STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, November 12, 2011

Taifa Stars yatakata Chad



Na Maulidi Kitenge, Chad
USHIRIKIANO wa wachezaji waliotokea benchi, Nurdin Bakari na Thomas Ulimwengu katika dakika za lala-salama uliipa Taifa Stars mwanzo mzuri wa mechi za hatua ya mchujo za kuelekea kwenye hatua ya makundi ya kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia 2014 kufuatia ushindi wa 2-1 ugenini kwa Chad jana.
Kiungo wa Yanga, Nurdin, aliyeingia katika kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Abdi Kassim anayecheza soka la kulipwa nchini Vietnam, aliifungia Stars goli la ushindi katika dakika ya 82 akitumia pasi ya mshambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Ulimwengu, ambaye pia aliingia katika kipindi cha pili kuchukua nafasi ya nyota mwenzake wa klabu hiyo ya Congo, Mbwana Samatta.
Katika mechi hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Idriss Mahamat Ouya mjini N'djamena, Stars walitangulia kupata bao la mapema katika dakika ya 11 kupitia kwa Ngassa aliyemalizia kiufundi pasi ya kiungo anayecheza soka la kulipwa nchini Canada, Nizar Khalfan.
Hata hivyo, wenyeji walihitaji dakika moja tu kusawazisha goli hilo walilopata kupitia kwa mshambuliaji wao anayecheza soka la kulipwa katika Ligi Daraja la Pili Ufaransa (Ligue 2) ya Club Laval B, Mahamat Labbo katika dakika ya 12 na kufanya matokeo ya 1-1 hadi wakati wa mapumziko.
Wakati mechi ikielekea ukingoni na wenyeji wakiamini kwamba wangeweza kupata angalau sare, Nurdin aliifungia Stars goli la pili na la ushindi katika dakika ya 80 lililoeafanya mashabiki wa Chad waliokuwa wamejaa uwanjani kuanza kuondoka kimyakimya.
Stars itarejea kifua mbele kesho kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere lakini itahitaji kutoruhusu kipigo katika mechi yao ya marudiano Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kama Stars itasonga mbele, itatinga katika Kundi C la kuwania kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2014 nchini Brazil, ambapo watajumuika timu ngumu za Ivory Coast, Morocco na Gambia.
Kocha wa Stars, Jan Poulsen aliwapongeza wachezaji wake baada ya mechi hiyo lakini alisema kazi bado haijamalizika na wanahitaji umakini mkubwa ili kusonga mbele.
Kikosi cha Stars jana kiliundwa na Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Idrisa Rajab, Agrey Morris, Juma Nyoso, Shaban Nditi, Henry Joseph, Abdi Kassim/ Nurdin Bakari, Nizar Khalfan, Mrisho Ngassa, Mbwana Samatta/ Thomas Ulimwengu.

BFT yapiga 'dochi' kozi ya makocha


KOZI ya ukocha wa ngumi ngazi ya kimataifa, iliyoandaliwa na Shirikisho la Ngumi za Ridhaa nchini, BFT ikishirikiana na Kamati ya Olimpiki Tanzania, TOC, imekwama kuanza leo Jumamosi kama ilivyopangwa badala yake sasa ifanyika Alhamisi ijayo.
Kozi hiyo itakayoshirikisha washiriki 30 watakaonolewa na Mkufunzi wa Kimataifa kutoka Algeria, ilikuwa imepangwa kuanza leo mjini Kibaha, lakini BFT imetoa taarifa kwamba imesogezwa mbele kutokana na kuchelewa kwa mkufunzi huyo.
Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga, alisema mkufunzi huyo, Azzedin Aggoune, aliwatumia taarifa za kupatwa na dharura na hivyo kutoweza kuwasili jana Ijumaa kama alivyokuwa amepanga ambapo sasa ameahidi kuwasili siku ya Jumatano..
Mashaga alisema kutoka na dharura hiyo iliyompata mkufunzi huyo wameona ni vema kuahirisha kozi hiyo na kutoa fursa kwa makocha walioteuliwa kushiriki kozi hiyo kushuhudia michuano ya ngumi ya Kova inayoendelea jijini Dar es Salaam.
"Ile kozi ya kimataifa ya ukocha wa ngumi iliyokuwa ianze Novemba 12-18 mjini Kibaha, imekwama kuanza kutokana na mkufunzi wa kimataifa toka Algeria kupatwa na dharura na kuchelewa kuja, sasa itaanza Novemba 17 huko huko Kibaha," alisema.
Mashaga alisema kozi hiyo inayotambuliwa na Shirikisho la Ngumi la Kimataifa, AIBA, itafungwa rasmi Novemba 25, ambapo washiriki watatunukiwa vyeti pamoja na wasifu wao kuwekwa kwenye database ya shirikisho hilo ili kuwaweza kutumika na kushiriki michuano yoyote ya kimataifa ya ngumi popote duniani.
Mmoja wa washiriki wa kozi hiyo, Rajab Mhamila 'Super D' alisema amefurahi kuteuliwa kushiriki kozi hiyo, akiamini itamsaidia kumpa ujuzi na kumjenga zaidi katika taaluma hiyo ya ukocha aayoifanya katika klabu za Ashanti na Amana zote za Ilala.

Mwisho

Matumla, Oswald kula X-mass ulingoni


MABONDIA wakongwe wa ngumi za kulipwa nchini, Rashid Matumla 'Snake Man' na Maneno Oswald 'Mtambo wa Gongo' wanatarajia kula Xmass wakiwa ulingoni watakapochapana katika pambano lisilo la ubingwa litakalochezwa jijini Dar es Salaam.
Wakongwe hao watapigana kwenye pambano la uzani wa Middle la raundi 10 litakalofanyika kwenye ukumbi wa Heinkein, Mtoni Kijichi na kusindikiwa na michezokadhaa ya utangulizi.
Kwa mujibu wa waratibu wa pambano hilo kampuni ya Adios Promotion kupitia afisa habari wao, Mao Lofombo ni kwamba kabla ya Matumla na Oswald kupanda ulingoni kuonyeshana kazi, mabondia Rashidi Ally na Hassan Sweet watapimana ubavu.
Lofombo alisema michezo mingine itawakutaniosha Kalulu Bakari dhidi ya Athuman Kalekwa na Shabani Kazinga ataonyeshana kazi na Kashinde.
Pambano la la nne kuwakutanisha mabondia mabingwa wa zamani, litafanyika huku kila mmoja akiwa na matokeo tofauti katika michezo yao ya mwisho ambapo Oswald alipigwa na Mada Maugo, wakati Matumla alimshinda Mkenya Ken Oyolo.
Katika michezo yao mitatu iliyopita, Matumla alimshinda Oswald mara mbili moja akimpiga kwa KO mnamo Oktoba 3, 2001 na jingine kwa pointi Oktoba 28, 2006 huku alikubali kichapo cha pointi mbele ya mpinzani wake Februari 4, 2001.
Tayari mabondia wote wameshaanza kutambiana juu ya pambano hilo, kila mmoja akijinasibu kutaka kuibuka na ushindi ili kulinda hadhi yake pamoja na kudhihirisha bado wamo katika mchezo huo licha ya umri kuwatupa mkono.
Matumla aliyewahi kuwa bingwa wa dunia wa WBU, kwa sasa ana umri wa miaka 43 miaka miwili zaidi ya mpinzani wake mwenye miaka 41 na mwenye rekodi ya kucheza mechi 64 akishinda 37, 26 kwa KO, akipigwa mara 24, 9 kwa KO na kupata sare tatu.
Mpinzani wake rekodi yake pia inaonyesha kapanda ulingoni mara 64 ameshinda mara 46 (33 kwa KO) amepoteza 16 (5 kwa KO) na kupata sare mbili.
Kwa kuangalia rekodi za mabondia hao ni wazi pambano lao lijalo litakuwa lenye mpinzani mkali kila mmoja akipenda kushinda ili kuendeleza rekodi aliyonayo katika mchezo huo wanaoendelea kuucheza karibu miaka 30 sasa.

Mwisho

Jumbe, atambia Shoka la Bucha

UONGOZI wa bendi ya Talent umedai kuwa, albamu yao mpya inayoendelea kuandaliwa itakuwa moto kuliko ile ya kwanza ya 'Subiri Kidogo' ambayo inaendelea kubamba sokoni.
Mkurugenzi wa bendi hiyo, Husseni Jumbe, alisema maandalizi wanayofanya kuipika albamu yao ya pili itakayofahamika kama 'Shoka la Bucha' ni ya aina yake kitu kinachompa jeuri kwamba itafunika kuliko ile ya awali.
Jumbe, alisema tayari wamesharekodi nyimbo nne kati ya sita za albamu hiyo katika studio za Sound Crafters na mara watakapomaliza mbili za mwisho wataanza kurekodi video kabla ya kufanya uzinduzi na kuziingiza sokoni mapema mwakani.
"Nadhani Shoka la Bucha itafunika zaidi kuliko Subiri Kidogo kwa namna tunavyoiandaa kwa sasa tukiwa tumesharekodi nyimbo nne kati ya sita," alisema.
Jumbe, alisema tayari baadhi ya nyimbo hizo zilizorekodiwa zimeshasambazwa kwenye vituo vya redio ili kurushwa hewani.
Alizitaja nyimbo zilizorekodiwa hadi sasa ni Kilio cha Swahiba, Shoka la Bucha, Kiapo Mara Tatu na Jipu la Moyo.
Aliongeza, wapo kwenye mipango ya kufanyta ziara mikoani kwa nia ya kujitangaza zaidi sambamba na kuitambulisha albamu zao mbili, ikiwemo hiyo inayomaliziwa kurekodiwa.

TMK waumwa kichwa videoni




KUNDI la muziki wa kizazi kipya la TMK Wanaume Family, limeachia mtaani video yake mpya ya 'Kichwa Kinauma', ikiwa ni maandalizi ya kupakuliwa albamu mpya ya kundi hilo.
Aidha, kundi la Tip Top Connection kesho linatarajia kuadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake kwa wasanii waliowahi kupitia katika kundi hilo na waliopo sasa kujumuika pamoja katika onyesho litakalofanyika Maisha Club Masaki, jijini Dar es Salaam.
Meneja wa kundi la TMK Wanaume Family, Said Fella 'Mkubwa Fella', alisema video ya wimbo huo ulioimbwa na wasanii Mheshimiwa Temba na Said Chegge, ni kati ya maandalizi ya kundi lao.
Mkubwa Fella alisema kukamilika kwa video ya wimbo huo ni mwanzo wa maandalizi ya upigwaji video wa nyimbo nyingine zitakazokamilisha albamu yao itakayokuwa na vibao 10 ambayo hata hivyo, hakuweza kuitaja jina lake.
"Mkubwa tumekamilisha video ya wimbo wetu mpya wa 'Kichwa Kinauma' tukiwa mbioni kufyatua video za nyimbo zetu nyingine za kukamilisha albamu ijayo ya TMK," alisema.
Mkubwa aliongeza sambamba na hilo, upande wake albamu yake ya miondoko ya taarab ya 'Kunguni Kunguni', ipo katika hatua ya mwisho kuachiwa hadharani ikiwa na nyimbo sita.
Nyimbo za albamu hiyo ya Mkubwa Fella ni 'Kusonakusonona', 'Simuachi', 'Midomo Imewashuka', 'Mchakamchaka', 'Sijapopoa Dodo' na 'Kimodern Modern'.
Nalo kundi la Tip Top Connection, moja ya makundi yanayotamba nchini, kesho litafanya onyesho maalum la kuadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake ambalo litapambwa na burudani mbalimbali ikiwemo soka na muziki utakaotumbuizwa na wasanii mbalimbali.
Onyesho hilo litawajumuisha wasanii wote waliowahi kupitia kundi hilo na wale waliopo sambamba na wengine walioalikwa kuwapiga tafu katika maadhimisho hayo yatakayofanyika kwenye ukumbi wa Maisha Club, Masaki jijini Dar es Salaam.

Young D, Aslay wote boda kwa boda




WASANII wanaokuja juu katika anga la muziki wa kizazi kipya nchini, Aslay Isiaka 'Dogo Aslay' na David Genz Mwanjela 'Young D' wanatarajia kuonyesha kazi watakapoungana na wakali wengine wa miondoko hiyo kwenye onyesho maalum litakalofanyika leo jijini Dar.
Dogo Aslay na Young D, wanaowatishia wakongwe wa muziki huo kwa namna ya kasi yao tangu walipoibuka, watashiriki tamasha lililopewa jina la 'Boda kwa Boda Beach Concert' ambalo litafanyikia kwenye ufukwe ya Mbalamwezi.
Mbali na wasanii hao wanaochuana kimuziki sambamba na chipukizi mwingine, Abdulaziz Chende 'Dogo Janja', pia tamasha hilo litawahusisha wakali kama msanii kutoka Kenya, Jaguar anayetamba na nyimbo za 'Kigeugeu' na 'Nimetoka Mbali' alioimba na nyota wa Tanzania, Ambwene Yesaya 'AY'.
Wengine watakaoshiriki tamasha hilo la 'Bodaboda' ni 'Mzee wa Hakunaga' Sumalee, Godzilla wa Salasala, Beca, Reycho, Country Boy & Stamina, na wengineo huku wakinakshiwa muziki huo na DJ Zero.
Kwa mujibu wa waratibu wa onyesho hilo, G5 Click, wakali hao watashirikiana pamoja kuangusha moja moja kuanzia saa moja jioni hadi 'kuchwee' ili kuwapa burudani mashabiki wa muziki wa kizazi kipya watakaoungana kwenye ufukwe huo.
"Ni tamasha la aina yake siku ya Jumamosi (leo) ambapo wasanii chipukizi na wakali wengine akiwemo Mkenya Jaguar watafanya vitu vyao katika ukumbi wa Mbalamwezi Beach Club."

Bundi wa Sikinde kupelekwa Studio

BENDI kongwe za muziki wa dansi nchini, Mlimani Park 'Sikinde' ipo mbioni kuingiza studio kibao kipya cha 'Bundi', ikiwa katika harakati za kufyatua albamu mpya itakayokuwa na nyimbo sita.
Kibao hicho kipya kimetungwa na Abdalla Hemba, mmoja wa waimbaji mahiri wa bendi hiyo ambayo kwa sasa inatamba na wimbo wa 'Jinamizi la Talaka', kinachodaiwa ni 'dongo' kwa mahasimu wao, Msondo Ngoma wanaotamba na kibao cha 'Suluhu'.
Mmoja wa viongozi wa Sikinde, Hamis Milambo, alisema kibao cha 'Bundi', kitarekodiwa wakati wowote kuanzia sasa sambamba na vingine vitakavyokuwa katika albamu yao mpya.
Milambo alisema mbali na Jinamizi la Talaka na Bundi, nyimbo nyingine za albamu hiyo zilizokamilika ni 'Asali na Shubiri' uliotungwa na Shukuru Majaliwa, 'Nitalipa Deni', uliotungwa na bendi mzima ya Sikinde, 'Kilio cha Kazi'-Hassani Bitchuka na 'Nisamehe'-Hemba.
Wakati Sikinde wakijiandaa kuhitimisha albamu yao hivyo, kwa upande wa mahasimu wao, Msondo Ngoma wameibuka na kibao kingine kipya kiitwacho 'La Kuvunda' utunzi wa mkali Shaaban Dede 'Mzee wa Loliondo' ambaye anatamba pia na kibao kiitwacho 'Suluhu'.
Msondo ambao wameanza kurekodi nyimbo zao mpya kwa ajili ya albamu yao mpya, imeachia kibao hicho kipya ikiwa ni maandalizi ya albamu ya mwaka ujao.
Albamu yao ya sasa wanaotarajia kuiingiza sokoni mara itakapokamilika kurekodiwa inatarajiwa kufahamika kwa jina la 'Nadhiri ya Mapenzi' ambayo ni jina la kibao kilichotungwa na Juma Katundu.
Nyimbo nyingine za albamu hiyo na watunzi wake kwenye mabao ni 'Kwa Mjomba Hakuna Urithi (Huruka Uvuruge), Dawa ya Deni (Is'haka Katima 'Papa Upanga), LIpi Jema na Baba Kibene za Edmund Sanga 'Eddo Sanga' na 'Suluhu' (Shaaban Dede).

Mwaikimba aahidi ubingwa Azam






SIKU moja tangu amwage wino wa kuichezea Azam kwa mechi za duru la pili la Ligi Kuu
Tanzania Bara, Mshambuliaji Gaudence Mwaikimba 'Andy Carroll' ameahidi kuipigania klabu hiyo ili iwe bingwa mpya wa soka nchini.
Mwaikimba aliyekuwa akiichezea Moro United, aliyotua mapema msimu huu akitokea Kagera Sugar, alisema anaamini ana deni kubwa la kulipa fadhila ya kuaminiwa na klabu ya Azam kiasi cha kumsajili, ila atakachofanya yeye ni kushirikiana na wenzake kuipa ubingwa msimu huu.
"Kwangu ni furaha kubwa kutua Azam, moja ya klabu zenye malengo na muono wa mbali
katika soka la Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Wajibu wangu kama mchezaji ni kuhakikisha naipigania ifanye vema ikiwemo kuwa mabingwa wapya nchini," alisema.
Mshambuliaji huyo anayeshikilia nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji mabao msimu huu, alisema kwa vile karibu wachezaji anayeenda kukutana nao Azam amewahi kucheza nao katika klabu mbalimbali na timu ya taifa, Taifa Stars hana hofu ya kuelewana nao mapema.
"Kwa mfumo wa soka letu toka klabu moja hadi nyingine kufanana, naamini itanichukua
muda mfupi kuzoeana na wenzangu na kubwa nalopenda kuwaahidi mashabiki wa Azam
kwamba watarajie mambo makubwa katika duru lijalo," alisema.
Kuhusu suala la uhakika wa namba kwa nafasi anayocheza ambayo tayari ndani ya Azam
inayo wachezaji nyota kama John Bocco, Mwaikimba alisema hana tatizo lolote kwa vile
anajiamini yeye ni mchezaji mzuri na mwenye uwezo mkubwa ndio maana amesajiliwa Azam.
Nyota huyo aliyewahi kuwika na klabu za Tukuyu Stars, Yanga, Ashanti United na Prisons Mbeya ni mmoja wa wachezaji wapya waliotua Azam ambayo imewatema wachezaji wao wawili wa kimataifa kutoka Ghana, Wahabu Yahya na Nafiu Awudu.
Mwingine aliyesajiliwa Azam katika dirisha hilo dogo ni beki wa zamani wa kimataifa wa Simba, Joseph Owino na huku mshambuliaji Jerry Tegete wa Yanga ni miongoni mwa
wanaowindwa na klabu hiyo.

Thursday, October 20, 2011

Filamu ya CPU kuzinduliwa rasmi Novemba 24




FILAMU mpya ya kisasa ya CPU, iliyowashirikisha wasanii nyota nchini kama Sauda Kilumanga, Dotnata Posh, Masinde, Dude na wengineo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi Novemba 24 kwenye ukumbi wa New World Cinema, Mwenge.
Mratibu wa filamu hiyo, Evance Bukuku, alisema CPU ambayo ni kifupi cha maneno Children Protection Unity (Kitendo cha Kuwalinda Watoto), imetengenezwa na kampuni ya Haak Neel Production ikishirikisha wasanii zaidi ya 150.
Bukuku, alisema filamu hiyo iliyorekodiwa kwa teknolojia ya kisasa kwa kutumia helkopta baada ya kuzinduliwa Novemba 24, itaanza kuonyesha eneo la Mlimani City kwa muda wa wiki moja kwa kiingilio kitakachotangazwa baadae.
"Filamu yetu ya CPU ambayo imewashirikisha wahusika wakuu wanne na wasaidizi 30, itazinduliwa Novemba 24 mwaka huu kabla ya kuanza kuonyesha kwenye juumba la sinema la Mlimani City kwa wiki moja kuanzia Novemba 25- Desemba 2," alisema.
Aliongeza baada ya maonyesho hayo, kampuni yao inafanya mipango ya kwenda kuionyesha bure filamu hiyo inayozungumzia masuala mbalimbali yanayopingana na unyanyasaji na ukatili wa watoto pamoja na matendo mengine ya kihalifu.
Bukuku aliitaja mikoa itakayoenda kuonyesha filamu hiyo bure ni Mwanza, Arusha, Dodoma, Dar, Mbeya na Zanzibar.
Baadhi ya washiriki wa filamu hiyo, Steven Singh Sandhu na Sauda Kilumanga waliiambia MICHARAZO kuwa, kile ambacho watanzania walikuwa wakikisubiri kwa muda mrefu katika tasnia ya filamu sasa wamekipata kupitia filamu hiyo ya CPU.
"Ni filamu bab kubwa, ikiwa imetengenezwa kwa kiwango cha hali ya juu na ni moja ya filamu yenye uhalisi na ujumbe maridhawa kwa jamii, kitu ambacho kabla ya hapo haikuwahi kutokea," alisema Sandhu maarufu kama Salvador au .The Pride'.
Naye Sauda alisema kama mhusika mkuu katika filamu hiyo ameonyesha namna gani jamii ikishirikiana inaweza kutatua matatizo yanayowakabili watoto vikiwemo vitendo vya kikatili na uhalifu mwingine.

Belle 9, Godzilla kupamba Miss Utalii Dodoma

WASANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Belle 9 na Godzilla wanatarajiwa kupamba shindano la kumsaka mrembo wa utalii wa Dodoma, Miss Utalii Dodoma litakalofanyika wiki ijayo mjini Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamati ya Miss Utalii Tanzania kupitia Rais wake, Gideon Chipungahelo, shindano hilo litafanyika kwenye ukumbi wa Club La Aziz siku ya Oktoba 29.
Taarifa hiyo inasema, shindano hilo ambalo ni muendelezo wa kusaka wawakilishi wa mikoa kwa ajili ya fainali za taifa za kumsaka Miss Utalii Tanzania 2011-2012 litakalofanyika mapema mwakani.
Chipungahelo, alisema shindano hilo litapambwa na burudani mbalimbali ikiwemo
la wasanii wa kizazi kipya wanaotamba katika miondoko ya R&B na hip hop, Belle 9, Godzilla, na vikundi vya ngoma asilia kikiwemo Yangeyange Arts cha Dodoma.
"Shindano la Miss Utalii Dodoma, linatarajiwa kusindikizwa na burudani za wasanii Belle 9, Godzilla na vikundi vya ngoma asilia. Maandalizi kwa ujumla yapo vema kwa nia ya kulinogesha shindano hilo," Chipungahelo alisema katika taarifa hiyo.
Tayari wadhamini mbalimbali wamejitokeza kwa nia ya kulidhamini shindano hilo ambalo mbali na kusaka kisura wa mkoa, pia itatoa wawakilishi wa kushiriki shindano la taifa litakalofanyika mwakani ambalo litrahusisha washiriki toka mikoa na kanda tofauti.

Mwisho

Sare zatawala daraja la Kwanza, Polisi Dar, Mbeya City moto

MECHI za raundi ya pili ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, zimetawaliwa na 'mdudu' wa sare baada ya michezo minne kati ya sita iliyochezwa jana kutoa matokeo hayo katika mikoa tofauti.
Katika mechi hizo nne, Rhino Rangers ya Tabora ililazimishwa sare ya 1-1 na AFC Arusha, huku Manyoni Fc na Polisi Morogoro zilishindwa kutambiana kwa kutofunga katika mechi za kundi C.
Katika mechi za kundi A, TMK United na Transit Camp zilitoshana nguvu kwa kutofungana katika pambano lililochezwa Mkwakwani Tanga, , sawa na ilivyokuwa kwa mchezo wa kundi hilo kati ya Morani- Manyara dhidi ya wageni wao JKT Mgambo ya Tanga.
Mechi pekee ya kundi hilo la A lililotoa ushindi ni ile ya Polisi Dar es Salaam iliyoifunga Burkina Faso mabao 5-3 kwenye uwanja wa Mabatini-Mlandizi, na kuwafanya 'maafande' hao maarufu kama 'Vijana wa Kova' kujikita kileleni mwa kundi hilo.
Timu hiyo ya Polisi Dar inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi sita, mabao sita ya kufunga na kufungwa mabao matatu, ikifuatiwa na Polisi Morogoro yenye pointi nne.
Katika pambano jingine lililotoa ushindi kwa mechi hizo za juzi ni kati ya timu ya Jiji la Mbeya, Mbeya City iliyoilaza JKT Mlale ya Ruvuma mabao 3-1 na kujikita kileleni mwa kundi hilo ikiwa na pointi sita na mabao manne ya kufunga.
Mechi nyingine za kundi hilo la B zinatarajiwa kuchezwa leo ambapo timu ya Small Kids itaikaribisha mjini Morogoro, Prisons ya Mbeya, huku Majimaji Songea itaumana na Polisi Iringa mjini Songea, na timu za 94 KJ na Polisi Tabora zitaumana katika kundi C kwenye pambano litakalochezwa uwanja wa Mabatini-Mlandizi.
Ligi hiyo inashirikisha jumla ya timu 18 ambazo zinawania nafasi tisa za kucheza hatua ya pili ya fainali za ligi hiyo ili kusaka timu nne za kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Pambano la Maugo, Odhiambo laiva Mwanza



BONDIA mchachari wa ngumi za kulipwa nchini, Mada Maugo, amesema maandalizi ya pambano lake dhidi ya Mkenya, Joseph Odhiambo litakalofanyika keshokutwa, yamekamilika ikiwemo kutarajia kumpokea mpinzani wake kesho jijini Mwanza.
Maugo na Odhiambo wanatyarajia kuonyesha katima katika pambano lisilo la ubingwa la raundi 10 uzani wa middle, litakalosindikizwa na mabondia wakongwe nchini Joseph Marwa na Rashidi Matumla, ambalo litafanyika Jumapili uwanja wa CCM -Kirumba.
Akizungumza na MICHARAZO kwa njia ya simu toka kwenye kambi yake mjini humo, Maugo, alisema mpinzani wake anatarajia kutua jijini Mwanza kesho tayari kwa ajili ya kupima uzito siku ya Jumamosi kabla ya kupanda ulingoni Oktoba 23.
Maugo, alisema pia ameshamalizana na wasanii watakaosindikiza pambano hilo ambalo lengo lake ni kuhamasisha na kuendeleza mchezo wa ngumi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
"Maandalizi ya pambano langu dhidi ya Mkenya Joseph Odhiambo yanaendelea vizuri na nawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi siku ya Jumapili kuweza kushuhudia mpambano huo na yale yatakayotusindikiza," alisema Maugo.
Maugo alisema miongoni mwa mapambano yatakayowasindikiza ni lile la Rashid Matumla dhidi ya Emma Kichere wa jijini Mara na Joseph Marwa atakayepigana na Chuku Dusso., huku Marwa atapigana na Chuku Duso.
"Emma Kichere ni bondia chipukizi wa mkoa wa Mara atazipiga na Matumla na Marwa atapigana na Chuku Duso anayetoka mkoa wa Mwanza, ndipo mimi na Odhiambo tutapanda ulingoni kuhitimisha michezo ya siku hiyo,' alisema Maugo.
Maugo alisema wasanii watakaosindikiza pambano lao ni H-Baba, Dudu Baya na wengine chipukizi ambao wanatokea mikoa hiyo ya Kanda ya Ziwa.
Pambano hilo la Jumapili kwa Maugo ni maalum kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa kimataifa dhidi ya Mjerumani, atayechuana nae kuwania mkanda wa IBF.

Mwisho

Kamanda Kova kushuhudia Mbwana, Miyeyusho wakipigana Diamond Jubilee

WAKATI Mbwana Matumla 'Golden Boy' na Francis Miyeyusho 'Chichi Mawe' wakianza kutupiana 'madongo' juu ya pambano lao la kuwania mkanda wa Mabara wa UBO, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika pambano hilo.
Mratibu wa pambano hilo la kuwania ubingwa wa Mabara wa UBO, litakalochezwa Oktoba 30, Mohammed Bawazir wa Dar World Link, alisema Kova ndiye atakayemvisha taji mshindi wa mchezo huo.
Bawazir, alisema kamanda Kova ambaye ni Mlezi wa mchezo wa ngumi nchini, amekubali mualiko wa pambano hilo litakalofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
"Maandalizi ya pambano la Mbwana Matumla atakayetetea taji lake la UBO -Inter Continental dhidi ya Francis Miyeyusho yanaendelea vema ikiwemo Kamanda Kova kukubali kuwa mgeni rasmi wa mchezo huo," alisema.
Mratibu huyo alisema kala ya wababe hao kupanda ulingoni yatafanyika mapambano mengine matano ya utangulizi likiwemo litakalowakuanisha mabondia wakike, Asha Ngedere na Salma Kiobwa.
Pambano jingine ni la kuwania ubingwa wa taifa wa PST kati ya Juma Fundi na Fadhil Majiha.
Wakati maandalizi yakiwa hivyo Mbwana na Miyeyusho kila mmoja kwa wakati wake jana amejitapa kuibuka na ushindi katika pambano hilo litakalokuwa la raundi 12 la uzani wa Bantam.
Miyeyusho alisema amejiandaa kumvua taji Matumla, licha ya kutambua ni bondia mzuri asiyetabirika.
"Niko fiti kwa ajili ya kushinda pambano hilo, sina wasiwasi, ila naomba mashabiki wake kushuhudia ninavyompiga Mbwana kwa KO," alisema.
Mbwana mwenyewe, alisema hana maneno mengi kwani anaamini yeye ndiye bingwa na haitakuwa rahisi kwake kukubali kupokwa taji lake na Miyeyusho.
"Mie sina maneno, nimezoea kutekeleza mabmbo kwa vitendo hivyo mashabiki wangu waje ukumbini kuona nitafanya nini, ila siwezi kukubali taji langu ya UBO liniondoke," alisema.
Mabondia hao watakutana katika pambano la tatu baina yao, ambapo mara mbili za mwanzo walipokutana Februari 21, 2004 na Januari 17, 2009, Mbwana aliibuka na ushindi kitu ambacho Miyeyusho amedai hakubali kupigwa tena katika mchezo huo wa Oktoba 30.

Mwisho

Ferguson awatoa hofu mashabiki Extra Bongo


RAPA nyota wa bendi ya Extra Bongo, Saulo John 'Ferguson' amewatoa hofu mashabiki wa bendi hiyo, juu ya taarifa kwamba yupo mbioni kuiacha na kurejea alipotoka.
Ferguson, ambaye ni mtunzi na muimbaji aliyetua Extra Bongo mapema mwaka huu akitokea African Stars 'Twanga Pepeta', alisema taarifa zilizosambazwa kwamba yupo mbioni kuondoka katika bendi hiyo ni uzushi wenye nia ya kumharibia.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, rapa huyo aliyewahi kuzifanyia kazi Double Extra, Majahazi ya Zanzibar, Mchinga G8 'Timbatimba' na Extra Bongo 3x3, alisema wadau wa bendi yake wasiwe na hofu, kwani hana mpango wa kuondoka.
"Sina mpango wa kuondoka na wala sijawahi kuwaza kufanya hivyo kwa sababu ni vigumu niache embe bivu nililonalo na kulifuata bichi kwingine," alisema bila kufafanua.
Alisema, uzushi wa yeye kutaka kuondoka zilitolewa wakati akiwa ziarani mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na bendi yake na kumfanya alazimike kuitisha mkutano huo ili kutoa ufafanuzi, kuwaondoa shaka wadau wa bendi hiyo wanaoweza kumfikiria vibaya.
"Nimepata usumbufu mkubwa kwa mashabiki na familia yangu wakiniona sina utulivu, ndio maana nimewaita ili kuweka bayana kwamba taarifa za mtaani uzushi unaoenezwa na watu wasionitakia mema," alisema.
Aliongeza kuwa, kuthibitiha kuwa 'yupo sana' Extra Bongo, amewaandalia mashabiki hao rapu mpya iitwayo Mdudu ambayo itawashindanisha mashabiki hao katika maonyesho yao ambapo mshindi atajinyakulia runinga ya inchi 24.
"Nimekuja na rapu mpya iitwayo mdudu, ili kuonyesha nipo sana Extra Bongo na kuzima uzushi huo kwamba natarajia kurejea nilipotoka," alisisitiza.
Wakati huo huo, Kiongozi wa Extra Bongo, Rogart Hegga 'Catapillar' ameeleza ziara yao mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, ilikuwa ya mafanikio na kuonyesha namna gani bendi yao inavyokubalika, huku wakiwapongeza wakazi wa mikoa hiyo kwa mapokezi waliyowapoa.
Hegga, alisema bendi yao iliyorejea jijini Dar juzi, imewafanya waamini malengo waliyojiwekea ya kuteka soko la muziki wa Tanzania, linaelekea kufanikio na kuwaomba mashabiki wao kuzidi kuwaunga mkono.

Mwisho

Friday, September 30, 2011

Msondo yaingia studio kurekodi albamu mpya



BENDI kongwe ya Msondo Ngoma, mapema leo asubuhi imeingia studio kurekodi kibao kipya kiitwacho 'Suluhu', ikiwa ni maandalizi ya upakuaji wa albamu yao mpya.
Mmoja wa viongozi wa bendi hiyo, Shaaban Dede, aliiambia MICHARAZO kuwa, nyimbo zao mpya zitarekodiwa katika studio za Fabreas Records na kwa kuanza leo anarekodi kibao cha 'Suluhu', ambacho amekitunga yeye.
Dede, alisema mara baada ya kibao hicho kurekodiwa kitasambazwa kwenye vituo vya redio kwa nia ya kukitambulisha huku, bendi yao ikiendelea kumalizia nyimbo nyingine tano zilizosalia.
"Tumeingia leo studio kwa Fabreas kwa lengo la kufyatua kibao cha Suluhu na vingine kwa ajili ya albamu yetu mpya ijayo," alisema Dede.
Alisema nyimbo nyingine za albamu hiyo ambazo zimeshakamilika ni 'Dawa ya Deni', 'Lipi Jema', 'Kwa Mjomba Hakuna Urithi', 'Baba Kibene' na 'Nadhiri ya Mapenzi'.
"Nadhani muda si mrefu mashabiki wetu na wale wa muziki kwa ujumla wataipata albamu yetu, kwani tutakuwa tukidondosha wimbo mmoja mmoja, kabla ya kuikamilisha na kuiachia mtaani, kabla ya kumalizika mwaka huu," alisema.
Msondo Ngoma imekuwa na desturi ya kutoa albamu kila mwaka, ila kwa mwaka jana haikuachia kazi yoyote, albamu yao ya mwisho ni ile ya mwaka juzi iitwayo 'Huna Shukrani'.

Siwezi kuchojoa nguo nicheze X-Skyner



MSANII wa filamu anayekuja juu nchini, Skyner Ally, amesema hata apewe kiasi gani cha fedha hawezi kucheza picha za watu wazima 'X' kwa madai kufanya hivyo mbali na kujidhalilisha, pia ni kwenda kinyume na mafundisho ya Mungu.
Akizungumza na MICHARAZO, Skyner, alisema ingawa yupo ndani ya fani ya uigizaji kwa nia ya kusaka fedha, lakini hayupo tayari kujivua utu wake, ili akubali kuchojoa nguo na kuigiza filamu za X.
Skyner, alisema anaamini kucheza filamu za namna hiyo ni kwenda kinyume na maadili na kukiuka mafundisho ya dini, mbali na yeye mwenyewe kujidhalilisha mbele ya jamii.
"Ingawa nasaka fedha kupitia kipaji cha uigizaji nilichonacho, lakini siwezi kukubali kucheza filamu za X hata nikiahidiwa kiasi gani cha fedha," alisema.
Kisura huyo, anayetamba kwenye filamu kama 'The Second Wife', 'Unpredictable', 'What is It', 'I hate My Birthday', 'Why I Did Love', 'Kizungumkuti' na nyinginezo, alisema kuwa msanii hakuna maana kujirahisisha na kufanya mtendo machafu, jambo alilolata wasanii wenzake kuepukana nayo ili kulinda heshima zao na fani zao kwa ujumla.
"Wasanii lazima tujiheshimu na kujithamini, kujiingiza kwenye skendo na matendo machafu ndiyo yanayotufanya tusiheshimike na kuichafua fani nzima ya sanaa, wakati imekuwa ikitusaidia baadhi yetu kumudu maisha na kuzisaidia familia zetu," alisema.
Skyner, anayetarajiwa kuolewa wiki ijayo, alisema wasanii wakijiheshimu na kuepuka skendo ni wazi jamii itawapenda na kuwathamini, hasa kama watajibidiisha kuboresha kazi zao.

Yanga sasa roho kwatu!


USHINDI mnono wa mabao 5-0 iliyopata kwa Coastal Union, umewafanya wadau wa klabu ya Yanga kuchekelea wakisisitiza kuwa hawana hofu ya kutetea taji lao msimu huu.
Yanga iliyokuwa ikichechemea katika ligi hiyo, iliishindilia Coastal mabao hayo katika pambano lilkilochezwa uwanja wa Taifa, na kuipandisha mabingwa watetezi hao hadi kwenye nafasi ya nne nyuma ya timu za Simba, Azam na JKT Oljoro zilizoitangulia.
Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema wanaamini ushindi waliopata kwa Wagosi wa Kaya ni salamu kwa watani zao na timu nyingine zilizokuwa zikiikejeli timu yao ilipoanza kwa kusuasua katika ligi hiyo.
Sendeu, alisema tangu awali walikuwa wakisisitiza kuwa, ligi bado mbichi na vigumu watu kuitabiria Yanga kwamba haiwezi kufurukuta msimu huu, bahati nzuri imethibitika kwa ushindi mfululizo ambao umewafanya wapinzani wao kuanza 'kuhema'.
Alisema anaamini mapumziko ya ligi kupisha pambano la Stars na Morocco itatumiwa vema na benchi lao la ufundi pamoja na wachezaji wao kuhakikisha wakirejea dimbani wanakuwa moto zaidi, ili kumaliza duru la kwanza katika nafasi stahiki.
"Nadhani waliokuwa wakitukejeli kwamba tumefulia, salama wamezipata na ninajua huko walipo presha zimeshaanza kuwapata, tunaombea tuendelee na mwendo huu huu ili tumalize duru la kwanza katika nafasi mbili za juu na kujiweka vema kulitetea taji letu," alisema.
Nao baadhi ya wadau wa klabu hiyo, wamedai pamoja na kuanza kuonyesha mwanga kwa timu yao, bado wachezaji hawapaswi kubweteka na badala yake waongeze juhudi ili kumaliza meechi tano zilizosalia kwa mafanikio.
"Tumefurahi mafanikio ya timu yetu, lakini naomba wachezaji na viuongozi wasibweteke, tuendelee kushinda mechi zijazo ikiwemo ile ya Simba Oktoba 29, ili turejeshe heshima yetu iliyopotea kwa matokeo mabaya ya mechi za awali," alisema Ramadhani Kampira.
Yanga kabla ya kuvaana na Simba katika pambano linalosubiriwa kwa hamu, itacheza na timu za Kagera Sugar, Toto Afrika na JKT Oljoro kabla ya kufunga dimba la duru la pili kwa kuumana na Polisi Dodoma mjini Dodoma Novemba 5.

Stewart ruksa kuinoa Zanzibar Heroes


UONGOZI wa klabu ya soka ya Azam, umekubali kwa moyo mmoja uteuzi wa kocha wao mkuu, Stewart Hall, kuinoa timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes kwa ajili ya michuano ya Kombe la Chalanji itakayofanyika Novemba, jijini Dar es Salaam.
Chama cha Soka Visiwani Zanzibar, ZFA, kilimtangaza Stewart kuwa ndiye atakayeinoa timu hiyo katika michuano hiyo, ikiwa ni mara ya pili kwa kocha huyo kupewa kibarua hicho cha kuinoa Zanzibar Heroes.
Katibu Mkuu wa Azam, Nassor Idrissa 'Father', alisema uongozi wao, hauna tatizo la kocha wao kwenda kuinoa Zanzibar Heroes, kutokana na ukweli kwa namna moja ni faida kwa Azam ambayo hutoa wachezaji wengi katika kikosi cha timu hiyo.
Idrissa, alisema pia kocha huyo ataenda kuinoa timu hiyo wakati klabu yao itakuwa imeshawapa likizo wachezaji wao kwa ajili ya mapumziko marefu kabla ya kuanza kwa duru la pili la ligi hiyo mapema mwakani.
Katibu huyo alisema pia ni vigumu kwa Azam kumzuia kocha huyo kwenda kutekeleza jukumu lake kwa timu ya taifa, ambayo ni sehemu ya Muungano wa Tanzania, labda kama angeteuliwa kwenda kuinoa Kenya au Uganda ndio wangweka pingamizi.
"Angekuwa ameteuliwa kuinoa Kenya au Uganda, hapo ingekuwa vigumu kumruhusu lakini kama ni Zanzibar au hata kama ingekuwa Tanzania Bara, tungemruhusu kwa vile ni faida kwa maendeleo ya soka letu, kwani Stewart ni kocha mzuri," alisema.
ZFA, ilisema kocha huyo angeungana na timu hiyo ya taifa, Novemba 10, siku tano baada ya duru la kwanza la ligi kuu kumalizika.
Kabla ya kutua Azam, Stewart anayetokea Uingereza aliletwa nchini kuinoa timu hiyo ya Zanzibar kupitia kampuni ya Future Century.

Skyner: Kisura anayetishia mastaa wa kike Bongo Movie





NI muda mfupi tangu Skyner Ally Seif, ajiingize kwenye fani ya uigizaji, ila tayari amekuwa na jina kubwa kutokana na umahiri aliouonyesha kupitia kazi alizoshiriki.
Mbali nba umahiri wa kisanii, pia mvuto wa sura na umbile vimemfanya msanii huyo, awe miongoni mwa wasanii wa kike wanaotamba nchini kwa sasa.
Sykner alikiri, licha ya kuwa na kipaji cha sanaa tangu utotoni, hakupata fursa ya kukionyesha hadi mwaka jana alipoibuliwa na Vincent Kigosi 'Ray' kupitia filamu ya 'The Second Wife'.
Alisema kabla ya 'shavu' la Ray, alishacheza kazi nyingine kama 'Mtumwa wa Mapenzi' na 'Johnson' ambazo hazikumtangaza sana.
Kazi nyingine alizoshiriki mara alipoibuliwa na Ray, ni 'What is It', 'Why I Did Love', 'I Hate My Birthday', 'Kizungumkuti', 'Unpredictable' na nyingine.
Skyner anayejiandaa kuolewa Ijumaa ijayo, alizaliwa mwaka 1992 jijini Dar, akiwa mtoto wa pili wa familia ya watoto watatu, alihitimu masomo ya sekondari Shule ya Cambridge, ya jijini Dar.
Nyota huyo, anayependa biriani na kunywa fanta, alisema licha ya kuwepo kwenye sanaa kwa muda mfupi, fani hiyo imemnufaisha mengi, akiota kuja kutamba kimataifa na mtayarishaji na muongozaji bora, akimiliki kampuni yake binafsi.
Kisura huyo, hutumia muda wake wa ziada kumuomba Mungu na kulala, pia ni shabiki wa
muziki akihusudu miondoko ya Arabian.
Juu ya madai ya rushwa na ngono katika sanaa, Skyner alikiri ni kweli amewahi kusikia, ila yeye hajawahi kukumbana nayo.
Ila, alisema wasanii wanaoombwa rushwa hiyo wana uhuru wa kukataa kwa kuringia vipaji vyao badala ya kujirahisisha na kudhalilika.
Skyner aliyewafiwa na wazazi wote mwaka 2006 wakipishana miezi mitano, akitangulia mama yake aliyefariki mwezi Aprili, kisha Septemba kufuata baba'ake, alisema licha ya kuwepo kwenye sanaa kusaka fedha, hayupo tayari kuchojoa nguo, ili acheze filamu za X.
Kimwana huyo, anayewazimia Irene Uwoya na Ray, alidai hawezi kucheza X hata akiahidiwa kiasi gani cha donge la fedha, kwa vile anajiheshimu na kujithamini kama mwanamke.
Aliwaasa wenzake, kujiheshimu na kuepukana na matendo machafu, aliyodai huwavunjia hadhi mbele ya jamii, na kusababisha sanaa yao kuonekana kama kazi ya wahuni wakati sio kweli.
Alisema, umaarufu wa msanii hupatikana kupitia ubora wa kazi zake na sio skendo chafu.
Skyner aliiomba serikali iwasaidie wasanii nchini kuweza kupambana na maharamia wanaowaibia kazi zao na kuwafanya wasanii wafe maskini tofauti na wenzao wa mataifa mengine.
Kadhalika, aliiasa jamii kuwa bega kwa bega na wasanii kwa kununua kazi zao halisi mara zitokapo, badala ya kukubali kuuziwa kazi feki, kitu kinachochangia wasanii kunyonywa na kuwafanya washindwe kusimama kimaisha na kiuchumi.

Mwisho

Azam yagomea nyota wake kwenda likizo, kisa...!

WAKATI nyota wa Simba na Yanga wakipewa likizo fupi ya kupisha mchezo wa timu ya taifa, Taifa Stars dhidi ya Morocco utakaochezwa ugenini mwezi ujao, uongozi wa Azam umewagomea mastaa wake, ukisisitiza kuwa timu yao itaendelea kujifua kama kawaida.
Simba kupitia Afisa Habari wake, Ezekiel Kamwaga, imetangaza kuwapa likizo ya wiki moja wachezaji wao, ili kupumzika kabla ya kurejea tena kujiandaa na pambano dhidi ya African Lyon litakalochezwa Oktoba 16, jijini Dar es Salaam.
Klabu hiyo imewapa likizo wachezaji hao baada ya kazi nzuri waliyofanya kwa kuiweka kileleni mwa msimamo timu yao ikiwa na pointi 18 kutokana na kucheza mechi nane bila kupoteza hata moja, ikishinda mechi tano na kutoka sare mechi tatu, .
"Wachezaji wetu tumewapa likizo ya muda mfupi, kabla ya kurejea tena kuanza maandalizi dhidi ya mechi yetu ijayo na zile zilizosalia katika ligi hiyo," alisema Kamwaga.
Hata hivyo timu inayoifukuzia Simba katika msimamo wa ligi hiyo, Azam imesema hawaendi mapumziko kama timu nyingine, bali wataendelea kujifua kujiandaa zaidi kwa mechi zao zijazo kabla ya kumaliza duru la kwanza mnamo Novemba 5.
Katibu wa Azam, Nassor Idrissa, alisema nyota wa timu yao wataendelea kufanya mazoezi kama kawaida, licha ya kwamba hawatakuwa na mchezo wowote hadi Oktoba 15 dhidi ya 'maafande' wa JKT Ruvu.
"Nyota wetu hawataenda likizo, wataendelea kujifua mazoezi kulingana na programu za kocha kwa nia ya kuwaweka sawa wachezaji kwa mechi zilizosalia za kumalizia duru la kwanza," alisema.
Idrissa maarufu kama 'Father' alisema yapo makosa ambayo yalikuwa yakifanyika katika kikosi chao, hivyo muda uliopo utatumiwa na benchi lao la ufundi kuweka mambo sawa kabla ya kurejea tena dimbani wakiwa moto kuliko hivi sasa.
Azam iliyopanda Ligi Kuu msimu wa 2008-2009, ndiyo inayoshikilia nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 15, tatu zaidi ya vinara Simba.

'Vijana wa Kova' wamsajili Mnigeria Ligi Daraja la Kwanza

MABINGWA wa Ligi ya TFF-Taifa, Central Stars (Polisi-Dar es Salaam), imetangaza kuwaongeza wachezaji sita wapya akiwemo Mnigeria kwa ajili ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza Oktoba 15 katika vituo vitatu tofauti.
Uongozi wa timu hiyo umedai, umewaongeza wachezaji hao kwa lengo la kuipa nguvu timu yao inayoendelea kujifua kwenye uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini kuhakikisha inakuwa miongoni mwa klabu zitakazopanda Ligi Kuu msimu ujao.
Katibu wa timu hiyo, Ngello Nyanjaba, aliiambia MICHARAZO kuwa, wachezaji hao wapya waliongezwa ni Mnigeria, Felix Ameche, Msiba Joto, Paul Skazwe, Juma Sedege na Awadh ambao tayari wameorodheshwa kwenye usajili wa timu yao.
Nyanjaba, ambaye pia ni kocha wa timu hiyo ya Polisi, alisema wachezaji hao wapya wataungana na nyota 22 wa kikosi hicho waliopandisha daraja timu hiyo kwa ajili ya ligi hiyo, akisema walitarajia kuwasilisha usajili wao wakati wowote kuanzia leo.
"Tunaendelea vema na maandalizi ya ligi daraja la kwanza, ambapo tangu turejee toka Tanga tunaendelea kujifua kwa mazoezi, lakini kubwa ni kuongeza wachezaji wapya sita akiwemo Mnigeria kwa lengo la kufanya vema kwenye michuano hiyo," alisema.
Michuano hiyo itakayochezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini itashirikisha timu timu 18 zilizopangwa katika makundi matatu, ambapo Polisi-Dar, imepangwa kundi A na timu za Mgambo-Tanga, Morani-Manyara, TMK United na Transit Camp za Dar na Burkina Faso ya Morogoro.
Kundi B lina timu za Majimaji-Songea, Mbeya City Council, Mlale JKT-Ruvuma, Polisi- Iringa, Small Kids-Rukwa na Tanzania Prisons ya Mbeya.
Timu nyingine zitakazoshiriki ligi hiyo ni pamoja na 94 KJ ya Dar, AFC-Arusha, Polisi-Morogoro, Polisi-Tabora, Rhino Rangers-Tabora na Samaria-Singida, zilizopangwa katika kundi C.

Mwisho

Kaseba, Oswald kumaliza ubishi kesho Dar


MABONDIA Japhet Kaseba na Maneno Oswald 'Mtambo wa Gongo', leo wamepima uzito tayari kumaliza ubishi katika pambano lao linalofanyika kesho jijini Dar es Salaam.
Kaseba na Oswald watapigana kwenye pambano lisilo la ubingwa la raundi 10 la uzani wa Middle, litakalofanyika kwenye ukumbi wa Travertine Hoteli, Magomeni.
Pambano hilo lililoandaliwa na mratibu Gervas Muganda chini ya usimamizi wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania, PST, litasindikizwa na mapambano kadhaa ya utangulizi yakiwemo yale ya mchezo wa kick boxing.
Mabondia hao kwa nyakati tofauti wametambiana kila mmoja akitamba ni lazima aibuke mshindi katika pambano hilo kutokana na anavyomchukulia mpinzani wake, sambamba na maandalizi wanayofanya.
Oswald, alisema kwa uzoefu alionao ni wazi atammaliza Kaseba raundi za awali, huku Kaseba, licha ya kukiri mpinzani wake ni 'ngangari', ila anaamini atampiga.
"Ni kweli Oswald ni mzuri na mzoefu wa ngumi, ndio maana amesaini mapambano mawili dhidi yangu na la Rashidi Matumla, lakini kwa nilivyojiandaa nitamshinda tu," alisema Kaseba.
Oswald nae alisema anachotaka ni mashabiki wa ngumi kufurika ukumbini kuona namna Kaseba anavyorejeshwa kwenye kick boxing, kwa jinsi atakavyompiga.
Alisema anajiamini uwezo alionao katika ngumi ni vigumu kuzuiwa na Kaseba, akisisitiza kuwa atawathibitishia wadau wa ngumi kwa nini aliitwa 'Mtambo wa Gongo' na watu wa Malawi.
Michezo ya utangulizi itakayolisindikiza pambano la Kaseba na Oswald ni la bingwa wa zamani wa ngumi za kulipwa nchini, Ernest Bujiku dhidi ya Mbukile Chuwa, Sweet Kalulu atakayepigana na Chaurembo Palasa na Venance Mponji kuzipiga na Jafar Majiha.

Villa kukutana J'pili, yamnyakua Habib Kondo

WAKATI wanachama wa Villa Squad wakitarajia kufanya mkutano wao mkuu keshokutwa, uongozi wa klabu hiyo umemnyakua kocha wa zamani wa Azam, Habib Kondo, ili kuokoa jahazi la timu yao linaloendelea kuzama katika Ligi Kuu Tanzania.
Makamu Mwenyekiti wa Villa, Ramadhani Uledi, aliiambia MICHARAZO kwamba klabu yao inatarajia kufanya mkutano wa wanachama kwa ajili ya kujadili mustakabali wa timu yao pamoja na mipango mingine ya kimaendeleo.
Uledi, alisema mkutano huo utafanyika Jumapili na kuwahimiza wanachama wake kuhudhuria kwa wingi kwa ajili ya kuisaidia klabu yao kuweka mikakati ya kuinusuru isishuke daraja.
"Tunatarajia kufanya mkutano wa wanachama siku ya Jumapili, kwa nia ya kujadili mustakabali wa timu yetu pamoja na mambo mengine ya maendeleo ya klabu yetu ikiwemo suala la uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi zilizo wazi," alisema.
Aidha uongozi wa klabu hiyo umemnyakua aliyekuwa kocha wa timu ya Azam, Habib Kondo baada ya aliyekuwa kocha wao, Said Chamosi, kurejea kwao Kenya.
Kondo, alithibitisha kunyakuliwa kwake, akisema ameombwa na uongozi wa Villa kuisaidia timu yao, hadi atakapopatikana kwa kocha mpya mkuu wa kuinoa timu hiyo.
"Aisee ni kweli bwana, baada ya kufuatwa na viongozi wa Villa ili kuisaidia timu yao, nimekubali kuinoa kwa muda, wakati wakiendelea kusaka kocha mkuu wa kudumu, kwa wanamichezo kama sisi ni vigumu kukataa ombi kama hilo," alisema.
Kondo, alisema licha ya kuanza kuinoa timu hiyo kwa kupata sare ya 0-0 dhidi ya JKT Ruvu, bado itabidi afanye kazi ya ziada kuisaidia timu hiyo kutokana na ukweli nafasi iliyopo sio nzuri, ingawa ligi bado ipo katika duru la kwanza.
Nyota huyo wa zamani wa Reli-Morogoro na Sigara, ndiye aliyeipandisha daraja hadi ligi kuu timu ya Azam msimu wa 2008-2009 kabla ya kuwa msaidizi wa makocha wa kigeni walioinoa timu hiyo kwa vipindi tofauti akiwemo kocha wa sasa Stewart Hall.

Timu za 'Maafande' zaitisha Azam Ligi Kuu T'Bara


TIMU ya soka ya Azam, imedai inakoseshwa usingizi ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu na kasi ya timu za jeshi, kuliko na vigogo vya Simba na Yanga.
Aidha klabu hiyo imeisifia safu yao ya ulinzi ambayo hadi sasa imeruhusu mabao mawili, ikiwa ndio timu pekee iliyofungwa mabao machache katika ligi hiyo.
Uongozi wa klabu hiyo, umesema mwenendo wa timu hizo za majeshi zilizopo katika ligi hiyo, umeifanya ligi ya msimu huu, kiasi cha kuwanyima raha wakizifikiria.
Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Nassor Idrissa 'Father', aliiambia MICHARAZO juzi kuwa, licha ya Simba na Yanga kuonekana tishio kwa klabu nyingine, wao Azam wanazihofu timu za JKT Oljoro, JKT Ruvu na Ruvu Shooting kwa jinsi zilivyo na upinzani mkali.
Idrissa, alisema timu hizo zimekuwa na upinzani mkali na kucheza soka la kusisimua na kutofungika kirahisi kitu kinachoifanya Azam zikiangalie kwa umakini timu hizo kuliko Simba na Yanga.
"Kwa kweli ligi ya msimu huu ni ngumu na yenye kusisimua na kati ya timu zinazotunyima raha ni timu za maafande ambazo zimekuwa na upinzania mkali na zenye kucheza soka la kusisimua," alisema Idrissa.
Alisema, timu hizo zimekuwa na matokeo bora zikiwa dimba la nyumbani au ugenini, na kudai uthibitisho wa ukali wao hata ukiziangalia kwenye msimamo zinafuata zikitofautiana kwa pointi chache na timu zilizopo juu.
Aidha Idrissa, aliipongeza safu ya ulinzi ya timu yake kwa kuruhusu kufungwa idadi ndogo ya mabao,ikiifanya iongoze kwa kuwa na ukuta mgumu hadi sasa nchini.
Azam katika mechi nane ilizokwishacheza hadi sasa imeruhusu mabao mawili, huku ikifuatiwa na Simba iliyoruhusu kufungwa mabao manne hadi hivi sasa.
"Kwa kweli tunaipongeza timu yetu na hasa safu ya ulinzi kwa kasi nzuri iliyofanya kwa kuruhusu mabao machache, naamini kwa mwenendo huu tunaweza kutimiza ndoto za kutwaa ubingwa au kuwa wawakilishi wa nchi kimataifa mwakani," alisema Idrissa.

Mwandido kuja nchini kuzindua kibao cha Assosa


MWANAMUZIKI nyota wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ny'boma Mwandido anatarajiwa kuja nchini kutumbuiza kwenye uzinduzi wa kitabu cha gwiji la muziki wa dansi nchini, Tshimanga Kalala Assosa kiitwacho 'Jifunze Lingala'.
Uzinduzi wa kitabu hicho unatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam, ingawa tarehe na jina la ukumbi, bado hazijawekwa bayana.
Akizungumza na MICHARAZO juzi, Assosa, alisema mipango ya uzinduzi wa kitabu chake yanaendelea vema ikiwemo kufanya mpango wa kumleta Ny'boma, aliyewahi kufanya naye kazi katika bendi mbalimbali nchini Congo, ili kushiriki uzinduzi huo.
Assosa alisema tayari wameshakubaliana na gwiji hilo linalotamba na nyimbo kama 'Double Double', 'Masua' na 'Abisina' kuja katika uzinduzi huo, kinachoendelea kwa sasa ni kumtafutia tiketi ya ndege ya kumleta na kumrejeshwa baada ya shughuli hiyo.
"Maandalizi ya uzinduzi wa kitabu changu yanaendelea vema, ambapo natarajia kuja

kushindikizwa na Ny'boma Mwandido, ambaye ameafiki mualiko wetu na kuhitaji tumtumie tiketi ya ndege," alisema Assosa.
Assosa, anayemiliki bendi ya Bana Marquiz, alisema umoja wao wa Wana 'Dar Kavasha Club', unafanya mipango ya kuisaka tiketi hiyo pamoja na ufadhili kwa ajili ya shughuli nzima ya uzinduzi wa kitabu hicho ambacho tayari kipo mtaani karibu miezi sita sasa.
"Kwa sasa tunasubiri majibu ya maombi yetu ya udhamini tuliotuma katika makampuni ya masharika mbalimbali ili kufanikisha uzinduzi huo utakaoenda sambamba na burudani ya muziki," alisema.
Aliongeza mbali na kitabu hicho cha 'Jifunze Lingala-Toleo la Kwanza', pia tayari ameanza maandalizi ya toleo la pili la kitabu hicho na na kile kinachohusu maisha yake binafsi.
Vitabu vyote vinafadhiliwa Klabu ya Dar Kavasha, umoja ambao Assosa ameomba mashabiki wa miondoko hiyo mikoani kuanzisha matawi yao, ili kuupanua zaidi.

Mwisho