajiwa kufanyika Agosti 3.
Rais huyo alisema kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo ili kuilinda katiba ya Simba na uanachama wa klabu hiyo katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
"Suala la Wambura lilijadiliwa lakini hatukufikia mwafaka na kuamua lipelekwe katika mkutano mkuu ili wanachama waamue, tumewasimamisha wale 69 na katika kesi ya mwaka 2010 aliyofungua Wambura alishirikiana na Juma Mtemi, naye tumemsimamisha," alieleza Aveva.
Alisema kuwa katika mkutano mkuu unaokuja wanachama watajadili pia ripoti ya fedha na mabadiliko ya katiba ambayo yameonekana kuwa na mapungufu.
Kiongozi huyo pia aliwashukuru wanachama wote wa Simba waliompigia na wasiompigia kura kwa sababu kila mmoja ametekeleza haki yake ya kidemokrasia.
Alisema uchaguzi umekwisha sasa wanachama wote ni kitu kimoja waungane kuijenga klabu yao.
"Sasa tuungane kutekeleza ahadi zetu ambazo ni pointi tatu uwanjani, umoja na maendeleo, tusahau tofauti zetu, Simba ni muhimu kuliko sisi sote," alisema kiongozi huyo.

WACHEZAJI KULIPWA LEO
Aveva alisema kuwa uongozi wake unatarajia leo kuwalipa mishahara wachezaji wake ili kuwaweka tayari kwa ajili ya kuanza maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Alisema kuwa kikosi cha timu hiyo kitaanza mazoezi yake Jumatano Julai 9 huku pia wakianza maandalizi ya tamasha la Simba Day litakalofanyika Agosti 8 mwaka huu.
Alisema kwamba kocha mkuu wa timu hiyo, Mcroatia, Zdravko Logarusic, atarejea nchini Jumatatu na taratibu za kumtumia tiketi ya ndege zimeshaanza.

WAJUME WAPYA, KAMATI MPYA
Aveva aliwataja wajumbe watatu wapya wa kuteuliwa watakaoingia katika Kamati ya Utendaji kuwa ni Mohammed Nassor, Musley Al Ruwey na Salim Abdallah huku wengine wawili waliobaki kwa mujibu wa matakwa ya katiba atawatangaza baadaye.
Uongozi huo mpya pia jana ulitangaza kamati tatu zitakazosimamia shughuli mbalimbali za kila siku lakini akisema Kamati ya Usajili itakuwa ni ya muda na itaongozwa na Hanspoppe Zacharia, Kassim Dewji, Saidi Tulliy, Musley Al Ruweh, Crescentius Magori na Rodney Chiduo.
Aliwataja wajumbe wanaounda kamati ya mashindano itakayokuwa chini ya mwenyekiti, Mohammed Nassor, kuwa ni Iddi Kajuna, Jerry Yambi, Hussein Simba na Mohammed Omary.
Mwenyekiti wa Kamati ya Vijana ni Tulliy, Ally Suru, ambao wote ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Patrick Rweyemamu, Mulamu Nghambi, Madaraka Suleiman na Amina Poyo.

NIPASHE

CHUJI ATUA AZAM, MCAMEOON AMKUBALI

BAADA ya kutangazwa kuachwa na Yanga, kiungo nyota wa zamani wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Athumani Iddi ‘Chuji’ amedaiwa kusajiliwa na mabingwa wa kandanda nchini, Azam kwa mkataba wa muda mfupi na tayari ameanza kujifua mazoezini na wenzake.
Hata hivyo bado uongozi wa Azam haujathibitisha taarifa hizo, ingawa kocha wa Azam Mcameroon amenukuliwa akimwagia sifa Chuji kwa jinsi alivyoshuhudia vitu vyake kwenye mazoezi ya timu hiyo yanayoendelea Chamazi, Dar es Salaam.
Kocha huyo alisema ameridhika na kiwango cha Chuji na kutokana na uzoefu alionao ataisaidia Azam katika msimu ujao na mashindano ya kimataifa watakayoshiriki.
Hata hivyo viongozi wa Azama wamekuwa wagumu kutjhibitisha taarifa hizo kwa madai mwenye maamuzi ya mwisho juu ya Chuji ni kocha ambaye ni wazi ameridhia mkali huyo aliyewahi kuichezea Simba na Polisi Dodioma kuitumikia timu hiyo msimu ujao na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Thursday, July 3, 2014

Suarez azigonganisha Liverpool, Barcelona

MSHAMBULIAJI nyota wa Uruguay aliyefungiwa na FIFA kwa kitendo cha kumng'ata beki wa Italia, Giorgio Chiellini, Luis Suarez amezigoinganisha klabu yake ya Liverpool na Barcelona inayowania saini yake.
Klabu hizo zinatarajia kuanza kufanya mazungumzo juu ya bei ya awali ya paundi milioni 80 ili kuuziana mshambuliaji  huyo.
Mtandao wa michezo wa Sportsmail unafahamu kuwa maofisa wa Liverpool, akiwemo mkurugenzi mtendaji, Ian Ayre, wamekubali kukutana na mkurugenzi wa michezo wa FC Barcelona, Raul Sanllehi,  mjini London ili kujadiliana thamani ya mchezaji huyo mwenye miaka 27.
Barcelona wanatazamiwa kutoa paundi milioni 60 kwa kuzingatia kuwa Suarez amefungiwa miezi minne kucheza soka baada ya kumng`ata beki wa Italia, Giorgio Chiellini.
Liverpool hawapo tayari kushusha bei ya Suarez, lakini wanataka kumhusisha mshambuliaji wa Barcelona Alexis Sanchez kama sehemu ya makubaliano hayo.
Barcelona wanasema mchezaji wao wa kimataifa wa Chile ana thamani ya paundi milioni 35, lakini tayari wameshakataa ofa ya paundi milioni 20 kutoka kwa Juventus ya Italia iliyokuwa na nia ya kumsajili nyota huyo mwenye miaka 25.

Domayo nje Azam kwa miezi minne kisa upasuaji

MABINGWA wa soka nchini, Azam Fc, imesema kiungo wake Frank Domayo atakuwa nje ya uwanja wa muda wa miezi minne kufuatia upasuaji wa mguu aliofanyiwa nchini Afrika Kusini.
Akizungumzia jiji Afisa Habari wa Azam, Jaffar Idd  amesema uchunguzi wa afya wa kiungo huyo aliofanyiwa na mganga mkuu wa klabu hiyo Dk Mwamkemwa ulibaini kuwa Domayo ana matatizo ya msuli wa mguu wake wa kushoto na kwamba atatakiwa kufanyiwa upasuaji.
Domayo alipekwa na uongozi wa Azam wiki iliyopita nchini Afrika Kusini akiambatana na Dk Mwankemwa ambapo juzi alifanyiwa upasuaji katika hospitali ya Vicent Parent na imeelezwa kuwa anaendelea vizuri huku akitarajiwa kurejea nchini Jumapili.
  Afisa Habari huyio amesema kiungo huyo atakuwa nje ya uwanja kwa kipindi miezi minne akiendelea kupata tiba na uangalizi wa karibu wa jeraha lake kabla ya kurejea uwanjani kuitumikia klabu yake hiyo mpya ambayo amejiunga nayo hivi karibuni.

Cameroon yachunguzwa kwa upangaji matokeo Brazil

TIMU ya soka ya taifa ya Cameroon, inachunguzwa kwa tuhuma za upangaji wa matokeo katika mechi zao za Kombe la Dunia waliotolewa hatua ya makundi nchini Brazili.
Maafisa wa Cameroon watapelelezwa kutokana na madai kwamba saba kati ya wachezaji wa timu ya taifa hilo walihusika katika kupanga mechi katika Kombe la Dunia linaloendelea nchini Brazil.
Kamati ya maadili ya shirikisho la kandanda la taifa hilo litachunguza shutuma za "udanganyifu" wa "wachezaji saba wabaya" katika mechi zao tatu za makundi.
Madai hayo yametolewa na gazeti moja la kijerumani na mtu aliyehukumiwa kwa kuhusika na kupanga mechi nchini Singapore.
Cameroon ilipoteza mechi zote za kundi A, ikiwemo ile waliolazwa na Croatia kwa mabao 4-0.
Mchezaji wa 'The Indomitable Lions' Alex Song, alionyeshwa kadi nyekundu kwa kumgota Mario Mandzukic mgongoni katika mechi hiyo, huku wachezaji wenzake Benoit Assou-Ekotto na Benjamin Moukandjo wakizozana baadaye katika mechi hiyo.
Ripoti kutoka katika shirikisho la kandanda la Cameroon lilisema: "Madai yaliyotolewa majuzi kuhusu udanganyifu katika mechi tatu za mwanzo za Cameroon katika Kombe la Dunia la 2014, hasa kati ya Cameroon na Croatia, na vile vile 'kuwepo na wacheza saba wabaya katika timu yetu ya taifa' hayaambatani na maadili na kanuni zinazopendekezwa na usimamizi wetu, pamoja na kanuni za Fifa na maadili ya taifa letu.
"Tuna nia kuu ya kutumia mbinu zote zinazostahili ili kutatua swala hili linalosumbua kwa muda mfupi iwezekanavyo."
Fifa haikusema iwapo ilikuwa ikichunguza swala hilo au la, kwani bodi hiyo inayosimamia kandanda ulimwenguni "ilitaka uchunguzi uwe wazi".

Mbeya City, Prisons kuzipima tiketi za Electronic

Mbeya City
Prisons-Mbeya
TIMU za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) za Mbeya City na Tanzania Prisons zinacheza mechi ya kirafiki Jumamosi (Julai 5 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mechi hiyo ambayo itakuwa ya kwanza kuchezwa jijini Mbeya katika mfumo wa matumizi ya tiketi za elektroniki kwa washabiki wanaoingia uwanjani itaanza saa 10 kamili jioni.
Kiingilio ni sh. 3,000 kwa majukwaa yote ambapo tiketi zimeanza kuuzwa leo (Julai Mosi mwaka huu).
Wakati huo huo, keshokutwa (Julai 3 mwaka huu) kutakuwa na mafunzo ya matumizi ya tiketi za elektroniki yatakayofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya kuanzia saa 3 asubuhi.
Washiriki wa mafunzo hayo ni wasimamizi wa mechi katika uwanja huo, viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA), meneja wa Uwanja wa Sokoine na msaidizi wake, makatibu wa Tanzania Prisons na Mbeya City, maofisa habari wa Mbeya City na Tanzania Prisons, Ofisa Usalama wa MREFA na wasimamizi wa milangoni (stewards).

Stars yapigwa 4 Botswana kujiuliza kwa Lesotho

TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) juzi ilikubali kichapo cha mabao 4-2 kutoka kwa wenyeji wao timu ya Botswana katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika jijini Gaborone.
Mechi hiyo iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa wa Gaborone, ilishuhudiwa hadi mapumziko Stars ilikuwa nyuma kwa mabao 3-0 licha kuonekana timu zote zikishambuliana kwa zamu.
Mabao ya Stars katika mchezo huo wa kirafiki yalifungwa na wachezaji wa klabu ya Azam, Khamis Mcha 'Vialli' na John Bocco 'Adebayor' kwa njia ya penalti.
Kikosi hichio cha kocha Mart Nooij kitashuka dimbani tena siku ya Jumamosi kupepetana na Lesothio katika pambano jingine la kirafiki la kimataifa kabla ya siku inayofuata kurejea nyumbani kujiwinda na mechi yao ya kuwania kufuzu hatua ya makundi ya kucheza Fainali za Kombe la Afrika za mwakani.
Taifa Stars imeweka kambi ugenini kwa ajili ya kujiandaa na mechi yake ya kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Msumbiji itakayofanyika Julai 20 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Stars ambayo ilisonga mbele katika mashindano hayo baada ya kuifunga Zimbabwe mabao 3-2 na kama itafanikiwa kuing'oa Msumbiji katika mechi zao itaangukia kundi moja na timu za Zambia, Cape Verde na Niger ili kuwania kucheza fainali hizo za Afrika zitakazofanyika nchini Morocco.

Tuesday, July 1, 2014

Lionel Messi kuendeleza makali yake Brazil

Lionel Messi
BAADA ya Neymar na Thomas Muiller kushindwa kuongeza bao lolote katika hatua ya 16 Bora ya Fainali za Kombe la Dunia na kusaliwa na mabao yao manne manne, nyota wa Argentina Lionel Messi ana nafasi ya kuwakacha wenzao hao wa kuwania Kiatu cha Dhahabu' iwapo atafunga leo na kumfikia kinara wa mabao wa sasa katika fainali hizo James Rodriguez mwenye mabao matano.
Rodriguez wa Colombia alifikisha idadi hiyo ya mabao baada ya kufunga mabao mawili wakati akiivusha nchi yake hadi Robo Fainali mbele ya timu ya Uruguay iliyokosa huduma za Luis Suarez aliuyefungiwa na FIFA kwa kosa la kumng'ata Giorgio Chiellini wa Italia.
Messi ambaye amefunga katika mechi zote zilizopita nchi yake leo itakuwa ikikabiliana na Uswisi katika mechi ya kuamua hatma ya timu ipi ya kuungana na Brazil, Uholanzi, Colombia, Ufaransa na Ujerumani katika Robo Fainali zitakazoanza Ijumaa.
Nyota huyo anayekipiga Barcelona katika fainali za mwaka huu ameonekana moto wa kuotea mbali kiasi cha kubashiriwa kuwa Mchezaji Bora na hata kunyakua kiatu cha Dhahabu kama ataendelea kutupia mabao kambani akichuana na wakali wenzake.
Nahodha huyo wa Argentina anategemewa kuendelea kuwatesa mabeki wakati wakikabiliana na Uswisi ambao kupitia kocha wake, Ottmar Hitzfeld ameahidi kutumia 'kijiji' kumkaba ili asiwaletee madhara kama alivyowafanyia timu hiyo katika fainali hizo za Brazil.
Nyota wenzake wa Brazil , Neymar na Muiller wa Ujerumani walishindwa kufunga bao lolote katika mechi zao za 16 Bora na kuendelea kusaliwa na mabao yao manne kama aliyonayo Messi na kuachwa kwa idadi ya bao moja na Rodriguez ambaye ameonekana ni mbadala halisi ya Radamel Falcao aliyezikosa fainali hizo kwa kuwa majeruhi.
Mbali na mechi ya Argentina na Uswisi pia leo kutakuwa na pambano jingine la kumalizia ratiba ya 16 Bora kati ya Ubelgiji dhidi ya Marekani.
ORODHA YA WAFUNGAJI:
5-James Rodriguez (Colombia)
4- Lionel Messi (Argentina)
    Thomas Muiller (Ujerumani)
    Neymar (Brazil)
3- Karim Benzema (Ufaransa)
    Arjen Robben (Uholanzi)
    Robin van Persie (Uholanzi)
    Xherdar Shaqiri (Uswisi)
    Enner Valencia (Ecuador)
2- Andre Ayew (Ghana)
    Wilfried Bony (Ivory Coast)
   Tim Cahill (Australia)
   Clint Dempsey (Marekani)
   Memphis Depay (Uholanzi)
   Asamoah Gyan (Ghana)

Kisiga afunikwa na Kisiga Mchangani

Na Adam Fungamwango
KIUNGO mshambuliaji wa Mtibwa Sugar Shaaban Kisiga, juzi alikutana na mchezaji mwingine kwenye uwanja wa shule ya msingi Mwananyamala anayetumia jina lake ambaye alimfunika vilivyo.
Shaaban Kisiga huyo 'feki' alikuwa anaichezea timu Morning Star ya Msasani, huku Kisiga mwenyewe akiwa anaichezea Morning Star ya Kiwalani.
Hata kwenye fomu za majina kwa waamuzi, pamoja na timu zote mbili kuwa na majina yanayofanana, lakini pia ilikuwa na majina yanayofanana, kila timu ikiwa na Shaaban Kisiga.
Ina maana kukawa na Kisiga halisi yaani 'original' na mwingine 'feki'.
Katika mchezo huo uliochezeswa na waamuzi wa kike watupu, Mwanahamisi Matiku, Germina Simon na Neuru Mushi, Kisiga 'feki' alionekana kumfunika Kisiga halisi kiasi cha kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye mechi ya robo fainali ya kwanza ya Wadau Cup.
Bao la Morning Star ya Msasani dhidi ya Morning Star ya Kiwalani lilifungwa na Oscar Magari katika dakika ya 52, baada ya pande safi kutoka kwa Kisiga 'feki'.
Mabeki wa Morning Star ya Msasani walikuwa na kazi moja tu, kuhakikisha kuwa Kisiga 'original' ambaye alicheza nafasi ya ushambuliaji haleti madhara na kweli walifanikiwa.
Timu hizo mbili zitarudiana wiki ijayo kwenye mechi ya robo fainali ya pili itakayochezwa kwenye uwanja huo huo wa shule ya msingi Mwananyamala.

Mbowe apigwa stop kugombea tena CHADEMA

Mwqenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe
Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Mutungi.
 
OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa imesema haitambui kuondolewa kwa kipengele cha ukomo wa uongozi uliofanywa na Chadema bila kufuata idhini ya mkutano mkuu wa chama hicho.
 
Mwaka 2006, Katiba ya Chadema ilifanya marekebisho yaliyoruhusu wanachama kugombea uongozi bila ukomo wakati awali, waliruhusiwa kugombea kwa vipindi viwili vya miaka mitano.
 
Barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema, inasema kipengele hicho katika Ibara ya 6.3.2 (C) kiliondolewa kwenye katiba bila idhini na mkutano mkuu wa chama hicho. 
Mutungi alisema baada ya kupitia muhtasari wa kikao cha mkutano mkuu wa mwaka 2006 suala la kuondoa kipengele cha ukomo wa uongozi halikuonyesha kujadiliwa katika mkutano huo.
Hata hivyo, akizungumza kwa simu jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema kipengele hicho kiliondolewa kwa vikao vya chama ambavyo ni wilaya na mkoa.
 
“Mjadala kuhusu ukomo wa uongozi ulishamalizika na haujadiliwi tena, ulishapitishwa na vikao halali vya chama, mkutano mkuu ulipitisha yale yaliyoamuliwa na vikao vya chini,” alisema Dk Slaa.
 
Hata hivyo, Jaji Mutungi alisema: “Chadema wamefanya mabadiliko bila kufuata katiba”
 
Alishauri waitishe mkutano rasmi na halali kwa mujibu wa katiba ya chama hicho ili waweze kurekebisha kasoro zilizopo.
Alisema kama chama hicho hakitarekebisha kasoro hiyo, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa haiwezi kuitambua ibara hiyo.
Alisema ingawa hoja hiyo iliwasilishwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba ambaye sasa si mwanachama wake, bado hoja hiyo ni muhimu na inahitaji kufanyiwa kazi.
 
“Ni vizuri mkaifanyia kazi hoja hiyo bila kujali kwamba aliyeiwasilisha si mwanachama tena wa Chadema,” alisema katika barua hiyo.
Credit:Info is Hot 

Subira ya Shaa sasa hiyooo

VIDEO ya wimbo mpya wa msanii Sara Kais 'Shaa' uitwao Subira unatarajiwa kuachiwa Ijumaa wiki hii baada ya kukamilika kwa kila kitu.
Meneja wa msanii huyo, Said Fella 'Mkubwa' alisema kuwa video hiyo imekamilika na wameshakabidhiwa na sasa wataanza kuisambaza wiki hii kabla ya kurushwa hewani siku ya Ijumaa.
"Ile video mpya yaShaa iitwayo 'Subira' itaachiwa rasmi siku ya Ijumaa, hivyo mashabiki waliokuwa wakiisubiri wajiandae kuipokea ni bonge la wimbo kama ilivyokuwa kwa 'Sugua Gaga'," alisema Fella.
Shaa yupo chini ya lebo ya Mkubwa na Wanae na wimbo huo ni wa pili kwake baada ya 'Sugua Gaga' unaoendelea kutamba kwenye vituo vya redio, runinga na mitandao ya kijamii.

Masai anasikilizia Yero Masai

Yero Subhai! Gilliard Severine 'Masai Nyota Mbofu latika pozi
MCHEKESHAJI mahiri nchini, Gilliad Severine 'Masai Nyota Mbofu' amesema bado hajaamua kufanya nini kwa sasa baada ya kuachana na kampuni ya Al Riyamy akidai anasikilizia kazi yake mpya 'Yero Masai' aliyoachia hivi karibuni.
Akizungumza na MICHARAZO mwishoni wa wiki, Masai alisema bado hajajua aibukie wapi kwa sasa akiendelea na mchakato wake wa kutoa video ya wimbo wake uitwayo 'Masai ya Wapi' alioimba na Christian Bella wa Malaika Band.
"Kwa kweli mpaka sasa sijajua hatma yangu itakuwaje, ila nahangaika kutoa video ya 'Masai ya Wapi' huku nikisikilizia kazi yangu mpya iliyopo hewani kwa sasa iitwayo 'Yero Masai' niliyoimba na Rich Mavoko na Kitokololo", alisema.
Mchekeshaji huyo alitangaza kujiondoa kwenye kampuni ya Al Riyamy inayozalisha filamu  na vichekesho vya kipindi cha Vituko Show na alisema anajiopanga kuibuka kampuni yoyote itakayokuwa ikimhitaji au aendelee kufanya kazi mwenyewe kama msanii huru.

Young Hassanal kumbe ni Mr Pendwapendwa

Muimbaji Hassani Ally
MUIMBAJI nyota wa muziki wa taarab wa kundi la Kings Modern, Ally Hassan 'Young Hassanal' anajiandaa kuingiza sokoni albamu yake binafsi ya 'Nyongo Mkalia Ini', huku akiendelea kutamba na wimbo mpya wa 'Mr Pendwapendwa'.
Wimbo huo upo kwenye albamu ijayo ya kundi lake la King Modern inayoandaliwa kabla ya kuja kuachiwa baadaye.
Akizungumza na MICHARAZO, muimbaji huyo alisema kuwa albamu yake aliyoizindua Machi mwaka huu itaingia sokoni wakati wowote kuanzia sasa ili mashabiki wake waipate.
"Naada ya uzinduzi uliofana kwa sasa nipo hatua za mwisho kabla kuingiza sokoni albamu yangu ya 'Nyongo Mkalia Ini'," alisema.
Young Hassanal aliongeza, wakati akijiandaa kuingiza sokoni albamu hiyo, kundi lake la Kings lipo katika maandalizi ya mwisho kukamilisha albamu yao mpya itakayokuwa na nyimbo tano.
"Albamu hiyo tayari inatambaulishwa hewani na wimbo nilioimba wa 'Mr Pendwapendwa' ambao unafanya vyema kwenye vituo vya redio," alisema.



Diamond: Asiyekubali kushindwa si mshindani

NYOTA wa nyimbo za 'My Number One' na 'Mdogomdogo', Naseeb Abdul 'Diamond Platnumz, ameonyesha uungwana kwa kuamua kukubali matokeo ya kushindwa kutwaa tuzo za kimataifa za BET 2014 alizokuwa akiwania na wakali wengine wa Afrika na kushuhudia Mnigeria Davido akimuangusha kwa mara nyingine tena.
Diamond alikuwa akiwania tuzo hiyo kupitia kipengele cha msanii wa kimataifa toka Afrika (Best International Act-Africa) na kujikuta akiangushwa na Davido ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu na Mnigeria huyo aliyemshirikisha katika wimbo wake wa 'My Number One remix' kumbwaga katika tuzo za MTV Africa 2014.
Dakika chache baada ya kutangazwa kwa mshindi wa tuzo hizo zilizofanyika nchini Marekani, Diamond alitupia ujumbe katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii akieleza kukubali matokeo hayo na kuwashukuru wote waliomuunga mkono kwenye tuzo hizo.
"Tusipopenda kukubali matokeo na ushindi wa wenzetu basi daima hatutaweza kuwa washindani...Muhimu ni kujua wapi tulipotoka na wapi tulipo leo, katika nchi zaidi ya 20 zenye wasanii zaidi ya milioni 40 kuchaguliwa Tanzania ni fursa, heshima na hatua kubwa...Cha muhimu ni kuitumia vyema fursa hii na kuhakikisha mwakani tunapiga hatua. Asante sana kwa wote wanaozidi kunisapoti," aliandika.
Katika tuzo hizo Diamond alikuwa akichuana na Davido pamoja na Mafikizolo wa Afrika Kusini, Sarkodie wa Ghana, Tiwa Savage na Toofan wa Togo. Nyota ya Diamond inazidi kung'aa hata hivyo baada ya Mafikizolo kumuomba kufanya naye wimbo.

Coutinho asainishwa mkataba wa miaka miwili Yanga


 


MABINGWA wa zamani wa kandanda nchini Yanga imeendelea kujipanga na mikakati ya kurudisha ubingwa walionyang'anywa na Azam msimu uliopouta kwa kumsainisha kiungo mshambuliaji kutoka Brazil.
Kiungo huyo Andrey Marcel Ferreira Coutinho raia wa Brazil jana alisaini mkataba wa miwili kuitumikia timu ya Young Africans (Yanga)  kwa ajili ya michuano mbalimbali ikiwemo ya Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Katibu mkuu wa Young Africans  Bw Beno Njovu amesema usajili wa mchezaji Coutinho ni sehem ya muendelezo wa maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu na kama ilivyokawaida wao mambo yao ni kimyakimya.
Coutinho ambaye alizaliwa tarehe 12 Januari 1990 amekulia kwenye mji wa Berem ambapo alianza kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Paysandu Sports Club kabla ya kwenda nchini Asia katika nchi ya Myanmar katika klabu ya Rukhapura United.
Mpaka anajiunga na klabu ya Young Africans Andrey Coutinho alikuwa akichezea timu ya Castanhal EC iliyopo kwenye Ligi Daraja la pili ambao aliweza kuichezea kwa michezo yote  ya mzunguko wa pili mwaka 2014.
Katika hatua nyingine kikosi cha Young Africans kinatarajia kuendelea na mazoezi kesho chini ya kocha Marcio Maximo katika ufuke wa Coco Beach ikiwa ni siku yake ya kwanza kuanza kazi baada ya leo kuwa na mkutano wa ndani na wachezaji wake pamoja na benchi la ufundi.

Mwenyekiti CCK yawapuuza wanaokiwabeza chama chao

Constantine Akitanda (kulia) alipokuwa akipokea hati ya usajili wa chama chake toka kwa aliyekuwa msajili wa vyama nchini, John Tendwa
MWENYEKITI wa Chama cha Kijamii (CCK), Constantine Akitanda, amewapuuza wanaokibeza chama chake kwa maamuzi yao ya kufanya ziara mikoani kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu na manufaa ya kupatikana Katiba Mpya.
Aidha, chama hicho, kimesisitiza kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) ndiyo adui yao namba moja, hivyo katu hakiwezi kukubali kuwa kibaraka katika kuwasafishia njia ya kuendelea kukaa madarakani zaidi kama baadhi ya watu wasiokitakia mema chama hicho wanavyodai.
Akizungumza kwa njia ya simu jana akiwa safarini, Akitanda, alisema CCK na chama mshirika cha NRA wameamua kufanya ziara hiyo mikoani kutoa elimu juu ya upotoshaji unaofanywa na baadhi ya wanasiasa kuhusiana na Katiba Mpya.
Alisema ziara hiyo wanaifanya kwa nguvu zao wenyewe kama njia ya kuonyesha ukomavu wao na kiu kubwa ya kuwazindua wananchi ambao wamekuwa 'kizani' kuhusu mchakato huo wa Katiba.
"Wale wanaotubeza wanafanya hivyo kwa sababu wana wivu na hawatujui vyema, CCK kama taasisi ina mipango na mikakati yake na inajiendesha kwa kujitegemea bila msaada wa yeyote kama baadhi ya vyama vinavyofanya," alisema.
Alisema dai kwamba wanafanya ziara hiyo mikoani kwa ufadhili wa CCM ili kuvuruga mambo ambayo Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umekuwa ukihubiri kuhusu mchakato mzima wa katiba, ni upuuzi.
"Tulishatangaza tangu awali kuwa, adui yetu namba moja ni CCM, sasa iweje adui huyo aje awe mfadhili wetu inaingia akilini kweli, watu waache mtazamo hasi kwa vyama vinavyotofautina na vingine," alisema.
Alisema chama hicho kipo tayari kutofautiana na chama chochote katika suala zima la upotoshaji wa Katiba Mpya kwani Rasimu ya Katiba Mpya kwani ina mambo mengi ya msingi yanayowagusa wananchi moja kwa moja kuliko suala la mfumo na muundo wa serikali.

"Vyama vidogo vimekuwa vikionekana mamluki vinapotofautiana na vyama vikuu, ila ukweli vyama vyote vina nafasi sawa mbele ya Msajili wa Vyama na Watanzania na tunachokifanya ni sahihi," alisema.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Akitanda na Mwenyekiti wa NRA, Rashid Mtuta walitangaza nia yao ya kuzungumza baadhi ya mikoa ili kutoa elimu kuhusu masuala ya Katiba kilichopokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya vyama vya siasa.

Mwanafunzi wa RUCO aliyechomwa moto Iringa afariki

Mwanafunzi (LEMA) aliyejeruhiwa kwa moto
Mwanafunzi huyu Daniel Lema alikuwa akisoma mwaka wa nne, kozi ya sheria katika chuo kikuu kishiriki cha Mt. Augustino cha Ruaha Iringa (Ruaha University College maarufu kama RUCO).
Mwanafunzi huyo alichomwa moto wiki iliyopita akihusishwa na tuhuma za wizi.
Baada ya kulazwa katika hospitali ya mkoa wa Iringa kwa wiki moja sasa, mwanafunzi huyo ameaga dunia majira ya saa nane mchana.
Taratibu za kuaga mwili wake zinaendelea kufanywa na uongozi wa chuo hicho, ndugu na wanafunzi wenzake.

Taarifa za awali zinaonesha kwamba mwili wake utaagwa kesho kuanzia saa moja asubuhi kabla ya kusafirishwa kupelekwa kwao mkoani Kilimanjaro kwa mazishi. Mazishi ya kijana huyo yanatarajia kufanyika jumatano ya wiki hii.

Juni 24, mwaka huu Daniel Lema alikutwa na mkasa wa kukamatwa na kuchomwa moto wakati akitoka kuangalia fainali za kombe la dunia katika moja ya Bar za mjini Iringa.

Akiwa amelewa aliingia katika moja ya migahawa ya mjini hapa akitafuta chakula, ilikuwa majira ya saa tano mwanafunzi huyo aliingia kwenye mgahawa ambao biashara hiyo ilikua imefungwa.

Binti aliyekuwepo katika mgahawa huo alianza kupiga kelele akidhani kavamiwa na mwizi. Mlinzi wa eneo hilo (mmasai) alimvaa kijana huyo na kumshambulia.

Baada ya tukio hilo taarifa zinasema walitokea watu wawili waliojitambulisha kuwa ni askari; askari hao walizuia watu waliozidi kujitokeza katika eneo hilo kuendelea kumpiga kijana huyo.

Wakiwa njiani, wananchi hao waliokuwa wakifuatilia kama atafikishwa kituo cha Polisi waliona wanachalewa na kuamua kuchukua sheria mkononi kwa kuendelea kumpiga kabla ya kumchoma moto.
chanzo: http://frankleonard.blogspot.com

Hatimaye Suarez aiomba radhi kwa kosa la kung'ata mtu Brazil

Suarez alipomng'ata Chiellini
MSHAMBULIAJI 'mtukutu' wa Uruguay aliyefungiwa na FIFA kwa kosa la kumng'ata mchezaji mwenzake wa Italia, Luis Suarez amepoza shutuma dhidi yake baada ya  kuomba radhi.
Suarez alimng'ata bega beki wa Azzuri Giorgio Chiellini katika mechi yao ya makundi na kufungiwa na FIFA kwa muda wa miezi minne.
Katika hali isiyo kawaida nyota huyo ameomba radhi usiku wa jana na kuahidi hatorudia kufanya kosa kama hilo, japo inaelezwa Barcelona ilimpa shinikizo la kufanya hivyo ili kuweza kuiwania saini yake.
Siku nne baada ya kufungiwa miezi minne na ameambia FIFA kwamba tukio hilo lilitokea katika mechi ya Kombe la Dunia kati ya Uruguay na Italia mjini Natal lilitokana na kushindwa kujizuia.
Mshambuliaji huyo wa Liverpool ameibuka kikamilifu na kujutia kosa lake. Lakini kuomba kwake radihi kunakuja katika wiki ambayo habari zimevuma mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 anatakiwa kwa dau la Pauni Milioni 80 Nou Camp.
Gary Lineker, mshambuliaji wa zamani wa Barcelona, amesema klabu hiyo ya Katalunya imemuambia Suarez bombe msamaha kama wanataka waendelee na jitihada za kumnunua.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwenye ukurasa wake wa Twitter, Suarez amesema: "Baada ya siku kadhaa za kuwa nyumbani na familia yangu, nimepata fursa ya kutuliza jazba na kufikiria haswa kilichotokea katika mechi ya Italia na Uruguay Juni 24, 2014.
"Kutokana na kilichotokea na yote yaliyofuatia baadaye, kiasi cha kuathiri hata kiwango cha timu yangu ya taifa, ukweli ni kwamba mchezaji mwenzangu Giorgio Chiellini ameumizwa na kilichotokea kwa kumng'ata,".
"Kwa hili: Najuta kwa kiasi kikubwa kufanya hivyo. Naomba radhi kwa Giorgio Chiellini na familia ya soka kwa ujumla. nauambia umma kwamba halitatokea tukio kama hili tena,".
Beki wa Juventus, Chiellini ameretweet msamaha wa Suarez katika mtandao wake, baada ya awali kusema adhabu ya kumfungia miezi minne Suarez ni kubwa. 
Chiellini amejibu kwenye akaunti yake ya Tweeter moja kwa moja akisema: "Yote yamesahaulika. Natumai FIFA itakupunguzia adhabu,".

Afrika majanga! Nigeria, Algeria zafurushwa Brazil



Andre Schuller akiifungia Ujerumani bao la kuongoza
WAAFRIKA hawana chao tena kwenye Fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini Brazil baada ya usiku wa jana timu pekee mbili zilizokuwa zimesalia kwenye michuano hiyo kung'olewa na timu za Ulaya.
Super Eagles ya Nigeria ilianza kuaga mapema na kuendeleza mzimu wa kushindwa kuvuka hatua ya 16 katika fainali zake zote ilizocheza kwa kukubali kipigio cha mabao 2-0 toka kwa Ufaransa, huku baadaye Mbweha wa Algeria walikufa kiume kwa kulazwa mabao 2-1 katika muda wa nyongeza baada ya kukomaa kwa dakika 90 bila kufungana na Ujerumani.
Katika mechi ya Nigeria na Ufaransa iliyoanza mapema, Nigeria ilishindwa kuonyesha soka kama ilivyoumana na Argentina na kuruhusu Ufaransa kuwatawala na kujipatia mabao yake kupitia ya Paul Pogba na jingine la kujifunga la beki Joseph Yobo na kuhitimisha mbio zao kwenye fainali hizo zinazoingia hatua ya Robo Fainali.
Pogba anbayekipiga Juventus alifunga bao lake katika mchezo huo uliochezwa uwanja wa Garrincha, Brasilia, katika dakika ya 79 kwa njia ya kichwa na dakika mbili baadaye Yobio alijhifunga bao katika harakati za kuiokoa mpira wa krosi na kuwafanya Tai hao wa Kijani kurejea nyumbani kama ilivyokuwa kwaIvory Coast, Cameroon na Ghana zilizoaga mapema na kukwama kutimiza ndoto za kutinga Robo Fainali kwa mara ya kwanza.
Katika mechi iliyiofuatailiyiochezwa Uwanja wa Beira-Rio mjini Porto Alegre, dakika 90 za mchezo kati ya Ujerumani na Algeria zilishuhudia timu hizio zikiwa nguvu sawa kwa kutofunaga na kuiongezewa dakika 30 zilizokuwa mwiba kwa Waafrika baada ya Andre Schurrle kufunga bao dakika mbili tangu kuanza kwa muda huo kabla ya Mesut Ozil kuiongeza la pili dakika ya 119.
Hata hivyo Algeria walioonyesha soka la ushindani katika michuano hiyo tofauti na walivyokuwa wakichukuliwa awali walipata bao la kufutia machozi kwenye dakika za ziada kabla ya mchezo kumalizika kupitia kwa Abdelmoumene Djabou.
Kwa matokeo hayo ni kwamba Ujerumani na Ufaransa watakutana kwenye mechi ya Robo Fainali huku timu za Afrika zikirudi nyumbani kishujaa hata hivyo.

Taifa Stars uso kwa uso na Botswana kirafiki leo Gaborone

Kikosi cha Taifa Stars
KIKOSI cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars jioni ya leo inatarajiwa kushuka kwenye dimba la Taifa la Botwana mjini Gaborone kuumana na wenyeji wao Botswana katika pambano la kirafiki la kimataifa.
Pambano hilo ni maalum kwa Stars kwa ajili ya kujiwinda na mchezo wao wa kuwania kufuzu kwenye Fainali za Kombe la Afrika hatua ya makundi dhidi ya Msumbiji mechi itakayopigwa wiki tatu zijazo.
Stars inayonolewa na kocha Mart Nooij, ipo Botswana tangu wiki iliyopita ikijifua na itashuka dimbani leo mjini Gaborone bila winga wake nyota Mrisho Ngassa aliyekuwa ameenda Afrika Kusini kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Free State Stars, p-ia itakosa huduma za nyota wake wengine kama Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaocheza TP Mazembe.
Hata hivyo bado ina kikosi bora kabisa ambacho kitaweza kutoa upinzani kwa wenyeji ambao wanakutana nao kwa mara ya kwanza tangu walipokutana mara ya mwisho mwaka 2012 katika pambano la kirafiki la kimataiafa lililoisha kwa sare ya 3-3 nchini humo.
Taarifa kutoka Botwana zinasema kuwa wachezaji wote wapo fiti tayari kwa mechi hiyo na baada ya hapo itashuka tena dimbani Ijumaa ya Julai 11 kuumana na Lesotho katika mchezo mwingine wa kirafiki wa kimataifa kabla ya kurejea nyumbani kuwasubiri Mamba wa Msumbiji.
Stars ambayo haijashiriki Fainali hizo za Afrika tangu ilipofanya hivyo mara ya kwanza na mwisho mwaka 1980 itarudiana na Mamba Agosti 2 mjini Maputo kama itafanikiwa kuvuka hatua hiyo itaingia kwenye kundi moja na timu za Zambia, Cape Verde na Niger kuwania kufuzu fainali zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.

Saturday, June 28, 2014

Kimbembe cha 16 Bora leo, nani kufuzu Robo Fainali?!


Colombia
Uruguay
KIVUMBI cha hatua ya mtoano cha 16 Bora cha Fainali za Kombe la Dunia 2014  kinatarajia kuanza kutimka rasmi leo wakati wenyeji Brazil na nchi nyingine tatu za Amerika Kusini zitakapochuana kuwania nafasi ya kutinga hatua ya Robo Fainali ya michuano hiyo inayoendelea nchini Brazil.
Brazil chini ya nyota wake wakiongozwa na Neymar watakawakabili majirani zao Chile, huku Colombia itapepetana na Uruguay itakayomkosa nyota wake Luis Suarez aliyefungiwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa kitendoi cha kumuuma mchezaji Giorgio Chiellini wa Italia.
Wenyeji waliongoza msimamo wa kundi A mbele ya Mexico watashuka dimbani mapema saa 1 usiku kwenye uwanja wa Governador Magalhães Pinto, kuwakabili Chile watakaomtegemea Alexis Sanchez katika mechi inayosubiriwa kwa hamu kuona kama Brazil watatoka salama kwa wapinzani wao.
Ingawa rekodi zinaonyesha kuwa, timu hizo zimeshakutana mara 68 na Brazil ikiwatambia wapinzani wao mara 48 na kufungwa mara 7 na kutoka sare michezo 13, huku wenyeji hao wakifunga jumla ya mabao 159-58 katika michezo waliyokutana, bado Chile siyo timu ya kubezwa.
Katika fainali za mwaka huu wakiwa kundi B waliweza kumaliza katika nafasi ya pili bila kutarajiwa mbele ya waliokuwa mabingwa watetezi Hispania na Australia walizozipatia katika mechi za makundi.
Katika michuano ya  Kombe la Dunia hatua ya Mtoano, Brazil na Chile zimekutana mara 3 na zote Brazil kushinda. Mwaka 1962, kwenye Nusu Fainali, Brazil ilishinda 4-2. Mwaka 1998, Raundi ya Mtoano ya Timu 16, Brazil walishinda 4-1 na huko Afrika Kusini, Mwaka 2010 pia Raundi ya Mtoano ya Timu 16, Brazil ilishinda 3-0.
Hata hivyo tayari kocha wa Chile, Jorge Luis Sampaoli Moya kutoka Argentina amesema watashuka dimbani leo kuhakikisha wanapata matokeo bora ili kuona kikosi chake kinavuka hatua hivyo, licha ya kukiri ni mtihani mgumu mbele ya Brazil yenye nyota kama Neymar.
Cha kuvutia katika mechi hiyo ni kwamba itachezeshwa na refa Howard Webb kutoka England ambaye hii itakuwa ni mara yake ya pili kuzipambanisha timu hizo katika hatua kama hiyo.
Ndiye aliyezihukumu katika Fainali zilizopita nchini Afrika Kusini ambapo Brazil waling'ara kwa kushinda kwa mabao 3-0 kabla ya kwenda kung';oka mbele na kuziacha Hispania na Uholanzi zikicheza fainali.
Pambano jingine litakalochezwa leo litazikutanisha timu za Colombia na Uruguay pambano litakalochezwa usiku wa saa 5 kwenye uwanja wa mkubwa wa Maracana.
Uguruay itashuka dimbani bila huduma za Suarez aliyerudishwa nyumbani kutokana na kitendo cha kufungiwa na FIFA kwa kosa la kumng'ata mchezaji wa Italia Giorgio Chiellini wakati wa mechi ya kufungia pazia la hatua ya makundi na Uguguay kushinda kwa bao 1-0 na kutinga bila kutrarajiwa nyuma ya Costa Rica.
Pambano hilo linatarajiwa kuwa tamu pengine kuliko lile la Brazil na Chile kutokana na Colombia kuwa miongoni mwa timu zisizotabirika na kati ya chache zilizoshinda kwa asilimia 100 michezo yao ya makundi.
Ikiongozwa na James Rodriguez aliyeziba kwa mafanikio pengo la Radamel Falcao ambaye aliondolewa kwenye kikosi hicho kutokana na majeraha, Colombia inatarajiwa kutoa upinzani mkali.
James Rodriguez ana mabao matatu mpaka sasa kwenye michuano hiyo akishika nafasi ya pili pamoja na nyota wengine wa timu zilizoshiriki michuano hiyo na atakuwa akisaidiana kusaka ushindi kuvuka hatua hiyo na wachezaji wenzake kama Jackson Martínez,Armero, Cuadrado na Gutierrez.
Hata hivyo Uruguay pamoja na kumkosa Suarez, bado ina silaha kali kama Edinson Cavani, Diego Godin, Arevalo na wengine kuhakikisha wanafanya kweli katika mechi hiyo ambayo itakuwa ni ya 15 kwa timu hizo kukutana katika michezo mbalimbali tangu mwaka 2005.
Rekodi zinaonyesha katika kukutana huko, Uruguay imeitambia Colombia mara 8 na kupoteza mechi nne na mbili zilizosalia walitoshana nguvu kwa kutoka sare.
Je, ni Brazil au Chile itakayokuwa ya kwanza kufuzu robo fainali na Colombia itaendelea kuwa mnyonge kwa Uruguay na kupigwa kumbo kutinga hatua inayofuata au watajitutumua na kuinyuka Uruguay bila ya Suarez? Tusibiri tuone baada ya kumalizika kwa mechi hizo kabla ya kesho kushuhudia kitupe kingine.

Liverpool sasa kumuua Suarez kuwabeba Lallana na Markovic

Suarez akiwajibika siku ya mechi dhidi ya England kabla ya kuja kuharibu wakiumana na Italia
KLABU ya soka ya Liverpool ipo kwenye mpango wa kumuuza nyota wake Luis Suarez katika klabu ya Barcelona, ili kupata fedha za kuwanyakua Adam Lallana na Lazar Markovic.
Barcelona imetajwa kuoingoza mbio za kumnyakua mchezaji huyo aliyefungiwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) baada ya kumng'ata beki wa Italia Giorgio Chiellini .
Klabu hiyo ya Hispania imeweka wazi kuwa hata kama Suarez amefungiwa miezi minne kucheza soka, hiyo haizuii nia yao ya kumsajili na mpaka sasa Liverpool hawajahangaika kutafuta mbadala wa mshambuliaji huyo hatari.
Ingawa Liverpool walikuwa wanaweka ngumu kwa dau hilo, lakini baada ya kupokea taarifa za FIFA kuhusu kumfungia Suarez wamelazimika kukubali na kumruhusu Muurguay huyo kuondoka klabuni hapo.
Licha ya kufungiwa, Liverool wanaamini Barcelona inaweza kulipa paundi milioni 80 na tayari mmiliki mkuu wa klabu hiyo John W Henry anaonekana kutokuwa tayari kumuuza kwa bei rahisi.
Mwanasheria wa Suarez Alejandro Balbi alikuwa Barcelona kujadili hatima ya mteja wake, wakati kocha mpya wa Barca Luis Enrique alisema hakuna tatizo lolote juu ya kumsajili nyota huyo mwenye miaka 27.
Alimfananisha Suarez na mshambuliaji gwiji wa Barca Hristo Stoichkov na alisema : ‘Stoichkov kiukweli aliwahi kufanya madhambi makubwa dhidi ya mwamuzi, lakini aliendelea kufirika kuwa mcheza mkubwa".
Kama Liverpool watamuuza Suarez kwa paundi milioni 80, hiyo itakuwa biashara nzuri kwa Brendan Rodgers ambapo atatumia mkwanja huo kuimarisha kikosi chake.
Wachezaji ambao Liverpool inawapigia jaramba kuwanasa ni Adam Lallana kutoka Southampton anayetajwa atakuwa mali ya Vijogoo hao wekundu  saa 24 zijazo baada ya Southampton kukubali ofa ya paundi milion 25 kwa mshambuliaji huyo wa England, na hii ni baada ya kupita wiki nne tangu apokee simu kutoka kwa maofisa wa Anfield ambao pia wameanza mbio za kumuwania mchezaji wa Benfica, Lazar Markovic.
Mserbia, Markovic ni moja ya wachezaji bora wenye umri mdogo katika soka la Ulaya na bei yake ni paundi milioni 20.

Neymar, Muiller, Messi wabanana kuwania kiatu cha Dhahabu

Neymar wa Brazil
Lionel Messi wa Argentina
Thomas Muiller wa Ujerumani  
WAKATI  kinyang'anyiro cha hatua ya mtoano ya 16 Bora ikianza rasmi leo kwa michezo miwili itakayozikutanisha timu za Amerika Kusini, hatua ya makundi ya Fainali za Kombe laDunia 2014 imevunja rekodi.
Jumla ya mabao 136 yamefungwa katika hatua hiyo, sita zaidi ya yale yaliyofungwa katika fainali za 2002.
Wachezaji watatu, Lionel Messi wa Argentina, Neymar wa Brazil na Thomas Muiller wa Ujerumani wanachuana kileleni katika orodha ya wafungaji bora.
Kila moja kati ya wachezaji hao amefunga mabao manne wakifuatiwa na wachezaji sita wenye mabao matatu kila mmoja.
Neymar ana nafasi ya kuongeza idadi ya mabao yake kama leo ataendelea kucheka kwenye mechi yao na Chile kuwania kufuzu Robo Fainali.
Messi atakuwa na nafasi ya kuendelea kunguruma wakati atakapoiongoza Argentina kuvaana na Uswisi siku ya Jumatatu katika mechi nyingine ya 16 Bora.
Ukiondoa wakati hao wenye mabao manne, wachezaji wenye magoli matatu kila mmoja ni pamoja na Robin van Persie, Arjen Robben wote wa Uholanzi, Karim Benzema wa Ufaransa, Enner Valencia wa Ecuador, James Rodriguez wa Colombia na Xherdan Shaqiri wa Uswisi.
Kati ya hapo ni Valencia tu ndiye hana nafasi ya kuongeza idadi yake ya mabao kwa vile timu yake imeshaaga michuano hiyo nchini Brazili.
Katika orodha ya wafumania nyavu hiyo pia wapo wachezaji wenye mabao mawili mawili ambao ni;Tim Cahill wa Australia, Mario Mandzukic wa Croatia, Martinez wa Colombia, Dempsey wa Marekani, Wilfried Bony wa Ivory Coast, Andre Ayew wa Ghana, Asamoah Gyan wa Ghana, Ahmad Mussa wa Nigeria na Slimani wa Algeria.
Ukimuondoa Dempey wa Marekani, Mussa wa Nigeria na Slimani wa Algeria waliosalia timu zaoi zimeshaaga michuano na hivyo hawana nafasi ya kuongeza idadi.

Mashetani Wekundiu wazidi kujiimarisha England

Jembe Jipya! Luke Shaw akiwa na jezi mpya ya klabu yake ya Manchester United
Ander Herrera alipotangazwa ramsi kujiunga kwa Mashetani Wekundu
MABINGWA wa zamani wa England, Manchester United imezidi kuimarisha kikosi chake baada ya kufanikiwa kumsainisha beki wa kushoto wa Southamptom na timu ya taifa ya nchi hiyo iliyotolewa kwenye Kombe la Dunia, Luke Shaw.
Kwa mujibu wa duru za kandanda za England zinasema kuwa, Mashetani Wekundu hao wamekamilisha uhamisho wa Shaw kwa gharama za Pauni Milioni 31.5 kwa mkataba wa miaka minne.rd.
Mchezaji huyo amekamilisha vizuri vipimo afya katika Uwanja wa mazoezi wa United, Carrington na ameambiwa atakuwa beki wa kushoto chaguo la kwanza la kocha Louis van Gaal.
Inafahamika amehakikishiwa namba na beki mkongwe mwenye umri wa miaka 33, Patrice Evra, ambaye atabakia United, anatarajiwa kupunguziwa majukumu klabuni hapo. 
Usajili wa Shaw umekuja siku moja baada ya klabu hiyo kufanikiwa kunyakua Ander Herrera kutoka Athletic Bilbao kwa ofa ya pauni milioni 29.
Man United ilikuwa na msimu mbaya ligi iliyopita chini ya kocha David Moyes ambaye alitimuliwa na nafasi yake kushikiliwa kwa muda Ryan Giggs kabla ya Luis van Gaal kupewa kibarua cha kuwa kocha mkuu sasa.

Soma orodha ya waliochaguliwa Kidato cha Tano 2014

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi nchini, imetoa  majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na shule mbalimbali kwa ajili ya kuendelea na elimu ya sekondari kidato cha tano, sanjari na vyuo mwaka 2014.

Orodha hiyo imetangazwa jijini Dar es salaam tangu Juni 17, ambapo idadi ya wasichana waliochaguliwa kwa nafasi hizo ni 9,378, waliochaguliwa katika machaguo 13 ya masomo mbalimbali ya kidato cha tano na masomo 11 ya vyuo vya ufundi.

Shule zilizopangiwa wanafunzi ni 201, ambapo shule za wasichana pekee ni 61, huku shule 34 zikiwa za jinsia zote mbili, wasichana na wavulana.

Idadi ya wanafunzi wavulana waliochaguliwa katika machaguo 13 ya masomo mbalimbali ya ngazi hiyo, ni 22,138.
Kupata Majina Hayo tafadhali bonyeza Links Hizi Hapa chini